GE2025 ACT Wazalendo wamjibu Monalisa Ndala

GE2025 ACT Wazalendo wamjibu Monalisa Ndala

Matukio, Taarifa, Habari na Mijadala ya Wananchi WAKATI wa Mchakato wa Uchaguzi Mkuu 2025

Elias Msuya

Senior Member
Joined
Dec 23, 2011
Posts
173
Reaction score
671
Siku moja baada ya Katibu Mwenezi wa ACT Wazalendo Mkoa wa Dar es Salaam na Naibu Waziri Kivuli wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Monalisa Ndala kumwandikia barua katibu Mkuu wa chama hicho akipinga kuteuliwa kwa Luhaga mpina kuwa mgombea urais, chama hiccho nacho kimemjibu.
Barua hiyo pia imepelekwa nakala kwa Msajili wa Vyma vya Siasa na kwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.

Soma pia: Mpina awekewa pingamizi kugombea urais

Andiko lililotolewa Agosti 16 na Naibu Katibu Mkuu Mstaafu na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Taifa, Joran Bashange, lina;opatikana mitandaoni limekanusha madai hayo.

*********

UPOTOSHAJI UNAODAIWA KUFANYWA NA MTU ANAYEITWA MONALISA NDALA

Utangulizi

Tarehe 15 Agosti, 2025; katika mitandao ya kijamii, kulionekana taarifa ya barua inayodaiwa kuandikwa na mtu aliyejulikana kwa jina la Monalisa Ndala akidaiwa kuwa mwanachama wa ACT Wazalendo na kiongozi wa Ngome ya Vijana mkoa wa Dar es Salaam. Barua hiyo inadaiwa kupelekwa kwa Katibu Mkuu wa Chama na kunakiliwa kwa Msajili wa vyama vya siasa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.

Upotoshaji uliotolewa unasemekana kuzingatia matakwa ya Kanuni za Kudumu za Chama za mwaka 2015 (Kanuni za Kudumu za Uendeshaji Chama Toleo la 2015) ambazo kwa sasa ni mfu. Hata hivyo, isivyo bahati upotoshaji unajidhihirisha wenyewe, kwani Kanuni inayodaiwa kukiukwa (kama ingalikuwa bado inaishi) inakataza mwanachama kumtuhumu mwanachama mwenzake kupitia njia zisizo rasmi; hususan, mitandao ya kijamii. Kanuni ya 10 ya Kanuni za Kudumu za Uendeshaji Chama Toleo la 2015 inatamka ifuatavyo;

“10 (1) Bila kuathiri Haki za mwanachama kama zilivyofafanuliwa katika ibara ya 10(1) ya Katiba ya Chama, mwanachama au kiongozi atakayemtuhumu mwanachama/kiongozi wake/mwenzake kwa njia zisizo rasmi ikiwa ni pamoja na kusema nje ya vikao, kwenye mitandao ya kijamii au mahali kwingine kokote nje ya vikao rasmi vya chama, anatenda kosa na anastahili kuchukuliwa hatua za kinidhamu kama ilivyoainishwa kwenye sura ya tatu ya Kanuni hizi. Taarifa zilizonukuliwa kwenye mitandao ya kijamii na kuthibitishwa kwamba ni za mwanachama au kiongozi wa ACT, zaweza kutumika kama ushahidi kwenye shauri la kinidhamu ndani ya chama.”

Kama ni kweli kulikuwa na ukiukwaji wa matakwa ya kanuni katika mchakato wa utezi wa mwanachama wa ACT Wazalendo kwa nafasi ya mgombea Urais kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika tarehe 29 Oktoba, 2025, basi ilitosha kumwandikia barua Katibu Mkuu bila kuitoa nje ya Chama na kuisambaza kwenye mitandao ya kijamii.

Kwa kuwa ni dhahiri upotoshaji ulikuwa na nia ovu, ulizua taharuki miongoni mwa wanachama na viongozi, ni muhimu kutoa ufafanuzi kwa lengo la kuweka kumbukumbu sahihi. Ifahamike kuwa nafanya hivyo nikitekeleza wajibu wangu chini ya ibara ya 12 ya Katiba ya ACT Wazalendo (Toleo la 2024).

Ufafanuzi

Kanuni za Kudumu za Uendeshaji Chama Toleo la 2015 zilizingatia matakwa ya Katiba ya Chama (Toleo la mwaka 2015) kabla ya marekebisho ya sheria ya vyama vya siasa ya mwaka 2019 (Political Parties Act, Chapter 258 R.E.2019).

Marekebisho ya sheria hiyo yaliweka sharti katika matakwa ya usajili wa vyama vya siasa la kuzuia ubaguzi wa aina yoyote katika uanachama na chaguzi zake. Matakwa hayo ya kisheria yamo katika kifungu cha 9(1)(c) na (d). Kifungu hicho kwa lugha ya Kiingereza kinasema;

“9(c) its membership is voluntary and open to all the citizens of the United Republic of Tanzania without discrimination on account of gender, disability, belief, race, tribe, ethnic religious profession or occupation;

(d) the election of its leaders at the General Elections is open to both gender.”

Aidha mabadiliko hayo kupitia kifungu cha 8D(1) yaliwekwa masharti ya kuzingatiwa katika utungwaji wa Katiba za vyama vya siasa. Moja ya sharti ni kuzingatia yaliyomo katika Jedwali la Kwanza katika sheria hiyo. Katika Jedwali la Kwanza fasili (e) inataka chama kubainisha haki na wajibu wa mwanachama.

Kutokana na matakwa hayo ya kisheria, ni dhahiri huwezi kuwa na Katiba au Kanuni ya chama inayoweka sharti la ubaguzi ama wa dhahiri au kwa taathira yake katika utekelezaji wa majukumu yake. Izingatiwe kuwa jambo hilo licha ya kuwa sharti katika sheria ya vyama vya siasa ni katazo katika Katiba ya nchi. Ibara ya 13(2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977) inatamka:

“13(2) Ni marufuku kwa sheria yoyote iliyotungwa na mamlaka yoyote katika Jamhuri ya Muungano kuweka sharti lolote ambalo ni la ubaguzi ama wa dhahiri au kwa taathira yake.”

Chama kwa kuzingatia mabadiliko hayo ya sheria ya vyama vya siasa na kutilia maanani matakwa ya Katiba ya nchi, kililazimika kufanya marekebisho ya Kanuni na Katiba zake.

Kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji wa mwaka 2019, Chama kilirekebisha Kanuni za Kudumu za Uendeshaji Chama Toleo la 2015 kwa kutunga Kanuni za uchaguzi wa Chama ndani ya Chama za mwaka 2019 [chini ya ibara 29(9)(viii) ya Katiba Toleo la 2015)] ambazo zilitoa maelekezo ya uchaguzi wa serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji wa mwaka 2019.

Ikumbukwe kuwa wakati huo Chama kilikuwa kinajiandaa kwa uchaguzi wa ndani ya Chama wa mwaka 2020 na hivyo marekebisho yalifanywa kwa kupiga ndege wawili kwa jiwe moja.

Katika utangulizi ili kufafanua sababu ya mabadiliko ya Kanuni hizo, imebainishwa ifuatavyo;

“Hatua hiyo inatokana na kutambua kwamba sisi kama familia ya watu wengi wenye mtazamo, maoni, na hulka tofauti tunahitaji kuweka taratibu kwa kila jambo tunalokusudia kulifanya ili kwamba kila mwanachama na kila kiongozi aweze kushiriki katika ujenzi na ustawishaji wa Chama na kufaidi matunda yatokanayo na ujenzi huo.”

Kila mwanachama pasipo kubaguliwa anashiriki katika ujenzi na kunufaika na matunda ya ujenzi huo.

Mwaka 2020 Chama kilifanya marekekebisho ya Katiba na kuwa na Katiba ya ACT Wazalendo Toleo la 2020 ambayo iliongeza mawanda katika haki za mwanachama.

Wakati Katiba (Toleo la 2015) katika ibara ya 10(1)(iii) ilitoa haki ya mwanachama kuchagua na kuchaguliwa kwa nafasi ya uongozi wa Chama tu;

10(1)(iii) Kuchagua na kuchaguliwa kuwa kiongozi ndani ya Chama;

Ibara ya 11(c) ya Katiba ya ACT Wazalendo Toleo la 2020 ilipanua wigo hadi uchaguzi wa kiserikali;

11(c) Kuchagua na kuchaguliwa katika uongozi, ujumbe au uwakilishi wa Chama, au Serikali kwa kupitia Chama kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii na Kanuni zilizowekwa.

Aidha zilitungwa Kanuni mpya kwa ajili ya uteuzi wa wagombea wa Chama (ACT Wazalendo) kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 [chini ya ibara 76(1)(i) na 79(1)(ii) ya Katiba Toleo la 2020)].

Katika utangulizi ilibainishwa ifuatavyo;

“Hatua hiyo inatokana na kutambua kwamba sisi kama familia ya watu wengi wenye mtazamo, maoni, na hulka tofauti tunahitaji kuweka taratibu kwa kila jambo tunalokusudia kulifanya ili kwamba kila mwanachama na kila kiongozi aweze kushiriki katika ujenzi na ustawishaji wa Chama na kufaidi matunda yatokanayo na ujenzi huo. Moja ya matunda hayo ni haki ya kuweka nia na kuteuliwa kugombea nafasi mbali mbali za kiserikali.”

Kwa upande mwingine, Kanuni zimetaka Kamati za Uongozi za Chama (ambazo wakati wa uchaguzi wa kiserikali hugeuka kuwa Kamati za Ushindi) kuhakikisha zinawajibika kubaini watu wanaokubalika (wagombea wazuri) na kuwashawishi kujiunga na Chama ili kurahisisha mchakato wa kampeni za uchaguzi na kukihakikishia Chama ushindi. Mantiki yake ni kwamba kwa marekebisho ya Kanuni na Katiba za Chama yaliyofanywa, mwanachama wa ACT Wazalendo ana haki; bila kubaguliwa, kuchagua au kuchaguliwa kwa nafasi yoyote ya uongozi ndani ya Chama au serikali kwa udhamini wa Chama. Sifa moja kuu ni uanachama wake.

Aidha, kutokana na ukweli kwamba wawakilishi wa chama cha siasa katika serikali ni wawakilishi wa wananchi; hususan wapiga kura, ni muhimu kuzingatia kuwa mara nyingi maslahi ya wananchi ndiyo hupewa kipaumbele panapozuka masuala kinzani kati ya maslahi binafsi, ya chama na ya umma.

Kwa muktadha huo, ni muhimu chama cha siasa kuweka sifa za kikanuni ambazo haziegamii sana kwenye maslahi binafsi ya chama kwani katika utendaji halisi kanuni hizo haziwezi kuwa kigezo cha utendaji wa mwakilishi huyo (Diwani, Mbunge, Mwakilishi au Rais) kwa wananchi (umma).

Mwaka 2024, Chama kilifanya marekebisho mengine ya Katiba (Katiba ya ACT Wazalendo Toleo la 2024) ambayo katika ibara ya 8(5) ilizingatiwa haja hiyo ya maslahi mapana ya umma, ikaruhusu viongozi kupokea wanachama wapya katika mikutano ya hadhara au ziara. Ibara hiyo inatamka;

“8(5) Bila kuathiri masharti ya ibara ndogo ya (4) hapo juu, kiongozi yeyote wa Chama au Serikali anayetokana na Chama anaweza kumpokea mtu au watu kuwa wanachama wapya pindi atakapokuwa katika mkutano wa hadhara au ziara za ujenzi wa Chama na kuelekeza kuzingatiwa kwa matakwa ya ibara ya 8 (2)(a) na (b).”

Marekebisho hayo yote yanazingatia maendeleo ya kisiasa ya Chama, sheria ya vyama vya siasa na nchi kwa ujumla kama ambavyo imebainishwa katika utangulizi wa Katiba Toleo la 2024 kama ifuatavyo;

“….. marekebisho hayo yanatilia maanani maendeleo ya kisiasa ya Chama chetu na ya Tanzania kwa ujumla yenye lengo la kukiimarisha zaidi ACT Wazalendo. Vilevile, marekebisho haya yameendelea kutilia maanani na kukidhi matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Sheria ya Vyama vya Siasa Namba 5 ya mwaka 1992 pamoja na marekebisho yake ya mwaka 2019.”

Ni Dhahiri mptoshaji si mwanachama wa ACT Wazalendo. Ndio maana kwenye utangulizi nikasema kuwa ni mtu aliyejulikana kwa jina la Monalisa Ndala akidaiwa kuwa mwanachama wa ACT Wazalendo na kiongozi wa Ngome ya Vijana mkoa wa Dar es Salaam. Kwa sababu mwanachama wa Chama hiki, chini ya ibara ya 12 anao wajibu wa kufahamu kinachoendelea ndani ya Chama kwa kusoma Katiba na Kanuni zake. Ibara hiyo inatamka:

“12. Kila mwanachama wa ACT atakuwa na wajibu ufuatao:-

(a) Kuisoma, kuifahamu, kuitetea na kuiheshimu Katiba hii na kuyatekeleza masharti yake yote, ikiwa ni pamoja na Kanuni zitakazotungwa.

(b) Kuwa tayari kupambana na namna yoyote ya uonevu,
ukandamizaji, udhalilisha na ubaguzi.

(c) Kujielimisha zaidi ili aweze kumudu dhamana zote
atakazopewa na Chama au dola ili azitekeleze vyema
kwa maslahi ya wanachama na wananchi wote wa
Tanzania.”

ACT Wazalendo haitayumbishwa na porojo za wahuni kwenye mitandao, bali kwa dhamiri ya kuwakomboa Watanzania; ambao kila uchao, wanagubikwa na lindi la umasikini, maradhi, uonevu na unyanyasaji, itaenelea kusimama imara kuhakikisha mambo hayo yanatokomezwa.

Kwa muktadha huo, sisi ACT Wazalendo tunasema LUAGA JOELSON MPINA tunaye na tunatamba naye.

“TAIFA LA WOTE KWA MASILAHI YA WOTE”

Na; Joran Bashange
Naibu Katibu Mkuu Mstaafu na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Taifa
 
Maelezo kibao hajajibu hoja ya msingi ya sifa ya mwanachama ambayo inataka atimize mwezi mmoja tangia kujiunga ambayo ndio msingi mkuu wa pingamizi? Je hapo ubaguzi uko wapi? Mnaandika taratibu ambazo mnazivunja wenyewe kama masisiemj vile namna gani?🤣🤣

No reform No Election
 
Kwa barua hii Agizo la Chama Tawala halina shida
 
Maelezo mareeefu ila hayajajibu hoja ya mwamamchama kuwa angalau na mwezi mmoja ktk chama ili.kuweza kugombea nafasi ya urais.

ACT walete majibu je kanuni za chama zimefuatwa au zimevunjwa?
 
Agizo la Chama Tawala😏
Na kwa mkutano wa hadhara aliofanya jimboni kwake Kisesa si ajabu tukasikia tume (huru) ya uchaguzi imemfutia sifa ya kugombea kwa kuanza kampeni kabla ya wakati. Niko pale
 
Maelezo kibao hajajibu hoja ya msingi ya sifa ya mwanachama ambayo inataka atimize mwezi mmoja tangia kujiunga ambayo ndio msingi mkuu wa pingamizi? Je hapo ubaguzi uko wapi? Mnaandika taratibu ambazo mnazivunja wenyewe kama masisiemj vile namna gani?🤣🤣

No reform No Election
Ameanza kwa kusema matakwa ya Kanuni za Kudumu za Uendeshaji Chama Toleo la 2015 (ambayo ndiyo msingi wa pingamizi la Monalisa) ni mfu, kufuatia marekebisho ya Katiba na Kanuni yaliyofanyika 2019 na 2020. Hayo maelezo mengine nadhani ni justification ya marekebisho yaliyofanyika.
 
dada monalisa ameptwa na nini? au ameshakula hela ya CCM?
 
Back
Top Bottom