Msemaji wa Serikali: Thamani misaada ya maafa ya Hanang imefikia Tsh. Bilioni 7.7

BARD AI

JF-Expert Member
Jul 24, 2018
3,376
8,119
Serikali ya Tanzania imesema thamani ya misaada iliyotolewa na wahisani mbalimbali kwenye maafa ya Hanang imefikia Sh7.7 bilioni.

Kiwango hicho kinajumuisha misaada ya chakula na mahitaji muhimu ya kibinadamu ambavyo thamani yake ni Sh2.5 bilioni huku fedha taslimu zikifikia Sh5.2 bilioni.

Taarifa iliyotolewa leo Jumapili Desemba 24, 2023 na Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi, imesema fedha taslimu zinajumuisha Sh2.5 bilioni zilizotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan na Sh2.7 bilioni zilizomo kwenye akaunti ya Mfuko wa Taifa wa Misaada ya Maafa, inayosimamiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu.

“Kati ya fedha hizo, kiasi cha Sh2.2 zimechangwa na taasisi na mashirika ya umma kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina na kiasi kilichobaki cha Sh419 milioni kimechangwa na wahisani mbalimbali,” imeeleza taarifa hiyo.

Hata hivyo, Serikali imeendelea kupokea na kugawa misaada ya chakula na mahitaji muhimu kwa waathirika wa maafa hayo asubuhi ya Desemba 3, mwaka huu huko Hanang mkoani Manyara.

“ Serikali inawashukuru Watanzania kwa utu, upendo, uzalendo na moyo wa kujitolea ambao umesaidia kupatikana kwa chakula cha kutosha na mahitaji muhimu ili kuwasaidia waathirika kuendelea na maisha yao,” imesema taarifa hiyo.

Kupitia taarifa hiyo, Serikali inatoa wito pia kwa wanaoendelea kuleta misaada kujikita zaidi katika vifaa vya ujenzi.

Misaada yaendelewa kugawiwa

Pia, katika taarifa hiyo Serikali imesema misaada mbalimbali imendelea kutolewa na kugawiwa kama mahindi, ngano, mchele , maharage, mafuta ya kula na maziwa.

Mingine ni unga wa lishe kwa watoto, mayai, sabuni, magodoro, mablanketi, mashuka, mikeka, ndoo, majiko ya kupikia ya gesi na mitungi yake, masufuria, nguo, viatu na kandambili.

Tangu wiki iliyopita, wananchi wamekuwa na ratiba za kwenda kupokea misaada kila siku kutokana na wingi wa misaada hiyo na kwa wastani kila kaya inapata chakula cha kutosha miezi sita au zaidi.

Kwa baadhi ya bidhaa kama sukari, wananchi hao wanapewa ya kutosha kutumia kwa zaidi ya miaka miwili kwa mujibu wa vipimo vya lishe.

“Utaratibu wa kugawa misaada hii unaoratibiwa na Idara ya Maafa chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu ikishirikiana na uongozi wa Mkoa wa Manyara na Wilaya ya Hanang pamoja na kamati zao za usalama, unatumia watalaamu kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu.

“Mgawo wa misaada hii unalenga kwanza waathirika 1,292 waliothibitika kupoteza nyumba zao ama kuharibika au kuingia tope. Idadi hii ilipatikana baada ya tathmini ya kina ya picha za satelaiti, rekodi za sensa, ukaguzi halisi wa nyumba hadi nyumba na rekodi za Serikali za mitaa katika ngazi ya vitongoji, vijiji na kata,” imesema taarifa hiyo.

Mpaka sasa ni siku 21 tangu kutokea maporomoko ya matope kutoka Mlima Hanang na kuathiri vijiji vinne vilivyokuwa kando ya mlima huo na kata nne za mji mdogo wa Katesh na kusababisha vifo vya watu 89.

“Hadi sasa majeruhi wanne bado wanatibiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara na mmoja amepelekwa Hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma. Jumla ya majeruhi walikuwa 139,” imefafanua taarifa hiyo.

MWANANCHI
 
Back
Top Bottom