Taifa Katika Fedheha

Sumaku

Member
Feb 17, 2009
53
1
*Siasa zisizo na tija zaharibu haiba ya nchi
*Misuguano ya chama tawala yazua hofu
*Udhaifu wa wapinzani waacha ombwe
*Mdudu CHADEMA mkono wa kigogo?
*Halmashauri Kuu yasubiriwa kukata ngebe


Na Mwandishi Wetu

KURUSHIANA maneno ya hasira, chuki na visasi vya wanasiasa wenye mvuto na ushawishi ndani ya chama tawala – Chama Cha Mapinduzi (CCM) kumeiweka nchi katika fedheha kubwa.

Suala la kufikia hata waliokuwa viongozi waandamizi ndani ya chama au Serikali, kwa nafasi kama za Waziri Mkuu au za uwaziri na sasa kuirudi Serikali, chama au viongozi wenzao, ni mpasuko ambao usipoangaliwa utaendeleza fedheha hadi nchi kukosa sifa machoni mwa wawekezaji na wahisani.

Uchunguzi uliofanywa kwa muda sasa, umebaini kuwa hata Kamati ya Wazee ya CCM inayoundwa na Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi, Makamu Mwenyekiti wa CCM na Spika Mstaafu, Pius Msekwa na Waziri wa zamani, Abdulrakhman Kinana haiwezi kuleta mwafaka ikisimama peke yake.

Wachunguzi wa masuala ya kisiasa na wataalamu wa menejimenti na uongozi, wanasema kwamba vitendo vya viongozi waandamizi kurushiana maneno ya kukashifiana, tena wanawake kwa wanaume, kunaonyesha kwamba nidhamu ndani ya chama imefika katika kiwango chake cha chini kabisa katika historia.

Mfano mmoja unaotolewa ni wa Waziri wa Nchi (Ofisi ya Rais) Utawala Bora, Sofia Simba kumshambulia Waziri Mkuu Mstaafu na mkewe, John Cigwiyemisi Samwel Malecela na Anne Kilango – Malecela kwamba wanajidai kupambana na mafisadi wakati wenyewe wamefadhiliwa nao; kwanza kwenye harusi yao na pili kwenye kampeni za Malecela kuwania kuteuliwa kugombea urais kwa CCM mwaka 2005.

Kana kwamba hiyo haitoshi, Malecela anayepewa heshima kubwa kitaifa mpaka sasa, alijibu kwa kusema kwamba mteule huyo wa Rais Jakaya Kikwete, yaani Sofia Simba ni mgonjwa wa akili na kwamba ilimpasa kabla ya kurudi Dar es Salaam apelekwe Mirembe kuchunguzwa akili na kutibiwa.

Watu wengine wamekwenda mbali zaidi na kumtaka Rais Kikwete amfukuze kazi waziri huyo, ambaye walifikia kupendekeza mambo mengine ya burudani anayoweza kupewa mamlaka nayo badala ya nafasi hiyo nyeti ya uwaziri.

Simba pia alilumbana na Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP, Reginald Mengi, akidai si mwanachama wa CCM na kwamba atakuwa anavuka mipaka akiingilia mambo ya chama hicho. Hata hivyo, siku chache baada ya kauli hiyo, CCM ilitoa kauli kwamba Mengi ni mwanachama tangu 1977 na wakamwomba aendelee kukisaidia chama hicho kama ambavyo amekuwa akifanya.

Licha ya kuwepo kwa taarifa kwamba Kamati ya Mwinyi ilizika tofauti za wabunge na kwamba sasa wameungana na watakuwa kitu kimoja kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka kesho, bado imeelekea makundi yapo.

Dhihirisho la makundi hayo ni kitendo cha Mbunge wa Igunga aliyepata kuwa Mweka Hazina wa CCM na mjumbe wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu, Rostam Aziz kutaka liundwe jopo la majaji ili kumsafisha na kashfa ya Richmond. Siku moja baadaye, Spika wa Bunge, Samuel Sitta anayetajwa kuwa katika kundi hasimu na Rostam, aliibuka na kusema anachotaka Rostam kamwe hakiwezekani.

Sitta anasema kwamba kinachosubiriwa sasa ni kumalizia suala hilo la Richmond bungeni kwa kumalizia utekelezaji wa maazimio na kwamba Serikali haina fedha za kupoteza kuwapa majaji kuanza kuchunguza suala hilo.

Anaonya kwamba suala lililofanyiwa kazi na Bunge kama hilo la Richmond, haliwezi tena kuangiliwa na mhimili mwingine wa dola na ikiwa Rostam ana fedha zake, wanaweza kumalizana na majaji “huko huko.”

Kitendo kingine kinachotia hofu nchini, ni kuwa na Upinzani uliodhoofu, hivyo kwamba inatia shaka kama kweli panaweza kupatikana chama mbadala, ikiwa chama tawala kinaanguka au kuvunjika.
Tayari kumekuwepo na tetesi kwamba kuna baadhi ya vigogo ndani ya chama hicho tawala wanaofikiria ama kujitoa na kujiunga na moja ya vyama vya upinzani au kuanzisha chama chao kipya.

Chama kilichokuwa kikitupiwa macho na watu kuweka akili zao humo, tangu wakati wa mchakato wa kupata rais kupitia CCM mwaka 2005 ni Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ambacho sasa kinaelekea kuwa katika mtafutano miongoni mwa viongozi wake waandamizi.

Hali hiyo ilianza kujidhihirisha pale Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe alipopeleka jina (kwa kumtumia Mkurugenzi wa Uchaguzi, Msafiri Mtemelwa) kutaka kuwania uenyekiti kupingana na Freeman Mbowe, ambaye tayari alishasema anatetea nafasi hiyo.

Ilibidi wazee wa chama hicho kukaa na kumshauri Zitto aondoe jina lake, kwa maelezo kwamba bado ni mdogo na kulikuwepo na haja ya kumuunga mkono Mbowe sasa kuliko wakati mwingine wowote, ili chama kiweze kusonga mbele.

Hata hivyo, kumekuwepo na habari kwamba kuna mkono wa kigogo au vigogo wa chama tawala au dola ndani ya chama hicho, unaopandikiza chuki miongoni mwa viongozi na hata wabunge wa chama hicho, ili kuvuruga mipango yoyote ya kukipaisha chama hicho kwa ajili ya kukamata dola.

Katika hali kama hiyo, hata walio ndani ya CCM ambao wangependa kujiunga CHADEMA wanakuwa na wakati mgumu, wakijua kwamba mkono wa dola ni mrefu na wapo wahisani wa chama hicho tawala walio tayari kuvuruga, hivyo wanachobaki kuona mbele yao ni ‘giza la kisiasa’ na kubaki na dhana ya zimwi likujualo halikuli likakwisha.

Chama kingine cha kufikirika kuwachukua vigogo au kuwa mbadala ni Chama cha Wananchi (CUF), lakini rekodi yake si nzuri kwa sababu hakina mbunge hata mmoja wa kuchaguliwa katika Tanganyika, jambo linalokifanya kuwa kama chama cha upande mmoja tu – Zanzibar. Inabidi kufikicha kichwa sana kwa vigogo watakaotaka kujitoa CCM na kujiunga CUF.

Vyama vingine vilivyokuwa juu ni NCCR – Mageuzi ambayo sasa imeanguka baada ya kujipambanua wazi kwamba ni chama kisichokuwa na tamaa kwa sasa ya kwenda Ikulu na Tanzania Labour Party (TLP) ambacho nguvu yake inakwenda chini siku hadi siku.

Yote kwa yote, mabadiliko, mpangilio au mwonekano mpya wa mambo utajulikana zaidi wakati na baada ya kikao cha Halmashauri Kuu ya taifa ya CCM, ambamo hoja kadhaa zitajadiliwa kuhusu mpasuko wa CCM.


CHANZO: KWANZA JAMII
 
Back
Top Bottom