Mtambuzi
Platinum Member
- Oct 29, 2008
- 8,810
- 15,398
Kuna jambo ambalo nimekuwa nikijiuliza mara nyingi sana. Nakumbuka katika kipindi changu cha mpito wakati natafuta jiko, nilibahatika kuwa na mitoko (dates) na wadada kadhaa…….. Naam, kipindi hicho nilikuwa katika pilika za kutafuta ni nani atakayenifaa kwa ajili ya kujenga familia.
Kama mjuavyo mtoko ni gharama na gharama hizi mara nyingi huzibeba mwanaume, ambaye ndiye anayetoa mwaliko. Ni vigumu kutabiri gharama za mtoko na hiyo ni kutokana na kutojua kama mwenzako anapendelea aina gani ya vinywaji au vyakula. Hivyo inabidi kabla ya mtoko basi ujikague kama mfuko unakidhi usije ukaumbuka bure.
Lakini pia inategemea ni sehemu gani mtakwenda kwa ajili ya mtoko wenu, kwani kila sehemu ina gharama zake. Kwa mfano, kuna kwenda sinema, kuna kutoka kwenda kupata chakula cha jioni na hii inategemea mnakwenda wapi, kwani kuna mighahawa ya inayouza vyakula vya kitalii, kuna hoteli za nyota tatu, nne mpaka tano, maeneo yote hayo yanatofautiana bei, na ndio maana nikasema mtoko ni gharama.
Swali kwa wanawake:
Inaweza kutokea baada ya mtoko wa kwanza mwanaume akavutiwa na wewe akiamini kwamba, mnaweza kujenga familia. Lakini ili kufahamiana zaidi akawa anakualika kwenye mtoko mara kwa mara ili mpate fursa ya kufahamiana zaidi.
Kwa kuwa mara nyingi hutokea wanaume ndio hubeba gharama za mitoko (dates) kwa sababu wao ndio waalikaji, Je mnadhani ni wakati gani mnapaswa kuanza kulipa gharama za mtoko…………?
Niliwahi kuzungumza na baadhi ya wafanyakazi wenzangu wa jinsia ya kike kuhusu jambo hili. Baadhi walisema wanaweza kutoa mwaliko wa mtoko wa tatu na kubeba gharama. Wengine walisema mtoko wa pili wanaweza kulipa gharama za matumizi ya mtoko huo, hata na kama wao ndio wamealikwa na ikitokea mwanaume analazimisha kulipa, basi watajaribu japo kuchangia gharama za vinywaji. Lakini wapo waliodai kwamba wao wataanza kulipa pale tu ambapo mwanaume huyo ataonyesha dalili zote za kuwavisha pete za uchumba au kufunga nao ndoa…………………..
Naomba kupata mtazamo wenu juu ya jambo hili, Je nyie mnasemaje?.