KIVULI (The Catching Shadow) Simulizi fupi Part 1

nasrimgambo

JF-Expert Member
Jan 10, 2017
1,858
2,349
Akiwa kashikilia nyaraka za kibenki mikononi mwake, kwa taratibu Johari alielekea chumba maalum cha maongezi cha benki yao. Chumba ambacho kilitengwa maalum kwa ajili ya kufanya maongezi na wateja wa hadhi kubwa wa huduma za kibenki zilizotolewa na benki ya National Investment Bank, ama NIB, ambayo ndiyo Johari alikuwa akiifanyia kazi. Moja ya majukumu ya Johari hapo benki ilikuwa ni kuonana na kufanya mazungumzo na wateja wakubwa wakubwa wenye uwezo na hadhi kubwa wa benki hiyo.

Ndani ya chumba alichokuwa akielekea mlikuwamo na bwana Jama Bhanji, ambaye alikuwa mfanyabiashara maarufu na mtu tajiri sana na aliyekuwa miongoni mwa wateja wakubwa kabisa wa benki ya NIB. Hivyo Johari alikuwa anaelekea kwenye mazungumzo na kumhudumia mteja mkubwa wa benki. Ndani ya hicho chumba bwana Jama Bhanji alikuwa kashikilia kikombe cha kahawa akiwa anainywa taratibu, huku macho yake kayarushia kwenye runinga ya kisasa iliyokuwamo ndani ya chumba hicho na ambayo kwa wakati huo ilirusha taarifa ya habari na wakati huo kiyoyozi kilipulizia hewa ya ubaridi kwenye chumba. Mara tu Johari alipofungua mlango wa chumba hicho na kuingia bwana Bhanji alitoa macho yake toka kwenye runinga na kumtazama Johari aliyeingia ndani ya chumba hicho, huku akiwa kajaza tabasamu usoni, akionekana nadhifu kwa suti aliyovalia.

Kwa bashasha Johari aliongeza tabasamu la uso wake na kuelekea kukaa kwenye kochi lililotazamana na kochi alilokaa bwana Bhanji, kisha akamkaribisha na kumwambia jinsi benki yao ya NIB ilivyo na furaha kuendelea kumhudumia mtu wa muhimu katika uwekezaji nchini. Maongezi yao yalihusisha mapitio ya faida za gawiwo ambazo bwana Bhanji alizipata kutokana na kuwekeza kwenye makampuni na miradi mbalimbali ambayo benki ya NIB ilimshauri mfanyabiashara huyo awekeze. Kwenye kikao hicho bwana Bhanji alijawa na furaha sana kwa maana miradi yote liyoshauriwa awekeze na watu wa benki hiyo ilikuwa imemuingizia faida nyingi sana na hivyo akamuahidi Johari kuwa ataendelea kutumia huduma za benki yao ya NIB na kufuata shauri za benki hiyo juu ya masuala ya uwekezaji.

Kikao cha siku hiyo na bwana Bhanji kilienda vizuri sana hivi kwamba Johari alisifiwa na wafanyakazi wezie na viongozi wake kazini kwa kuweza kushughulika na wateja wakubwa wakubwa wa benki hiyo, wateja ambao walikuwa wa hadhi kubwa na kila benki iliwalilia na kufanya jitihada kuwapata.

Johari alijawa na furaha na kujiona mwenye bahati na akili nyingi kwa kuweza kufanya kazi na kushughulika na watu wa hadhi ya juu. Alijivunia sana moyoni.

Kwa hakika Johari alikuwa ni mwanamke mwenye bahati sana. Alikuwa msomi, mrembo, mnyenyekevu, aliyependwa na watu kila mahala,maofisini, majirani na koote alikokwenda alipendwa, alikuwa na uwezo mkubwa kwa maana kazi yake ya benki ilimlipa vizuri na kumpa heshima. Na pia Johari alikuwa keshaolewa, na alimpenda sana mume wake ambaye aliitwa Malcom Munyisi. Malcom alikuwa akifanya kazi katika wizara ya mambo ya nje, kazi ambayo ilimfanya asafiri sana kwenda nje ya nchi katika nchi za ulaya, arabuni, uchina na hata amerika, Johari alifurahia sana kazi hiyo ya Malcom.

Hakika Johari alionekana mwenye bahati sana kwa wakati huo. Ila!, kama inavyosemekana miongoni mwa waswahili ya kuwa hakuna kizuri kisicho kasoro, basi ndivyo vivyo hivyo ilivyokuwa kwa Johari Chande Munyisi.

Na kichwani mwake Johari aliwaza sana mambo yaliyomtia kasoro. Pamoja na furaha zake na bahati zake alizo kirimiwa na mwenyezi mungu, katu hayakutoka kichwani mwake mambo yaliyomtia kasoro na aliyawaza sana.

Mambo yenyewe yaliyomtia kasoro yalianza kama miaka kumi na nne kabla ya wakati huo. Enzi ambazo Johari alikuwa binti yatima, mwenye maisha magumu ila binti aliyekuwa kajawa akili hivi kwamba alipata nafasi kujiunga na chuo kikuu.

Kwa ugumu wa maisha aliokuwa nao Johari kipindi hicho alichokuwa akisoma, alijikuta akiingia kwenye mahusiano na kijana mtukutu aliyeitwa ‘Kutu’. Kutu alimpenda sana Johari na alimpa kila kitu. Na akawa akimshawishi Johari ajiunge na kundi la kiharifu la kivamizi lililoitwa ‘mapanya’. Johari katu hakukubali kujiunga na kundi hilo la kiharifu.

Basi ikafika siku moja ambayo Johari alitimuliwa chuo na kuambiwa kuwa hatofanya mitihani ya mwisho wa ‘semester’ hadi atakapolipia ada ya chuo. Kitendo hicho kilimuuma sana na kumtia hasira, hivyo akafanya maamuzi mazito ya kuamua kujiunga na kundi la kiharifu la ‘mapanya’, ikiwa kama njia yake ya kujinasua toka kwenye ukata.

Hivyo kwa msaada wa bwana ake, Kutu, Johari alifanikiwa kujiunga na kundi hilo la kiharifu. Na akiwa ndani ya kundi hilo, haraka sana Johari alipata ada ya kulipa chuo na pesa nyingi za kufanyia mambo mengine. Na akawa mshirika mkubwa wa waharifu wa kundi hilo, ambalo lilifanya uharifu katika maeneo mbalimbali kwa kupora, kukaba na kuibia watu na kusaidia usambazaji wa madawa haramu ya kulevya.

Johari aliona kila kitu kinaenda sawa kwa kushiriki kwake kwenye uharifu wa kundi la ‘mapanya’. Mpaka usiku mmoja mambo yalipoanza kwenda kombo baada ya kuvamia nyumba ya mfanyabiashara mmoja wa madini mwenye asili ya kieshia.

Katika usiku huo mnene wa manane, kundi la ‘mapanya’ wakiwa wamevalia vinyago usoni, na silaha za bunduki, masime na mapanga, walivamia nyumba ya mfanyabiashara wa madini na vito vya thamani. Walifika na gari yao aina ya ‘Noah’, wakiwa kundi kubwa sana na waliojipanga wakiwa na uelewa wa ramani nzima ya nyumba ya mfanyabiashara huyo na walikuwa wakifahamu kila mahala ambapo vitu vya thamani vilikuwa vimefichwa kwenye nyumba mfanyabiashara huyo, tena walikuwa na funguo zao wenyewe za milango ya kila kona ya nyumba hiyo.

Bila huruma kundi la mapanya walimshushia mfanyabiashara huyo kipigo kikali mbele ya familia yake na kisha kuanza kupekua kila walipofahamu pana vitu vya thamani na kuanza kuchukua vitu hivyo.

Johari akiwa miongoni mwa waharifu wa kundi hilo la ‘mapanya’, tena mtoto wa kike pekee kundini, alishiriki vyema katika tukio hilo la kikatili. Na alishuhudia jinsi waharifu wezie walivyo mdhalilisha yule mfanyabiashara na mkewe mbele ya mabinti zao wawili. Alishuhudia jinsi yule mfanyabiashara na mkewe na mabinti zao walivyolazimishwa kulala kifudifudi kwenye sebule ya nyumba yao na kuzuiwa kutoa kelele za aina zozote na kupewa vitisho vya kukatishwa maisha dakika yeyote watakayo neng’eneka kwa namna yeyote ile. Mfanyabiashara wa watu alikuwa hoi kagalagazwa sakafuni, damu zikimtoka mdomoni na puani, alikuwa kakosa kabisa la kufanya zaidi ya kulia shahada kwa sauti ya chini, “la ilaha illa llah, la ilaha illa llah”, huku akiomba waharifu wabebe kila walichoona kinawafaa na kuondoka. Johari aliyekuwa kavalia kinyago alimuangalia mzee huyo na kuona jinsi alivyolia kwa mungu wake na kuwalilia wao, na mara akamuona Kutu akitoa bunduki na kumnyooshea mzee huyo na familia yake ili awaue.
Hapo sasa Johari alijikuta akiingiwa na huruma kidogo na akamuomba Kutu amwache mzee huyo na asimuue. Kutu ambaye alikuwa ni muharifu sugu alimtazama Johari na kuangua kicheko cha kishetani shetani kisha akafyatua risasi toka kwenye bunduki hiyo na kumuua mzee huyo. Hivyo Johari akashuhudia mzee huyo wa watu jinsi ambavyo risasi ilitawanyisha kichwa chake na kumpoteza uhai ndani ya sekunde, huku mke wa mzee huyo na mabinti zao wakishuhudia na walishindwa kujizuia na wakatoa ukelele wa kilio. Mara Kutu akawafyatulia risasi wote, huyo mama wa kiarabu na mabinti zake wawili na kuwaua.

Johari sasa hata kinyago akakivua hakuamini alichoshuhudia kikitendwa na Kutu. Johari alijikuta akitetemeka kwa kuogopa alichokiona. Macho yalimtoka na akajikuta kamvamia Kutu na kumhoji kwa hasira umuhimu hasa wa kuwaua yule mama na mabinti zake pamoja na baba yao mfanyabiashara. Kutu akamtazama Johari kwa jicho la ukali sana na kisha akamnyooshea bunduki na kumuwekea kichwani. Johari alikuwa na hasira sana wakati huo, hata hakuogopa hiyo bunduki aliyowekewa kwenye paji la uso. Tena wakati huo Johari mwenyewe alikuwa na bunduki yake mkononi. Mara wale waharifu wengine ambao hawakushtushwa na kilichotendwa na Kutu walikuwa washamaliza kubeba vitu vya thamani vya ndani ya nyumba hiyo, hivyo wakaamrisha Kutu na Johari waache upumbavu wao na kuamuru kuwa wote waondoke haraka toka kwenye nyumba hiyo. Hivyo wote wakiwamo Johari na Kutu walitoka nje haraka na Kurukia kwenye ‘Noah’ yao na ‘kuondoka’ pamoja na pesa na vito vya thamani walivyoiba.

Usiku wa siku hiyo na wiki kadhaa zilizofuatia Johari alishindwa kulala kabisa kwa maana kila mara alipolala ilikuwa lazima aote juu ya ile familia aliyoshuhudiwa ikiuwawa na Kutu. Kwenye ndoto moja, aliota wanawake watatu waliovalia mavazi meupe na kujifunika hijabu wamelala kifudifudi kwenye sakafu huku damu zikiwavuja toka vichwani mwao na kuchafua nguo zao nyeupe, aliota akihangaika kuwapindua ili aone sura zao na kujua ni akina nani, ila ghafla waliamka wenyewe na kumtazama na aliona sura zao ni zile za yule mama na mabinti zake wawili waliouwawa na Kutu. Kila mara taswira za yule mama na mabinti zake zilimjia, mara nyingine aliota wakimlilia kwa uchungu mwingi, mida mingine alilala akahisi wapo nje ya dirisha la chumba chake wakimlilia. Kila mara Johari aliisikia sauti ya yule mzee aliyokuwa akiitoa muda mchache kabla hajauwawa, aliyasikia maneno ya shahada ya yule mzee, alisikia “la ilaha illa llah, la ilaha illa llah”, alisikia sauti hiyo ikianza kidogo na kisha kupanda na mara ikawa inageuka na kuwa kilio kikubwa cha mzee yule akimlilia.

Kama hiyo haikutosha, miezi michache baadae, Kutu alihusika katika ajali mbaya sana. Johari ambaye alikuwa na mahusiano na Kutu alipopokea taarifa alishtuka sana kujua kuwa Kutu alikufa kinyama kwa kuteketea kwa moto huku akijiona baada ya basi alilokuwa akisafiria kupata ajali na kusha kuwaka moto, tena katika hali isiyo eleweka abiria wote wa basi hilo waliwahi kutoka kwenye basi kasoro Kutu peke yake, ambaye alinasa kwenye basi na alichelewa kutoka hivyo akateketea kwa moto huku watu wakishindwa kumuokoa kutokana na ukali na ukubwa wa moto hivyo akafa akijiona. Johari alishtuka sana kwa taarifa ya kifo cha Kutu, alitetemeka na moja kwa moja alielewa huo ulikuwa ni mkosi.

Kama haikutosha waharifu wengine wawili wa kundi la mapanya walipata ajali mbaya sana na kufariki huku ndani ya wiki hiyohiyo waharifu watatu wa kundi la mapanya waliuwawa kinyama na maaskari walipokwenda kufanya uvamizi katika nyumba moja mitaa yenye ulinzi mkali. Waharifu wengine wakapotea hivyo Johari hakuwasikia wala kuwaona tena zaidi ya kuona matangazo kwenye vyombo vya habari wakitafutwa na ndugu zao.

Johari aliuelewa mkosi huo, kuwa ulitokana na Kutu kuua ile familia ya yule mfanyabiahara wa madini pamoja na familia yake. Ila kichwani mwake Johari alijiuliza sana mbona yeye hayamkuti ya kumkuta, na hivyo aliishi kwa hofu na wasiwasi. Ila hakupatwa na lolote japo ndoto aliendelea kuota ndoto za ajabu ajabu hadi usiku mmoja alipopata ndoto ya kutisha.
Usiku huo aliota akitembea na kukimbia kimbia katikati ya msitu mnene wa kutisha, akiwa na kiu, jasho likimtoka, nywele zikiwa zimemtimka, gauni lake likiwa chafu kwelikweli, huku akiwa kajawa na hofu, wasi na mashaka, na huku huku akisikia sauti za vilio na vicheko.

Mara akajikuta katokea nje ya msitu huo mnene ulioshonana na kuufikia uwanja mkuubwa. Katikati ya huo uwanja Johari aliona kuna watu wamekaa kwenye jamvi, wamevalia mavazi meupe. Walikuwa watu kama sita hivi.

Johari alipoangalia kwa makini aliona kuwa kumbe miongoni mwa wale watu walikuwamo yule mfanyabiashara aliyeuwawa, pamoja na mkewe na mabinti zao wawili, huku wakiwa pamoja na wanaume watatu wengine warefu sana na waliovalia mavai meupe.

Kwa hofu Johari alishindwa kuwakimbilia akabaki akiwaangalia hadi walipomuona na kunong’onezana jambo. Kisha moja kati ya wale wanaume watatu akainuka na kusimama na kumuelekea Johari huku uso kaukunja, alijongea hadi akamfikia, Johari alijikuta akiishiwa nguvu na kushindwa kusimama na kujikuta akipiga magoti mbele ya mwanamume yule.
Yule mtu alipomfikia Johari alisimama pembeni yake na kuanza kuongea kwa sauti ya kutisha, “Johari, Johari, binti mrembo uliyeingia kwenye majanga. Binti uliyekosa imani juu ya mungu wako akupaye riziki ukachukua maamuzi ya kujiunga na kundi la kiharifu ili kufanya maovu ulijiaminisha kuwa yangeweza kukuondolea ukata na kukuondoa kwenye lindi la umaskini”, aliongea mtu huyo huku mavazi yake meupe yakiwa yanang’aa hata yakaweza kuumiza macho ya Johari.

“Wezio wewe Johari, wezio wa kundi lenu la kiharifu, wamepata mikosi na kupoteza uhai wao na hakika nakwambia wao ni wa motoni. Hivi wewe muharifu unaweza kujua uchungu wa yule baba na mkewe kupoteza uhai na kuona mabinti zao wakiwa pamoja nao akhera?”, aliuliza huo mwanaume huku kaakimnyooshea Johari mkono awaone yule baba na mkewe na mabinti zake waliokuwa wamekalia kwenye jamvi pale kati uwanjani. Na kisha akaendelea kumwambia “Wewe Johari utabeba mzigo wa utasa, ujue uchungu wa kukosa mwana. Huo ndio utakuwa mtihani wako wa kukufunza kuwa na imani.Huo utakuwa ni mtihani ili kukurudisha katika mstari wa binadamu mtenda mema, nenda tenda kwa akili ikiwezekana tubu popote itapobidi na fanya toba, mungu atakusamehe na utakuwa miongoni mwa waja wema, ila ukiendekeza ubinafsi wako mikosi zaidi itakuwa yako”, alimaliza kuongea huyo mtu na kutoweka kisha wale watu wengine wote waaliokuwamo uwanjani wamekalia jamvi, akiwamo yule baba na familia yake wakatoweka pia. Baada ya kuamka toka kwenye ndoto hiyo, Johari hakuota tena ndoto mbaya mbaya. Ila kutokana na imani yake ndogo alipuuzia ndoto hiyo na hakutilia maanani nini hasa ilimaanisha kwenye maisha yake kuanzia wakati huo na akaendelea na maisha yake ya kawaida.
Baadaye Johari alihitimu elimu yake ya chuo kwa ufaulu wa alama za juu sana na hivyo akapata ufadhili wa kuendelea kusoma kwa ngazi ya ‘masters’ na kupata ajira, hivyo akabadilisha kabisa hali ya maisha yake na ya shangazi yake aliyeitwa Roda ambaye ndiye aliyemlea baada ya wazazi wake kufariki alipokuwa mdogo. Johari akaja kufahamiana na mtu aliyeitwa Malcom Munyisi na kupendana na kufunga ndoa. Kisha akajaliwa kupata nafasi muhimu ya kufanya kazi katika benki ya NIB, iliyokuwa moja ya mabenki makubwa nchini. Kwa ujumla maisha yake yalionekana yamekamilika, yaliyobarikiwa na mungu na ambayo kila mwanamke wa angeyatamani. Ila!, Johari aliishi katika ndoa na mumewe kwa miaka kumi pasina kupata mtoto, wala ujauzito wala dalili yeyote na ‘unukio’ wa ujauzito.

Johari alifahamu vizuri tatizo lake lilitokana na mkosi ‘aliojiokotea’ kutokana na maasi yake aliyotenda huko nyuma ila akiwa pamoja na mume wake walihangaika mahospitali kwa wataalam wa tiba za uzazi ambako tatizo lilionekana liko upande wake, tena tatizo lililowastaajabisha wataalamu kwa maana viungo na maumbile yake hayakuwa na kasoro yeyote ile iliyoeleweka kusababisha asishike ujauzito kwa sababu za kuelezeka.
Kadiri miaka ilivyokuwa ikienda Johari alizidi kuwa mwenye wasiwasi kuwa ipo siku eidha Malcom ama ndugu zake watazidiwa na hamu ya kuwa na mtoto kwenye familia na pengine hata kulazimisha ndoa yao kuvunjika, aliwaza sana juu ya jambo hilo na aliombea lisimtokee.
Kwa upande wa Malcom yeye alikuwa ni mtu mwenye mambo ya kizunguzungu, pengine ilitokana na maisha yake yaliyojawa na kwenda ulaya kila mara kila mwezi, hivyo yeye aliangalia tatizo la mkewe la kutopata ujauzito kama tu tatizo la kuendelea kulishughulikia na alizidi kuonesha mapenzi kwa mkewe. Ila sasa tatizo lilikuwa ni mama yake Malcom na mdogo wake wa kike aliyeitwa Snura, ambao wao walikuwa ni waongeaji na wenye mambo ya ukorofi sana.
Basi siku moja Malcom alimchukua Johari na kwenda nae kwao kwa mama yake kutembea. Siku hiyo walikuta kuna wajomba, baba wadogo, shangazi, mama wadogo wa Malcom wote wapo, kwa mshangao walioupata kwa kutotarajia uwepo wa ndugu wote hao, Malcom na Johari wakaambiwa kuwa hao ndugu wote walialikwa wajumuike siku hiyo kuzungumza mambo mbalimbali ya msingi ya kifamilia ikiwemo na kumshauri Malcom kwenye masuala muhimu ya kimaisha.

Wakiwa ndugu wote wamekaa chini ya mwembe nje ya nyumba ya kina Malcom, na Johari akiwa yuko hapo akijinyenyekeza mbele ya maongezi yao, mara mmoja wa wajomba wa Malcom akaanza kuongelea jinsi alivyojaaliwa kuwa na watoto watano wa kiume ambao aliwaita majembe na kuwasifu ni vidume hasa, na mara shangazi yake Malcom akadakia na kueleza jinsi ambavyo alijaaliwa kuzaa watoto saba na mwenyezi mungu na kushangaa hasa kwanini vijana wa kileo hawaelewi umuhimu wa kuwa na watoto mapema ilihali uhai ni mfupi.
Johari hakufurahia maongezi hayo aliona kabisa yanamsakama yeye na mumewe kwa kukosa mtoto.

Mara katikati ya mazungumzo hayo alifika binti mdogo, mzuri na aliyeonekana mpole na kuwaamkia kwa heshima na kujieleza kuwa kaja kumtembelea Snura, yani mdogo wa kike wa Malcom, mama Malcom kwa furaha sana alimkaribisha binti huyo na kumuelekeza aelekee huko nyuma ya nyumba kwenye jiko ambako Snura alikuwako akipika, na binti huyo akaelekea huko huku nyuma yake hapo chini ya mwembe ndugu zake Malcom walimtupia macho huku wakiwa na furaha na kuanza kumsifu.

Alianza baba ake mdogo Malcom kusifia, “kabinti kapoole, kazuuri, kanafaa kweli kuwa mke wa mtu ila laa!, vijana wetu wanaokoteza wanaacha mawari kama hawa mikoani”, akadakia mama ake mdogo Malcom, “tena kwa jinsi alivyo mpole binti huyu akiolewa wala hababaiki anazaa ‘fasta’, sio mijanamke mingine miaka dahali ‘no’ mtoto ‘no’ nini”, mama mdogo huyo aliongea kwa sauti. Maneno hayo yalikuwa wazi yakimlenga Johari. Mara akadakia mama ake Malcom, “Unajua enzi zetu mtu ukienda ukweni unafikia jikoni, unakaa huko unapika siku hiyo wakwe zako wanakula chakula ulichopika”, kisha akamuangalia Johari na wakaonana macho. Johari ikabidi ajibalaguze na kujiongelesha, “unajua mama mimi ni mpishi hodari tu sasa ngoja nika wakaangazie huko jikoni leo mle msosi niloupika mimi na mtaufurahia”, aliongea Johari na kujichekesha na kuinuka kwenda huko nyuma ya nyumba kulikokuwa na jiko, alijua lazima aondoke hapo ili kumuacha Malcom aongee na ndugu zake.

Hapo chini ya mwembe ndugu zake Malcom walimjiaa juu, wakimtamkia kuwa umri unaenda anahitaji mtoto, na kwamba kama mkewe hazai aachane nae aoe mwanamke mwengine. Malcom ambaye alijawa mambo ya kizungu, huku kavalia mawani yake, alikosa maneno ya kujibizana nao hao waswahili wa maneno akawekwa mtu kati wakimshambulia na kumuelimisha, aache ‘uboya’.

Wakati huo, huko jikoni alikokwenda kukaa Johari apike hapakuwa na amani, kwa maana Snura aligoma kupisha ‘mtu’ apike. Hivyo Johari akawa kakaa pembeni akimsaidia kupika kwa kumsogezea kopo la mkaa, mara amsogezee kopo la vitunguu na chumvi ama maji . Halafu mbaya zaidi muda wote Snura alikuwa anaongea na rafiki yake kana kwamba hawamuoni Johari, waliongea mambo yao ya kijijini ambayo Johari hakuweza kuchangia.
Ila kilichomuuma zaidi Johari ni pale alipokatiza kuku nje ya jiko hilo, kuku huyo mtetea alipita pamoja na vifaranga vyake. Basi Snura akaanza kumsifia huyo kuku, “Kuku si ndo huyu, kuku kuku kweli, kuku anatotoa vifaranga tunaona faida yake, mana raha ya kuku atotoe, sio kuku miaka nenda rudi kuku hatotoi, yani huyu kuku jinsi anavyototoa mfugaji anakupa raha ambayo hata binadamu mwengine hawakupi”, maneno hayo yalimuuma sana Johari pale alipoyaelewa maana yake, na alipoelewa kuwa kwa Snura, yule kuku ‘mdudu’ alikuwa na thamani kwa kutotoa kwake kuliko yeye Johari.

Ilimuuma hivi kwamba alilia njia nzima kwenye gari wakati yeye na Malcom wanarejea Dar es Salaam. Na Malcom alielewa kilichomliza mkewe, na safari hii alishindwa hata kumfariji, kwa maana hakuwa na pa kuanzia ndugu zake walifanya mambo ya kiroho mbaya bila kuficha safari hiyo.

Wiki nzima iliyofuatia Johari alikuwa mtu mwenye huzuni, na alijaribu kuficha hisia zake asionekane huzuni yake. Ila huzuni ilimtawala hivi kwamba bosi wake kazini alimuuliza baada ya kikao kimoja , kama ana tatizo lolote lililomtatiza, pia wafanyakazi wezie ‘walinotisi’ na kumuuliza kulikoni. Hadi mteja wa benki hiyo bwana Jama Bhanji ambaye alihudumiwa ‘private’ kwenye benki hiyo mara kwa mara na Johari alinotisi huzuni ya Johari na alimuhoji kulikoni alipoa sana.
Kwa kuwa Malcom alikuwa tayari keshaenda nje nchi kama kawaida yake -maana yeye Malcom alikuwa akifanya kazi wizarani kuhusu masuala ya mashirikiano ya kimataifa- Johari hakuwa hata na hamu ya kuwahi kwake, alibakia ofisini hadi jioni sana, katika ofisi yake hata kama alikuwa hana la kufanya alibaki kakodolea macho yake dirisha la kioo la ofisi yake iliyokuwa ghorofa ya nne ya jengo la benki hiyo ya NIB, hivyo akabaki hapo akiangalia jinsi giza lilivotua na majengo marefu ya mjini kati yakiwashwa taa ndipo aondoke kwenda kwake, huko mitaa ya Kijitonyama.
Aliwaza na kuwazua na hatimaye akafanya maamuzi kuwa, kwa kuwa kashahangaika sana kwenda mahospitali ya nchini na nje ya nchi basi suluhisho lililobaki ni kwenda kwa mganga wa kienyeji. Maamuzi yake yalifika huko kwasababu alifahamu fika tatizo lake lilitokana na kuhusika na kundi la kiharifu na kiuaji la mapanya. Na alifahamu fika kuwa wezie waliokuwa katika kundi hilo eidha walikufa kinyama ama kupotea, aidha Johari alielewa kuwa yeye pekee ndiye alliyesalia katika lile kundi la mapanya na kwamba kukosa kwake kupata ujauzito ni sehemu ya lana ya matendo yale maovu. Hivyo kwa imani kubwa aliamini mganga wa kishirikina ndiye angekuwa na msaada mkubwa sana kwake kwa tatizo hilo lake la muda mrefu.
Basi, siku moja wakati mumewe yuko nje nchi, bi. Johari alifunga safari ya mbali hadi katika kijiji kilichoitwa Sadani, kilichokuwa porini mbali kweli na kwenye kutisha. Huko alienda kumuona mganga. Mganga aliyekuwa mashuhuri, na watu toka kona zote za Tanzania nzima walienda kwa nguli huyo wa kishirikina kupata nusura ya matatizo yao.

Na Johari alipowasili tu kwa mganga huyo alikubali kuwa kweli alienda kwa mganga na sio matani. Kwanza palikuwa chini ya mti mnene na mkubwa wa mbuyu uliotisha na kufuka moshi, ulioning’inizwa vitambaa vyeusi na vyekundu na mahirizi makubwa makubwa yaliyotuna na kupumua. Johari aliingia kwa mganga huyo huku akitetemeka na kujifunga vizuri kanga zake alizovaa huku kaukumbatia mkoba wake alokwenda nao hapo. Mganga mwenyewe alikuwa pande la mtu, aliyejaa mahirizi na macheni ya mifupa ya wanyama na yale maganda ya konokono na viumbe wa baharini, usoni kajichora kwa maandishi meupe, huku akiwa kavalia kaniki na huku yuko kifua wazi.

Kabla hata Johari hajaeleza shida yake huyo mganga alimtolea macho makali sana Johari, macho makali kama ya chuki na kuanza kuongea, “Kweli leo umenijia wewe mwanamke mbaya. Hata waungwana unawapa mtihani, mizimu ya mababu zetu wa Sadani unawapa wakati mgumu kukupokea wakiwa wametulia, wanatetemeka kwa uovu ulioshuhudia na uovu wa watu uliojihusisha nao”, aliongea mganga huyo, na Johari alijikuta akiangausha chozi alielewa kuwa mganga kashafahamu maovu yote yanayomletea mkosi uliomfanya afike hapo mizimuni.
“Wewe mama unaitwa Johari Chande na mumeo anaitwa Malcom”, aliongea mganga na Johari kwa uchungu akaitikia, “tawile ‘baba’ angu ndio mimi, Johari”, na mganga akaendelea, “shida yako ni kupata mtoto, ila hupati kutokana na mkosi na nuksi ulizopata baada ya kuwa moja ya wafuasi wa kundi la kijambazi waliowahi kuua familia nzima na wewe ulikuwako siku ya tukio ukishuhudia”, aliendelea mganga huyo nguli, na Johari akaitikia, “tawile mganga”.
“Wezio woote, waliohusika wamepatwa na vifo vya kutisha na wengine kupotea, ila wewe walau umepewa utasa tu. Ila bado hujakubali unahaha kupata mtoto kama hivi kwa kututafuta waganga”, aliongea mganga huyo na kuangalia juu mawinguni, huku Johari akimtazama pia kwa hofu, kwa muda mganga huyo alibaki akiangalia mawinguni na ghafla akamgeukia Johari na kumkazia macho na kuendelea kuongea kuwa, waungwana wake, yani akimaanisha mizimu ya mababu zake wanampa hizo nguvu za kimiujiza wanayo dawa ya kutibu utasa wa Johari na kumsaidia kupata watoto, ila tatizo ni ugumu wa masharti, na mganga akamuuliza Johari kama yu tayari kufuata masharti magumu ya mganga. Na mganga akamsisitizia kuwa si jambo la kirahisi tu kukubali masharti hayo, na kwamba hatomtajia hayo masharti mpaka Johari ayakubali kwa moyo wote kabisakabisa kuwa vyovyote yatakavyokuwa hayo masharti kwa ugumu wake, yawe mepesi ama magumu kwelikweli shurti lazima ayatimize. Kuwa Johari ilimbidi akubali kutenda masharti kabla hajatajiwa na kuwa akishatajiwa basi hakuwa na jinsi ingine zaidi ya kuyatimiza. Johari alijikuta katika wakati mgumu sana, akawa kabaki kamtolea macho mganga. Hivi kweli akubali tu masharti kabla hajatajiwa, aliwaza, yakiwa magumu je itakuwa vipi ilihali ndio mganganga keshasema akimtajia sharti ayafanye hayo masharti.

Basi mganga akamuamuru Johari aondoke akatafakari ili kuamua kama yu radhi kutimiza masharti yeyote atakayopewa na mganga ama la. Na mganga akamwambia Johari kuwa akirejea tena aende na mbuzi wa kafara wa rangi yeyote ili walau kufidia vile vifo vya familia ile iliyouwawa na kundi la Mapanya, na pia aende na fedha zisizopungua milioni tano. Na akamsisitizia Johari kuwa iwe ni siri yake kati yake na mganga kuwa anatafutia hapo dawa ya kupata ujauzito. Na mganga akamsisitizia Johari tena kuwa akiwa anaondoka akumbuke kuwa, atakapoamua kurejea kwa mganga huyo, awe tayari kaamua kufuata masharti ya kiganga, na kumkumbusha kuwa siku akishamtajia masharti hayo basi Johari atakuwa kama aliyevulia nguo maji hivyo sharti lake ayaoge.

Baada ya kuondoka kwa mganga Johari alitafakari sana, kwanza alionywa asimwambie mtu hivyo hakuwa na mwengine wa kushiriki nae hayo mawazo yake, pili sasa alitafakari kuwa hadi wakati huo, hakuwa akiyajua hayo masharti ya mganga, ila mganga alimuambia kuwa siku akienda tena na akatajiwa hayo masharti ni lazima ayakubali bila ya kuyakataa, hivyo Johari aliwaza kuwa lazima afikie mkataa na kuamua hasaa kufuata masharti ya mganga.
Johari aliwaza sana itakuwa vipi kama masharti ni magumu mno, ila kichwani mwake zikamjia picha akicheza na watoto wake ambao pengine mganga angemsaidia kuwapata, pia aliona jinsi Malcom angefurahia uzao huo na mkewe, hivyo Johari akaamua kuwa ataenda tena kwa mganga na kukubali masharti atakayopewa yawe magumu kwa vyovyote vile, yeye atakuwa yu radhi na tayari kuyafanya.

Basi siku ikawadia na Johari akaelekea tena huko kijiji cha Sadani kwa mganga. Na siku hiyo alienda na mbuzi mweusi na pesa taslim ambazo mganga alimwambia aende nazo.
Mganga alimtakia Johari kuwa ni mwanmke jasiri sana kwa kurejea tena kukabiliana na masharti magumu ambayo angemtajia. Basi mganga akamchinja yule mbuzi na kutoa kama kafara kwa mizimu ya mababu zake.
Kisha akaanza kumpa masharti Johari na kumuambia kuwa, namna pekee ya Johari kupata watoto ni kuzaa na kichaa, yani mwehu, mwendawazimu wa akili, mwanamume aliyechizi kabisa muokota makopo.
Johari alishtuka sana. Alishtuka kwa maana hakutarajia sharti hilo hata kidogo. Ila mganga akamsisitizia kuwa hiyo ndio njia pekee ya kwake Johari kuweza kupata watoto vyenginevyo, asahau uzao. Na mganga kwa hasira alimkumbusha Johari kuwa masharti hayo ni lazima ayafuate, kwamba sasa ilikuwa ni lazima kwa Johari kumtafuta chizi muokota makopo na kulala nae ili azae na huyo chizi na kwamba Johari hakuwa na chaguzi tafauti na kulitekeleza sharti hilo ‘la aina yake’ alilompa.

Huo ulikuwa ni mtrihani mkubwa kwa Johari. Hakufikiria kabisa kuwa mganga angeweza kumpa sharti kama hilo. Njia nzima akiwa anarejea Dar machozi yalimtirirka akiwaza wapi atapata mtu chizi, na ‘atamkovisi’ vipi chizi hadi alale nae na aliwaza sana kuwa ikigundulika ‘mishe’ yake hiyo ya kutembea na wehu wa akili waokota makopo, ili apate watoto kama masharti ya mganga yatakavyo, uso wake ataufichia wapi, na alifikiria sana kwanini yeye Johari mfanyakazi wa benki kubwa kama NIB na mke wa Malcom Munyisi, mtu tajiri na alojaa uzungu uzungu, mfanyakazi wizarani, kwanini yeye ilimlazimu kulala na machizi ili kuzaa. Ila alikumbuka kuwa ni maovu yake yanyomtafuta na kumkimbiza, yakimfuatilia kama kivuli kila aendako.
........................

Malcom aliporejea toka nje ya nchi na kutembelea kijijini kwa mama yake, ndugu zake walimjia juu zaidi na safari hiyo wakamwambia kuwa wamemtafutia mchumba hivyo kazi yake ilikuwa kumuacha tu Johari na kumuoa huyo mwari mpya wa uhakika wa kuleta mtoto katika familia yao ya akina Munyisi.

Na Malcom hakuficha kitu kwa mkewe akamwambia alichoambiwa na ndugu zake, mama zake wadogo, mashangazi na wajomba, kuwa katafutiwa mchumba. Mbaya zaidi sasa kwa Johari huyo mchumba aliyetafutwa akaanza kumpigia simu Malcom. Hivi kwamba wakati mmoja Johari alipokea moja ya simu hizo na kumtukana sana huyo mwanamke.

Basi, siku moja Johari alikuwa kampitia mfanyakazi mwezie aliyeishi maeneo ya huko Mbezi Beach, ili waende mahala. Johari akiwa kakaa kwenye gari lake akimsubiri huyo mwezie atoke, mara akamuona mwanamume mmoja aliyevalia rafu sana, nywele zimetimka, yuko peku, akikatiza mbele ya gari lake akielekea mbele ya duka la rejareja lililokuwa mtaa huo. Moja kwa moja Johari alielewa huyo mtu alikuwa ni chizi mwendawazimu muokota makopo. Na akabaki akimtazama jinsi yule chizi alivyokuwa akifanya uchizi wake na mambo ya hovyo akielekea kwenye duka la mtaa.

Johari aliona jinsi, watu waliokuwa wamekaa wakianza kumcheka yule chizi. Na mara muziki ukasikika toka ndani ya duka. Na yule chizi akaanza kucheza huo mziki kwa furaha kabisa na wale wa dukani wakaendelea kumshangilia na kumcheka sana, walimgeuza kituko chao. Johari mwenyewe alijikuta akicheka vituko ambavyo yule chizi alikuwa akifanya kwa ‘kusakata’ muziki.

Mara rafiki yake aliyekuwa akimsubiri aliingia kwenye gari na kukaa kwenye kiti cha pembeni ya Johari huku akiomba radhi kwa kumchelewesha.
Na Johari aliondoa gari eneo hilo kuelekea kwenye safari yao waliyokuwa wakielekea. Walipokuwa njiani Johari alimuuliza rafiki yake juu ya yule chizi aliyekuwa akicheza mziki, na rafiki yake akamwambia kuwa yule mtu ni kichaa kabisa muokota makopo ambaye huzururazurura mitaani kwao na kuwa aliishi kwenye boma la nyumba ambayo haijakamilika jirani kabisa na pale palipokuwa na duka. Na kwamba hakuna mtu aliyefahamu yule chizi anaitwa nani, ama ndugu zake ni akina nani na wapi ama kwa namna gani aliupata uchizi, ila watu walipenda tu kumuona akicheza muziki na kumgeuza kituko chao na kumcheka.
Johari alisisimka mwili wake kusikia habari za yule chizi. Alianza kufikiria sana kichwani mwake kuwa huenda kapata aina ya chizi sahihi ambaye angefaa katika kutimiza masharti aliyopewa na mganga ili alale nae na kupata ujauzito. Aliwaza sana Johari na kujiapia kuwa lazima amchunguze yule chizi vizuri ili amjue tabia zake na kuelewa namna gani atamuingia na kumshawishi hadi afanye nae tendo la ndoa.

Na kweli, Johari alifanya uchunguzi wake na akapajua yule chizi alipokuwa akilala, aina ya taka alizokuwa akila na zuri zaidi alilofurahia ni kuwa chizi yule hakuwa na tabia ya kupiga watu. Johari alidhamiria kabisa kuwa lazima alale na chizi yule.
Usiku mmoja baada ya chunguzi zake kwisha, Johari alimfungia safari yule chizi. Ilikuwa ni usiku wa manane, Johari alifika kwenye boma la nyumba ambayo haikukamilika ambako yule chizi alilala. Kwa hofu Johari aliingia hadi ndani ya boma hilo na kumkukuta yule chizi kalala. Kwa muda kidogo Johari alimmulika kwa tochi na kumtazama na Kuona jinsi alivyokuwa mchafu na kulala kwenye udongo na nyasi za boma hilo tena harufu ya uchafu wa mwili wa chizi huyo ilitapakaa boma zima, hakika Johari alihisi kinyaa.

Mara yule chizi akaamka kutokana na mwanga wa tochi ambao Johari alimmulika nao. Na chizi yule alishtuka sana kwa maana hakuzoea ugeni bomani humo, hasa usiku manane. Johari mwenyewe alipoona yule chizi anaamka alishtuka hakujua yule chizi angewaruka kwa mtindo gani baada ya kumuona humo bomani.

Basi Johari ambaye mkononi alikuwa kabeba mfuko wenye machungwa, aliingiza mkono mmoja mfukoni na kutoa chungwa na kuanza kula kwa kumringishia chizi yule. Mara yule chizi akamvamia Johari na kumpokonya mfuko wa machungwa aliobeba na lile chungwa alilokuwa akimlingishia kisha, yule chizi akaenda kujikunyata na kula yale machungwa haraka haraka. Wakati huo Johari alikuwa kamtolea macho yule chizi. Kwanza hadi wakati huo Johari alijiona jasiri sana kufika katika boma hilo na kendelea kuwamo humo usiku huo wa manane pamoja na huyo chizi. Ila sasa Johari alifikia ukomo wake wa kufikiri hakuelewa ataanzaanza vipi kuhamsha hisia za chizi, hivi kwamba wafanye tendo la ndoa humo bomani na yeye mwenyewe alijiwazia sana ‘msambwanda’ na mtu chizi hufanania vipi, kichwani mwake, Johari alikuwa na mawazo kama alfu hivi, aliwaza kama akifumwa bomani humo na chizi usiku huo watu wangemchukiliaje.
Basi yule chizi baada ya kumaliza kula yale machungwa, ghafla akatulia na kumtizama Johari. Alimtazama kwa kutulia kabisa kama mtu mzima na timamu awezavyo kumuangalia mtu mwezie akiwa katulia, hadi Johari akastaajabu sana. Alistaajabu kwa jinsi ile yule chizi alivyotulia. Yule chizi alimungalia Johari machoni moja kwa moja na kutulia kabisa kama vile hakuwa na kawehuka kichwani.

Kumbe yule chizi alitulia vile kutokana na uzuri aliokuwa nao Johari. Alimuona Johari kuwa ni mrembo sana. Pamoja na uchizi wake alitambua kuwa hakuwahi kuona mwanamke mzuri kama Johari. Yule chizi alimuangalia Johari hadi machozi yakaanza kumlenga na kuona haya akageukia pembeni.

Johari hakutarajia kuwa mtu chizi anaweza kutulia namna hiyo, akabaki kaduwaa. Ila sasa aligundua kuwa, kama yule chizi aliweza kutulia namna ile basi kazi yake ilompeleka bomani mule ilikuwa nyepesi sana.

Mara moja Johari akavua na kuangusha nguo zake alizovalia mwilini na kumfuata yule chizi, ambaye nae alipomuona Johari yuko utupu alishtuka sana. Pamoja na uchizi wake alitambua kuwa si kawaida kwa mwanamke kuwa utupu. Johari akamsogelea.
Nia ajabu ilioje hadi wakati huo kile kinyaa alichokuwa akiona Johari kilimtoka kabisa na hakukisikia, hadi wakati huo alilenga tu kulala nae tu yule mwendawazimu.
Katika hali ngeni kabisa kwa yule chizi, alijikuta kasisimka sana na mara Johari alikuwa juu yake. Naam!, kilichotendeka hapo ilikuwa ni starehe ambayo chizi yule hakuwahi kuipata. Ilikuwa ndio mara ya kwanza kwa yule chizi kufanya tendo lile la aina yake na kwa Johari ilikuwa ndio mara yake ya kwanza kufanya vile na mataahira, yani ni kama walijiondoa ubikira kila mmoja wa aina yake, khatari!.

Johari akawa kafanikiwa lengo lake la kulala na chizi. Na usiku huo aliporejea kwake alikesha bafuni akioga akiwa haamini namna alivyofanikisha lile tendo na yule chizi. Hakuamini kama kweli msomi kama yeye alifanya alichokifanya, hakuamini kuwa yeye alikuwa ni jasiri wa kufanya kitu kama kile wakati aliona kuwa ni sharti zito sana pale alipotajiwa na mganga kuwa afanye vile, na ajabu aliona kuwa mbona ilikuwa na kauwepesi kidogo katika kutekeleza kuliko alivyokuwa akifikiria ugumu wake. Na alijishangaa na kujiuliza kinyaa chake cha kulala na chizi mchafu, anukae asieoga kilienda wapi muda wa tendo. Ni maswali mengi aliyojiuliza na akakosa majibu kichwani mwake.

Basi, maisha yaliendelea na wiki chache tu mbele Johari alianza kupata dalili ambazo hakika yeye aliamini ni ujauzito. Na hata alipokwenda kumuona daktari majibu yalionesha hivyo kuwa alikuwa ni mjamzito. Ilikuwa ni furaha sana kwa Malcom, kwa maana alishamkatia tamaa mkewe, Malcom hakuwa akitarajia kama mkewe angeweza kuleta kiumbe duniani, ilikuwa ni miujiza kwenye ndoa yao.

Ndugu zake Malcom walistaajabishwa sana na taarifa hizo, hawakuamini hata kidogo. Walijiuliza sana iwaje mgumba kapata ujauzito. Miezi tisa baadae, Johari alijifungua mtoto wa kiume, na kwa furaha Malcom akamuita mtoto huyo, Miujiza, kwa maana alikuwa ni muujiza kwa familia yake. Sasa mama yake Malcom, mdogo wake Malcom na ndugu wengine wakajikuta wana mapenzi ya dhati na Johari na kusahau viroja walivyokuwa wakimtendea. Sasa safari hiyo, Johari nae akawa anawaletea nyodo za ‘kimtindo’ za waziwazi katika kile kiitwacho kutesa kwa zamu, sasa Johari alionesha dhahiri kutopenda mtoto wake ashikweshikwe na ndugu wa mumewe na kujifanya mtoto wake anamlea kizungu sana na si kiswahiliswahili kama ndugu wa Malcom aliowachukulia kuwa hawana elimu walivyotaka kujishirikisha kwenye malezi ya mtoto.
Johari alikuwa ndiye mwenye furaha zaidi baina ya wote waliofurahia kuzaliwa kwa Miujiza. Yeye kama mama alifahamu shuruba na masharti aliyopitia na kutimiza ili kumpata mtoto wake. N akichwani mwake Johari akawa kafikia mkataa mwengine kuwa lazima atembee tena na yule mwanamume chizi ili apate mtoto mwengine wa pili.

Kwake yeye Johari kutembea na yule chizi ilikuwa ni jambo rahisi sana, kwa maana Malcom alikuwa ni mtu mwenye kusafiri safiri sana kwenda nje ya nchi, hivyo Johari aliweza kuwa na uhuru wa kuamua kuchelewa kurudi nyumbani na kufanya lolote huko mitaani, ikiwemo kulala na machizi, bila ya kuhofia kujulikana na mtu yeyote wala kumtia wasi Malcom.
Baada ya mwaka mmoja kupita, Johari, kwa awamu ya pili alirejea bomani kwa yule chizi. Na safari hiyo Johari alishangazwa kugundua kuwa yule chizi alimkumbuka vyema. Kwa maana safari hiyo ya pili, yule chizi alipomuona tu Johari machozi yalimdondoka toka kwenye macho yake hadi Johari mwenyewe akajikuta machozi yakimdondoka, hata bila ya kuelewa yule kichaa alilia nini kwa kumuona yeye Johari. Kumbe yule chizi alilia kwa mapenzi. Alimkumbuka vizuri Johari na urembo wake, na toka usiku ule wa mara ya kwanza wafanye tendo bomani yule chizi alimkumbuka na kumuwazia.

Kwa namna hiyo, hiyo safari hiyo ya mara ya pili ilikuwa rahisi zaidi kwa Johari kumuingia chizi huyo na kulala nae , kwasababu chizi mwenyewe alikuwa kaingia ‘laini’, yani haleti papara, ‘mzigo’ kauelewa na picha alijua kulicheza, na chizi yule alikuwa na hamu kweli ya kulala na Johari.

Hivyo Kama kawaida kwa maraya pili mambo yalitiki tena kwa Johari. N kweli akapata ujauzito na kuzidi kumfurahisha Malcom na ndugu zake.
Na miezi tisa baadae akajifungua, safari hiyo alijifungua watoto mapacha wawili, wasiofanana, wa kike na wa kiume, na kuzidisha furaha maradufu kwenye familia hiyo ya Malcom na ndugu zake ya akina Munyisi.

Johari alifurahia sana mafanikio ya mchezo wake mchafu. Na akafurahi pia kuwa hana haja ya kuuendeleza kwasababu watoto watatu walimtosha sana yeye na Malcom. Hivyo Johari alijiona ni shujaa aliyeweza pambana na lana ya uovu aliowahi kuufanya na kuushinda. Na nyodo zake kwa ndugu wa Malcom zikazidi maradufu hadi wakajutia madhira waliyomfanyia. Kwanza Johari watoto zake hakutaka mtu awaguse, aliwalea kama kitu gani sijui!, aliwalea kama ‘maprince’ na ‘princess’. Ndugu wote kimdomomdomo ‘kikawakatika’ wakabaki kuangalia malezi ya kiulaya ulaya.
...................................

Basi miaka ikaenda, na kichwani mwake Johari akamsahau kabisa yule chizi utadhani hakuwahi kutokea kwenye maisha yake kutembea na mtu chizi, yeye aliwaza furaha yake na Malcom na watoto wao watatu, Miujiza, Flora na Florian. Kwake watoto walikuwa ni wa Malcom sio mtu chizi. Hakuwa hata na haja ya kujua yule mtu aliishia vipi maisha yake, hakuwa na umuhimu wowote kwake. Kwake kilichokuwa umuhimu ilikuwa ni furaha ya familia yake na mumewe.

Na kweli hakuna kilichowabughudhi tena familia yao, kwa upande wao. Waliishi kwa raha mustarehe. Ila sasa mikasa ikawa upnde wa yule chizi.
Wakati Johari, alisahau juu ya yule chizi, kwa upande wa yule chizi haikuwa hivyo. Kwa upande wake alimuwaza Johari kwa mapenzi makubwa.
Pamoja na uchizi wake, aliikumbuka vizuri sura ya Johari, harufu yake, sauti na miguno yake na hasa alikumbuka uzuri wake. Na alimuwaza sana na ‘kummiss’ sana. Alipokuwa akilala alimuota Johari. Mara nyengine alihisi Johari kamsimamia pembeni na kuamka kwa furaha kumkumbatia na kumkaribisha bomani kumbe hakukuwa na Johari bali mawazo yake tu ya kichizi. Na alipogundua kuwa Johari hakuwa akija tena bomani yule chizi alikuwa akilia. Haikuwa kawaida, siku moja alikatiza mbele ya duka moja la mtaani na akasikia wimbo wa mapenzi ukipigwa redioni. Wimbo ambao ulikuwa na mashairi ya mtu aliyemkosa mpenzi wake, na uliokuwa na ‘tune’ ya kusikitisha ikionesha huzuni ya mapenzi, kwa hali ya kushangaza kabisa yule chizi alitoa ‘mchozi’ na kulia, na kushindwa kuendela na safari zake za kichizi na akakaa chini kulia kwa uchungu. Watu waliomuona walishangazwa sana na kumjaalia na kumuwazia iwaje mtu taahira ashikwe na hisia kali za wimbo wa mapenzi toka redioni hivi kwamba atoe machozi.
Hali ilikuwa ya namna hiyo kwa yule chizi. Na hivyo ndivyo maisha yake ya uchizi mitaani yalivyoendelea. Huku watu wakiwa hawamjui alikuwa ni nani hasa, hakuna liyejua jina lake wala asili yake, ilionekana mungu kampangia maisha yake yawe ya uchizi na uzururaji.


Itaendelea.............................................................
 
PW2.jpg
 
KIVULI
(sehemu ya pili na ya mwisho)



Basi miaka ikaenda na kichwani mwake Johari alimsahau kabisa yule chizi, utadhani haikuwahi kutokea kwenye maisha yake kutembea na mtu chizi, yeye aliwaza furaha yake na Malcom na watoto wao watatu, Miujiza, Flora na Florian. Kwake watoto walikuwa ni wa Malcom sio mtu chizi. Hakuwa hata na haja ya kujua yule mtu chizi aliishia vipi maisha yake, kwake yule mtu hakuwa na umuhimu wowote. Kwake kilichokuwa na umuhimu kilikuwa ni furaha ya familia yake na mumewe. Na kweli hakuna kilichowabughudhi tena familia yao. Waliishi kwa raha mustarehe.

Ila sasa mikasa ikawa upande wa yule chizi. Wakati Johari, alisahau juu ya yule chizi, kwa upande wa yule chizi haikuwa hivyo. Kwa upande wake alimuwaza Johari kwa mapenzi makubwa.

Pamoja na uchizi wake, alimkumbuka vizuri Johari, kwa sura na hasa alikumbuka uzuri wake. Na alimuwaza sana na ‘kummiss’ sana. Alipokuwa akilala alimuota, tena mara nyengine alihisi Johari kamsimamia pembeni na kuamka kwa furaha ili kumkumbatia na kumkaribisha bomani ilihali hakukuwa na Johari bali mawazo yake tu ya kichizi. Na alipogundua kuwa Johari hakuwa akija tena bomani yule chizi alikuwa akilia.

Katika hali isiyo ya kawaida, ilitokea siku moja, yule chizi kakatiza mitaa fulani na kusikia wimbo wa mapenzi ukipigwa toka kwenye redio ya duka la mtaani huko. Wimbo huo ulikuwa na mashairi ya mtu aliyemkosa mpenzi wake, na ulikuwa na ‘tyun’ ya kusikitisha iliyogusa moyo na kuwasilisha huzuni ya kimapenzi. Basi katika hali ya kushangaza kabisa yule chizi alijikuta akitoa machozi na kulia. Kwa uchungu na maumivu ya moyo alijikuta akikosa nguvu kabisa ya kuendelea na kuzurura kwake na akabaki mbele ya duka hilo kusikiliza wimbo wa hisia uliokuwa ukipigwa hadi akashindwa kuendela na safari zake za kichizi na akabaki chini kulia kwa uchungu hivi kwamba watu waliomuona walishangazwa sana na kumjaalilia, na kumuwazia iwaje mtu taahira kama yeye, ashikwe na hisia kali za wimbo wa kimapenzi toka redioni hadi afikie hatua ya kutoa machozi. Hivyo ndivyo maisha ya ya yule chizi yalivyoendelea mitaani.

Basi siku moja, jambo la ajabu lilitokea kwenye maisha ya yule chizi. Siku hiyo akiwa katika kuzurura kwake na kuokoteza alikutana na mwanamama mmoja na bintiye. Katika hali isiyokuwa kawaida yule mwanamama alishtuka sana kumuona yule mwanamume chizi kisha ghafla akaanza ku,piga ukelele mkali na kulia kwa nguvu sana na kushtua wapita njia wengine ikiwamo yule chizi, huku binti wa mama huyo akiwa haelewi mama yake kapatwa na kitu gani.

Yule mama katika kulia kwake alitoa kauli, akisema, “nimekwisha, nimekwisha, hakika leo hii nimekwisha”, alilia yule mama na mara akaanza kukimbia hovyo huku mwanae akimfukuzia na kumkamata. Ndipo yule mama akamgeukia yule chizi na kumnyooshea kidole na kusema kwa uchungu, “wewe Rashad wewe, ulipaswa utokomee wewe, usiwepo tena, kijana mbaya kabisa. Nyota yako niliyo ipotezea mbali naona sikuipoteza vya kutosha”, alilia huyo mwanamama, huku bintiye akiwa kamshikilia huku kachanganyikiwa na kutoamini kilichokuwa kinaendelea, na wapita njia wengine walikuwa wakiwamshangaa huyo mama na bintiye.

Wakati huo yule chizi, alikuwa katulia ghafla. Alitulia visivyo kawaida kwa mtu mwenye uchizi kama yeye, huku akiwa kawatolea macho yule mama na bintiye. Mara akaanza kutetemeka, na kupepesuka, hivi kwamba akawa akijaribu kusimama vizuri ili asianguke. Na mara, kwa hali ya kustaajabisha alihisi kama kitu kkikimtoka mwilini mwake ghafla. Huku yule mwanamama aliyekuwa na binti yake alianza kupiga mayowe zaidi kama mtu aliyeingiwa na ukichaa.

Kumbe ule uchizi ulikuwa umehamia kwa yule mama na kumhama yule chizi. Na watu wote waliokuwapo eneo hilo walibaki wakishangaa walichokuwa wakishuhudia kwa macho yao mawili, walistaajabu kuona jinsi yule mama alivyowehuka kwa ukichaa huku yule chizi akiwa katulia na aliyeonekana kama kupona ukichaa.

Basi yule mama aliyeingiwa na ukichaa alizidi kuchanganyikiwa na kisha akajinasua toka kwenye mikono ya binti yake na kuanza kutokomea mitaani huku bintiye akimlilia na kumfuatia na kumkamata. Na mara umati mkubwa wa watu ukawa umezunguka eneo hilo kujionea hekaheka.

Basi yule mwanamume ambaye uchizi ulimtoka, alikuwa kapigwa bumbuwazi, na kujishangaa na kujiuliza, amepatwa na nini na kuwauliza watu hapo ni wapi, na aliwauliza kwanini yeye alikuwa mchafu namna ile. Watu walimzunguka na kumjaalilia wakimshangaa kwa kuona jinsi mtu chizi alivyopona na kuwa na akili timamu katika namna ya kushangaza kabisa na huku wengine wakimuonea huruma yule mama aliyegeuka chizi.

Wingi wa watu walizunguka eneo lile na kushangaa ulifanya polisi kufika eneo lile, kufuatilia nini kilikuwa kinaendelea. Na kisha wakambeba yule mama aliyegeuka chizi na binti yake pamoja na yule jamaa aliyepona uchizi na kwenda nao kituoni.

Walipofika kituoni, binti wa yule mama alijitambulisha kuwa alikuwa anaitwa Zena, na kueleza kuwa mama yake alipatwa na ukichaa ghafla baada ya kumuona Rashad ambaye ni mpwa wa mama ke huyo, yani Rashad alikuwa ni mtoto wa kaka yake yule mama aliyegeuka chizi. Kumbe yule mwanamume chizi aliyepona, jina lake halisi lilikuwa ni Rashad. Na yule mama aliyeingiwa na uchizi kisha yeye akapona alikuwa ni shangazi yake na hivyo yule binti wa yule mama alikuwa ni binti wa amu yake ama shangazi. Askari walistaajabu hata zaidi kujua uchizi ulimuhama yule jamaa na kumhamia shangazi yake ulikuwa ni mkasa ulioshangaza kweli mapolisi hasa ikizingatiwa dola haimini katika kutokea mambo yanadhanika kuwa ya kichawichawi.

Basi huo ukawa mwisho wa Rashad kuishi maisha ya kusikitisha ya uchizi na kuzurura na kulala majalalani, maisha ambayo aliyaishi kwa zaidi ya miaka kumi.

Ukweli hasa wa maisha ya Rashad ulikuwa ni mkasa mrefu na wa aina yako nao ulikuwa kama ufuatao;

Rashad alikuwa kazaliwa kwa baba yake na mama yake waliokuwa wakimpenda sana. Yeye alikuwa ndiyo mtoto wao wa kwanza, tena wa kiume na mwenye akili sana toka utotoni hivi kwamba kila mtu alimpenda. Pia alikuwa na mdogo wake wa kike aliyeitwa Sarha. Yeye Rashad na Sarha waliishi kwa furaha sana na upendo wakiwa pamoja na wazazi wao, walipata kila kitu na walikuwa na akili hasa. Baba yao alikuwa ni mfanyabiashara mwenye mali kubwa. Na alikuwa na moyo wa kutoa sana kwa ndugu zake. Na alikuwa kaizoesha familia yake kuchangamana na ndugu zake kwa furaha na kusaidia ndugu zake kila walipohitaji msaada.

Maisha yao yaliendela hivyo mpaka siku moja ya bahati mbaya, baba yao alipokuwa akitoka safari ya mbali na kupata ajali ya gari na kupoteza maisha. Lilikuwa ni pigo kubwa, kwa familia na kwa ndugu wote. Na msiba ulikuwa mkubwa na ndugu wote walionesha kuguswa saana na msiba. Ila mambo yakaanza kubadilika baada ya msiba kuisha.

Kwanza kabisa kaka wa marehemu wakaanza kudai kuwa nyumba ambayo ndugu yao kaacha ilikuwa imejengwa kwenye kiwanja cha marehemu baba yao. Hivyo nyumba hiyo ni mali ya familia nzima na si ya mke na watoto wa marehemu kaka yao peke yao. Mzozo ukawa mkubwa hivi kwamba nyumba hiyo ikauzwa ili wagawane fedha eti kila mtu apate chake, na hilo lilifanyika haraka bila hata ya kujali hali ya familia iliyoachwa na marehemu.

Kama haikutosha mama yao akina Rashad akataka aende kuishi kwa ndugu zake, mara familia ya mumewe ikang’ang’ania kuwa kwa mila za kwao watoto wa marehemu hawapaswi kuishi ujombani bali kwa mashangazi zao. Hivyo kama mama huyo ataondoka basi aondoke yeye na aache watoto kwa shangazi na baba zao wakubwa na wadogo. Mama yao akina Rashad, bi Aisha alishindwa kukubali kuacha wanae peke yao kwa shangazi zao, kwa maana alifahamu aina ya maisha waliyoishi, maisha yaliyokosa muamko na kuishi kizamani na kienyeji sana na alijua watoto wake wasingeweza kuishi kwa furaha bila yeye.

Hicho kilikuwa ni kipindi cha majonzi sana kwa Aisha na wanawe, Rashad na Sarha. Yale maisha ya kula na kusaza, ‘family picnics’ na kupata kila walichokuwa wakikitaka yalitoweka. Sasa walikuwa wakiishi kwa watu, shangazi zao kina Rashad, huko mikoani tena kijijini, maisha magumu tena yale ya kilimo tu na hakkukuwa na kipato chochote cha maana na watu waliokuwa huko walikuwa na roho mbaya mtindo mmoja.

Ila maisha yaliendelea vivyo hivyo na Rashad na mdogo wake walijiunga na shule ya jirani na huko kijijini. Kwa kuwa walitoka shule za ‘international’, walijikuta wakiwa wanafahamu vitu vingi kuliko wanafunzi wezao wa kijijini, tena walikuwa wakiijua lugha ya kiingereza vizuri, na kuwafanya wafanye vizuri sana darasani.

Walimu wao waliwapenda sana na kuwatumia kama mifano ya kuelekezea wanafunzi wengine namna uvaaji wa sare ya shule, utulivu darasani na bidii katika masomo.

Hatimaye mama yao alianza kupata matumaini kuwa ipo siku ya inakuja ambayo watoto wake wangemtoa kimasomaso kwa kuondokana na umaskini na majanga yaliyowapata na kuishi tena yale maisha ya furaha waliyoishi awali.

Wakati huo, walikuwa wakiishi nyumba moja na shangazi yao akina Rashad aliyeitwa mama Zena. Shangazi huyo alikuwa na roho mbaya tena ya waziwazi. Hakupenda familia ya marehemu kaka yake hata kidogo. Aliwaona kuwa ni watu waliokuwa wakiringa sana enzi baba yao yu hai na chuki zake zilimfanya awazie sana jinsi familia ya kaka yake ‘itakavyosoma joto ya jiwe’.

Wakati huo Aisha, alikuwa mwema kwa wifi yake, kwa kumtabasamia na kumtabasamia na kumuongelesha maongezi ya kufurahisha, kumbe wifi yake huyo alikuwa akimchukia vibaya sana.

Sasa, Zena binti wa huyo mama Zena, alikuwa akisoma darasa moja na Rashad. Ila sasa yeye alikuwa ni ‘kilaza’, darasani hajiwezi kabisa, alikuwa mtu wakushika nafasi za mwisho darasani. Tofauti kabisa na Rashad ambaye alijulikana kama mwenye akili sana darasani. Kumbe kitu hicho kilimuuma sana mama Zena. Hakupenda kabisa kuona akina Rashad na mdogo wake wanakuwa watoto wa kutolewa mfano. Ilimuuma kuwa watototo zake yeye ndio walikuwa wakitolewa mifano ya kijinga kijinga.

Maisha yaliendelea, na Rashad aliendelea na elimu yake hadi akafika kidato cha nne na kufanya mtihani wa taifa. Matokeo yalipotoka, Rashad alifaulu kwa alama za juu sana na kupongezwa na kila mtu. Kijiji kizima kilimsifu kwa kufanya vizuri darasani. Zena kwa upande mwengine naye alikuwa kafaulu vizuri tu na alipongezwa na watu, na alijiunga kufurahia matokeo ya mtihani pamoja na Rashad.

Katika hali ya roho mbaya ya waziwazi, mama Zena hakufurahia jinsi mwanae alivyofurahia matokeo ya mtihani pamoja na Rashad. Yeye hakufurahia kuwa mwanae hakupata alama za juu kumzidi Rashad. Yeye hakupenda hilo hata kidogo alitaka binti yake ndio awe amefaulu zaidi na Rashad awe aliyefeli kabisakabisa. Sasa roho yake ilimuuma zaidi pale nafasi za shule zilipotoka na Rashad akawa kapangiwa kwenda kusoma shule moja iliyokuwa ikisifika sana kuwa ni shule ambayo wanafunzi wanaoenda ni wale waliofaulu vizuri kupitiliza.

Kwa jinsi alivyojawa na roho mbaya, mama Zena akaamua kuwa Rashad ni kijana wa kupotezwa kwa namna yeyote ile. Akaamua kuwa lazima amkomeshe kijana huyo na mama yake kwa ujumla kwa kumpoteza kabisa na kumfuta toka kwenye maisha na kufupisha kabisa safari yake ya kimasomo. Hivyo akaamua kumuendea kijana huyo kwa mganga wa kichawi, ili kumroga na kumtokomeza kabisa. Hakuna mtu aliyefikiria mama Zena alikuwa na uwezo wa kufikiria kufanya jambo baya kama hilo pamoja na kuwa walifahamu roho mbaya yake.

Basi usiku mmoja wa kuamkia asubuhi ambayo Rashad ilikuwa anapaswa aondoke kwenda shule aliyopangiwa, Bi Aisha alikaa na wanawe mkekani kwenye baraza ya nyumba waliyokuwa wakikaa ili kuzungumza nao na kuwaambia jinsi alivyokuwa na matumaini kuwa siku moja shida zao zote zitaisha na wataishi kwa furaha kama zamani. Aisha alizungumza na wanawe kwa kujivunia, maana alijua kuwa walikuwa ni watoto wenye akili nyingi na vile Rashad alikuwa akienda kusoma katika shule bora kabisa ya serikali nchini, Aisha aliuhisi kabisa kuwa mkono wa mungu ulikuwa unaanza kuinua tena familia yake. Kwenye maongezi hayo Rashad alimuambia mama yake ni jinsi gani anavyompenda na kumuahidi kuwa atafanya jitihada huko shuleni anakokwenda na kuja kuwa mtu mwenye mafanikio sana na kurudisha yale maisha ya furaha mama yake aliyokuwa akiombea yarudi tena.

Kumbe, maongezi ya usiku ule kati ya Aisha na watoto zake akiwamo Rashad, yalikuwa ndio maongezi ya mwisho kufanyika kati ya Aisha na mwanae Rashad. Kwa maana usiku wa manane wa usiku huo Rashad aliamka kwa mayowe na makelele, na kupiga kelele nyingi na kuwaamsha mama yake na mdogo wake na ndugu zao waliokuwa wakiishi nyumba moja na majirani wa hapo kijijini.

Aisha, Sarha na ndugu wengine walipokimbilia chumbani kwa Rashad walimkuta akiruka ruka juu ya kitanda kama mtu aliyewehuka. Walishtuka sana kwa maana haikuwa hali ya kawaida kwa mtu mzima aliyetimamu kufanya kitu kama kile usiku wa manane. Basi wakajaribu kumuongelesha na kumtuliza bila mafanikio, na wao wakazidi kuchanganyikiwa na kujiuliza nini kilikuwa kimempata Rashad. Majirani walipoingia ndani humo walishangaa sana kuona kilichokuwa kikiendelea. Na wote wakabaini kuwa Rashad alikuwa kapandwa na wendawazimu. Na ukweli ulikuwa ndio huo kuwa Rashad alikuwa kaingiwa na uwendawazimu.

Kumbe wakati huo Rashad anaingiwa na ukichaa, shangazi yake, mama Zena alikuwa yuko kwa mganga ‘akimkoroga akili’ ili awe mwendawazimu. Kwa mganga kwenyewe kulikuwa porini kwelikweli na kunakotisha na giza lililokuwepo kulifanya kutishe hata zaidi, ila shangazi huyo kutokana na jinsi alivyodhamiria hasa kumfanyia Rashad ubaya, alikuwa na ari yote iliyomuwezesha kuwepo huko mizimuni. Akiwa huko mama Zena alipewa ‘kizizi’ na mganga kisha mganga akamwambia kuwa anuie kumtokomeza Rashad na kisha atupe hicho kizizi kama ishara ya kumpoteza Rashad atokomee kusikojulikana. Basi mama Zena alishika kizizi cha mganga na kuanza kunuia. “ninataka, Rashad aingiwe na ukichaa, na ukichaa wake umpande hivi kwamba apotee na atokomee mbali, mbali sana na asirudi tena na asipatikane tena” baada ya kusema maneno hayo alikitupa kile kizizi mbali kwenye vichaka.

Naam! wakati mama Zena akinuia maovu yale, basi Rashad uchizi wake ukamkolea kichwani na akajinasua toka mikononi mwa watu waliomshikilia kumtuliza, na akatoka ndani mwao mbio na kuanza kukimbia hovyo kwenye njia za kijiji huku mama yake na watu wengine wakijaribu kumfukuzia bila mafanikio. Hadi jua lilipochomoza asubuhi, wanakijiji walikuwa hawajampata Rashad na hakuna aliyejua kakimbilia wapi. Basi hivyo ndivyo Rashad alipata ukichaa na kutokomea asipatikane tena na ndugu zake.

Lilikuwa ni pigo kubwa kwa mama yake. Alichanganyikiwa na kushindwa kuelewa ni janga la namna gani lilimpata mwanae. Hakuna polisi wala mtu aliyeweza kumpata Rashad miaka na miaka ikapita. Bi Aisha aliumia sana, kwa kilio na kufanya sala, akiamini kupitia dua zake mungu angemsaidia mwanae kuonekana tena, ila wala halikutokea. Alimuwaza sana mwanae na kumkumbuka jinsi alivyomlea, hasa hakusahau ule usiku wa mwisho kabla hajapatwa na ukichaa. Alikumbuka ule usiku jinsi Rashad alivyomwambia kuwa anampenda sana, alikumbuka jinsi Rashad alivyoahidi kufanya vizuri ili kumtoa kimasomaso siku moja na kuagana na dhiki zilizokuwa zimetamalaki kwenye maisha yao, aliwaza sana bi Aisha hadi akafika hatua ya kukufuru na kumuuluza mungu, “ina maana zile dua na sala za kumuombea afanye vizuri na kule kufaulu kwake, kote kulitokea ili tu kunipa tumaini kabla ya janga la kupatwa kwake na uchizi ili nije kulia zaidi kama niliavyo sasa”, aliuliza swali hilo bi Aisha huku akiangalia kwenye mbingu kwenye anga la bluu huku kapiga magoti, kavalia khanga zake kuukuu na mashavu yake yalikuwa yamejaa machozi.

Bila ya kujificha moyo wake, mama Zena alifurahia hasa yaliyompata Rashad. Mwanzoni kiunafiki nafiki alijitia akionea huruma, baadae akaanza kumsimanga wifi yake. “unajua hata misiba watu hulia halafu wananyamaza” alikuwa akitoa kauli za hivyo, “na mtu kama haonekani mnalia kisha mnanyama na kuendelea na maisha. ila sio watu wa nyumba hii toka huyo Rashad apotee mnatujazia vilio na simanzi. Imekuwa kama mnatuchuchuria sasa, mana watu mmekuwa tena ninyi ni kujiliza mtindo mmmoja, utafikiri nyie ndo wa kwanza kupata matatizo duniani wakati wapo watu wana matatizo, hayo yenu hayaingizi mguu ”, aliongea hiyo kauli mama Zena huku bi. Aisha, Sarha na ndugu wengine wakimsikia. Kauli hiyo ilizua utata sana kwenye familia hivi kwamba Sarha alipigana na shangazi yake na kusababisha ugomvi mkubwa zaidi kuwahi kutokea hapo kijijini. Hayo ndiyo yakabaki kuwa maisha yao baada ya Rashad kuwa chizi na kutokomea kusikojulikana.

Ila sasa, kumbe kule kwa mganga, mama Zena alipewa sharti kuwa, isitokee hata siku moja kukutana na Rashad, kwa maana kuwa siku ambayo Rashad atakutana tena ana kwa ana na mama Zena basi uchizi utahama toka kwa kwake na kumuhamia mama Zena.


Naam baada ya usiku ule miaka mingi ilipita. Na hakuna aliyekuwa na tumaini la kumuona tena Rashad, hata mama yake mwenyewe alikuwa kakata tamaa kumuona tena. Na Mama Zena alijiona kuwa kafanikiwa mpango wake wa kiovu na kamwe hakufikiri kuwa uovu wake ulikuwa una mwisho na alisahau ule usemi wa ‘milima haikutani, binadamu hukutana’.

Basi ikatokea siku moja Mama Zena na binti yake walikuwa kwenye matembezi mjini. Na kwa bahati mbaya sana, wakakutana na Rashad na hapo ndipo uchizi ukamtoka Rashad na kuhamia kwa mama Zena, na mama huyo akageuka kuwa kichaa kabisa na huku Rashad akipona na kurudi kwenye akili zake timamu kabisa.



Basi huo ndio ulikuwa mkasa wa maisha ya Rashad jinsi alivyopata uchizi na kisha akapona kurudia akili zake timamu. Na hatimaye bi Aisha na Sarha walimpata tena Rashad. Kwao ilikuwa ni zaidi ya muujiza. Kwa maana walikuwa washakata tamaa ya kumuona tena. Na waliumia sna kugundua kuwa uchizi wa Rashad ulisababishwa na mama Zena ambaye sasa uchizi ulimuingia mwenyewe. Hatimaye bi. Aisha na Sarha waliona kabisa kuwa mungu kajibu dua zao.

Mambo mengi yalikuwa yamebadilika toka Rashad apotee, Sarha alikuwa tayari kashamaliza elimu yake na alikuwa tayari kashakuwa daktari mkubwa. Hivyo maisha ya Sarha na bi Aisha yalikuwa mazuri kwa wakati huo sio ya kimaskini tena na walikuwa washahama kijijini siku nyingi na waliishi Dar es Salaam. Tena Sarha alikuwa tayari kashaolewa. Kwa kifupi maisha ya mama na dadake Rashad yalikuwa yamerejea kwenye ile hali nzuri ambayo walikuwa wakiiombea hapo zamani, na kurudi kwa Rashad kwenye maisha yao kuliongeza furaha kwao hata zaidi.

Mambo mengi sana ya kimaisha yalikuwa wamempita Rashad kutokana na unyama aliotendewa na shangazi huko miaka ya nyuma. Na kamwe hakukuwa na njia ya kufidia hasara yote aliyoipata kwa kushindwa kuendelea na ndoto zake za kimaisha na hasa kumalizia elimu yake. Hivyo alikuwa na kazi ya kujifunza mambo mengi ili aje kuweza kuishi maisha yake kama watu wengine wenye maisha ya kawaida. Ila pia alimshukuru mungu kuwa walau alikuwa mwenye bahati vya kutosha hata akabahatika kurejea kwenye akili zake timamu.



Rashad alitokea kuunda urafiki mkubwa na wa karibu sana na shemeji yake, mume wa Sarha. Kwa haraka sana walijikuta wameshibana. Shemeji yake huyo aliitwa Imran, na alimfundisha Rashad vitu vingi sana kwa haraka, ikiwamo kuendesha gari, kumtembeza mitaa mbalimbali ya mji na kumkutanisha na watu wengi aliofahamiana nao na ndiye aliyemtafutia mwalimu wa kumsaidia kusoma tena, ili siku moja Rashad aendelee na elimu yake aliyokuwa kakatizwa. Walikuwa ni zaidi ya mashemeji wakawa kama mtu na kaka yake ama mtu na rafiki yake wa karibu.

Rashad mwenyewe tangu apone uchizi wake alikuwa keshabadilika sana, hata haikuwa rahisi kwa mtu asiyemfahamu kujua kuwa yeye alikuwa ni mwanaume aliyewahi kuwa chizi, kichaa na taahira kabisa. Kwanza alikuwa yuko nadhifu sana, aliyejipenda, msafi na mtanashati. Muda wote alivalia vizuri na kunukia marashi. Hayo yote, ukiongezea na urefu wake na mwili wake ulioanza kujijenga vizuri ulifanya wanawake wengi kuanza kuvutiwa naye. Ila mwenyewe alikuwa yuko ‘serious’ sana na maisha yake, alikuwa yuko bize na kusoma kwake na mambo yake mengine hivi kwamba hakuwa akijiweka karibu na mwanamke yeyote yule.

Kumbe kwake yeye Rashad sio kwamba alikuwa hawatamani ama hawaoni wanawake waliokuwa ‘wakimshobokea’, aliwaona sana, ila tatizo lilikuwa ni moyo wake na akili yake. Yani katika hali ya kushangaza sana. Rashad alikuwa akimkumbuka sana Johari. Sura ya Johari ilikuwa bado haijamtoka kichwani mwake.

Katika hali isiyokuwa ya kawaida, hakuona mwanamke yeyote ambaye alifikia uzuri wa Johari. Kichwani mwake alimuwaza, na alipolala alimuota. Aliposikia nyimbo za mahaba redioni, kichwani mwake ilimjia sura ya Johari. Rashad katu, hakuona wanawake wenye sifa ya uzuri na kuvutia kiasi cha kumshinda Johari. Na moyo wake ulisononeka sana kwa maana hakujua wapi angekutana naye tena.

Basi bwana, jioni moja, Rashad, na Imran walikuwa wamemaliza kufanya mazoezi ya kucheza mpira wa kikapu na walikuwa wamekaa pembezoni mwa uwanja wa michezo wakiangalia wachezaji wengine wakiendelea na mazoezi yao. Ndipo mara Imran akamuona mwanamke aliyeitwa Sandra akikatiza kwa mbali kidogo nje ya uwanja huo wa mazoezi, huyo Sandra alikuwa ni jirani yao.

Imran akamuonesha Rashad amuone Sandra na kumsifia huyo mwanamke kuwa ni mzuri sana, na akamkumbushia Rashad kuwa Sandra alikuwa akimkubali sana. Kwamba kila mara Sandra alipomuona Rashad mtaani basi alikuwa akimchangamkia sana na kuleta mazungumzo mengi. Imran akamwambia Rashad kuwa siku atakayo mtaka Sandra basi mwanamke huyo ‘hatochomoa’ atakubali moja kwa moja.

Rashad alicheka maongezi ya Imran na kumwambia Imran kuwa kuna mwanamke anayempenda sana, na si Sandra, tena mzuri kumzidi Sandra hata kwa mara alfu. Mwanamke aliyevutia kwa kila kitu na mwanamke ambaye yeye Rashad aliwahi kuwa kwenye mahusiano nae kipindi anaumwa ugonjwa wa akili.

Mwanzoni Imran alichukulia Rashad anamletea masihara, kwa maana haikuingia akilini hata kidogo, kuwa Rashad aliyekuwa akiugua ukichaa aliweza kuwa na mahusiano wa kimapenzi na mwanamke yeyote yule. Haikuingia akilini kuwa kuna mwanamke aliyeweza kuwa na mahusiano na mtu chizi.

Lakini Rashad akaendelea kumsimulia Imran kuwa kipindi yuko chizi na kuishi mabomani, mitaani na majalalani. Kulikuwa na mwanamke ambaye alikuwa akimfuata usiku kwa lengo la ‘kulala’ nae. Na kwamba yeye Rashad kichwani mwake sura ya yule mwanamke bado ilibakia. Na kwamba kila usiku alimuota yule mwanamke na kwamba hakuna mwanamke yeyote atakayeweza kumfanya amsahau yule mwanamke.

Imran akazidi kuona maajabu, hakuamini kabisa kuwa Rashad aliamini kwamba aliwahi kuwa na mahusiano na mwanamke kipindi yuko chizi. Imran aliona pengine Rashad uchizi wake haujapona vizuri kwa kuongea mambo kama hayo. Ila Rashad mwenyewe alijiamini hisia zake kuwa ni kweli aliwahi kuwa na mahusiano kipindi yuko chizi na kwamba pamoja na uchizi wake aliokuwa nao kumbukumbu zake zilikuwa sahihi kabisa bila wasi.

Jambo hilo lilimshangaza sana Imran, na akajikuta akimwambia Sarha, mke eake. Na kumwambia kuwa pengine Rashad bado hajapona vizuri uwendazimu kwa kuongea mambo aliyokuwa kaanza kuongea.


................



Kwa upande wa Johari maisha yalizidi ‘kunoga’. Alifurahia jinsi Malcom alivyowafurahia watoto watatu aliompatia. Alijiona kila kitu kimekamilika. Kamwe hakudhania kuwa ipo siku yule chizi aliezaa nae watoto wake watatu atarejea kwenye maisha yake, tena akiwa si chizi tena bali mwanaume mwenye akili zake timamu.

Basi kama wasemavyo waswahili kuwa ‘milima haikutani, binadamu hukutana’, siku ya siku ikafika ambayo Rashad alikutana na Johari. Siku ambayo kibao kilipoanza kumgeukia johari.

Siku hiyo, Rashad alikuwa kaingia kwenye ‘super market’ kununua kinywaji fulani hivi alichoagizwa na Sarha. Akiwa yumo dukani, kwenye kabati za vinywaji mara kwa mbali alimuona mwanamke aliyependeza, aliyekuwa kasimama pembeni ya ‘keshia’ wa ‘supermarket’ na aliyeonekana kama vile kuna mtu anamsubiri, na wanamke huyo alikuwa anaangalia saa yake ya mkononi mara kwa mara. Alikuwa kavaa gauni refu la rangi nyekundu, na nywele ndefu zilizovutia. Kwa haraka Rashad alimfikiria kuwa yule mwanamke ni mrembo sana na akajikuta akimuangalia vizuri.

Ndipo mara akagundua kuwa yule mwanamke hakuwa mtu mwenye sura ngeni kwake. Na akamtazama vizuri sana na moja kwa moja akili yake ikatambua kuwa yule alikuwa ni yule mwanamke ambaye alikuwa akimjia kwenye boma lake alilokuwa akilala kipindi yuko chizi, alimuangalia vizuri na kukubaliana na akili yake kwa asilimia mia kuwa yule mwanamke ni yuleyule ambaye alikuwa akimjia usiku wa manane kipindi yuko chizi na kukutana nae kimwili bomani. Yani yule mwanamke alikuwa ni Johari.

Rashad hakuamini macho yake kuwa hatimaye kakutana na yule mwanamke. Moyoni mwake alijikuta akihisi hisia ya ajabu ya furaha iliyochanganyika na huzuni, pengine ya kutokana na kuwa hatimaye kamuona mwanamke aliyekuwa akimuota kwenye njozi zake. Mara hisia kali zilikita kwenye moyo wake na mara chozi lilidondoka toka kwenye macho yake na kulowesha mashavu yake. Kwa muda alibaki kasimama akimuangalia.

Mara akaona mwanamume mmoja aliyekuwa ndani ya duka akimuendea yule mwanamke pale kwa keshia, akiwa kabeba mfuko wenye bidhaa, kisha akalipia zile bidhaa na akamshika yule mwanamke mkono na wakatoka nje ya supermarket. Kwa haraka sana Rashad alijikuta akitoka haraka nje ya supermarket hiyo hadi nje ili tu kuwawahi. Alipofika nje aliwaona jinsi walivyopanda kwenye gari lao na kuondoka eneo lile la supermarket. Rashad alibaki akisononeka moyoni mwake na kujiuliza wapi atakutana tena na yule mwanamke. Ila pia alielewa akilini mwake kuwa yule mwanamume aliyeongozana nae lazima atakuwa ni mume wake.

Kitendo cha kumuona tena Johari kilimzidishia mawazo Rashad, sasa kila alipokaa mawazo yake yalikuwa nikumuwazia Johari. Kwanza ieleweke hadi wakati huo, Rashad hakuwa akimfahamu Johari kwa jina zaidi ya kumjua sura tu na kumfahamu kama mwanamke aliyewahi ‘kulala’ nae kipindi yuko chizi.

Baada ya kilichojiri pale ‘supermarket’, maisha ya Rashad yakawa ndio ya kumuwaza tu Johari, hata watu wengine walianza ‘kunotisi’ jinsi ambavyo Rashad alivyozidi kuwa mtu mwenye mawazo na aliyezidi kuwa mkimya sana. Hali ambayo ilitia watu wa karibu yake hofu kuwa huenda yale matatizo yake ya akili ndiyo yanayomtia ukimya huo, hivyo wote wakawa na wasiwasi na kutaka hali hiyo ikome.

Basi Imran na Sarha wakawa ndio watu wa mwanzo kumhoji Rashad kulikoni hata amekuwa akipoa sana na kuonekana mwenye mawazo mengi. Ndipo Rashad akawasimulia kuwa alikuwa kakutana na yule mwanamke mzuri, aliyewahi kuwa na mahusiano naye kipindi yuko chizi, mwanamke mzuri kuliko wote aliokuwa akiwafahamu. Na aliwaambia jinsi moyo wake ulivyoumia na kusikitika sana kwasababu alishindwa kuongea naye pale alipomuona supermarket na mbaya zaidi alimuona yule mwanamke akiongozana na mwanaume mwengine, na ilionekana kuwa lazima yule mwanaume atakuwa ni mumewe.

Hayo masimulizi ya bwana Rashad yalikuwa mazito kwa Sarha na mume wake bwana Imran. Yalikuwa mazito sana. Kwanza walifahamu fika kuwa ndugu yao ‘alikuwaga chizi’ wa zaidi ya miaka kumi, tena chizi mchafu muokota makopo, iwaje ikatokea eti alitembea na mwanamke mwenye akili timamu, suala hilo halikumkinika kabisa akilini mwao. Ila pia walishangazwa na ‘userious’ wa Rashad juu ya kile alichowasimulia. Walimuona akiongea kwa kujiamini.

Sarha alishindwa kuvumilia na kumwambia kile alichokuwa akifikiria, “sikia Rashad kakaangu, hebu achana na hizi habari zako za kuwa kuna mwanamke ulikuwa na mahusiano nae kipindi uko mwendawazimu. Tafadhali achana nazo hizo habari. Haiyumkiniki hata kidogo kuwa kuna mwanamke mwenye akili timamu ambaye angeweza kuwa na wewe wakati akili zako hazikuwa sawa.”, aliongea Sarha na kumsisitizia Rashad kuwa haina haja ya kumuwaza huyo mwanamke muda wote na kama ana shida sana ya mapenzi atafute mwanamke mwengine, “kaka yangu kama unajiona una hamu sana ya mapenzi tafuta mwanamke mwengine uoe, hizo habari zako za mwanamke anayekujia ndotoni, sijui!, mwanamke ukilala unamuota achana nazo, zinatupa shida kuamini kiwango cha kupona kwako tatizo lako la akili, unatutia wasiwasi kuwa pengine bado kichwani sio mzima”, aliongea Sarha maneno hayo kwa msimamo huku Imran akisapoti alichoongea mkewe.

Hali yao ya kutomuamini ilimtia hasira Rashad na kuwatamkia kuwa haina haja ya wao kumuamini kile ajuacho kuhusu yeye na maisha yake kipindi yuko chizi ama mahusiano yake na huyo mwanamke aliyekuwa akimpenda. Na kwa hasira akawaahidi kuwa hatozungumzia tena suala la mwanamke ampendaye mbele yao kwa maana alihisi kuwa wanamvunjia heshima kwa kumuona bado kichaa baada ya kuwaeleza kuhusu hisia zake. Basi Rashad akabaki hivyo akijiamini yeye nafsi yake kuwa ipo siku atakutana na yule mwanamke ampendaye na atamueleza jinsi anavyompenda.

Pamoja na nia yake ya kutaka kuonana tena na Johari, Rashad hakuwa na pa kuanzia kumtafuta. Hakujua lolote juu ya Johari, hakupajua kazini kwake wala hakupajua alipokuwa akiishi.

Kwa bahati nzuri sana, ikatokea siku moja, Rashad anaangalia taarifa ya habari. Akiwa hana umakini sana na kile kilichokuwa kikiendelea kuoneshwa luningani, ambacho kilikuwa ni habari za uchumi, mara ghafla akaona sura ya Johari kwenye luninga. Ilikuwa ni bahati sana, hatimaye Rashad alimuona tena Johari kwenye taarifa ya habari akihojiwa na mtangazaji juu masuala ya kifedha.

Basi, kwa utaratibu wa hali ya juu na kwa umakini, Rashad alisoma jina la Johari lililokuwa limewekwa kwenye ‘skrini’. Hatimaye sasa Rashad akafahamu vizuri jina la Johari, alilisoma, tena lilikuwa limeandikwa vizuri kabisa, ‘Johari Chande Munyisi’. Tena kama haikutosha kwa chini ya jina paliandikwa maneno, ‘mchumi, benki ya NIB’. Rashad alifurahi sana. Alifurahi sana na kutoamini kuwa hatimaye alimfahamu Johari kwa jina na hata akawa amefahamu kuwa alikuwa akifanya kazi kwenye benki ya NIB.

Alijikuta akimuangalia Johari kwa umakini mkubwa. Na ajabu eti kwa muda huo mfupi, chozi lilimteremka tena kwenye macho yake, chozi la furaha, huku likiambatana na tabasamu. Hatimaye haja yake ya kumfahamu Johari ilitimia na alikuwa na pa kuanzia kumfahamu vizuri zaidi.

Usiku huo kwa mara ya kwanza aliingia mtandaoni kumtafuta Johari kwa kutumia majina yake kamili kuona kama atakuta lolote la zaidi la kumfahamu. Naam, alipoweka tu jina la Johari mitandaoni yalimjia majibu tele, yalioonesha akaunti za Johari za mitandao tofauti tofauti ya kijamii.

Basi bwana, kama waswahili tujuavyo, kupitia mitandaoni aliweza kufahamu kuwa Johari alikuwa ni mwanamke msomi sana, aliyefanya kazi benki na mwenye cheo kikubwa. Si hivyo tu aliona kuwa Johari alikuwa kaolewa na mtu aliyeitwa Malcom Munyisi ambaye alikuwa ni mfanyakazi wa wizara ya mambo ya nje. Kupitia picha za mitandaoni Rashad aligundua kuwa Johari alikuwa akimpenda mumewe sana kwa maana alikuwa kamposti kwenye picha nyingi sana za kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii na kuambatanisha na picha nyinginyingi zenye ujumbe wa kumpenda kwa moyo wote.

Rashad alifurahi kupata taarifa nyingi zilizo mfanya amuelewe vizuri Johari. Ila pia hakufurahia yale mapenzi ambayo Johari alikuwa akimuoneshea mumewe humo mitandaoni. Kwa maana yeye Rashad alikuwa anampenda Johari.

Basi sasa moyo wake na akili yake akavigeuzia kwenye upande mwengine kuwa lazima afanye namna ya kukutana na Johari na kumkumbushia mahusiano yao ya bomani kipindi yeye Rashad alipokuwa chizi.

Hadi muda huo lengo hasa la Rashad lilikuwa ni kukutana nae Johari na kumueleza jinsi gani anampenda sana na kuwa hajawahi ona mwanamke mwengine mzuri kama yeye Johari. Lengo lake likamfanya kuunda tabia ya kuendelea kupekuapekua akaunti za mitandao za Johari.

Mchana mmoja Rashad alikuwa anatoka zake kwenye masomo yake aliyokuwa akisoma na akiwa anarejea nyumbani alipokuwa akiishi, kwa Sarha. Mara akahisi kuwa simu yake inaita, hivyo akaiangalia na kukuta ‘facebook’ imemtumia ‘notification’ juu ya Johari ambaye yeye Rashad alikuwa ‘keshamfollow’-, ujumbe huo ulimuambia kuwa Johari alikuwa yupo eneo jirani na alikokuwako. Basi naam, kiroho kikamlipuka na kuanza kumuenda mbio. Akaangalia kwa makini kwenye ‘map’ na akaona kuwa kumbe Johari mwenyewe alikuwa amesimama nje ya mgahawa uliokuwa jirani tu kwa mbele yake eneo hilohilo.

Na kweli alimuona Johari. Basi kijasho chembamba alihisi kinamtoka. Taratibu akamuendea Johari hadi pale alipokuwa amesimama. Alimuendea huku akimuangalia usoni hadi Johari akashtuka kuwa alikuwa anaangaliwa.

Kwa upande wake Johari, hakumtambua Rashad, hakumuona kabisa kuwa kafanania na yule chizi aliyelala nae kwenye maboma huko zamani. Kwa sababu wakati huo Rashad alikuwa kabadilika kabisa, alikuwa nadhifu, matanashati, msafi aliyevutia na mwili uliojengeka na hakika alionekana kuwa hakuwa chizi.

“Makubwa, mbona unanitazama sana hadi naogopa?”, aliongea Johari baada ya kumuona Rashad akimkaribia huku akimuangalia kwa makini usoni kama mtu anayetaka kukumbukwa. Johari hakuwa na wazo hata kidogo kuwa chizi wake wa zamani ndio alikuwa akimtazama na kumkaribia.

Alipomfikia alianza kumwambia kuwa alikuwa anamtafuta kwa muda mrefu sana, kauli hiyo ilimshtua Johari. Na kuhoji chanzo hasa cha kutafutwa kilikuwa ni nini, hasa ikizingatiwa kuwa yeye Johari hadi wakati huo aliona hamfahamu Rashad.

Mara Rashad akaanza kumwambia Johari amuangalie vizuri uso wake, alimuomba amuangalie kwa makini ili amkumbuke. “Niangalie vizuri Johari, niangalie vizuri utanikumbuka. Nitazame.”, aliongea Rashad huku akimuangalia Johari usoni nae Johari wakati huo alikuwa akimtazama Rashad kwa umakini hasa. Naam! ghafla kumbukumbu zikamrejea Johari na kwa hakika kabisa alimtambua Rashad kuwa alikuwa ni yule mwanaume chizi ambaye alilala nae kwenye boma, miaka ya huko nyuma.

Johari alishtuka sana na kuanza kujiongelesha moyoni mwake kuwa haiwezekani yule mwanaume chizi kapona na ndiye alikuwa huyo aliyemsimamia mbele yake wakati huo.

Rashad alihisi kuwa Johari keshamkumbuka, alihisi hivyo kutokana na namna Johari alivyoshtuka, alishtuka katika namna iliyodhihirisha kuwa alimkumbuka vizuri.

“Johari ni mimi. Mimi yule mwanamume chizi niliyekuwa naishi mabomani na majalalani. Ni mimi ndiye uliyekuwa unamtembelea kule majalalani usiku na kuwa naye ni mimi.”, aliongea Rashad kwa kujiamini na kuamini kuwa Johari alimkumbuka vizuri.

Hadi hapo Johari alikuwa kachanganyikiwa. Kichwani mwake alijawa na maswali kama alfu ambayo alikosa majibu ya kujipa. Alijiuliza vipi chizi kapona uchizi?, vipi mtu aliyekuwa chizi kaweza kumkumbuka miaka ya baadae jinsi hiyo, hakupata majibu kichwani mwake. Hasira zikampanda kidogo na alijikuta ‘akimkata’ Rashad jicho kali la kiroho mbaya. Kisha akamtolea kauli ya kumuonya. “Samahani sana. Sikufahamu. Samahani sana wewe kaka, tena tafadhali, usiniletee habari za kujuana. Wewe na mimi tumefahamiana watu hadi uniletee habari za kujuana? Mpuzi we”, aliongea Johari kwa kupayuka na hasira, akijifanya hamjui Rashad na hamkumbuki kabisa.

“Johari mimi ninaitwa Rashad, mimi ni yule chizi uliyekuwa ukilala nae kule bomani. Ndio mimi nimepona. Tena nakupenda sana, nimekutafuta sana”, aliongea Rashad na Johari kuzidi kuchanganyikiwa. “mama yangu nini hiki tena”, alijiuliza Johari moyoni, Rashad alikuwa akiongea kwa akili timamu kabisa. Johari alichanganyikiwa hakutegemea kuwa kuna siku yule chizi angemfuata kwa namna hiyo na kumueleza kuwa anakumbuka yale waliyofanya bomani.

“Sikufahamu, na naomba kaa mbali na mimi, ‘i am not a rat like you’, mwehu wewe, sikukumbuki. Tena kama unavyojieleza kuwa ulikuwa chizi hakika naamini uchizi wako bado umekujaa kichwani, chizi mwanga wewe”, aliongea Johari kwa hasira.

Mara mwanadada aliyebeba chakula cha ‘take away’ alitoka toka kwenye mgahawa ambao Johari na Rashad waliusimamia kwa mbele wakati huo, na yule mwanadada akampa Johari mfuko huo na kuondoka. Kumbe Johari alikuwa yuko pale kuchukua ‘take away’ ya chakula toka mgahawani.

Basi baada ya kupokea chakula chake, kwa sonyo na madharau Johari alimtukana matusi Rashad kisha akaelekea kwenye gari lake na kuondoka eneo hilo na kumuacha Rashad kasimama hapo.

Akiwa njiani na gari lake anarudi kwake, Johari alifikiria sana juu ya Rashad, alishangaa sana kuwa mtu yule chizi kapona na kurejea. Kilichomkera zaidi Johari ni ile kauli ya Rashad kuwa eti alikuwa akimpenda na kwamba alikuwa anamkumbuka na kuwa alikuwa kamtafuta sana. Hiyo kauli ilimfanya ajiulize sana, hasa alijiuliza, hivi yule chizi alianza kumtafuta kwa muda gani, na ni mangapi aliyokuwa akiyafahamu kumhusu yeye hivi kwamba aliweza kumpata na kumfahamu kwa jina. Hasira zilimpanda Johari na akajikuta akipiga piga usukani wa gari kila mara kwa hasira.

Alipofika kwake mawazo juu ya jinsi alivyoonana na Rashad yalimjia zaidi. Alikaa kwenye sebule ya nyumbani kwake na wanawe Muujiza, Flora na Florian huku akifikiri jinsi ambavyo walikuwa wakimpa furaha kwenye maisha yake yeye na Malcom na akawaza na kukumbuka kuwa hao watoto wake walikuwa ni watoto wa Rashad. Watoto wa mtu ambaye zamani alikuwa akiugua ugonjwa wa akili. Alifikiria sana Johari juu ya jinsi Rashad alivyomjia na kuongea kuwa alikuwa kawahi kutembea nae kipindi yuko chizi, Johari aliwaza, hivi itakuwa ni watu wangapi Rashad keshawaambia kuwa kawahi kutembea na yeye.

Aliwaza mengi sana Johari. Jioni ya siku hiyo, ilimkuta kajikunyata chumbani kwake kitandani. Akiwaza yale aliyoyafanya miaka ya nyuma na jinsi alivyopata watoto wake kishirikina. Alikumbuka ile familia ya mfanyabiashara ya vito ambaye aliuwawa na wezake wa kundi la kiharifu na mapanya na kukumbuka ndoto za kutisha alizoota baada ya hapo na kukumbuka ile ndoto aliyooteshwa kuwa hatopata watoto maishani mwake na akakumbuka ile kafala aliyofanyiwa na mganga na kufuata sharti a kukutana kimwili na mtu mwendawazimu, hadi hatimaye akapata watoto aliokuwa nao.

Alikaa kitandani mwake na kuzitazama picha ya harusi yake na Malcom, pamoja na picha ya watoto wake zilizokuwa karibu na kitandani. Na kwa uchungu alijiambia moyoni “ ’Nimeisoma namba’ katika kuhakikisha najenga familia ya kujivunia kama hii”, na wakati huo hofu na presha juu ya Rashad aliyejitokeza na kudai kuwa anakumbuka kila kitu na kumpenda, ilimpanda hasaa.



.......................................



Sasa Rashad alizidi kumfuatilia Johari na maisha yake na akagundua kuwa alikuwa na watoto watatu. Alijua hadi hao watoto walikosoma. Rashad akajua hadi Malcom alikokuwa akifanya kazi na maisha yake ya kusafiri mara kwa mara, kwenda nje ya nchi. Aliweza kufahamu hadi sehemu ambazo Johari alipendelea siku za mapumziko. Hadi Johari mwenyewe alifahamu sasa kuwa Rashad alikuwa anamfuatilia. Maana alianza kuona jina lake likijitokeza kwenye watu waliokuwa ‘wakilaik’ posti zake za mitandaoni. Na hiyo ilimtia hasira sana akamblock kila mahala. Mara nyengine alimuona akimfuatilia akiwa katika mizunguko yake, madukani, migahawani, akiwa anapeleka watoto shule ama hata akiwa anakatiza mitaa fulani mjini.

Wakati huo, Imran na Sarha walizidi kujawa na hofu na nyendo za Rashad. Hawakutaka kabisa kumsikia anamuongelea Johari. Ikabidi wamwambie na mama yao bi Aisha, ili amkanye mwanae mawazo yake yasiyo yumkinika, kwa kufikiria kuwa aliwahi kuwa na mahusiano na mwanamke kipindi yuko chizi. Kwao waliona madai ya Rashad ni dalili ya uchizi wake kuwa pengine haujapona. Mwenyewe Rashad aliamini akili zake tu. Hakutaka kabisa kuaminiwa na mtu mwengine, alishaona watu wanamdharau hivyo akaamua kuwa hatamshirikisha mtu kwenye kumfuatilia kwake Johari. Na moyoni mwake alijiaminisha kwa asilimia mia kuwa siku moja Johari atamuacha mumewe na kuolewa nae yeye.



Basi siku moja Johari alikuwa anaondoka toka ofisini mwake, NIB na kuelekea kwenye maegesho ya magari ili aondoke kurejea kwake. Alipofikia gari lake mara akashangaa kumuona Rashad yuko pembeni akimsubiria. Johari alikasirika sana na moyo kwenda mbio na hofu kumjaa hadi akaanza kuongea kwa kulia, “Unataka nini?, unataka nini?”, aliongea Johari, Rashad alimjibu kuwa yupo hapo ili kuonana nae waongee mambo ya muhimu sana. Kwa hasira na kushindwa kutafuta njia ya kumkwepa Johari alimwambia Rashad kuwa apande kwenye gari wakazungumzie mbali na hapo. Basi Rashad akapanda kwenye gari pamoja na Johari na wakaondoka eneo hilo la maegesho la benki ya NIB, na kuelekea maeneo ya ‘Ocean road’, ambako Johari alisimamisha gari na kuanza kumuongelesha Rashad, akimhoji anachokitafuta hasa ni nini.

Rashad alimuonya Johari asijifanyishe kuwa hamjui na hamkukumbuki. Na kumwambia anafahamu vyema kuwa Johari alimkumbuka ila tu alikuwa akijifanyisha hamjui. Rashad akamuambia Johari sababu ya kumtafuta sana, na kumueleza ilitokana na ukweli kuwa alimpenda sana. Alitaka amwambie jinsi anavyompenda na alitaka kuwa nae, na kwamba hajawahi kuwa na mwanamke mwengine kimapenzi zaidi yake, na aliamini kuwa hakuna mwanamke mwengine mzuri kuliko yeye. Hadi wakati huo machozi yalikuwa wamemjaa Johari, akilia kwa kuchoka mambo aliyokuwa akiambiwa na Rashad. Alibaki akimuangalia huku machozi yakimtoka.

Johari alilia kwasababu alimuona jinsi Rashad alivyokuwa ‘serious’ kuwa anampenda na anakumbuka kila kitu walichofanya huko numa. Johari alilia kwasababu hakuwaza kuwa siku moja kitu kama hicho kingekuja maishani mwake, na alilia kwasababu alimtazama Rashad na kuona kuwa alikuwa ni mtu aliyekuwa na uwezo wa kufikia hatua kubwa zaidi ya aliyofikia katika kumfuatilifuatilia.

Safari hiyo, Johari alishindwa kujifanya hamfahamu Rashad na akakiri kuwa ni kweli kumbukumbu za Rashad ziko sahihi kuwa waliwahi kukutana kimwili huko zamani kipindi Rashad akiwa chizi.

Kukiri kwa Johari kulimfurahisha sana Rashad na kujikuta akitoa machozi ya furaha na kujikuta akianza kumshushia mabusu humo ndani ya gari, kitendo ambacho kilimfanya Johari alie zaidi, na kwa uchungu akaanza kuwaka na kupayuka.

“Nimeolewa, nina maisha yangu, nina familia yangu, nina watoto wangu. Wewe unanitakia mimi kitu gani hasa”, alilia Johari kwa uchungu mwingi na kushindwa kujizuia. Wakati huo Rashad naye alikuwa akilia.

“Sijali juu ya mume wako mimi nakupenda wewe”, aliongea Rashad huku akilia, kauli hiyo ilimtia hasira Johari, “Acha upumbavu Rashad, mimi ni mke wa mtu, nakuomba kaa mbali na mimi, chochote kilichotokea baina yetu hakina maana tena, niache na maisha yangu, achana na mimi”, alilia Johari na kuanza kuufungua mlango wa kutokea kwenye gari wa upande wa Rashad na kumuomba ashuke na asimtafute tena. Rashad alishindwa kugoma akashuka toka garini huku akilia, na Johari akimsukuma ashuke haraka huku naye machozi ya hasira yakimtoka basi Johari aliwasha gari na kuliondoa na kuondoka eneo hilo huku nyuma akimuacha Rashad akimuangalia. Ilikuwa ni hali ya kushangaza kabisa, Rashad alikuwa akihisi mapenzi makubwa kwa Johari wakati akijua kabisa Johari ni mke wa mtu, tena mwenye watoto wake kabisa.


Rashad aliumia sana moyo wake siku hiyo Johari aliyomfukuza toka garini. Aliwaza sana na kujiuliza, kwanini Jihari kamtendea vile. Katika hali ya kushangaza Rashad hakutaka kuelewa akilini mwake kuwa Johari alikuwa ni mwanamke aliyekuwa akipenda ndoa yake na familia yake hivyo hakutaka kujihusisha na Rashad.

Ila sasa kilichompa nguvu zaidi bwana Rashad, ni ukweli kuwa Johari alikiri kuwa kweli wao walikutana kimwili bomani, hivyo Rashad hatimaye akajiamini kabisa kuwa kumbukumbu zake za kutembea na Johari wala haikuwa ni uchizi wake bali ni kumbukumbu sahihi kabisa ambazo muhusika mwenyewe, Johari alikuwa kakiri kuwa kweli hilo suala lilijiri.

Basi Rashad wala hakukoma aliyokuwa akiyafanya akawa anaendelea kumfuatilia Johari. Mpaka siku ya siku akakutana na ‘article’ ya ‘interview’ aliyowahi kufanyiwa Johari na muandishi mmoja maarufu aliyekuwa akiandika juu ya masuala ya wanawake mitandaoni. Kwenye makala hayo, Johari alizungumzia jinsi ambavyo alikaa kwenye ndoa yake kwa muda mrefu bila ya kupata ujauzito wowote hadi mungu alivyotenda miujiza akapata mtoto wa kwanza kisha akapata watoto wawili mapacha. Hilo lilikuwa ni moja kati ya mengi tu aliyoendelea kuyafahamu juu ya Johari. Johari alikuwa ni mwanamke ambaye habari zake zimezagaa tu mitandaoni, kutokana na cheo chake kikubwa katika benki ya NIB na kazi ya mumewe katika wizara ya mambo ya nje, ilikuwa ni kawaida kuingia ‘youtube’ na kukuta habari zake.

Rashad aliendelea kumfuatilia Johari, na Johari alitafuta mbinu zote za kumkwepa Rashad, hivi kwamba hata Malcom alianza kunotisi mabadiliko kwa mkewe, kwanza kabisa alimuona mke wake kuwa alikuwa kama mtu mwenye hofu muda wote, na pili aligundua kuwa mke wake alianza tabia ya kuficha ficha shughuli zake za mitandaoni, tena akamuuliza mbona yuko tofauti na Johari akajitetea kuwa kagundua haina haja ya kuposti kila kitu mitandaoni hivyo ndio maana alikuwa akipendelea faragha za kimtandao kadri siku zilivyokwenda.

Pamoja na kumkwepa Rashad kwa mbinu zote hatimaye Johari aliamua kukutana na Rashad kwenye mgahawa fulani. Katika maongezi hayo, Rashad alimuuliza Johari kwanini, alikuwa akimfuata kule bomani kipindi yuko chizi. Johari alishindwa kujibu jibu hilo, huku hofu ikimjaa.

Mara Rashad akaachia tabasamu na kukamata mkono wa kuume wa Johari kwa nguvu kumvutia kwake na kumbusu shavuni kwa nguvu bila ya ridhaa ya Johari na kumwambia kuwa, yeye Rashad anafahamu vyema kuwa Johari anampenda hivi kwamba alikuwa yu radhi kulala nae kipindi yuko chizi, na kwa maana hiyo, kama Johari alimpenda yeye kipindi yuko chizi basi kwa hakika lazima atakuwa anavutiwa nae kipindi yuko mzima mwenye akili timamu.

Kwa hasira Johari alimtamkia Rashad kuwa anampenda mumewe sana tena sana. Na katu hatomuacha Malcom kisa Rashad na kumuonya akae mbali nae na akasimama na kuondoka zake.

Eti hadi wakati huo, Rashad alikuwa kajiaminisha kuwa lazima Johari atakuwa anampenda sana hivi kwamba alikuwa radhi kulala nae kipindi yuko chizi. Aliona lazima yatakuwa ni mapenzi ya dhati kwenye kwelikweli ndio yaliyomvutia Johari kujihusisha naye kimapenzi kipindi yuko chizi. Hivyo Rashad alijiaminisha kuwa alichohitaji Johari ilikuwa ni kuachana na Malcom na kuolewa nae yeye ambaye anampenda. Na mawazo hayo yakaanza kumea na kukomaa.



................................

Basi bwana katika tabia ya Rashad kumfuatilia sana Johari, alijikuta akimfuatilia nyendo zake za kila siku ikiwamo kila alipokuwa akiwapeleka watoto zake shule. Lengo lilikuwa ni kujibana kwa pembeni na lango la kuingia shule na kisha kukaa hapo hadi Johari alipofikisha watoto zake shule, lengo lilikuwa ni kumpiga picha tu. Na baada ya kumpiga picha Johari, Rashad basi angefuraaahi na roho yake na kuangaliaangalia hiyo picha. Na Johari hakujua kuwa Rashad alikuwa akimfuatilia hadi kufikia hatua hiyo.

Sasa bwana Rashad akaanza kufikiria sana kuwa kitu pekee kimfanyacho Johari akatae kuwa nae ni Malcom ambaye Johari alikuwa kaolewa nae na kuwa na watoto nae watatu. Rashad aliwaza kuwa kama ataweza kujenga mazoea na kupendana na watoto wa Johari basi angekuwa na nafasi kubwa ya kupendwa na Johari zaidi, na pengine kupitia ukaribu wake na watoto, Johari angeweza kuona urahisi wa kuachana na Malcom. Hayo mawazo yalikuwa ni finyu sana ila ndio hivyo Rashad alivyoamini.

Hivyo mchana mmoja wakati watoto wa Johari walipokuwa wanatoka shule wakisubiri dereva kuwafuata, Rashad aliwaendea na kuwasalimia na kujaribu kuongea nao. Watoto walikuwa wote watatu, Muujiza, Flora na Florian. Walikuwa wadogo, wazuuri waliochangamka na ajabu walikuwa huru na bila wasiwasi kuongea na Rashad ilihali hawakumfahamu. Rashad alifurahia sana kuongea na watoto wa Johari.

Ila sasa, kuna kitu ambacho kilianza ‘kumgonga’ akilini mwake. Katika hali isiyo ya kawaida, kupitia sauti za wale watoto, Rashad alijikuta anahisi kama anayesikia sauti za udogoni mwake. Kabisakabisa! Kichwani mwake alikuwa akisikia sauti ya kike ya mdogo ake wa kike, Sarha kila mara mtoto wa Johari, Flora alipoongea na alisikia sauti yake kwenye kila sauti iliyotoka mdomoni mwa Florian na Muujiza.

Ghafla kichwani mwake taswira za utotoni mwake zilimjia na aliona kabisa kuwa alikuwa sahihi kuwa sauti za wale watoto zilikuwa zinafanania kama za kwake yeye na Sarha walipokuwa wadogo. Na mara taswira za udogoni mwake zikamjia zaidi na kuona kabisa sura za watoto hao zilikuwa ‘kopiraiti’ na sura yake na Sarha kipindi wako wadogo.

Mara ghafla tawira na sauti hizo zilimtoka kichwani, na kusikia kauli za watoto wa Johari wakimuaga huku wakielekea kwenye gari iliyofika hapo kuwachukua na kuwarudisha nyumbani. Hapo akashtuka kuwa kumbe mawazo yake yalimuhama toka eneo hilo alilokuwako hivi kwamba hakugundua pale dereva wa kuwafuata watoto wa Johari alipofika.



Haikuwa hali ya kawaida kabisa. Wazo la ajabu sana lilimuingiza Rashad kichwani. Alijiaminisha kabisa watoto wa Johari walifanania kabisa na jinsi yeye na Sarha walivyokuwa kipindi wako wadogo.

Alipotoka eno lile la shule moja kwa moja alirejea nyumbani alikokuwa akiishi na huko akajikuta akitafuta picha ya zamani sana aliyopewa, picha iliyoonesha yeye na Sarha walipokuwa wadogo. Naam! bila ya kukosea, zile sura za watoto wa Johari zilirandana vyema na sura zao Rashad na mdogo wake kabisakabisa. “watoto wapo kama sisi tulivyokuwa wadogo”, alijiambia Rashad.

Sasa mawazoni mwake mawazo yakazidi kumzidia Rashad. Alijiuliza kwanini wale watoto wa Johari walifanana na familia yao. Alijiuliza kama wale watoto ni wake na sio wa Malcom kama ijulikanavyo. Alijuliza sana. Ila hakuwa na mtu wa kushea nae mawazo yake maana aliona kuwa Imran na mkewe Sarha wangepuuzia mawazo yake. Ila yaliyo kichwani mwake yalikuwa mazito hivi kwamba ilibidi amuelezee shemeji yake. Sasa Imran akatatizika zaidi. Alidhani Rashad kashaachana na habari za mwanamke aliyeitwa Johari, kumbe ndio kwanza alikuwa anakuja na habari mpya kuwa Johari ana watoto ambao yeye Rashad alihisi ni wa kwake.

“Kwa nini unafanya hivi shemeji yangu. Hivi unajua unachosema utasababisha kuleta mgogoro kwenye ndoa ya mdada wa watu”, aliongea Imran kumuomba Rashad aache habari hizo, ambazo hazikuyumkinika kwa akili ya kawaida.

Safari hii Rashad alimjia juu Imran wala hakumlazia damu, “Yani Imrani, nakuja kwako shemeji yangu, nakwambia kitu cha maana kama hichi wewe unanichukulia mimi nina matatizo ya akili”, alilalamika Rashad kwa hasira na kuanza kumvimbia shemeji yake. “Unanichukulia mimi ni mwehu, ilihali nina akili zangu timamu. Ninakwambia yule mwanamke ana watoto na wale watoto nimewaangalia vizuri na mimi naapia kwa mungu na mtume, wallahi wale wale watoto kwa jinsi walivyo tu ni wa kwangu, sio wa mume wa huyo mwanamke”, aliendelea kulumba Rashad tena kwa sauti kubwa. “wewe unaniletea habari za niongee vitu vyenye kuyumkinika akilini, inamaanisha unanichukulia mimi ni chizi mwehu. Na mimi nakwambia wewe na mkeo huyo Sarha, acheni mambo yenu ya madharau mimi niwaambiapo mambo naombeni muwe na heshima, naelewa niwaambiacho” aliendelea.

“Hivi nikiwauliza miaka zaidi ya kumi na kitu niliyoishi naranda mitaani mnieleze nillikumbana na nini mtaweza nieleza ninyi. Walau mwenyewe nakumbukakumbuka yaliyonisibu, sasa ndo nakwambia, yule mwanamke anaitwa Johari, nilitembea nae nilipokuwa chizi na nakwambia tena watoto alionao ni wa kwangu” alifoka Rashad, hivi kwamba mtu yeyote aliyekuwako nyumbani hapo angeweza kusikia kelele zake, zilizotoka hapo barazani walipokuwa wamesimama na kulumbana, mabishano yao yalisikika hadi ndani na kuwatoa nje Sarha na mama yake bi.Aisha.

Sarha na mama yake walitoka mbiombio na kuhoji ni nini kilikuwa kinajiri nje hapo. Ndipo Rashad akaanza kumwambia mama yake na dada yake kuwa ana watoto watatu aliozaa na yule mwanamke aliowaambia siku nyingi kuwa alikuwa na mahusiano nae kipindi yuko chizi.

Bi. Aisha kama walivyo Imrani na Sarha hakuamini na kutaka Rashad aache maneno yake. Rashad akawa akitumia nguvu kubwa akitaka wamuamini hadi akawa sasa analia, hatimaye mama yake, bi Aisha nae imani ikaanza kumuingia na kumwambia kuwa yeye kama mama yake anaelewa mwanae akiongea ni kwa vipi huuelezea ukweli na kwamba alikuwa keshamuamini, “mwanangu, ukielezacho huenda ikawa ngumu kwa mtu mwengine kuelewa ila mimi mama yako, sina shaka kabisa, nimekuamini kila unachokisema”, kwa kauli hiyo hata Imrani na Sarha ikabidi waamini kabisa kuwa huenda ni kweli Rashad alikuwa na mahusiano na huyo Johari kipindi yuko chizi na wakaamini kuwa huenda kweli watoto wa huyo mwanamke ni wa Rashad kweli.

Walau sasa moyo wake Rashad uliweza kutulia. Hatimaye walau mama yake, shemeji yake na Sarha walikuwa wakiamini alichokuwa akiwaambia.

Basi sasa Rashad akaamua kuonana na Johari. Na kama kawaida akamsubiria nje ya jengo la ofisi yake na kusimamisha gari lake pale Johari alipokuwa akitaka kuondoka, basi katika hali isio kawaida Johari alisimamisha gari na Rashad akapanda na kama kawaida Johari aliendesha gari hilo hadi Ocean road kisha akapaki gari pembeni na kumgeukia Rashad.

Alipomtazama aliona kuwa Rashad alikuwa na machozi uso wake wote. Mara akamuona Rashad akiingiza mkono mfukoni na kutoa picha mbili za ‘hardcopy’. Kisha akachukua moja na kumuoneshea Johari. Picha yenyewe ilikuwa ni ya familia yao, yani, Rashad, Sarha, Imrani na mama yao bi. Aisha.

Johari hakuelewa hao watu wa pichani na wala hakuelewa kilichomliza Rashad na akawa akiona kama analetewa uchuro garini mwake.

Ndio mara Rashad akafuta machozi yake na kuanza kuongea. “Unaona hawa pichani, hawa ndio familia yangu, mama yangu, shemeji na Sarha dada yangu”, aliongea Rashad na kumfanya Johari ashangae na kupayuka, “enhe, sasa ndio vipi yani?”, aliuliza Johari.

“Kwa mara ya kwanza, kwa mara ya kwanza, wameamini nilichowaambia kuwa niliwahi kuwa na mahusino na wewe”, aliongea Rashad. Maneno hayo yalikuwa kama bomu kwa Johari. Aliwaza kwa haraka na kujiuliza kama Rashad kaanza kushirikisha familia yake kwenye ishu ilokuwa inaendelea nini kilikuwa kinafuata.

“kwanini umewambia ndugu zako kuhusu sisi, hivi unajua unachofanya ni kuharibu maisha yangu” aliongea Johari kwa hasira na Rashad akajitetea kuwa ilikuwa lazima awaambie familia yake inayompenda.

“Johari najua humpendi mume wako kama unavyonipenda mimi, ndio mana ukadiriki kutembea na mimi hata nilipokuwa chizi na mimi nakwambia nakupenda pia, tena nakupenda sana, mimi niko radhi kukuoa hata ukisema unamuacha mumeo leo hii mimi nakuoa”, aliongea Rashad.

Kauli hiyo ilimtia hasira Johari na kuanza kupayuka jinsi alivyompenda mume wake na kuwa hawezi kuwa na Rashad na kujinadi kuwa tayari ana familia na mumewe, tena familia ya watoto watatu.

Kauli hizo za Johari sasa zilimuumiza Rashad na hivyo akjikuta akichukua picha ya pili na kumuoneshea Johari, “Ona Johari, huyo pichani ni mimi na mdogo wangu wa kike Johari.”, Johari aliangalia hiyo picha kwa jicho baya sana.

“Ona Johari jinsi nilivyofanania nilipokuwa mdogo. Ona jinsi nilivyo fanana na watoto wetu, Muujiza, Flora na Florian”, aliongea Rashad sasa akimuangalia Johari machoni na kumshtua Johari kwelikweli na kufanya atoe macho. Hakuamini kama alikuwa kweli kamsikia Rashad akiwaita akina Flora kuwa ni watoto wake, alishtuka sana.

“Acha. Kushtuka Johari na kuogopa na usithubutu kujitia hujui hili, ukweli unaujua kuwa hawa ni watoto wangu.” Aliongea Rashad.

Johari alipanda hasira na kupayuka ila alishindwa kukana alichozungumza Rashad kuwa watoto ni wa Rashad na sio wa Malcom, akabaki akilia kwenye magari.

“Johari nakupenda sana. Mimi natamani umuache mume wako hata kesho, ili nikuoe. Hebu fikiri tutavyoishi kwa furaha, wewe mimi na wanetu watatu pamoja na mama yangu na Sarha, familia iliyokamilika kabisa.”, alimaliza kuongea Rashad.

Kwa akili za Rashad aliona kuwa kuna namna ya kumshawishi Johari kuachana na Malcom ili aolewe na yeye, ambacho Rashad hakutaka kukubali wakati huo ilikuwa ni ukweli uliowazi kwamba Johari alimpenda mume wake, tena alimpenda sana na aliipenda ndoa yake, na hakutaka Rashad awepo kabisa kwenye maisha yake.



Basi, jioni ya siku hiyo Johari alijifungia chumbani mwake na kulia sana. Alilia kwa kuogopa na kujiuliza nini kilikuwa kinaenda kutokea kwenye maisha yake. Aliogopa, kwa maana aliona jinsi Rashad alivyokuwa ‘serious’ kuwa anataka yeye Johari aachane na Malcom, tena alitaka waoane wao na zaidi ya yote alijua ukweli kuwa watoto watatu ambao Johari aliwalea na Malcom walikuwa ni wa kwake. Johari alihofia sana, na kujiuliza itakuwaje Malcom akijua ukweli.

Aliwaza sana Johari hadi usingizi ukamjia na kulala. Baada ya kulala, ndoto ya ajabu ilimjia. Katika namna isiyo ya kawaida Johari aliota anakimbia na kurandaranda mwitumi, huku nywele zake zikiwa zimetimka na mwili wake kujaa jasho, vumbi na kuchoka. Mara ghafla mwanamume mrefu sana, aliyevalia mavazi meupe mwenye mwili mkubwa alitokea mbele yake na kumshtua sana hivi kwamba akajikuta akipoteza nguvu na kushindwa kukimbia tena na akajikuta akisimama na kumuangalia yule mtu aliyemtokea. Mtu mwenyewe alikuwa amevalia mavazi ya kung’aa sana hata ya kamuumiza Johari machoni.

Mara yule mtu akaanza kuongea, “Kivuli humfuata mtu na huonekana na mtu pale awapo kwenye mwanga lakini nacho kila mara hupotea mwanga upunguapo na kuondoka, lakini mwerevu huelewa kuwa kivuli kitarudi tena na kuonekana kumfuatilia mtu kila mwanga utapokolea tena, basi vivyo hivyo ndivyo ilivyo mikosi itokanayo na maovu ya mtu, huonekana kisha hupotea na kufanya mtu aamini kuwa ayamepita ila baadae hurudi tena palepale kumtesa mtu”, alimaliza kuongea yule mtu.

Japokuwa Johari alikuwa akimuogopa huyo mtu kwenye ndoto alijikuta akipandwa na hasira na kumhoji, “unamaanisha nini, wewe jitu la kutisha, mbona unanizibia njia yangu niliyokuwa napita humu mwituni”.

Basi yule mtu akamjibu kuwa yeye hakuwa jitu la kutisha bali yeye alikuwa ni malaika wa mungu na kwamba alikuja tu kumkumbusha Johari kuwa alipewa mtihani, ili Johari atafute nusura ya mwenyezi mungu ila, ndio kwanza akaenda kwa waganga na kufanya ushirikina.

“Kwa maana hiyo, ule mtihani wa utasa ulioupata kutokana na maovu yako ya huko awali, ulipaswa ukufundishe kumtumainia tena mungu wako na kuzidisha maombi na dua kwake, ili akupe nusura na kukujaza imani yako, ila wewe umeenda kwa waganga na kumkufuru muumba wako, ama kwa hakika wewe ni miongoni mwa waja wale waliojichagulia wenyewe njia ya upotevu” na huyo mtu akaendelea kumwambia Johari kuwa, kukubuhu kwake katika kufanyia watu maovu kumefika tamati na kwamba nguvu za miujiza za wao malaika ndizo zilikuwa zinaingia kwenye vita dhidi yake Johari ili kuzuia uovu wake ulioota mapembe na kukomaa.

Basi hiyo ndiyo ilikuwa ndoto ya Johari.

...................................



Kwa upande wa Rashad ndugu zake walikuwa washamuamini alichowaambia. Ila sasa waliona ni mtihani wa aina yake uliokuwa ukimkabiri huyo mwanamke aliyeitwa Johari kwa maana walifahamu kuwa Johari alikuwa keshaolewa, walifikiria sana na kujiuliza, itakuwaje sasa mume wa huyo Johari atakapo jua ukweli juu ya mkewe.

Ila yote kwa yote Rashad alifurahia sana jinsi walivyomuamini na kichwani mwake alijipa imani mia kwa mia kuwa ,hatimaye Johari atambwaga Malcom na kisha ataolewa nae yeye.

Kumbe kipindi Rashad akiwaza hayo, Johari nae alikuwa akiwaza yake. Si ya kutubu uovu aliowahi kufanya huko zamani ambao ulikuwa chanzo cha majanga yake yote aliyokuwa akipitia, wala si ya kukubalina na kila alilotamani Rashad, bali aliwaza namna ya kumpoteza Rashad. Johari aliwaza namna ambayo Rashad anaweza kufutika kwenye ramani. Na basi akapanga njama za kuagiza watekaji nyara wamteke Rashad, kisha wamtese na kumuulia mbali. Naam! hilo lilikuwa suala rahisi sana. Johari alikuwa na pesa za kutosha kumpoteza mtu.

Basi alifanikiwa kukodi watekaji nyara nao walimteka Rashad na kumpeleka mbali kwenye eneo la magofu ambako kulikuwa ni nje ya mji, karibu na mwituni na kusikokuwa na watu kabisa. Huko walimtesa sana kwa lengo la kumuua.

Mateso aliyopewa yalimfanya Rashad apoteze kabisa tumaini la kuishi na kujiona kuwa anakufa muda wowote. Hakukuwa na namna ambayo aliweza kujing’amua toka mikononi mwa watesi wake. Alijikuta akiishiwa nguvu na kuanguka kwa kuzirai huku watesi wake wakiendelea kumpa kichapo.

Hadi giza linaingia, huko alikokuwa akiishi Rashad, bwana Imran na mkewe Sarha na bi. Aisha walikuwa na wasiwasi mwingi, kwa maana toka mchana wake hawakumuona Rashad akirejea na wala hakupatikana kwenye simu walijawa na hofu kweli na wakashindwa hata pa kuanzia wakabaki wamejikusanya kwenye sebule ya nyumba yao huku wakisubiri labda angeingia hapo ndani muda si muda.



................................


Basi, Rashad alipoamka aliwaza kwa haraka sana kuwa lazima atafute mbinu ya kuwarubuni watesi wake. Nao watekaji nyara waligundua kuwa mateka wao kazinduka hivyo wakamuendea kwa ajili ya kummaliza.

Na Rashad alijua kuwa sasa walikuwa wanataka kummaliza kabisa hivyo aliamua kufanya maamuzi ya mwisho kabisa ya kutetea uhai wake. Na kujaribu kuwashawishi watesi wake kuwa yeye anatoka kwenye familia ambayo dada yake na shemeji yake wana uwezo sana. Hivi kwamba wanaweza kuwa na pesa zozote za kuwalipa, na hivyo Rashad akaomba wamueleze sababu za kumtekea, ndipo wakamwambia wametumwa na mwanamke anayeitwa Johari.

Rashad ilimuuma sana, hakutarajia hata mara moja kuwa Johari alikuwa na uwezo wa kumtumia yeye wateka nyara, tena mbaya zaidi watekaji waliotaka kumuua kabisa. Ilimuuma kwa maana yeye alidhani alikuwa na uwezo wa kumfanya Johari aachane na Malcom ili aolewe na yeye. Ila kumbe, Johari alikuwa hataki hilo kwa kiasi cha kujaribu kuthubutu kumtumia wauaji, ilimuuma sana.

Katika harakati za kujitetea Rashad akawaambia kuwa dada yake anaweza kutoa dau kubwa kuliko la Johari, hivyo akawapa dili kuwa wamuachie na dada yake atawalipa pesa nyingi zaidi.

Mara wale watesi wakacheka sana na kumuongezea kipigo na kumwambia kuwa hawana shida na nyongeza yeyote ya pesa, kwanza alikwisha waona sura hivyo wao waliona ilikuwa upumbavu wa hali ya juu kuamua kukubali dili alilokuwa akiwaofa kwa maana wakikubali na kumuachia lazima angetumia vyombo vya dola kuwapata na isitoshe walikuwa wameridhika na pesa za Johari.

Basi kwa kumuoneshea Rashad kuwa hawarubuniki, walimpigia simu Johari na kumwambia dili ambalo Rashad alitaka kuwapa pesa nyingi zaidi. Basi kupitia kwenye simu Johari alimrushia matusi Rashad na kujinadi kuwa yeye ndiye mwanamke mwenye pesa kuliko dada wa Rashad, tena ndiye aliyemiliki pumzi ya Rashad wakati huo, tena Johari akatoa kauli za kufuru, “hata mungu wako na malaika zake hawawezi kuokoa pumzi yako kwa sasa” alijinadi Johari, “yani ni kama vile iwe kheri unisujudie mimi kwa maana ndiye mmiliki wa pumzi yako” aliendelea kujinadi kishetwani shetwani kabisa. Kisha akakata simu.

Basi wale watesi waliendelea kumpiga Rashad hadi akapoteza fahamu tena na kumpa mapigo ya mwisho hadi ikafikia tamati wao wenyewe wakaona kuwa washaua. Rashad alikuwa kashakwisha.


Katika namna isiyolezeka wakati Rashad anapigwa na wale watesi mama yak, bi Aisha alikuwa akihisi maumivu mwilini na uchungu mwingi, ijapokuwa hakujua mwanae alikuwa wapi ama alikuwa na akina nani na bila kujua kuwa alikuwa katekwa alihisi kusikia maumivu na kutoa machozi, hiyo ilikuwa ni hisia ya kipekee hasa ambayo inasemekana huwa inawapata wa mama ama ndugu wenye mapenzi ya dhati sana, hivi kwamba bila kujua huhisi tabu zote apitiazo mtu wampendae kila awapo tabuni, hata kama hawajui hasa aliko.

Wakati huohuo Johari akiwa kwwake alikuwa kajawa na furaha sana na mumewe. Wakati huo Johari alijiona kawini. Alijua Kuwa usiku huo Rashad alikuwa anakufa na kumuacha aishi raha mustarehe yeye na Malcom wake na watoto wao watatu. Johari alijawa na furaha usiku huo hivi kwamba watoto wake walipolala aliwasha muziki wa taratibu sebuleni kwake na kisha kufungulia shampeini na kumimina kwenye glasi na kisha kunywa pamoja na mume wake huku wakicheza ‘love songs’ kwa kukumbatiana na kwa mapenzi makubwa, Malcom alishangaa jinsi mke wake alivyokuwa kachangamka kupita maelezo. Na wakati huo Johari alifahamu furaha yake ilitokana na kujua ukweli kuwa usiku huo kauwawa Rashad, mtu ambaye alikuwa ndie kauzibe pekee kilichobaki katika kumfanya Johari aishi kwa kujiamini kwa asilimia mia na familia yake.

Basi, kule ambako, Rashad alikuwako wale watesi wake walikuwa wamempiga vya kutosha hadi wakaona kuwa wamemuua kisha wakaamua kuondoka.


Basi Rashad akiwa anaamini kuwa anakufa na kukata roho, aliona kuwa wale wateka nyara wameondoka na kumuacha kwenye baridi la usiku hapo kwenye magofu ili afe, na aliamini anakufa kweli. Na mara akazima, fahamu akapoteza na kuzirai kama mfu hata pumzi yake ilikuwa kama imempotea, ilikuwa ni mtu ambaye tayari kafa ila kumbe alikuwa bado yani Rashad alikuwa katika hali ambayo ilikuwa ngumu kuieleza, nusu mfu nusu mtu hai, ila aliyekuwa akielekea kufa kuliko kupona.

Mara njozi ikamjia, njozi kuwa katokewa na malaika akimwambia ajikaze, ajikaze asikate tamaa mwisho wake haujafika. Kwamba yeye yupo ili kumuangusha mwanamke aliyemuovu ambaye amechagua njia ya upotevu na kuacha njia iliyokuwa sahihi njia ya watu wema.

Mara malaika alimwambia Rashad awahi awahi na awahi kurejea ulimwenguni kabla milango iliyotenganisha uhai na ufu haijafungwa. Basi Rashad humohumo ndotoni akajikuta akianza kutimua mbio, mbio, mbio akikimbilia kwenye lango kuu lililotenganisha uhai na kifo ili aweze kutoka nje na kurudi kwenye uhai kabla lango hilo halijafungwa na yeye kujikuta kabakia kuzimu.


Basia ndani ya yale magofu ambayo Rashad aliachwa, hakuamka tena mpaka asubuhi jua lilipochomoza na kumuangaza humo ndani ya magofu na kumunguza kidogo ndio akaamka.

Japokuwa alikuwa na damu na maumivu mengi mwilini alijiona ana nguvu za kutosha hivi kwamba aliweza kujiinua. Hakika aliona kuwa ilikuwa ni muujiza wa mungu pekee uliomfanya awe bado mzima hadi wakati huo.


..............................



Asubuhi ya siku hiyo, Imrani na mkewe waliripoti polisi juu ya kupotea kwa Rashad. Na walikuwa wapo pamoja na mama yao bi. Aisha, ambaye alikuwa anashindwa kabisa kutulia, huku akikumbushia kuwa mwanae aliwahi kupotea kwa zaidi ya miaka kumi na kumlilia mungu aepushe mwanawe asipotee tena kama jinsi alivyopotea mwanzo.

Basi wakiwa wamekaa sebuleni mara walishaangaa mlango wa sebule hiyo ukifunguliwa na wakashangaa kumuona Rashad akiingia huku akiwa hoi, mwili umetapakaa damu na kujaa vumbi.

Wote walishtuka kumuona katika hali kama hiyo na kuogopa. Walijkuta wote wakiangua machozi ya mchanganyiko wa furaha ya kumuona karejea na pia majonzi kwa ile hali aliyokuwa nayo.

Basi baada ya kutulia Rashad alisimulia familia yake kuwa kilichotokea kilikuwa ni mipango ya Johari na kwamba alikuwa kanusurika kifo kwa mipango ya mungu tu. Ndugu zake walimuhurumia sana. Na kumuahidi kuwa hakika Johari lazima aozee jela kwa aliyoyafanya.


.........................



Basi bwana, kwa upande wa Johari siku hiyo ilikuwa nzuri sana, tena ilikuwa jumamosi yani siku ya mapumziko. Hivyo mchana wa siku hiyo alibeba mume wake na watoto zao watatu na kuwatoa piknik, huko ufukweni mwa bahari kupunga upepo na kuota jua na kufurahia siku nzima. Ambacho Johari hakukijua hadi wakati huo ilikuwa ni kwamba Rashad alikuwa hajafariki kama jinsi wale watekaji nyara walivyomtaarifu kuwa walikuwa washamuaa. Tena hadi wakati huo anafurahia pikinik Rashad na ndugu zake walikuwa tayari washamshtaki polisi na wakati huo askari walikuwa wakimfuatilia na kumtia chini ya ulinzi.

Naam akiwa mwenye furaha na familia yake polisi walimjia Johari na kumuweka chini ya ulinzi na kumpeleka selo, huku nyuma akiacha mume wake, Malcom na watoto wao watatu.


.............................



Basi bwana, kesi ya Johari kutaka kumuua Malcom ilikuwa ni ya aina yake. Malcom hakuelewa kitu, yeye aliona kama mke wake anaonewa, kwanza hakuwa akimjua Rashad na wala hakufahamu hata chembe ya sababu ya kumfanya mkewe kudhamiria kumua Rashad. Hivyo pale alipoambiwa kuwa mkewe alikuwa akitaka kumuua Rashad kwa lengo la kuficha ukweli juu ya uhalisia wa baba wa watoto wa wao usijuliakane, Malcom alichanganyikiwa. Siku zote alijiona yeye ndiye baba wa watoto wa mkewe, na hakutaka kuamini madai kuwa Rashad ndiye alikuwa baba halisi wa watoto.

Pia kwa kuwa Johari alikuwa ni mwanamke mwenye cheo kikubwa na alijulikana na wengi, stori yake ilifikia waandishi wa udaku na hadi wale watangazaji wa redio. Ilikuwa ni hekaheka ambayo kila mtu mji mzima alikuwa akiifuatilia.

Johari alishindwa kabisa kujitetea na akakamatisha wale watekaji nyara aliowatuma kumteka Rashad, ambao nao walitumika kuwa ushahidi wa uovu wa Johari dhidi ya Rashad.

Basi watoto walipimwa DNA na kugundulika kuwa ni kweli walikuwa ni watoto wa Rashad na si wa Malcom. Naye Johari alihukumiwa kifungo cha miaka kadhaa kwa kosa la kujaribu kufanya mauaji ya kudhamiria, pia wale wateka nyara walihukumiwa.

Basi mwishowe Rashad na familia yake walipata haki yao ya kujualikana nani hasa ni baba wa watoto wa Johari na Johari akaishia jela kutokana na uovu wake.




......................



Basi mwaka mmoja baadae Johari akiwa jela alipata ugeni toka kwa Malcom. Johari alikuwa na michozi mashavuni kwa uchungu siku hiyo. Ilikuwa ndiyo mara ya kwanza kwa Malcom kwenda kumtembelea toka afungwe. Malcom alikuwa hana hamu hata ya kumuona mkewe toka ajue ukweli kuwa watoto walikuwa ni wa Rashad.

Malcom mwenyewe sasa alikuwa kachoka na aliyeonekana kuwa na maumivu mengi ya moyo. Siku ambayo alikwenda kumuona Johari kwa mara ya kwanza alikuwa kaenda na fomu za kimahakama za kutiliana saini ya talaka na kumwambia Johari asaini kwa maana alikuwa anamtaliki ili aoe mke mwengine.

Baada ya Johari kusaini talaka hiyo Malcom huku akilia kwa kwikwi kabisa, Malcom aliingiza mkono mfukoni mwake na kutoa picha ya mwanamke aliyevutia sana na kumuonesha Johari.

Johari alipoangalia picha hiyo alimuona kuwa yule mwanamke alikuwa ni mjamzito, moja kwa moja akaelewa kuwa Malcom alikuwa akitaka kumuoa mwanamke yule wa pichani ambaye alikuwa akitarajia kujifungua na hivyo kumfanya Malcom kuwa baba wa mtoto wake halali kwa mara ya kwanza.

Kisha Malcom akaanza kumwambia Johari jinsi gani alihisi kupotezewa muda mwingi wa maisha yake, “miaka hii yote uliyoniaminisha nina familia yangu, mke na watoto, ingelikuwa najua kuwa wale watoto ni wa yule chizi wako hakika ningekuwa nimeachana nawe muda mrefu sana na kuwa na mke mwengine na kuwa na familia ya uhalisia na si ya kilaghai kama uliyonitengenezea wewe”, hatimaye aliongea Malcom maneno ambayo aliyahifadhi moyoni mwake kwa muda mrefu akisubiria kumwambia Johari. “Ila namshukuru mungu kuwa walau kanifungua macho kabla sijafa na kujua ukweli nikiwa bado ninawexa kuanza familia nyengine”.

Kisha Malcom akamwambia Johari kuwa alikuwa anafunga ndoa wikendi iliyokuwa inakuja na tena akaamua kumtajia jina la mkewe mtarajiwa, “Lulu, mke wangu mpya jina lake ni Lulu” kisha akamuaga, “bye Johari, I loved but your evil heart loved you most from the behind bars” halafu akaondoka, na kumuacha Johari akilia kwelikweli kwa kilio cha kwikwi, huku akimtzama jinsi alivyokuwa akiondoka kwenye hicho chumba cha kuongea na wafungwa.



MWISHO....................
 
wadau hiyo stori nimemalizia. Na sasa hivi nawaandalia stori ingine kaeni tayari.
Kwa ujumla naombeni sapoti yenu ndugu zangu ndio kwanza nimelianza hili gurudumu la uandishi, mwenyewe napenda kweli kuandika andika visa mbalimbali, hivyo karibuni, hasa ukitoa maoni naomba unikomentie pa kuongeza na kurekebisha kwenye kazi zangu. Asanteni
 
Back
Top Bottom