Rushwa ya Ngono 'inavyobemenda' Masomo na Ajira nchini

BARD AI

JF-Expert Member
Jul 24, 2018
3,377
8,121
“RUSHWA ya ngono ipo, lakini haizungumzwi maana inachukuliwa kama jambo la kawaida na lisilozungumzwa hadharani. Vyuoni, ipo kutoka kwa mwalimu wa kiume kwenda kwa wanafunzi wa kike, au kutoka kwa mwanafunzi wa kike kwenda kwa mwalimu wa kiume.”

Ndivyo anavyosema Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), Dk Rose Reuben anapozungumzia madhara ya rushwa ya ngono katika taasisi za elimu ya juu. Anaongeza: “Umma unapaswa kujua na kuzingatia ukweli kuwa, digrii bila rushwa ya ngono ni digrii yenye tija kwa jamii na taifa.”

Kuhusu madhara ya tatizo hilo, Dk Rose anasema: “Rushwa ya ngono inasababisha wanafunzi wengi wanaosoma uandishi wa habari kuwa wachache katika vyombo vya habari na waandishi wa kujitegemea.

Utafiti wa Tamwa na Mfuko wa Udhamini wa Wanawake Tanzania (WFT-T) uliofanyika mwaka 2021 umegundua taarifa zao nyingi hazitumiki kwa sababu ya rushwa hiyo maana tatizo hili lipo hata katika baadhi ya vyombo vya habari.”

Izingatiwe kuwa, kwa mujibu wa Kifungu cha 25 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11/ 2007, mtu yeyote ambaye kwa kutumia nafasi yake au mamlaka yake katika kutekeleza majukumu yake anaomba au kutoa upendeleo wa kingono au upendeleo mwingine wowote kama kigezo cha kutoa ajira, kupandishwa cheo, kutoa haki au upendeleo wowote unaotambulika kisheria, atakuwa ametenda kosa chini ya kifungu hiki.

Adhabu ya mtu huyu ni faini isiyozidi Sh milioni tano au kifungo kisichozidi miaka mitatu au adhabu zote kwa pamoja.

Utafiti uliofanywa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mwaka 2020 katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) ulibainisha sababu tano kuu zinazochochea rushwa ya ngono vyuoni kuwa ni pamoja na ukosefu wa maadili na ushawishi wa watu wenye madaraka.

Nyingine ni mfumo dhaifu wa kushughulikia tatizo hilo, mfumo wa utoaji taarifa kutokuwa rafiki kwa waathirika pamoja na mamlaka ya utoaji alama za mitihani kuachwa chini ya walimu pakee.

Mkufunzi wa Masuala ya Mawasiliano ya Umma, Mary Kafyome, anasema kutokana na ukweli kuwa katika vyuo vikuu wahadhiri wana mamlaka makubwa kwenye alama na matokeo ya mitihani ya wanafunzi, kama mhadhiri si mwadilifu, anaweza kutumia mwanya huo kudhalilisha wanafunzi.

Hata hivyo, kwa upande mwingine mtaalamu huyo anasema: “Mchakato wa kupitisha matokeo hufanywa na wahadhiri wote wanaofundisha darasa husika. Kwa hiyo ikitokea mwanafunzi mmoja amefeli somo moja, lakini mengine amefaulu, basi kikao huagiza matokeo yafuatiliwe ili kubaini kilichotokea.”

Kafyome ambaye pia ni Mjumbe wa Bodi ya Tamwa na mhadhiri aliyefundisha katika vyuo vikuu nchini, anasema: “Lakini pia, kama mwanafunzi amefelishwa na anajua kwa hakika alifanya vizuri, ana nafasi ya kukata rufaa ili mtihani wake usahihishwe na mwalimu mwingine.”

Kwa mujibu wa Jarida cha Taasisi ya Door of Hope Tanzania To Women and Youth Tanzania (DHWYT), katika shule au chuo, mwalimu au mkufunzi humshawishi mwanafunzi kufanya naye tendo la ngono ili ampe maksi asizostahili, au amfaulishe hata kama hajafanya vizuri katika mitihani yake.

Katika semina ya hivi karibuni iliyoandaliwa na Tamwa kwa wahariri na waandishi wa habari Dar es Salaam, washiriki walisema kwa nyakati tofauti kuwa upo uwezekano mwalimu asiyemwadilifu, akajenga kasumba ya kutishia wanafunzi ili awanase.

Walisema baadhi ya wanafunzi wasio na uwezo huenda kujisalimisha ili mwalimu husika wa kiume ‘akiingia kwenye mtego wake,’ iwe rahisi kumshawishi ampe alama na ufaulu wa upendeleo.

Mmoja wa wahadhiri katika Taasisi ya Ustawi wa Jamii (ISW), Rhobi Kyaruzi (si jina halisi), anasema katika vyuo vyenye tatizo hilo, viashiria vya walimu kutaka rushwa ya ngono kwa wanafunzi ni vitisho vya kitaaluma visivyo na msingi.

“Si wote, lakini wenye tabia hiyo, silaha yao kubwa ni kuwatishia wanafunzi kuwa ‘atawakamata.’ Mara nyingi hizo si dalili nzuri.” Kwa upande wa wasichana wanaotaka kutoa rushwa hiyo kwa walimu, anasema uzoefu wake katika taasisi mbalimbali unaonesha kuwa hao huwa hawaingii darasani na hawafanyi kazi (mazoezi) kwani muda mwingi huutumia kwa starehe.

“Hivyo ni viashiria vibaya kwani katika mazingira yote hayo, huja wakiwa na mavazi ya kutisha; karibu nusu uchi na mwenendo wao huonesha kuwa, huyu hahitaji msaada wa kimasomo, bali ana ajenda yake ndiyo maana anakuja pekee muda huu.”

Mhariri Msanifu wa gazeti la HabariLEO aliyewahi kuwa mkufunzi katika vyuo vya uandishi wa habari vya DSJ, Royal na Times mkoani Dar es Salaam, Bantulaki Bilango anasema wanafunzi wengine wa kike hutumia fedha za ada kwa mambo binafsi kisha kuomba wasajili au wahasibu wa kiume ‘wasaidiane vyovyote’.

Bantulaki anasema: “Mwingine anajijua ni dhaifu kimasomo, anakuja ofisini na kuomba asaidiwe; ukimwambia aje na wengine uwasaidie ‘topic’ husika kwa pamoja, anasema nataka unisaidie tu nipate cheti; mimi ni mwanamke na wewe unajua; sasa kama hauko makini, unaingia katika kosa hilo.”

Mwanafunzi wa Mwaka wa Pili, Shahada ya Kwanza, Mawasiliano ya Umma katika Chuo Kikuu cha Tumaini (TURDACo), Dar es Salaam, Anna Hangwa, anasema sababu ya baadhi ya wasichana kutumbukia kwenye mtego wa rushwa ya ngono, ni pamoja na kutojithamini, kutojitambua na kutojiamini.

“Dawa ya hili ni kila mmoja kutafuta ufaulu ama ‘A’ au ‘B’ bila kulazimika kutoa ngono maana ‘A’ hailetwi na mhadhiri, bali juhudi za mwanafunzi,” anasema Anna.

MADHARA YA RUSHWA YA NGONO VYUONI
Kuhusu madhara ya tatizo hilo, Anna anasema: “… Rushwa ya ngono inaweka jamii katika hatari ya kuwa na wahitimu wenye ufaulu wa ‘A’ ambayo hakuikalia darasani wala kuitafuta hivyo hajui hata kuifanyia kazi na hao ndio wasomi ambao si halisi.”

Anatofautiana na mawazo kwamba wasichana wengi huingia katika rushwa ya ngono kutokana na mazingira magumu ya maisha vyuoni, lakini wapo wenye maisha mazuri kutoka familia tajiri, ambao huingia katika mkumbo huo.

Kwa mujibu wa mwanafunzi huyo: “Wasiojitambua hawasomi na hawataki hata kuhudhuria darasani, lakini wanataka wapewe ufaulu, hao ndio hujisogeza wenyewe kwa wahadhiri wenye uchu na wasiowaadilifu,” anasema Anna. Mhadhiri wa ISW (Rhobi), anasema nchi inapokuwa na vyuo ambavyo wahitimu wanapata vyeti kupitia rushwa ya ngono, ni hatari kwa usalama na maendeleo ya taifa.

Kielimu anasema madhara ya rushwa ya ngono kwa taifa vyuoni na shuleni, ni uwezekano walipata vyeti kwa rushwa, kuonekana wanafaa na hivyo, kurudi kufundisha katika vyuo vyao au vingine japo hawana uelewa.

“Aliyepata cheo au kazi kwa vyeti vyenye alama za kupewa atapata kazi asiyo na uwezo nayo, wakiwamo wengine wanaorudi kufundisha vyuoni au shuleni maana vyeti vinaonesha amefaulu vizuri kumbe ni ufaulu wa kupewa. Hivyo, vyuo vinakuwa na walimu mbumbumbu na hivyo kuzalisha wahitimu mbumbumbu…”

HABARI LEO
 
Mmebwabwaja sana tu, lakini hakuna popote mlipoonesha njia sahihi na mujarabu ya kuweza kudhibiti na kukomesha vitendo hivyo.

Wanaokamatwa siku zote kwa rushwa ya ngono ni wanaume pekee wanaoshawishi, lakini sijawahi kusikia mwanamke kadakwa kwa "kugawa kama njugu" rushwa ya ngono, wakati kumbe uozo upo pande zote!

Katika maelezo ya topic hii inaonekana kuwa asilimia kubwa ya rushwa ya ngono hutokana na wanawake wenyewe "kutega" kuliko rushwa ya ngono inayotokana na ushawishi ama vitisho kutoka kwa wanaume.

wataalamu na viongozi mnaopambania kukomeshwa kwa mambo hayo, wekeni wazi njia na hatua madhubuti zinazoeleweka kuweza kukomesha tatizo.

Maana adhabu zake ndogo ndogo zilizotajwa haziwezi hata siku moja kusaidia kudhibiti ubazazi huo.
 
Rushwa ya ngono ipo na imetamalaki sana, lakini niongelee kwa upande wa vyuoni, hawa wadada wa vyuoni huwa wanajipeleka wenyewe ....yaani unakuta bint kazi yke ni kuwatega ma lecturer tu na ni mzuri , na ma lecturer amejizuia lkn unakuta bint yuko moto kila saa ofisini kwa lecturer au vimeseji Hi sir, tusiwalaumu hawa ma lecturer kwakweli wanapitia kwenye mitihani mizito sana hasa inatokea pale bint hana uwezo darasani hapa atatumia kila mbinu, kuna baadhi ya mabint wana mpeleleza lecturer mpk anakoishi na anajipeleka...ingawa pia wapo ma lecturer wengine ni wataalam wa kutongoza ma bint lkn ni kwa asilimia ndogo sana .....unakuta kwa week ma bint zaid ya 5 wanaomba outing na wewe. Sasa kwa wale wenzangu ambao hawawezi kujizuia hapa ngono ni lazima ....huko ma ofisini ndio kuna ubabe sasa ingawa nako mabos wanategwa sana .....yaani ni shida hawa wanawake wanajipeleka kwa asilimia kubwa
 
Back
Top Bottom