Maandamano vyuo vikuu

VUTA-NKUVUTE

JF-Expert Member
Nov 25, 2010
6,135
17,802
KITOVU CHA MAANDAMANO YA WANAFUNZI VYUO VIKUU HIKI

Si tena habari ya kusimuliwa.Kila macho na masikio yanaona na kusikia yanayotokea.Karibu Vyuo vikuu vyote vimeshaandamana kulalama juu ya utendaji kazi wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu.Lawama lukuki zatupwa kwa Bodi.Bodi yajitetea.Haisikiki,haieleweki.Watupa lawana wanaamini wanachokilalamikia,Bodi inaamini kwa inachojitetea.Jamii inashindwa kumjua mkweli nani.Mambo shaghala-baghala!

Kwa kifupi,Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu ilianzishwa kwa Sheria Nambari 9 ya Mwaka 2004 ijulikanayo kama Sheria ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu.Bodi hii ilizinduliwa tarehe 30/03/2005 na aliyekuwa Waziri wa iliyokuwa Wizara ya Elimu ya Juu,Sayansi na Teknolojia,Mh.Dr.Pius Ng’wandu.Ikaanza kufanya kazi mwezi Julai,2005.Hii yamaanisha kuwa wanafunzi wa kwanza kutumia huduma za Bodi hii ni wale wa mwaka wa masomo wa 2005/2006 ambao ulianza mwezi Septemba,2005.

Bodi hii ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu ‘yajiuza’ na kaulimbiu kuwa ipo kwa ajili ya wanafunzi waliopata udahili kwenye Vyuo Vikuu lakini hawana uwezo wa kugharimia masomo yao.Kwa kifupi,ipo kwa ajili ya ‘maskini’ waliodahiliwa Vyuoni.Je,yatenda haki katika kufanikisha kauli mbiu yake hiyo? Wanaopata mikopo ndio kweli waliotegemewa? Tatizo hasa liko wapi?

Ingawa mimi si mtaalamu wa Bajeti(hasa ya Serikali) lakini naamini kuwa Serikali zilizopita na iliyopo hazikuwa na wala haina uwezo(kulingana na Ilani zao) wa kulipia masomo ya Vyuo Vikuu kwa wadahiliwa wote.Kuna sababu nyingi lakini mojawapo ni kuwa si kila mwanafunzi ni asiye na uwezo.Wapo wahitajimikopo kweli na wale wa ‘nasisi-tupate’ hata kama wana uwezo wa aina gani.Ilimradi tu-kuleta vurugu.Hawa nao ni tatizo.

Matatizo yaliyopo sasa kwenye Mikopo yalianza punde tu Bodi ilipoanza kuchapa kazi.Ikumbukwe kuwa Chama cha Mapinduzi na Serikali yake kilikuwa kwenye maandalizi ya kutetea kiti chake cha uongozi wa nchi hii kupitia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 uliomweka madarakani Rais Jakaya Kikwete kwa Muhula wake wa kwanza,2005-2010.Ili kusafisha njia na kuteka nyoyo za wananchi wapenda elimu,Serikali ikatangaza kuzaliwa kwa ukombozi kwa wanafunzi wa elimu ya juu.Ikatangaza kuanzishwa na kuanza kazi kwa Bodi ya Mikopo.Kila mwenye nacho na asiye nacho asahau utajiri na umaskini wake na ajongee Serikalini kupata mikopo.Yeye alitakiwa kuja na kitambulisho kimoja tu muhimu:udahili.Udahili umetoka wapi lilikuwa si swali la msingi kwa Serikali ‘sikivu’.

Wale waliokuwa wakijisomesha kwa fedha zao wenyewe pia hawakusahauliwa.Nao walialikwa kwenye tafrija hiyo nono ya mikopo.Na zaidi,hata wanafunzi wa kidato cha sita waliomaliza Mwezi wa Machi mwaka 2005,walihamasishwa na kukaribishwa kujiunga na Vyuo Vikuu bila hata ya kulaza mwaka mmoja na miezi minne mitaani kama ilivyokuwa hapo mwanzo.Wakaunganisha moja kwa moja Vyuoni.Kipaza sauti cha Serikali kikaita huku na kule na kutangaza neema ya kupatikana faraja kwa ‘maskini’ wengi:mikopo.CCM,kwa sera yake hiyo ikakomba kura zaidi ya aslimia 80 katika Uchaguzi mkuu wa mwaka huo huku ikiacha moto sintofahamu kati ya Bodi na Wanafunzi wa Elimu ya Juu.Walijitokeza akina Julius Mtatiro(sasa Naibu Katibu Mkuu wa CUF-Bara) kuongoza migomo na maandamano pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam-Mlimani kulalamikia utendaji usioridhisha wa Bodi ya Mikopo.

Malalamiko yakaendelea,migomo ikakaendelea,Serikali na Bodi zikajitetea-kila mtu akasema na kufanya lake.Hakuna kiongozi yeyote wa Serikali aliyewahi kukiri kitovu cha tatizo.Ukweli ni kuwa siasa iliharibu kila kitu.Kura zikawala wanafunzi na Bodi.Kumbe wakati Serikali inatangaza faraja ilikuwa haijaangalia mifukoni mwake.Haikuwa na fedha za kuwalisha na kuwanywesha waalikwa wote.Baadaye,ikatangaza sasa ni daraja la kwanza na la pili tu litastahili mikopo.Lakini wa-ualimu na sayansi wangeruhusiwa hata kwa daraja la tatu.Pia madaraja mbalimbali ya mikopo yakawekwa.Vigezo vya kuwapata wa daraja husika vikaendelea kuwa tatizo.Ilikuwa too late! Vyuo Vikuu vikaongezeka kama Shule za Sekondari.Kwanini? Jibu ni rahisi:Serikali ilihitaji barua ya udahili tu bila ya kujali zinapotoka.Makosa makubwa!

Yaweza kusemwa kuwa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu imezidiwa nguvu na mikopo.Haina fungu la kutosheleza gharama za kila mwombaji.Sasa,Chuo Kikuu cha Dar es Salaam-Mlimani,Chuo Kikuu cha Ardhi na Chuo cha Ustawi wa Jamii wameanza mchakato kwa njia ya mgomo na maandamano(kuanzia tarehe 03/02/2011) wa kutaka kuongezewa fedha za kujikimu kutoka 5000 hadi 10000 kwa siku.Wanahoji kuwa ikiwa gharama za maisha zimepanda pamoja na mishahara,kwanini ‘boom’ lisipande? Wana malalamiko mengine zaidi ya hayo ambayo si sehemu ya makala hii.Huu utakuwa msumari wa moto mwingine kwa Bodi.Jamani huruma!

Serikali isingalipelekeshwa na joto la Uchaguzi wa 2005.labda isingalifanya ilivyofanya.Labda ingeanza na wafaulu vyema kwanza kama ilivyokuwa kabla ya Bodi,halafu wa Vyuo vya Umma,halafu vya binafsi.Hatua kwa hatua.Ikumbukwe kuwa kabla ya Bodi ya Mikopo,Serikali ilikuwa ikifanya jambo jema sana la kuwasomesha wanafunzi wa Vyuo Vikuu vya Umma waliofaulu kwa kiwango cha juu na waliokuwa hawana uwezo.Iliamininika na kufanyika kuwa wale waliokuwa na ufaulu wa wastani na wa chini walijisomesha wenyewe.Hivi ndivyo ilivyokuwa kabla ya mwaka 2005 katika Vyuo vya Umma na Binafsi.Lakini sasa wote wanapanga foleni ya Mikopo.Sina hakika kama wote wanastahili.Si wameitwa na Serikali kwanini wasije?

Serikali iangalie vyema suala hili na kulifanyia kazi.Yaweza kurudi nyuma halafu kusonga mbele ikitokea nyuma.Wanaostahili wapate wapate,wasiostahili waambiwe:hamstahili.Au,Bajeti ya Bodi iongezwe maradufu ili kila aliyealikwa kwenye tafrija ya mikopo anywe na ale.Hata kama Bodi itavunjwa kama ilivyopendekezwa na UVCCM,tatizo litabaki.Kwani ikishavunjwa,haiundwi nyingine? Serikali itimize ilichoahidi kwa kipaza sauti kikubwa mwaka 2005 au iwe tayari kupokea lawama badala ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu.
 
Back
Top Bottom