Mtatiro: Mjue edward ngoyai lowassa: Nani ni nani uraisi ccm

BUSAMUDA

JF-Expert Member
Nov 12, 2014
612
358
EDWARD NGOYAI LOWASSA: NANI NI NANI URAIS CCM?
HISTORIA YAKE
Edward Lowassa alizaliwa Agosti 26, 1953 katika Kijiji cha Ngarash, Monduli na ndiye mtoto mkubwa wa kiume kwa Mzee Ngoyai Lowassa (atafikisha miaka 62 Agosti mwaka huu). Alianza kusoma katika Shule ya Msingi Monduli kati ya mwaka 1961–1967.
Kisha akaendelea kwenye Shule ya Sekondari Arusha kwa kidato cha kwanza mpaka cha nne kati ya mwaka 1968 - 1971, kabla ya kumalizia kidato cha tano na sita katika Shule ya Sekondari Milambo mkoani Tabora mwaka 1972–1973.
Alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1974–1977 na kuhitimu Shahada ya Sanaa katika Elimu (B.A Education) na baadaye Chuo Kikuu cha Bath Uingereza kwa Shahada ya Uzamili ya Sayansi katika Maendeleo (mwaka 1983–1984).
Baada ya kumaliza chuo kikuu, Lowassa alifanya kazi ndani ya CCM akiwa ofisa wa ngazi ya juu kuanzia wilaya, mkoa na baadaye makao makuu kati ya mwaka 1977–1989.
Aliajiriwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Mikutano ya Kimataifa Arusha (AICC), mwaka 1989–1990.
Lowassa amemuoa Regina na wana watoto watano, wasichana wawili na wavulana watatu. Watoto hao ni Fredrick, Pamella, Adda, Robert na Richard.
MBIO ZA UBUNGE
Lowassa alichaguliwa kuwa Mbunge kupitia kundi la Vijana ndani ya CCM na akashikilia nafasi hiyo kati ya mwaka 1990 hadi 1995 na mwaka 1993 aliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais (Haki na Mambo ya Bunge), kabla ya kuhamishiwa Wizara ya Ardhi na Makazi akiwa Waziri mwaka 1993–1995.
Kwenye Uchaguzi Mkuu wa kwanza wa vyama vingi (mwaka 1995), Lowassa alishinda ubunge kwa asilimia 87.3. Alikaa bila uteuzi wowote kwa miaka miwili. Mwaka 1997–2000, Rais Benjamin Mkapa alimteua kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira na Kuondoa Umasikini).
Kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000 aligombea tena ubunge wa Monduli na kushinda kwa mara ya tatu. Rais Mkapa akamteua kuwa Waziri wa Maji na Mfugo hadi mwaka 2005.
Kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2005, aligombea ubunge na kushinda kwa asilimia 95.6. Rais Jakaya Kikwete alimteua kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania na Bunge likamthibitisha kwa kura 312.
Uwaziri mkuu wa Lowassa ulikoma Februari 2008, alipojiuzulu kutokana na kashfa ya Richmond. Kamati Maalumu ya Bunge ya watu watano iliyoongozwa na Dk Harrison Mwakyembe ilisisitiza kuwa wizara ya Nishati na Madini na Ofisi ya Waziri Mkuu ndizo zinazopaswa kubeba lawama ya uingiaji wa mkataba mbovu na Richmond, kampuni ambayo uchunguzi ulionyesha kuwa ni ya mfukoni mwa watu huku Serikali ikilazimika kulipa mabilioni ya fedha katika mkataba ambao una upungufu makubwa.
Wakati Lowassa analitaarifu Bunge kuwa amemuandikia Rais barua ya kujiuzulu, alisisitiza kuwa “…anafanya hivyo ili kulinda taswira ya chama chake na Serikali na kuwa shida ya wabaya wake ni u-waziri mkuu na siyo kingine…”
Baada ya kujiuzulu, Lowassa aligombea ubunge kwa mara nyingine Monduli (mwaka 2010) na kupata asilimia 90.93 ya kura zote na hadi sasa ndiye mbunge wa jimbo hili japokuwa amekwishaaga kwamba hatagombea tena kiti hicho.
MBIO ZA URAIS
Lowassa ni miongoni mwa wana CCM 17 waliochukua fomu kuwania urais mwaka 1995 lakini aliyepitishwa ni Mkapa.
Mwaka 2005, hakugombea urais ila alikuwa na mipango ya muda mrefu ya kumsaidia rafiki yake, Kikwete na inadaiwa kuwa makubaliano ya Kikwete na Lowassa yalikuwa kwamba mwenzake akishaongoza nchi kwa miaka 10 (yaani 2005 – 2015) atamtengenezea njia 2015 – 2025.
Kabla mipango hiyo haijatimia ndipo Lowassa akapata kile ambacho Kikwete anakiita “ajali ya kisiasa”. Lakini hata baada ya ajali ya kisiasa kutokea, nimeambiwa walikuwa na makubaliano mengine kuwa “Kikwete angesaidia kumsafisha rafiki yake” ili mwaka huu 2015 ufikapo aweze kumuachia Ikulu ya Magogoni.
Tangu Lowassa aachie uwaziri mkuu na tangu agundue kuwa Kikwete ‘amemkalia” kimya, alianza juhudi zake mwenyewe za kujitengenezea njia ya kuelekea Ikulu na amefanya mambo mengi yanayoashiria kuwa amedhamiria kuingia Magogoni.
Kama kuna mtu nchi hii ametoa michango mingi ya rasilimali fedha katika kuchangia misikiti, makanisa, vijana, vikundi, harambee na vinginevyo, hakuna kama Lowassa. Michango hiyo, wachambuzi wengi wanaihusisha na mbio zake za urais.
NGUVU YAKE
Nguvu ya kwanza ya Lowassa ni umaarufu, yeye ni maarufu kuliko wagombea wote wa CCM, ndani na nje ya chama hicho. Yeye ndiye anatajwa kuliko wenzake wote na hili halina shaka.
Nguvu ya pili ya Lowassa iko kwenye uwezo wa kirasilimali (watu na fedha). Lowassa na mtandao wake wana rasilimali za kutosha kuendesha harakati hizi. Kwa siasa za CCM ya miaka hii iliyowatupa mkono wakulima na wafanyakazi, rasilimali (fedha na watu) ni kila kitu. Jambo hili linampa nguvu zaidi dhidi ya wagombea wenzake ambao nao wanahaha huku na kule kuzisaka.
Jambo la tatu linalompa Lowassa nguvu ni kuwahi kuwa Waziri Mkuu na kuijua kwa undani mifumo ya uendeshaji wa nchi na hata kuisimamia. Ushawishi wake kwa mifumo hiyo umeendelea hadi sasa na nimeambiwa kuwa kuna taasisi muhimu za kidola zimegawanyika kwa sababu ya kumuunga mkono, watendaji serikalini nao wamegawanyika kwa ajili yake na kila mmoja ana hofu kuwa asipofanya “booking” kwenye kambi ya Lowassa, anaweza kukosa vyeo bwerere kwenye Serikali ijayo.
Alipokuwa Waziri Mkuu alionyesha misimamo ya kiuongozi na kuthubutu kwingi kunakotakiwa kufanywa na mkuu wa nchi, lakini misimamo yake na uthabiti wake unahusishwa pia na kujikuta mara nyingi akifanya uamuzi wenye makosa mengi au wenye kuzua maswali mengi ya kisheria.
Lakini jambo la nne ni kuzijua njia zilizompa madaraka Kikwete mwaka 2005. Kati ya wagombea wote wa CCM kwa sasa, huenda ni Lowassa peke yake ndiye anayezijua vizuri njia alizotumia Kikwete kujenga mtandao mkubwa wa ushindi mwaka 2005, makanisani, misikitini, vyuoni na kwingineko, hadi nyumba za ibada zikaimba “Kikwete ni chaguo la Mungu”. Kwa hiyo anajua njia ipi apite kuwashinda wagombea wengine.
UDHAIFU WAKE
Udhaifu wa kwanza wa Lowassa ni kuwa karibu mno na watu wenye majina yenye taswira zinazotia shaka. Kuna msemo mmoja wa Kiingereza unaosema, “The bird with same feathers, flocks together” (Ndege wenye mabawa yanayofanana, huruka pamoja). Marafiki wakubwa wa Lowassa ni watu wenye pesa na matajiri, hilo linaweza kumkwamisha katika harakati zake.
Ndiyo maana jamii imegawanyika mno juu yake, wengine wakimuona kama mtu mwenye mipango mingi ya kifedha na mfanyabiashara zaidi kuliko kiongozi wa nchi huku wengine wakimuona kama kiongozi anayethubutu.
Ikiwa Lowassa hataweka wazi mgongano wa masilahi ulioko kati yake na baadhi ya wafanyabiashara wenye tuhuma lukuki, jamii itaendelea kumuona kama mtu asiyeweza kukemea maovu.
Kiongozi mmoja wa CCM ameniambia kuwa, hata mwaka 1995, moja ya mambo yaliyomfanya Mwalimu Julius Nyerere asimuone Lowassa kama chaguo, ni suala la uhusiano wake na matajiri na watu wenye fedha na ilifikia wakati mwalimu akahoji, “…kijana huyu anatoa wapi fedha zote hizi?”
Udhaifu mwingine wa Lowassa uko katika eneo la mapambano dhidi ya rushwa. Ikumbukwe kuwa Tanzania ilipofikia na uchumi wake unavyozidi kuporomoka, moja ya kazi kubwa ya Serikali ijayo itapaswa kuwa “mapambano dhidi ya rushwa” kwa maneno na vitendo vinavyoonekana.
Alipokuwa Waziri Mkuu hakuonyesha makeke yake kwenye mapambano dhidi ya rushwa na hakutaka kujihusisha wala kujionyesha kuwa anawachukia wala rushwa. Pamoja na kuonyesha utendaji mzuri akiwa Waziri Mkuu, kipengele hiki kilimuangusha na hadi leo hii kokote kule anakokwenda hapendi kuzungumzia rushwa na wala rushwa. Huu ni udhaifu wake mwingine mkubwa.
NINI KINAWEZA KUMFANYA APITISHWE
Lowassa ana uzoefu wa zaidi ya miaka 38 ya kuitumikia CCM na Serikali, ameongoza wizara kadhaa hadi kufikia kuwa Waziri Mkuu, bila shaka, uwezo wake wa kiuongozi, utendaji na usimamizi vilidhihirika. CCM inaweza kuhitaji mtu wa aina yake, ambaye iliwahi kupima utendaji wake na labda kuridhishwa nao.
Jambo la pili ambalo linaweza kumvusha ni woga wa CCM ‘kuvunjika’. Kuna taarifa nyingi zinazoonyesha kuwa vikao vya CCM visipolipitisha jina lake likafikishwa mkutano mkuu ili kura ndizo ziamue, wajumbe wa mkutano huo wanaweza kutoshiriki na huenda anaweza kukihama chama hicho na kundi kubwa la viongozi na wanachama. Ikiwa CCM inazifahamu taarifa hizi, inaziamini na kuzithibitisha, huenda ikampitisha na kukubali yaishe.
Jambo la tatu linaloweza kumfanya apitishwe ni kuwa na mtandao mkubwa na ufuasi uliopitiliza kuliko mgombea mwingine yeyote wa chama hicho. Ukimgusa Lowassa kwenye mtandao wa kijamii utajibiwa haraka mno, ukimsema gazetini makala itajibiwa haraka na ukimsema vibaya kijiweni kwa vijana utakodolewa macho. Amejipanga vilivyo na CCM inaweza kuhitaji mgombea wa aina yake ambaye ana nguvu ya kipekee ya kuweza kukisaidia chama hicho kupata ushindi.
NINI KINAWEZA KUMWANGUSHA?
Mambo matano yanaweza kumwangusha Lowassa. La kwanza ni makundi. Kama nilivyoeleza, yeye ndiye mtu mwenye kundi kubwa kuliko wagombea wote ndani ya CCM, ikiwa chama hicho kitaamua kumpata mtu wa kati ‘neutral’ ili kukifanya chama kisitetereke, yeye ndiye atakayekuwa wa kwanza kuenguliwa.
Lakini jambo la pili ni kashfa ya Richmond. Tangu kashfa hiyo ilipotokea, Lowassa hakuwahi kuiongelea tena na hajawahi kuwaeleza Watanzania alihusikaje na kama yeye hakuhusika ni kina nani waliohusika kwa majina. Ukweli ni jambo muhimu kwa mtu anayehitaji kuongoza nchi. Ukituhumiwa kwa kashfa kubwa kama ya Lowassa halafu unasema tu hukuhusika bila kueleza nani walihusika huku wewe ndiye ulikuwa Waziri Mkuu, inajenga taswira kuwa kuna jambo kubwa unalificha na husemi ukweli kwa jamii yako. Hili linaweza kumhukumu. CCM inaweza kumuondoa Lowassa ili kuondokana na mgombea mwenye madoa hata kama haina uthibitisho na madoa hayo kwa asilimia 100.
Jambo la tatu linaloweza kumchuja Lowassa ni afya yake. Pamoja na kuwa afya ni jambo binafsi na siri ya mtu lakini kwa kiongozi, kila jambo lake ni mali ya umma. Rais Kikwete alipougua tezi dume aliutangazia umma na hakuficha. Kwa kipindi kirefu Lowassa amekuwa akionekana kama mgonjwa na si siri kuwa amekuwa akipata matibabu katika hospitali za kimataifa nje ya nchi.
Anapaswa awaeleze Watanzania nini kinamsibu, la asipofanya hivyo wapinzani wake kisiasa wanaweza kuendelea kulitumia jambo hili ipasavyo na chama chake kikaona lina mantiki na kikalitumia kumsulubu kama “unfit person to lead the nation”. Kila chama kinahitaji mgombea urais wake awe na afya bora, isiyofichwa na inayoeleweka. Anapaswa kujitokeza na kufafanua hili haraka na hasa ikizingatiwa muda umekwenda sana.
Michango ya kujitolea kila kukicha katika taasisi mbalimbali, harambee, nyumba za ibada na maeneo mengine ni jambo jingine linaloweza kumhukumu. Lowassa amejitolea mno katika eneo hili. Chama chake kinaweza kujiuliza kwa nini mtu anayejiandaa kugombea urais ajitolee kwa kiwango hiki kusaidia kuchangisha fedha na hata yeye mwenyewe kuchangia kila panapotokea matukio makubwa?
Je, nia yake ni sahihi? Mwalimu Nyerere aliwahi kusema kuwa “Ikulu hakuna biashara” na CCM inaweza kujitathmini ikiwa mgombea wa namna hii akiingia Ikulu hataanza kutafuta mbinu ya kujirudishia fedha alizokuwa akichangia. Eneo hili si salama kwa Lowassa.
Jambo la tano ni madai kuwa kuna maelewano hafifu na Rais Kikwete. Jambo hilo hakuna aliyethibitisha, lakini huwezi kulidharau moja kwa moja. Katika siasa, ukishindana na walioshikilia “mpini” unaweza kuanguka mahali usipotarajia. Pamoja na kuwa “hawakukutana barabarani”, ukweli ni kuwa Lowassa na Kikwete wa sasa si wale ‘ma-comrade’ wa 2008 kurudi nyuma. Hawa wa sasa ni watu tofauti na duru za ndani ya Serikali zinaonyesha kuwa haziivi.
Kama hivyo ndivyo basi, karata za Lowassa zinaweza kuingia shakani kwa sababu ya kutoimarisha uhusiano wake na Rais anayeondoka madarakani, maana kwa siasa za kurithishana kwa kujuana katika vyama tawala barani Afrika, lazima tukubali ukweli kuwa, Rais aliyeko madarakani ana mchango na ushawishi mkubwa katika kutengeza rais ajaye.
ASIPOCHAGULIWA (MPANGO B)
Namuona Lowassa akiwa na mipango mitatu ikiwa hatapitishwa kugombea urais:
Mpango wa kwanza ni kuendelea kuihamasisha jamii kimaendeleo katika taasisi za kidini, za kiraia, makundi ya vijana, wazee na wanawake kwa mtindo huuhuu ambao amekuwa akiufanya kati ya 2008 –2015 na hata kutoa michango yake na marafiki zake kwa jamii.
Mpango wa pili ni kuishauri Serikali katika maeneo mbalimbali ya kisera na kiusimamizi. Kwa sababu alipokuwa Waziri Mkuu alionyesha usimamizi mzuri na ufuatiliaji imara katika ofisi za umma, anaweza kuifanya kazi hiyo kiushauri.
Mwisho ni kurudi kwenye biashara. Lowassa ni mfanyabiashara katika sehemu kubwa ya maisha yake. Ikiwa hatagombea urais kwa tiketi ya CCM itakuwa muda muafaka kwake kurejea na kusimamia biashara zake na kuachana na siasa za majitaka kama alivyowahi kutamka mmoja wa marafiki zake.
HITIMISHO
Nguvu ya Lowassa ndani ya CCM haimithiliki na hofu ya chama hicho kuwa kumuacha nje ya ulingo kutakitetemesha haikwepeki. Lakini ukweli ni kuwa ndani ya CCM “kuna minofu mingi” ambayo inawazuia vigogo wakubwa wasiondoke na kuhamia vyama vingine hata kama hawakupitishwa kugombea urais. “There is too much stake to eat in CCM than going out”.
Ndiyo maana bado CCM ina nafasi ya kujichagulia mgombea inayemtaka na vigogo wanaotajwa kuitikisa kama Lowassa wakiogopa kuondoka kwa sababu wamekaa serikalini muda mrefu na sasa hawawezi kumalizia maisha bila mfumo huo waliouzoea.
Kwa hiyo, nadhani Lowassa ataendelea kuwa mwanachama mtiifu kwa CCM akiwa Rais au akiwa raia wa kawaida. Kama kuna vyama vya upinzani vilikuwa “vinamtumbulia” macho kama fisi asubirivyo mkono wa binadamu udondoke, ni vyema vikajipanga kupata wagombea wake imara na vijijenge. Pamoja na yote haya namtakia kila la heri Mzee Edward Lowassa katika safari yake ya kisiasa.
KUHUSU MCHAMBUZI:
Julius Mtatiro ni Mchambuzi wa Masuala ya Kisiasa na Kijamii, ana uzoefu mkubwa wa uongozi wa kisiasa hapa Tanzania. Ana Cheti cha Juu cha Sarufi na Lugha, Shahada ya Sanaa “B.A” katika Elimu (Lugha, Siasa na Utawala), Shahada ya Uzamili ya Utawala na Uongozi (M.A) na ni mwanafunzi wa fani ya sheria (L LB) – Anapatikana kupitia
call_skype_logo.png
+255787536759,(juliusmtatiro@yahoo.com) Uchambuzi na huu unatokana na utafiti na maoni binafsi ya mwandishi). (Uchambuzi huu umechapishwa na Gazeti la Mwananchi la Jumatatu, 11 Mei 2015).
 
Ameongea ukweli kabisa kwenye swala la afya mgombea uraisi kutoka chama chochote lazima akubali kwenda kupimwa afya na iwekwe wazi kwa wananchi wote.
 
Ameniudhi kidogo japo uchambuzi mzuri
,--fedha ni kila kitu''- Hili halikathibitika vema
 
Mimi ningekuwa member wa CUF ningejiuliza mno
inakuaje kiongozi wa CUF anapata muda wa kuwajadili wagombea wa CCM?

hata kama ni 'taaluma' yake kujadili haikwepeki kwamba yeye ni kiongozi wa CUF
na jukumu lake la kwanza ni kuiuza CUF kwa wananchi
 
Mojawapo ya changamoto ninayoiona ni hii hapa...
Jambo la pili ambalo linaweza kumvusha ni woga wa CCM ‘kuvunjika’. Kuna taarifa nyingi zinazoonyesha kuwa vikao vya CCM visipolipitisha jina lake likafikishwa mkutano mkuu ili kura ndizo ziamue, wajumbe wa mkutano huo wanaweza kutoshiriki na huenda anaweza kukihama chama hicho na kundi kubwa la viongozi na wanachama. Ikiwa CCM inazifahamu taarifa hizi, inaziamini na kuzithibitisha, huenda ikampitisha na kukubali yaishe

Naona ile njozi ya utawala kutoka kanda ya kaskazini ukianzia hapa, maana SIASA ni majukwaani tu wakishuka chini ni cheers kwenda mbele. Ucheleweshwaji wa kutotaka kumtaja mgombea mapema jwa CDM ni moja ya green light kwa huyu jamaa very soon.

Wanajamvi:
Tuvute subra.
 
Mimi ningekuwa member wa CUF ningejiuliza mno
inakuaje kiongozi wa CUF anapata muda wa kuwajadili wagombea wa CCM?

hata kama ni 'taaluma' yake kujadili haikwepeki kwamba yeye ni kiongozi wa CUF
na jukumu lake la kwanza ni kuiuza CUF kwa wananchi

The Boss huyu Julius Mtatiro alistep aside mambo ya chama na cheo chake akamuachia Mwana Mama wa CUF Mama Sakaya yeye akaenda kupiga Shule.So wakati anafanya hayo yote kwa sasa yuko nje ya mfumo wa uongozi wa Chama cha CUF mpaka atakapomaliza Shule hapo UDSM kama sikosei.
 
The Boss huyu Julius Mtatiro alistep aside mambo ya chama na cheo chake akamuachia Mwana Mama wa CUF Mama Sakaya yeye akaenda kupiga Shule.So wakati anafanya hayo yote kwa sasa yuko nje ya mfumo wa uongozi wa Chama cha CUF mpaka atakapomaliza Shule hapo UDSM kama sikosei.

Still kuna kitu hakiko sawa..ninavyoona...
ni kama anakubali 'udhaifu wa CUF' kiaina...
 
Still kuna kitu hakiko sawa..ninavyoona...
ni kama anakubali 'udhaifu wa CUF' kiaina...
The Boss kwa kuwa ndiyo fani aliyosomea ni sawa...tena ni very advantageous to him as a Politician & Analyst of his Career..Itawasaida sana vyama vya upinzani kuwatambua CCM, lakini pia itawainua na kuwapolomoa baadhi ya CCM Politicans ...na toka ameanza mpaka sasa amefanya analysis nzuri sana kupia SWOT ANALYSIS na watu wengi wamemwelewa kwa kina kiasi kuwa ametumika kama kipimo cha kuwapima.

Upinzania na wao CCM wakiwa waerevu kupitia uchambuzi huo ni murua sana kujua mambo makuu manne [SWOT] ambayo ni STRENGTH, WEAKNESS, OPPORTUNITIES AND THREATS na hivyo itawasaidia sana kusimama na kujua mwerekeo pande zote mbili.
 
Mimi ningekuwa member wa CUF ningejiuliza mno
inakuaje kiongozi wa CUF anapata muda wa kuwajadili wagombea wa CCM?

hata kama ni 'taaluma' yake kujadili haikwepeki kwamba yeye ni kiongozi wa CUF
na jukumu lake la kwanza ni kuiuza CUF kwa wananchi

The boss you must be a very weak. Mtatiro Hana muda wakupoteza he is a politician as well as a political analylist so what you expect of him. Tunakushukuru Sana ndugu Mtatiro nakumbuka Sana enzi zetu DARUSO .

Achana na wavivu wakusoma Kama the Boss
 
Mimi ningekuwa member wa CUF ningejiuliza mno
inakuaje kiongozi wa CUF anapata muda wa kuwajadili wagombea wa CCM?

hata kama ni 'taaluma' yake kujadili haikwepeki kwamba yeye ni kiongozi wa CUF
na jukumu lake la kwanza ni kuiuza CUF kwa wananchi

Mtatiro ni kiongozi wa nn cuf?
 
Back
Top Bottom