Waziri Pindi Chana: Tunafanyia kazi ushauri wa Wadau kuhusu mabadiliko ya Adhabu ya Kifo

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,812
11,989
Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Pindi Chana amesema Serikali inaendelea kufanyia kazi maoni ya baadhi ya Wadau kuhusu kuondoa adhabu ya kifo.

Akizungumza Oktoba 10, 2023 kwenye Kongamano la kujali adhabu ya kifo lililoandaliwa na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kwa kushirikiana na wadau wengine, Waziri Pindi Chana amesema licha ya Sheria kutambua adhabu ya kifo lakini Serikali imeendelea kuthamini na kulinda uhai wa kila Mtanzania.
photo_2023-10-10_15-21-03.jpg
"Tanzania pamoja na kuwa na adhabu ya kifo ambayo ipo kwa mujibu wa Sheria lakini Serikali bado inathamini na kulinda uhai wa kila Mtanzania na ndio maana hata wale waliopewa adhabu ya kifo wakihukumuwa wanatibiwa kwa gharama za Serikali."

Ametolea mfano "Mmeshuhudia juzi kwenye Mitandao ya Kijamii picha ya mfungwa wa kunyongwa akipewa matibabu hospitali baada ya kupata ajali tena kwa gharama za Serikali.”
photo_2023-10-10_15-21-07.jpg

photo_2023-10-10_15-20-47.jpg
Pia amesema kesi ambazo adhabu yake ni hukumu ya kifo Mahakama zimekuwa zikizipa uzito zaidi.

"Kwa mfano katika kesi hizo hata kama mshtakiwa akikiri kosa ni lazima ushahidi uwasilishwe na Mahakama ijiridhishe ndio itatoa adhabu hiyo tofauti na makosa mengine ukikiri Mahakama inakutia hatiani kwa kukiri kwako binafsi, lakini hata mtu akitiwa hatiani suala la kukata rufaa ni lazima."

Akifafanua juu ya Sheria na aina ya makosa ambayo adhabu zake ni kifo endapo mtuhumiwa anatiwa hatiani, amesema Tanzania baada ya uhuru iliendelea kutumia baadhi ya Sheria ambazo zimekuwa zikitumika kutoa adhabu ya kifo mfano wa Sheria hizo ambazo amezitaja ni pamoja na Sheria ya Kanuni ya Adhabu, ambapo kupitia mtu akiua kwa kukusudia na ikabainika mbele ya Mahakama adhabu yake ni kifo, makosa mengine ambayo ametaja ni makosa ya uhaini.

Amesema baada ya Tanganyika kupata uhuru ni Sheria moja imetungwa ambayo endapo mtuhumiwa akitiwa hatiani anaweza kuhukumiwa adhabu ya kifo, ambayo ni Sheria ya kupinga ugaidi (Ant Terrorism Act No. 27 of 2002) ambayo ilifanyiwa marekebisho Mwaka 2016 kupitia (The written Laws Miscellaneous amendment Act No. 2 of 2016).

Ameeleza Sheria hiyo inatamka kama kitendo cha ugaidi kitakuwa kimesababisha mauaji basi adhabu yake itakuwa kama ilivyo kwenye Kifungu cha 197 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, kifungu ambacho kinahusika na makosa ya mauaji ya kukusudia.

Hata hivyo, Waziri Pindi ameeleza licha ya uwepo Sheria ambazo zinaweza kuwatia watuhumiwa hatiani na kusababisha kupewa adhabu ya kifo bado kuna kesi nyingi za mauaji hali ambazo kama Taifa kuna haja ya kuangalia chanzo au mzizi wa tatizo hupo wapi.

"Takwimu za miaka mitatu kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka zinaonesha kwa Mwaka 2021 kulikuwa na kesi za mauaji zilizofunguliwa Mahakamani ni 3155, Mwaka 2022 kesi 3,548 hadi kufikia Juni 2023 kesi 1,210.

Aidha, kwa niaba ya waandaji wa Kongamano hilo, Rais wa TLS, Wakili Harold Sungusia amesema Serikali inatakiwa kuchukua hatua kwenye suala hilo kama ambavyo mataifa mengine tayari yameonesha mwelekeo mabadiliko ya kuondoa adhabu hiyo.

"Zipo Nchi nyingi ambazo zipo kwenye mwelekeo wa kufuta adhabu ya kifo na kwa upande wa Afrika Nchi takribani 20 Kusini mwa Jangwa la Sahala tayari zimeanza kuondoa adhabu hiyo kwa ufupi baadhi ya Nchi ni Guinea-Bissau, Afrika Kusini, Senegal, Rwanda, Burundi, Togo, Gaboni, Msumbiji, Angola na Nchi nyingine," amesema Wakili Sungusia .

Amesema kufikia Mei 2023 idadi ya wafungwa ambao walihukumiwa kunyongwa hadi kufa Nchini ilikuwa ni 691. Ambapo amedai hayo yamebainishwa kwenye Ripoti ya Tume ya Haki Jinai ambayo iliundwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Ameongeza "Tume ilibaini kwamba adhabu hiyo haijatekelezwa kwa miaka mingi jambo ambalo linalosababisha wafungwa waliohukumiwa kunyongwa kuishi kwa hofu na mashaka wakisubiri utekelezwaji wa adhabu hiyo, kwa kuzingatia msingi huo Tume ilipendekeza kwamba Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 ifanyiwe marekebisho ili kuweka tafsiri ya kifungo cha maisha na kuweka muda maalumu."

Sanjari na hayo, Ali Magogwa mkazi wa Tabora ambaye ameshiriki Kongamano hilo, ameeleza wazi amewahi kuhukumiwa adhabu ya kifo baada ya kukaa mahabusu miaka 10 tangu Mwaka 1994 kutokana na tuhuma za mauaji baadaye akashinda rufaa na kuachiliwa huru.

Amedai akiwa Gerezani baada ya adhabu hiyo ilimuathiri Kisaikolojia ambapo ameeleza "Nilipokuwa Gerezani ukikaa unawaza kesho au lini nanyongwa kwakweli hali hii ni ngumu sana kwangu iliniathiri sana kisaikolojia lakini nashukuru nilishinda rufaa na sasa nipo huru."

Magongwa ameomba Wadau kuendelea kupaza sauti zao ili sheria ziondoe adhabu hiyo ambapo amesisitiza ina athari kubwa ambazo sio rahisi kuzibaini.

Aidha, Prof. Chris Peter Maina ambaye anafundisha somo la Sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam amesema katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Katiba ya Zanzibar zinakataza uteswaji wa raia na kutambua haki ya kuishi, hivyo Sheria ya Kanuni ya adhabu ambayo inaruhusu adhabu kifo inakinzana na baadhi ya Ibara kwenye Katiba JMT na vifungu kwenye Katiba ya Zanzibar.

Ameshauri wadau wanaweza kuishawishi Serikali kufanya mabadiliko ya vifungu kwenye Katiba hiyo ili kuwezesha adhabu kifo kupoteza uhalali wa moja kwa moja kisheria.
 
Back
Top Bottom