Wazazi tukumbuke kuimarisha misingi ya maadili mema kwa watoto wetu si jambo linalofanyika mara moja, bali ni mchakato endelevu

Miss Zomboko

JF-Expert Member
May 18, 2014
4,502
9,280
Maadili na tabia njema huchangia kwa kiasi kikubwa katika kujenga na kuimarisha jamii yenye amani na umoja. Tunapolea watoto katika misingi ya maadili mema na tabia njema, tunaimarisha uelewa na uwezo wao wa kupambanua matendo mema na mabaya.

Pamoja na hivyo, wazazi tunapaswa kuwajengea watoto mtazamo wa kutambua kua maadili na tabia njema si kanuni na sheria tu, bali ni mwenendo na tabia nzuri. Kwa sababu hii, wazazi tunapaswa kuanza kujenga misingi imara ya maadili mema tangu mtoto akiwa na umri mdogo kama wasemavyo Waswahili, samaki mkunje angali mbichi.

Wataalamu wanasema ni muhimu kutambua kwamba, marafiki na mitandao ya kijamii kama X, Instagram na Whatsapp ni vichochezi vikubwa katika kubadilika kwa tabia na maadili ya mtoto.

Mtoto anaweza kubadili tabia yake ili tu akubalike na marafiki wanaomzunguka, hivyo basi, wazazi tunapaswa kuweka misingi imara ili kuhakikisha mtoto ana uwezo wa kusimamia misimamo yake hata kama ni kinyume na ile ya marafiki zake.

Kuna baadhi ya njia ambazo tunaweza kuzitumia kuimarisha misingi ya maadili na tabia njema kwa watoto wetu.

Kwanza, tujizoeshe kuwaonesha watoto tabia zipi ni sahihi na zipi si sahihi kwa kuwaelekeza na kuongea nao. Mtoto hawezi kujua yaliyo mema na mabaya bila kuelekezwa, hasa pale akiwa katika umri mdogo.

Kwa kumuelekeza, ndipo mtoto anakuwa na utambuzi yakinifu kuhusu maadili mema. Njia mojawapo ya kufanya hivi ni kwa kutumia hadithi na michezo. Hadithi zinaweza kutoka kwenye vitabu vyenye simulizi kuhusu maadili na tabia njema au tunaweza kutumia mifano halisi ya maisha kupitia uzoefu wetu na kuyaishi kwa mfano sisi kama wazazi yale tunayowafunza watoto wetu.

Pili, tujifunze kumuelewesha mtoto umuhimu wa kuwa na tabia njema na faida zake katika maisha. Kuwa na mazungumzo ya namna hii kutawasaidia watoto kuelewa umuhimu wa kuonesha tabia nzuri na kutenda wema, kuheshimu wengine, na kuwa waaminifu, vyote ambavyo ni misingi ya maadili mema.

Tunaweza kufanya hivi pale akikosea kwa kumuelewesha kosa lake na kumuadabisha kwa namna isiyoumiza ambayo itamfanya ajifunze kutokana na makosa, na akifanya vizuri kumpongeza ili aendeleze tabia hiyo.

Pia, tujitahidi kuweka wazi matarajio yetu kwa watoto wetu. Tunapowaelekeza watoto maadili na tabia njema, tujitahidi kuwaelezea vitu na tabia tunazotarajia kwao. Je, ni nini hapaswi kufanya na kwa sababu gani, na je, akifanya kitu hicho, mama au baba watalichukuliaje?

Ni muhimu kutambua kwamba mtoto hujifunza zaidi kwa kuona, hivyo hatuna budi kuwa mfano bora wa tabia njema na maadili mema kwa watoto wetu.

Jambo lingine ni kuwa na mawasiliano yenye uwazi na watoto wetu ili wawe huru kujieleza na kutushirikisha katika maisha yao, wawe huru kutoa mitazamo yao juu ya jambo fulani, na wakati mwingine, kwa kupitia maongezi yetu hayo, tunawea kuwaelekeza watoto usahihi wa mambo watakayotushirikisha, kama yana maadili mema au la.

Tusisahau kusimamia matumizi ya teknolojia na mitandao ya kijamii. Kama tulivyosema hapo awali, katika ulimwengu huu wa sasa ni rahisi sana kwa watoto kuharibikiwa kupitia mitandao ya kijamii. Tunapaswa kutoa muongozo na kufuatilia mienendo yao kwenye mtandao ili kuhakikisha wanapata maudhui yanayofaa kulingana na umri wao.

Kuwaelimisha watoto kuhusu madhara ya matumizi mabaya ya mitandao na kusisitiza umuhimu wa kujenga tabia njema ni njia ya kuwapa ufahamu na kuwawezesha kufanya maamuzi sahihi na kuwa waadilifu mtandanoni.

Njia nyingine nzuri tunayoweza kutumia kuimarisha misingi ya maadili kwa watoto wetu ni kujenga utamaduni wa familia kushiriki katika shughuli za kusaidia jamii. Kwa mfano, kuwapeleka watoto kusalimia wagonjwa hospitalini, kutembelea vituo vya watoto yatima, au kushiriki katika miradi inayotoa mchango chanya kwenye jamii.

Hii itawasaidia watoto kujenga uelewa wa umuhimu wa kujali na kuthamini utofauti wa maisha, na pia kuwawezesha kugundua thamani ya kusaidia wengine. Kwa njia hii, tutawasaidia kujenga tabia ya kuwa na moyo wa kujitolea na kusaidia wenzao.

Wazazi tukumbuke kwamba kuimarisha misingi ya maadili mema kwa watoto wetu si jambo linalofanyika mara moja, bali ni mchakato endelevu unaohitaji uvumilivu na umakini.

Ni muhimu kuzitekeleza mbinu hizi mara kwa mara kama azimio letu ni kujenga misingi imara ndani ya akili za watoto wetu. Tukifanya hivyo, basi mafundisho ya maadili yatakuwa sehemu ya utamaduni wa maisha yao ya kila siku, na hivyo kuwawezesha kukua na kuendeleza tabia njema na maadili mema.


Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto.
 
Ninashauri pia sheria za ulinzi wa mtoto ziongeze makali. kuna watoto wengine ni yatima, hawana mtu wa kuwalea kwa karibu hivyo, na wanadondokea kwenye mikono ya mashetani, na kujikuta wamekuwa sivyo walivyotakiwa kuwa. Mungu waokoe watoto wetu.
 
Back
Top Bottom