Salamu za pongezi kwa washindi na washiriki katika uchaguzi ngazi ya UVCCM wilaya

Stephano Mgendanyi

JF-Expert Member
May 16, 2020
1,903
945
PONGEZI UVCCM WILAYA - SALAMU ZA PONGEZI KWA WASHINDI NA WASHIRIKI WOTE KATIKA UCHAGUZI NGAZI YA UVCCM WILAYA

Na Komredi, Ndugu Victoria Charles Mwanziva: Katibu wa Idara ya Uhamasishaji na Chipukizi, Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM)

Uongozi ni dhamana ambayo mtu hukabidhiwa na watu wakiamini atafanya kazi kwa weledi na kuyafikia matarajio yao katika cheo au nafasi waliyompa. Katika nadharia ya uongozi na demokrasia halisi ya kiafrika na Chama Cha Mapinduzi (CCM) tunaamini nafasi yoyote ya uongozi ni dhamana ambazo zimetokana na kudra za Mwenyezi Mungu. Wakati wa Mungu wa kukufanya uwe kiongozi katika ngazi fulani ukifika hakuna mtu au kitu chochote kinachoweza kuzuia wewe kufika ambapo Mungu amekupangia.

Kama vijana katika uongozi ndani ya Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) lazima tuyaishi mawazo ya Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere ambapo aliwahi kusema; "Tunataka kuona vijana jeuri katika Taifa hili na wenye kujiamini na sio waoga akina ndiyo bwana mkubwa. Tunataka kuona vijana wenye ujasiri wa kuhoji na kupiga vita mifumo ya kidhalimu isiyoshabihiana na matakwa na matarajio ya jamii ya kitanzania. Tunataka vijana waasi mifumo kandamizi, ubwana na ufisadi katika Taifa”

Hivyo naamini kwa ujasiri mkubwa wale wote waliochaguliwa kwa kuzingati Kanuni, Miongozo na Tamaduni za Jumuiya yetu ya UVCCM na Chama chetu yaani CCM mtakwenda kubeba ajenda za vijana katika ngazi ya Wilaya kwa weledi mkubwa bila woga na mtatimiza majukumu yenu ya kikanuni kama yalivyoainishwa kwenye Kanuni zetu za Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM).

Kipekee napenda kumpongeza sana Mweketiki wetu wa Chama cha Mapinduzi ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayoifanya ya kuwaletea Watanzania Maendeleo huku jicho lake kuu likituangazia Vijana, pamoja na hayo kwa namna anavyokiongoza Chama chetu katika misingi ya Umoja na Mshikamano wa hali ya juu. Lakini pia Napenda kwa dhati ya Moyo wangu kumpongeza sana Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM ambaye pia ni Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa kazi nzuri na kubwa anayoifanya ya kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020-2025 Visiwani Zanzibar.

Waswahili wanasema “Mnyonge Mnyongeni lakini haki yake mpeni” Kwa hakika Katibu Mkuu wa Jumuiya yetu ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Komradi Ndugu Kenani Labani Kihongosi (MNEC) anastahili pongezi za dhati kwa kazi nzuri iliyotukuka anayoifanya katika Jumuiya yetu ambaye pia ndiye Mkurugenzi wa Chaguzi zote za UVCCM.

Mpaka sasa tumeshuhudia chaguzi nzuri zenye utulivu na uwanja mkubwa wa Demokrasia kwa kuwapa vijana wengi fursa ya kuonyesha na kudhihirisha vipaji vyao ya uongozi katika ngazi mbalimbali kuanzia Uchaguzi wa kwenye Mashina, Matawi, Kata, Majimbo (Zanzibar) mpaka Wilaya na baadaye Mkoa na Taifa. Katibu Mkuu UVCCM Ndugu Kenani Kihongosi ameendelea kuwadhihirishia vijana kuendelea kusimamia kanuni katika Chaguzi zote za Jumuiya zinazoendelea ili vijana wote wanaotimiza vigezo vya kikanuni wanapata fursa ya kuonyesha uwezo wao wa kiuongozi. Hakika nakupongeza sana Katibu Mkuu wetu.

Hongereni sana Vijana wenzangu wote ambao mmeshiriki mchakato wa uchaguzi ndani ya Jumuiya yetu ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) ngazi ya Wilaya nchi nzima. Kujitokeza kwenu kwa wingi katika mchakato mzima wa uchaguzi kumedhihirisha ni kwa kiasi gani Jumuiya yetu ina uwanja mpana na demokrasia iliyokomaa. Nawapongeza sana kwa uthubutu wenu na utayari wa kubeba ajenda za vijana katika Wilaya zenu kupitia Jumuiya yenu adhimu ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM). Ushiriki wenu ni alama kubwa kwa Jumuiya na imetudhihirishia ni kwa kiasi gani hamasa imekuwa kubwa na ya kutosha katika chaguzi zetu za UVCCM.

Kwa wale waliopata nafasi na kushinda nafasi za uongozi na uwakilishi katika ngazi hii ya Wilaya nawapongeza sana kwa kuaminiwa na vijana wenzenu katika Wilaya zenu, mmepewa Imani, walipeni utumishi uliotukuka pamoja na mambo yote ya kiuchaguzi. Nawasihi jambo moja kubwa na muhimu sana katika uongozi vitu ambavyo uwe navyo makini kamwe kama kiongozi usiruhusu cheo kikakubadilisha ukadharau wengine, ukajiona bora sana kuliko wale ambao hawakuipata nafasi hiyo, ukajiona mwenye haki sana kuliko hata wale unaowaongoza, ukajiona mwenye weledi, upeo na uwezo sana, la hasha! Amini uongozi ni huduma na kamwe usijitenge na marafiki zako au jamii yako kwasababu umepata uongozi.

Tuungane kwa umoja wetu kuendelea kuijenga Jumuiya yetu. Matokeo ya uchaguzi yasiache makovu mioyoni mwetu bali yawe ni sehemu ya kujifunza na kuendelea kuwa wamoja. Kiuhalisia uchaguzi ili uwe bora na wenye uwazi wa kidemokrasia ni lazima tuwe na wagombea na sio mgombea lakini mwisho wa uchaguzi katika wote wenye vigezo mmoja huchaguliwa katika nafasi moja. Hivyo basi, ni lazima kwa Miiko na Kanuni zetu za Jumuiya ya UVCCM na Chama chetu CCM kuungana na aliyechaguliwa kumuwezesha kutimiza majukumu yake katika nafasi yake aliyochaguliwa.

Kumbukeni sasa mnaenda kusimamia Utekelezaji wa Ilani ya uchuguzi ya CCM 2020-2025 katika wilaya zenu; nawasihi sana hakikisheni mnatumia fursa hii kwa kufuata kanuni za Jumuiya yetu ya Umoja wa Vijana huku mkizingatia miiko na Katiba ya Chama cha Mapinduzi. Lakini pia mnapaswa kuyarejelea majukumu yenu ya kikanuni huku mkizingatia weledi na kuyatumia maarifa yenu ya kiuongozi katika kutimiza majukumu yenu ya kila siku. Nendeni mkashirikiane na viongozi wenzenu waliowatangulia kwa maana wana mambo mengi mazuri ya kuwashauri ili msikwame katika kutimiza majukumu yenu. Hali kadhalika, msiwatenge wale mligombea nao kwa maana wanazo ajenda nzuri na bora, kashirikianeni nao ili kuendelea kuing’arisha Jumuiya yetu na Chama cha Mapinduzi.

Aidha, Viongozi lazima tuwe wanafunzi endelevu wa kuendelea kujifunza maana hakuna mwisho wa kujifunza, na kuupata uongozi kusikupe kiburi cha kuona unajua kila kitu. Kuna tabia iliyopo miongoni mwetu vijana kuona hatuna cha kujifunza baada ya kushika nafsi za uongozi; tunaona kama tumeshaumaliza mwendo na kujiona sisi tayari ni bora kuliko wengine kwa sababu ya uongozi, la hasha! Haya ni makosa makubwa tunayoyafanya na katika hili nawiwa kumnukuu Mwalimu Nyerere ambapo aliwahi kutusihi watanzania viongozi kuendeleaa kujielimisha kwa kusema “Kosa jingine ni kutojielimisha. Kanuni yetu moja inasema: Nitajielimisha kwa kadiri ya uwezo wangu wote na kutumia elimu yangu kwa faida ya wote.Wengine hufikiri kuwa kujielimisha ni kujua kusoma na kuandika. Hilo ni kosa, lakini si kubwa kama la pili. Wengi wetu, hasa baadhi ya viongozi, hufikiri kuwa tunajua kila kitu na hatuna haja kujifunza jambo lo lote zaidi.”

Ni wakati wenu kama viongozi mlioaminiwa kuungana na wenzenu wote mlioshiriki nao mchakato wote wa uchaguzi mpaka nyie kupatikana kuwa viongozi wa Wilaya zenu. Kumbukeni kuwa hata wale mlioshindana nao katika uchaguzi huu walikuwa na ajenda nzuri ambazo ni jenzi kwa Jumuiya, msisite kufanya nao kazi, msisite kuomba ushauri kutoka kwao, msisite kuchukua ajenda zao bora zenye utofauti na za kwenu na kuzitekeleza kikanuni kwa maslahi ya Jumuiya na vijana katika Wilaya zenu, msisite kujifunza kutoka kwao. Baba wa Taifa ambaye aliwahi kusema; “Watu walio hatari sana ni wale ambao wanafikiri kuwa wanajua kila kitu, wala hawana haja ya kujifunza zaidi. Hii ni tabia mbaya ambayo huzuia kabisa maendeleo” Tukajitahidi kujifunza tusije tukawa kikwazo cha kuleta maendeleo kwa Vijana wenzetu na Jumuiya yetu.

Viongozi wote mlioaminiwa nendeni mkatekeleze majukumu yenu kwa kuzingatia Kanuni zetu za Umoja wa Vijana wa CCM na Katiba ya Chama Cha mapinduzi, tukumbuke kuwa yote tunayoenda kuyatekeleza ni kwa maslahi ya vijana wenzetu na Chama cha Mapinduzi. Nendeni mkaunganishe nguvu mkawe chachu ya mapinduzi ya maendeleo katika Wilaya zenu na kuhakikisha mnakuwa madaraja ya huduma kwa jamii inayotuzunguka. Tuunganishe nguvu katika ujenzi wa Chama na Taifa - tuunganishe nguvu katika kuhakikisha uwepo wetu ndani ya Chama una thamani na manufaa kwa Vijana wenzetu.

Mwisho japo sio kwa umuhimu; Nawatakia kila la heri katika majukumu yenu mapya katika Wilaya zenu viongozi wote mliochaguliwa, mkatekeleze majukumu yenu kwa weledi huku mkitanguliza utumishi mbele kama aliyotuasa Makamu Mwenyekiti wa Chama chetu CCM, Komredi Ndugu Abdulrahman Omari Kinana kwa kusema “Niwaombe viongozi wenzangu kuchaguliwa na kupewa nafasi ni utumishi wa umma, ukifanya kazi nzuri utatukuzwa, usijitukuze mwenyewe”

IMG-20220928-WA0010.jpg
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom