SoC02 Uwajibikaji na Dhana ya kuamini na Kumpa mtu nafasi ya pili (second chance!)

Stories of Change - 2022 Competition
Aug 31, 2021
66
125
Ndugu wana jukwaa na jamii kwa ujumla. Mara nyingi kuna mazingira na namna ambazo wengi huzizingatia na hatimaye kutoa majibu ya hatma ya watu kwamba labda flani anafaa au hafai kutokana na hayo mazingira au namna au mwonekano au tabia iliyojionyesha kwa wazi au haikuwa ya wazi lakini tukaitafsiri kwa namna ya kuhitimisha kwamba huyu anafaa au hafai!

Mimi ni muumini wa kumpa kila mtu nafasi ya pili (second chance!) bila kujali mazingira yaliyojionyesha tayari ambayo ni kama yanataka uhitimishe kuona huyo mtu yupo hivi au vile!

Miaka karibu 12 hivi iliyopita nilikuwa mfanyakazi katika shirika mojawapo la kimataifa hapa Tanzania; majukumu yangu yalikuwa ni Meneja wa Miradi ambayo ilikuwa inatekelezwa kwa kushirikiana na asasi nyingine za kiraia (NGOs) hapa nchini.

Ninamshukuru Mwenyezi Mungu kunipa fursa hiyo na nafasi hiyo! Kwa umri wangu na mwonekano hata wewe msomaji huenda ungeniona kwa mara ya kwanza usingeamini kwamba nilikuwa na nafasi hiyo kubwa! Mara kadhaa niliwahi kwenda kwenye matukio huko mikoani na wakaribishaji wakasema wanamsubiri Mgeni rasmi aingie na kumbe nilikuwa ndiye mimi!

Pia namna yangu ya kutokujikweza na kushuka chini nafikiri nayo ilichangia!
Sasa siku moja kulikuwa na tukio la usaili wa kazi (job interview) katika moja ya Miradi ambayo shirika langu lilikuwa linaiwezesha; na nafasi ya usaili huo ilikuwa ni Mkurugenzi wa Mradi (Project Director).

Utaratibu ulitaka huyo partner wetu afanye usaili wa awali na kupata watahiniwa (shortlisted candidates) watatu ili baada ya hapo mimi niende na tufanye usaili wa mwisho kwa pamoja na kumpata mmoja ambaye tungempa hiyo nafasi ya kazi!

Kabla ya siku ya usaili huo wa mwisho, partner wetu ambaye ndiye mtekelezaji Mkuu wa Mradi alinipigia simu na akasema tayari wameshafanya usaili na kuwapata watu watatu wa mwisho (shortlisted candidates), na kwamba wawili wana sifa zote isipokuwa mmoja! Yeye mmoja huyo ana Diploma tu wakati wenzake wawili wana degree ya kwanza na post-graduate Diploma! Nilimuuliza kwa nini amempa nafasi mwenye Diploma kuwa mmoja wa hao watatu wa mwisho wakati vigezo vya kazi vinataka wote wawe na angalau degree ya kwanza?!

Alijitetea na kujieleza kwamba huyu mwenye Diploma ni Secretary wake hapo ofisini, anamfahamu sana kwamba ni mchapa kazi sana, anajua kuongea kiingereza vizuri sana (kuongea kiingereza ilikuwa sifa mojawapo!), na kwamba ana matatizo makubwa ya kifamilia (mmewe hana kazi, wana watoto) na kipato chake hapo ofisini ni kidogo sana hivyo angeipata hiyo nafasi ingemsaidia sana!!!

Kwa hiyo huyu partner wetu akahitimisha kwa kuniomba msamaha sana na pia kuniomba kwamba nikienda kwenye huo usaili wa mwisho tafadhali sana nione namna ya kumsaidia huyo dada ambaye ni Secretary wake kwa sababu nilizotaja hapo juu!

Siku ya usaili ikafika na nikaenda mwenyewe nikiendesha Gari la kazini! Nilifika, nikapaki sehemu husika na kuelekea kwenye ofisi ya partner wetu. Nilipofika nikakuta dada mmoja hapo mapokezi! Nilimsalimia na kwamba ninaomba kuonana na Mkurugenzi wa hiyo taasisi.

Yule dada aliniangalia kuanzia juu mpaka chini kwa haraka hadi nilijisikia vibaya! Akauliza, “una shida gani na Mkurugenzi?” Nikajibu “nina shida tu ya kibinafsi” akaniangalia tena kwa namna ile ya kutoka juu mpaka chini! Akaniambia “kama huwezi kusema shida yako hiyo ya eti binafsi, basi kaa hapo kwenye benchi “ nikasema “Sawa”.

Basi nikakaa hapo, na mara wakaja watu wawili kwa kufuatana na wakanikuta na kunisalimia na kumsalimia huyu dada wa mapokezi (ambaye sasa ndo akawa mwenyeji wetu wote pale) wakasema wamekuja kwenye interview! Akawakaribisha vizuri tu na akawauliza kama wanatumia kahawa au maziwa! (Kumbe hizo huduma zipo hapo kwa ajili ya wageni!).

Hao watu wakasema wanachohitaji na wakapewa! Basi tukawa wote tupo na wale wageni wenzangu wawili wanaendelea kupata vinywaji vyao huku wakipiga story mbili tatu juu ya mambo ya kazi na hususani usaili (interview) uliokuwa mbele yao! Na yule dada mwenyeji (mtu wa mapokezi) akawa anawambia wasiwe na wasiwasi huyo “bosi” anayekuja kuwafanyia usaili hajafika!

Akawambia pia kwamba actually hata yeye ni mtahiniwa wa huo usaili na kwahiyo wanamsubiri tu “bosi” aje!!! Kwahiyo watahiniwa wote watatu wakawa wapo na “bosi” yaani mimi tayari nipo na wao lakini hawajui ndiye mimi!!!

Mara simu yangu ikapigwa na aliyepiga ni Mkurugenzi wa hiyo taasisi! Akaniambia “Mheshimiwa vipi umepata dharula?! Maana muda umefika na nimeambiwa watahiniwa wetu wote wamefika na wapo tayari” nikamjibu “Ndugu Mkurugenzi, nilifika kama nusu saa iliyopita na nipo hapa kwenye benchi mapokezi, nje ya ofisi yako”

Mkurugenzi akatoka ndani na kunikuta nimekaa kwenye benchi na wale watahiniwa wawili (wageni waliokuja)! Akaniuliza “kwa nini hukuingia ndani moja kwa moja?” Nikamjibu “Niliomba kukuona kupitia huyu dada wa mapokezi, na alitaka niseme nina shida gani ndo aweze kuniruhusu, na mimi nilimwambia nina shida binafsi hivyo akanikatalia kukuona”.

Mkurugenzi akalazimika kuniomba msamaha mbele ya huyo dada na akanitambulisha kwa watahiniwa kwamba Mimi ndiye “bosi” waliyekuwa wananisubiri!! Nikaingia ofisini kwake, akanipitisha kwenye kiti chake (cha kuzunguka ) ili sasa nianze kazi ya kufanya usaili wa mwisho!

Kabla sijaanza akaniambia yule dada wa reception (mapokezi) aliyeninyima kuingia ndiye yule ambaye ana Diploma, ni Secretary wake, ana matatizo makubwa ya kifamilia, na ndiye alikuwa anaombewa ili nikiona Sawa nimpatie hiyo kazi pamoja na kukosa “vigezo” muhimu ikiwemo elimu! Na Mkurugenzi akasema “ bahati mbaya huyu dada amekukosea sana, naendelea kukuomba msamaha Mkuu na kwa kweli lakini hata usipompatia hiyo kazi siwezi kukulaumu”

Interview ikaanza na kwa kweli wale wawili wenye “sifa na vigezo” vilivyotimia walikuwa vizuri sana sana! Nilianza nao hao wawili (mmoja baada ya mwingine). Yule dada wa mapokezi akawa wa mwisho kuingia (tulifanya hivi ili kumsaidia maana alikuwa analia sana!).

Alipoingia aliendelea kulia na akashindwa hata tu kujitambulisha jina lake kwangu! Tukampa dakika 10 atulie asilie ili tufanye interview lakini bado hakuweza! Basi nikamwambia atoke tu nje ili mimi na Mkurugenzi wake tushauriane!

Mkurugenzi “bosi” wake naye ile hali ilimpa shida sana! Akaniambia “Mkuu naomba useme tu ni yupi kati ya wale wawili unayemchukua na kumpa hii kazi” nikamjibu “ninamchukua huyu dada Secretary wako na siyo yeyote kati ya wale wawili” akataka anipigie magoti nikamkataza na kusema asifanye hivyo!

Hivyo tulimpa kazi huyu dada wa mapokezi na Secretary wa hiyo partner wetu! Alifanya kazi yake kwa ufanisi mkubwa na mafanikio makubwa sana! Lakini pia toka siyo hiyo na miaka yake karibu mitano ya kutekeleza huo Mradi hatukuwahi kuonana uso kwa uso!!! Siku zote alikuwa ananikwepa kwa yale yaliyotokea siku ya usaili!

Kila mtu anaweza kupewa nafasi ya pili bila kujali ameharibu kiasi gani hapo mwanzo! Vyeti vya kitaaluma na vigezo vya kuonekana wakati mwingine siyo ndo kila kitu! Kila mmoja wetu hapa duniani ana nafasi ya kipekee ya kumwinua mtu mwingine! Mungu awabariki.
 
Back
Top Bottom