SoC03 Sanaa na wasanii: Je wasanii wetu bado ni kioo cha jamii?

Stories of Change - 2023 Competition

Mrema David

Member
Jul 19, 2022
5
3
“Mimi ni msanii, mimi ni msanii,
Kioo cha jamii, kioo cha jamii,
Mimi naona mbali, mimi naona mbali,
Kwa darubini kali, kwa darubini kali.”


Nani anakumbuka huu wimbo? Mimi ninaukumbuka sana. Enzi hizo nilikuwa nasoma pale Shule ya Msingi Zanaki, Kata ya Upanga Mashariki. Wimbo huu uliimbwa na ‘wakongwe wa kazi hizi’, Afande Sele akimshirikisha Ditto. Ukiachana na ubunifu wa kutunza vina, kuna ujumbe mkubwa ndani ya wimbo huu: Mimi ni msanii, kioo cha jamii.

Sanaa
imebeba mambo mengi lakini kwa ujumla wake ni kazi yoyote ya ubunifu inayogusa jamii, na wakati huo huo kumtambulisha mtu au eneo fulani. Shuleni ukijifunza mada ya fasihi kwenye somo la Kiswahili, kuna kipengele cha kusoma riwaya. Na kila ukimaliza kusoma riwaya, kuna swali la ‘nafasi ya mwandishi katika fasihi’. Nafasi ya msanii inaakisiwa na ujumbe uliobeba kazi yake. Sekta ya sanaa katika nchi yetu kwa miaka mingi imebebwa na muziki, maigizo, bila kusahau urembo na mitindo. Tangu enzi tumeishi na dhana kuu kwamba msanii ni kioo cha jamii. Tumeona dunia ikibadilika, zama zikipita, sanaa pia ikipitia mabadiliko kulingana na nyakati. Lakini swali la kujiuliza ni Je, dhana ya kwamba “msanii ni kioo cha jamii” bado ipo? Twende pamoja kwa kuchambua maeneo matatu niliyotangulia kuyataja ya muziki, maigizo, urembo/mitindo ambayo yanaibeba sanaa yetu kwa kiasi kikubwa…..

Muziki wetu umetoka mbali sana! Kuanzia enzi za bendi kama vile bendi ya TOT, Msondo ngoma, bendi ya Sikinde, bendi ya Kilimanjaro “wananjenje”, kina King Kikii, n.k; kisha zikaja Twanga pepeta, Akudo, FM Academia; upande wa mahadhi ya pwani tulikuwa na marehemu Bi. Kidude, n.k. Tukaja kwa wasanii binafsi kina Profesa Jay, Ferouz, Afande Sele, Sugu, Dully Sykes, marehemu Ngwair, na makundi mbalimbali kama vile Daz Nundaz, East Coast, East zoo, na kadhalika. Zama zile zimepita, lakini bado hata leo hii wimbo wa “kitambaa cheupe” ukipigwa kwenye sherehe, unaona msisimko wake. Wasanii wa enzi hizo walifuata misingi ya utunzi wa mashairi kwa kiasi kikubwa, ala za muziki zililia ipasavyo, na ujumbe uliobeba kazi zao ulikuwa wenye kugusa sana. Nakumbuka mwalimu wetu wa somo la stadi za kazi darasa la nne, kwenye eneo la muziki alituimbisha nyimbo kama vile LEAH wa Dully Sykes, na STAREHE wa Ferouz akimshirikisha Prof. Jay, na tulikuwa tunafurahia sana sio kuimba pekee, bali kufahamu jumbe zilizobeba nyimbo hizi ambazo zilihusu athari za starehe na magonjwa ya zinaa. Ningetamani sana kurudi enzi zile, lakini inabidi maisha yaendelee.

Zama zimebadilika, muziki pia umebadilika! Taratibu wengi wa wasanii waliokuja baadae wameshau lengo kuu la kazi zao – kuelimisha, kuburudisha, kuonya. Muziki sasa hivi umekuwa ni chaka la kutoka kimaisha au kupata kiki. Wasanii wanatunga kazi zao kwa mihemko, kutafuta wafuasi kwenye mitandao, kupanda chati, na kushindana na wasanii wengine. Leo hii imefika wakati ambao nyimbo nyingi zina maudhui mabovu. Unaweza kukuta matusi, kejeli, lakini pia baadhi ya video zimekuwa na uchafu mwingi kiasi cha Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kuingilia kati. Hivi karibuni kulikuwa na video imesambaa ya watoto wanaimba wimbo fulani kwenye basi la shule. Video ile ilileta hisia tofauti kwa wengi sana; sidhani kama ishu ilikuwa wao kuimba, lakini ishu ni walichokuwa wanaimba. Sasa watoto hawa ndio baadhi watakuja kuwa wasanii baadae, unategemea watakuwa wanatunga nyimbo za namna gani?

Sasa hivi baadhi ya wanamuziki wanadai kwamba wanatoa kazi zao kulingana na mahitaji ya soko, yaani kulingana na watu wanataka nini. Msanii anapaswa kuwa na jicho la tatu kujua kwamba wakati mwingine anapaswa kutoa ujumbe ambao jamii inauhitaji na sio inaoutaka.

Ukiangalia muziki kama “singeli”, ulitakiwa kuwakilisha ladha za pwani. Tumekuwa na miziki ya taarabu, miduara, minanda na michiriku ambayo yote imebeba mahadhi ya pwani. Singeli ilianza vizuri sana na wakongwe kina Msaga sumu na Sholo mwamba, lakini leo hii singeli haitazamiki tena! Muziki huu umeleta udhalilishaji mkubwa wa wanawake kutokana na uchezaji wao hivi karibuni, lakini pia hakuna ujumbe wa kueleweka; ni vurugu tu.

Kwenye eneo la maigizo napo kuna changamoto zake. Wakati ule tulikuwa na maigizo kutoka vikundi kama vile Kaole, wana kidedea, n.k; katika vichekesho tulikuwa na marehemu King Majuto, mizengwe, orijino komedi, kina Bambo, Kingwendu, na kadhalika. Ilikuwa dhambi kubwa wiki kupita hujawaona hawa watu na maigizo yao. Mungu akatujalia tukaanza soko la filamu, na tukaanza kutoka kimataifa pia (Mfano, marehemu Kanumba). Leo yako wapi? Maigizo yetu ya sasa hivi kwa asilimia kubwa huwezi kukaa ukatazama na mtoto mdogo, kwa nini? Tumeacha asili yetu, tumechukua vya wenzetu. Utandawazi umetafuna utamaduni na sanaa yetu. Nashangaa sana hata baadhi ya wanaojiita “wachekeshaji” siku hizi wamekuwa hawachekeshi tena. Badala yake wamekuwa wakiwasilisha kazi zao kwa njia ya kejeli na kutumia wanawake wenye maumbile makubwa na video nyingi za utupu. Mbaya zaidi tupo kwenye kizazi ambacho mmomonyoko wa maadili umekithiri, hivyo watu wanaona kawaida tu. Inasikitisha sana!

Tukija kwenye eneo la urembo na mitindo, sasa hivi soko la mitindo limekua sana na tuna wanamitindo wengi sana. Lakini tujiulize, wanamitindo wetu wanatunza utamaduni wa kitanzania? Ukipita mitandaoni utaona wengi wakijiita mamodo, lakini wanachokiwasilisha na kuwakilisha ni vya kutiliwa mashaka. Leo hii kuna hawa wanamitindo ambao maudhui yao kwa asilimia kubwa ni picha za utupu. Tumepoteza asili ya mtanzania, tumeiga wengine; tunatafuta chati, tunakwepa uhalisia.

Tufanye nini ili kurekebisha? Turudi kwenye asili, kwenye chanzo, kwenye dhumuni halisi la sanaa; hata wahenga walisema “jasiri haachi asili”. Ni jukumu la Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Wizara inayosimamia sanaa, wadau, na wasanii wenyewe kuhakikisha kila kazi ya msanii inafanywa kwa weledi, kwa nidhamu, na kutunza utamaduni wa kitanzania.

Kama jamii tunapaswa kudhibiti kasi ya mmomonyoko wa maadili haswa kwa vijana na watoto, kwani hawa ndio Taifa la kesho na wasanii wa kesho watakaoibeba na kuipeperusha bendera ya Tanzania. Tusimamie nidhamu na kuhakikisha elimu inaendelea kutolewa ili kutengeneza wasanii bora nchini.

Uandishi pia ni sanaa kwa sehemu yake. Waandishi na wachapishaji wa maudhui mbalimbali wahakikishe yanalenga kujenga, kwa manufaa ya mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

Msanii ni kioo cha jamii. Msanii anapaswa kuona mbali, kwa darubini kali. Na jamii inapaswa “kujifunza, kuona, kusema, kuelimika, kupitia, kuhamasika” kama alivyoimba Prof. Jay kwenye wimbo wake wa J.O.S.E.P.H.



Nawasilisha wakuu!
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom