emmapetertz

Member
Jul 15, 2021
12
28
MHESHIMIWA JOYCE NDALICHAKO (WAZIRI WA ELIMU) NAOMBA TUZUNGUMZE KIDOGO)
Screenshot_20210717-092933.png
Mhe Waziri,
Heshima kwako.................... …..
Nakupa salamu kwa lugha ya kikwetu Usukumani, "Ulimholla mayu ungumbyala"

Ni matumaini yangu u mzima wa afya tele, kama nakuona vile unavyozunguka zunguka katika kiti cha Uwaziri ofisini kwako, teh teh teh teh.

Mimi kawaida yangu si msemaji sana, ila leo nataka nikupotezee muda wako kidogo kwa kunisikiliza kama hutojali nina machache ya kuteta na wewe. Kabla hatujafika mbali, kwanza naomba nikuulize maswali machache...

1. Je, ulishawahi kufikiria kuiboresha Elimu ya Tanzania ili iwe na tija kwa kila mhitimu haijalishi amefaulu /amefeli?
Kama ni Ndiyo, kivipi? ...
Kama ni Hapana, Kwanini? …

2. Unafikiri ni kwanini tunazalisha vijana wengi wasomi ambao kila siku wanalalamika serikali haiwapi ajira, wanashinda vijiweni ili hali wana elimu na vyeti vyao?

Mhe, naomba unisikilize kwa umakini:
Kwa miaka mingi Elimu inayotolewa Nchini Tanzania imekuwa haina tija katika jamii zetu kutokana na changamoto katika namna zifuatazo:

UTOLEWAJI
Elimu yetu imekuwa ikitolewa kwa nadharia mno kuliko vitendo tena wakati mwingine katika mazingira magumu sana. Elimu ya Tanzania imeendelea kuwa ni Elimu ya kwenye makaratasi tu (bookish-in nature), ndio maana tunazalisha vijana wengi wasomi wenye vyeti safi lakini hawana hata uwezo wa kubuni wafanye nini ili kuzalisha kipato zaidi ya kusubiri ajira serikalini. Aidha, Mentality (dhana) iliyojengeka katika vichwa vyao ni kusoma ili waajiriwe (education for public employment). Amini kwamba zaidi ya 80% ya wanafunzi wa kitanzania wanaosoma wana ndoto za kuajiriwa na serikali, "a very stupid idea" (wazo la kijinga sana hili).

Ushauri wangu katika hili: Serikali kupitia Wizara yako ifanye kila liwezekanalo kuziwezesha Shule zote Tanzania ziwe zinatoa pia Elimu ya Ufundi na ujuzi mbalimbali e.g Mechanics, Driving, Ushonaji, Muziki, Uchongaji, Seremala, Kompyuta na kadhalika ili kutatua tatizo la ajira nchini. Hapo hata mwanafunzi anayefeli hatakosa cha kufanya maana atakuwa ameshika hata ujuzi mojawapo. Hii itasaidia kupunguza wavuta bangi na wadangaji mitaani.

Tanzania sio ajabu kukutana na kijana aliyemaliza kidato cha sita ambaye ukitoa theory ya masomo aliyosoma darasani, hakuna ujuzi au taaluma nyingine anayoijua. Kiufupi hakuna kitu kingine anachoweza kufanya zaidi ya notisi alizokariri. Kwa namna hii hatuwezi kufika Mheshimiwa waziri na adhima ya Mhe, Raisi ya KAZI IENDELEE! Itabaki midomoni tu.

Tunapowaambia watanzania KAZI IENDELEE, lazima tuwe tuna uhakika tumewafundisha kazi za kufanya tofauti na hapo tusishangae kuona vijana wanashinda office za betting wakitegemea maisha ya kubahatisha kila siku bila kuwa na uhakika na kesho yao.

MISHAHARA YA WAALIMU
Ni dhahiri kuwa sio rahisi kufanya kazi kwa ufasaha huku ukiwa na njaa kali, nafikiri hata wewe unalijua hilo. Waalimu ndio chanzo cha taaluma zote unazozifahamu; Nesi, Daktari, Askari, Mwanajeshi, Mbunge, Waziri mpaka Raisi wote hupita katika mikono ya waalimu. Sasa;

3. Kwanini hamtaki kuwalipa mishahara mizuri Waalimu wakafundisha kwa moyo mmoja na kuzalisha wataalamu zaidi?
Kwanini Madai na Malimbikizo ya Mishahara yao yanasuasua kulipwa?
Kwanini hamtaki kuwaboreshea makazi na mazingira yao ya kufundishia?

Nilipojaribu kupitia wasifu (CV) za viongozi mbalimbali nchini nikagundua kuwa wengi wenu ni waalimu kitaaluma, hata; wewe (Prof Ndalichako), Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa) na aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania awamu ya tano, Hayati Mhe. John Pombe ni waalimu kitaaluma. Napata mashaka kidogo, kwanini hamzikumbuki changamoto wanazokumbukana nazo waalimu ikiwamo mishahara midogo isiyokidhi na mazingira duni ya kuishi na ya kufundishia? Endelea kunisikiliza kwanza, majibu ya maswali yangu utanipa baadae.

UBOVU WA MITAALA
Siyo siri Mheshimiwa Waziri, Mitaala ya Elimu ya Tanzania ni mibovu. Wanafunzi wanasoma vitu vingi vilivyopitwa wakati na havina tija kwa taifa kwa sasa. Kwa mfano, Mambo ya akina Zwangedaba, Ghana Empire, Ntemi System yanasaidia nini kwa sasa? Sina tatizo na somo la Historia bali kilio changu watoto wafundishwe Historia itakayowasaidia i.e. Historia ya ugunduzi wa teknolojia mbalimbali. Aidha tunawabebesha watoto mzigo wa kusoma mambo mengi kwa wakati mmoja kitendo kinachopelekea kuzalisha wasomi wababaishaji wasio wabobezi.

Tujiulize; Kuna hasara gani ikiingizwa Mitaala na masomo mapya yatakayosaidia kuongeza uzalishaji na kutatua matatizo current ili kuifikia azima ya Mheshimiwa Rais ya TANZANIA YA VIWANDA?

Kwa Mfano: Uti wa mgongo wa UCHUMI wa Tanzania ni KILIMO lakini je, SOMO la KILIMO bado linafundishwa shule za msingi?
Hatuko serious.

MUDA WA MASOMO
Kwa mujibu wa tafiti zilizofanywa na wanasayansi miaka ya hivi karibuni zinaonyesha kiwango cha kadirio la miaka ya kuishi kwa mtanzania (Life expectancy) kimeshuka sana. Mtanzania sasa hivi anakadiriwa kuishi miaka 47 tu. Sasa, kwanini serikali kupitia Wizara yako isipunguze miaka ya masomo ili kutoa fursa ya watu kuhitimu masomo mapema ili kumalizia maisha yao wakiwa kazini. Kwa Mfano ikawa:

Shule ya Msingi (PrimaryLevel)-Miaka Mitano (5 years)
Sekondari Msingi (Ordinary Level)-Miaka Mitatu (3 years)
Sekondari ya juu (Advanced Level)-Mwaka Mmoja (1 year)
Chuo/Chuo Kikuu (College/University Level)-Miaka Miwili (2 years).

Tofauti na ilivyo sasa mtu anatumia miaka kumi na nane (18 years) akiwa masomoni ukijumlisha na umri wa kuanzia shule anagota miaka 27 akiwa hajaanza kazi. Mbona nchi za wenzetu katika hili wamefanikiwa. Nakumbuka nikiwa sekondari kidato cha tatu nilishawahi kufundishwa na mwalimu wa kigeni mwenye degree (shahada) aliyekuwa na umri wa miaka 19 tu wakati huo mimi nikiwa nina miaka 18 pia. Mheshimiwa waziri sisi tunakwama wapi?

UDHAIFU WA ADVANCED LEVEL [KIDATO CHA 5-6]
Kuna wakati pia huwa nafikiria hakuna ulazima sana wa kuwa na elimu ya kidato cha tano na sita (Advanced Secondary Level) kwa hapa nchini, kwa sababu utolewaji wake hauna tofauti na ile ya kidato cha nne. Tunapotezeana muda tu, na kutengeneza taifa la wasomi mafundi wa kukariri.

Mimi nafikiri ingelikuwa bora zaidi, mwanafunzi akifaulu vizuri aende college level na baadae university level halafu yule aliyepata ufaulu wa chini may be ndio apite kidato cha tano na sita ili aongeze competence yake kabla ya kufika chuo kikuu.

Tukubali tukatae, Ukitaka kuniamini nisemalo, linganisha wanafunzi wawili waliofaulu vizuri: graduate wa diploma ya clinical medicine na graduate wa kidato cha sita mchepuo wa PCB, jaribu kuwalinganisha. Hao wote kimakaratasi wanahesabika wako sawa kwa sababu ACSEE is equivalent to DIPLOMA. Kati yao yupi ana sifa za kuajiriwa na kuhudumia jamii? Kiufupi elimu ya kidato cha sita ni upuuzi mtupu. Huwezi kumlinganisha kidato cha sita hata na graduate wa certicate level, huwezi. Kwa sababu aliyesoma certificate amesomea profession anaweza kuajiriwa kwa taaluma yake na akafanya vizuri. Je graduate wa kidato cha sita ataajiriwa wapi, na kazi gani?

Tuende mbele turudi nyuma, Elimu ya kidato cha nne ndio msingi mkuu wa Elimu ya Juu Tanzania. Kumbe tunapaswa kuhakikisha shule zetu zinatoa Elimu iliyojitosheleza. Nasikia hata jirani zetu Kenya wana mfumo kama huu ninaoupendekeza, hawana ujinga unaitwa Elimu ya Kidato cha sita (Advanced Secondary Education, ACSEE). Mwanafunzi akimaliza Form Four anaingia college level akimaliza anaweza kuamua kuendelea na University Level au akatafuta ajira, that’s it. Elimu ya Kenya imeendelewa kuaminiwa kuliko hata yetu, ni vigumu mtanzania ku-compete kwenye employment market na mkenya, mara nyingi tunashindwa kwa sababu hatuko competent.

KUBADILIKA BADILIKA KWA MADARAJA YA UFAULU
Swali langu jingine kwako mheshimiwa, ni mpaka lini mustakabali wa Madaraja ya Ufaulu katika Mitihani ya Taifa na mfumo wa Elimu kiujumla utaendelea kutegemea siasa za nchi hii? Huyu akiingia madarakani anapanga hivi, akija mwingine anapangua na kuweka vile atakavyo yeye. Je umeshajiuliza mpaka sasa tuna wasomi wa makundi mangapi Tanzania? Niandalie majibu tafadhali ila kwa sasa naomba uendelee kunisikiliza kwanza. Naomba nikukumbushe;

a. Tuna watu wana vyeti vya madaraja ya mfumo wa DIVISION ule wa zamani.

b. Tuna wasomi wetu wengine wana vyeti vya Mfumo wa G.P.A.

c. Tuna wataalamu wenye vyeti vya madaraja mapya ya mfumo DIVISION.

Na mpaka sasa hatuuji baada ya wewe kutoka ofisini, mtu gani mwingine atakabidhiwa rungu na atakuwa na mawazo gani. Kwanini kusiwe na madaraja ya ufaulu ya kudumu (standard grades) hata kama ni magumu watu watazoea na watapambana kulingana na hali halisi. Sasa hivi mnachinja mnavyojisikia, mkiamua wafaulu wachache mnajua pa kuwakamatia wanafunzi. Sawa mama ninyi ndio mmeshikilia mpini, wanyonge wenzangu wameshikilia makali ya panga, acha wawe wapole tu, hawana chaguo jingine. Kazi kwenu wasomaji, Mimi nilishachinjwa kivyangu tangu 2016 (Form IV) na 2019 (Form Six) nikamalizana na adui anaitwa NECTA.

NB: Kuendelea kupandisha madaraja ya ufaulu sio suluhu ya kuapata wasomi wenye tija kwa taifa. Bali ni kuwalazimisha wanafunzi kujituma kukariri zaidi kuliko kuelewa. Kamwe taaluma ya miaka minne (4 yrs) darasani sio busara kuipima kwa masaa matatu (3 hrs) kwenye chumba cha mtihani. Mimi nafikiri serikali ibuni mbinu mbadala za kuimarisha mifumo ya Elimu yetu.

Hongera kwa kusoma makala hii mpaka mwisho. Nifollow Instagram, username yangu ni emmapetertz au bonyeza link iliyopo hapa chini itakupeleka moja kwa moja kwenye akaunti utanifollow kwa urahisi zaidi.


Asante.

By: Emmanuel P. Peter Jr
Email: emmapeter759@gmail.com
Call/WhatsApp: +255 788000273
Emma Peter Ink.
 
Back
Top Bottom