Waraka wa wazi kwa rais jakaya kikwete, kuhusu mgogoro mpya udom

Ubumuntu

JF-Expert Member
Oct 21, 2010
14,316
10,782
WARAKA WA WAZI KWAKO KUHUSU MGOGORO MPYA UDOM

Mheshimiwa Jakaya M. Kikwete,
Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,


Mheshimiwa Raisi, pole kwa kazi ngumu ya kuongoza nchi yetu Tanzania, salamu nyingi kutoka UDOM hasa jumuiya ya wanataaluma (UDOMASA). Mheshimiwa Raisi, jukumu kuu la waraka huu ni kutaka kukujuza wewe na kutoa taarifa katika ofisi yako juu ya mgogoro mpya unaokikumba Chuo Kikuu cha Dodoma. Mheshimiwa Raisi, pamoja na majukumu makubwa uliyo nayo tunaomba tukukumbushe juu ya maelezo ya matatizo ambayo jumuiya ya wanataaluma wa UDOM waliwasilisha kwako mwanzoni mwa mwaka wa 2011. Pamoja na kutambua kuwa tuliwahi kutuma salamu zetu za pongezi na shukurani kwako kupitia Mh Waziri Mkuu na viongozi wengine wa serikali yako, tunaomba pia tutumie fursa hii kukushukuru na kukupongeza tena kwa kuitikia wito wetu na kumtuma mwakilishi wako ambae ni Waziri Mkuu Mh Mizengo Pinda, nae alifika UDOM na tuliweza kuonana nae ana kwa ana.

Huu ni ujasiri, upendo na usikivu mkubwa ambao umedhihirisha kwa vitendo si kwetu tu bali pia kwa makundi mengine ya kijamii mfano ulipokutana na madaktari kutatua mgogoro wao na wanasiasa wa vyama vya upinzani kuhusu masuala ya katiba. Ujio wa Mh Waziri Mkuu uliweza kupunguza baadhi ya matatizo tulio ainisha wakati huo. Mh Rais tuliweza kumdokeza Mh Waziri Mkuu wasi wasi wetu wa kutokea migogoro mingine baada ya ule wa awali hasa vitendo vya ulipizaji kisasi. Tunachoshuhudia kwa sasa si hisia wala ndoto bali ni uhalisia wa kile tulichokitia shaka. Jumuiya ya wanataaluma imebidi iandike tena waraka huu kwa sababu mazingira yanavyoonesha, mgororo tulio nao sasa tunachelea kusema ya kuwa ni visasi vilivyo tokana na matokeo ya mgogoro ule wa mwanzo. Mheshimiwa raisi, tunaomba tutumie nafasi hii kukutanabaisha juu ya mgororo huu mpya. Labda tuanze na mambo yaliyojiri baada ya kutatuliwa kwa mgogoro wa kwanza.

Mheshimiwa Raisi, katika kipindi cha hasa mwishoni mwa 2011, kumekuwepo na matukio ya kufukuzwa kazi wafanyakazi wa UDOM hasa wanataauluma tena kwa kunyemelewa na kushtukizwa. Jambo la kusikitisha zaidi ni ukiukwaji mkubwa wa taratibu halali za kisheria (Sheria Na 6, 2004 ya Ajira na Mahusiano kazini) pamoja na sheria na kanuni nyingine za utumishi wa umma. Mheshimiwa Raisi, wanataaluma hao wahanga wa fukuza fukuza, kwa kutoridhika na uhalali wa wao kufukuzwa, baadhi yao waliamua kuchukua hatua za kukata rufaa kwenye vyombo husika vilivyoundwa kwa mujibu wa sheria ili waweze kupata haki zao. Wanataaluma hao walipeleka rufaa zao katika kamati ya usuluhishi na uamuzi (CMA) iliyoko chini ya wizara ya kazi. Baada ya majadiliano kati ya wanataaluma hao na chuo – kwa pamoja walikubaliana kurudisha rufaa zao kwenye KAMATI YA RUFAA YA NIDHAMU KWA WAFANYAKAZI (Staff Disciplinary Appeal Committee) kwa mujibu wa sheria inayoongoza chuo yaani “University of Dodoma Charter” kanuni 58 (1). Kamati hii ilichelewa sana kuundwa lakini baada ya mchakato mrefu, hatimae mchakato ulikamilika mwishoni mwa mwezi wa kumi (10) 2011. Mnamo tarehe 14/12/2011 katika kikao cha Baraza la Chuo, kamati ilipewa baraka ianze kazi rasmi ya kupokea na kusikiliza mashauri ya rufaa za wafanyakazi tarehe 15/12/2011. Punde tu baada ya kamati kuanza kazi, rufaa za wafanyakazi watano (5) waliofukuzwa na tayari walishapeleka rufaa zao sehemu husika zilianza kutafutiwa utaratibu wa kusikilizwa. Kamati hatimae ilipanga na ilifanikiwa kusikiliza rufaa hizo mnamo tarehe 10/02/2012. Sheria Na 6 ya ajira na mahuisano kazini imeweka wazi kuwa shauri la rufaa hutakiwa kusikilizwa na kuhitimishwa ndani ya siku 30 lakini mlalamikaji ajulishwe maamuzi ya shauri lililosikilizwa ndani ya siku tano. Kwa maelezo ya mdomo, kamati iliahidi ya kuwa majibu ya rufaa za wafanyakazi wote yangetolewa baada ya kufikishwa kwenye baraza la Chuo ambalo lilipangwa kufanyika tarehe 30/03/2012 siku ya Ijumaa. Kamati ilitimiza wajibu wake wa kupeleka taarifa ya majibu ili yapewe baraka ndipo yaweze kutolewa kwa wahusika. Mheshimiwa raisi, kwa mshangao mkubwa na kwa kukatisha tamaa, Baraza la Chuo lilikataa kabisa kupokea taarifa ya kamati kwa madai kwamba Menejimenti ya Chuo haikujulishwa kwa maandishi siku ambayo rufaa ilisikilizwa na hivyo mchakato wote haukuwa sahihi. Mbaya zaidi, Baraza liliamuru kamati irudie kusikiliza rufaa hizo upya.

Mheshimiwa raisi, sisi wanataaluma wa UDOM tulishtushwa na maamuzi hayo ya baraza la chuo kwa sababu zifuatazo.
1. Kamati ya rufaa ni chombo huru tena chenye mamlaka ya kuamua (Appelate Powers) kwa mujibu wa sheria na kazi yake ilikuwa ni kuwasilisha maamuzi yake ya rufaa za wafanyakazi kwenye baraza hilo, na ilifanya hivyo.
2. Kwa sababu kamati hiyo ni huru, haitegemewi wala kutarajiwa baraza la chuo kukataa kopokea taarifa ya majibu ya rufaa iliyowasilishwa na kamati hiyo.
3. Kwa mujibu wa sheria zinazoongoza chuo na sheria nyingine za utumishi wa umma, baraza la chuo halina mamlaka ya kuhoji na kuhukumu kazi ya kamati huru ya rufaa za wafanyakazi.
4. Hoja ambayo ilipelekea ripoti hiyo kukataliwa ni kile ambacho menejimenti ya chuo kudai ya kuwa haikujulishwa na hivyo haikuwakilishwa. Hoja hii haikuwa na mashiko, kwa sababu menejimenti ya chuo iliwakilishwa na maafisa wa chuo wanaotambulika. Na muhtasari wa kikao cha kamati ya rufaa hiyo ni ushahidi tosha.
5. Hata hivyo, Kitendo cha Menejimenti ya Chuo kupeleka malalamiko yake kwenye Baraza ya kwamba haikutendewa haki ni kuvuruga utaratibu wa kisheria uliopo kihalali. Hii ni kwasababu Baraza la Chuo lilishahukumu kwa kuwafukuza wafanyakazi hao na haliwezi kurudia kujitetea kwa kile kilichofanya.
6. Sheria iko wazi, kama Menejimenti iliona haikutendewa haki, kwa mujibu wa sheria majibu yanatakiwa kutoka –ndipo menejimenti inatakiwa kukata rufaa katika ngazi za kisheria zinazofuata na si kurudi kwenye baraza.
7. Uamuzi wa Baraza la Chuo kuagiza kamati irudie kusikiliza rufaa upya ni kupindisha sheria kwa makusudi na kwa maslahi yasiyojulikana na kutufanya wanataaluma kujiuliza maswali mengi bila majibu.

Hatua zilizochukuliwa na jumuia ya wanataaluma (UDOMASA) Mheshimwa Raisi, baada ya baraza la chuo kukataa kupokea taarifa ya maamuzi ya kamati huru ya rufaa, jumuia ya wanataaluma wa UDOM haikuridhishwa na kitendo hicho kwa sababu zilizoainishwa hapo juu na kuchukua hatua zifuatatzo.
1. Jumuia iliamua kumuandikia mwenyekiti wa Baraza la Chuo (barua imeambatishwa) kulitaarifu baraza juu ya ukiukwaji wa taratibu uliotokea na kuliomba liridhie taarifa ya maamuzi ya kamati huru ya rufaa za wafanyakazi.
2. Pia kupitia barua hiyohiyo, jumuia ilishauri kuwa kama menejimenti inahisi kutotendewa haki, ifuate taratibu za kisheria kudai haki yake kama ambavyo walalamikaji walivyofuata taratibu hizohizo za kisheria kudai haki zao.
Kilichofuata baada ya barua ya UDOMASA kwa mwenyekiti wa baraza la chuo
1. Mheshimiwa Raisi, kwa masikitiko makubwa, kamati tendaji ya baraza la chuo mnamo tarehe 11.4.2012 ilikaa na maamuzi yaliyofikiwa ni kutafsiri kutokukubaliana kwetu (disagreement) juu ya maamuzi ya kikao cha baraza kutopokea taarifa ya majibu ya kamati ya rufaa kuwa ni mgogoro (dispute) baina ya jumuia ya wanataaluma na baraza la chuo na kuacha hoja ya msingi ambayo ni majibu kutolewa ndipo hatua nyingine zifuate.
2. Mbaya zaidi, kamati tendaji ya baraza la chuo badala ya kuamuru majibu ya kamati ya rufaa yatolewe ili kukidhi madai ya barua ya UDOMASA, imemwagiza makamu mkuu wa chuo kwenda kufungua kesi mpya CMA baina ya baraza la chuo na jumuia ya wanataaluma (UDOMASA), na hivyo kuweka pembeni hoja ya msingi yaani taarifa ya majibu ya kamati ya rufaa za wafanyakazi kutolewa.
3. Kama vile haitoshi, baraza la chuo halikuchukua jukumu la kuijibu UDOMASA iliyoandikia barua juu ya madai ya ukiukwaji wa sheria na taratibu uliofanywa na baraza hilo; badala yake, kamati tendaji ilitoa tangazo la jumla lililosainiwa na mwenyekiti na kuliweka kwenye tovuti ya chuo (website) na baadae kusambazwa maeneo mbalimbali ya chuo.

Mheshimiwa Raisi, kitendo cha kamati tendaji ya baraza la chuo kufikia maamuzi ya kuamuru rufaa mpya kuanzishwa baina ya jumuia ya wanataaluma (UDOMASA) na baraza la chuo ni
1. Kutengeneza mazingira ya kuendeleza ukandamizaji na ukiukwaji wa haki za wafanyakazi hapa UDOM. Mheshimiwa Raisi, jumuia inalichukulia suala la kucheleweshwa kwa haki kama kunyimwa haki (Right delayed is right denied). Sisi wanataaluma wa UDOM, tumeonesha ustaarabu wa kuridhisha kwa kuwashauri wenzetu waliofukuzwa kufuata njia na taratibu za kisheria ya kudai haki zao kwenye vyombo vilivyoundwa kisheria kwa kukata rufaa badala ya kuingia kwenye mikutano au migomo. Ustaarabu wetu huu bila shaka unapaswa kutambuliwa na yeyote mpenda haki na amani.
2. Kitendo cha baraza la chuo kuunda mgogoro na UDOMASA ni dalili mbaya na tafsiri pekee ni upindishwaji na ukiukwaji wa utaratibu halali kwani UDOMASA haipaswi kamwe kuwa mlalamikiwa. Tukiwa kama wanataaluma, elimu yetu tuliosomeshwa na serikali yetu inatusuta kwa sababu tunashindwa kuitumia inavyostahiki katika mazingira haya korofi na yaliyojawa na hofu
.
Pamajo na hilo jumuiya ya wanataaluma (UDOMASA) kwa mujibu wa katiba yake lengo kuu ni kulinda haki na maslahi ya wanataaluma wote wa UDOM na mustakabali wa elimu chuoni kwetu. Hivyo basi matukio haya ya fukuzafukuza na “ ulipizaji wa kisasi” kwa wanataaluma katika chuo chetu vimejenga hofu, woga na kupunguza morali ya uchapaji kazi. Kila kukicha tunaona ni afadhali ya jana na hatujui ya kesho. Mheshimiwa Raisi, kwa nafasi yako jumuia ya wanataaluma wa UDOM inapenda kwa namna ya pekee:
1. Ufahamu hali halisi ya taasisi hii ambayo ni zao la wazo lako
2. Ufahamu uhusiano wa mgogoro huu mpya na mahusiano yake na mgogoro uliopita ambao ulisababishwa na ile mikutano isiyokuwa na ukomo ambayo uliingilia kati kupitia Mheshimiwa Waziri mkuu
3. Uelewe kile UDOMASA inachokisimamia na kutetea katika mgogoro huu
4. Aidha, tunaomba kwa nafasi yako uweze kuingilia kati maana hali inavyoonesha Mh. Raisi kuna fukuto kubwa linaloweza kupelekea mgogoro mkubwa zaidi ya uliokwisha tokea

Imetolewa na kamati tendaji ya UDOMASA
16/04/2012
UDOMASA-University of Dodoma, Chimwaga Complex, P.O. Box 259,Udom, Cell +255 755 210310,+ 255 713 004127, 0714 477 180, 0653 331 003 Email: udomasa2011@gmail.com
 
Back
Top Bottom