Uchaguzi Busanda: Majigambo, Uteuzi na Kampeni kuelekea uchaguzi

Date::5/7/2009
Malecela, Msekwa wazomewa Nyarugusu katika kampeni

Na Frederick Katulanda, Busanda

Mwananchi

KAMPENI za uchaguzi za CCM katika uchaguzi mdogo wa jimbo la Busanda jana zilizidi kukumbana na upinzani mkali baada ya makamu mwenyekiti wa chama hicho, Pius Msekwa na makamu mwenyekiti wa zamani, John Malecela, kujikuta wakizomewa wakati walipokuwa wakijinadi katika mkutano uliofanyika Nyarugusu wilayani Geita.

Mbali na vigogo hao wa CCM, mgombea wa chama hicho katika uchaguzi huo mdogo, Lolencia Maselle Bukwimba na mumewe, Maselle Buziku walizomewa wakati walipotambulishwa kwenye mkutano huo wa kampeni.

Tukio hilo limetokea siku moja baada ya chama hicho kujikuta kikiwa na watu wachache wakati wa kuzindua kampeni zake kwenye kata ya Kaseme, tofauti na mikutano ya vyama pinzani vya Chadema na CUF.

Dalili za hali mbaya katika mkutano huo zilianza wakati viongozi hao wakiingia eneo la Nyarugusu ambalo ni maalumu kwa wachimbaji wa dhahabu. Viongozi hao walipokelewa na alama ya vidole viwili kila walikopita. Alama ya vidole viwili hutumiwa na Chadema.

Zomea zomea hizo ziliwakabili viongozi hao wa CCM wakati walipokuwa wakimnadi mgombea wao. Hali mbaya ilianza kwa katibu mwenezi na uhamasishaji, Simon Mangelepa wakati aliposimama jukwaani na kuanza kuwatambulisha wageni walioambatana nao na kufuatiwa na mbunge wa viti maalum mkoani Mwanza, Maria Hewa ambaye alizomewa baada ya kuwaeleza wananchi kuwa wanapaswa kutulia.

Kutokana na hali hiyo mwenyekiti wa CCM mkoani Mwanza, Clement Mabina alisimama jukwaani kabla ya kumkaribisha Malecela ili amnadi mgombea wa chama hicho na kuwaeleza kuwa anazo taarifa kuwa kuna watu ambao wamepangwa hapo kwa ajili ya kuzomea, naye kuzomewa.

Baadaye ikawa zamu ya Malecela ambaye baada ya kusimama jukwaani aliwaeleza wananchi kuwa shutuma za ufisadi hazina nafasi katika kampeni kwa sasa na kuwataka wenye ushahidi wa ufisadi kuupeleka polisi, kauli ambayo iliwafanya wananchi ambao walikuwa wametulia, kuanza kuzomea wakimtaka aondoke huku wakionyesha vidole viwili.

Hata hivyo, Malecela aliwatuliza na kuwaeleza kuwa hiyo ndio njia sahihi ya kushughulikia mafisadi na kuendelea kuwaeleza wananchi kuwa iwapo wataichagua CCM katika uchaguzi huo watapatiwa umeme pamoja na kutengewa maeneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo.

"Nataka kuwaeleza iwapo mtamchagua mgombea huyu, basi serikali italeta umeme eneo hili….na kutenga maeneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo," alisema lakini akakatwa kauli na kelele za wananchi ambao walisema miaka yote wameichagua CCM na kuahidiwa mambo hayo bila ya kufanikiwa.

Kutokana na hali hiyo Malecela aliamua kuwatuliza na kuomba Busanda isigeuke kama Tarime na kwamba wao CCM wanataka kampeni za amani na utulivu.

Ndipo ilipofika zamu ya Msekwa kumnadi mgombea na baada ya kupanda jukwaani alimkaribisha mgombea aliyemsimamisha mumuwe, Maselle Buziku, ambaye naye alipoeleza kuwa iwapo watamchagua mkewe atatumia nafasi yake SEDA kuhakikisha wanapata mikopo, lakini akazomewa na wananchi hao.

Hata hivyo zomea zomea hizo hazikuweza kuhatarisha amani katika mkutano huo na mgombea huyo alijieleza bila ya matatizo na kupiga magoti lakini alipoomba kura, naye akajikuta anazomewa.

Katibu mkuu wa CCM, Yusuf Makamba amekiri kuwa kuna hali ngumu kwenye Jimbo la Busanda na kuwataka viongozi wa chama hicho kupigana kufa au kupona ili kuhakikisha jimbo haliangukii mikononi mwa upinzani kwa kuwa machungu ya kushindwa Tarime anayajua.

Kauli hiyo ilitolewa na Makamba juzi mchana wakati alipokuwa akizungumza na viongozi mbalimbali wa chama hicho katika mkutano wa ndani kwenye ofisi za CCM wilayani Geita baada ya kuwasili kwa ajili ya uzinduzi wa kampeni wa chama chake zilizofanyika juzi katika kata ya Kaseme.

Makamba alikiri kuwa hali ni ngumu na hivyo kuwaomba kila mmoja kuhakikisha mgombea wa CCM anashinda, akilalamika kuwa makali ya kushindwa alishayaonja Tarime.

Habari zilizopatikana kutoka ndani ya kikao hicho na kuthibitishwa na mmoja wa viongozi wa chama wilayani humo zimeeleza kuwa Makamba aliamua kufanya mkutano huo kwa lengo la kuwekana sawa kutokana na CCM kukabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa wale walioenguliwa katika kura za maoni za kuwania kuteuliwa kuwa mgombea wa chama hicho.

Makamba amesema "jamani kushindwa ni kubaya, mwenzenu Tarime nilionja ubaya wake mpaka ilibidi nitoroshwe na Green Guard ili kuepuka kuzomewa, sasa tusiposhikamana mambo yatakuwa magumu tutoe tofauti zetu,'" alisema mmoja wa wajumbe waliokuwa kwenye kikao hicho akimnukuu Makamba.

Hata hivyo, baada ya kauli hiyo Makamba alishtuka na kuhoji iwapo walikuwemo waandishi wa habari ukumbini humo na kuonya utoaji wa taarifa hizo baada ya kujibiwa hawakuwemo.

Aidha baada ya kujibiwa kuwa hakuna waandishi makamba alishtuka baada ya kubaini kuwa kulikuwa na mpiga picha wa chama na kumuagiza kuhakikisha mkanda huo anaukabidhi kwa katibu wa CCM wa mkoa.

Makamba alipoulizwa kuhusu suala hilo alijibu kuwa hajawahi kukiri kuwepo kwa hali ngumu kwa vile hana wasiwasi na uchaguzi huo na kusema alikuwa akieleza masuala ya kushikamana.

"Wewe unataka nikueleze mikakati yangu, kama nilikuwa nawahimiza watoto wangu kulima we unakutakia nini," alihoji katibu huyo wa CCM alipoulizwa na Mwananchi kuhusu kikao hicho.

Sambamba na hatua hiyo Makamba alimtaka mjumbe wa halmshauri kuu ya chama hicho mkoani Mwanza, Anthony Diallo kutumia uwezo wake kuhakikisha kampeni hizo zinakuwa na hamasa ya kutosha ikiwa ni pamoja na kurusha taarifa zake katika vyombo vya habari.

Uchaguzi katika jimbo la uchaguzi la Busanda umepangwa kufanyika Mei 24 kwa lengo la kujaza nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, marehemu Faustine Kabuzi Rwilombe.

Vyama vingine vinavyowania kiti hicho ni Chadema, CUF na UDP
 
CCM lazima sasa watambue kuwa watanzania si mabwege tena. Ahadi ya maisha bora kwa kila mtanzania kugeuka kuwa maisha bora kwa kila mwanamtandao sasa yatosha. Na bado mwakani ndo wataonja joto ya jiwe zaidi.
 
“Nataka kuwaeleza iwapo mtamchagua mgombea huyu, basi serikali italeta umeme eneo hili….na kutenga maeneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo," alisema lakini akakatwa kauli na kelele za wananchi ambao walisema miaka yote wameichagua CCM na kuahidiwa mambo hayo bila ya kufanikiwa.

Ina maana bwana Malecela anataka kuwaambia wananchi kuwa masharti ya kuletewa umeme ni kumchagua mbunge wa CCM?

Ina maana wananchi wakimchagua mgombea asiye wa CCM serikali itaacha kuleta umeme kwa sababu hiyo?

Huyu Malecela vipi?
 
Umeme imegeuka hongo, kule mbeya vijijini sijui kama wamepeleka,maana walisema wakati wa kampeni. Kuzomewa ni njia nzuri ya kufikisha ujumbe moja kwa moja kwa mhusika kwa sababu ni silaha inayobebwa bila kujulikana. Mwanzo mzuri Bagosha.
 
Heeee,heee.... safiiiiiii!! CCM watakoma kuringa,huu ni mwanzo tu!. Huyu mzee malecela haoni aibu kusema akichaguliwa wa CCM ndio umeme utapelekwa huko? Hivi kweli umeme ni ishu ya kupigia kampeni? Unahitaji kuwa na mbunge wa CCM kupata umeme? Inamaa km mbunge akiwa si CCM hao jamaa wataendelea kuishi gizani (kama si kutumia majenereta ya watu binafsi km kibondo)?
 
Tokea ianzishwe CUF imekuwa haipati cofreji ya maana katika vyombo vya habari apa tanzania hatuna vyombo huru vya habari si nipashe wala tanzania daima wala mwanahalisi.gazeti kidogo unaloweza kuliweka katika uhuru ni MWANANCHI.

Ni mafisadi ndo wamekuwa wakilisimamia hilo kwa ticket ya udini. na nyinyi kina mwanakijiji mkaingia kundini.

Cofreji?? una maana gani? Hata hivyo naona unataka kulazimisha watu kusapoti unachoona wewe ni sawa. Ukweli mara nyingi hujitenga na uwongo si kwa kulazimishwa mkuu!!
 
Ndipo ilipofika zamu ya Msekwa kumnadi mgombea na baada ya kupanda jukwaani alimkaribisha mgombea aliyemsimamisha mumuwe, Maselle Buziku, ambaye naye alipoeleza kuwa iwapo watamchagua mkewe atatumia nafasi yake SEDA kuhakikisha wanapata mikopo, lakini akazomewa na wananchi hao.

Yaani bongo tit for tat wazi wazi, hivi hakuna sheria dhidi ya rushwa hii ya kura?
 
Yaani nimefarijika saaaaaaana. Kwakeli Mungu ni mkubwa, watu wa Busanda mbarikiwe mno. Hapa kumekucha, mwendo mdundo, 2010 kama kumsukuma mlevi tu yaani, kwani hao viongozi wote hawataweza kujigawa majimbo yote ya uchaguzi Tanzania.

Bythe way, hawa wazee kama Malecela kwanini wanataka aibu ya uzeeni? si wangetulia tu wakastaafu na heshima zao kuliko sasa kuanza kuzomewa hovyo mtu ulisha wahi kuwa waziri mkuu? aibu gani sasa?

Tulia babu, ubaki na heshima yako, chama kina nuka hakibebeki tena, wacha kujitafutia aibu ya uzeeni.
 
Yaani bongo tit for tat wazi wazi, hivi hakuna sheria dhidi ya rushwa hii ya kura?

Yaani hadi Malechela, a previous presidential hopeful, anahonga umeme kwa kura? This is sad. Sijui mbunge wa same Mhe. Anna Kilango atasemaje kuhusu huu ufisadi wa waziwazi.
 
“Nataka kuwaeleza iwapo mtamchagua mgombea huyu, basi serikali italeta umeme eneo hili….na kutenga maeneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo," alisema lakini akakatwa kauli na kelele za wananchi ambao walisema miaka yote wameichagua CCM na kuahidiwa mambo hayo bila ya kufanikiwa.

Ndipo ilipofika zamu ya Msekwa kumnadi mgombea na baada ya kupanda jukwaani alimkaribisha mgombea aliyemsimamisha mumuwe, Maselle Buziku, ambaye naye alipoeleza kuwa iwapo watamchagua mkewe atatumia nafasi yake SEDA kuhakikisha wanapata mikopo, lakini akazomewa na wananchi hao.

Haya ni mawazo Mgando na yaliyopauka: Marekela kafanya nini hapo Mtera, Msekwa kafanya nini uko Ukerewe, kwa kweli hawa wazee wanawafanyia mbaya sana wananchi.
 
Nakumbuka wiki chache zilizopita niliwasihi wanaJF wasife moyo, uwezekano wa kuing'oa CCM upo in 2010, never underestimate the Tanzanian public. Watu wamechoka sana! They need real change and it is coming.
 
Nimesikia kuwa bwana mchonga njia/tingatinga kazomewa katika kampeni, hapa kuna mawili 1. watu wamechoshwa na uongo/ahadi hewa na ufisadi ndani ya chama tawala 2. Ni siasa chafu yaani kikundi cha watu kimeamua kuzomea tu ili kupigia kampeni chama kingine.

Ila kwa mwaamko huu natumaini uchaguzi ujao utakuwa wa kueleweka zaidi, kidogo kidogo mpaka kieleweke. Nafurahi haya yanatokea nje ya miji mikubwa ikianisha kwamba mjini watu watakuwa waelewa zaidi na kutoa hii FALME ya kifisadi madarakani.
 
Back
Top Bottom