SoC03 Sekta ya mifugo ifanyiwe maboresho ili kuleta maendeleo nchini

Stories of Change - 2023 Competition

Reginald paul

Member
Jul 6, 2023
5
4
Sekta ya mifugo ina nafasi kubwa katika kujenga uchumi imara wa taifa, kuongeza kipato kwa watanzania wanaotegemea mifugo, kutoa fursa za ajira pamoja na kuhifadhi rasilimali za taifa, Jukumu kubwa ni kujenga mazingira mazuri yatakayotoa fursa za kuongeza kipato na ajira kwa wafugaji wadogo, kufuga kibiashara na kuongeza ajira, kuendeleza sekta ya mifugo itakayokuwa na mwelekeo wa kibiashara yenye ufanisi na itakayohimili ushindani wa kimataifa, kuibua mifumo bora ya uzalishaji itakayoongeza tija miongoni mwa wafugaji wadogo pamoja na kuhifadhi rasilimali za mifugo na kuunda sera na taasisi zitakazosimamia maendeleo na matumizi endelevu ya rasilimali hizo.

Yapo mabadiliko chanya katika sekta ya mifugo nchini ambayo yameanza kujionesha hususan katika uzalishaji na uuzaji wa mifugo na mazao yake nje ya nchi, utoaji wa huduma na upatikanaji wa pembejeo za mifugo, mkazo wa serikali uendelee kuwekwa katika kugharamikia huduma za ufugaji zanazohitajika kukuza sekta kwa ufanisi, huduma hizo ni pamoja na miundombinu ya vijijini, utafiti, huduma za ugani, uzuiaji wa magonjwa ya mlipuko na uzuiaji wa wadudu waenezao magonjwa ya mifugo, aidha serikali ihamasishe wafugaji na wadau wengine kuchangia gharama za utoaji wa huduma kama vile ujenzi wa malambo na majosho.

Changamoto kubwa inayoikabili sekta ya mifugo ni namna ya kufikia viwango vya ubora wa mifugo na mazao yake vitakavyokidhi mahitaji ya soko la ndani na kimataifa kwa kuongeza uuzaji wa mifugo nje ya nchi na kukabili ushindani wa bidhaa zinazoingizwa nchini ambapo ulinzi pekee uliopo kwa viwanda vya ndani ni kuweka viwango muafaka vya ushuru na ubora unatakiwa, marekebisho ya kisera ya kufanya biashara ya mifugo nchini inatakiwa kutiliwa mkazo Ili kuleta maendeleo mapana katika mifumo ya biashara hiyo.

Katika nchi za kanda ya Afrika mashariki na kusini mwa Afrika juhudi za kutekeleza itifaki ya soko la pamoja la jumuiya ya Afrika mashariki (EAC) na jumuiya ya maendeleo ya nchi za kusini mwa Afrika (SADC) zinaendelea kwa lengo la kuwa na biashara pana inayohusisha mazao ya mifugo ambayo yatachangia ukuaji na maendeleo ya biashara. Inatia moyo kwamba mabadiliko ya haraka yameendelea kutokea katika sekta ya mifugo nchini katika miaka ya hivi karibuni yaliyochagizwa na wadau wa sekta ya mifugo nchini wakiwemo wazalishaji, wasindikaji, wafanyabiasha, wauzaji wa pembejeo za mifugo na watoa huduma wengine wapya, hatahivyo bado kuna baadhi ya maeneo ya vijijini hususan vile vya ndanindani havipati huduma zakutosha, taratibu zifanywe na serikali kuboresha huduma za mifugo katika maeneo hayo.

Magonjwa ya mlipuko kwa mifugo ni yale yanayoenea kwa kasi na yanatakiwa kuchukuliwa hatua za kuyadhibiti mapema iwezekanavyo kabla hayajaleta madhara makubwa kwa mifugo, ushirikiano mkubwa unahitajika katika kudhibiti magonjwa haya kwa kuwa na mfumo thabiti wa tahadhari, kutambua, kuratibu na kuoaniasha mikakati ya udhibiti. Magonjwa ya mlipuko yanayotokea mara kwa mara hapa nchini ni pamoja na homa ya mapafu kwa ng'ombe, kichaa cha mbwa, ugonjwa wa kwato na midomo (salabu) magonjwa mengine ni pamoja na mdondo na kideri kwa kuku na homa ya nguruwe, udhibiti wa magonjwa ya mlipuko kwa mifugo unakwazwa na huduma hafifu za afya ya mifugo, miundombinu duni, udhaifu wa sekta binafsi katika kutoa huduma za afya ya mifugo, bei kubwa ya dawa zinazotibu magonjwa ya mifugo na uelewa mdogo wa wafugaji na wadau kuhusu magonjwa hayo, aidha serikali inatakiwa kuimarisha huduma za kitaalamu katika kudhibiti na kutokomeza magonjwa ya mlipuko kwa mifugo, serikali kwa kushirikiana na wadau wengine inatakiwa kuhamasisha na kuhimiza uwekezaji katika kuzalisha chanjo na pembejeo za mifugo pia kuimarisha miundombinu kwa ajili ya kudhibiti magonjwa ya mlipuko kwa mifugo.

Mfumo wa maabara za mifugo unaathiriwa na uhaba wa miundombinu, uhaba wa vifaa na wataalamu, uelewa mdogo wa wadau na muundo dhaifu wa kitaasisi hivyo kuwa na mfumo imara wa maabara za mifugo ambao utatoa huduma bora za maabara kwa ajili ya kudhibiti magonjwa na ubora wa bidhaa za mifugo. Licha ya matumizi mazuri ya bio-teknolojia bado kuna athari za moja kwa moja zinazojitokeza katika afya ya binadamu, wanyama pamoja na mazingira, matumizi ya bio-teknolojia yanaathiriwa na uelewa mdogo wa jamii, uhaba wa wataalamu, miundombinu na vifaa, Hivyo kuhamasisha matumizi ya bio-teknolojia na matumizi salama ili kuboresha uzalishaji wa mifugo na kuongeza tija, kutoa huduma bora za ugani zinazokidhi mahitaji ya wafugaji na wadau wengine, kutoa wataalamu makini wa mifugo na wafugaji wenye ujuzi kwa ajili ya idara ya mifugo, kutoa taarifa na takwimu sahihi kwa wadau kwenye sekta ya mifugo ili kuwezesha kupanga na kutoa maamuzi sahihi zitakazoleta maendeleo.

HITIMISHO
Licha ya vikwazo vingi vinavyoikabili sekta ya mifugo kama vile uhaba wa ardhi, maji na malisho, aina ya mifugo na mifumo ya uzalishaji, magonjwa ya mifugo na uhaba wa elimu na ujuzi kwa wafugaji, serikali inapaswa kufanya maboresho makubwa katika kudhibiti vikwazo hivyo ili kuleta mafanikio makubwa katika sekta hii na kwa wafugaji kwa ujumla, serikali pia inatakiwa kuongeza maafisa mifugo angalau kwa kila kijiji awepo mmoja ili kuongeza ufanisi na kufikia malengo tuliyojiwekea.

MWISHO.
 
Back
Top Bottom