SoC01 Ushairi: Kulinda maadili na kupinga udhalilishaji

Stories of Change - 2021 Competition

AbduAbdulla09

New Member
Sep 6, 2021
4
9
Kutokana na kukithiri kwa udhalilishaji na kuyasahau maadili yetu . Nimeamua kuja na makala ya ushairi yashajihishayo kulinda maadili na kupinga udhalilishaji

TUYALINDE MAADILI KUPINGA UDHALILISHAJI

Bismillahi awali ninaandika shairi
Naandika bila ukali maneno yangu mazuri
Naituliza akili yapate kaa vizuri
Linda yetu maadili pinga udhalilishaji



Nasimama mbele yenu huku namwomba Manani
Niweze kusema kwenu maneno yenye mizani
Nanyi awajaze tunu nisemapo yashikeni
Linda yetu maadili pinga udhalilishaji



Lengo hasa madhumuni wezangu ninawambia
Yaliyo mwangu nyoyoni nataka wasimulia
Yapaswa tuyatunzeni na kazi kuyafanyia
Pinga udhalilishaji linda yetu maadili



Ya sasa na ya dahari leo nataka wambia
Yalo siri na dhahiri nataka kuyafichua
Wazee wana kariri vibaya twajivalia
Linda yetu maadili pinga udhalilishaji


Utamaduni ni kama tuutendao nchini
Nchini twacheza ngoma za babu wa asilini
Hima tusirudi nyuma jama mbele tusongeni
Linda yetu maadili pinga udhalilishaji


Tumesahau ya kale ya sasa twayapania
Twakumbuka enzi zile za bibi wakitwambia
Fanya hiki acha kile heshima kujitunzia
Linda yetu maadili pina udhalilishaji


Tusifu kwa kuonesha bayana na hadharani
Tufungue matamasha tuoneshe vya zamani
Kwani inafurahisha tunapoona machoni
Pinga udhalilishaji linda yetu maadili



Watu wa kiafrika tutunze utamaduni
Walio acha makaka na mababu wa zamani
Ili tupate Baraka za mola alo mbinguni
Linda yetu maadili pinga udhalilishaji



Pale mwanzo vibaraka wale wa kaskazini
Walisema takataka mila zetu mila gani
Haikuwa kweli aka ukweli ni kuthamini
Linda yetu maadili pinga udhalilishaji



Tulinde kwa kuuremba na kufunza mashuleni
Na midomoni kuimba na huko maredioni
Mila zetu kuzipamba ni fahari si huzuni
Linda yetu maadili pinga udhalilishaji



Kila kukicha jamani ni afadhali ya jana
Tivii na redioni waharibiwa vijana
Ni yepi yetu maoni twalia ama twasema
Linda yetu maadili pinga udhalilishaji



Tuwache kuwarubuni kwani wamekosa kipi
Kujifanya ni wahuni kwa kuwahonga na pipi
Huoni ni ukisirani jamiii yaenda wapi
Linda yetu maadili pinga udhalilishaji



Leo twazizima ndoto walizo nazo vijana
Twawabebesha mazito mwisho wanaacha soma
Kuwapa ujauzito watoto waitwa mama
Linda yetu maadili pinga udhalilishaji


Hawachagui kaumu wote wana dhalilishwa
Wanyama na binadamu wote wana najisishwa
Wengine hupewa sumu yao kuyafanikisha
Pinga udhalilishaji linda yetu maadili


Wanawake wanaume wote wameharibika
Jama tusimame shime kuyaondosha mashaka
Ukatili tuuhame ili tupate Baraka
Linda yetu maadili pinga udhalilishaji


Watoto wetu wadogo nao pia wanabakwa
Na kuchezea kipigo mbele nyuma wanashikwa
Hua ni tirigi vyogo aibu ndo hutushika
Pinga udhalilishaji linda yetu maadili


Sharti na tuyaseme midomo tusiifumbe
Kidete na tusimame tuyakalie kimbembe
Ukatili na ukome tuukate kwa viwembe
Linda yetu maadili pinga udhalilishaji


Tena ndime asharati tahata mburi akale
Kana badili ja shati mpaka vijana kele
Kazidi uafiriti ta vya tumboni avyale
Linda yetu maadili pinga udhalilishaji


Sisi tutawaapiza wajione ni najisi
Tena tutawatangaza mabarazani kwa kesi
Wala hatutonyamaza kimya kina wasi wasi
Linda yetu maadili pinga udhalilishaji


Jama tupaze sauti zifike hadi majuu
Tuanzishe na kamati hadi makao makuu
Maovu kuyadhibiti ili tupate nafuu
Linda yetu maadili pinga udhalilishaji


Maadili yajifichi tangu uwazi ungile
Ela sasa tuyavishi wajane wamama tele
Na sababu hatarishi utamaduni tugele
Linda yetu maadili pinga udhalilishaji


Nasifu tunapocheza magoma ye ya zamani
Huwa mifano ya chaza au kaa baharini
Hakika inapendeza anaebishaa ni nani
Lindayetu maadili pinga udhalilishaji


Na mambo haya mawili makubwa afrikani
La kwanza zetu methali za kale za uzeeni
Na pili vitendawili fumba fumbo fumbueni
Linda yetu maadili pinga udhalilishaji


Na hadithi vile vile ziwemo humu kundini
Hadithi za toka kale zinatufunza juweni
Tongoweni kama vile alikua mzamani
Linda yetu maadili pinga udhalilishaji


Maadili ndio ngao yapaswa kuyahimiza
Tuvae sitara nguo ubakaji kutuliza
Tuepuke machafuo ambayo yatumaliza
Linda yetu maadili pinga udhalilisahaji



Sitara kubwa kuvaaa vazi refu miguuni
Msiige bia njia wazee kunradhini
Vazi refu kulivaa ni sitara muilini
Pinga udhalilishaji lindayetu maadili


Kuvaa fupi si njia huo ni u kisirani
Baya ni baya tambua ingawa la uzunguni
Hujahoji kwa hatua mja rudi kwa manani
Linda yetu maadili pinga udhalilishaji



Moto usipochochea hufukutia mekoni
Bali uki upepea unazidi muwakoni
Vivyo nguo kupania mwazidisha matamani
Linda yetu maadili pinga udhalilishaji



Ni wengi wanaovaa kanzu na kushusha chini
Wake na waume pia waendao macho chini
Wengi zimewapamia motakaa za njiani
Linda yetu maadili pinga udhalilishaji


Baibui za sitara zapandishwa magotini
Kanga ndefu barabbara hazishushwi miundini
Ukiwambia wafura eti wapo uzunguni
Linda yetu maadili pinga udhailishaji



Siwafanyii hasira kutia mambo kichwani
Nawaunza yalo bora maovu yatue chini
Huoni hizi hasara tutembeapo njiani
Linda yetu maadili pinga udhalilishaji


Shungi kufunika sura jambo zuri lenye shani
Mja hapauki sura kwa jua barabarani
Ipi apate madhara na aonea tunduni
Pinga udhalilishaji linda yetu maadili



Jambo hili la busara hupunguza matamani
Linazuia fikira mbaya kupenya moyoni
Wanawake wa sitara waheshimiwe njiani
Linda yetu maadili pinga udhalilishaji



Wasubiri kulemaa ndipo uvae za chini
Watu wasije kujua una ulema mwilini
Kumbe una jikudia wakujue rasmini
Linda yetu maadili pinga udhalilishaji


Heshima kitu muhimu jamii nina wambia
Hili ni letu jukumu wajibu kutimizia
Maadili kuyahimu tena ya kitanzania
Linda yetu maadili pinga dhalilishaji


Mola katupa hekima na busara na elimu
Ametupa takrima kujua chungu na tamu
Katujalia kupima kwa mizani ya fahamu
Linda yetu maadili pinga udhalilishaji


Udhalilishaji nchini tupinge kwa nguvu zote
Utokomee mbalini ufukiwe usitoke
Ukomeshwe duniani tuwe ahueni sote
Pinga udhalilishaji linda yetu maadili


Pinga udhaliishaji pale ulipo popote
Kama wewe mtendaji usiogope chochote
Na nyinyi watangazaji endeleeni msichoke
Linda yetu maadili pnga udhalilishaji


Wasalamu ninatoa ni mwisho wa kutamka
Yangu haya fikiria zinduka mja zinduka
Kheri tupu mekwambia shika yangu ukitaka
Twaomba kwako Rabuka khusnil khatimia



Tamati beti tufiki mambo sheti tupambile
Sumu ya kweche hilaki ni samaki na komale
Mno uchu wa samaki hadhari bunju na ngole
Msiache kushitaki chini mpka kilele


Alietunga shairi jina Abdurahima
Sisemi ka ni mahiri ni kwake tu kujituma
Mungu anilipe kheri mbele nisirudi nyuma
Niwe mtunzi mzuri kwa uma ulosalia
 
Back
Top Bottom