SoC03 Wakati Sahihi wa Mabadiliko yenye tija katika Kilimo cha Mifugo kuelekea ufugaji wenye tija kwa jamii ya Kitanzania

Stories of Change - 2023 Competition

captain ruto

New Member
Jun 18, 2023
1
1
Mabadiliko yenye tija katika ufugaji ni ubeti unaoimbwa kila muda Tanzania,Afrika na duniani kwa ujumla wake. Hii inachagizwa na umuhimu wa suala la ufugaji katika maeneo makubwa matatu ambayo ni

01. Utunzaji wa Mazingira

02. Afya za wanaadamu na

03. Afya na haki za mifugo zenyewe. Licha ya sera zetu za kitaifa za ufugaji kila uchwao kujikita katika uboreshaji wa ufugaji na kufikia kile kinachoitwa ufugaji wenye tija lakini bado, lakini bado mabadiliko yenye tija katika ufugaji hayafikii lengo.

Katika nchi zilizoendelea ufugaji umejikwamua kwa kiwango kikubwa kabisa katika mambo mawili ya Msingi, mosi afya za wanaadamu na pili afya na haki za mifugo, kumekua na ukwamo katika kufanikisha juhudi za utunzaji wa Mazingira kupitia ufugaji lakini bado juhudi kupitia sheria, sera na tafiti mbalimbali kupitia serikali zao na mashirika zinafanyika kuhakikisha ufugaji unachagiza moja kwa moja utunzaji wa mazingira yao.

Hali ni tofauti kabisa katika jamii yetu ya kitanzania, hakuna tulichokikamilisha kwenye mabadiliko yenye tija katika ufugaji wetu (Kilimo cha Mifugo). Mazingira yetu yanaharibika kila uchwao kupitia ufugaji holela na uwekezaji katika mifugo, Afya za watanzania zinaharibika na kuwa mashakani kila kukicha kupitia mazao ya mifugo mfano Nyama, Maziwa n.k na ufugaji holela na afya na haki za mifugo zinachezewa na kuvunjwa kila siku katika kila kona ya nchi hii, Swali la msingi linabaki Je, ni lini Mabadiliko sahihi yenye tija katika kilimo cha Mifugo yatafikiwa?

Ufugaji wenye tija katika utunzaji wa mazingira; Nchi yetu imebarikiwa mazingira yenye ardhi kubwa na iliyo bora, ufugaji holela na uwekezaji katika kilimo cha mifugo una matokeo hasi katika mazingira ya nchi yetu, mfano makundi makubwa ya ng’ombe, mbuzi na kondoo yanayofugwa kiholela yanasababishwa ukame na hali ya ujangwa katika mazingira yetu, mfano ng’ombe mmoja jamii ya kienyeji aina ya Zebu wenye mapembe mafupi anayefugwa kiholela atahitaji wastani wa miezi sitini kufikisha kilo 300 za uzito wake muda ambao atakuwa ameharibu mazingira kwa kiwango kikubwa ukilinganisha na ng’ombe mmoja jamii ya kisasa aina ya Borani atahitaji wastani wa miezi 40 kufikisha kilo 500 za uzito wake muda ambao atakua amechangia uharibifu wa mazingira kwa kiwango kidogo kabisa katika ufugaji ulioboreshwa.

Pia inawezekana Kabisa kufuga Mbuzi Zaidi ya elfu mbili katika eneo ambalo mti hautokatwa wala majani kuchomwa moto.

Hivyo basi muda sahihi wakua na mabadiliko yenye tija katika kilimo cha ufugaji kwenye utunzaji wa Mazingira ni sasa.

Ufugaji wenye tija katika kuimarisha afya za wanadamu; Nchi yetu imebarikiwa kuwa na watu wacheshi, wenye busara na wapenzi na watumiaji wa bidhaa za mifugo, hivyo basi afya za hawa watanzania wenzetu ni jukumu letu sote katika kuzilinda dhidi ya maradhi na uimarishaji. Ufugaji holela na uwekezaji katika kilimo cha mifugo una matokeo hasi katika afya za watanzania.

Hivi karibuni na hapo awali kumekua na machapisho mengi ya tafiti mbalimbali yenye kuonesha uhatari uliopo katika afya za watanzania unaosababishwa na matumizi ya bidhaa za mifugo.

Mfano matumizi holela ya dawa za kuua vijidudu vya magonjwa katika mifumo ya mwili ya mifugo zinasababisha mabaki ya vimelea vya dawa katika mazao ya mifugo, hivyo kuhatarisha usalama wa afya za watumiaji wa bidhaa hizo.

Pia milipuko ya magonjwa ya mifugo yanayoweza kumuathiri binadamu yameziweka hatarini afya za watumiaji wa mazao hayo. Mifano yenye kuonesha hali ya uhatari katika utumiaji wa mazao ya mifugo yaliyopita katika mnyororo usio sahihi ni mengi sana.

Hivyo basi muda sahihi wakua na mabadiliko yenye tija katika kilimo cha ufugaji kwenye utunzaji wa afya za watumiaji wa mazao ya mifugo ni sasa.

Ufugaji wenye tija katika kuimarisha afya na kulinda haki za mifugo; Nchi yetu imebarikiwa kuwa na mifugo ya aina mbalimbali, kuanzia ndege kama kuku, Wanyama wa miguu minne kama Punda, na Wanyama wa ulinzi kama Mbwa. Je ni watanzania wangapi wanafahamu kuwa Wanyama hawa wana haki zao?

Haki za mifugo zinavunjwa kila siku katika kila pembe ya Tanzania, Tembea Dodoma uone Punda wanavyobebeshwa mizigo mizito kwenye Maguta wakiwa na vidonda, simama njia kuu itokayo Morogoro kuelekea Dar es salaam ujione kuku wanvyosafirishwa kwenye magari huku wakipigwa na upepo, nenda Mbeya ujionee Nguruwe wanavyosafirishwa kwenye pikipiki kwa maumivu makali, tembelea wawekezaji na wafugaji wakuku uone walivyowajaza kuku kuzidi nafasi za mabanda yao na tembelea makazi ya watanzania wanaofuga Mbwa katika mikoa kama Shinyanga, Mtwara, Lindi, Kigoma na uwaulize lini wamerisha Mbwa zao. Hivyo basi muda sahihi wakua na mabadiliko yenye tija katika ufugaji kwa kuimarisha afya na kulinda haki za mifugo ni sasa.

Jamii ya watanzania, wafugaji, Viongozi wenye dhamana kuanzia ngazi ya nyumba hadi ngazi za kitaifa, Wawekezaji, Mamlaka za kiserikali, Mashirika yasiyo ya kiserikali, Serikali na kila Mtanzania ana jukumu la kuchukua hatua stahiki katika kulikamilisha hili linaloitwa “Mabadiliko yenye tija katika Kilimo cha Mifugo kuelekea ufugaji wenye tija kwa jamii ya kitanzania” kwa maslahi mapana ya taifa letu pendwa, vizazi vyetu vya sasa na apo baadae na mifugo yetu.

Tunahitaji sera bora, sheria, uwekezaji wenye tija, elimu, uongozi imara na watanzania waliothabiti katika kuharakisha na kuhakikisha haya yanasimama imara

Wako Katika Ujenzi wa Leo na Kesho ya Taifa letu pendwa,
Saidi Bakari Lusewa,
Simu; 0742 925 159
Email; lusewalegacy@gmail.com
 
Back
Top Bottom