Papara za Kugawa Vitalu Vipya vya Utafiti wa Gesi Asilia Bila Sera, Sheria na Kanuni: Tumerogwa...?

HKigwangalla

JF-Expert Member
Feb 6, 2008
717
971
Papara za Kugawa Vitalu Vipya vya Utafiti wa Gesi Asilia Bila Sera, Sheria na Kanuni: Tumerogwa, Ujasiriamali Binafsi ama Uzalendo Uliopitiliza? (I)

Na Hamisi Kigwangalla, MB.


Wakati wa kipindi cha bunge la bajeti, Prof. Sospeter Mwijarubi Muhongo, Waziri wa Nishati na Madini, aliliarifu bunge kuwa serikali ilikamilisha kazi ya kuipitia mikataba ya gesi asilia mnamo mwezi Novemba 2012 na akasema kuwa “kukamilika kwa kazi hiyo kumeiwezesha serikali kubaini maeneo yanayohitaji kuboreshwa katika mikataba hiyo. Pia, matokeo ya uchambuzi wa mikataba hiyo yatasaidia katika uundaji wa sera, sheria na kanuni za usimamizi wa sekta ndogo za mafuta na gesi asilia itakayokidhi matakwa ya watanzania.” Kanuni hii ilinithibitishia jambo moja, kuwa hatuko sawa katika njia tunayopita kuelekea kufanya uvunaji wa raslimali hii adhimu na urithi wetu wa bure; kwamba hatuna sera, sheria na kanuni, sasa tunaendeleaje kutoa vitalu vipya kila siku?


Ufahamu wangu mdogo kwenye mambo haya umeniwezesha kuamini kuwa sheria ya petroli (The petroleum (exploration and production) act) ya mwaka 1980 haikidhi haja ya kuendesha kazi za utafiti na uzalishaji wa gesi asilia, na hata biashara ya gesi asilia. Hata nilipoisoma ile sera mpya ya gesi (draft) nilibaini wazi kabisa nayo inakiri kuwa hatuna mfumo madhubuti wa kisheria na kitaasisi, yaani ‘legal and regulatory framework’, wa kuendesha vizuri sekta hii nyeti.


Prof. Sospeter Muhongo aliwahi akinukuliwa akisema kuwa tusipokimbia kuanza kuvuna gesi, majirani zetu watatuwahi. Kwani gesi inaoza? Sasa tunavyokimbia namna hii bila kujua tunafaidikaje si tutajikuta tumefika kwenye gesi sawa na wenzetu ama tumewawahi lakini hatuifaidi, kipi bora sasa? Leo hatuna sera, tunajuaje wajibu wa kila mtu kwenye shughuli za uvunaji? Ambapo gesi inachimbwa, watu wenyeji wana haki na wajibu upi? Masuala ya fidia kwa wananchi watakaoathirika kwa namna moja ama nyingine yamekaaje? Wenzetu wa Kenya wamezuia mafuta yao yasichimbwe mpaka kwanza wawe na sera, sisi tunakimbilia wapi?


Wakati tukikiri kuwa hatuna sera, sheria na kanuni mpya na za kisasa zinazoweza kukidhi mahitaji ya Taifa ya uvunaji na uwekezaji kwenye sekta hii nyeti, hivi majuzi Wizara ya Nishati na Madini imetoa tangazo la kualika wawekezaji kwenye ‘mkutano na maonesho ya pili ya Tanzania ya mafuta na gesi 2013’ utakaofanyika Dar es salaam ukumbi wa Mwalimu Nyerere International Convention Center kuanzia tarehe 23 hadi 25 mwezi huu (oktoba), ambapo mzunguko wa nne wa kugawa leseni za vitalu vya gesi kwenye bahari kuu na kaskazini mwa ziwa Tanganyika (The 4[SUP]th[/SUP] Tanzania offshore and North Lake Tanganyika licensing round) utazinduliwa.


Katika tangazo hilo lililotolewa na Wizara ya Nishati na Madini kupitia shirika letu la uendelezaji petroli nchini (Tanzania Petroleum Development Corporation, TPDC) vitalu saba vyenye ukubwa wa wastani wa kilomita za mraba 3000 kila kimoja vitagawiwa kwenye bahari kuu kwa mtindo wa kuwapa wawekezaji leseni za utafiti kwa asilimia 100 na vitalu viwili vitabaki kuwa mali ya serikali chini ya shirika lake la TPDC ambapo atatafutwa muwekezaji mshirika wa kufanya naye utafiti wa pamoja. Vitalu vikigawanywa kwa mtindo wa kuwaachia wawekezaji jukumu la utafiti (exploration) maana yake ni kwamba kuanzia siku ya kwanza ya utafiti wanaanza kurekodi gharama zao na wakimaliza na kufanikiwa kugundua gesi, wanapoanza zoezi la kuivuna na kuiuza sasa hiyo gesi wanaanza kukata asilimia si chini ya 70 ya mauzo yote kama gharama zao. Asilimia 30 tu inayobaki ndiyo itagawanywa kwa Tanzania kupata asilimia 60 na wawekezaji kupata asilimia 40. Hii kwa lugha ya kitaalamu wanaita ni ‘production sharing agreement (PSA).’ Hapa kuna maswali mengi sana ya kujiuliza, nani anafanya kazi ya kuzihakiki gharama wanazoingia hawa wawekezaji ili watakapokuja kuanza kuzikata tuwe na uhakika kuwa ndizo gharama halisi walizotumia?


Na katika vile vitalu viwili ambavyo anapewa TPDC mkataba utakuwa tofauti kwa kuwa kuanzia mwanzoni shirika letu wenyewe litaingia kwenye utafiti hadi uzalishaji na hatimaye mauzo. Na hapa kwa hakika tutarajie kuwa na mgao mkubwa zaidi wa faida kwa kuwa tutakuwa tumeshiriki toka mwanzoni. Na hata kama mbia wetu akisema ameweka gharama fulani tutaweza kuzihakiki maana na sisi tumo. Pia hata uhamishaji wa utaalamu na teknolojia (technology transfer), kujenga uwezo wetu wa kiuendeshaji wa zoezi hili la uvunaji wa raslimali za gesi asilia na mafuta na hata wa kifedha ni jambo litakalofanyika kirahisi katika mtindo huu, na siyo ule wa kuligeuza taifa letu shamba la bibi kwa kuwaachia mabeberu waje wavune tu. Huu ndiyo mfumo wa kufuatwa na nchi yoyote ile yenye watu wazalendo, wanaojitambua na wanaojua biashara. Na ambao wako ‘serious’ dhidi ya vita ya kupambana na umaskini. Wanaoguswa na shida za wananchi za siku hadi siku, wanaoongozwa na utaifa na si na njaa za matumbo yao.


Leo kampuni ya Statoil ya Norway aliyegundua visima vya gesi huko kwenye bahari kuu ya Tanzania ni kampuni inayomilikiwa na serikali yao kwa zaidi ya asilimia 67, na imeitajirisha nchi yao. Pia kampuni kama Petronas ya Malaysia, National Gas Company ya Trinidad and Tobago zinafanya kazi kwa kufuata ‘model’ ya Norway.


Kwa nini sasa TPDC isiwe ‘Statoil’ ya Tanzania? Hili ni swali lenye thamani ya zaidi ya dola za kimarekani milioni moja. Namtaka Prof. Sospeter Muhongo, ambaye amekuwa akijinasibu kwa usomi wake awajibu watanzania. Aoneshe uwezo wake. Awaambie watanzania elimu yake imetusaidia nini kuleta majibu ya swali hili.


Swali lingine lenye kunitatiza na naamini pia watanzania wengi linawatatiza ni kwamba, ni kwa nini tunaharakisha namna hii kuingia kwenye ugawaji wa vitalu vya gesi ilhali hatuna sera, sheria na kanuni mpya? Waziri huyu msomi na mtafiti haoni hatari ya hizi papara zetu kweli? Haoni hatari ya kumaliza kugawa vitalu vyote kisha kurudi kinyume nyume sasa kuanza kuomba mikataba na wawekezaji irekebishwe kufuata sera, sheria na kanuni mpya? Na hapo wanasheria watakuwa wameishaweka vipengele vya kutuzuia kufanya hivyo (stability clauses) kwenye mikataba na hatimaye kuishia kuwapigia magoti kuwabembeleza tu?


Kila siku tunazungumzia uwazi kwenye sekta hizi za raslimali ya gesi, mafuta na madini na Tanzania imesaini mkataba wa kimataifa wa uwazi kwenye sekta hizi (Extractive Industries Transparency Initiative), hivi kuna uwazi kweli hata kidogo tu kwenye haya maamuzi ya Prof. Muhongo na maluteni wake pale Wizara ya Nishati na Madini? Kwanza wanapata wapi uhalali (legitimacy) wa kusaini mikataba kwa kutumia sheria ambayo wao wenyewe wanakiri imepitwa na wakati na ndiyo maana wameanzisha mchakato wa kutunga sera, sheria na kanuni mpya?


Hakuna atakayebisha kuwa ili tuwe salama ni lazima twende kwa hesabu sana, kwanza tuwe na mfumo thabiti wa kisheria na kitaasisi (strong legal and institutional framework); sasa leo hii ndiyo tunahangaika kuandika sera, na kusomesha raslimali watu kwenye sekta hizi, ni lini wataiva na kuanza kutumika - miaka zaidi ya mitatu ni lazima ipite!


Prof. Muhongo hivi anazo kweli takwimu za kodi tulizopata kutokana na migodi mikubwa ya uchimbaji wa dhahabu? Hana taarifa kuwa tulianza kupata kodi pale Rais Kikwete alipoamua kuingilia kati na kuanzisha mazungumzo na wawekezaji hawa kufuatia tume ya Jaji Bomani ndipo tuliposhuhudia wakianza kulipa kodi ya kampuni (corporate tax) ya asilimia 30? Kabla ya hapo kila siku walikuwa wakisema hawafanyi faida na hivyo hawapaswi kulipa kodi. Leo kuna kampuni ngapi za uchimbaji wa dhahabu zimefunga migodi yao bila kulipa hata shilingi moja na nyingine kulipa miaka miwili hadi minne ya kurashia rashia tu kwa ‘soni’ ili kujijengea mazingira rafiki ya kupewa kitalu kipya wavune tena dhahabu? Wakati wimbi la kuingia kwa wawekezaji hawa wakubwa kwenye migodi ya dhahabu linashika kasi, kisingizio cha kuwaondoa kwa nguvu wachimbaji wadogo na wananchi wenyeji wa maeneo hayo kwenye maeneo yao (kama wageni kwenye nchi yao) kilikuwa tuwakaribishe wawekezaji watalipa kodi, watajenga shule na hospitali, wataongeza ajira nchini n.k. Hivi ni shule ngapi zimejengwa kwa mfano na Resolute pale kwetu Nzega? Wananchi wenyewe wameweza kujenga shule ngapi kwa pesa ya kilimo cha jembe lao la mkono tu? Sheria mpya ya madini ilipokuja imetusaidiaje sisi kama Taifa? Tumekuwa na sheria nzuri lakini haina meno kwenye mikataba ya zamani.


Wawekezaji hawakuleta maendeleo yoyote ya kupigia mfano, ambayo hata leo unaweza kuonesha. Hakuna tofauti kati ya Nzega iliyokuwa na mgodi mkubwa wa dhahabu na Igunga ambayo haikuwa na mgodi mkubwa kama ule katika kipindi hicho hicho – inakuwa bora hata Mwadui ya Williamson Diamonds kule Shinyanga ina utofauti na vijiji jirani na hata mjini Shinyanga kwa wakati ule! Wawekezaji kwenye sekta ya dhahabu hawakuleta maendeleo kwa wenyeji wanaowazunguka wakidai kuwa hawawajibiki kimkataba kufanya hivyo. Je, tumejipangaje kwenye sekta ya gesi? Kwa nini tusitulie kwanza, tukatengeneza sera ya kuwahudumia wenyeji ( a policy on local content initiatives) ili ‘tuwawajibishe’ wawekezaji, tujue wenyeji watafaidikaje na nchi itafaidikaje, na wao washirikishwe kwenye mchakato huo ili twende pamoja?


Kama ilivyo kwa mambo yote yanayoendelea kwenye gesi, na kama ilivyokuwa kwenye ile sekta ya madini, usiri wa maksudi ama wa kutojua umegubika namna ya wenyeji kufaidika. Tunaambiwa watanzania wataajiriwa, watauza bidhaa zao kwenye makampuni ya madini na uchumi wa maeneo hayo utakuwa kwa kasi, mchanganuo wa kina wa namna haya yatakavyotekelezeka umeandikwa kwenye sera, sheria ama kanuni ipi? Mkakati wa kuwawezesha wazawa wafanikishe haya kwa viwango vinavyotakiwa uko wapi? Maana haya makampuni huja na ‘viwango’ vyao vya nyanya na vitunguu na vinginevyo, sasa je sisi tumejiandaa vipi kuwawezesha wenyeji wafaidike na soko hili jipya na la uhakika?


Je, tuna sera gani ya kutunza na kutumia mapato yanayotokana na gesi? Kwa sasa, kwa ufahamu wangu, hatuna. Kwa nini tusijipange tukatunga sera, sheria na kanuni safi za kutuongoza, tukajenga mtaji wa raslimali watu ya kutosha, tukawekeza mtaji kwenye TPDC yetu ndipo tukaingia sasa kutafuta ‘wabia’ wa kusaidiana nao kutafiti na hatimaye kuwekeza, siyo wa kuwapa vitalu ‘wawekeze!’. Watanzania tunatamani tuwe na TPDC inayofanana na Statoil. Je, Prof. Muhongo yuko tayari kutupa hiyo?


Tukikamilisha mchakato wa kujenga mfumo thabiti wa kisheria na kitaasisi kwa njia ya kidemokrasia ya uwazi na shirikishi tutakuwa tumewapa uhalali akina Prof. Muhongo na wenzake sasa kufanya maamuzi ya utekelezaji yanayofuata sera, sheria, kanuni na mikakati iliyowekwa.


Kwa nini tusijipange kuifanya TPDC yetu kuwa ‘Statoil’ (mwekezaji) kwenye nchi nyingine huko tunakoelekea? Kama tungeliamua vema huko tutokako, STAMICO leo ingekuwa tajiri na ingekuwa inachimba dhahabu kama Ashanti Goldfields Corporation ya Ghana. Tusikosee tena kwenye gesi.


Tuna haraka gani, na ya nini? Ya kwenda wapi? Kuhakikisha tu gesi imechimbwa – na kwamba sisi kufaidika ama kutofaidika siyo ishu? Kwani kuna umaarufu gani tunaupata kwa kugawa vitalu vya gesi vyote leo? Na mwani ni lazima wavigawe vyote hao waliopo wizarani leo? Tunatunga sera, sheria na kanuni mpya ili zije zitumike kwenye nini wakati vitalu vyote tunagawa leo kwa kutumia sheria ya kizamani? Haya ni maswali yanayohitaji majibu kuntu. Prof. Sospeter Mwijarubi Muhongo akipenda anaweza kuja kutukata kiu yetu ya kujua. Atuelezee kwa kina. Na kama anataka nchi hii imkumbuke kwa kushiriki kuijenga afanye uamuzi sahihi - asimamishe ugawaji wa vitalu vipya vya gesi, akamilishe mchakato wa kujenga mfumo wa kisheria na kitaasisi ndipo aendelee. Ila kama anataka alaumiwe na vitukuu na vining’ina vyake mwenyewe aendelee na hii papara yake.

Dkt. Hamisi Kigwangalla (MB) ni Mbunge wa Jimbo la Nzega na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).
 
Jamaa yangu Kigwangala hivi mnapokuwa bungeni ile akili yenu ya kuunga kila kitu kinachofanywa na serekali huwa mnakitoa wapi, Yaani wabunge wa CCM ambao huwa wanajua wajibu wa mmbunge ni wawili watatu tu, filikunjombe, lugora, na bulaya basi.

Wengine wote haswa wewe na Nchemba ni kujipendekeza tu kwa serekali sijui ni kwakuwa hata nafasi ya kuwania ubunge uliipata kimagumashi ama vipi.

Kama ni kweli hayo uyasemayo ukifika bungeni safari hii ongelea hilo ama hata muulize waziri mkuu kwenye maswali ya papo kwa papo kama sio mnafiki.

Bado una miaka miwili kuprove unachosema hapa jamvini ukiwa huko bungeni.
 
mada ni nzuri sana, nadhani tunapaswa sisi ndio tuwailize nyie hayo maswali, haiwezekani mjadali kitu halafu mtoke nje mje kutuhadaaa, vipi mzee aliapata pesa ya matibabu? Usiitupe sana familia:A S-confused1:
 
Papara za Kugawa Vitalu Vipya vya Utafiti wa Gesi Asilia Bila Sera, Sheria na Kanuni: Tumerogwa, Ujasiriamali Binafsi ama Uzalendo Uliopitiliza?
HKigwangalla
Hongera kwa kuliona hili LEo, lakini nashangaa ulikuwa wapi sikuzote wengine tulishasema hilo tokea mwaka jana thread hii hapa https://www.jamiiforums.com/jukwaa-...tu-4th-tanzania-offshore-licensing-round.html

Ila kumbuka MACCM ndio wanaofaidika na washachukua 10% zao na ndio maana kwamiaka hii Mitano/10 huko Uswiss Matrilion yameongezeka.
 
Last edited by a moderator:
mkuu nikusaidie

ujaribu kuwa makini wakati wa vikao vya bunge

hili swali wapinzani walishaliuliza bungeni wakati wa mkutano wa bajeti kama sikosei .... ila kwa kuwa mnaendesha mambo kwa ushabiki wa vyama hamkulipa kipaumbele .... sasa unaliuliza tena ili iweje?

wabunge wa CCM mngekua mnaweka maslahi ya watanzania mbele badala ya chama chenu, hii nchi ingekua mbali sana kimaendeleo!
 
sasa naanza kuelewa kumbe mambo mnayajua ila ni njaa zenu ndo zinazowaponza wengi wenu mnaogopa mkifutwa chama mtakufa na njaa ajira hakuna ila kumbukeni mtakufa vinywa wazi nyie endeleeni na uccm wenu kiasi cha kwamba hata udakitari wako umefunikwa na akina lusinde!

hivi hamjisikii vibaya alichosema kikwete ya kuwa mrudi bungeni mujadili katiba upya? jk anaonesha ndio mwenye akili ccm na hata hivyo nchi ikiingia vitani yeye ndio wa kulaumiwa sio nyie wapiga makofi bungeni!!
 
Kigwangalla, nyinyi CCM ndiyo wenye serikali inayogawa hivyo vitalu...

Mmejaa wasomi, wenye mashahada lukuki lakini mkikaa pale mjengoni Dodoma kazi yenu ni ndiyooooo....na yule spika wenu, atasema, naona waliosema ndiyo wameshinda, tuendeleee...!!!

Kwa taarifa bwana mkubwa, sisi wananchi hatujarogwa, kama ni kurogwa basi ni wewe, chama chako cha CCM na serikali yako ya CCM...ninyi ndiyo mmerogwa.... elimu mnayo haiwasaidii, macho mnayo hamuoni, maskio mnayo hamsikii....CCM Mmerogwa, tafuteni tekelo awazingue au subirini tekelo wa mwaka 2015.
 
Hii nchi imejaa matahira kila kona sasa wewe ndo wa kutusemea sisi wanyonge halafu na wewe pia unalalamika kama sisi unaonaje ukipeleka muswada binafsi bungeni kulipinga hilo? Atleast do your party
 
HKigwangallah unajua fika kuwa hiki ulichokieleza hapa karibu kila mwanaCCM anakijua, lakini tatizo Ni kuwa fedha zimeishawekwa kwenye akaunti huko Uswisi. Je Nani ndani ya CCM anao ujasiri wa kurudisha hela ya rushwa kwa wawekezaji? Chenge alikula hela za Rada na hadi chenji tumerudishiwa je amefanywa nini?

Kwa kifupi Ni kuwa nyie CCM Ni majizi, hapa hata wewe umepiga kelele kidogo watakuweka sawa siku mpinzani akitoa hoja hii hii bungeni wewe ndio utakuwa wa kwanza kusema hana akili nzuri na wewe ndio huwa unamtibu. Tamaa na ubinafsi ndani ya CCM ndio zimetufikisha hapa, Muhongo na wajanja wachache ndani ya CCM wanataka kutajirika na kuacha mamilioni ya watanzania wakifa kwa kukosa huduma za kiwango za matibabu
 
Sawa tena ni hoja nzito sana ulizotoa, lakini tatizo lako mambo haya unayoyaona ni upuuzi huku uraiani ukienda Bungeni unayounga mkono, tena kwa mbwembwe!

Sasa sijui humo ndani ya Bunge kuna nini??!!
heshima yako mkuu, pale kwenye lango lakuingilia bungeni ukiingia tu kwa kupitia chama cha magamba akili inaganda kabisa, kuna mbuzi alichinjwa pale na mwenyekiti wa CCM, lazima wapelekwe watu wakufanya maombi kuvunja zile nguvu za giza.
 
Upuuz sana huu,hivi nyinyi wabunge wa CCM mna nin lakin??

Wewe sasa unakuja na blah blah kama hizi ili iweje??si ndiyo ninyi mlikuwa kimbele mbele kushangilia maamuz yenu huko bungen wakati watanzania wanapigwa na kuuwawa wakilipinga hili unalolisema??


Sasa unakuja kuzungumza ili kufurahisha kijiwe au ili kutaka uonekane kama unaguswa nalo kinafiki namna hii??

Akili zenu mbovu sana nyinyi mafisadi wa taifa hili,mungu atawalipa hapa hapa ulimwenguni kwa dhula zenu kwa maelfu na maskini wa kitanzania,mnatia hasira sana nyinyi makalubandika
 
Jamaa yangu Kigwangala hivi mnapokuwa bungeni ile akili yenu ya kuunga kila kitu kinachofanywa na serekali huwa mnakitoa wapi, Yaani wabunge wa CCM ambao huwa wanajua wajibu wa mmbunge ni wawili watatu tu, filikunjombe, lugora, na bulaya basi.

Wengine wote haswa wewe na Nchemba ni kujipendekeza tu kwa serekali sijui ni kwakuwa hata nafasi ya kuwania ubunge uliipata kimagumashi ama vipi.

Kama ni kweli hayo uyasemayo ukifika bungeni safari hii ongelea hilo ama hata muulize waziri mkuu kwenye maswali ya papo kwa papo kama sio mnafiki.

Bado una miaka miwili kuprove unachosema hapa jamvini ukiwa huko bungeni.


Generally ukiangalia maoni anayoyatoa mheshimiwa mbunge Hamisi Kigwangala humu jamvini ni unafiki tu, mahali sahihi pa kuweza kuyaongelea haya masuala anayoyaleta kwenye mitandao ya kijamii papo (Bungeni) lakini kwa hulka yake ya kinafiki na ujanja ujanja huwa haongelei masuala haya mahali hapo, mbali ya hivyo ukisoma mada zake nyingi ni marudio na masuala ambayo watu wengine wameshayajadili na kuyachambua kwa kina, sema yeye (mheshimiwa Hamisi Kigwangalla)huwa anayakusanya pamoja mawazo ya watu mbalimbali na kuyaandika kwa pamoja na kujifanya ni mawazo yake kumbe ni marudio tu ya mawazo ya watu wengine, huwa anaogopa kuhoji masuala haya Bungeni kwa sababu ya kuogopa kuonekana sio ‘’MWENZAO’’, badala yake anatumia ujanja ujanja na kujifanya kuandika nyaraka ndefu kwenye mitandao ya kijamii ili kujifanya aonekane ni mzalendo wa kweli wa nchi yetu ya Tanzania ili ajijengee msingi na kupata watu ambao watayapenda mawazo yake (kumbuka kwamba ameyachukua mawazo ya watu wengine) katika kujitengenezea njia ya kutimiza ndoto zake za kugombea uraisi, SHAME ON YOU KIGWANGALLA, unacheza mchezo huku na huku, huo ni UDHAIFU NA UNAFIKI, simama mahali pamoja ili msimamo wako ueleweke, mchezo unaoucheza kwenye siasa ni mchezo hatari, wewe sio mtu wa kuaminika hata kidogo.
 
mkuu nikusaidie

ujaribu kuwa makini wakati wa vikao vya bunge

hili swali wapinzani walishaliuliza bungeni wakati wa mkutano wa bajeti kama sikosei .... ila kwa kuwa mnaendesha mambo kwa ushabiki wa vyama hamkulipa kipaumbele .... sasa unaliuliza tena ili iweje?

wabunge wa CCM mngekua mnaweka maslahi ya watanzania mbele badala ya chama chenu, hii nchi ingekua mbali sana kimaendeleo!


Generally ukiangalia maoni anayoyatoa mheshimiwa mbunge Hamisi Kigwangala humu jamvini ni unafiki tu, mahali sahihi pa kuweza kuyaongelea haya masuala anayoyaleta kwenye mitandao ya kijamii papo (Bungeni) lakini kwa hulka yake ya kinafiki na ujanja ujanja huwa haongelei masuala haya mahali hapo, mbali ya hivyo ukisoma mada zake nyingi ni marudio na masuala ambayo watu wengine wameshayajadili na kuyachambua kwa kina, sema yeye (mheshimiwa Hamisi Kigwangalla)huwa anayakusanya pamoja mawazo ya watu mbalimbali na kuyaandika kwa pamoja na kujifanya ni mawazo yake kumbe ni marudio tu ya mawazo ya watu wengine, huwa anaogopa kuhoji masuala haya Bungeni kwa sababu ya kuogopa kuonekana sio ''MWENZAO'', badala yake anatumia ujanja ujanja na kujifanya kuandika nyaraka ndefu kwenye mitandao ya kijamii ili kujifanya aonekane ni mzalendo wa kweli wa nchi yetu ya Tanzania ili ajijengee msingi na kupata watu ambao watayapenda mawazo yake (kumbuka kwamba ameyachukua mawazo ya watu wengine) katika kujitengenezea njia ya kutimiza ndoto zake za kugombea uraisi, SHAME ON YOU KIGWANGALLA, unacheza mchezo huku na huku, huo ni UDHAIFU NA UNAFIKI, simama mahali pamoja ili msimamo wako ueleweke, mchezo unaoucheza kwenye siasa ni mchezo hatari, wewe sio mtu wa kuaminika hata kidogo.
 
HKigwangalla,

..hii hoja yako nadhani imechelewa.

..itakuwa MIUJIZA kama utaweza kubadilisha msimamo wa Prof.Muhongo kugawa vitalu btn now and October 23.

..wabunge wenzako kama Zitto Kabwe wamekuwa wakilipigia kelele suala hili kwa muda mrefu. response ya Prof.Muhongo imekuwa dharau na kejeli. labda ungemuunga mkono Zitto wakati ule, na haswa ukizingatia kwamba unatoka chama tawala, mngeweza kuokoa jahazi.

cc Zitto, Pasco, THE BIG SHOW
 
Last edited by a moderator:
Back
Top Bottom