Ni aibu gani uliipata kwenye Interview yako ya Kwanza? Mimi yangu hii

Robert Heriel Mtibeli

JF-Expert Member
Mar 24, 2018
21,340
51,900
AIBU NILIYOIPATA KWENYE INTERVIEW YANGU YA KWANZA.

Anaandika Robert Heriel.

Simulizi hii ni ya kweli, nimekumbuka tukio hili nikabaki nacheka Sana, naomba nishiriki pamoja nanyi huenda kuna atakayepata somo.

Baada ya kumaliza elimu ya Chuo kikuu nikaamua kuwa fundi cherehani, nikiwa nashona nguo, Fani ambayo nilijifunza tangu nasoma mwaka wa Kwanza pale UDSM. Nilijifunza kushona nguo Kama Fani ya akiba na dharura ikiwa mambo ya elimu yaliniendea mrama, namaanisha kama nisipoajiriwa niwe na pakukimbilia. Basi nikiwa pale Sinza KWAREMI, nikamuomba Fundi mmoja ambaye Kwa miezi sita niliunga urafiki naye, nikamsihi anifundishe kushona hata Kwa kumlipa pesa.

Fundi akaona namzingua Kwa hoja kuwa Mimi ni msomi wa Chuo kikuu wapi na wapi na Kushona nguo, hoja ya pili ni muonekano wangu, fundi alidai muonekano wangu haufanani na kazi ya ufundi nguo, isipokuwa napaswa kuwa katika Ofisi zenye viyoyozi. Basi baada ya Mimi kung'ang'ania Kwa majina kadhaa alikubali.

Basi nikajifunza Kwa bidii kila nilipokuwa natoka Chuoni au pasipokuwa na vipindi, ingekuwa ngumu kunikuta Mabibo Hostel au mti mdigrii au love horizon au vimbwetani nikipiga Stori Kama hakuna vipindi.

Baada ya kubobea kwenye ufundi huku pale mtaani wakiniita FUNDI UCHWARA kutokana na Kauli aliyoitoa Tundu Lissu kipindi kile kuhusu Dikteta uchwara basi nami wakawa wananitania hivyo. Huku wamama wa mtaa ule wakinipa nguo zao za viraka.

Fundi Godfrey (Mungu akubariki) alichukua pesa ya miezi miwili tuu, lakini miezi mwingine akasema Haina haja Mimi kulipia, basi Mimi kazi yangu ikawa kuwahi Asubuhi Asubuhi kufungua ofisi Kwa maana yeye alikuwa anakaa Mbezi mwisho hivyo alikuwa akichelewa.

Saa mbili nilikuwa nimeshafanya Usafi nikiendelea na kazi za ushonaji Kama Ratiba ya siku hiyo ilivyo, Ila nisikatae ukweli kuwa moja ya sababu ya kuwahi kufungua mapema ni kupata wateja WA viraka nijipatie Pesa. Na kweli nilikuwa nikipata, hela ambayo ilikuwa ikinikimu nje ya pesa za bumu ambalo nilikuwa nikizihifadhi Kwa mipango yangu.

Baada ya miaka mitatu nilimaliza shahada ya Kwanza, nilifurahi, nilimshukuru Mungu kwani ilikuwa ni moja ya ndoto yangu tangu ningali mtoto kuwa siku moja NAMI niwe msomi WA elimu ya juu Kabisa.

Sasa muda wa kurejea nyumbani(Makanya) uliwadia. Nani angekubali Kurudi nyumbani?
Wote twajua vijijini hakuna fursa nyingi kama huku mjini, wote mjini kwa sehemu kubwa ndio elimu inaweza kuwa applicable kuliko kijijini. Kijijini labda ishu ya kilimo na mifugo lakini mambo mengine ni uongo tuu.
Utafungua Tuition lakini wanakijiji hawatakuwa na pesa ya kuwapa watoto wao ili wakulipe.
Utafungua Zahanati lakini utamuajiri nani Kwa Mshahara upi akae kijijini, wanakijiji waliozoea kutumia miti Shamba au kusingizia wamelogwa watakujaje kwenye zahanati yako, labda waone magonjwa makubwa.

Nikakaa mjini nikiendelea na harakati za ushonaji huku nikiipigia Hesabu akiba ya pesa ya bumu niliyokuwa nimejibana nikiwa nasoma, haikuwa pesa mingi, ilikuwa 2.3M.
Nikafungua biashara Maeneo ya Tegeta.

Huku nikiendelea kupata shinikizo kuwa nirudi nyumbani, wazazi wakitaka kujua nafanya nini, nami nikawa nawaficha ili wasiniombe pesa 😀😀 ingawaje mara moja Kwa miezi miwili mitatu nilikuwa nawatumia hata elfu 50 lakini siongopi, nikiwatumia hiyo ndio ntolee mpaka miezi sita huko😭😭 sio kwamba nilikuwa napenda Bali majukumu hayana uwiano mzuri na kipato.

Shinikizo la kuajiriwa likawa kubwa,
"Ajiriwa wewe!"
"Hivi una akili, ajiriwa, hujasoma ili uwe fundi nguo"
"Wewe utakuwa umelogwa mbona wenzako wanaajiriwa, wewe tuu ndio huzioni Ajira?
Kwa kweli maneno ya kushinikizwa yalikuwa yanatoka pande zote, sio mchana sio usiku.

Kila nikiwaelewesha hawakuwa wanaelewa, nawaambia Ajira Hakuna nilianza kutafuta Ajira tangu nipo mwaka WA Kwanza Kama sehemu ya kufanya uchunguzi wangu kuhusu upatikanaji wa Ajira, sehemu zingine nikawa nawaambia wasinilipe chochote Mimi niwe nachapa kazi nitatumia pesa zangu kwani Mimi bado nasoma Chuo, lengo langu ni kuijenga CV na uzoefu na kugundua changamoto mpya huko niendapo baada ya Kuhitimu Chuo kikuu. Lakini wapi!

Ndio maana nilifikia uamuzi wa kujifunza Kushona nguo Kwa sababu nilijiuliza Kwa mfano nikakosa Ajira nitafanya nini, na kazi za nguvu Mimi siziwezi, au hata nikipata Ajira alafu nikafukuzwa kazi nitafanya kazi gani, hapo wazo la kuwa fundi cherehani likawa Bora baada ya kuyashinda mawazo mengine ya ufundi magari (sikuwa na connection), ufundi welding, ufundi umeme halikadhalika sikuwa na connection.

KAZI ya fundi cherehani mademu wakawa wananizingua, hawanitaki😀😀 ati walivyo wajinga wakawa wananitania; nitatoboa nguo ngapi ifike milioni sita walau ninunue Gari ndogo 😀 nilikuwa nabishana nao huku moyoni nikiona ugumu kweli wa kupata hiyo pesa. Hata hivyo sikuwajali Sana. Baadaye nikaacha kushona nikaenda Tegeta kufungua Duka.

Biashara Kwa miaka mitatu ikanipa faida kadha WA kadhaa lakini baadaye ukapata anguko kuu.
Kurudi nyumbani siwezi kwakweli, kubaki mjini nitabakije tena wakati Kodi Mimi, Kula Mimi, umeme na maji vyote Mimi.

Ndipo wazo la kuomba kazi ya ualimu shule moja kubwa hapa jijini DAR es salaam likapata nguvu kichwani.

Nikaomba kazi Kwa bahati nikaitwa interview. Ilikuwa ndio interview yangu ya Kwanza.
Nilikuta wenzangu wengi Sana wapatao Mia na kitu hivi, nafasi ni waalimu watano😀😀

Tukapiga Written Interview nikapasua, si unajua Sisi wengine ni vipanga😀😀

Sasa kwenye Oral hapo ndipo nilipatwa na aibu kubwa ambayo mpaka Leo nahisi ilinidhalilisha Mno.

Ukiingia kwenye interview CV na vyeti vyako vinakuwa mbele ya Anayekusaili.
Sasa embu piga picha umeshika CV ya Taikon mwenye ufaulu mkubwa usio na Shaka, ufaulu wa juu wa daraja la Kwanza, kuanzia primary mpaka Chuo kikuu GPA ya juu kabisa.
Angalia umri wangu ungali bado ni mdogo kuashiria kichwa kinachaji.

Sasa wasaili huuliza maswali kulingana na CV na vyeti vya msailiwa.

Wakauliza maswali nikayapangua Kama maswali ya kitoto tuu😀😀
Sasa walivyoona karibu kila swali najibu tena Kwa kingereza changu cha shule ya Kata lakini kilichonyooka.

Kimya kikatokea huku nikiwatazama nikiwa nimepata Moto wa kutaka kuulizwa maswali mengine magumu zaidi.

Nikawaambia waulize zaidi magumu magumu, wote wakacheka huku baadhi Yao wakiona Kama nawadhihaki.
Akauliza Mzee mmoja swali lakizushi, nikamjibu Kwa reference, wakanipigia makofi huku wakinisifia.

Sasa Mimi nikawa najitukuza nikiwaambia hapa nina miaka mitatu sijashika daftarii Wala kitabu, sijahusika na mambo ya Taaluma nipo hivi, mngenikuta Enzi zangu nyie si ndio mngekoma. Wakacheka😀😀

Sasa kumbe ajikwezaye hushushwa na ajidhiliye hukwezwa.

Mwalimu mmoja akaniambia nielezee Term iitwayo "Reconnaissance" nikatabasamu nikaelezea Kwa mbwembwe kubwa nikijua hawana maswali ya kuniuliza.

Wakanipigia Makofi, lakini Yule mwalimu aliyeniuliza swali kumbe alijua ningejibu akasema ananiomba niandike "Reconnaissance" ubaoni.

Hapo ndipo kizaa kikatokea, awlai niliona ni rahisi lakini nilipoanza kuliandika ubaoni nikagundua hii Ngoma nalala Yoo!
Nikawa nachanganyikiwa kwenye Hizo herufi zilizo-double. Nikashindwa kuandika Asee!

Nikaandika Reconaissanse" badala ya "Reconnaissance" hapo Yule mwalimu akaruka Kwa kushangilia huku nami nikijua swali hilo limenichenga. Yule mwalimu akasema umeshindwa.

Nikawaambia Kama nimeshindwa basi sistahili kazi hii tukufu ya kufundisha, wakanilazimisha kuwa hiyo hutokea na mbona mengine yote nilijibu vizuri.

Ila ukweli nilisikia aibu kubwa, nikaacha Ile KAZI.

Matambo yangu ndio yaliniponza, Sisi wenye sifa tukiumbuka tunaumbuka haswa Jamani!

Shule hiyo inaneno "FUTURE" Katika jina lake la shule, ni shule kubwa mno. Waalimu WA hapo waliokuwepo miaka minne iliyopita nafikiri mtakuwa mnakumbuka.

Robert Heriel
Taikon wa Fasihi
Kwa Sasa Dar es salaam
 
Haya sema kwa ufupi aibu uliyoipata ni ipi? Maana maelezo kama kitabu naona tu fundi,fundi...
 
Back
Top Bottom