Kusema mtoto kulelewa na Bibi na Babu ataharibika ni Uongo kwa sababu tupo wengi ambao hatujaharibika

Robert Heriel Mtibeli

JF-Expert Member
Mar 24, 2018
21,340
51,900
KUSEMA MTOTO KULELEWA NA BIBI NA BABU ATAHARIBIKA NI UONGO KWA SABABU TUPO WENGI AMBAO HATUJAHARIBIKA.

Anàandika, Robert Heriel
Mtibeli.

Katika vitu najivunia na kumshukuru Mungu katika maisha yangu ni kulelewa na Bibi na Babu. Kwa kweli Mungu kwa hili namshukuru sana. Ulikuwa mpango mzuri ambao matunda yake ninayaona na nina kila sababu ya kushukuru.

Tangu nipo mdogo, nilikuwa nikisikia Watu wakisema mtoto akilelewa na Bibi na Babu anakuwa na sifa mbaya kama uvivu, kudeka na zaidi kuharibika. Nilikuwa nasikia hivyo na hata sasa wapo Watu wanaamini hivyo.

Lakini imani hiyo ni uongo na kasumba potofu kabisa.

Elewa kuwa Baba na Mama ndio watakuja kuwa Babu na Bibi. Ikiwa Baba na Mama walikuwa hawana maadili tafsiri yake hata wakizeeka watakuwa vivyo hivyo tu.

Kama Baba na mama walishindwa kuwalea watoto wao kwenye maadili watawezaje kulea wajukuu kwenye maadili?

Mtoto kuharibika inategemea mambo yafuatayo:

1. Aina ya wazazi na walezi wanaomlea mtoto.
2. Mazingira anayolelewa mtoto.
3. Asili ya mtoto mwenyewe. Silika na akili yake ya kuzaliwa.

Mtoto kuharibika wengi wanamaanisha yafuatayo:
1. Mtoto kutokuwa na maadili kama vile;
Kutoheshimu wazazi, walezi na wakubwa wake, kufanya uhalifu na matendo ya hovyo yaliyokinyume na maadili.

2. Kutokuwajibika kama mtoto.
Kukataa wajibu wake kama kusaidia kazi za nyumbani, kusoma, n.k.

Kusema watoto wakilelewa na Babu na bibi wataharibika wakati bibi na babu ni Baba na mama zako ni dalili ya Watu kushindwa kufikiri vizuri.

Labda kama Baba na mama yako hakukulea vizuri na Unawajua kabisa ni vichwa maji ndio maana unahofu kuwa hawana uwezo wa kumlea mtoto wako (mjukuu wao).

Kuna sababu nyingi zinazopelekea Mtoto kulelewa na Babu na bibi yake. Sababu hizo ni pamoja na hizi:

1. Uyatima.
2. Mzazi kuzaa kabla hajajipanga, mara nyingi inatokana na ukosefu wa maadili yaani kupata mimba katika michezo ya kihuni ya ujana.
3.. Kutengana kwa Wazazi na hii kusababisha usalama wa mtoto uwe zaidi kwa Babu na bibi yake.
4. Majukumu mengi ya wazazi ikiwemo kusoma au majukumu ya kikazi inapelekea mtoto kupelekwa kwa babu na bibi yake.
Na sababu zinginezo.

Kuna watoto tulijikuta kwenye bahati ya kulelewa na Babu na bibi ambao kwa kweli walikuwa na sifa ambazo wazazi wengi yaani baba na mama wengi Hawana. Sifa hizo ni kama ifuatavyo;

1. Imani na maadili
Kulelewa na Babu na bibi mwenye imani safi na maadili ni jambo la kujivunia.
Babu na bibi sio walevi. Babu na bibi wanapenda kusali, kuomba mungu na kusoma neno la mungu. Babu na bibi wenye kukufundisha neno la mungu na kumjua mungu. Kila asubuhi na jioni ni kusali na kusoma neno la mungu.

Ni wababa na wamama wangapi ambao sifa hii hawana? Bila shaka wapo kwa mamilioni.
Au ukiulizwa ni lini wewe na baba na mama yako mlikaa pamoja kusali na kuomba na kujifunza habari za Mungu.

Tangu nimezaliwa mpaka ninamaliza kidato cha nne sijawahi kusikia Matusi katika nyumba yetu. Matusi ya nguoni sijawahi kusikia mule ndani. Na tulifundishwa kutoto lugha chafu katika midomo yetu. Mara ya kwanza mimi kutukana ilikuwa nipo chuo mwaka wa pili.

Nimeshuhudia Baba na mama wengi wakitukanana matusi ya nguoni na kudhalilishana mbele ya watoto wao na mbele za majirani. Na hao ni baba na Mama. Je bado mtasema kulelewa na babu na bibi ni shida? Sio kweli shida ipo kwa mtu mwenyewe na tabia zake.

Babu na bibi walitufundisha kuheshimu wakubwa na wadogo na hilo tuliliona kwa mfano wao. Kwa sababu wao walituheshimu sisi wajukuu zao kaa vitendo. Na sio kutunyanyasa kisa ukubwa wao. Walitufundisha heshima inajengwa kwa matendo mema na sio umri wala cheo.

Ni wazazi (baba na mama) wangapi wanawakosea heshima watoto wao dhahiri shayiri alafu muda huohuo wanataka kuheshimiwa na hao watoto. Yaani mzazi ufanye upuuzi wako mbele ya mtoto alafu unataka mtoto akuheshimu kwa kisingizio cha kumzaa kwani alikutuma umzae.

Wazazi wangapi wanafanya zinaa za wazi mpaka kufumaniana mbele ya watoto wao. Wababa wangapi wanafanya ngono zembe mpaka kupelekea Wake zao kugombana mbele ya watoto wao alafu wanataka kuheshimiwa.

Elewa kuwa binadamu ni mnyama kama wanyama wengine. Kuzaa ni sifa ya mnyama. Kinachomfanya binadamu kuwa mtu (utu) ili aheshimiwe utu wake ni matendo yake mema na sio ubinadamu (unyama wake). Kumzaa mtoto hakumfanyi mtoto akuheshimu ikiwa matendo yako ni yakinyama(hujiheshimu).

Kwa bahati nzuri, Taikon pia nilifundishwa kutokuwa mnafiki. Babu na bibi yangu walinifundisha kutokuwa mnafiki. Kumheshimu mzazi asiyejiheshimu ni Unafiki wa kiwango cha juu kabisa na ndio kunazalisha jamii ya hovyo.

Ni sawa na jamii inayoheshimu Kiongozi kwa cheo chake badala ya matendo yake. Au kuheshimu mtu kwa sababu ya pesa zake. Huo ni Unafiki.

Kutokudhulumu haki za wengine na haki zako yaani kuwa mwaminifu. Kuwa mwaminifu ni pamoja na kumlipa mtu sawasawa na matendo yake. Kama ni mwema alipwe mema na kama ni Muovu alipwe mabaya. Lakini kama ataomba Msamaha kwa wakati kumpa nafasi ya pili na yatatu(kumsamehe). Hiyo ndio Haki.

Kuridhika na maisha uliyonayo na ukipatacho ili usiwe na Kijicho, wivu na husda. Ambapo itakuepusha na tamaa kwa kutokujilinganisha kutakakokufanya udharau wengine au ujione duni mbele ya wengine.

2. Babu na Bibi mwenye elimu na mwenye kupenda Elimu.
Kuishi na Babu na Bibi kama wangu ni bahati. Walikuwa na elimu ya kawaida, Darasa la nane ya mkoloni. Kingereza kwao hakikuwa tatizo. Nyumba ilikuwa na vitabu na mara zote tulisisitizwa tusome sio kwa mdomo pekee bali mpaka ilikuwepo ratiba ya kusoma bedtime stories.

Wazee wanaoamini katika Mungu na elimu.
Kama kuna vitu vingekufanya uonekane huna maadili basi ni kutofuata mafundisho ya dini pamoja na kupenda elimu. Mambo hayo makuu mawili ndio yalikuwa yanasisitizwa kwetu wajukuu.

Uganga na uchawi ulidharauliwa na kudharaulika pale nyumbani. Na kamwe isingekuwa ruhusa kuwa na urafiki wa Watu wanaoenda kinyume na maadili ya pale nyumbani. Babu na bibi wangekopa na kuuza chochote ili sisi tupate elimu. Walifanikiwa.

Wangapi wamelelewa na Baba na mama wasiothamini elimu? Wengi.
Wangapi wamelelewa na Baba ña Mama wachawi na Washirikina? Wengi.

Sipo hapa kumlaumu yeyote au kumuona yeyote hafai kama wao wanavyoona waliolelewa na bibi na babu kuwa wanamapungufu. Nipo hapa kuonyesha kuwa Kuharibika kwa mtoto hakusababishwi na malezi ya Babu na bibi isipokuwa sababu zake nilishazitaja huko juu.

Malezi ya Babu na Bibi yalitusisitiza;
1. Ni mwiko kuoa Oa hovyo.
Ni bora uchelewe kuoa lakini ukioa utulie na mmoja.

2. Ni mwiko kumpiga mke hata kofi moja na kumdhalilisha.

3. Ni mwiko kuiba cha mtu na kudhulumu haki za Watu.
4. Ni mwiko kwenda kwa waganga, wachawi na walozi na kuamini imani hizo.n ni bora mara milioni Ufe na kuzikwa kuliko kwenda huko. Au ni bora uabike na maisha ya ufukara kuliko kwenda kwa mganga.

5. Ni mwiko kulala na mke wa mtu
6. Ni mwiko kukataa mtoto lakini pia kumnyang'anya mwanamke mtoto.
7. Ni mwiko kufanya biashara yoyote inayodhuru afya ya binadamu au kiumbe yeyote hata kama imehalalishwa na ulimwengu.
8. Ni mwiko kuwa shoga.
9. Ni mwiko kuyaharakisha mambo mazuri kabla ya wakati wake.
10. Ni mwiko kuishi na mwanandoa mchawi, mshirikina na mlozi.
11. Ni mwiko kuishi na mwanamke msaliti.

Acha nipumzike sasa.

Robert Heriel
Taikon wa Fasihi
Kwa sasa Dar es salaam
 
KUSEMA MTOTO KULELEWA NA BIBI NA BABU ATAHARIBIKA NI UONGO KWA SABABU TUPO WENGI AMBAO HATUJAHARIBIKA.

Anàandika, Robert Heriel
Mtibeli.

Kwa sasa Dar es salaam
Uandishi wako wa kitu kizima/ guadiani wakati wewe bado hujafika hata miaka 50, ni ishara kwamba alilelewa na bibi na babu huishi kuendena na umri wako, huo pia ni kuharibika. Kisaikolojia au kitaalamu huo ugonjwa tunauita........ mental fixation
 
KUSEMA MTOTO KULELEWA NA BIBI NA BABU ATAHARIBIKA NI UONGO KWA SABABU TUPO WENGI AMBAO HATUJAHARIBIKA.

Anàandika, Robert Heriel
Mtibeli.

Katika vitu najivunia na kumshukuru Mungu katika maisha yangu ni kulelewa na Bibi na Babu. Kwa kweli Mungu kwa hili
Taikon wa Fasihi
Kwa sasa Dar es salaam

Kwenye haya, Obama mmoja wao.
 
Uandishi wako wa kitu kizima/ guadiani wakati wewe bado hujafika hata miaka 50, ni ishara kwamba alilelewa na bibi na babu huishi kuendena na umri wako, huo pia ni kuharibika. Kisaikolojia au kitaalamu huo ugonjwa tunauita........ mental fixation

😀😀😀
Wataalamu mtanipa majina mpaka kamusi ziishe.
 
Sio kila bibi analemaza mtoto ila asilimia kubwa hulea mtoto kimayai mtoto anakua wa hovyohovyo muhimu mzaz kama uko hai lea mtoto wako mwenyewe
 
Back
Top Bottom