Tamko la TAPO la Wanawake na Wasichana: Haturidhishwi na kasi ya mchakato wa kubadilisha Sheria ya Ndoa

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,815
11,991
TAMKO LA TAPO LA WANAWAKE NA WASICHANA KUHUSU MCHAKATO WA MABADILIKO YA SHERIA YA NDOA YA MWAKA 1971

Ndoa za utotoni ni tatizo kubwa nchini Tanzania linalo sababisha wasichana kutotimiza ndoto zao hasa za kielimu. Ndoa hizi mara nyingi husababishwa na hali duni za kimaisha, mila na desturi potofu, ukeketaji, ukosefu wa elimu juu ya madhara ya ndoa za utotoni n.k.

Kutokana na takwimu za TDHs za mwaka 2015/16 zinaonyesha wasichana 2 kati ya wasichana 5 wanaolewa kabla ya kufikisha umri wa miaka 18. Hii ni hatari sana na inapelekea idadi kubwa ya wasichana wadogo kupoteza malengo yao, haki zao za msingi na hata wengine kupoteza Maisha.

Kwa kuzingatia huu ni mwezi wa wanawake duniani, tumekuwa tukifanya shughuli mbalimbali zilizobeba kauli mbiu inayozungumzia umuhimu wa usawa wa kijinsia kwa maendeleo ya kesho. Hivyo basi, sisi kama tapo la wanawake na wasichana tarehe 10 Machi 2022 tulikutana kwa lengo la kujadili mambo mbalimbali yanayohusu ndoa za utotoni ambazo zimekuwa ni sababu kubwa ya kukatisha ndoto za wasichana na kama tunavyofahamu kwamba maendeleo ya wasichana yanahusiana na ujenzi wa mwanawake imara kwenye jamii ya sasa na ya baadae.

MCHAKATO WA MABADILIKO YA SHERIA YA NDOA
Mnamo mwaka 2019, Mahakama ya Rufani kupitia kesi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali dhidi ya Rebeca Gyumi ilitoa maamuzi ambayo yaliitaka Serikali ndani ya mwaka mmoja kubadilisha Sheria ya Ndoa na kuweka miaka 18 kama umri wa chini wa kuoa/kuolewa kwa wasichana na wavulana. Hata hivyo, mpaka sasa ni takribani miaka 3 tangu kutolewa kwa hukumu hii na bado Serikali haijatekeleza uamuzi huu. Pamoja na hayo, tumekuwa tukiona matamko mbalimbali ya Serikali kuhusiana na mwenendo wa mchakato wa mabadiliko ya Sheria hii ya ndoa lakini bado hatuoni maendeleo yoyote. Matamko haya ni yakiwemo;

“Serikali imeanza mchakato wa kupitia baadhi ya sheria ili zifanyiwe marekebisho na kuendana na wakati pia Serikali kupitia Wizara imeandaa mswada wa mapendekezo yamarekebisho ya Sheria ya Ndoa utakao wasilishwa Bungeni ili kuiboresha kwa lengo la kulinda makundi ya wanufaika wa Sheria hii.” Mh. Geofrey Pinda, Naibu Waziri Wizara ya Katiba na Sheria.

“Wizara ilianzisha mchakato wa marekebisho ya Sheria ya Ndoa hatimaye FEB/2021 Serikali iliwasilisha Bungeni mswada wa marekebisho ya Sheria ya Ndoa na kwakuwa marekebisho ya Sheria ya Ndoa yanahusisha jamii kiujumla wake, Serikali ilishauriwa kuwashirikisha wananchi ili kupata maoni kuhusu mapendekezo ya marekebisho ya Sheria hiyo. Hivyo, tarehe 17/3/2021 Wizara ilianza tena kufanya mikutano na viongozi wa dini na makundi mengine ilikupokea maoni husika na imeandaa mpango kazi wa kuyafikia makundi yote katika jamii ili kupata maoni yatakayo wezesha kupata Sheria iliyoridhiwa na wote.” Mh. Palamagamba Kabudi, aliyekua Waziri wa Wizara ya Katiba na Sheria.

MSIMAMO WETU

Kwa kuzingatia utawala wa Sheria na uwajibikaji wa mihimili yetu ya nchi, sisi kama tapo la wanawake na wasichana Tanzania haturidhishwi na kasi ya mchakato wa kubadilisha Sheria ya Ndoa. Aidha, tunapenda kuonyesha msimamo wetu kuhusu kutokukubaliana na msimamo wa Serikali kusema kwamba mchakato wa mabadiliko ya Sheria ya Ndoa umerudishwa kwa wananchi kabla ya kufanya marekebisho ya Sheria hii. Kitendo hiki ni kwenda kinyume na misingi ya utawala bora lakini pia, bunge kama chombo kilichopewa dhamana ya kutekeleza maamuzi yaliyotolewa na mahakama linakuwa halijatimiza jukumu lake la kikatiba.

Ikumbukwe kuwa Mahakama katika shauri la Rebeca Gyumi iliamuru Serikali kufanya marekebisho ya sheria ndani ya mwaka mmoja na kusahihisha vifungu vya kibaguzi vya 13 na 17 na kuweka miaka 18 kama umri wa chini unaostahili kwa ndoa kwa wavulana na wasichana.

Ucheleweshwaji huu wa kufanya mabadiliko haya muhimu yanawafanya wasichana kuendelea kupitia ukatili wa ndoa za utotoni sababu bado vifungu kandamizi vya Sheria ya Ndoa vinaendelea kuwepo. Na katika kipindi kifupi kati ya Novemba 2021 na Februari 2022 kuna matukio mengi ya wasichana kuozeshwa ambapo mengi yao yamepelekea vifo vya wasichana wadogo yakiwemo;

Taarifa ya kujinyonga kwa binti Rebeca Benjamini mkazi wa Mkoa wa Geita, Kata ya Izunya, Wilaya ya Nyang’hwale mwenye umri wa miaka 17 kulikosababishwa na msongo wa mawazo sababu ikiwa ni athari za kuolewa katika umri mdogo. ‘’Rebecca amefariki dunia baada ya kujinyonga hadi kupoteza maisha kwa kutumia Kamba iliyosukwa kwa chandarua kwenye kenchi ya nyumba yake, chanzo alikuwa alikuwa akilalamika kwamba kwanini kila akiolewa anaachika na tayari alikuwa aeshaachika mara tatu’’ Henry Mwaibabe, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita.

Taarifa ya kisa kilichotokea Mkoa wa Songwe, kijiji cha Ilanga, kata ya Mlale, kilichomuhusisha mtoto wa miaka 16 kumuua mkewe wa miaka 16 kisha kumchoma moto na kumtupa kwenye korongo.

Pamoja na tukio lililotokea Mkoa wa Kigoma, Kijiji cha Lufubu, Wilaya ya Uvinza, lililomuhusisha binti Mbaru Juakali(17) kulazimishwa kuolewa kwa ng’ombe 13, ambapo baada ya kukataa alipigwa fimbo na baba yake hadi kupelekea kifo chake.

Aidha pamoja na mifano hai hapo juu, zipo athari kubwa zaidi zinazowakumba wasichana kutokana na ndoa za utotoni ikiwemo athari za kiafya, kiuchumi, kijamii na hata kisaikolojia.

Baadhi ya athari hizi ni kama vile:​
  • Kupoteza fursa za elimu na ujuzi wa kazi​
  • Kupata maambukizo ya virusi vya ukimwi (VVU) au magonjwa ya zinaa (STD)​
  • Kunyanyasika kisaikolojia, kimwili na kijinsia​
  • Kuyumba kiuchumi na kudumu katika umasikini​
  • Vifo vya watoto wachanga na watoto wa kike pindi wanapojifungua kwa kuwa viungo vyao vya uzazi bado havijakomaa​
  • Kuongezeka vifo vya wajawazito​
  • Kuharibika kwa mimba​

HITIMISHO
Sisi kama tapo la wanawake na wasichana Tanzania tunahitaji kuona haya yafuatayo;​
  • Wabunge kupitia Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania wakitekeleze jukumu lao la kikatiba la kuitaka Serikali ilete mswada kwaajili ya mabadiliko ya Sheria ya Ndoa.​
  • Kamati ya Katiba na Sheria ambayo ina jukumu la kupitia na kupitisha miswada inayojadiliwa bungeni kuitaka Wizara ya Katiba na Sheria kuleta mswada wa mabadiliko ya Sheria ya Ndoa kwenye bunge hili la Aprili, 2022.​
  • Wizara ya Katiba na Sheria kusitisha mchakato wa kukusanya maoni kwa wananchi na kujielekeza kwenye kutekeleza maamuzi ya Mahakama Rufani kama Ilivyoelekezwa kwenye hukumu ya kesi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali dhidi ya Rebeca Gyumi.​

Imetolewa na;
  • Msichana Initiative Organisation.
  • Tanzania Women Cross-Party Platform (T-WCP/ULINGO)
  • Tanzania Feminist Initiative
  • Her-Ability Foundation
  • WAJIKI- Wanawake katika Jitihada za Kimaendeleo
  • TAWIA- Tanzania Widows Association
  • WiLDAF- Women in Law and Development Africa
  • TGNP- Tanzania Gender Networking Programme
  • Mtandao wa Wanawake na Katiba
  • Hope for Young Girls
  • Her Initiative
  • Soma
  • OYO- Open Youth Opportunities
  • JIDA -Jikomboe Integral Development Association
  • ICCAO- Integrating Capacity and Community Advancement Organization
  • TAMWA- Tanzania Media Women Association
  • Men Engage
  • C-SEMA
  • Mwanamke na Uongozi
  • Binti Makini Foundation
  • TECMN- Tanzania Ending Child Marriage Network
  • Women Fund Trust – Tanzania
  • Binti Salha Foundation
  • LHRC- Legal Human Right Centre

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Katiba na Sheria imeeleza kuwa Wizara inaendelea kukusanya na kuchambua moni kabla ya kuwasilisha Bungeni mapendekezo ya maboresho ya Sheria husika kwa ajili ya kuijadili na hatimaye kuipitisha
WhatsApp Image 2022-09-28 at 6.28.18 PM.jpeg

WhatsApp Image 2022-09-28 at 6.28.19 PM.jpeg

WhatsApp Image 2022-09-28 at 6.28.19 PM (1).jpeg

WhatsApp Image 2022-09-28 at 6.28.20 PM.jpeg
 
... kutapakaa kwa panya road, vibaka, na makundi ya vijana wasiotaka kujishughulisha na kazi rasmi za kuwaingizia kipato kama kilimo huchangiwa pakubwa na sheria kama hizo.

Ndoa za utotoni hazina faida zaidi ya kuongeza matatizo kwenye jamii. Sijui kwanini Serikali inakuwa na kigugumizi kurekebisha hiyo sheria.
 
hawa wanaharakati wanataka wakasagane tu hawana lingine. kuna watu wameoa na kuolewa wakiwa na 30+ lakini bado wanafanyiana vitendo vya kikatili sana
 
WALIANZA ZAMANI HUU UPUUZI WAO. hwataki mabinti waolewe, na wao wao karibuni tutakuja kuwaona wanapigania mashoga waolewe.
 
Back
Top Bottom