Wizi kupitia mitandao waichanganya TCRA

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,318
33,125
Boniface Meena
WIZI wa Kimafia unaofanywa kupitia mitandao umeichanganya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), kwa kuamua kuita kampuni zote za simu nchini, benki pamoja na mamlaka nyingine za serikali ikiwamo polisi ili kuangalia wanavyoweza kuzuia wizi huo.

Suala hilo ambalo linatikisa nchi sasa hivi limeelezwa kuwa watu wengi ambao wanafanya matumizi ya uhamishaji na uhifandhi wa fedha kwenye mitandao ya simu wamekuwa wakilizwa.

Habari zilizopatikana zimeeleza kuwa wafanyabiashara wa fedha kupitia mitandao hapa nchini wamekuwa wakilizwa fedha nyingi kwa njia za utata kiasi cha kuamua kuripoti kesi hizo polisi kila wakati.

Chanzo cha habari kutoka ndani ya Jeshi la Polisi kimeeleza kuwa kuna mtindo unaotumiwa na wezi hao wa mtandao kwa kuangalia namba zenye fedha kisha wanazifunga (swap) kwa muda fulani na kuzitumia wao kama mali zao na kuweza kuiba fedha hizo kisha kuzirudisha namba zile kwa wenyewe.

"Mtindo huo unaweza kufanywa na watu walioko ndani ya kampuni hizo au mawakala ambao wameruhusiwa kuwahudumia wateja ambao namba zao zimepotea na wanahitaji namba zilezile zilizopotea,"kilieleza chanzo chetu.

Chanzo hicho kilieleza kuwa mamilioni ya fedha yameshaibiwa na kwamba TCRA iliamua kuwaita wote wanaohusika katika kuhakikisha wizi huo unatokomea kutafuta njia za kuweza kutatua tatizo hilo ambalo ni tishio hapa nchini.

Akizungumzia mkutano huo Mkurugenzi Mtendaji wa TCRA, Profesa John Nkoma alisema huduma za kampuni hizo na benki zimeonekana kuwa ni nzuri lakini kila kitu kizuri kina kasoro zake.

Alisema wamekutana na kampuni zote za simu, benki pamoja na polisi kuona jinsi gani wanaweza kuboresha huduma hizo.

"Tumekutana na kampuni ya Tigo, Vodacom, Airtel, Zantel, mabenki pamoja na polisi ili kuweza kuangalia uboreshaji wake,"alisema Prof Nkoma.

Alisema wizi wa fedha husababishwa na baadhi ya wananchi wenyewe ambao wamekuwa wakitoa namba zao za siri kiasi kwamba namba inapofungwa na kuibiwa anayeiba anakuwa akijua namba ya siri ya anayemuibia.

Prof Nkoma alisema kutokana na tatizo hilo wameyaonya makampuni hayo kutokuruhusu namba zibadilishwe kienyeji.

"Kampuni za simu tumeziambia zisifanye 'swaping' ya namba kizembezembe lazima anayehitaji huduma hiyo wamuone 'physically ',"alisema Prof Nkoma.

Hadi sasa kiasi kilichoripotiwa Polisi kuhusina na wizi kwa njia ya mtandao hapa nchini ni Tsh 1.3 bilioni, Euro 8,897 na dola za kimarekani 551,777, imefahamika.

Kauli hiyo ilitolewa hivi karibuni na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Pereira Ame Silima wakati akijibu swali la Hussein Mussa Mzee (Jang’ombe-CCM) aliyetaka kujua ni kiasi gani cha fedha kimeripotiwa polisi kutokana na wizi kwa njia ya mtandao.

Mzee alihoji serikali imejipanga vipi ili kudhibiti wizi wa mtandao pamoja na kutaka kujua wahalifu wangapi wamekamatwa na akataka itungwe sheria maalumu kwa ajili ya kushughulikia wizi wa mtandao.
Silima alisema kuwa serikali imetunga sheria inayoshughulikia uhalifu unaofanywa kwa njia ya mtandao Electronic and Posta Communication Act, 2010 na Sheria ya Kudhibiti Fedha Haramu (The Anti – Money Laundering Act – 2006.

Alisema serikali kupitia vyombo mbalimbali vya dola kama vile Polisi, Taasisi za Fedha, Vyombo vya Habari, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania(TCRA) imejiwekea mikakati ya kuelimisha wananchi kuhusiana na aina ya uhalifu wa kimtandao na jinsi ya kupambana nao.

Waziri alibainisha kuwa Jeshi la Polisi limeanzisha kitengo cha Makosa ya Kimtandao (Cyber Crime Unit) ambacho kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kinafanya kazi kubwa ya kupambana na majanga hayo.
Wizi kupitia mitandao waichanganya TCRA
 
Back
Top Bottom