Kitabu: Ukisoma historia ya Wachaga lazima usikie harufu ya damu

Lycaon pictus

JF-Expert Member
Jan 31, 2021
7,310
12,859
Asili na habari za Wachaga
Wachaga walikuwa ni moja ya makabila ya kwanza kwanza kabisa Tanzania kukutana na kupata ustaarabu wa Kizungu. Hilo limefanya kuwa kabila ambalo historia yake imeandikwa na kutunzwa zaidi. Sasa historia yao imejaa damu hasa, kuisoma tu lazima usikie harufu ya damu. Sijui kama makabila mengine nayo walichinjana namna hii(historia zao hazijatunzwa kama ya Wachaga). Nilichogundua baada ya kusoma kitabu hiki ni kuwa 1. Kilimanjaro ilikuwa tajiri hata kabla ya wazungu. 2. Utajiri wa Kilimanjaro ndiyo ulifanya watu wachinjane sana kuugombania. 3. Mangi Meli ni Mangi mdogo sana kwenye historia na inawezekana alikuwa kibaraka wa wadachi, kulikuwa na Mamangi hasa.

Kitabu hiki Asili na Habari za Wachaga kiliandikwa mwaka 1932 na mtafiti wa masuala ya wenyeji aliyeitwa Charles Dundas. Jisomee mwenyewe.








DIBAJI​

KWA Wamangi, wazee na watu wa Kilimanjaro, Salamu ! Habari hizi za kale za kabila la Kichaga zilitungwa kwa maneno niliyoambiwa na wazee wa kila umangi. Maarifa niliyoyapata kwao ya kabila lenu yalinisaidia sana katika kuiendesha nchi kwa desturi za sheria zenu, na kusudi maarifa hayo yasipotee na kusahauliwa na ninyi na watoto wenu, nimeyaandika katika kitabu. Natumaini kitasaidia kuhifadhi haki katika nchi yenu mliyoirithi kwa babu zenu, kiwafanye mwone kiburi na upendo kwa nchi yenu, na kiwafanye mwatii Wamangi wenu na kutumainia mambo ya mbele. Tabia hizi mtaziona katika watu ambao habari zao zimesimuliwa kitabuni humu, na mkizifuata, mtawastahili babu zenu, na kuwasifu kwa ushujaa waliokuwa nao ambao uliuhifadhi urithi wenu. Pia, mtasoma mumu humu habari za mambo maovu na ya upuzi yaliyofanywa na watu wabaya, maana mambo kama hayo yamo katika habari za kila nchi.

Kumbukeni sana ya kuwa mambo mema na mabaya yaliyofanywa na watu huandikwa na kukumbukwa kwa miaka mingi baada ya kufa kwao.

Nawapeni kitabu hiki kiwafundisheni, na tena kiwe ukumbusho wa miaka ile niliyokaa miongoni mwenu, na kiwe alama ya upendo nilio nao kwenu.

Natumaini ya kuwa habari za sasa na za baadaye za nchi yenu zitakuwa za amani na usitawi, na kama hatuonani tena, kitabu hiki kiwe alama ya urafiki kati yetu.

Nataka kuwashukuru sana Nathanael Mtui na Joseph Merinyo walionisaidia sana katika kukitunga kitabu hiki.

Natia sahihi yangu, nikikitaja cheo kile cha heshima mlichonipa.

CHARLES DUNDAS,

Wasahuye-O-Wachaga (Elder of Kilimanjaro).





ASILI NA HABARI ZA

WACHAGA


SEHEMU YA KWANZA

SURA YA KWANZA

ASILI YA KABILA LA WACHAGA.​

TANGU asili Wachaga si watu wa kabila moja, wala asili yao haitoki Kilimanjaro. Tukirudi nyuma na kuchungulia habari za asili ya koo mbali mbali zilizoko sasa, tutaona ya kuwa babu zao walikuja vikosi vidogo vidogo kutoka nchi nyingine nyingine hata wakafika Kilimanjaro. Pengine mtu tu na nyumba yake walifika, au pengine mtu peke yake, akaja akasimamisha ukoo au Kishari. Walikuja katika nyakati mbali mbali; kuna waliofika miaka mia kadhawakadha iliyopita, na wengine waliofika si zamani sana. Sasa yapata vizazi 20 vimepita tangu watu wa kwanza katika hao walipohamia Kilimanjaro; kwa hivi twaweza kuhesabu kuwa miaka 500 au 600 imepita tangu wakati huo hata hivi leo.

Wazee hao wote wa zamani waliotangulia kuhamia huko walikuwa karibu wote Wakamba, Wataita, Wapare, Washambala, Wamasai, na Wandorobo, lakini waliokuwa wengi zaidi ni Wakamba, Wataita na Wamasai, na katika hawa pia waliokuwa wengi sana ni Wakamba. Basi Wakamba na Wataita walifika kutoka kaskazini na mashariki ya Kilimanjaro, na kwa hivyo, upande wa mashariki na wa kaskazini wa mlima ulifikiwa na hao watu wa kwanza. Tangu nyakati hizo, koo nyingi nyingine zimeingia na kukaa kuuzunguka mlima. Nyingi zimegawanyika katika sehemu sehemu, na vita vya siku nyingi vilivyofuata vilifanya watu kuhamahama sana. Husemwa ya kuwa hao waliotangulia kufika katika nchi ya Kilimanjaro walipofika, waliwakuta washenzi wengine waliokuwa wakikaa mwituni wanaokumbukwa hata sasa kuwa ni Wakonongo au Watarimba. Sasa hawaonekani kabisa, maana labda walifukuziwa mbali au kuangamizwa na wageni waliokuja nyuma yao. Husemwa kuwa walikuwa watu wadogo sana wenye vichwa vikubwa, na hujipatia chakula chao kwa kuwinda; na ingawa hii ni hadithi tu, twaweza kusadiki ya kuwa walikuwa mbilikimo. Watu wengi wa namna hiyo walikuwapo katika Afrika, na baadhi yao wapo hata leo katika sehemu nyingine nyingine, na huonekana hasa katika nchi zenye misitu mikubwa mikubwa. Siku hizo yadhaniwa kuwa mitelemko ya Kilimanjaro ilikuwa imefunikwa na mwitu mkubwa uliotambaa mpaka chini uwandani, maana nchi yote inayokaliwa na Wachaga sasa ilifyekwa na watu hao waliotangulia kufika huko, ambao hawakuweza kabisa kulima mpaka walipokwisha kufyeka nafasi. Mwitu huo ulikuwa mkubwa na wa kushikana sana, hata mara nyingi watu wa ukoo huu hawakuwa na habari za watu wa ukoo mwingine, na kwa hivyo hawakujua kuwa walikuwapo watu wengine wanaokaa mlimani; basi kwa muda mrefu kila ukoo ulikaa peke yake, wala hawakuungana ila kwa taratibu kidogo kidogo hata wakawa jamaa kubwa wanaokaa mahali pamoja.

Kila ukoo ulikuwa na mkuu wake, au mzee, na ndiye aliyetawala ukoo. Mara nyingi koo mbili tatu hupigana, na pengine ukoo mmoja hushindwa na kulazimishwa kukubali utawala wa ule ulioshinda. Hivi basi, nguvu ya ukoo huo huwa nyingi, ndipo hupigana na wa tatu, na ushindapo, nguvu yake na mali huzidi kuongezeka, na vivyo hivyo mpaka ukoo mmoja hutawala koo nyingi; na mkubwa wao huwa Mangi. Basi kwa namna hiyo baada ya kupita muda mkubwa nchi yote ya Kilimanjaro iligawanyika na kutawaliwa na Wamangi mbali mbali. Wakuu hao walipigana wao kwa wao, pengine mkuu mmoja huwashinda wengi wengine, na kuwaweka chini yake. Hatimaye wakuu wengineo wachache walipigana ili wapate ukubwa wa kutawala mlima wote, na mambo yakaendelea hivyo mpaka siku za Wazungu zilipofika, ndio walioyakomesha mapigano hayo yote.

Katika kitabu hiki tutasoma habari jinsi Wamangi wengi walivyoinuka, na jinsi walivyotawala na kuzilinda nchi zao au jinsi walivyoshindwa; basi hapo tutafahamu jinsi watu walivyokuwa mashakani kabla ya kuja Wazungu, na jinsi walivyofaidiwa na utawala wao.

Kabla hatujaanza habari za Wachaga, lazima tuangalie jinsi Wachaga walivyogawanyika katika sehemu mbali mbali za utawala. Kuanzia upande wa magharibi twaona: Shira (iitwayo na Wazungu Kibongoto), Machame, Kibosho, Kindi, Uru, Mbokomo, Moshi. Nchi hizi tutaziita Kilimanjaro ya magharibi, au Kiboo. Tukiendelea kuuzunguka mlima, tutaona nchi iitwayo Vunjo; nayo ni milki ya Kirua, Kilema, Marangu, Mamba na Msae (ambayo sasa ni sehemu ya Mwika) na Mwika. Kutoka hapo twaona nchi ya upande wa mashariki ya Kilimanjaro inayoitwa sasa Rombo. Jina hili latokana na mkuu maarufu Horombo au Orombo. Katika nchi hii ziko milki hizi: Mengwe, Mriti, Keni, Mkuu, (hata hivi karibuni Chimbili ilikuwamo) Mrau, Kirua, Machati, Olele na Useri (hata hivi karibuni Ngasini ilikuwamo). Nchi yote ya Rombo hapo zamani iligawanyika katika nchi kubwa tatu, yaani Chimbili, Mkulya, na Useri.

Hivi, zamani nchi ya Uchaga iligawanyika katika sehemu kubwa tatu kufuatana na pande tatu zilizomo katika sehemu ya mlima inayoweza kukaliwa na watu. Tutaona ya kuwa katika habari za zamani za kabila, wakuu wa kila sehemu hizi walipigana wao kwa wao, lakini hapana aliyeweza kuruka sana mpaka wa sehemu yake ya nchi. Baadaye walipokuwa wakuu wenye nguvu nyingi, pengine wengine hujiunga pamoja, na kupigana na sehemu moja au mbili nyingine. Basi yafaa tukumbuke majina haya: Kiboo, Vunjo na Rombo. Rombo ina sehemu tatu, ndizo Chimbili, Mkulya na Useri.

2.jpg
 
ASILI YA UMANGI KATIKA KILIMANJARO YA MAGHARIBI.​

SASA tuangalie asili ya utawala wa Wachaga tangu mwanzo.


SHIRA AU KIBONGOTO.​

Watu wa asili wa Shira wote ni Wamasai. Isipokuwa kwa wakati mfupi ambao tutasoma habari zake baadaye; hawakuwa na mkuu, na Shira ikawa siku zote sehemu ya milki ya utawala wa Machame. Wengine wa Wamasai hao walikaa pia katika Ngumi ambayo ni sehemu ya Machame, ingawa mara kwa mara walishirikiana na Wamasai wa Shira, na mara nyingi waliwaasi wakuu wa Machame. Waliokuja baada yao ni watu wa ukoo wa Mtui waliokimbia kutoka Marangu katika vita vya Mmoii na Marasha. Tutasikia habari zao baadaye.

Baada ya hao ulifuata ukoo wa wakuu wa sasa wa Machame. Walitoka Ushambala makundi makundi kwa sababu ya kushindwa vitani; mkubwa wao ni Nyare. Njiani, Nro nduguye aliachana naye akashika njia kwenda Meru. Lakini Nyare naye alisogea polepole toka nyandani mpaka akaenda kukaa katika Sujenyi, ndiko alikofia. Machame mwanawe alipigana na Watarimba waliokuwa wengi sana, akawafukuza mpaka nyandani, nao wakatawanyika wakafanya makao mahali mbali mbali. Na wana wa Uroki mwana wake wa kwanza wakafanya vile vile, na kwa hivi nchi nzima ilijaa watu wa ukoo huo. Mtoto wa Uroki jina lake Sawoe aliuvuka mto Kikofu akafanya maskani yake Wari anakokaa mkuu wa Machame hata hii leo.

Sawoe alirithiwa utawala na Talondo mwanawe, na yeye alirithiwa na Tuwari mwanawe mkubwa. Baadaye Kimaro mwana wa kwanza wa Tuwari akarithi.

Kila mzee wa jamaa katika sehemu nyingi za nchi inayoitwa sasa Machame, alihesabiwa kuwa mkuu wa mahali au mji wake, lakini hawakuwa na nguvu zaidi ya ile ya uzee juu ya jamaa zao. Kimaro ndiye wa kwanza aliyeanza kuhukumu watu na kuleta amani katika pande zile, kwa hiyo akawa mkubwa halisi. Tena watu walimtii Ntemi mwanawe pia, lakini mara Ntemi aliposhika utawala uasi ukaanza, maana Yansanya ambaye halafu aliusimamisha utawala wa Kibosho, alijibagua akajifanya mtawala wa peke yake wa Nwaa ili makusudi apate kumnyang'anya Ntemi ng'ombe zake alioweka kwake. Ntemi akapigana naye, na Yansanya akakimbilia Kibosho.

Katika siku alizotawala Ntemi watu wengi walitoka pande nyingine wakaja kukaa Machame, maana wakati huo nchi ilianza kuwa na mali, na watu walianza kupata ng'ombe wengi kwa kubadili asali kwa mafahali ya Kimasai, ambao Ntemi aliwabadili kwa mitamba ya ng'ombe.

Baada ya kufa Ntemi, Kombe wa kwanza mwanawe alishika mahali pake, yeye naye akafuatwa na Kiwaria mwanawe. Wakati huo ndio mwanzo wa fitina baina ya jamaa ya mkuu huyu. Nkulema nduguye akapatamani mahali pake, na tamaa yake ilizidi kwa vile Kiwaria asivyokuwa na mwana wa kumrithisha utawala. Wakati huu Kiwaria alikuwa na binti tu, lakini baadaye alijaliwa kupata wana wawili wanaume Kombe na Urere. Aliwapeleka Meru wakakae na jamaa zake wazao wa Uro ndugu yake Nyare aliyetoka Ushambala. Hata walipokua, akawarudisha kwa siri, wakamwua Nkulema ili kumlinda baba yao.

Kombe wa pili akaurithi utawala wa baba yake, akawa jasiri sana, sifa yake ikaenea mbali hata watu wa Kombe wakajiweka chini yake, na nchi iliyokaliwa kwanza na Muungo mwana wa Sawoe, ikawa chini ya utawala wa wakuu wa Machame mpaka siku za Sina.

Baadaye Kombe aliinyang'anya nchi ya Narumu waliyokuwa wakikaa Wakamba, Wandorobo na Wamachame, akamweka wakili wake jina lake Kifumu chini yake. Huyu Kifumu alirithiwa na mwanawe wakati wa utawala wa Rengwa mwana wa Kombe. Habari zake zitasimuliwa katika sura ifuatayo.



KIBOSHO.​

Waliotangulia kufika Kibosho ni watu wa ukoo wa Wammari nao ni wazao wa Wakikuyu. Walipokuja Kilimanjaro, kwanza walikaa Useri. Mmari na mkewe Nanyinda yasemekana ya kuwa ndio walioleta miche ya migomba na kuipanda huko Kibosho. Wengine waliofika Kibosho baada yao walipata miche ya migomba kwao, ndiyo sababu kwa Kichaga ndizi huitwa Nyinda, yaani kwa ukumbusho wa jina la Nanyinda mkewe Mmari; hii ni hadithi tu wala haijulikani kama ni kweli. Tangu siku za Mmari hata hii leo, watu huhesabu vizazi kumi na viwili vimepita. Wengine waliokuja Kibosho ni Wamsele ukoo wa Wakamba, Wambishi, na ukoo mmoja wa Kimasai uitwao Wangila, na Wamreo nao ni Wakamba, na Wakyah ukoo wa Konono walio Wamasai. Kulaya alimfuata Mmari. Imesimuliwa kuwa Ndumalya mjukuu wa Kulaya alimwomba Mungu amjalie mtoto mwanamume. Mungu akamjalia, akazaa mwana, ikawa wakampa jina Mono Ruwa, yaani mtoto wa Mungu. Ikawa katika siku za Mono Ruwa palitokea njaa kubwa, akawaambia watu washirikiane katika vyakula, maana yake mtu asiseme chakula fulani ni chake peke yake, ila kila mtu awe na haki ya kula chakula cha mwenziwe kwa kubadilishana. Jambo hili liliwashangaza watu sana, wakanung'unika na kusema haiwezekani. Hapo basi Mono Ruwa akafungua soko moja ambalo ndilo la kwanza, na huko watu waliweza kubadilishana chakula, na hivyo kila mtu alikula cha mwenziwe. Wakulaya hawa wanadhaniwa kuwa ndio walioileta mbegu ya mbeke katika nchi ya Kibosho, na hata hivi leo ni desturi ya ukoo huu kutangulia kupanda mbeke, ndipo koo nyingine wapande. Mwisho, ukoo wa Orio ulifuata, nao ndio ukoo wa wakuu wa Kibosho, Orio wa kwanza alikuwa Mmasai wa ukoo wa Oruwaya. Wamasai wa Segirari na Laiseri waliwashinda Wauruwaya wakawafukuzia Arusha Chini, na kutoka huko wakakimbilia Chala na kupigana na Wagweno wa Upare. Lakini walishambuliwa tena na Wamasai, wakakimbilia katika nyanda chini ya Ushambala waliko hata leo, na sasa wanaitwa Walumbwa. Katika maskani yao mpya, palizuka fitina kati yao, na kwa sababu hiyo, mmoja wao aitwaye Msanya alikimbia pamoja na Yansanya mwanawe kwendea Meru. Njiani Msanya akafa, na Yansanya alioa mke wa Kimeru akazaa naye mwana jina lake Orio wa pili. Baada ya kupita siku, Wameru walimwonea wivu Yansanya na mali yake, naye kwa kuwa aliogopa, alikimbilia Shira akamwacha Orio huko Meru, wakaako wazao wake mpaka leo. Baada ya kupita miaka michache Yansanya alihamia Wari katika Machame na baadaye tena akahamia Narumo akakaa pamoja na Wamanushi. Kisha alihama tena akaenda kukaa Uchau katika Kibosho. Kila alipokaa aliacha mwana, na wazao wake wanajulikana mpaka siku hizi.

Yansanya alikuwa na mali nyingi na rafiki wengi aliowapata kwa kuwakirimia ng'ombe katika karamu. Hasa alifanya urafiki na Mbishi wa ukoo maarufu wa Wambishi, na mapatano waliyoyafanya yana nguvu hata hivi leo, maana mkuu wa Wambishi huwapa sehemu ya nyama iliyo mali yake mwenyewe na maziwa; kwa sababu kwa desturi ya Wambishi, mkuu hatoi nchi kwa watu wasio Wambishi.

Baada ya kufariki Yansanya, Orio mwanawe aliushika utawala wake, akaiongeza milki yake kwa kupatana na koo nyingi. Wengine walikataa kupatana naye, lakini pamoja na hayo, wakati huo alikuwa na wafuasi wengi. Akawafundisha askari zake na kuwavisha kama Wamasai, na kwa msaada wao aliweza kuwatiisha Wakimale baada ya kumwua mkubwa wao.

Katika nyakati za Orio, nchi ya Kibosho au Kiwoso ilipata kuitwa hivyo kwa sababu hii: Katika miaka hiyo, palitokea njaa kubwa katika nchi nzima, na watu wengi walikimbilia pande nyingine. Mtu mmoja wa Useri jina lake Mambonda alisafiri kwenda Ushambala na huko akawakuta Waumbo. Waumbo walikuwa watu wakali kabisa wasiolima wala kujijengea nyumba za kukaa; akawahadithia habari za utajiri wa Wachaga, na kuwakaribisha waandamane naye mpaka Kilimanjaro. Waumbo wakakubali, wakatoka na wake zao na watoto wao wengi wengi kama walivyozoea. Tutazisikia tena habari za Waumbo tusomapo habari za Vunjo. Husemwa walikuja wengi sana wakaendea upande wa magharibi kando kando ya mlima, na hata mwishowe wasionekane tena. Kila walipotua walikusanya chungu chungu za mawe, ambazo huonekana hata leo katika Kilimanjaro.

Kwanza watu waliwaogopa sana kwa wingi wao, maana hawakudhani kuwa waliandamana na wake zao na watoto, walifikiri wote ni wanaume, na bila shaka walionekana kuwa wengi, tena wasioweza kushindika wakipigana nao; lakini kwa kweli sivyo ilivyokuwa. Orio mwenyewe aliogopa kukutana nao, ikawa akawaambia askari zake hodari wawili Kisoke na Kiwoso wawazuie wasiingie. Basi Kiwoso akagundua kuwa wingi wa adui zao ni wanawake na watoto, na baada ya kujua hivi, aliwakusanya wanaume wa Kibosho wawezao kupigana, akawaongoza wapigane na Waumbo. Aliwashinda na kuwaua wengi mno hata jeshi lao zima likaangamia kabisa. Kwa tendo hilo, watu walimsifu Kiwoso sana, hata ikawa wakamwita "baba wa nchi "; na tangu siku hiyo nchi imeitwa Kiwoso kwa ukumbusho wa jina lake, lakini sasa Wazungu wanaiita Kibosho.

Orio alipokuwa mzee, alimwachia Kiletua mwanawe kazi ya utawala. Kinyanyukie mwanawe mdogo aliyeitwa baadaye Iringo, alisafiri kwenda Ushambala, na huko akajifunza uaskari, kisha akarudi na jeshi la Washambala akawashambulia watu wa Mzinga waliokuwa adui za Orio, wakawanyang'anya ng'ombe zao wote. Imesimuliwa ya kuwa alipofika mto Karanga aliukuta umejaa, basi akayapiga maji kwa fimbo yake, na maji yakatengana, na yeye na watu wake wakaweza kuvuka, akakutana na baba yake. Hata hivi leo lipo jiwe lisemwalo kuwa aliliweka kando ya mto kwa ukumbusho wa tendo hilo. Alimgawia baba yake makundi ya ng'ombe na mbuzi ya Mzinga, na Washambala wakapewa mateka ya wanawake, maana hakuna walichokitaka zaidi ya hicho. Basi Wakibosho walishangazwa na Iringo hata ikawa wakamfanya awe mkuu mahali ра Kiletua. Kiletua hakupendeza kwa sababu kwanza ni bahili, tena mpumbavu. Lakini Iringo alikuwa shujaa sana tena mtu wa vita, naye ndiye aliyeanzisha vita juu ya Wamachame vilivyoendelea mpaka Wazungu kufika katika pande zile. Hakuthubutu kuwashambulia Wamachame peke yake, na kwa hivi, kwanza alikwenda Ushambala akarudi na jeshi kubwa la Washambala, wakawaingilia Wamachame na kukamata ng'ombe zao wengi. Pamoja na hayo aliwaua watoto wanamume aliowakuta jandoni; na ingawa tendo kama hilo ni ovu kabisa, alijifanya kama hakukosa, akasema ya kuwa alijilipiza kisasi cha Yansanya aliyeuliwa wanawe Machame.

Baadaye Kibosho ilishambuliwa na Wamasai wa Segirari. Iringo alipokutana nao walikuwa wamekwisha ishinda Kindi, lakini pamoja na hayo aliwafukuzia mbali. Katika vita hivyo alijeruhiwa sana, na kabla ya kupita muda mrefu, akafa. Yasemekana ya kuwa wanawe waliokuwa wakimfitini, walimtia sumu katika jeraha na kwa njia hiyo wakamwua.

Baada ya kufa kwake watoto wake wakaanza kugombana wao kwa wao, kila mtu akitaka yeye awe mkuu. Mwishowe wazee walimchagua Okure mwana wa pili wa Iringo awe mkuu wao. Okure hakutawala sana, na hata Malamisha nduguye aliyeurithi ukuu, alitawala kwa miaka mitano tu. Wote wawili waliuawa kwa sumu, na yasadikiwa ya kuwa sumu hiyo walipewa na wake zao wanawake wa Kiuru. Jambo hili liliondokesha uadui kati ya watu wa Kibosho na wa Uru. Hapo basi palisalia mrithi mmoja ambaye ni mwenye haki ya utawala; jina lake Kimboko mwana mdogo wa Malamisha. Kwa kuwa wakati huo alikuwa mtoto bado, asiyeweza kuendesha ufalme, jamaa yake mmoja jina lake Mirengi alimshikia ufalme. Tumeambiwa ya kuwa aliogopa yule mtoto asije akadhurika, na kwa hivi akawa akimvisha nguo za kike mpaka alipokuwa mkubwa wa kuweza kutawala mwenyewe. Kimboko alijaliwa kutawala tangu ujana wake mpaka uzeeni, na kwa kazi yake nchi yake na watu wake walifanikiwa sana. Pamoja na hayo yote, watu hawakumpenda, wakazidi kumchukia kwa sababu aliipoteza nchi ya Kindi iliyokuwa sehemu ya nchi ya Kibosho mpaka wakati huo.

Watu wa kwanza waliofika Kindi walikuwa wa koo tatu, Wamwacha waliokuja kutoka Vunjo, Wakisoke na Wakwai. Hawa wa mwisho walitokea pande za Arusha Chini. Iringo, mkuu wa Kibosho alimchukua binti yake akamwoza Kwai ambaye ni msingi wa ukoo wake, na Kimboko alimfanya Nsilo mwanawe Iringo kuwa mkubwa wa Kindi akamruhusu aitwae kodi yote ya Kindi iliyokuwa kwa kweli haki yake. Baada ya muda kupita Nsilo akawa mtawala wa peke yake, akajiita mkuu wa Kindi; na kwa vile Wakindi walivyokuwa watu wa vita, kisha mashujaa, Kimboko hakuthubutu kumtiisha Nsilo. Lakini juu ya hayo ingalifaa zaidi kama Wakindi wangaliendelea kuwa raia za wakubwa wa Kibosho, maana kujitenga kwao hakukuleta lo lote ila vita visivyokwisha na mafukuzo ambayo mwisho wake watu walikuwa hawana budi kuhamahama huko na huku, kama tutakavyoona halafu. Kimboko alipokuwa mzee alitaabishwa mno na ushindani wa wanawe, lakini mwishowe alimtangazia mwanawe aliyekuwa kipenzi chake awe mkubwa mahali pake. Mambo haya hayakuyatuliza mashindano na magomvi yao. Kwanza mama wa mwanawe mwingine jina lake Oshiri alimpa sumu Kimboko, na alipokufa, kila mwana alijiona ndiye mrithi utawala, na kwa hivi nchi nzima ikaingia vita. Zaidi ya haya nduguze Oshiri walipata msaada kwa Warsingi mkuu wa Uru, maana alijiona amezungukwa na maadui. Iwere naye akaona ni lazima amwondoe Oshiri mshindi wake, basi ikawa akamshawishi mmoja wa wafuasi wake, akaenda akamwua. Hapo basi wafuasi wa Oshiri wakamfanya Makichami mama yake Oshiri awe mkubwa wao, naye ingawa alikuwa ni mwanamke tu, lakini kwa jinsi alivyokuwa shujaa aliliongoza jeshi lake mwenyewe kwenda kupigana na Iwere; na kwa msaada wa Warsingi, Iwere alishindwa. Katika mapigano hayo Iwere alipata habari ya kuwa Wauru walishinda kwa sababu walitumia mishale na pindi, naye vile vile aliwapa askari zake mishale na pindi na baadaye alipigana na Wauru, akawashinda na kuwafukuza, hata aliwahi kuingia Uru. Lakini alipokuwa akishughulika hivi na vita, alishikwa na ndui zilizokuwa zimeenea katika nchi nzima, akafa. Kashenge Ringwa mwanawe Iwere akaurithi utawala. Tutasoma habari zaidi za Kibosho katika sura ifuatayo.



URU​

Wageni wa kwanza waliokuja kukaa Uru walikuwa Wakiwaru ukoo wa Wandorobo, na ukoo wa Kikamba ulioitwa Wamcharo wakaja wakakaa karibu nao, lakini Wamcharo sasa karibu wote wamekwisha. Pande za chini zaidi kuelekea nchi za uwanda, walikaa Watemba. Asili ya ukoo wa Watemba haijulikani, ila hudhaniwa kuwa ni wazao wa Teemba aliyeshindwa na Mmori wa Mshiri katika nchi ya Marangu. Watemba walikaa kwa urafiki sana na Wakiwaru. Kadhalika, asili ya hawa Wakiwaru haijulikani. Kiwaru alikuwa mzee wa awali katika nchi ya Uru, na ukoo wa watu hawa sasa huweza kuhesabiwa vizazi 18. Katika siku za kizazi cha tano cha watu hao, Mmasai mmoja jina lake Mkuruo mwana wa Akwe alikuja akakaa pamoja nao.

Watu wa Uru siku hizo walikuwa maskini sana wala hawakuwa na ng'ombe, lakini Mkuruo alikuwa na ng'ombe wengi sana, akapendwa sana na watu kwa sababu aliwagawia nyama ya kula, tena aliwaazimia ng'ombe majike wawaweke katika nyumba zao ili wajipatie maziwa. Watu wale waliona shukrani, na kwa hivi walimjengea Mkuruo nyumba na kumlimia mashamba yake. Tena walimfanya kuwa mwamuzi wao, na kwa kweli alikuwa mkuu wa Uru.

Baada ya Mkuruo, Amuula mwanawe akatawala. Jamaa zake wengi wa Kimasai walifika Uru wakafanya biashara ya kubadilisha ng'ombe kwa asali na ndizi, kwa hivyo watu waliendelea sana, wakapata ng'ombe wengi. Wakuu wengine watatu waliofuata baada yake, ni Amoni, Anuda na Aruma, na wote walikuwa watu wa amani waliopendwa na watu, tena walikuwa watawala wenye haki, na kwa hivi wakati huo nchi ya Uru ilifanikiwa na kutulia. Lakini mpaka wakati huo wazao wa Mkuruo hawakukubaliwa kuwa ni Wakuu, na wakuu wa koo za Wakiwaru, Waruinga na Wangowi walikataa kabisa kutawaliwa nao. Swati mwana wa Aruma alifuata namna ya baba zake, naye hakujaribu kuwatiisha, ila alifanya mapatano nao wamsaidie kuilinda nchi. Alifanya hivi kwa sababu Wamasai walikuwa wakianza kufanya udhia, na Swati hakutaka vita; basi kwa mapatano hayo waliweza kuwapiga Wamasai kwa umoja.

Waumbo waliotoka Ushambala wakaja Uru kama walivyokuja mahali pengine, wakaitwaa nchi. Haya yalitokea katika siku za uzee wake Swati, kwa hivi tunaweza kusema ya kwamba aliishi katika siku za Talondo wa Machame, Ngowi na Riwa wa Marangu na Marawite wa Mamba.

Siku moja Washambala walishtushwa ghafala katika kambi yao na askari watatu mashuhuri majina yao Kibura, Mamkoche na Singila pamoja na wafuasi wao wachache, na baada ya kuwaua Washambala wengi, hofu kuu iliwashika waliosalia, wakakimbia. Miaka michache baada ya tukio hili, Swati akafa, na Mshanga mwanawe alirithi mahali pake. Utawala wake ulianza na fujofujo na bahati mbaya iliyofuliza katika nchi ya Uru mpaka kufika siku za utawala wa Kizungu. Watu wale watatu hodari waliowafukuza Washambala ndio waliokuwa washauri wakubwa wa Mshanga. Kwa shauri lao, Mshanga akashika kazi ya kuzitiisha kwa nguvu koo zile zilizokuwa bado zinajitegemea wenyewe, na tendo lake la kwanza lilikuwa la hila mbaya, akawaua Wakiwaru. Kwa sababu ya hila mbaya hiyo, watu wa koo nyingine walivunja agano walilokuwa wamefanyiana na Swati, kisha vita vya siku nyingi vikafuata. Lakini katika vita hivyo Mshanga aliwashinda. Baada ya hivi Mshanga aliugua na kwa hivi hakuweza tena kuitawala nchi, na kwa kuwa Maimbi mwanawe alikuwa mtoto bado, Ngoolyi ndugu yake akamshikia utawala. Baada ya siku kupita, Ngoolyi alifanya shauri la kumwua Maimbi ili ajipatie utawala kwa yeye mwenyewe na wanawe, lakini mama yake Maimbi na rafiki zake wakaling'amua shauri hili baya, wakampeleka mtoto kwa mkuu Mafuluke wa Mamba, ambaye alikaa na Mshanga kwa urafiki. Halafu tena Mafuluke akampaleka Maimbi kukaa Ugweno, maana alihofia ya kwamba vijana wa Mamba watamdhuru kwa sababu walimwonea wivu kwa uhodari wake wa kupiga upindi. Baadaye, Maimbi alipopata umri wa kutosha kuurithi utawala, wafuasi wake walimrudisha, na Ngoolyi akauawa.

Wakati huo Wamasai walikuja Uru mara nyingi wakajifanya kuwa wanataka kufanya biashara, ila kwa yakini walikuja kupeleleza, maana waliazimu kufanya vita na nchi ya Uru kwa sababu ilikuwa na ng'ombe wengi. Haikuchukua muda mrefu, wakaja wakashambulia kwa ghafala, wakakamata mateka mengi, lakini Maimbi alikusanya watu wake upesi, wakawafuatia Wamasai kwenye mto Kikaju, na huko baada ya vita vikali Wamasai walikimbizwa, na watu wa Uru walipata ng'ombe zao tena. Mara baada ya siku chache, Wamasai walirudi wengi sana wakatwaa mateka tena, lakini walishindwa tena katika nchi za tambarare, na safari hii, watu wa Maimbi licha ya kuwapata ng'ombe zao walioibiwa, walikamata ng'ombe wengi wa Wamasai na wanawake wao wengi pia.

Sasa Maimbi alijua ya kwamba Wamasai hawataridhika wala kuacha kushambulia tena, akafanya mahandaki ya kuilinda nchi yake. Basi, baada ya muda kupita Wamasai walirudi kwa nguvu nyingi sana, na kwa kuwa madaraja yaliyovuka mahandaki na milango yake ilikuwa wazi, Wamasai walijiingiza ndani ya nchi ya Uru. Mara walipoingia, Maimbi akaamuru milango ifungwe na madaraja yabomolewe, na kwa hivi Wamasai hawakuweza kurudi nyuma. Watu wa Maimbi waliokuwa na pindi waliwekwa nyuma ya Wamasai, na wengine waliokuwa na mikuki wakapigana nao kwa mbele. Basi, vita vikali vikashikana, na wale watu wenye pindi wakawatupia Wamasai mishale kwa nyuma yao na kwa hivi ngao zao hazikufaa kitu. Hivi machinjo makuu yaliandama, na adui wachache tu walinusurika. Zaidi ya hayo, Maimbi alishuka katika kambi za Wamasai akazichoma moto, akachukua ng'ombe wengi pamoja na wanawake na watoto. Hii ndiyo mara ya mwisho Wamasai kujaribu kumshambulia Maimbi. Basi, Wamasai wakaja wakaomba amani, wakasihi warudishiwe wanawake na watoto wao, na Maimbi alikubali. Baadaye Wauru walikaa kwa amani na Wamasai kwa miaka mingi.

Sasa Maimbi alikuwa tajiri sana na hodari, kisha akaogopwa kotekote, akaanza kuwa mtawala dhalimu na baba katili. Husemwa ya kuwa mchawi mmoja alikuja kutoka Ugweno akamwonya ajihadhari juu ya watu walio wekundu au weupe kidogo, na baadaye Maimbi alitaka kujiondolea raia wote wa namna hiyo. Kwa hiyo alianza kumwua kila mtu aliyekuwa mng'avu hata na watoto wake mwenyewe hakuwahurumia kwa sababu walikuwa weupe kidogo kama watoto wote walivyo wanapozaliwa. Kwa sababu hiyo angalimwua mwanawe Warsingi pia wakati alipozaliwa, lakini alikuwa amewaua watoto wengine wa mama yake Warsingi, na kwa hivi alimwacha aishi, lakini alimrudisha mtoto pamoja na mama yake kwa baba yake, na huko walikaa kwa kujifichaficha miaka mingi.

Maimbi aliyajutia sana matendo haya katika uzee wake, maana amewaua watoto wake wote, naye amesalia pasipo mrithi. Lakini mkewe mkubwa aliyajua haya, basi akamfunulia ya kwamba mtoto wake Warsingi yu hai, wala hajafa bado kama alivyopata kuambiwa. Basi, Maimbi alimkiri Warsingi kuwa ni mwanawe, akatangaza kuwa ni mrithi wake. Lakini kabla ya kumpa kijana utawala, alimjaribu ili apate kujua kama amestahili kuwa mtawala wa watu wake. Ikawa siku moja usiku, alipeleka ujumbe kwa Warsingi ya kwamba Wamasai wamo njiani wanakuja kuwashambulia. Mara ile Warsingi alipiga pembe lake kuwaita askari zake, na wachache walipokwisha kuja akawaongoza uwandani kuonana na adui. Mara habari ilienea ya kuwa kijana mkuu wao amewaendea adui, na papo hapo watu wote katika nchi wakaenda kujiunga pamoja naye, na kwa hivi Warsingi hakuchelewa kupata wafuasi wengi. Baadaye kidogo akarudi nao kwa Maimbi, akatoa habari ya kwamba hawakuwaona adui kamwe, na baba yake alipoliona jeshi lililokusanyika kumzunguka yule kijana, akamwita kwa jina la mkuu wa nchi, na papo hapo akasema ya kwamba amekwisha kuitwaa nchi, akamtangaza awe mtawala.

Habari za utawala wa Warsingi zitasimuliwa baadaye katika habari za wakuu wa Kichaga waliopigana na jirani zao.



Мвокомо.​

Watu wa kwanza waliokaa katika nchi ya Mbokomo ni wale wanaoitwa sasa Wakahe, na asili yao ni Wandorobo. Baadaye wakaja baadhi ya Wataita chini ya mkubwa wao Kyelea, na baada ya hawa watu toka nchi mbali mbali wakaja wakaungana na Wataita wakawafukuza Wakahe.

Asili ya ukoo wa Wamrima ambao ndio ukoo wa Mkuu, haijulikani, lakini jina hili la Wamrima hudhaniwa kutokana na jina la watu wanaokaa pwani, maana hata sasa huitwa pengine watu wa Mrima. Iko hadithi inayosimulia ya kwamba walikuwa watu weupe wenye asili ya Kizungu, na ya kwamba walikuwa na vitabu vya dini iliyofunuliwa kwao. Zamani watu hao walikaa Pangani, wakahamia toka huko mpaka nchi ya Wadigo kaskazini ya Tanga. Lakini walifukuzwa kutoka nchi zote mbili kwa sababu walifundisha watu wasiwaue wazee wao, maana ndiyo iliyokuwa desturi ya watu waliokaa pande za pwani siku hizo. Walipohamia Mombasa, huko nako kadhalika waliwakuta Wadigo wanaimiliki nchi, basi walisafiri kwenda Utaita. Watu wengine husema ya kuwa walizidi kusafiri kwendea pande za kaskazini katika nchi ya pwani mpaka Pokomo, na hudhaniwa ya kwamba jina hili Mbokomo latokana na jina hilo Pokomo, iliyo nchi moja kando ya mto Tana katika nchi ya Kenya. Wataita waliwapokea vizuri, na husemwa ya kuwa watu walikwenda kwa hiari yao kwenye kanisa lao ambalo lilikuwa na kengele kubwa, na huko wakafundishwa dini yao. Lakini baada ya muda kidogo njaa ikaingia katika nchi na kwa hiyo Wataita walisema ni Wamrima ndio walioleta njaa, na hasa waliilaumu kengele yao. Basi hapo Wamrima walihama wakaenda hata Serengali, na mkubwa wao alikuwa Owaa. Kutoka huko wakaendelea mpaka Tela katika mlima. Huko pia wakajenga kanisa lao wakaigongagonga kengele yao, na watu waliokuwa jirani zao wakaiogopa wala hapakuwa hata mmoja aliyethubutu kwenda karibu nao. Kutoka Tela sehemu moja iliondoka ikaenda Moshi, na sehemu nyingine ikaenda Machame.

Mwana wa Owaa aliitwa Riringa, na kwa sababu ya ugomvi alihamia Mbokomo. Iko hadithi inayosimulia ya kuwa ile kengele waliyoileta ilitundikwa katika mvule mkubwa ambao chini yake Owaa alizikwa. Kidogo kidogo wazao wake waliacha dini yao wakaisahau ile kengele hata ikaanguka, nayo husemwa ya kuwa ingalipo ndani ya ardhi chini ya mti ule ule. Lakini Riringa alipohama alichukua kengele ya namna ile ile, ila ndogo zaidi pamoja naye.

Mrima mwana wa Riringa akawa na uadui na watu wa Tela, na uadui huo haujasahauliwa mpaka leo hivi. Katika wakati wa mwanawe Kanyaka, Washambala au Waumbo waliwasili Mbokomo kama walivyofika katika nchi zote za Kilimanjaro. Husemwa ya kuwa Mrima ni wa mwisho wa ukoo wake uliyeshika dini yao ya asili.

Lyamrufu mwana wa Mrima alifanya vita juu ya watu wa Tela pamoja na koo nyingine za Mbokomo, lakini alishindwa. Tena alishirikiana na Wataita kuwafukuza Wakahe.

Lyamrufu alimwoa binti wa mkuu Marawite wa Mamba, akazaa naye mwana aliyemwita Marawite kwa jina la mkwewe. Alipokufa Lyamrufu, mwanawe mkubwa Msaule aliyezaliwa na mkewe mdogo alidai kwa nguvu awe mtawala, lakini mama yake Marawite alipata msaada kwa mkuu Maimbi wa Uru, na Msaule akafukuzwa. Wakati huo, Uru ilishambuliwa na Wamasai, lakini walishindwa, kisha walijaribu kuishambulia nchi ya Mbokomo, lakini na huko kadhalika walishindwa.

Marawite alirithiwa na Mwasha mwanawe wa pili ambaye katika siku zake, Mbokomo ilitekwa na Warsingi wa Uru.

Mwasha alirithiwa na Lowiho mwanawe mkubwa.



MOSHI.​

Nchi inayoitwa Moshi sasa imepata kuitwa jina hili kwa sababu ya mambo haya yanayofuata. Huko Moshi kuna kilima kiitwacho Kilyarogho, na juu ya kilele chake, zamani sana, mtu aliyeitwa Kimochi alianzisha soko likaitwa soko la Kimochi. Soko hilo la Kimochi liliangaliwa vizuri sana, na watu wote walilipenda kwa sababu ya utaratibu wake. Basi, ikawa walipokuwa wakienda katika soko hilo, husema ya kwamba wanakwenda kwenye soko la Kimochi, na jina lake lilikumbukwa sana kwa siku nyingi baadaye. Ikawa mlima wote ulipata kuitwa kwa jina hili la Mochi.

Wakuu wa Moshi walitoka Ushambala. Wakati mmoja wa njaa kuu katika nchi ya Ushambala, mtu mmoja jina lake Makilo alikwenda kuwinda uwandani pamoja na wenzake wachache, na baada ya kukaa huko Arusha Chini kwa muda, wakahamia Kahe. Makilo akafa huko. Rasiyo mwanawe alikuwa mdogo sana alipokufa Makilo, basi, mama yake aliyeitwa Makitoonyo akawa mkubwa wao. Wakati huo walikutana na Washambala wengine wakaendelea pamoja mpaka mlima Moshi, wakakaa mahali palipoitwa Kitoonyo kwa jina la mama yake Rasiyo.

Lyamalyo mwana wa Rasiyo akafanya urafiki na watu wa koo nyingine. Alikuwa kiongozi hodari na wa kwanza kupata sifa katika ukoo wake. Katika mambo mengine aliyoyafanya, mojawapo ni kufanya mfereji wa Sairo. Tena alikuwa mtu wa kwanza wa ukoo wake kupanda migomba na kufuga ng'ombe. Lyamalyo alikuwa na wana wanne: Tuu, Makilo, Kaale na Iringo. Tuu alikuwa mwana wa kwanza, naye ndiye aliyerithi ukuu, lakini alikuwa mzembe wala hakuangalia mambo yaliyomhusu, na baada ya wakati mfupi watu walimchagua Iringo, maana ndiye aliyewapendeza watu. Iko hadithi inayosimulia ya kuwa Iringo alikuwa na baragumu au pembe zuri ambalo Tuu alitaka kulinunua, lakini Iringo alimdanganya, akisema kwamba atalibadilisha kwa konzi moja ya ardhi. Basi, ikawa watu walipomwona Tuu akimpa Iringo konzi ile ya ardhi wakadhani anamtolea nchi yote, na kwa hivi walimfanya Iringo kuwa mkuu wao. Lakini Makilo hakuridhika kwa jambo hili, maana alidhani kwamba ikiwa Tuu hataki ukuu yeye mwenyewe, kwa nini kumpa Iringo aliye mdogo wao?

Basi, Makilo alikwenda Ushambala na alipokwisha kukaa huko kwa miaka kadhawakadha, alirudi na jeshi la Washambala, ndio Waumbo wale walioshambulia nchi zote za Kilimanjaro, wakaacha ukumbusho uliopo hata leo hivi, unaoitwa "Mawe ya Waumbo." Iringo hakujaribu kupigana nao, ila akafanya nao urafiki, na matokeo ya urafiki huo yakawa kumwacha kwa amani, ya hivyo shauri la Makilo halikumfalia kitu. Basi Makilo akarudi tena Ushambala, lakini watu walipomwona anarudi bila kufuatana na jeshi alilolichukua, walitaka kumwua, naye punde si punde akamrudia Iringo akataka masamaha, akasamehewa.

Tarimo mwana wa Iringo alikuwa wa kwanza kuusimamisha Umangi wa Moshi, na wakati huo alipoanza kutawala watu wa ukoo wa Wamola walishambuliwa na Wakimamba, wakamsihi Tarimo awasaidie. Lakini Tarimo hakuwa na nguvu za kutosha kufanya vita na Wakimamba peke yake, kwa hivi alipata msaada kutoka Ushambala, akawashinda Wakimamba akawaua wengi wengi akawafukuzia mbali nchini. Baada ya hayo, aliwashinda Wamasai walioshambulia nchi yake, na kwa hivi alipata sifa nyingi, na watu wa Tela waliokuwa wenye nguvu kupita wote katika nchi walitaka kufanya urafiki naye.

Tarimo alirithiwa na Saliko mwanawe, na katika siku zake Wauru pamoja na Wamasai waliiudhi sana nchi yake, mpaka yeye na watu wake walifanya mahandaki ya kuilinda nchi, na kwa hivyo waliwapinga adui. Tena Saliko alifanya urafiki na Kombo wa Kilema aliyempa askari wengine wamsaidie, akampa na mishale aliyoipata kutoka kwa Wataita. Kwa msaada huo wa Kombo, alifanya vita na watu wa Shia na Sango, maana walikataa kujiweka chini ya utawala wake.

Sunza mwana wa Saliko aliishi katika wakati wa wakuu hawa: Horombo wa Kini, Rongoma wa Kilema, Mosha wa Kirua, Warsingi wa Uru, Kashenge wa Uru na Rengwa wa Machame. Katika siku zake njaa kubwa iliyoitwa Kisoli iliingia nchini. Sunza aliendelea na urafiki wa Kilema ulioanzishwa na baba yake, akajiweka chini ya ulinzi wa Rongoma. Tutasoma habari nyingine za Rongoma katika sura inayofuata.

Kwa siku nyingi za utawala wake, Sunza alikuwa akifanya vita juu ya mtu jina lake Baloso, aliyekuwa na jeshi kubwa akaazimu kumnyang'anya ukuu wake. Baloso alimshauri Mkuu Rengwa kwenda kuingilia nchi, naye kukosa ushujaa wa mwanamke mmoja jina lake Magole, angaliitwaa nchi. Lakini yule mwanamke Magole mwenyewe aliwaongoza watu wa Moshi vitani wakapigana na watu wa Rengwa. Zaidi ya hayo, katika mapigano, Magole alimtupia jiwe mkubwa wa watu wa Rengwa, yaani Wamachame, akamwangusha, na watu wake walipoona mkubwa wao ameangushwa waliona hofu wakakimbia.

Vita hivi vikaendeshwa na mwana wa Sunza aliyeitwa Ndekawo, naye alifanya urafiki na koo za Wammari na Wamalisa wakamsaidia juu ya Baloso. Husemwa ya kuwa kwa shauri la Wammari, Ndekawo alianza kuwaua adui zake hata kama hawakutaka vita, ingawa haikuwa desturi ya vita. Tena alifanya shauri na Molen wa Uru akashambulia usiku bila kuwaonya adui zake. Tendo hili vile vile halikuwa desturi ya vita, maana desturi ilikuwa kumwonya adui kabla ya kufanya vita naye. Basi, Baloso alishindwa akakimbilia Marangu, na baadaye alikimbilia Tela, ambayo wakati huo ilikuwa nchi yenye mkuu wa peke yake, jina lake Ndelamio. Ndelamio aliishambulia Tela kwa ajili ya Baloso, na Baloso alikimbilia Mbokomo kwa mkuu Laviho. Laviho alikataa kumtoa Baloso katika mikono ya Ndekawo, akashindwa katika vita. Basi, hapo Baloso na Laviho walikimbilia Kilema. Baada ya muda kupita, Laviho alirudi akajiweka chini ya Ndekawo, ikawa wakuu wa Moshi kuwa wakuu wa Tela na Mbokomo.

Mpaka wakati huo Moshi ilikuwa imegawanyika chini ya wakuu wengine mbali mbali, nayo ilikuwa nchi ya mwisho kuwekwa chini ya mkuu mmoja, kama ilivyokuwa nchi ya mwisho kukaliwa na watu. Tena nchi hii ikadumu kuwa ya namna ya peke yake, maana ingawa nchi nyingine zote za Wachaga zilikuwa zikivurugika kwa vita vya wakuu wakati huo, lakini Moshi ilikaa kwa amani, wala haikushughulika na nchi nyingine mpaka wakati wa Rindi aliyekuwa mjukuu wa Sunza.

Lakini baada ya mapigano hayo, Ndekawo alikuwa mkuu wa nchi yote ya Moshi, na wakati huu aliitwa Siria. Lakini mara alipopata utawala wa nchi yote, Ndetia nduguye alifanya fitina juu yake, akamwua kabla ya wakati wake kwa kumpa sumu alipokuwa akiugua.

Ndetia alikuwa amemkimbilia Mkuu Marenga wa Kirua, lakini Siria alipokufa, watu walimwita arudi Moshi. Marengo alionyesha dalili ya kubishana nao juu ya kumrudisha Ndetia, lakini watu wa Moshi walipoahidi kumpa nusu ya nchi, alimruhusu Ndetia arudi, akafanya wema na kukubali kumpa ruhusa kama wakimpa ng'ombe thelathini tu. Tendo hili la fadhili lilikuwa asili ya urafiki wa siku nyingi kati ya watu wa Moshi na watu wa Kirua, wala haukuvunjika mpaka wakati wa Rindi alipouvunja kwa kuwataabisha Wakirua.

Ndetia alimwoa mwanamke jina lake Machaki, akazaa naye mtoto jina lake Mchau, ambaye baadaye aliitwa Mandura, na baadaye tena akajulikana kwa jina la Rindi aliyejulikana sana kuwa mkuu mwenye nguvu kupita wakuu wote wa Kichaga. Ndetia alikufa kitambo kidogo baada ya kuzaliwa kwake Rindi, akarithiwa na ndugu yake Salia.

Tutasoma habari za Salia na kijana Rindi katika habari zinazofuata.
 
ASILI YA UMANGI KATIKA NCHI YA VUNJO

SURA YA TATU

ASILI YA UMANGI KATIKA NCHI YA VUNJO.


KIRUA.​

WATU wa kwanza kukaa Kirua ni wa ukoo wa Wakominja waliotoka pande za Upare. Baadhi ya Wakamba walifuata nyuma wakaenda kukaa Sumi, wakashawishi wengine wafuatane nao kushirikiana katika kufyeka mwitu. Hao waliofika mwisho waliongozwa na Mvela, naye ndiye chanzo cha ukoo wa Wakombela. Upande wa Lyambongo pia uliingiliwa na Wakamba, na baada ya kupita siku walijichagulia mtu aitwaye Mtune awe mkuu wao. Tangu kutokea haya, vizazi kumi na viwili vimepita.

Ukoo mwingine wenye maana uliokuja toka Ukamba ni Wakombela, nao ndio walioleta desturi za unyago wa ngashi, ambao siku hizi umeachwa.

Nchi ya upande wa Nduonyi ilikaliwa na watu wa koo nne za Kindorobo: Wakomgochana, Wakomombo, Wakoleti, na Wakomaacha. Hawa wote walikuja juu ya mlima kutoka pande za Ngasini, wakahama kidogo kidogo mpaka nyandani. Walipoongezeka kuwa wengi, walijichagulia mkuu wao jina lake Lyamgora. Huyu Lyamgora alijenga kijiji cha nyumba za mawe, na magofu yake yako hata leo. Yasemwa kuwa vizazi kumi na kimoja vimepita tangu mambo hayo yalipotokea.

Wakuu wa Kirua ni wa asili ya Kitaita, nao ni wa uzao wa Msanya mwindaji mkubwa aliyejia pande za Kilimanjaro. Kwanza walikaa katika kilima cha Manu, lakini Msanya wa pili, mjukuu wake Msanya, aliungana na Wakamba na Wakombela katika Lyambongo. Msanya huyu alikuwa na mwana aliyeitwa Asei ambaye hatuna habari zake, lakini Pakula mjukuu wake alikuwa maarufu, akawa wa kwanza katika ukoo wake kuiongeza nchi yao.

Pakula aliona ya kuwa Wakombela na Wakonyambo wana ng'ombe wengi sana akawaonea kijicho. Lakini aligombezwa na mama yake asiwadhuru kwa sababu babu yake alikuwa amefanya udugu nao. Basi Pakula alijaribu kuwapata ng'ombe kwa hila. Siku moja alimwongoza mama yake mpaka katika njia waliyokuwa wakipita Wakonyambo pamoja na makundi yao kwenda kuwanywesha maji kila siku, akamwambia akae kule mpaka atengeneze shauri lililotokea mjini. Yule mama alikuwa kipofu, basi alipokuwa amekaa vile, kundi kubwa la ng'ombe likapita na kwa vile asivyoona alikanyagwa na ng'ombe, akafa. Basi, hapo Pakula akadai alipwe fidia kwa kuuliwa mama yake, na kwa kuwa wale wenye ng'ombe walimwogopa, wakamlipa ng'ombe mia moja.

Tendo ovu hili lilimfanya Pakula aogopwe katika nchi nzima ya Kirua.

Kisha, alijifanya tayari kufanya vita na Wakombela, lakini mkubwa wao alimshawishi afanye suluhu, akafanya mapatano nao ya kuwa atakuwa mkuu wao, lakini kwa sharti moja, yaani atawaachia nchi yao. Mapatano hayo yalifungwa kwa desturi katili ya siku zile, yaani mtoto mwanamume na mtoto mwanamke walizikwa hai mipakani mwa nchi yao. Mapatano hayo yameshikwa mpaka leo hivi na wakuu wa Kirua.

Basi, nguvu za Pakula zikazidi, akaanza kufanya vita na wengine wa jirani zake. Kwanza alifanya vita na watu wa Maande. Watu hawa waliongozwa na mkubwa wao Kikuru nao walimzuia mpaka alipofanya hila, ndipo alipowashinda. Aliwaagiza watu wake watupe mishale yenye moto katika mapaa ya nyumba zilizokuwa katika boma la Kikuru, na kwa namna hii ziliteketea. Kikuru alipoona moto, alidhani adui wameingia boma lake na kwa hivi akaliacha, na mara ile Pakula aliingia bomani akawaua wanawake na watoto walioachwa humo. Kikuru pia aliuawa katika vita hivyo, na watu wake waliobaki walihama wakaenda mlima wa Lego, na baadaye mkuu Kombo wa Kilema aliitwaa sehemu ya mlima iliyo upande wa mashariki.

Baada ya vita hivi, Pakula alipigana na Wakolesha, akawashinda vile vile kwa hila. Alifanya kama anataka kufanya amani na Ndafu mkubwa wa Wakolesha, akayafunga mapatano naye kwa kumpa mtoto wa kike wa katika mji wake. Lakini alipatana na yule mtoto amfungulie mlango wa boma la Ndafu, na kwa hivi aliweza kulishika kwa ghafala, akamwua Ndafu. Tendo hili linakumbukwa hata leo katika Kirua, maana Wakolesha hawakubali kuwaoa wanawake wa ukoo wa mkuu.

Basi Pakula alijifanya mkubwa wa Kirua kwa kutumia hila hizi, lakini hakuwahi kuendelea kushinda, maana alikufa ghafula.

Singila mwanawe Pakula aliipata Lego upande wa Kirua kwa njia hii: Wakati huu Lego ilikuwa imeingiliwa na Wagweno, na Ngowi mkubwa wa Wakominja aliomba msaada wa Singila kuwatoa katika nchi. Singila alipofika Lego, Wagweno walikuwa wamewishaondoka, lakini aliogopa kuwa labda watarudi na kwa hivi alichimba handaki kubwa kukizunguka kilima. Kumbe, Singila alibahatisha vizuri, maana Wagweno wakarudi, na ingawa waliwahi kulifikia handaki, lakini hawakuweza kulivuka, wakauawa wengi walipokuwa wakijaribu kulivuka. Baada ya mambo haya, Singila aliweka ng'ombe wengi mikononi mwa Ngowi, naye Ngowi aliwatumia, na kwa hivi ikamlazimu aitoe nchi yake kwa Singila kulilipa deni lake.

Singila alirithiwa na Mosha mwanawe, na habari zake zitasimuliwa baadaye.

MARANGU.​

Watu wa kwanza waliokuja kukaa Marangu ni Wataita. Baada ya kufika hao, watu wengine wakaja kutoka Ugweno, Kahe na Arusha Chini. Wengi katika hao walikaa Kilema na Mamba, lakini wachache walifuata mto Kimo wakakaa Marangu. Wote walikuwa hawana mali, na wote walikaa vivi hivi mpaka wale waliokaa Mshiri walijichagulia mkuu wao jina lake Kilaweso.

Labda Kilaweso alikuwa mkuu wa Kichaga, na kwa hivi tutaona jinsi alivyopata ukuu wake, na jinsi ukuu wake ulivyokwisha. Imehadithiwa ya kuwa siku moja Kilaweso alimwua mtu mmoja aliyemwua mtu mwingine mbele ya macho yake, na kwa kuwa watu wote walikuwa wamechoka kabisa mauaji na fujofujo, walipendezwa kwa tendo lake, wakamfanya mwamuzi wao, wakamwambia awaadhibu wahalifu wote katika nchi, na malipo yake walimwahidia kumlimia mashamba na kumjengea nyumba. Huu ndio mwanzo wa desturi waliyo nayo Wachaga ya kuwalimia na kuwajengea wakubwa wao. Kilaweso alikuwa mwenye nguvu nyingi, tena shujaa kama simba, na kabla hazijapita siku nyingi aliiweka nchi ikae kwa taratibu, maana kwa mkono wake mwenyewe aliwaua wote waliokosa. Lakini Mtui mwanawe hakuwa hodari wala mwenye nguvu, na kwa hivi alikuwa hana budi aweke askari wa kutekeleza amri zake na kumlinda. Basi, askari hao lazima wapewe chakula, na chakula hicho alipata kwa watu wake. Lakini baada ya wakati kupita, watu wengi walikataa kumtolea chakula, na kwa kuwa Mtui hakuweza kuwalisha askari zake, ikawa kuwatawanya. Mara ukazuka udhia na fujo, na watu wake walitambua ya kuwa ni heri kumsaidia mkubwa wao, ikawa wakamletea chakula kwa askari zake kama kwanza.

Wakubwa wa sehemu nyingine za Marangu wakaanza kufanya vivyo hivyo kumfuatisha Mshiri, hata ikawa falme ndogo ndogo kadhawakadha zilisimamishwa. Mwanawe Mtui akapigana na wakubwa hao, hapo basi ni chanzo cha vita vita katika nchi ya Marangu, ambavyo vyadhaniwa ni vya kwanza katika nchi za Kilimanjaro. Kwanza alipigana na wakuu walio wadogo waliokaa katikati ya Mshiri na mwitu, wakawagombeza watu wa Mshiri wasipitishe ng'ombe zao katika nchi yao. Aliwashinda hao akawafukuza katika maboma yao, akawazunguka kwa muda wa siku kumi mpaka wakaomba amani, wakakubali awe mkuu wao.

Kisha, Mmori alimtaka mkuu mwingine jina lake Teemba aliyekaa mashariki ya kaskazini ya Marangu ajiweke chini ya utawala wake. Teemba aliwaua matarishi wa Mmori akampelekea ujumbe Mmori wapigane kwenye mto Mongo. Lakini Mmori alipita mwituni akamshambulia Teemba kwa nyuma. Kwa hiyo Teemba alishindwa akakimbilia Uru, na wazao wake wanakaa huko hata hivi leo.

Basi, hivyo Mmori alitawala nchi yote ya Marangu iliyo masharikini. Lakini alipokuwa akipigana na kushinda nchi, kumbe nguvu mpya ilikuwa ikija ambayo hatimaye ilimshinda.

Wakamba wengi walikuja Useri chini ya mkubwa wao Mlambaki. Kutoka huko walivuka mlima wakakaa chini ya kilima Kifinika kilicho upande wa juu wa mwitu wa Marangu, na hapo walikaa wakiwinda. Mlambaki alikufa huko, akarithiwa na mwanawe jina lake Temi; naye akatelemka mpaka mwituni. Wamba mwanawe akazidi kutelemka mpaka Makishingo. Wamba alikuwa na wana wawili, Mremi na Lyimo. Lyimo alikuwa mwindaji hodari, lakini Mremi hakuweza kuwinda hata kidogo wala hakuwaletea jamaa zake nyama, na kwa hivi mama yake alimlaani, akamwita "kite,” maana yake mbwa. Basi, hapo Mremi alifukuzwa akaenda kukaa pamoja na watu wa Makishingo, na wazao wake ni wa ukoo wa Wakomkite.

Wamba alipokufa, Lyimo mwanawe alirithi ukubwa. Hawakuwa na ng'ombe wengi, na hao waliokuwa nao walikwisha upesi, maana Lyimo alikuwa mtu mkubwa mwenye nguvu, tena alitamani sana kula nyama. Basi, Wakamba waliona makundi makubwa ya ng'ombe wanono wa Mshiri katika nchi ya chini, na Lyimo akatamani sana kuwapata, kwa hivi aliwafundisha vijana wake namna ya kutumia bunduki, ili siku moja apate kuwanyang'anya Wamshiri ng'ombe zao.

Imehadithiwa ya kuwa mama yake Lyimo alimlazimisha mwanawe apigane na Wamshiri kwa kuwasingizia watu wa Makishingo kuwa wamemdhuru, akamtaka mwanawe amlipie kisasi. Basi, Lyimo akashuka katika nchi yao akateka ng'ombe wengi, lakini hakuwapata bila kupata hasara mwenyewe, maana Wakishingo waliwaomba watu wengine waje wawasaidie, na Lyimo akawa karibu kushindwa. Lakini alipata msaada wa Wapare wakawashinda Wakishingo. Baada ya haya, vita vya siku nyingi vilizuka juu ya nchi ndogo ndogo, lakini zilishindwa moja moja hata ikawa hazina budi kujiweka chini yake. Mkuu wa nchi aitwaye Nyaki wa Kyaale aliyetaka amani alifanya udugu na Lyimo, lakini Lyimo alipoona mali ya Nyaki alijuta kwa kufanya udugu naye, akafanya hila kupata sehemu kubwa ya kundi la ng'ombe zake. Kwanza alipatana na Nyaki wapeane kijana mwanamke mmoja awatumikie kazi, na baadaye alimwomba Nyaki ampatie majani ya migomba kwa kujengea. Hapo alimwua kwa siri yule kijana aliyepewa na Nyaki, akaficha maiti katika majani yale ya migomba. Kisha, yeye na watu wake walipokwenda kwake kuyachukua matita ya majani ya migomba, akamwulizia yule kijana; na kwa kuwa hakuonekana, alimshtaki Nyaki kuwa amemwua. Nyaki alikataa, lakini mwishowe maiti ilipoonekana katika mizigo ya majani ya migomba, akasadiki kuwa watu wake ndio waliofanya hivyo, na kwa hivi aliingiwa na fedheha sana kwa kukivunja kiapo chao cha udugu, hata akawa hana neno la kufanya ila kujitoa yeye na nchi yake mikononi mwa Lyimo awafanye apendavyo. Lyimo mwenye hila akawafanya wawe chini yake, akawachukua watu wengi kwake. Wazao wa watu hao ni Wakonyaki ambao hata sasa huhesabiwa kuwa ni kama watumishi wa Wakuu wa Marangu. Wakati huo huo Lyimo aliwachukua watu wake wengine akawaweka Kyale, na wazao wao wanakaa huko mpaka siku hizi.

Nchi ya Lyimo ilikuwa imeenea sana sasa, lakini hata hivi hakutoshewa, na tena nchi yake ilikuwa imegawanyika katika sehemu mbili kwa kuwa wakuu wengine wa Marangu walikuwa wakikaa katikati ya nchi yake, na mkubwa wa wakuu hawa alikuwa Mbero wa Lyamrakana. Basi, Lyimo akafanya hila tena kumshinda mkuu huyu. Alipeleka kijana mwanamke mzuri kwa Mbero, naye Mbero alisadiki maneno ya kijana huyu ya kuwa amefukuzwa na Lyimo. Basi, siku moja Mbero na watu wake walipokuwa hawapo mjini, ila wamekwenda uwandani kukata nyasi, huyu kijana wa kike alimpelekea habari Lyimo, naye akaja na watu wake wakajificha katika nyumba za watu wa Mbero. Mbero aliporudi asishuku kitu, basi hapo Lyimo na watu wake wakawashambulia ghafala wakawaua watu wengi. Mbero na wana wawili wake waliuawa walipokuwa wakijaribu kuuvuka mto Mongo.

Basi kwa njia hiyo Lyimo alimshinda Lyamrakana. Baada ya hayo, alikusudia kuzitiisha sehemu nyingine za nchi ziitwazo Moori na Sambeti. Lakini Tilya mkuu wa Moori akajiweka kwa hiari yake chini ya Lyimo, kisha akamwua Kingaga mkuu wa Sambeti kwa amri yake Lyimo.

Basi, hapo zilisalia sehemu mbili tu za nchi zisizomkubali Lyimo kuwa mkuu wao, ndizo ya Mongi mkuu wa Samanga na ya Mmori wa Mshiri. Hawa hakuweza kuwashinda, akafa uzeeni na vita vingali vinaendelea. Iko hadithi inayosimulia ya kuwa Mmori alimwomba Mungu amsaidie, akapewa konokono aliyewahuisha wale watu wake waliouawa, mpaka mwanawe Lyimo aliyeitwa Ngowi alifaulu kumwua yule konokono, na baada ya hivi aliweza kumshinda Mshiri.

Basi, ikawa Lyimo akajifanya mkuu wa sehemu kubwa ya Marangu kwa vita visivyokwisha, kwa hila na kwa maovu. Mwanawe Ngowi alimtiisha Mwache mwanawe Mmori akamwua baada ya kujitia katika mikono yake, na watu wake waliobaki walikimbilia nchi nyingine za Uchaga, na huko huitwa Wakomtui, lakini wengine wanakaa Marangu hata leo.

Ngowi alipokuwa mzee, nchi iliingiliwa na Washambala, na yeye alifanywa mkuu, na mwanawe alimfuata. Lakini Riwa mwanawe mdogo alisalia akawazuia Washambala, na kwa hivi watu wa Marangu walimfanya mkuu wao ingawa alikuwa mwana mdogo wa Ngowi. Riwa alipata msaada wa Marawite wa Mamba, akamtiisha Mingi wa Samanga aliyekuwa wa mwisho kutawala peke yake.

Baada ya mambo haya nchi ilitulia, kukawa amani kwa muda, na Riwa aliishi mpaka akawa mzee, naye akarithiwa na Ngaramite mwanawe. Masanjuo mwana mkubwa wa Ngaramite kwa mkewe mdogo alishika makamo ya baba yake, lakini wakati huo huo, mkewe mkubwa ambaye hajazaa, alizaa mwana aliyeitwa Iwite. Ikawa Masanjuo hakupendwa na watu wake, na kwa hivi Iwite alipopata umri wa kutosha, alidai haki yake kuwa mkuu wa Marangu akamfukuza Masanjuo.

Iwite alimwonea wivu mwanawe mkubwa aliyeitwa Simba, kwa sababu alipendwa sana na watu, na kwa hivi alimwua. Basi, hapo watu wote walimchukia Iwite kwa tendo hili ovu, wala hawakushughulika naye hata kidogo, na yeye alipoona ya kuwa ametupwa, akaazimu kujiua. Kabla hajajiua alitangaza ya kuwa mwanawe Kilewo atakuwa mkuu, lakini Kilewo alikuwa mtoto bado, na kwa hivi wakati huo Marangu ilichafuka kabisa. Maana, kila mwana wa Iwite alitaka kuwa mkuu, ikawa pengine mmoja aliwahi kujifanya mkuu, kisha mwingine alimwondoa na vivi hivi, wala nchi haikutulia mpaka Kilewo alipopata umri wa kutosha kutawala. Kilewo alitawala miaka michache tu, akafa.

Baada ya kufa Kilewo, nchi ya Marangu iliingiwa na machafuko na bahati mbaya, na wakuu wenye nguvu walitokea kila upande wa Marangu, na kwa muda wa miaka mingi watu wa Marangu walionewa sana.



KILEMA.

Watu waliokuja kukaa katika nchi ya Kilema walitoka zaidi Utaita, Upare na Ukamba; na kama zilivyokuwa pande nyingine, hawakuunganika, ila walitawanyika wakakaa kila jamaa na mkuu wake, mpaka Ngowi alipotoka Marangu kama ilivyokwisha elezwa.

Huko Kilema, Ngowi alifanya urafiki na Moye ambaye babu yake alikuwa Kinyaga yule aliyeuawa kwa amri ya Lyimo. Moye alimshauri Ngowi achinje ng'ombe dume 100 aliowapata kwa Riwa wa Marangu mwanawe, na kuwafanyia karamu watu wa koo za Kilema. Basi, kwa njia hii alijifanya apendwe na watu, na kwa kuwa waliyakumbuka yale yaliyowapata watu wa Marangu walikuwa wamekwisha kujua faida ya kuwa na mkuu, wakamchagua Mremi mwanawe Ngowi awe mkuu wao. Basi, hivyo wakuu wa Marangu na wa Kilema ni wa ukoo ule mmoja.

Wakuu wote ila Mosha tu aliyetawala sehemu ya juu ya Kilema, walimkiri Mremi, na hata yeye, alitiishwa baadaye akawa chini ya Mremi. Mremi alipokuwa mzee alimwachia Ngowi mwanawe ukuu. Katika siku za Ngowi paliondokea watu wengine waliokuja kukaa Sango bondeni mwa mlima, na mkubwa wao ni Kitangu. Wageni hawa walikuwa watu wa vita kweli kweli, wakajilinda sana wasiingiliwe na Ngowi, naye hakuweza kuwashinda, maana hakutawala siku nyingi, akafa kabla ya Mremi baba yake hajafa.

Iko hadithi ya kuwa Ngowi alikufa kwa sababu alitoa siri ya kuwa Mungu amemtokea na kumwamuru atawale kwa hekima na haki. Alirithiwa utawala na Nyange mwanawe, lakini Nyange hakuwa na nguvu wala uwezo wa kutawala, na kabla siku si nyingi hazijapita, Musuo mjomba wake alimwondoa akaushika ukuu. Walakini Nyange alikimbilia Mamba, na kwa msaada wa Soka mwanawe Moye aliyekuwa rafiki ya Ngowi wa kwanza, alimwomba Mafuluke mkuu wa Mamba aje amsaidie kumfukuza Musuo. Musuo alishindwa upesi sana, akauawa vitani. Sasa Nyange akaurudia utawala, akatawala mpaka uzeeni, kisha akaiacha kazi ya utawala, na Kombo mwanawe akashika mahali pake.



MAMBA.​

Watu wa kwanza kukaa Mamba walikuwa Wakokimei ukoo wa Wandorobo toka Useri, Wakomnene waliotoka Taveta, Wakomangia na Wakomarangu ambao ni Wakamba, na Wakoteri ukoo wa Kindorobo.

Wakoteri walikuwa wahunzi na watumishi wa Wamasai waliokuja Mamba kuwafuatia Wandorobo, maana hawakuweza kuishi bila kuwa nao. Mkubwa wao aliyeitwa Mun alifanya urafiki na koo nyingine upesi, akabadili nao nyama kwa maziwa, na mwishowe alikaa huko kwa sababu alipapenda.

Nyange mwanawe Mun ni wa kwanza wa ukoo huo aliyejipatia umaarufu. Yasemwa kuwa yeye na vijana wake walizoea kucheza ngoma pamoja na Wakokimei, na kucheza michezo ya vita ya uwongo uwongo kwa kutumia majani ya migomba yasiyofumbuka bado mahali pa mikuki. Basi, siku moja Nyange alificha mikuki katika majani ya wafuasi wake, na kwa hila hii waliwaua vijana wa Wakokimei. Baada ya haya, watu hawa walihamia Rombo na huko walisimamisha utawala wa Kerio. Katika jambo hili Nyange alisaidiwa na Wakoteri, na Wakomangi wakajiweka chini yake kwa sababu walimwogopa Nyange kwa jinsi alivyowaua vijana wa Wakokimei kwa hila. Lyakimale mwanawe Nyange naye kadhalika aliendelea kufanya hila kama alivyofanya baba yake. Aliuogopa sana ukoo wa Mangi kwa sababu walikuwa hodari mno kwa pindi na mishale, basi alifanya hila kuwaua. Siku moja walipokuja ngomani kucheza, aliona kuwa hawana silaha, na mara Lyakimale na watu wake waliwashambulia kwa ghafula wakawachinjachinja. Lyakimale alimpenda sana Marawite mwanawe mkubwa, lakini Righu mwanawe wa pili alikuwa hana mapendeleo mbele ya baba yake. Basi, Righu alipoona ya kuwa hapendwi, alifanya shauri la kuutwaa utawala. Kwanza aliomba msaada kwa Ngowi wa Marangu, naye alikuwa tayari kumsaidia, lakini wakati huo alikuwa akishughulika sana katika nchi yake, akamshauri Righu angoje kwa wakati unaofaa. Lakini Righu hakuweza kusaburi, akaanza kutunga mashauri yake pekee, hata mwishowe alimwua Lyakimale baba yake. Ndipo alipokimbilia Marangu, lakini Ngowi hakumpokea, basi ikawa hana budi kukimbilia Samanga. Ndipo Marawite na Ngowi walipatana pamoja, wakaenda wakaipiga Samanga, wakaigawanya sehemu mbili, nusu wakaiweka chini ya Marangu, na nusu chini ya Mamba; na baadaye Samanga yote iliwekwa chini ya Marangu. Tutasikia habari zaidi za Marawite halafu.





ROMBO.​

Kadiri inayojulikana, habari za zamani za Rombo ni habari za jamaa nyingine ambazo hapana moja iliyokuwa ya maana sana. Hapakuwa na mkuu katika nchi ya Rombo mpaka wakati wa Horombo, na hata hivyo, haikudumu sana baada ya kufa Horombo isipokuwa katika Useri.

Sababu ya tofauti kubwa ya Warombo na Wachaga wengine si vigumu kueleza. Nchi ya Rombo ni nzuri kwa mifugo ya ng'ombe, lakini sehemu nyingine ya Kilimanjaro inayokaa watu ni nchi ya kilimo hasa. Wachaga walikuwa hasa walimaji, lakini Warombo walipenda kufuga ng'ombe. Basi, sababu za tofauti ni hizi: ya kwanza, kwa desturi watu wafugao ng'ombe hawashirikiani sana pamoja, wanapenda zaidi kukaa kila jamaa peke yake, basi Warombo walishika desturi zao za zamani walizopata katika nchi ya Ukamba ambako hapakuwa na wakuu wa kutawala. Ya pili, wale watu waliokuwa walimaji walitamani sana kupata ng'ombe, na kwa hivi walikuwa tayari kujiweka chini ya mkuu awezaye kupigana na jirani na kukamata ng'ombe zao, na hivyo kuwatajirisha kwa mifugo. Ya tatu, ni dhahiri kuwa mifereji ya maji ya walimaji haikuweza kutengenezwa na kuangaliwa bila watu kushirikiana pamoja chini ya wakuu waliojulikana au kuchaguliwa. Lakini nchi ya Rombo ni kavu, wala haina vijito vilivyo lazima kutumika katika mashamba. Basi, hapo Warombo walikuwa hawana haja ya kujiweka chini ya watawala, ndiyo sababu wakuu hawakuwekwa katika nchi yao.
 
SEHEMU YA PILI

SURA YA KWANZA

VITA KATI YA WAKUU.

VUNJO.​

MPAKA hapa tulipofika tumesoma habari za Wachaga hata za wakati ule wakuu wa Kichaga walipojisimamisha kuwa watawala wa nchi ndogo ndogo. Basi, sasa tutaendelea na kusimulia habari ya majira watawala walipopigana wao kwa wao, na wakuu wengine waliokuwa na nguvu walipojimilikisha katika sehemu kubwa ya nchi.

Wakuu wa Vunjo walianzisha hali hii kwanza, nao waliwatangulia wengine kadiri ya vizazi kadhawakadha kabla hawajajaribu kufanya hivyo.

Wakuu wa Mamba. Labda Marawite mkuu wa Mamba alikuwa wa kwanza wa Kichaga kuweka na kuwafundisha askari kwa taratibu. Kisha kuwafundisha, aliwachukua, akaenda nao nchi ya Rombo, na huko aliwatiisha watu mpaka kufika nchi ya Mkuu. Marawite alirudi kwake na mateka mengi, na huku nyuma watu waliasi, lakini aliwaendea tena akawaadhibisha kwa kukatakata na kuharibu viunga vyao vya migomba.

Marawite alirithiwa na Mafuluke mwanawe ambaye alifanya vita na mkuu Iwite wa Marangu akamshinda, lakini baada ya muda kupita alipatana naye. Tena, Mafuluke alimsaidia Nyange wa Kilema ajipatie tena utawala wake na kumfukuza Musuo. Watu wa Msae na wa Kondeni walijiweka chini ya Marawite kwa hiari yao. Wakati ule, nchi ya Mwika pia ilikuwa sehemu ya Mamba, wala haikuwa utawala wa peke yake mpaka baadaye, na mkuu wake alikuwa Kyasimba ambaye ni baba wa mtawala wa sasa wa Mwika. Wakati alipokuwa akitawala mwanamke Mashina, Kyasimba aliasi akauawa vitani.

Pia Mafuluke alishughulika na mambo ya Kilimanjaro ya magharibi, maana alimsaidia Warsingi mkuu wa Uru kuwafukuza Wamachame waitoke nchi, na kwa kuwa alikuwa rafiki wa Warsingi alimsaidia pia kumpiga Iwere mkuu wa Kibosho. Hivi nguvu za Mafuluke zikajulikana kotekote; ikachukua muda mrefu kabla ya kutokea mkuu mwingine wa Kichaga aliyefanya nguvu yake ijulikane pande zote mbili, yaani mashariki na magharibi ya Kilimanjaro.

Malamia mwanawe Mafuluke alipopata umri wa kutosha, Mafuluke akajiuzulu, lakini Malamia aliishi miaka michache tu akafa. Malamia alipokufa, ndugu yake Ngawondo alikuwa mdogo tu, na kwa hivi Mafuluke akaushika tena utawala. Wakati huo watu wa nchi ya Mkuu waliasi, lakini walitiishwa upesi, wakaadhibiwa kwa kuharibiwa mashamba yao na viunga vyao vya migomba.

Mara Ngawondo alipopata umri wa kutosha kushika utawala, Mafuluke akajiuzulu tena. Ngawondo alikuwa mtu wa vita, akashughulika sana katika kuwafundisha askari wake, akawavisha ngozi nyeusi za ndama, kofia za ngozi na kanda mikononi na miguuni. Kila askari alijaribiwa uhodari wake kwa kupiga upindi, na wale walioshinda waliwekwa katika jeshi la pekee lililoitwa Wasaghara, ila wale waliosalia hawakupata jina wala kuruhusiwa kuwinda.

Basi, alipokwisha kuwafundisha askari wake hivi, Ngawondo alifanya vita na watu wa Kahe, Ugweno, na Waukuma, yaani Waarusha. Akaendelea kufanya vita na majirani zake wote, akajipatia sifa katika nchi nzima. Siku moja Ngawondo alifanya vita na watu wa nchi ya Mkuu waliokuwa wameasi tena, akateka ng'ombe wengine alioweka Mafuluke huko Mkuu. Basi, Mafuluke alikasirika, maana yeye hakutoa ruhusa Ngawondo afanye vita na Mkuu. Basi alipokutana na ng'ombe wanaletwa, alimwua mtu mmoja wa Ngawondo aliyekuwa akiwatangulia. Ngawondo alikuwa nyuma ya ng'ombe, naye alipopata habari ya tendo hili, alighadhabika, akawafukuza ng'ombe mbele kwa nguvu sana, wakamwangusha Mafuluke, wakamkanyaga, akaumia vibaya hata kesho yake akafa. Baada ya siku chache tu, Ngawondo mwenyewe akafa.

Hapo paliondokea ushindani juu ya mtu wa kuurithi utawala, maana Keenya mwana mkubwa wa Ngawondo alikuwa mtoto mdogo tu. Kweli, nduguye Ngawondo Lyombe alipendwa na watu, lakini waliogopa ya kuwa hatakubali kumwachia Keenya utawala hapo atakapopata umri wa kutosha. Basi, watu walifikiri sana wakapata shauri la kufaa. Mafuluke alikuwa amemwoa binti ya Iwite mkuu wa Marangu, na kwa kuwa Iwite alimwonea wivu Mafuluke kwa ajili ya nguvu zake, alimshawishi binti yake amwue mumewe kwa sumu. Lakini Mafuluke aliambiwa habari hizi na kijana mwanamke jina lake Mashina ambaye Iwite alimpa binti yake awe kijakazi chake. Basi, Mafuluke kwa kuwa alikuwa na shukrani, alimwoa yule kijana Mashina akapendwa sana na watu kwa sababu ya busara yake. Basi, hapo Ngawondo alipokufa, watu walimchagua Mashina atawale mpaka Keenya awe amepata umri wa kutosha, naye hata Lyombe alitoa nchi kwa hiari yake mwenyewe, akahama akaenda kukaa Uru. Kirumi, mwanawe Lyombe alirudi baada ya miaka kupita, akakaa Mamba tena.

Mashina alikuwa na busara, na watu wote wakamheshimu, lakini kwa kuwa ni mwanamke ilikuwa lazima aweke wanaume kuwaongoza askari wake vitani, na mmoja aliyesifiwa zaidi alikuwa Mawinje.

Mashina alikuwa mtawala mwenye nguvu wa mwisho wa Mamba, na katika wakati wa utawala wake, nchi yake ilishindana na wakuu wawili wenye maarifa mengi ya vita, ndio Rongoma na Horombo, ambao kila mmoja alipata kutawala nchi yote ya Vunjo.



RONGOMA.​

Tuliposimulia habari za Kilema, tulifika mpaka wakati Kombo alipourithi ukuu. Katika utawala wake, Kilema iliingiwa na Ngaramite mkuu wa Marangu aliyesaidiwa na watu wa Chimbili na wengine wa Ugweno. Kombo alikimbia pamoja na watu wake wote mpaka Kirua alipotawala Mosha. Basi, ikatokea ya kuwa Mosha alimtamani mkewe Kombo, akajaribu kumshawishi ampe sumu mumewe na mwanawe Rongoma pia. Lakini yule mwanamke alikimbia, akarudi Kilema, na Kombo na watu wake wote walimfuata. Mara alipopata habari hii, Ngaramite aliingia tena Kilema pamoja na rafiki zake Wagweno. Kombo alitaka kukimbia tena, lakini mke wake alijipatia silaha, akawaongoza watu wa Kilema kuonana na adui, na hapo Kombo aliona haya, na yeye mwenyewe akaja akawaongoza. Watu wa Kilema walijipa moyo kwa kuwa wameona ushujaa wa yule mwanamke, wakapigana kwa nguvu nyingi sana wakawashinda kabisa adui zao.

Basi, baada ya hayo, Kombo alinuia kumpiga Mosha kwa kuwa alifanya tendo ovu lile wakati alipokuwa mgeni wake. Akampeleka mwanawe Rongoma Utaita ili apate msaada lakini alikawia sana, na huku nyuma yeye mwenyewe alipata msaada kutoka Ugweno akawashinda watu wa Mosha, akawaweka chini yake. Baada ya muda kupita Rongoma alirudi kutoka Utaita ameleta watu wa kupigana pamoja naye, na kwa kuwa nchi ya Kirua ilikuwa imekwisha wekwa chini ya baba yake Kombo, walifanya vita na Marangu iliyotawaliwa na Masanjuo, wakateka sehemu ya nchi ile.

Baada ya miaka michache kupita, Kombo alijiuzulu, na Rongoma mwanawe aliurithi utawala. Wakati huo huo Kilewo aliyekuwa mkuu wa Marangu akafa pia, na mara ile Rongoma alipeleka tarishi kuwakaribisha wanawe Kilewo waje kukaa pamoja naye ili apate kuwatunza, maana kwa kuwa ni mzao wa Mremi, alifanya kama anataka kuwa kaka yao. Silawe na Ishosho wana wawili wa Kilewo walikwenda Kilema wakapokewa vizuri, lakini walipotaka kurudi kwao, Rongoma aliwafanya wafungwa, kisha, aliingilia Marangu akajitangaza mkuu kwa haki, kwa kuwa ni mkubwa wa ukoo, uliotoka wakuu wa nchi zote mbili.

Sasa na tuache habari za matendo ya Rongoma, tupate kuchungua habari za sehemu nyingine, na kusimulia habari za matendo ya Horombo aliyekuwa mkuu, kushindana na Rongoma.



HOROMBO.​

Tumesoma jinsi wakuu wa Mamba walivyowashinda watu wa Rombo. Katika siku zile hapakuwa na wakuu katika upande ule wa pili wa mlima, ila kulikuwa na watu wachache wachache tu walioongozwa na wakubwa wao, kama ilivyokuwa katika sehemu nyingine za Kilimanjaro kabla ya kusimamishwa wakuu. Katika nchi ya Useri tu kulikuwa mkuu, lakini Useri haikuwa sehemu ya milki ya Mamba. Mtu mmoja jina lake Moosinyi wa ukoo wa Kumba alikuja na wafuasi wake wakakaa Keni, na kijukuu chake jina lake Ukongi alipigana na Marawite wa Mamba kwa muda, na ingawa alishindwa, hata hivi alifanywa mkubwa wa nchi ya Chimbili chini ya Marawite. Chimbili ni nchi iliyo kati ya Mriti na Mkuu. Urio mwanawe Ukongi alimwasi Mafuluke, pia akashindwa baada ya vita vikali vya siku nyingi. Katika vita hivi nchi iliachwa ukiwa wala haikuwa na ng'ombe, lakini Mafuluke aliweka ng'ombe wake wengine kwa watu, na kwa miaka kadhawakadha walikaa kwa amani chini yake. Urio alikuwa na wana wawili, mkubwa alikuwa Msangaro na mdogo aliitwa Horombo. Msangaro alikuwa kijana mpole, lakini Horombo alikuwa mkali wala hawezi kutulia, akamwudhi sana baba yake kwa kuwaua ng'ombe waliowekwa kwao na watu wa Mamba na kuila nyama yake. Alikuwa na nguvu nyingi sana, tena mrefu kuliko wote wa nchi, na kwa hivi hapana mtu aliyethubutu kumchokoza. Katika ujana wake Horombo alijipatia sifa nyingi kwa sababu alimwua tembo peke yake, na watu wa Waalenyi walipokuja wakachukua nyama ya tembo yule, basi, hapo aliwanyang'anya ng'ombe zao wote akawachinja akafanya karamu. Matendo aliyoyafanya Horombo yaliwaogofya sana watu wa Keni mpaka walimwomba awe mkuu wao, maana waliona ya kuwa hakuna njia ila hii ya kupata amani katika nchi. Lakini watu wa nchi zilizo jirani, yaani Mriti, Mengeve, Chimbili, na Mkuu hawakumkubali Horombo, na kwa hivi alifanya vita nao akawanyang'anya ng'ombe wengi sana. Lakini ng'ombe wale aliowachukua, kwa kweli walikuwa ng'ombe za watu wa Mamba, na yule mwanamke Mashina alikuwa mkuu wa huko. Basi, mara alipopata habari ya matendo haya, alipeleka jeshi chini ya amri ya Mawinge kumwadhibu Horombo.

Horombo hakuogopa, lakini alijua ya kuwa hana nguvu ya kupigana na jeshi la Mamba, na kwa hivi yeye na watu wake wakarudi wakakaa mwituni. Baada ya muda kupita, askari wa Mamba walichoka kukaa siku zote tayari kwa vita, wakaanza kukaa kwa raha katika nyumba zilizoachwa tupu na Wakeni. Usiku mmoja walipokuwa wakifanya karamu katika nyumba zile, Horombo akaja na watu wake kwa werevu sana, wakazichoma moto nyumba, na watu walipojaribu kutoka nyumbani waliwaua. Hapana mtu mmoja aliyeokoka katika jeshi zima isipokuwa Mawinge, maana yeye alikuwa akikaa peke yake mbali kidogo na watu wake akikesha.

Baada ya hayo, vita vikaendelea miaka minane kati ya watu wa Mashina na watu wa Horombo. Hapana aliyeweza kumshinda kabisa mwenziwe, wala hapana mmoja aliyeweza kupita mlango uliojengwa kwenye korongo liitwalo Kishingonyi. Basi vita vikaendelea hivi mpaka Mashina akatambua ya kuwa nguvu za nchi yake zinapotea bure, akakubali Horombo awe mkuu wa nchi ya Rombo. Tena akafanya urafiki naye akachanjia na udugu uliodumu mpaka kufa kwake Mashina.

Basi, sasa Horombo alianza kutiisha nchi iliyo- kuwa mbele ya nchi ya Mkuu. Aliwahi kufanya bila shida mpaka alipofika Useri, na hapo Kafuria aliyetawala Useri na Ngasini alimzuia. Kafuria alipata askari zake walio bora Ngasini. Horombo hakuwahi kuitiisha Useri wakati huo kwa sababu mambo mengine yalitokea, ikawa lazima aende kwa haraka kumsaidia Mashina rafiki yake.

Ule urafiki kati ya Mashina na Horombo haukumpendeza Rongoma, maana alishuku ya kuwa kwa namna hii watakuwa na nguvu kushinda zake. Basi, alimwagiza Mashina avunje urafiki na mapatano aliyoyafanya na Horombo, na Mashina alikataa kabisa. Basi, hapo Rongoma alifanya vita naye. Pigano kali sana likafuliza mahali palipoitwa Palenyengi, lakini hapana upande mmoja ulioshinda, na baada ya pigano hilo, vita vikaendelea kwa muda wa miaka sita, na vile vile hapana upande mmoja ulioshinda kabisa. Basi, Rongoma alipoona ya kuwa shauri lake halisitawi, alifanya jambo lisilofuata desturi ya vita. Usiku mmoja alituma kundi la watu, wakaingia Mamba kwa hila, wakamwua Mawinge mkubwa wa askari, wakamchukua Mashina amefungwa mpaka Kilema. Horombo alikuwa amefanya haraka kwenda kumsaidia Mashina rafiki yake, lakini alipofika aliona ya kuwa Mashina ana nguvu ya kuwazuia adui zake. Basi, akarudi kwake ndipo alipopata habari ya kukamatwa kwake, na mara ile alipeleka msaada ili kuzuia nchi ya Mamba isitekwe na Rongoma, lakini alipofika, aliona ya kuwa watu wa Mamba wamekwisha kujiweka katika mikono ya Rongoma, naye amemweka Tarimbo mke wa Ngawondo awe mkuu wa nchi ya Mamba. Horombo alifika mpaka Msae, na hapo alitaka Rongoma aje apigane naye. Kwanza watu wa Horombo walishindwa, wakakimbia na huku wanafukuzwa na watu wa Rongoma, lakini Horombo aliwatia moyo watu wake, wakasimama wakapigana, na watu wa Rongoma walishindwa wakakimbia. Kwa muda, vita vikaendelea, kisha, wakuu wote wawili walitambua ya kuwa hapana mmoja anayeweza kushinda kabisa, na kwa hivi walifanya mapatano, wakaweka mpaka pale penye korongo liitwalo Kishingonyi. Hapo walifanya kama ilivyokuwa desturi yao, yaani walizika mtoto wa kike na mtoto wa kiume wangali hai, na tangu wakati ule, Kishingonyi ni mpaka unaotenga nchi za Rombo na Vunjo.

Basi, sasa Horombo akarudi kufanya vita na Kafuria, akawahi kuteka sehemu ya nchi ya Useri, lakini Kafuria alifanya uhodari sana Ngasini akailinda nchi vizuri sana, wala hakushindwa huko kwa muda mrefu.

Basi, huku nyuma Rongoma alikwenda kuiingilia nchi ya Kirua, na hapo Kikare mwana wa Mosha alikuwa mkuu. Kikare alijaribu kupata mapendeleo mbele ya Rongoma akampa ng'ombe wote waliokuwa katika nchi, lakini hakupata kitu ila kuuawa na watumishi wa Rongoma.

Basi, sasa Rongoma alikuwa akitawala nchi zote toka korongo liitwalo Kishingonyi mpaka Nanga, akaogopwa kotekote. Hata Wamasai waliokuwa wakikaa uwandani wakamwogopa, na walipokwenda kufanya vita na Wagweno, aliwashurutisha warudishe ng'ombe zote walioteka, maana Rongoma aliwapenda Wagweno kwa ajili ya msaada waliompa Kombo baba yake.

Kombo babaye Rongoma alipojiuzulu, mwana wa Rongoma alikuwa amekwisha kuwa mtu mzima. Kombo aliishi mpaka wakati baada ya kufanya amani kati ya Rongoma na Horombo, na kwa hivi hakosi alikuwa mzee wa miaka mingi sana. Rongoma aliishi kadiri ya miaka kumi baada ya kufa kwake babaye.

Basi, baada ya vita na Horombo, miaka kumi ya amani ilifuata, na kwa muda huo Silawe na Ishosho na Mashina walikuwa wamefungwa Kilema. Mwisho, Rongoma alifanya shauri la kuwaua Silawe na Ishosho, lakini mwanawe alilichukia sana shauri hili ovu, na usiku uliotangulia ule uliofanywa kuwa usiku wa kuwaua, alijaribu kuwaokoa. Alikwenda kwa werevu mpaka nyumba waliyofungwa, akaona ya kuwa askari walinzi wamelala usingizi, basi akavunja ukuta wa nyumba. Ishosho alitambaa akatoka katika tundu lililofanywa, lakini Silawe alikuwa mnene, na kishindo alichofanya alipokuwa akijaribu kuongeza tundu ukutani, kiliwaamsha askari. Basi, hapo ikawa kumwacha Silawe, na kesho yake akauawa, lakini Ishosho alikimbilia Uru akapata ulinzi kwa mkuu Warsingi.

Rongoma alishuku matata akajaribu kumdanganya Horombo, akatoa habari ya kuwa anataka kumwoa Mashina, lakini siku iliyofuata ile aliyouawa Silawe, Mashina alinyongwa. Baada ya muda kidogo, Rongoma aliugua akafa. Imehadithiwa ya kuwa Mashina alijua ajali itakayompata, akamwambia Rongoma ya kuwa akimwua, basi roho yake haitatulia ila itamsumbua na kumtesa mpaka amtolee kafara ya barafu kutoka mlima Kibo. Basi, Rongoma alipoanza kuugua, alitoa kafara nyingi za ng'ombe kumtuliza roho ya Mashina, lakini zilikuwa bure, maana alizidi kuugua. Kisha, alimtoa mwanawe awe kafara, na hata hivyo akazidi kuugua. Hatimaye alikumbuka maogofya yale aliyoonywa na Mashina, akawatuma watumishi wengine walioaminiwa sana wapande mlima Kibo wakalete barafu, ambayo alisadiki kuwa ndivyo roho ya Mashina ilivyotaka. Watumishi wale hawakuthubutu kukataa kwenda, wala hawakuthubutu kwenda kupanda mlima Kibo, basi, walijificha mwituni mpaka kupata habari za kufa kwake Rongoma, ndipo walipothubutu kurudi kwao.

Kifo cha Rongoma kilifichwa muda wa miaka miwili, lakini baada ya muda huo, habari ikapata kujulikana kidogo kidogo, na Horombo alifanya haraka kutoka Useri kwenda Mamba, akawaruhusu watu wa huko wamrudishe Keenya kutoka Ugweno. Horombo akaendelea mpaka Marangu, na baada ya vita kidogo tu, alimfukuza Kirita nduguye Rongoma. Kirita alikimbilia Kilema akajiunga na watu wa mwana wa Rongoma aliyeitwa Tewuo. Basi, sasa watu hawa wakaja kufanya vita na Horombo, na vita vikali vikashikana, ikawa Horombo alikuwa karibu kushindwa, lakini mwisho aliwashinda kabisa Kirita na Tewuo. Hapo watu wa Kilema waliingiwa na hofu kuu, na usiku ule ule Tewuo pamoja na watu wengi na ng'ombe zote walitoka nchi ile wakahama kwenda Machame. Hawangaliweza kufanya hivi, lakini Horombo alikuwa amekaa mpakani ili watu wake wapumzike baada ya vita vikali. Basi, alipoingia Kilema aliona ya kuwa watu walio wengi wamekwisha kimbia, akachoma moto nyumba, akachukua mateka yaliyobaki, akarudi kwake. Tewuo na watu wake walipokewa na Rengwa mkuu wa Machame, akawapa nchi ya Kombo wakae huko. Basi, wakakaa huko muda wa miaka ishirini, maana Masaki mwanawe Tewuo alizaliwa huko, na waliporudi Kilema alikuwa amekwisha kuwa mtu mzima.

Katika nchi ya Kirua, Kikare mwana mdogo wa Mosha alirithi utawala, ikawa Horombo kumwambia lazima ajiweke chini yake. Kikare alikataa, na mara Horombo akashika njia kwenda kuitiisha nchi yake.

Basi, sasa Horombo aliweza kutumia nguvu zake zote kutiisha nchi ya Useri, lakini hakufuata desturi yake na kuyaongoza majeshi yake mwenyewe, ila aliwapeleka wakubwa wa askari wapigane na Kafuria, akawaambia washambulie usiku bila kuonya watu. Basi, kwa kuwa alighafalika hivi, Kafuria alishindwa upesi sana, akakimbilia pamoja na watu wake mwituni akajilinda huko kadiri alivyoweza. Lakini baada ya muda alishindwa tena, na Malamia mwanawe alihama pamoja na watu wengi wakaenda Machame, wakakaa huko mpaka kufa kwake Horombo.

Basi, sasa mkono wenye nguvu wa Horombo ulitawala na kuweka amani katika nchi zote za Rombo na Vunjo, lakini kabla ya muda mwingi kupita, nchi ilivurugika na upuzi wa wakati ule. Wakubwa wote waliokuwa chini ya Horombo walikuwa na lazima kutoa ng'ombe wengine kila mwaka, ndio kodi, na Keenya mkubwa wa Mamba alilazimishwa vile vile. Basi, ikawa mtu mmoja jina lake Ndakawo mwana wa yule kijakazi wa Mashina, alitaka kushika ukubwa wa Keenya, akatoa habari ya kuwa ng'ombe aliopeleka Keenya wawe kodi kwa Horombo wametiwa uchawi ili kumwua Horombo. Basi, Horombo alipata habari akasadiki ya kuwa ni kweli, na mara ile aliingilia Mamba akamfukuza Keenya, na Keenya alikimbilia Ugweno. Huko Ugweno alikusanya jeshi la watu, akawatumainia sana hata alimwambia Horombo aje kupigana naye, lakini alishindwa upesi, na watu wa Ugweno walibaki wachache sana hata waliogopa kurudi kwao, na kwa hivi walijificha Marangu. Hapo, Keenya alimshawishi Ishosho kumsaidia kupigana na Horombo na hawa wawili walianza kuiweka nchi ya Marangu tayari kwa vita. Walijenga safu mbili za nyumba za mawe, wakafundisha askari wao kila siku. Mara Horombo alipopata habari ya mambo hayo, alikuja Marangu akawaamuru wajitoe katika mikono yake. Lakini Ishosho na Tewuo walikuwa na tumaini kuu, na licha ya kukataa kujitoa, walipeleka maneno ya ufidhuli kwa Horombo. Ikawa Horombo hakuleta askari wa kutosha pamoja naye kuwashambulia wakati ule, na kwa hivi alirudi kwake, lakini alikamata punda sitini akawachinja wote mpakani, akasema ya kuwa hii ndiyo alama ya kuwaonyesha namna atakavyowatendea na wao. Basi, kwa kuwa hawakushindwa pale, Ishosho na Tewuo walipata moyo, wakaondoka wakaingia nchi ya Mamba. Hapo kukawa vita vikali sana, na askari mia mbili wa Horombo waliuawa, na wengine walikimbia. Sasa adui zake walifikiri ya kuwa vita vimekwisha, wakaanza kujishughulisha kuokota na kukusanya silaha za watu waliouawa vitani, lakini huku nyuma Horombo alikuwa amewakusanya askari wengine wa Rombo na kuwaweka mafichoni, nao wakatoka ghafula wakawashambulia watu wa Marangu wakawachezea mpaka wakachoka sana, wala hawakuweza kuwafuatia wale watu wa Horombo waliokimbia.

Labda Horombo alikuwa akipigana na Wamasai wakati huo wakamshughulisha sana, hatujui, lakini hakuwashambulia watu wa Marangu tena kwa muda wa miaka miwili. Ndipo alipowashambulia akafanya jeshi lake sehemu tatu. Sehemu moja ilimshambulia Keenya, na moja nyingine ikamshambulia Ishosho mbali mbali. Lakini hawakusitawi, ikawa walikuwa karibu kukimbia, kumbe sehemu ile ya tatu ikatokea ikamshambulia Ishosho kwa nyuma yao. Sasa ikawa machinjo tu, na Ishosho mwenyewe aliuawa. Imesemwa ya kuwa mahali walipopigana palitapakaa mifupa mpaka siku za utawala wa Mareale. Keenya aliposikia habari za kuangamizwa Ishosho alishikwa na hofu, akakimbilia Machame, na hapo aliuawa na mkuu Rengwa.

Kwa muda wa miaka minne mitano iliyofuata Mamba haikuwa na mtawala, mpaka Horombo alipomweka Kuwese mwana mdogo wa Mafuluke awe mkuu. Baada ya miaka michache kupita, Kuwese aliuawa pamoja na Horombo katika vita vya mwisho alivyopigana na Wamasai.

Ishosho aliposhindwa, watu wa Marangu walijinyenyekea mbele ya Horombo, akawasamehe akawaambia wamlete mkubwa wanayemtaka wao. Basi, walimleta Shamtembonyi ndugu wa Ishosho na Horombo akamkubali. Shamtembonyi alikuwa mjinga, ndiyo sababu Horombo alimkubali, maana alijua ya kuwa hana haja kushuku kuwa atamwasi. Lakini kabla ya kupita siku si nyingi, watu wa Marangu walichoka upuzi wake, wakamwomba Horombo amweke Itosi ndugu yake mdogo badala yake, na baada ya kupita muda, Itosi alimwua Shamtembonyi ndugu yake.

Wakati huo, Horombo alikuwa akijenga maboma katika nchi ya Keni kwa ajili yake mwenyewe na kwa ajili ya Msangaroa nduguye na wakuu wa askari zake. Wakati ule, Marinde alikuwa mkubwa wa askari aliyejulikana zaidi. Katika maboma hayo, Horombo alipatengeneza mahali pa kuwazika watu wote waliokuwa na nguvu katika nchi yake, maana alitaka kujua kwa hakika kuwa wamezikwa; wala hawakuitoka nchi yake ili wamfanyie matata. Mahali pengine katika boma lake kubwa ni mahali walipofanya kazi wahunzi waliofua chuma cha kutengenezea silaha. Mahali pengine bomani huitwa "mahali ра masikitiko," ndipo mahali walipokuja watu wa Useri kutoa vyungu vyao kuwa kodi, maana walikuwa wamekwisha toa kila kitu walichokuwa nacho vikabaki vyungu vyao tu, na huyu mkuu alividai hata vyungu vyao. Ipo miti mikubwa mingi nje ya boma, ndiyo iliyopandwa na watu wa Marangu kwa amri ya Horombo. Watu wote wa Vunjo na wa Rombo walishurutishwa kufanya kazi ya kujenga maboma hayo, na hasa watu wa Marangu, maana hao walikuwa waoga, na kila mara vita vilipotokea kati kati ya Horombo na Wamasai, hao watu wa Marangu walijaribu kuepuka wasiingizwe vitani, kwa hivi Horombo aliwadharau akawafanya watu wa kazi badala ya kuwa askari. Wengine wa Marangu lakini walikuwa mashujaa, ndio wale waliongozwa na Nderima nduguye Itoshi, na Nderima alipata sifa hata Horombo alimfanya kuwa mkuu wa nchi ya Samanga iliyo katika Marangu. Lakini baada ya kufa kwake Horombo, Itoshi aliitwaa Samanga akamwua Nderima. Basi sasa Horombo aliitawala nchi yote toka Gasini mpaka Nanga, ambayo ilikuwa nchi kubwa kupita nchi yo yote iliyotawaliwa na mkuu ye yote kabla yake Horombo na baadaye. Lakini hata sasa Wamasai walitembeatembea katika nchi za nyandani, wakashindana naye juu ya malisho waliyotaka kwa ng'ombe zao.

****

Baada ya kushindana sana, Horombo aliteka kundi kubwa la ng'ombe za Wamasai, akawaambia ya kuwa hawawapati tena mpaka wakubali kutoka katika nchi za nyandani. Wamasai walikataa kuondoka, na baada ya muda mfupi wakaja kupigana na Horombo. Walipigana vita vikali kwa siku kadhawakadha, kisha, Wamasai walirudishwa mpaka mto Rombo. Na Wamasai wale waliokuwa katika nyanda za Marangu walirudishwa vile vile, na kwa muda wa miaka mingi hapana Wamasai waliothubutu kuingia katika nchi za Horombo. Baada ya kushindwa mara ya kwanza Wamasai waliomba amani, na Horombo akapatana nao kwa sharti ya kuwa wasipite mpaka kuja kusini ya mto wa Rombo. Lakini Wamasai walilivunja agano hili mara nyingi, na kwa hivi ikawa lazima Horombo kupigana nao mara kwa mara, na vita vya Horombo na Wamasai viliendelea miaka kadhawakadha, hata husemwa kwa muda wa miaka kumi na mitano.

Huku nyuma Wamasai waliongezeka katika nyanda zilizo chini ya Useri, na Kafuria akawa anatafuta njia ya kujilipiza kisasi juu ya Horombo, akawatumia Wamasai katika kupata mradi wake. Basi, akawapelekea ujumbe waje kumsaidia kupigana na Horombo. Wamasai walitaka sana, lakini walikuwa hawana moyo kupigana na Horombo peke yao, basi Kafuria alifanya shauri. Alipata kwao ng'ombe dume thelathini, na kwa hao akanunua mikufu mingi ya chuma akaipeleka kwa Wamasai waliokuwa katika nchi za mbali, iwe zawadi ya kushuhudia mali waliyo nayo Wachaga. Shauri hili lilisitawi, na Wamasai wengi sana toka pande zote wakaja kwenye nchi chini ya Shira.

Wakati huo huo Kikare mwana wa Mosha aliyekimbia Uru wakati wa utawala wa Rongoma, alirudi Kirua, na mara Horombo alipopata habari alipeleka mwanawe Mapusu pamoja na jeshi kumtaka Kikare ajitoe. Basi, hapo Mapusu alipata habari za jeshi la Wamasai akampelekea baba yake taarifu ili kumwomba ruhusa ya kuwashambulia. Kwanza Horombo alisitasita, lakini baadaye akakubali, maana alikusudia kumpa mwanawe nafasi kuonyesha ushujaa wake, na tena yeye mwenyewe aliazimu kuwashambulia Wamasai na jeshi jingine kutoka upande mwingine. Walakini Mapusu alitamani sana kujipatia sifa, akawashambulia Wamasai kwa jeshi dogo tu alilokuwa akiliongoza peke yake. Basi watu wake wakashindwa kabisa na yeye mwenyewe aliuawa vitani pamoja na askari zake wote ila wawili tu, ndio waliorudi kumwambia Horombo habari. Imehadithiwa ya kuwa Horombo alipowaona wanakuja, alisema: "Ninyi mmekuja kuniambia ya kwamba mmemwacha mwana wa mkuu maiti. Vyema, nimesikia." Na pale pale akawaua wote wawili mwenyewe.

Sasa jeshi kubwa la Wamasai lilitapakaa kwenye uwanda wa Chimbili, na watu wote walijaa hofu, tena walikuwa wamechoka vita vya daima. Lakini Horombo alisema "Watu hawa wametupa ng'ombe wengi katika siku zilizopita, na sasa wamekuja kutupa zaidi." Akawakusanya askari zake wote akawaahidia ya kuwa vita hivi vitakuwa vya mwisho kupigana na Wamasai. Wamasai walishauriwa na watu wa Kafuria, wakagawanya jeshi vikosi vitatu, na kimoja lazima kiende kwa nyuma ya watu wa Horombo. Horombo naye aliligawanya jeshi lake vikosi vitatu, na kikosi cha kwanza kiliongozwa na Kuwese wa Mamba, akafaulu kuangamiza kabisa kikosi cha kwanza cha Wamasai. Horombo mwenyewe alishambuliwa na askari wenye nguvu wanne waliochaguliwa kusudi, lakini aliwaua wote wanne peke yake. Kikosi cha pili cha Wamasai kilishindwa pia. Basi, karibu na jioni, kikosi cha tatu cha Wamasai kilikuwa kimewahi kufika nyuma ya Wachaga, wakateka ng'ombe wengine wa Horombo. Horombo aliwaongoza watu wake kupigana nao, wakawaua wengi. Basi, ikawa usiku ulipoingia, wakaacha kupigana. Imesimuliwa ya kuwa uvundo wa maiti ulikuwa mbaya sana hata watu hawakuweza kupata usingizi. Basi, kulipokucha vita vikashikana tena, wakapigana vikali. Panapo saa tisa, watu wengine wa Horombo walijaribu kumshawishi atafute mahali ра salama kwa sababu wamepungua sana, lakini alikataa. Baada ya kupita muda kidogo, sana, mkono wake wa kushoto ulivunjwa kwa pigo la rungu lililotupwa, na kwa hivi hakuweza kuishika ngao yake na kujilinda, na kwa kuwa alikuwa mtu mrefu tena mkubwa, adui zake waliweza kumfanya shabaha kweli kweli, nao hasa nia yao ilikuwa kumwua. Basi ikawa baadaye kidogo alipigwa mshale wa mbavuni, na mara akaonekana kuruka juu hewani, kisha akaangukia mahali penye miamba.

Usiku ukaingia, na watu wa majeshi ya pande zote mbili walikuwa wamechoka kabisa, wakaanza kurudi nyuma. Katika upande wa Wachaga watu wengi waliokuwa wakubwa na mashujaa walikuwa wamekwisha kufa, pamoja na Horombo, na Kuwese wa Mamba, na karibu wakubwa wote wa askari, na askari wengi sana. Lakini Wamasai walipata hasara zaidi, nao walikimbia usiku wakaacha ng'ombe wale waliowakamata. Basi, ikawa ingawa Wachaga walipata hasara nyingi mno, lakini kwa kweli walikuwa wameshinda.

Habari za kufa kwake Horombo zilipofika kwake, Manyaki mke wake mpenzi alijinyonga kwa hofu ya mambo yatakayowajia, pia akawanyonga watoto wake wawili wadogo. Lakini ikatokea ya kuwa Horombo alipoanguka hakufa pale pale, na Mfumo mwanawe alikwenda mahali pale akamkuta bado yu hai lakini karibu kukata roho, akamkata kichwa chake akakichukua kwao, maana aliogopa ya kuwa adui watakuja na kufanya vivyo na kukichukua kichwa cha Horombo kiwe ukumbusho.

Horombo amepata sifa kuwa ni hodari, tena shujaa mkubwa wa watu wote wa Kichaga, akafa katika kupigana na adui wa watu wote wa kabila lake. Nchi ya Horombo ilikuwa kubwa kuliko nchi aliyotawala mkuu ye yote wa Kichaga, lakini tutaona ya kuwa utawala aliousimamisha haukudumu siku nyingi baada ya kufa kwake.



MAMBO MENGINE YALIYOTOKEA ROMBO NA VUNJO BAADA YA KUFA KWAKE HOROMBO.​

Mara alipokufa Horombo, ufalme aliousimamisha ulivunjika. Watu wa kila sehemu ya nchi yake wa- kajiwekea mkuu wao wenyewe, na hata katika nchi ya Chimbili, yaani toka Mriti mpaka Mkuu, wana wa Horombo walishindana wao kwa wao juu ya ukuu. Watu wa nchi iitwayo Mkuu waliasi kwa waziwazi, lakini Kisuma mwanawe mkubwa Horombo aliwashawishi ndugu zake wengine washirikiane naye, wakawatiisha watu wa Mkuu kwa muda. Huyu Kisuma alikuwa na nguvu hata akaweza kujitia katika mambo ya Vunjo na kumtoza faini mkuu wa Marangu kama tutakavyosoma halafu, tena mpaka wakati aliotawala Rindi aliushika utawala wa nchi kutoka Kishingonyi mpaka mto Tumi. Lakini Rindi alipotawala, sehemu zilizobaki za nchi za Horombo zilitengana na kutekwa, na husemwa ya kwamba Kisuma alikufa kwa huzuni.

Nguvu za Horombo zilipokwisha, Wamasai walirudi tena katika nyanda, na watu wa Rombo wanalilia hasara ya nchi hizo za malisho mpaka sasa. Hata hivyo zilipotea kwa sababu ya upuzi wao, maana badala ya kumtegemeza mkuu mmoja awezaye kupigana na kuwapatia haki zao, waliwaruhusu watu wajisimamishe ovyo ovyo mpaka kila kilima kilikuwa na mkubwa wake. Basi nchi ilitengana, ikawa nchi ndogo ndogo zisizo na nguvu, kama hali ile iliyokuwa nayo wakati wa zamani walipokuja watu kukaa kwanza katika nchi za Kilimanjaro.

Katika nchi ya Mamba Kuwese alirithiwa na Maricha ndugu yake. Maricha alikuwa mwoga, lakini alifikiri ya kuwa akipata msaada wa Waswahili wengine waliokuwa na bunduki, ataweza kumshinda Kisuma. Lakini alishindwa, na Waswahili wale waliomsaidia waliuawa, na Maricha pamoja na watu wengine wa Mamba walikimbilia Kirua. Kwa muda mrefu kufuata mambo hayo, Mamba ilikuwa haina mkuu, na nchi ilitawaliwa na Kisuma mpaka Kisamaka alipopata msaada wa Itosi wa Marangu akajifanya mkuu wa Mamba akawafukuza Warombo. Warombo walijaribu kuiteka Mamba mara mbili tena, lakini kila mara walishindwa.

Itosi aliendela kutawala katika Marangu mpaka akaugua akafa. Kifo chake kilifichwa na mkubwa wa askari Sarika kwa muda wa kadiri ya miaka miwili, naye ndiye aliyeushika utawala, lakini watu walipopata habari, ikawa Sarika lazima kukimbia, na Salego nduguye Itosi aliushika utawala mahali pa Ndaalio mwana wa Itosi, maana Ndaalio alikuwa mtoto bado. Salego alitawala kwa muda wa miaka ishirini, ndipo Ndaalio akataka haki yake. Salego alipata mapendeleo mbele ya wazee, lakini Ndaalio alipendwa na askari na vijana. Sehemu mbili za watu zilikuwa karibu kupigana, lakini Oshami mkubwa wa askari wa Salego alimtangazia Ndaalio ukuu, na kwa hivi shauri lilikatwa. Basi, Salego alihama akaenda kukaa na Kisamaka, akamwoa dada yake. Alijaribu kushawishi Kisamaka kwenda kufanya vita na Ndaalio, lakini alikataa kwa sababu watu wa Marangu walimsaidia alipopigana na Horombo na Kisuma. Lakini hata hivyo, vita vikatokea, maana Mamganga mama yake Kisamaka alitaka kumsaidia mume wa binti yake, yaani mkwewe, akawashawishi watu wengi wa Mamba kuingia katika nchi ya Marangu, na yeye mwenyewe aliliongoza jeshi mpaka kufika mpakani, kisha akawapa amri Salego na mwanawe mdogo Ndelaiyo. Kisamaka alipoisikia habari hii alikasirika, na husemwa ya kuwa alimwomba Mungu jeshi liangamizwe. Mama yake Ndaalio aliwatia watu wa Marangu moyo kushindana na watu wanaowashambulia, ila aliwaagiza wasiwaue Salego na Ndelaiyo. Basi, watu hao walioingia Marangu waliweza kuingia kidogo, lakini walishindwa katika pigano la kwanza, nao walipotaka kukimbia waliona haiwezekani kwa kuwa kila njia imezibwa. Basi walikimbia huko na huku kwa muda wa siku nne, kisha jeshi zima liliangamizwa. Salego na Ndelaiyo walikamatwa, lakini mama yake Ndaalio aliwaokoa wasiuawe, wakapewa ruhusa kurudi kwao.

Basi, hapo Ndaalio aliwapa watu ruhusa kuingia katika sehemu zile za nchi za Mamba Salego alipopata wafuasi wake, lakini kwa amri ya mama yake hapana mtu aliyeuawa.

Kisamaka alifadhaika mno kwa msiba aliouleta mama yake juu ya nchi yake, akataka kumwua, lakini wazee walimshauri asifanye hivi ila apelike wajumbe kuomba amani. Basi, kama ilivyokuwa desturi alipeleka wajumbe, yaani mzee mmoja amefuatana na mtoto wa kike na mtoto wa kiume wanaongoza kondoo aliyevikwa majani ya msale. Kwa desturi ya Kichaga, wajumbe wa namna hii hawawezi kudhuriwa hata kidogo, na mtu akiwadhuru huwa amefanya kosa lililo kubwa sana. Hata hivyo, Sariko alionana nao akawaua, na mama yake Ndaalio alikasirika mno. Kisamaka aliposikia habari akafikiri ya kuwa sasa hakuna hata tumaini kidogo la kupata amani, akapeleka ujumbe Rombo kuomba msaada kwa Mjumo, mwana mdogo wa Horombo ambaye alimchukia Kisuma kwa kuwa alimwua baba yake. Basi, Mjumo pamoja na wakubwa wengine wa Rombo walimpelekea habari Ndaalio ya kuwa Kisamaka yu chini ya ulinzi wao, na ya kuwa wakimdhuru, basi, lazima watakuja na kupigana na Marangu. Ndaalio alikubali kufanya amani, lakini aliweka sharti ya kuwa Mlawi mwanawe Kuwesa afanywe mkuu wa sehemu moja ya Mamba. Wakati huo huo watu wa nchi ya Msae wakajitenga na Mamba, wakajiweka chini ya mtu jina lake Mrimia. Kwa hivi Mamba ikawa imetengwa sehemu tatu, na kila sehemu ilikuwa na mkuu wake.

Sasa Mlawi alitaka msaada wa Ndaalio kumtoa Kisamaka, kwanza alikataa, lakini baadaye alipeleka kundi la askari katika nchi ya Mamba wakauzunguka mji wa Kisamaka. Waliwaua watu wengi, lakini Kisamaka alijitega mlangoni ameweka silaha tayari, na hapana mtu aliyethubutu kumshambulia. Basi, hapo wale watu walizunguka nyuma ya nyumba yake wakaichoma moto, na moto ulipofika karibu naye, Kisamaka aliruka juu ya mgongo wa fahali mkubwa mweusi akatokea mlangoni ghafula. Mtu mmoja wa Ndaalio alimtupia mkuki, ukampenya mwilini, na alipoanguka, wale wengine walijitupa juu yake wakampiga tena na tena kwa mikuki yao. Katika nyumba hiyo mke wake Kisamaka aliunguzwa mpaka akafa. Basi, hapo askari wa Marangu waliteka nyara nchi ya Kisamaka, na sehemu ile iliyotawaliwa na Mrima, wakamtangaza Mlawi mkuu wa nchi yote ya Mamba. Tendo ovu hilo liliwakasirisha wakuu wa Rombo wakadai fidia kwa ajili ya kila mtu wa Mamba aliyeuawa, tena walidai ng'ombe zote waliochukuliwa warudishwe. Ndaalio aliogopa ya kuwa Warombo wakija kumshambulia, basi na Wakilema nao watamshambulia upande mwingine, akakubali shauri lao. Hapo Warombo walidai ng'ombe 500, mbuzi 500, na majembe 500. Ndaalio alimwomba Mlawi alipe sehemu kwa kuwa alikuwa akimsaidia yeye, Mlawi hakuweza kulipa, lakini alikubali kutoa sehemu ya nchi iliyo upande wa magharibi. Nchi hiyo isipokuwa sehemu ile ya Chero imekuwa chini ya wakuu wa Marangu tokea wakati huo.

Kwa muda huo wote, Tewuo na watu wake walikuwa wakikaa katika nchi ya Machame walikokimbilia, lakini walipata mali nyingi sana, na kwa hivi watu wa Machame waliwaonea wivu. Tena Tewuo na watu wake waliingia katika vita vilivyofanywa na Rengwa juu ya jirani zake, na kwa kuwa walikuwa hodari sana, ikawa Wamachame kuwachukia kama kwamba ni adui zao. Rengwa mwenyewe hakuwaogopa, lakini alipokufa, Mamkinga mwanawe alikubali shauri la kuwaua. Wakati huo huo Horombo alikufa, na mara wale Wakilema waliposikia habari hii waliomba ruhusa kurudi kwao. Lakini walishuku ya kuwa hawataruhusiwa, na kwa hivi walitengeneza mashauri yao kwa siri, wakapata ruhusa ya Kasenga mkuu wa Kibosho kupita katika nchi yake. Tewuo alikusanya ng'ombe zao walio wazuri wakawaacha wengine, na siku moja usiku walitoka katika nchi ile. Lakini Wamachame waliwafukuza wakakutana nao mpakani. Sasa ikawa Mamkinga kuogopa kwenda mbele zaidi, asishambuliwe upande mmoja na Wakilema na upande wa pili na Wakibosho. Basi, hivyo ndivyo walivyorudi kwao wale Wakilema baada ya miaka mingi. Waliikuta nchi yao ukiwa inatumiwa na watu wa Marangu kama mahali pa kuwindia tu. Wamarangu walijaribu kuwazuia, lakini Wakilema walikuwa hawana mahali pengine kwenda wakapigana vikali sana, na kwa hivi Wamarangu waliona ni bora kuwaacha waingie katika nchi yao tena wakakae kwa amani. Baada ya muda kupita, Tewuo alikufa, na Masaki mwanawe aliirithi nchi.

Tendo la kwanza la Masaki lilikuwa kufanya vita na nchi ya Kirua. Ikawa Kikare akajiuzulu katika nchi ile, na Marengo mwanawe wa pili aliurithi utawala. Pengine Marengo huitwa Momino. Marengo alikuwa mtawala mwema akafanya mambo mengi kuwalinda watu wake wasiwe na shida, na wakati wa utawala wake unakumbukwa kuwa wakati wa neema katika nchi, lakini wema alioufanya ulilipwa uovu. Mara Mrumi mtoto wake alipotoka jandoni akafanya shauri la kuutwaa utawala na vijana wengi wa hirimu yake walipatana naye. Tena wazee wengine walikuwa upande wake kwa sababu walimwonea chuki Marengo kwa kuwa aliwashurutisha kuwapa watu maskini ng'ombe wao wengine ili wasiwe na shida. Basi, Marengo alipoona ya kuwa watu wanaomfuata Mrumi mwanawe wamezidi, alimkimbilia Masaki wa Kilema. Mara ile, Masaki aliingia nchi ya Kirua, na ingawa kwanza alirudishwa nyuma, lakini alipata msaada wa Wagweno, wakawashinda watu wa Kirumi, na Kirumi na watu walio wengi walikimbilia kwa Salia mkuu wa Moshi.

Baada ya hayo, Marengo aliona ya kuwa hapana watu wanaomfuata, akaona ni vizuri zaidi kumweka Leminyi mwanawe awe mkuu wa nchi. Leminyi alikuwa amekimbilia Machame wakati alipotawala Mamkinga, na Marengo akashika njia yake kwenda kumleta, lakini alipokuwa akipita katika nchi ya Moshi alikamatwa akarudishwa Kilema. Basi, sasa watu walimwonya ya kuwa watamwua asipokubali kujiuzulu na kumweka Kirumi mwanawe awe mkuu, na hivyo ikawa hana budi kukubali.

Wakati huo wote, mkuu mwenye haki ya Kirua alikuwa Masaki, lakini sasa amani iliyofanywa kati ya Marangu na Kilema ilivunjika, na siku za maisha yake zilizosalia zilikuwa za vita alivyofanya na Ndaalio. Vita hivi vilianzishwa namna hii;- Mwizi aliyejulikana sana alikuwa amekamatwa akiiba katika Marangu, na watu wakamfukuza mpaka Kilema, na huko wakamwua. Basi, tendo hili lilikuwa kama kudharau nguvu ya mkuu wa Kilema katika nchi yake mwenyewe, ikawa fitina kuzuka. Watu wa Kilema walianza kuibaiba ng'ombe za watu wa Marangu, na watu wa Marangu waliibaiba ng'ombe za watu wa Kilema, na mambo haya yakaendelea hata yakawa kama vita vya chini chini. Kweli, wakuu wawili wa nchi zile hawakutoa ruhusa mambo hayo yatendeke, lakini hata hivyo walikuwa kama wametoa ruhusa kwa sababu walikubali kupokea sehemu za mateka yaliyotekwa. Wakati huo ilikuwa desturi ya vita ya kuwa wanawake wasidhuriwe, ila watembee-tembee bila hofu; lakini sasa ikawa wanawake wengine kuuawa katika safari zile walizofanya za kuiba ng'ombe. Basi, Masaki alitambua ya kuwa mambo hayo ni mabaya kuliko vita vya wazi, akamwambia mkuu wa Marangu ajifanye tayari kwa vita, akaingia Marangu. Marangu. Lakini alishindwa akafukuzwa. Basi, hapo watu wa Marangu waliingia katika nchi ya Kilema, nao vile vile walishindwa na kufukuzwa. Basi, vivyo hivyo vita vikaendelea, wala hapana upande mmoja ulioshinda. Sasa Masaki alipata msaada wa askari kwa mkuu mmoja wa Wataita, na askari hao walifanya hasara nyingi katika jeshi la Marangu, maana walitumia mishale yenye sumu, na kwa hivi wakaweza kufanya hasara nyingi kuliko watu wa Kichaga. Lakini Masaki hakupata faida nyingi katika vita hivi, maana Wataita walikataa kushambulia tena kwa kuwa wamekwisha kupata mateka waliyotaka, tena habari walizochukua kwao juu ya utajiri wa nchi ya Kilema ziliwafanya Wataita wengine wakubali kumsaidia Ndaalio. Ikawa Kilema kuingiliwa tena, ikatekwa, na Wataita wakarudi kwao tena. Masaki aliwakaribisha tena Wataita waje kumsaidia, na Ndaalio akafanya vile vile, ikawa Wataita wakaja wakapigana kila upande, wakateka mateka mengi wakarudi kwao tena, na kwa hivi hakuna mkuu mmoja aliyepata faida katika vita walivyofanya wakuu hao wawili, ila Wataita.

Masaki aliwakaribisha Wataita waje tena kumsaidia, na safari hii Ndaalio aliwakaribisha Warombo na Wataita wengine waliokuwa wakikaa karibu na Taveta, waje. Hao Wataita walikuwa askari mashuhuri, na wengine wao walikuwa na bunduki. Basi, walipigana, mkubwa wao akauawa, na mara Wataita walijitoa katika vita, na Wamarangu walikuwa hawana budi kurudi nyuma pia. Vita hivi vilikuwa vya mwisho. Nchi zote mbili zilikuwa zimechoka, mali zimekwisha, na watu wakawa maskini kabisa, wala hakuna upande mmojawapo uliopata faida hata kidogo. Basi, katika msiba huu uliowapata, kwanza Masaki aliwakusanya watoto wa kike akawaamuru kupanda kilima kiitwacho Ngangu na kuwalaani adui zao, kisha, Ndaalio naye aliwakusanya watoto wa kike wote wa nchi yake nao wakafanya vile vile. Tendo hili lilikuwa mwisho wa vita, maana watu waliona ya kuwa ni tendo la kuogofya sana, wakasema vita lazima viishe. Baada ya muda kidogo kupita Ndaalio akafa, na baada ya muda kidogo Masaki naye alishikwa na ndui akafa, basi sasa misiba ya nchi zote mbili ilizidi.

Ndaalio alipokufa hakuacha mrithi ila ndugu zake wanne, na katika ndugu hao, Marangu na Kinabo ndio waliojulikana zaidi baadaye. Hapana mmoja katika ndugu hao aliyeonekana kuwa atafaa kuwa mtawala, na kwa hivi watu walimchagua Msanjo mama yake Ndaalio awe mkuu wao. Msanjo alikuwa mtawala mpole mwenye busara, akafanya mapatano na wakuu wote wa Vunjo, kwanza waondoe desturi iliyoitwa Kilya Shigu, na tena ya kuwa ni marufuku mkuu mmoja kujaribu kumwua mkuu mwingine. Lakini utawala wake haukudumu kwa amani. Wana wawili wa Masaki walikuwa wakikaa Kilema, ndio Seiya na Fumbo, lakini kwa kuwa walikuwa wadogo bado, watu walimchagua mtu jina lake Makindara atawale. Baada ya muda kupita Seiya alikufa, na watu walifikiri ya kuwa Makindara ndiye aliyemwua kwa uchawi, na kwa hivi aliuawa. Sasa Maambo nduguye alishika utawala, naye alikuwa mtu wa vita akawakaribisha Waarusha waje wamsaidie kushambulia Mamba. Lakini Waarusha wakaja wakateka nyara si Mamba tu, ila na Kilema pia, kisha, wakaenda zao. Sasa watu wa Kilema walifikiri ya kuwa wakimweka mkuu, hapo hapatakuwa na vita, maana haikuwa desturi ya mkuu kwenda vitani mwenyewe, na kwa hivi walifanya shauri la kumweka Fumba awe mkuu wao.

Maambo na wasaidizi wao Waarusha waliposhambulia Mamba, yule mwanamke mkuu Msanjo aliwapeleka askari zake katika nchi ya Mlawi wakawafukuza Waarusha, wakawaua wengi na kuteka ng'ombe waliowachukua. Baadaye Waarusha wakarudi wakaingia Marangu, na kwa kuwa wakati huo ndugu zake Ndaalio walikuwa wakishindana wao kwa wao, basi watu hawakujaribu kuwazuia Waarusha. Lakini hata hivi, askari walilinda nyumba ya Msanjo kwa hiari yao, na kwa hivi ingawa Waarusha waliteka ng'ombe wengi sana kila mahali, lakini ng'ombe za Msanjo walikuwa salama. Sasa ikawa ndugu zake Ndaalio kusema ya kuwa Msanjo alikuwa amefanya shauri na Waarusha waje kuteka ng'ombe za nchi, na ya kuwa nchi imepata hasara kwa sababu ilitawaliwa na mwanamke. Basi, kwa maneno haya waliyosema, watu wakaanza kumwasi Msanjo, na baadaye aliona afadhali akimbie, akakimbilia Msae. Lakini, watu walimfuata wakamwomba arudi pamoja nao. Ndugu zake Ndaalio waliendelea kushindana wao kwa wao juu ya nani atakayekuwa mkuu, ikawa Mlawi akafanya haraka akaja kumsaidia Msanjo. Watu wa Marangu wakamwambia Mlawi ya kuwa hawana nia ya kumdhuru Msanjo, waliyotaka ni yeye kumchagua mmoja wa ndugu zake Ndaalio awe mkuu wao. Basi, Msanjo alimchagua Kinabo, na Mlawi alimsaidia kumweka imara ingawa watu wengi hawakulipenda shauri hili.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom