Kwa vijana: Hivi ndivyo nilivyofanya kuondoa aibu kufanya kazi duni ili nipate kipato

Robert Heriel Mtibeli

JF-Expert Member
Mar 24, 2018
21,340
51,895
Anaandika, Robert Heriel
Mtibeli.

Nilikuwa nasababu kuu tatu za kunifanya nizionee aibu kazi ambazo wengi huziona Duni.
Sababu ya kwanza, ni Malezi na makuzi.

Nimelelewa na kukuzwa kwenye familia ya Wasomi wa kati, wote walikuwa wafanyakazi wa serikalini. Mtazamo wao kuhusu maisha ni kusoma kisha kuajiriwa. Hivyo nilipokuwa mtoto moja ya mkazo walionipatia ni kusoma ili nije kupata kazi nzuri(wakimaanisha za kuajiriwa). Hii ni moja ya sababu ambazo ziliathiri ubongo wangu na kunifanya niwe na aibu mbele ya baadhi ya kazi.

Pili, Mwonekano Wangu
Sisemi mimi ni Super Handsome lakini atleast ninaonekana nina mvuto kwa Wadada wengi. Wakati wengine wakisema pesa za wanawake haziliwi au wanawake ni wabahili na hawatoi pesa zao sisi wengine hizo pesa tumeshazichezea Sana. Unakula pesa za demu na bado anakunyenyekea.

Akizingua anajua kabisa listi ni ndefu na wapo wenye uwezo kama yeye. Muonekano huweza kuathiri mtazamo wa maisha wa mtu. Hivyo kwa mwonekano wangu uliweza kunifanya nijihisi kuwa baadhi ya kazi sizistahili kuzifanya.

Hii naiona kwa vijana wengi pia wenye mionekano ya kuvutia wanawake wengi hujikita maskini wa elimu na vipato kwa sababu ya kujiona hawastahili kazi za shurba.

Tatu, uwezo wa akili Darasani na Elimu ya chuo kikuu
Akili huweza kuathiri mtazamo wa mtu kwenye utafutaji. Ukiwa na akili nyingi inaweza ikakupa mtazamo wa kiburi juu ya utafutaji na unajiwekea mipaka katika baadhi ya kazi. Vivyohivyo kwenye Elimu kubwa.

Akili + elimu kubwa badala iwe fursa kwako inaweza geuka kifungo cha mafanikio yako kisa KIBURI.
Kwamba mimi siwezi kufanya kazi fulani, kama sio kiburi kinachoisumbua ni nini?

Nikiwa Kidato cha sita, nilishagundua kuwa nina matatizo gani. Na tayari picha ya mbele nilikuwa nayo. Niliandaa mipango minne; Mojawapo ya mipango hiyo, miwili ni hii;

1. 7 Diamonds 7 Years Plan.
2. BS Plan (Break the Shame Plan).

7 Diamonds 7 Years Plan huu nilishawahi kuugusia hapa. Ulihusu kutafuta mwenza wa maisha ambapo ungechukua miaka saba ili kufanikiwa kumpata mwenza niliyekuwa nimemchora katika akili yangu.

BS Plan " Break the Shame Plan" huu ulikuwa ni mpango mkakati wa kukabiliana na kile kiburi kilichokuwa kinanifanya nijione wa maana mpaka kufikia kudharau baadhi ya kazi. Kukata mizizi ya kimakuzi na malezi niliyochimbiwa tangu nikiwa mdogo kuhusu baadhi ya kazi.

Hiyo ilikuwa ni likizo baada ya kumalizika kwa mtihani wa kidato cha sita. Mpango wangu ungeanza rasmi mara tuu nitakaporipoti chuo Kikuu. Hivyo chuo kikuu nilikuwa na majukumu zaidi ya kusoma,

Wakati wa kusubiri matokeo nilibahatika kuitwa na Baba mdogo DSM kumsaidia shughuli zake ndogondogo katika Kampuni yake na pia kusimamia nyumba yake aliyokuwa anaijenga huko Goba. Hapo akawa ananipa posho ambazo zilikuwa zinanikimu. Tulikubaliana kwa mwezi anilipe laki mbili unusu.

Lakini Mungu alimbariki kila siku alikuwa akinipa elfu kumi kama sehemu ya mizunguko, na wakati mwingine alikuwa akiniagiza nichukue Tax pale anaponituma lakiniimo nilikuwa napanda Daladala ili kuhifadhi pesa. Nilikuwa na miaka 18 tuu.

Baba mdogo mara kwa mara alikuwa akinisisitiza nisipende Wanawake (umalaya) pili, niache dhambi, kwa kumpenda Yesu. Kwani yeye alikuwa Mlokole. Alijua sinywi pombe na sina kilevi chochote ndio maana hakutoa ushauri wa vilevi. Lakini alihisi huenda nina mambo ya wanawake.

Pesa! Pesa! Pesa! Nilikusanya vipesa pale nikaona raha sasa ya kufanya kazi. Ukipata pesa unapata ari zaidi ya kufanya kazi.

Ubahili wangu ulinisaidia mno. Mimi siwezi kuhonga mademu huo ni mwiko ambao nilijiwekea.
Baada ya miezi mitatu matokeo yalitoka nikiwa nimefaulu vizuri sana. Hapo Baba mdogo aliposikia akanipongeza.

Kwa wenge langu nikaharakisha kurudi Kijijini kwetu Makanya, si unajua utoto nao. Baba mdogo akaniambia sasa hivi ni mapema, chuma chuma pesa ndipo uende. Muda huo nina kama laki saba hivi kwani nilimuelewa. Nakiri hili nilikuja kugundua nilikosea baada ya kufika kijijini. Nisingetakiwa kuwahi.

Mzee akanihesabia pesa za miezi mitatu akanipa laki saba zingine. Ikawa kama milioni moja na ushee. Ilikuwa ndio mara yangu ya kwanza kushika milioni moja.

Njia nzima nilikuwa naogopa nikiwa kwenye Daladala 😃. Nyingine niliweza kwenye Soksi za kiatu hiki na zingine kiatu hiki. Zingine kwenye mifuko ya suruali. Nilikuwa na hofu Aiseeh!😊

Nikanunua zawadi, nikanunua na nguo zangu na maandalizi ya chuo yakawa yamekamilika. Hapo nikabakiwa na milioni moja.

Sasa chuo kimefunguliwa nikakumbuka habari za Laptop. Kuulizia bei naambiwa laki sita, sijui laki nane. Kudadadeki! Nikakumbuka maneno ya Baba mdogo. Nilikosea!

BS Plan ilionyesha kuwa sikutakiwa kuishi kwenye Compound ya Chuo. Serikali ilinipangia Hosteli za Mabibo. Nikakumbuka wakati nimepata matokeo niliwasiliana na Mjomba angu mmoja aitwaye Dr. Ringo Tenga, ambaye aliwahi kuwa mhadhiri pale Udsm na pia ni mwanasheria. Nilitaka anishauri nichukue kozi gani. Hapo bado selection ya vyuo haijatoka.

Nikampigia tena kumwambia nimepangiwa Udsm. Akafurahi sana. Hapohapo akaniuliza kuhusu Hosteli. Nikadanganya kuwa nimekosa. Nilijua yuko na nyumba pale sinza ambapo ni karibu na chuo. Akaniambia nikaiangaklie ile nyumba ya Sinza kama nitaona inanifaa basi naweza kuweka makazi yangu kwa muda hapo nikiwa nasoma.
Nikashukuru.

Sikuwa nashinda chuoni isipokuwa kwenye vipindi na discussions za muhimu. Muda mwingi ungenikuta niko Sinza huko. BS ilianza, nilikuwa nafikiria nini ningefanya ambacho kitani-keep busy na kuondoa ile prestige niliyokuwa nahisi ninayo.

Hapo nikajiingiza kwenye mafunzo ya ushonaji kutoka kwa Fundi mmoja ambaye kwa sasa ni rafikianhu licha ya kuwa yeye ni mtu mzima, kisha mafunzo ya Martial Arts ambayo ni kutoka kwa Mwanamke wa kijamaika ambaye pia ni Neurologist( NI speshalisti wa mifumo ya ufahamu).

Kushona ndio ilizidisha mafanikio ya BS kutelekezeka Kwa upesi. Nilikuwa naona aibu mwanzoni, nikiri wazi lakini nilijikaza mpaka nikazoea. Sasa ungeweza niita Taikon Mshonaji kabla ya Taikon Master.

Sikupungukiwa na mahitaji ya umri wangu kama nilivyokuwa nadhani kabla. Nilifikiri kwa kufanya kazi ya kushona basi Watu wangenionaje, si unajua tena mawazo ya kiburi. Nilihisi labda ningekosa Watoto wakali. Kwa umri wangu wakati ule ilikuwa haki kuwaza hayo.

Lakini nataka kukuambia kuwa mabadiliko hayo yalitokea mwanzoni tuu lakini baadaye hali ilirudi kama zamani. Ni kweli mwanzoni walinizodoa, wakaniona kama nimeishiwa step. Na baadhi ya mademu walinikimbia😃.

Moja ya ubora na udhaifu wangu hapohapo ni msimamo na ninaamini kwa kile ninachoamini. Acha waondoke! Watakuja watakaonipenda vivihivi. Sikujali!

Kwani nafanya dhambi? Hapana
Kwani navunja sheria za nchi? Hapana.
Kwani kuna yeyote namdhulumu? Hapana.
Sasa kwa nini nijali au nihofie?
Nilifanikiwa kuondoa aibu kwa kiwango cha kati.
Sasa nilihitaji matokeo zaidi.

Kuna tofauti ya kufanya kazi kwa kukaa sehemu moja na kazi ya kutembeza vitu. Niliona siku nilipojaribu. Nilifikiri kuwa aibu zangu zimeisha lakini sio kweli. Bado kulikuwa na kiwango fulani cha aibu.

Nilikuwa nimemaliza chuo sasa. Nipo jijini. Ingawaje nilikuwa na pesa za kutosha lakini nilikuwa na hofu ambayo ilitokana na kuwa Njiapanda. Nàam njiapanda ya maisha. Sijui kipi nifanye. Bado sikuwa nimeamua nini nifanye kwenye maisha. Ni kweli naweza kufanya kazi yoyote halali lakini jambo zuri ni kuspesholaizi. Hapo ndipo mtiti ulipo.

Nilijifunza ushonaji nikawa nashona sio kwa sababu ya kuifanya iwe ndio kazi yangu. Bali nilijifunza ili niondoe aibu. Basi. Lakini pia nilijifunza ili niweke akiba ya ujuzi ambapo niliamini ipo siku inaweza kuwa silaha nzuri ya kutumia.

Katika Ujasusi na katika vita usidharau silaha. Sio ajabu makomandoo hutembea na silaha za kila aina mpaka zile silaha ndogo kabisa. Zote zinatumia.

Sikutaka kuwa na mbinu au silaha moja. Ambapo nikinyang'anywa basi ujanja wangu ungekuwa umeisha.

Nikapata wazo. Dagaa! Ndio Dagaa! Hawahawa Dagaa wa kukaanga wa Mwanza. Nikasema ngoja niagize mzigo. Nitapata wapi pakuagiza hilo lilikuwa jambo dogo. Nikapata mshikaji mmoja huko Mwanza.

Yule jamaa akaniambia nitume pesa ndipo akitengeneza. Kudadadeki! Kutapeliwa, utatapeliwa Robert! Hapana siwezi kutapeliwa. Nikasema acha nijaribu kwa debe Tatu. Ni pesa ndogo isiyozidi lakini na ishirini. Hapohapo nikaingia mtàndaoni nikaanzisha page chapuchapu nikaiita "Dagaa Online Market" anza kushare na lipia Ad kwaajili ya matangazo.

Nashangaa simu hizo. Dadeki! Krriiii! Krriiii!umeongea na huyu hujamaliza anapiga huyu. Nikasema anhaà! Nikaandika kwenye kidaftari changu kama ilivyo desturi.

Mzigo wa dagaa ukatumwa muda huo nilishakuwa nimenunua mashine ya kubania mifuko(vifungashio vya kuwekea dagaa) zinauzwa elfu 30. Nitatembeza Dagaa! Mguu kwa mguu! Zako kwa bako. Nikaweka pakti kama hamsini hivi. Nikatia ndani ya Begi la mgongoni.

Aiseeh! Hapo ndipo nikagundua kuwa aibu haikutoka yote. Nilikuwa naogopa kutembeza Dagaa. Kutoka Taikon Msomi, Taikon Mshonaji, Taikon Master sasa ni Taikon muuza Dagaa! Kubabake!

Ni katika na begi langu mgongoni likiwa na Pakti ya Dagaa. Huku Pakti mbili tatu nimeshika mkononi. Wazee sio poa ujue. Wabaridi! Lakini unajikaza hivyohivyo. Kwani nani unamuonea aibu bhana.

"Toka aibu! Shindwa aibu! Na kukemea pepo aibu ushindwe!" Napita huku nikisema maneno hayo kimoyomoyo.

Nikaanza kuingia katika nyumba ya kwanza. Majira ya saa tatu kwenda saa nne. Hawakununua walikuwa wakinitazama tafikiri wanamwangalia sijui nani. Sikujali. Niliuambia moyo Utazoea tuu. Kaa kwa kutulia.

Siku ile niliuza Pakti 42 sawa na Tsh 42,000/= ambapo faida ni elfu kumi. Na ni masaa matatu tuu. Kutoka saa 3 mpaka saa saba. Kesho yake aibu ikawa imepungua, nilifanya kazi ile kwa mwezi mmoja na nusu.

Biashara sio tuu spirit, nidhamu na mtaji bali pia uaminifu. Mama mmoja mstaafu aliyekuwa anafanya kazi ubalozi wa Marekani tusiyejuana alinipigia simu, akiwa kapata namba zangu mtandaoni akanieleza kuwa wajukuu zake wamemaliza chuo hawana kazi. Hivyo anaomba nimsaidie walau kumpa bidhaa za dagaa ili wapate chakufanya. Akatuma kama Laki tano na nusu. Hizo ni debe kumi na usafiri. Aiseeh! Hanijui simjui.

Sasa kuna dada mwingine alikuwa anakaa Sengerema, yeye akaniambia kuwa hizo dagaa anazipata kwa bei rahisi zaidi. Aliponitajia bei mimi si nikaingiwa na tamaa ya faida kubwa. Hapo ndipo nilipokosea lakini nilijifunza. Yule Dada akaandaa mzigo nikamtumia pesa naye akatuma mzigo.

Kuna kampuni moja ya rafiki yangu ya usafirishaji ndio ninaitumia kwa ishu hizi. Mzigo umefika DSM, ile kampuni inanisaidia kufanya delivery kama sitakuwepo Dsm kisha mimi nawalipa. Mzigo Unafika kwa Mhusika, kufungua Sio dagaa wale ambao aliniagiza. Nikahisi kama napatwa na uchizi sio kwa sababu tuu ya hela bali kwa sababu ya uaminifu. Ndio mteja amekuja alafu katoa oda ambayo kwangu ni kubwa kwani inanipa faida zaidi ya laki moja alafu namzingua,

Yule mama akanipigia simu. Tukazungumza. Nikamwambia atulie kwanza nizungumze na aliyetuma huo mzigo. Nawasiliana na yule dada naona anapiga Blahblahblah! Nilichukia mno.

Mteja asingenielewa zaidi angeniona Tapeli. Nikampigia tena yule Mama, nikamweleza kila kitu nikiwa najua hawezi kunielewa. Ila nikamwambia naweza kumrudishia nusu ya pesa aliyotuma kwa muda ule kisha baada ya Wiki mbilo nitaikamilisha Pesa yake.

Kisha niandae mzigo mwingine alafu aliipata ndipo alipoenda.l Maskini yule mama akasema tuu nisijali, kwani tayari ule mzigo ameshaugawa nusu kwa Watu. Nikamwambia sio kesi. Nikamtumia nusu kisha hiyo nyingine Akanisisitiza nisijali, hiyo kwenye biashara inatokeaga. Tunamalizana hivyo lakini nilipoteza mteja.

Nilijifunza jambo kuwa kwenye biashara usipende faida ya haraka inayokuja kwa ghafla. Mara nyingi huwa ni mtego wa kukurudisha chini.

Aibu ilitoka. Sasa niliweza kuona kazi ni kazi tuu. Hakuna kazi bora kuliko kazi nyingine. BS plan ilikamilika na kufanikiwa kwa asilimia moja ikinijenga zaidi na kunifanya niwe mtu bora ambaye ni mnyenyekevu nisiyedharau mtu wala kazi ya mtu.

BS ilinifanya nijitegemee mapema bila kutegemea ajira. BS ilimenisaidia naweza kuhudumia familia yangu bila kumpa lawama wala mzigo yeyote.

BS ilinifundisha kuwa Mafanikio ni hatua. Lakini pia BS ilinifanya nigundue kuwa hakuna chochote ambacho utakifanya ambacho Mungu hatakubariki. Lazima ipate riziki yako. Huwezi ukafanya kazi alafu ukalala njaa. Kwa kweli hiyo ni kweli.

NS ilinifundisha kuwa Jambo unalolitilia mkazo ndilo litakalokupa matokeo zaidi. Poa matokeo bora hutokana na consistency yako katika jambo husika.

Kijana, nimeandika hapa sio kuonyesha wapi nimefika, au labda nimefanikiwa, bali ni kwaajili ya kukupa Moyo kuwa hakuna chochote ambacho kinakuzuia usiishi maisha yako. Jina lako, maumbile yako, elimu yako isikufanye ushindwe kuishi.

Mfano, Taikon japo sio mashuhuri sana lakini ni jina kubwa kwa kiasi chake. Lakini hiyo hainifanyi niishi maisha Feki(bandia) ati kisa najulikana. Hicho ni Kiburi. Na sisi Watibeli tunaongozwa na Haki, upendo, Akili na kweli.

Nawatakia siku njema. Acha Nipumzike sasa.

Robert Heriel
Taikon wa Fasihi
Kwa sasa Dar es salaam
 
hongera sana
Eti na mimi chuo nilitaka niwe mfanyabiashara eti niagize chupi nje ya nchi alafu niwauzie wadada 🤦‍♀️

Nasikitika kusema biashara ilikufa ndani ya mwezi hata leo ukiniuliza mtaji wa ile biashara uko wapi hata sijui 😭

Aliyewaumba wanawake alitutega sana wanaume
 
Maudhui yenye roho nyeupe peeeeeee.
Wasomi wengi wanafeli Kwa dharau zao.

Wanaopona ni wale wenye connection tu🐍.
Ila elimu uipatayo,hakikisha unaibadili kuwa fedha.
Vijana wengi wanafeli Kwa kuishi maisha feki,akiamini kwamba wale,au yule ama Hawa watanionaje.

🦅Big up mkuu.Elimu+maarifa+Mahesabu=Mafanikio.

Mafanikio sio mpaka uwe Tajiri,hapana bali uweze kukidhi nahitaji ikiwemo kumiliki familia pia.
 
Maudhui yenye roho nyeupe peeeeeee.
Wasomi wengi wanafeli Kwa dharau zao.

Wanaopona ni wale wenye connection tu🐍.
Ila elimu uipatayo,hakikisha unaibadili kuwa fedha.
Vijana wengi wanafeli Kwa kuishi maisha feki,akiamini kwamba wale,au yule ama Hawa watanionaje.

🦅Big up mkuu.Elimu+maarifa+Mahesabu=Mafanikio.

Mafanikio sio mpaka uwe Tajiri,hapana bali uweze kukidhi nahitaji ikiwemo kumiliki familia pia.

Kheri wenye moyo Safi kwa maàna hao watamuona Mungu
 
Back
Top Bottom