SI KWELI World Economic Forums, Bill Gates na Albert Bourla wana mipango ya kupunguza idadi ya watu duniani

Baada ya kuitathmini taarifa hii, tumebaini kuwa si ya kweli.
FAKE (5).jpg

Hivi karibuni kumekuwa na taarifa zinazohusisha taasisi na watu maarufu duniani kuwa na mpango wa kupunguza idadi ya watu duniani. Miongoni mwa mambo hayo ni pamoja na Bill Gates kuelezwa kuandika katika mitandao wa kijamii akimshauri kiongozi wa World Economic Forums (WEF), Klaus Schwab juu ya matumizi ya "death panels" kupunguza watu duniani.

Lakini pia, video nyingine ambayo imesambaa mtandaoni inamuonesha Mtendaji Mkuu wa Pfizer, Albert Bourla, akidaiwa kusema wanatazamia kufanikisha kupunguza idadi ya watu duniani kwa 50%.

Je, taarifa hizi zina ukweli?
 
Tunachokijua
Tukianza na taaraifa ya Bourla, idadi kubwa ya watu kwenye mitandao ya kijamii wameshiriki kusambaza kipande hicho cha video, ikiwa ni pamoja na mtumiaji mmoja wa Facebook aliyeuliza, "Ni nani atakayewakamata wanaume hawa wawili na kuunda mahakama ya raia kuwafungulia mashtaka ya mauaji ya halaiki?" Kipande hicho pia kimetumiwa katika mjadala huu ulioanzishwa na mwanachama wa JamiiForums.

Kufuatia uchunguzi tuliofanya, kipande hicho cha video ni sehemu tu ya video ndefu ambayo imekatwa kwa lengo la kuondoa muktadha kamili wa mazungumzo yaliyofanyika. Katika video halisi tuliyoiona, Bourla alikuwa akizungumzia juu ya uzinduzi wa makubaliano mapya ya Pfizer ambayo yangeweza kutoa dawa na chanjo zake zinazolindwa na hatimiliki kwa gharama kwa nchi maskini 45 duniani, ambayo inawakilisha takriban watu bilioni 1.2.

Kipande hicho cha video pia kimekatiza sehemu ya maneno ya Bourla ili kusikika kama alisema kitu ambacho hakukisema, na kinamnukuu akisema:

"Ninaamini kuwa hii ni utekelezaji wa ndoto ambayo tumekuwa nayo, pamoja na timu yangu ya uongozi tangu tulipoanza mwaka 2019 - wiki ya kwanza tulipokutana, mwezi Januari 2019 huko California - na tukaamua malengo ya miaka mitano ijayo. Na moja wapo ilikuwa, ifikapo 2023, tutapunguza idadi ya watu duniani kwa 50%. Ninaamini leo, ndoto hii inakuwa ukweli."

Hata hivyo, uchunguzi wetu umebaini kuwa maneno yaliyokolezwa hapo chini ndiyo ambayo yameondolewa katika video halisi.

“Ninaamini kuwa hii ni utekelezaji wa ndoto ambayo tumekuwa nayo, pamoja na timu yangu ya uongozi tangu tulipoanza mwaka 19 - wiki ya kwanza tulipokutana, mwezi Januari wa 19 huko California - na tukaamua malengo ya miaka mitano ijayo, na moja wapo ilikuwa, ifikapo 2023, tutapunguza idadi ya watu duniani ambao hawawezi kumudu dawa zetu kwa 50%. Ninaamini leo, ndoto hii inakuwa ukweli."

Uchunguzi wetu umegundua kuwa ni Dhahiri kwamba kipande cha video kimebadilishwa ili kuunda tafsiri isiyo sahihi ya kauli ya Bourla.

Katika hatua nyingine, baadhi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii wanadai kuwa mwanzilishi wa Microsoft, Bill Gates alitoa hotuba katika mkutano wa G20 wa mwaka 2022 na kutabiri kuwa hivi karibuni "death panels" zitakuwa ni muhimu kutumika kutokana na gharama kubwa za huduma za afya.

"Death panels" ni mjadala ulioibuka kuhusu sera za huduma za afya nchini Marekani, ambapo watu walidai kuwa kuna vikundi au kamati zinazoamua juu ya hatma ya maisha ya watu wasiyokuwa na thamani. Wazo hili limekuwa likisababisha hofu na utata katika mijadala kuhusu mageuzi ya huduma za afya, lakini wataalamu wengi wamekuwa wakipinga kuhusu uwepo wake.

Kichwa cha habari cha makala ya Novemba 15, 2022 iliyochapishwa na tovuti moja kinasomeka, "Bill Gates anawaambia viongozi wa G-20 kuwa 'death panels' zitahitajika hivi karibuni. Makala hiyo inaeleza kuwa ameitumia hotuba yake katika Mkutano wa G-20 huko Bali, Indonesia, kuibua mjadala kuhusu 'death panels’.

Makala hiyo pia inasema kuwa kulingana na Gates, ‘death panels’ zitakuwa muhimu karibu sana hapo baadaye kuondoa Maisha ya watu wenye magonjwa na wasio na afya kutokana na 'gharama kubwa sana ya matibabu.' Lakini pia chapisho la Instagram la Novemba 17, 2022 linajumuisha screenshot ya makala hiyo na video ya Gates akizungumzia gharama ya huduma za afya kwa watu katika hatua ya mwisho ya maisha.

Hata hivyo, ingawa Bill Gates amehudhuria baadhi ya mikutano ya G20 ya awali (ikiwa ni pamoja na mmoja kwa ombi la Rais wa zamani wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy), mwanzilishi huyo wa kampuni ya Microsoft hakuwepo Bali wakati huo.

Pamoja na kuwa ripoti kadhaa kabla ya mkutano zilidai kwamba Gates alipanga kuhudhuria tukio hilo, ukweli ni kwamba wakati huo alikuwa nchini Kenya, akikutana na viongozi na maafisa kujadili maendeleo katika huduma za afya, kilimo, na teknolojia ya habari.

Gates alifanyiwa mahojiano na vyombo vya habari vya Kenya wakati mkutano wa G20 ulipokuwa ukiendelea na ali-tweet akiwa Nairobi akionekana na viongozi wa nchi hiyo. Lakini pia hakuna ushahidi wowote unaoonesha kuwa Gates alifanya mawasiliano na kiongozi wa World Economic Forums (WEF), Klaus Schwab kuhusu suala la kupunguza idadi ya watu duniani.

Kwa kuzingatia taarifa hizo, tunajiridhisha kuwa taarifa hizo zimesambazwa kwa malengo ya kuudanganya umma.
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom