SoC02 Mambo haya yanaweza kuboresha Sekta ya Michezo nchini Tanzania

Stories of Change - 2022 Competition

Shitumbula

New Member
Jul 13, 2022
2
1
Kwa muda mrefu sana nchi yetu imekuwa ikipambana kwa kila hali ili kuhakikisha inajiweka kwenye nafasi nzuri katika sekta ya michezo hususani kwenye mashindano ya kikanda, bara na yale ya kimataifa. Jitihada hizi zimekuwa zikifanyika mara kwa mara lakini bado mafanikio yake hayaendani na mategemeo ya watanzania kuhusu sekta hii.

Yafuatayo ni mambo ambayo nchi ikiyazingatia tunaweza kuishangaza dunia kwa siku zijazo na huenda tukaondoa tatizo la ajira kwa kizazi hiki.

1. Kuanzishwa kwa shule maalumu za michezo nchini.
Idadi kubwa ya shule zilizopo nchini na zinazoitwa shule za vipaji hazijawekewa mfumo wa kuwatenga wale wenye hamasa za Michezo dhidi ya wale wenye hamasa katika taaluma zingine. Mfano mwanafunzi anachaguliwa kwenda katika shule hizo si kwamba anacho kipaji bali ana alama nyingi au uwezo wa kitaaluma. Shule hizi zinapaswa kutengwa na kuwa na miundombinu ya michezo husika tu. Kwa kufanya hivi kutaongeza ari na hamasa katika kuinua sekta ya michezo nchini Tanzania.

2. Kuhimiza na kufufua michezo kwa kuzingatia uzoefu wa kikanda au mazingira husika.
Ni jambo la ajabu na la kustaajabisha kwa leo kuona makundi ya timu za wanamichezo wetu wanaotuwakirisha kwa zaidi ya miaka hawaendani na uzoefu wa kikanda au mazingira husika. Kwa mfano nini kinasababisha tusipate wawakilishi wa mchezo wa kuogelea kutoka Zanzibar, Kilwa, Ukerewe, Mwanza, Musoma, Songwe, Ruvuma, Geita au Kigoma ambako Kuna makundi makubwa ya wavuvi na ambao wamekuwa na uzoefu wa maji katika mazingira mbalimbali? Kwa kuwachukua watu hawa ambao wanao uzoefu tutatumia muda mdogo na gharama chache kuwaelekeza mbinu na kanuni za kufuata ili kushinda mchezo huu. Pia leo utashangaa Tanzania hatuna wawakilishi katika mchezo wa baiskeli wakati kuna ndugu zangu kule Shinyanga, Tabora, Geita, Tanga, Simiyu na Mwanza ambao wanasifika katika kuzidhibiti baiskeli ukanda huo. Hawa wakiundiwa mikakati na kupewa kanuni na taratibu za kufuata ili kushinda mchezo huu tunaweza kuishangaza dunia kwa muda mchache.

Pia tunaweza kuzingatia hivyo kwa michezo mingine Kama tunavyoona mafanikio yalivyo katika riadha na mikoa ya Manyara, Arusha na Singida. Mamlaka ziangalie kwa kuhimiza kupata wawakilishi wa michezo kadhaa kwa kuzingatia uzoefu wa kikanda au mazingira husika ya wanamichezo wetu na jinsi wanavyoweza kumudu

3. Kujengwe kituo cha pamoja cha michezo nchini( National Sports Academy).
Nchi nyingi ambazo zimeweza kufanikisha katika michezo mbalimbali zimewekeza katika vituo vya michezo ya pamoja ya nchi. Mfano Uganda wana Kampala Sports Academy, Kenya wanacho kituo cha michezo cha Kasarani. Leo hii tunaona mashindano mengi ya michezo yanafanyika katika sehemu hizo na kuibua vipaji ambavyo vinavunja rekodi kwenye mashindano ya kimataifa kama vile jumuiya ya madola. Kwa mfano mashindano ya michezo shule za msingi na sekondari yaani UMITASHUMTA na UMISETA yangepaswa kuwa yanafanyika katika kituo kimoja cha kitafa kuliko kuwa na mizunguko ya kila mwaka jambo ambalo limekuwa likirudisha nyuma morali na ari ya michezo nchini. Hebu chukulia pasipo kuwa na kituo cha pamoja mikoa Kama Katavi, Rukwa, Kigoma, Mara, Ruvuma, Geita na Simiyu itapewa nafasi ya kuandaa michezo kwa kuzingatia vigezo na mazingira ya michezo yenyewe

4. Kuanzishwa kwa mfuko wa pamoja wa kitaifa wa udhamini kwa wanamichezo wetu.
Serikali kupitia wizara na mamlaka za Michezo nchini zinapaswa kuja na mpango wa kuwa na mfuko utakaolenga kuboresha vipaji vya wanamichezo wanaoibiliwa katika mashindano mbalimbali. Leo hii kuna vijana wengi sana nchini ambao miaka takribani kumi hivi waliong'ara kwenye mashindano ya kitaifa ya UMISETA, UMITASHUMTA, KILI Marathon, SERENGETI Marathon, Rock City Marathon hawajulikani walipo kwa sababu tu ya kukosekana kwa udhamini kwa wanamichezo hao. Mfano mdogo mwaka jana nilkutana na kijana ambaye miaka ya hivi karibuni alishika nafasi ya pili katika mchezo wa riadha kwenye mashindano yaliyofanyika mkoani Pwani lakini huwezi amini anavyo vyeti vya ushindi alivyokabidhiwa akiviangalia huku ajira yake kwa sasa ikiwa ni saidia fundi mtaani.

Naamini kama huyu kijana aliyekuwa wa pili ndivyo alivyo hata huyo wa Kwanza pia atakuwa katika kundi hili la kukosa udhamini wa kuendeleza vipaji vyao. Hivyo mamlaka ziangalie kwa jicho la tatu katka kuendeleza kwa kuweka mikakati ya mfuko wa pamoja kuwasaidia.

5. Jamii yetu itambue kuwa michezo ni ajira kwa Sasa.
Kwa kuasi kikubwa sana jamii bado haijatilia mkazo katika kutambua umuhimu wa michezo Kama ajira. Leo hii tunayo mifano mingi sana ya vijana wetu wa kitanzania ambao kupitia michezo wamejiwezesha na kutambulika kwa kiasi kikubwa sana. Mfano Mbwana Samatta, Simon Msuva, Hassan Mwakinyo, Felix Simbu, Mwanamisi Omar, Thomas Ulimwengu na wengine wengi. Hawa Kama wangebanwa au kuambiwa kuwa michezo si kitu chochote au kutiwa moyo basi huenda tusingekuwa nao katika historia ya michezo nchini Tanzania.

Kwa kuhitimisha, ni vyema wadau wa michezo nchini kuangalia dunia inaendaje kwa sasa ili kuingiza na kuchochea ushindani kwenye tasnia ya michezo ili nasi tuanze kuleta medali, makombe na tuzo kadhaa kwenye nchi yetu. Tukifanya hivi tunaweza kuondokana na ile dhana ya kuwa sisi ni kichwa cha mwendawazimu.
 
Back
Top Bottom