SoC03 Umuhimu wa matunzo kwenye hifadhi za barabara Tanzania

Stories of Change - 2023 Competition

Safari79

Member
Sep 15, 2022
6
7
Utangulizi
Hifadhi nyingi za barabara nchini Tanzania zimeingiliwa kwa matumizi mbalimbali ya wananchi wakiwemo wafanyabiashara na watoa huduma wadogo wadogo wakati na wakati mwingine wale wakubwa.

Maeneo kama Tegeta kwa mfano, ama Bunju ama Banana ama Gongo la Mboto ama Mbagala kumekuwapo na wafanya biashara wengi sana katika huifadhi ya barabara. Lakini swali la kujiuliza hapa, ni kitu gani kinachosabaisha watu kujiweka katika hifadhi za barabara?

Nimewahi kufanya kazi Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam na kubahatika kujifiunza kuwa kuna wafanya biashara wengi kutoka Zimbabwe, Comoro, DRC na kwingineko wanaokuja Kariakoo kwa lengo la biashara. Lakini ukitazama mazingira ya biashara yaliyopo hapo Kariakoo utashangaa!

Changamoto
Mbali na kwamba baadhi ya barabara zina alama kuonesha ukingo wa hifadhi, bado watu wengi wamekuwa na uthubutu wa kuingia kwenye hifadhi na kufanya watakacho.

Hii imeleta changamoto kubwa sana kwa watumiaji wa barabara wakiwemo waenda kwa mguu, waendesha baiskeli, ama pikipiki hata wenye malengo ya kufanya mazoezi ya kukimbia ama kutembea.

Kwa kiasi kikubwa matumizi haya mabovu ya hifadhi za barabara sio tu yamechafua mazingira ya uso wa nchi bali pia yameondoa ustaarabu ambao umekuwa ukizungumzwa vizuri na wageni wanao tembelea Tanzania.

Kariakoo kwa mfano, eneo ambalo limekuwa likitiumika na wafanyabiashara wengi kutokea nje ya nchi, barabarani kumekuwa na wafanyabiashara wengi waliotanda sio tu kwenye hifadhi za barabara bali pia na kuziba kabisa njia za wagari na hivyo kuzuia kwa kiasi kikubwa upitishaji wa mizigo wakati wa kwenda na kutoka madukani.

Nimekuwa nikifuatilia mwenendo wa kampuni za usafi wa barabara, wengi wao wanachelewa kubeba taka zinazokusanywa kwa wakati, wengi wa wafanyakazi wamekuwa wakitupa mchanga pembezoni mwa barabara ama kwenye bustani zenye majani badala ya uchafu husika kukusanywa na kutupwa panapohusika.

Kampuni nyingi zinatopewa kazi ya kupanda miti ama majani zinashindwa kutunza majani husika ama miti husika kwa kumwagilia ama kuwekea mbolea ama kuwekea miti ya kuikinga isikanyagwe na watumiaji wa barabara.

Maswali ya kujiuliza
Tunawezaje kuitangaza kariakoo ama kuifanya kuliendeleza eneo hili ili liendelee kuwa soko kubwa la kimataifa kwa kuchochea wafanya biashara wa zamani na wapya kutoka nchi jirani kuja na kufanya manunuzi kwa ukizingatia vurugu za karioakoo zilizopo na ukizingatia hakuna mpango wa kuziondoa na kuweka ustaarabu?

Ni lini sasa tutakuwa na suluhisho la kudumu la kuondoa na kudhibiti biashara na huduma zote zisizo na mahusiano na usafiri katika hifadhi za barabara zetu Tanzania? Maana mvua ikinyesha mjini ni shida na jua likiwaka mjini napo ni shida.

Tunahitaji tamko la aina gani ya suluhisho katika kurudisha ustaarabu na kupendezesha njia zetu za barabara? Tunamhitaji nani ili aseme nini? Maana kupanga ni kuchagua. Kila mtu katika utawala wake aje kujivunia kwa kuchukua hatua katika kulinda na kupendezesha miji yetu.

Ni lini tutarudia kikamilifu harakati za kutuunza mazingira kwa kupanda miti ama maua ili kupendezesha miji yetu na kukinga waenda kwa mguu na jua kali haswa nyakati za mchana?

Tunawezaje kuwa na wafanya biashara ndogo ndogo wanao thamini na kutunza hifadhi za barabara nchini Tanzania bila kuzua tafrani na kusababisha madhara kwa pande zote zinazohusika?

Je kuna changamoto ya utashi wa kisiasa katika kutunza hifadhi zetu za barabara Tanzania? Maana inawazisha pia kuwa pengine wenye mamlaka wanashindwa kutimiza waji bu wao kwa kuhofia kuchukuliwa hatua kwa kuwaondoa wafanya biashara katika maeneo yao pembezoni mwa barabara.

Je kuna pesa ngapi zilizotumika katika uhifadhi wa mazingira na kupendezesha miji lakini hazijasaidia katika utunzaji wa barabara zetu na upendeshaji wa miji yetu?

Mamlaka zetu
Mamlaka zetu za barabara kama TANROADS na TARURA zimetumika vipi katika kulinda na kuzisimamia barabara zake ili zisiingiliwe kwa matumizi ambayo hayakupangwa wakati wa ujenzi?

Vipi pia kuhusu mipango miji na mamlaka zingine za serikali kama Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Wizara ya kazi na Ajira, na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi. Wamefanukiwa vipi katika kuweka ustaarabu mzuri wa biashara na huduma kando ya barabara zetu?

Fursa mbele yetu
Naamini kuwa kuna nafasi ya kuboresha hali ya mambo na kututoa tulipo kwa kuzuia wafanya biashara kuvamia na kutumia maeneo ya barabara kama wapendavyo wao. Huu sio ustaarabu na hatupashwi kujifanyia mambo pasipo utaratibu.

Kuna haja ya kuhamisha wakazi katika maeneo yaliyotekwa na wafanya biashara na kuyatenga maeneo hayo kwa matumizi ya biashara? Maana inawezekana ni rahisi sana kuhamisha wafanya biashara kutoka sehemu moja kwenda nyingine lakini ni ngumu sana wakati huo huo kupingana na mazoea ya watu kwa kuhamisha biashara.

Mfano huu unaweza kutumika kwa uzoefu wa kuhamishwa stendi ya Ubungo na kuelekea Mbezi. Ijapokuwa stendi imehamishwa lakini mazoea bado yanataka huduma hiyo iwepo maeneo ya Ubungo ndio maana ofisi nyingi za mabasi bado zinafunguliwa Maeneo ya Shekilango, Manzese, Urafiki na hata RiverSide.

Kuna umuhimu wa kuwapatia watunza bustani nafasi ya kutunza miti na majani yaliyopandwa pembezoni mwa barabara kwasababu tayari wanabidhaa husika, pili wako jirani na maeneo hayo lakini tatu ni sehemu ya kuwajengea uwezo na kuwainua kiuchumi. Hivyo wakiwa wanalipwa kila baada ya miezi 2 kwa mwaka mmoja kutahakikisha miti na majani yako vizuri.

Hitimisho
Inawezekana maboresho haya yasifanyike kwa wakati mmoja kwa barabara zote Dar es Salaam ama Tanzania yote, lakini kila barabara inaweza kuwekewa mpango na maboresho vizuri ili kusiweko na athari kwa upande wowote ili biashara ya soko ikae vizuri, maegesho ya teksi ama bodaboda yakae vizuri na kadhalika na kadhalika.

Tunahitaji mjadala wa aina fulani ili pamoja na mambo mengine usaidie katika kuboresha mawazo haya na mengine ili kupunguza kero za watumia barabara lakini pia katika kupendezesha miji yetu hapa Tanzania.
 
Back
Top Bottom