Mke kukimbia nyumba, ni kuzidiwa?

Mzee Mwanakijiji

Platinum Member
Mar 10, 2006
33,483
40,002
Nipe kalamu nishike, hoja zangu niandike,
Nipe nami nisikikike, walimwengu wapilike,
Mnipe niliandike, na hili lifahamike,
Mke kukimbia nyumba, si wizi ni kuzidiwa!!!

Kapigwa mtu kikumbo, mke kaachia nyumba
Kalia bwana Mahimbo, kwa jaji kenda kuomba
Akatungia na wimbo, kamshinda hata Komba,
Mke kukimbia nyumba, si wizi ni kuzidiwa!!!

Kaja dada Josephina, kamuaga kwa kuzira
Mumewe akamnuna, na kusema kwa hasira,
Huyo mama akanena, pamekuwa na ukora,
Mke kukimbia nyumba, si wizi ni kuzidiwa!!!

Kibanda nakuachia, baba nanii naondoka,
Huku mama analia, na mizigo ameshika,
Kwangu nakukimbilia, kwako hapa nimechoka,
Mke kukimbia nyumba, si wizi ni kuzidiwa!!

Kaenda alikokwenda, maisha kuyaanzia,
Akataka pa kupenda, na moyo kutulizia,
Kampata wake nyonda, zilipendwa kaachia,
Mke kukimbia nyumba, si wizi ni kuzidiwa!!

Mtu kumwacha mwenziwe, huyo anayo sababu,
Kulazimisha isiwe, ni mwanzo kupata tabu,
Kamwe mgonjwa usiwe, nenda upate tabibu,
Mke kukimbia nyumba si wizi ni kuzidiwa!

Kaondoka ana kisa, si letu hilo ni lao,
Kumhukumu mkosa, ati kaacha mbachao,
Vikizidi vinatesa, mtu hurudia kwao,
Mke kukimbia nyumba, si ziwi ni kuzidiwa!!

Ukimtenda mwenzio, wengine wanangojea,
Mnyanyase na vilio, wapo wanaoombea,
Wawe ndio kimbilio, ndio wenza wagombea,
Mke kukimbia nyumba, si wizi ni kuzidiwa!

Ukiwa naye mwandani, mpende akakupende,
Simfanye kisirani, mtoto wa watu akonde,
Utenda mahakamani, ati jaji akulinde,
Mke kukimbia nyumba, si wizi ni kuzidiwa!

Utadai bilioni, ati mke umeporwa,
Kakuaga hadharani, hakusubiri kuparwa,
Watakucheka watani, umezidiwa hujaporwa,
Mke kukimbia nyumba, si wizi ni kuzidiwa.

Natama ninatuwama, wa kijiji nimesema,
Shujaa amesimama, kapendwa na huyo mama,
Haki yako kulalama, lakini kwanza tazama,
Mke kukimbia nyumba si wizi ni kuzidiwa!

Na. M. M. Mwanakijiji (Sauti ya Kijiji)
 
Thanx Mwanakijiji nimeupenda utunzi wa shairi hili
Lakini hii ni spesho kwa nani ?utunzi wako umebobea
 
uh uuh:smile-big: aaah:smile-big:..spesho dekikesheni to mr. MYmbo..hii imetulia Mwanakijiji, naomba fanya uwezavyo kwa gharama yoyote ile patia sisi utenzi mzuri kwa jina la SARAKASI JUKWAANI-AISEE.
 
Asante mzee! heshima kwako. mahimbo aache kwenda kudai kama alishindwa kulea wenzake mafundi.
 
Mwanakijiji uko juu. We noma...
Na mimi yakinishinda si naweza mkimbia tu ee..
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom