Unafiki kwenye siasa zetu na hatma ya maisha yetu; tukiendelea hivi ni suala la muda tu, kila mtu atalia kwa wakati wake

Azizi Mussa

JF-Expert Member
May 9, 2012
9,172
7,429
Dunia kwa asili yake ina machanguo mawili, wema au ubaya, haki au dhuluma, ukweli au uongo, unafiki au kutokuwa mnafiki, na kila mtu au jamii ina hiari ya kuchagua upande. Aidha, kila mbegu ioteshwayo na mtu mmoja mmoja, kundi au jamii huzalisha matunda yafananayo na mbegu husika. Kinachotokea tu ni kwamba mbegu hiyo hujiongeza ‘multiply’ na kuzalisha matokeo mara mia kwa maelfu.

Tumechagua kuwa jamii ya watu wanafiki. Wnasiasa wengi wao wanafiki, wanachama wengi wao wanafiki, washabiki wanafiki, waliokaa kimya wanafiki, wanaoongea wanafiki yaani karibu kila mtu mnafiki na anajijua kuwa ni mnafiki na pia anajua wenzake ni wanafiki ila kila mtu anajifanya kama vile hakuna tatizo.Tunasahau kwamba siasa ya taifa lolote ndio huamua mueleko wa watu wa taifa hilo, kwa hiyo inapokuwa imesismama juu ya msingi wa unafiki jamii husika inahatari ya kujikuta kwenye balaa kubwa.

Katika hili, hakuna chama kinachoweza kudai kwemba eti chenyewe hakina tatizo hili, ukiona kinadai hivyo au wanachama wake wanadai hivyo huo peke yake ni ushahidi wa unafiki wa anayedai.

Matokeo yake sasa, hakuna mtu anayesema ukweli wala kutetea jambo la maana. Ukiona mtu anasema jambo katika uzuri wake au ubaya wake, ujue kuna namna ameona linamnufaisha au linanufaisha watu wake wa karibu au kundi lake. Ukiona pia mtu anapinga jambo kwa uzuri au ubaya wake, ni kwa sababu kuna namna linamuumiza au limeumiza mtu wake wa karibu au wa kundi lake. Hali hii inasababisha kwenye jamii tusiwe na kitu kibaya wala kizuri bali uzuri ni pale ninaponufaika mimi au watu wangu wa karibu na ubaya ni pale ninapodhurika mimi na watu wangu wa karibu.

Hatimae, hatusemi kweli wala kuchukua hatua zitakazosaidia tuwe na jamii ya kusimamia haki na kukemea na kuzuia dhuluma katika upana wake.

Matokeo yake, mtu akiona mwenzake anaumia, anadhulumiwa au anaumizwa maadam muhanga sio mimi, sio mtu wangu wa karibu au wa kundi langu, naamua kukaa kimya, kushangilia, au kupuuzia kama hakuna shida ya msingi.Hili tatizo linakuwa siku hadi siku.

Ikitokea siku mimi ndio naumia, nadhulumiwa au naumizwa, ninakuwa nalia kwa uchungu, sio kwa sababu napinga dhuluma au kuumizana, bali kwa sababu kwa wakati huo mimi ndio naumizwa. Hayo yakitokea, wengine nao wanajiuliza kwani ni mimi? Kwani ni mtu wangu wa karibu? Kwani huyu wa kwetu? Hivyo hivyo na mzunguko unaendelea hadi kila mtu zamu yake ikifika inakuwa hivyo hiyo.Kwa bahati mbaya zaidi, hata wakitokea wakunisaidia, na mimi nikitoka kwenye uonevu, hata kama walionisaidia nao wako kwenye maumivu yalijotokana na uamuzi wao wa kunisaidia; nalala zangu mbele nawatosa, kwa sababu hiyo hiyo ya tatizo la unafiki. Hali hii hupelekea kutoaminiana kwa sababu anayeaminiwa naye haaminiki.

Ndugu yangu unayesoma hapa:

Acha kusema ukweli ukiona mwenzako anaumia au kuumizwa ila ujue ipo siku utaumia au kuumizwa na hakuna atakayesema ukweli.

Shangilia na kucheka wakati unaona mwenzako anaumia au kuumizwa ila ipo siku utaumia au kuumizwa na wakati unalia wengine watakuwa wanashangilia na kucheka huku nao kila mtu akisubiri muda wake ufike aumie au kuumizwa ili wengine washangilie na kucheka

Sema ukweli unapoona unanufaika, ila ujue wengine nao watasema ukweli wanaponufaika na hakuna atakayesema wakati unaumia au kuumizwa.

Ni suala la muda tu, tunaposema unafiki ni tatizo kubwa, kuna watu wanaona kama ni mzaha lakini matokeo yake katika hatua ya juu kabisa ni maangamizi makuu kwetu sote. Ni suala la muda tu, tuendeleeni kushindana kwa kuendekeza unafiki ila kila mtu atalia kwa muda wake, na anayemliza mwenzake leo au kushangilia mwezake akilia au kukaa kimyaa, atalia kesho huku wengine wakiwa ndio wanaomliza, washangiliaji au wakiwa wako kimya.

Ndugu zangu, tumechagua unafiki kuwa msingi wetu mkuu ila unafiki ni njia mbaya. Ni njia kuu ya maangamizi itakayotumaliza sisi wenyewe kila mtu kwa wakati wake. Kwa atakayeona inaleta maana, ni bora akabadilika na kusaidia kutoa elimu na hamasa ya kuwabadili wengine. Akafanya jitihada ya kupanda mbegu mbadala kulingana na ukubwa wa shamba lake na uwezo wake.

Vinginevyo, tuendeleeni, kushangilia, kukaa kimya, kunafikiana, kulumbana ujinga, kushabikia upuuzi, kila mtu kumlaumu mwezake, kila mtu kufikiria kujinufaisha kwa kusababisha maumivu kwa mwenzake, ila kila mmoja wetu atalia muda wake ukifika na hakuna atakayejali. Hili ni hakika, ni swala la muda tu!.

Kupanga ni kuchagua, ama kutumia akili na busara tulizopewa na Mungu, au kuendelea kujitia ununda ila nunda wa leo, ndio atalia kesho na nunda wa kesho atalia kesho kutwa, na hili linamuhusu kila mmoja wetu. Hakuna atakayeweza kulikwepa kama hatutapanda mbegu mbadala. Hata anayemliza, kumdhulumu au kumuumiza mwingine leo, muda wake ukifika naye atalizwa, kudhulumiwa au kuumizwa. Huo ni mfumo wa maumbile ya dunia. Tujitafakari sana!


Mambo yote ya kushangaza, kusikitisha, kuhuzunisha, kuudhi na kutia aibu ambayo yanatokea mara kwa mara ni matokeo tu, ni kama homa kwenye mwili wa binadamu lakini mzizi wa tatizo ni kitu kilichojificha; unafiki wetu.
 
Back
Top Bottom