Si zaidi katika historia ya muungano bali ni katika wimbo huu wa Western Jazz Band

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
20,924
30,273
SI ZAIDI KATIKA HISTORIA YA MUUNGANO BALI NI KATIKA WIMBO HUU WA WESTERN JAZZ BAND 1964




Ilikuwa nawasha gari langu usiku nikaliegeshe kwa walinzi mtaa wa pili.
Gari limewaka na radio inasema.

Nimeshtuka naisikia sauti ya rafiki yangu Juma Mnonji anahojiwa kuhusu maisha ya Ahmed Kipande Band Leader wa Iliyokuwa Kilwa Jazz.

Majina yanayomtoka ni majina ya watu niliowajua toka udogoni hadi nakuwa kijana na akili zangu.

Ahmed Kipande, Juma Mnonji anamwita Amadi, Hassan "Kichwa" Shabani, Duncan Njilima, Ndume na dada yetu Pili Abeid.

Nimezima gari nisikilize radio kwa utulivu.

Hayo yote niliyoandika hapo juu yote yana historia na kufungamana na maisha yangu ya udogoni.

Juma Mnonji anahadithia anamweleza Ahmad Kipande mpiga saxophone na clarinet katika Kilwa Jazz lini aliasisi Kilwa Jazz.

Kilwa Jazz iliasisiwa mwshoni mwa miaka ya 1950 Mtaa wa Gogo nyumbani kwa akina Abdul Kigunya.

Nimeitaja nyumba kwa anuani ya Abdul Kigunya kwa kuwa Abdul ni rika langu tukicheza pamoja.

Hii nyumba ilikuwa ya mama yake.

Nyumba hii ilikuwa jirani sana na nyumba ya mmoja wa baba zangu wadogo Mzee Abdallah.

Sisi watoto wa mtaani tukisikia Kilwa wanafanya mazoezi na walikuwa wakifanya nyakat za usiku kama saa moja hivi basi sote tutajazana nje dirishani tunachungulia ndani.

Siku ya pili nyimbo zote tunaziimba.

Nawakumbuka rafiki zangu hawa niliouwanao wengi waetangulia mbele ya haki, Abbas Mwamba na nduguye Kurwa, Abdul Kigunya, Hamza Msanga Mapesa, Selemani na ndugye Kibira, Gopi, Mohamed Kitunguu na nduguye Ali ''Nakioze'' Hussein.

Juma Mnonji anamweleza mtangazaji anamwambia Kilwa Jazz ilianzishwa Mtaa wa Gogo nyumbani kwa Mama mmoja kutoka Kilwa.

Juma Mnonji anaendelea na simulizi yake anamtaja Hassan Kichwa mpiga lead guitar wa Kilwa Jazz na Ndume muimbaji.

Jina la kwanza la Ndume silifahamu.

Ndume nitakuja kukutananae ukubwani miaka ya 1970 sote tukiwa wafanyakazi wa East African Cargo Handling Services.

Hassan Kichwa ni mume wa dada yetu Pili Abeid.

Mdogo wake Dada Pili, Juma "Spencer" Abeid ni rika langu na mchezo wetu mmoja na nyumba zetu jirani.

Nikimfuata Spencer nyumbani kwao namkuta Hassan Kichwa na guitar lake anapiga.

Mimi umri wangu miaka 12 mwaka huo 1964 Tanganyika na Zanzibar zinaungana.

Juma Mnonji anaendelea na simulizi sasa anaeleza ilikuwaje nyimbo hii ikatungwa.

Juma Mnonji anaeleza kuwa ilikuwa kawaida ya Kilwa Jazz kutunga nyimbo zinazoakisi hotuba za Mwalimu Nyerere kama juhudi za kuwahamasisha wananchi katika maendeleo.

Kilwa Jazz Band ndiyo waliopiga nyimbo ya uhuru wa Tanganyika mwaka wa 1961 ambayo Juma Mnonji kaeleza kuwa ilikuwa dua ya kuiombea nchi, ''Ewe Mola tunakuomba ibariki Tanganyika na majiranI zake.''

Nyimbo hii ilikuwa na mashairi ya kuomba msaada kwa Mungu kuwa nchi nyingine zilizokuwa chini ya ukoloni zigomboke.

Naikumbuka sana nyimbo hii kwani ilikuwa katika maktaba ya baba yangu na ni zile santuri kubwa za 78 RPM.

Sasa siku hiyo ya kutia saini makubaliano ya muungano dada yetu Pili Abeid akamwambia mumewe Hassan Kichwa kuwa Kilwa Jazz Band lazima itunge wimbo wa muungano.

Wimbo wa muungano uliokuja kurekodiwa na Western Jazz Band na haukuwa wimbo waliotunga wao.

Huu ni mwimbo wa CoBantu bendi ya Congo Brazzaville iliyokuwa na mpigaji guitar hodari sana Papa Noel.

Hilo guitar ambalo linasika katika nyimbo hii ya Western Jazz Band limepigwa na Duncan Njilima ambae amefariki majuma machache yaliyopita.

Juma Mnonji alieleza kuwa Kilwa Jazz Band walikuja kumchukua Duncan Njilima aje kupigia kwao kwa sababu Hassan Kichwa lau alikuwa ''soloist,'' hodari lakini alielemea zaidi katika mipigo ya Cha Cha.

Wakati ule vijana wengi wakipenda Pachanga ambayo Duncan Njilima alikuwa bingwa kana unavyosikia anavyomuiga Papa Noel.

Kwangu mimi muungano haukunigusa hapa kama nilivyoguswa na hii nyimbo ya muungano na watu hawa niliowataja hapa, watu ambao nikiwaona katika mitaa ya Kariakoo ya 1960s.

Iko siku nimepita Mtaa wa Mchikichi nje ya Kumekucha Auction Mart.
Huu ulikuwa mnada maarufu wa Mzee Hamza kumekucha.

Pale niliona baadhi ya vyombo vya Kilwa Jazz Band vikisubiriwa kupigwa mnada.

Nakumbuka katika siku zake za mwisho kumuona Ahmed Kipande wakati huo mgonjwa kapooza lakini anaweza kujikongoja akipita Mtaa wa Sikukuu akitembea kwa miguu.

Mtaa wa pili tu kutoka mtaa hhu ni Mtaa wa Gogo ambapo Ahmed Kipande alianzisha Kilwa Jazz.

''Nyerere na Karume wastahili kusifiwa na wananchi wote wa Tanzania kwa kutuletea muungano wa Tanzania.''

Picha: Ahmed Mohammed Kipande, Abdul Kigunya na Mwandishi kama walivyo hivi sasa, Western Jazz band na Duncan Njilima


1654231546056.png
1654231701033.png

1654231417495.png
1654231613597.png
 
Back
Top Bottom