Wabunge CCM wataja tiba ya maandamano

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,789
288,015
[h=3]Wabunge CCM wataja tiba ya maandamano [/h]

*Wasema ni serikali kutekeleza mahitaji ya wananchi
*Mnyika atishia mengine ya kupinga mgawo wa umeme


Na Grace Michael, Dodoma
Majira


IKIWA ni takriban wiki tatu za mjadala na mashambulizi ya wabunge kuhusu maandamano na tuhuma za kuchochea migomo ya wanafunzi vyuoni, jana
wabunge wawili wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliibuka na kukemea kitendo cha kunyoosheana vidole bungeni kwa suala hilo badala ya kutatua madai ya wanaoandamana.

Tangu bunge la bajeti suala la maandamano limekuwa ni gumzo huku baadhi ya wabunge wa CCM wakiwashambulia wenzao wa CHADEMA, ambao pia wamekuwa wakijibu kwa kueleza sababu za kufanya hivyo na kusisitiza kuwa hawatakakoma hadi matatizo ya wananchi yatakapomalizwa.

Kauli ya James Lembeli

Wa kwanza kuzungumzia suala hilo ni Mbunge wa Jimbo la Kahama Bw. James Lembeli aliyewataka wabunge kuacha kunyoosheana vidole bungeni kuhusiana na tatizo la migomo na maandamano yanayofanywa katika maeneo mbalimbali nchini, badala yake waishinikize serikali kushughulikia kero zinazosababisha matatizo hayo.

Alisema kuwa bila kushughulikiwa matatizo yanayofanya wananchi kuingia barabarani na wanafunzi kugoma, kamwe matatizo hayo hayatamalizika, hivyo akaitaka serikali kusoma ujumbe unaoandikwa kwenye mabango wakati wa maandamano na kuufanyia kazi.

Akizungumza kwa hisia kali huku akiwazuia wabunge wenzake kumpigia makofi, alisema kuwa "Ukiona watu wanarandaranda mtaani ujue kuna tatizo kubwa...serikali ifanyie kazi matatizo ya wananchi na haya maandamano na migomo kamwe hatutayaona," alisema Bw. Lembeli.

Alisema kuwa hakuna haja ya suala hilo kuzua mjadala mkubwa bungeni kwa kuwa dawa yake ni kuitaka serikali kutekeleza madai yanayodaiwa na wananchi wanaoandamana, lakini pia madai ya wanafunzi yanayowafanya kugoma vyuoni na akatoa mfano wa mikopo.
"Kama wanafunzi wanadai mikopo wapewe...hakuna sababu ya kubaki tulumbana humu na huku hao watu wana matatizo yanayowafanya waone njia pekee ni kugoma au kuingia barabarani," alisema Bw. Lembeli.

Alisema kuwa nchi nyingi duniani ziko kwenye migogoro na wananchi wake wanaandamana, hivyo kwa kupinga suala hilo bila ya suluhu haitawezekana kwa kuwa Tanzania si kisiwa.

Akizungumzia sekta ya madini, Bw. Lembeli alihoji Serikali kuendekeza wawekezaji huku wananchi wanaozunguka kwenye maeneo hayo wakibaki na matatizo lukuki.

Alisema kuwa hivi sasa mji wote wa Kahama umegawiwa kwa Kampuni ya Barrick inayojishughulisha na uchimbaji madini huku wananchi wa maeneo yale wakikosa maeneo ya wachimbaji wadogo wadogo.

Alionya kuwa hali hiyo isipoangaliwa na kushughulikiwa kwa uharaka wa aina yake, basi hapo mbele itasababisha matatizo makubwa na akatolea mfano wa matatizo yaliyotokea katika Mgodi wa North Mara.

"Hivi huyu Barrick ni nani ambaye yeye leo hii anathaminiwa kuliko hata wananchi ambao wamekuwa katika eneo hilo miaka nenda rudi?...hata wewe ndugu yangu Ngeleja (Waziri wa Nishati na Madini) leo wewe ni waziri uko kwenye benchi la hapo mbele...siku ukitoka hapo utawaeleza nini wananchi? Hii ni hatari kubwa," alisema Bw. Lembeli.

Profesa Mwakuyusa atia neno

Kwa upande wake Mbunge wa Rungwe Magharibi, Prof. David Mwakyusa alishauri iundwe tume itakayochunguza vyanzo vya migomo na matatizo katika vyuo vikuu hususan Chuo Kikuu cha Dodoma ili kupata ufumbuzi utakaowezesha kukoma kwa migomo hiyo.

Prof. Mwakyusa alisema kuwa serikali haina budi kutafuta suluhu ya matatizo hayo ili wanafunzi waweze kusoma katika mazingira tulivu na kuondokana na hali iliyopo sasa ambayo inawafanya kutokana makini darasani.

Alisema kuwa wapo wanafunzi wanaokubwa na mikasa hiyo kutokana na mkumbo na akaonya kuwa endapo hali hiyo itaachwa na kuendelea kuna hatari ya kushuka kwa taaluma ambayo athari zake zitaonekana katika miaka ijayo.

Kutokana na hali hiyo, aliiomba serikali kuhakikisha inapata suluhu mapema iwezekanavyo ili wanafunzi waliofukuzwa warejee darasani.

"Wakati wananchi na sisi humu tukinyosheana vidole na kutafuta mchawi, vijana wetu wanakosa masomo na taaluma yao inashuka hivyo hakuna budi ya kumaliza matatizo haya," alisema.

Alisema kuwa njia moja wapo ya kumaliza tatizo hilo ni wanafunzi kupewa taarifa sahihi na kwa wakati sahihi, hivyo akawataka viongozi wanaoongoza vyuo hivyo kuhakikisha wanaacha woga na kuzungumza na wanafunzi.

Profesa Mwakyusa ambaye bunge lililopita alikuwa Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, aliwaomba wanasiasa kuacha kupenyeza mkono wao katika migomo hiyo na akasema kuwa wanafunzi waachwe wasome ili hapo baadaye waweze kusaidia katika uongozi.

"Tuache kuwapa sumu ya siasa hawa vijana ili wasome kwani tukipata madaraka hawa ndio tutawahitaji baadaye," alisema.

Alisema kuwa malumbano yanayoendelea hivi sasa juu ya migomo katika chuo hicho hayana tija yoyote iwapo suluhu ya matatizo hayo haitapatikana na kwamba pande zote zilizo katika malumbano hayo ikiwemo serikali hakuna aliyeshinda.

Mbunge huyo alisema kuwa Chuo Kikuu cha Dodoma kinaongoza kwa migomo kati ya vyuo vikuu takribani kumi vilivyopo nchini, huku akikipongeza Chuo Kikuu cha Mzumbe kwa kutokuwa na migomo ya mara kwa mara na akataka vyuo vingine kuiga mfano huo.

Mnyika aitishia maandamano

Wakati huo huo, Mbunge wa Ubungo, Bw. John Mnyika (CHADEMA), alivunja ukimya kwa kuomba mwongozo bungeni akitaka majibu kutoka kwa Waziri Mkuu hasa katika sakata la mgawo wa umeme ambalo alisema wananchi wanajipanga kuandamana kupinga hatua hiyo.

Bw. Mnyika alifikia hatua hiyo kutokana na kutokuwepo kwa kipindi cha Maswali ya Papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu ambacho hutoa fursa kwa wabunge kuhoji mambo ya kitaifa ili kupata msimamo wa serikali.

Wiki iliyopita serikali iliomba kipindi hicho kiahirishwe kwa muda ili kumpa Waziri Mkuu kuwasilisha hotuba yake ya bajeti na kupata fursa nzuri kuzikiliza michango ya wabunge.

Bw. Mnyika alisema kuwa endapo serikali haitatoa msimamo wa suala la umeme leo, basi wataendelea na hatua wanazoombwa na wananchi za kuandaa maandamano kwa ajili ya kuhoji suala hilo.

"Tunapata ujumbe kupitia simu za mkononi na barua pepe, wananchi wanataka tuandae maandamano kupinga tatizo la umeme hivyo wasipotoa tamko tutaendelea," alisema.

Alisema kuwa kutokuwepo kwa kipindi hicho ni kuwanyima fursa wabunge ya kupata majibu ya mambo makubwa ambayo yanayumbisha nchi kwa sasa, kama kauli ya Waziri Mkuu aliyoitoa kuhusu mchakato wa katiba, suala la mgawo wa umeme na sakata la kurejeshwa kwa wanafunzi waliokuwa wamefukuzwa Chuo Kikuu cha Dodoma ambapo alidai kuwa itikadi za vyama vua siasa zinatumika kuwarejesha wanafunzi hao.

Kauli ya Kawambwa UDOM

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dkt. Shukuru Kawambwa, alipotakiwa kuzungumzia madai ya Mnyika kuhusu Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), alisema hana uhakika na taarifa za wanafunzi waliosimamishwa masomo kurudishwa chuoni kwa itikadi za chama.

"Siamini kama suala hilo liko namna hiyo, waliositisha masomo ya wanafunzi ni uongozi wa chuo, na wanaorudisha ni uongozi wa chuo na kwa taratibu za chuo chenyewe," alisema Dkt. Kawambwa.
 
Back
Top Bottom