Nasaha za kikwete zilivyo na utelezi!

KAMBOTA

Senior Member
Mar 21, 2011
176
103
Na Nova Kambota,

Watanzania wangali wanaendelea kushangazwa na vituko vya viongozi wao hususani wale wa chama tawala. Kwa jinsi hali ya uropokaji inavyozidi kukithiri miongoni mwa makada wa chama cha Mapinduzi ambao wengi wao ni viongozi wa serikali inayoongozwa na rais Jakaya Kikwete basi hakuna ubishi kuwa itakuwa vigumu sana kubaini yupi mwenye busara miongoni mwao?



Ikiwa takribani mwaka mmoja tangu watanzania watangaziwe "operation vua gamba" ambapo kabla hilo halijaisha ikafuatiwa na vituko vya uchaguzi wa Igunga ambapo yakuandikwa hakika yameandikwa na jalada likafungwa.

Wangali watanzania wakiwa wanatafakari kile kilichomfanya Mkapa kwenda "kuaibika Igunga" huku baadhi wakimpongeza rais Kikwete kwa "kumponza mwenzake" na baadhi wakiamini walau yeye (Kikwete) ana "kabusara kadogo".


Kufumba na kufumbua likaibuka la Arumeru Mashariki ambapo "uozo" umejikita katika sura mbili, huku ya kwanza ikiwa ile ya kitufe cha "ufalme" na "rushwa" ambapo baadhi ya vyombo vya habari vimetueleza jinsi Sioi Sumari alivyofanikiwa kupenya ndani ya kura za maoni ndani ya CCM kwa nguvu nyingine anayoijua yeye ukiacha ile ya hoja ambayo ndiyo haswa inayotakiwa kwenye siasa, sambamba na hilo likaja lile la "Mr Clean Ben Mkapa" ambapo alianza utani majukwaani dhidi ya Vincent Nyerere kama mwenyewe alivyosema , lakini likaibuka la kuibuka tena ambalo pasi na shaka linaihusu CCM na Mkapa, ni lile la " madai ya Vincent Nyerere kuhusu kifo cha Nyerere"

Kama vile hii haitoshi , sasa kila mtanzania ameona kile kilichodhaniwa kuwa ni "kabusara kadogo" ka rais Kikwete kumbe nako hakapo kabisa, hii ni baada ya kauli yake yenye utata aliyoitoa kwenye tuzo za waandishi wa habari hivi karibuni , eti Kikwete "amewataka waandishi wa habari kuzingatia maadili" huu kama si msiba wa kitaifa ni nini?


Kila mwenye akili timamu ameshangazwa na kauli hiyo ya Kikwete ambayo kwa wale waaminio katika ufufuko wa wafu wanajua kuwa haiwezi kufufuka siku ya mwisho. Hivi Kikwete hafahamu mchango wa wanahabari wa nchi hii? Hajui kuwa kuna waandishi wa habari walioimbua serikali yake kwa kashfa za Richmond na Dowans? Hivi Kikwete hatambui kuwa ni waandishi wa habari hawahawa mara kadhaa wamemwambia jinsi alivyoboronga kumteua Ngeleja, Nkya na Mponda? ambao badala ya kupiga kasia sasa wanatoboa mtumbwi ili maji yaingie serikalini? Hivi Kikwete anataka kutwambia hajui ubabe wa serikali yake lilipoliweka gazeti machachari la Mwanahalisi katika kile ambacho mwanaharakati mkongwe Ndimara Tegambwage anakiita ni "uhuru gerezani?"


Ni vigumu kuamini kuwa Kikwete hayajui haya, na kama anayajua kwanini hataki kukiri mchango wa wanahabari? Hivi anataka wafate maadili gani? Kuisifia serikali inayoendesha mgao wa giza? Au inayozalisha sifuri za kidato cha nne? Nini anataka waandishi wafanye? Au anataka wasiandike jinsi mochwari zilivyokuwa ndiyo pekee zinafanya kazi wakati ule wa mgomo wa madaktari? Wakati yeye "akiwakingia kifua" wateule wake? Ama anataka waandishi washike adabu hasa linapokuja swala la kuhoji yale maisha bora aliyoahidi kwa kasi zaidi yameishia wapi? Au ndiyo hizi ajira mpya za kufungua vizibo baa? Hakika Kikwete amejitumbukiza kwenye mgogoro mkubwa na wavuja jasho wa Tanzania ambao wanawaona waandishi wa habari ndiyo sauti yao inayowafanya makada wa CCM kuinamisha vichwa chini kila wanapotakiwa kujibu "maadili ya viongozi" yalifutwa kwa faida ya nani?

Sasa eti Kikwete anatoa wapi "ubavu" wa kuwaasa waandishi wa habari kuwa wasije kugeuza mjadala wa katiba mpya kuwa vurugu? Au Kikwete anataka kuwaaminisha masikini wa Tanzania kuwa waandishi wa habari ni hatari kuliko makada ving'ang'anizi wa CCM? Kwani yeye hafahamu mara zote nchini vurugu husababishwa na watawala waliolewa madaraka? Au ameshasahau ya Pemba na Arusha?


Vyovyote Kikwete anavyofanya atambue kuwa mawazo yenye utelezi ya namna hii kamwe hayawezi kuubadili ukweli kuwa mpaka sasa ni waandishi wa habari pekee waliofanikisha wananchi kutambua kushindwa kwa sera za CCM na serikali yake, huu ndiyo ukweli ambao hata iweje hauwezi kubadilika. Na hakuna ubishi wakati yeye Kikwete na makada wenzake wa CCM wanafaidi posho na mishahara minono huku wakiwataka waandishi "kuzingatia maadili" masikini wote wa Tanzania wanajua hayo ni mawazo yenye "utelezi" kamwe hawawezi kuyashika maana yanaponyoka, badala yake wanawataka waandishi wa habari kuendeleza mageuzi kwa kuzidisha kile kinachojulikana kama "uandishi wa kichokonozi".
 
JK anatakiwa aanze kwanza kuwakumbusha viongozi wa serikali wazingatie maadili ndipo ageukie watu wengine kuwapa ushauri huo.
 
mkuu kweli unayosema yana mantiki lakini kwa pointi iyo uliompigia siungi mkono eti ''waandishi wa habari zingatieni maadili'', ni hiii tu au? simsapoti kikwete lakini leo mkuu tuseme ukweli mengine tunataka vichaka tu ili tutoe madukuduku yetu, ungekumbushia ata za dowans, maisha bora, ahadi zake kidogo pia ningekuona wa maana, mkuu pamoja na yote sie wengine tukiambiwa tunachanganya na zetu.
 
da, umeandika vizuri na hoja zako umezitetea na hii inanipa hamasa kuwa mwisho wa ssm umefika, ni hilo tu!
 
Ujumbe wako utafikia kwenye masikio yaliwekwa pamba na wakati huo wakiwa wanapata wine kwenye viti virefu huku wanawacheka kwa umaskini wenu na kwa kuwa waandishi mnapiga piga tuu kelele ambazo haziendi kokote
 
Back
Top Bottom