Candid Scope
JF-Expert Member
- Nov 8, 2010
- 11,890
- 6,898
Rais kikwete kutoguswa na shinikizo la maandamano ya wananchi wa Mtwara kuhusu usafirishaji wa bomba la Gas kwenda Dar es Slaam ni kutokuangalia kwa makini mambo ya msingi kwa mtazamo wa kiuchumi, usalama wa mradi na uwiano wa maendeleo kitaifa.
Usalama:
- Ulimwengu wa leo wakati unakabiliwa na hatari ya maadui wenye kuharibu miundo mbinu sina hakika usalama wa bomba hilo la gas usalama wake toka Mtwara hadi Dar, kwani pamoja na umuhimu wake, kunaweza kutokea hujuma kubwa katika bomba hili kutokana na umbali huo, wakati vinu vya kufua umeme vingewezekana kujengwa eneo ambalo maliasili inapatikana.
- Hatari kubwa Electric power plant kuwa sehemu moja, hujuma ikifanyika, au itokeapo vita shabaha moja italitia taifa zima gizani. Muhimu Electric power plants zikawa sehemu mbalimbali na grid network power iunganishwe. Ukikatwa umeme Dar es salaam basi nchi nzima gizani.
- Ndege moja tu inatosha kudondosha bomu moja Ubungo na lingine Kinyerezi kisha taifa zima likawa gizani mara moja, no alternative, tutaonekana si watu wa kuona mbali. Ukaribu uliopo Ubungo na Kinyerezi vigumu kupata muda wa papo kwa papo emergency respond.
Kiuchumi:
Ujenzi wa vinu vya kufua umeme karibu na eneo inakopatikana rasilimali ni bora na inapunguza gharama nyingi. Litakapotokea tatizo la gas kutofika kwa kiwango kinachotakiwa toka Mtwara kuna ziada ya kuhangaika kutafuta uvujaji uliko kwa umbali mkubwa toka Dar hadi Mtwara, jambo ambalo linaweza kusababisha uhaba wa umeme kwa muda mrefu.
Ukuzaji wa bandari ya Mwara kwa uanzishwaji wa viwanda huko papo kuunganisha ukanda wa kusini na ukanda wa kusini nyanda za juu kunakopatikana makaa ya mawe na chuma kutaongeza msisimko wa maendeleo zaidi wakati Wachina wanampango wa kujenga reli toka Mkoa mpya wa Njombe hadi Mtwara. Uanzishwaji viwanda mikoa ya Ruvuma, Njombe, Lindi na Mtwara ni muhimu kutokana rasilimali nyingi kupatikana eneo hili.
Wanaosoma jiografia, mtakumbuka eneo la Essen nchini ujerumani lilivyo na viwanda vizito tokana na upatikanaji wa maliasili huko, Wajerumani hawakujenga miundo mbinu ya kuhamishia maliasili iende Berlin na kwengineko kwani kufanya hivyo kungekuwa na athari zaidi kiutendaji, kiuchumi na kiusalama pia, hali kadhalika kusahaulika wananchi wanaoishi maeneo inakopatikana maliasili.
Uwiano wa maendeleo
Uwiano wa maendeleo kitaifa ni jambo linalotakiwa kutiliwa maanani, kwani kushinikiza gasi ipelekwe Dar es Salaam kwa mahitaji ya nchini nzima si vema kwani ni kuongeza zaidi msongamano wa viwanda jijini Dar es Salaam hatari ya uchafuzi wa mazingira na hali ya hewa na papo kuzidi kuongeza mmiminiko wa watu kutafuta ajira huko badala ya kuanzishwa viwanda eneo la maliasili ili kuvutia watu wabaki huko kwa vile ajira ipo eneo lao.
Pamoja na kwamba uwiano wa maendeleo si rahisi kuwa sawa, lakini kuna sababu za msingi kutumia vyanzo vya rasilimali za mahali zinakopatikana kusaidia kuleta maendeleo kwa kuanzisha kwa makusudi miradi ya maendeleo kama uanzishwaji wa viwanda. Hatuhitaji machinga kuendelea kumiminika Dar es Salaam kwani wanachofuata ni hali njema ya maisha na ajira. Lakini ukishaweka mtego wa ajira na vivutio vingine kama hali nzuri ya umeme, viwanda nk hawatakuwa na sababu ya kuja Dar kwa vile wanachofuata dar kinapatikana kwao.
Tutakuwa tumekuwa na mtazamo finyu kama tutakubaliana na kauli ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano kwamba kwa sababu Dar es Salaam wanaota mapato makubwa ya kodi kwa kulisha nchini nzima basi iwe hoja ya kupeleka rasilimali pale. Nakumbuka Hayati Nyerere aliamua kiwanda cha SPM Mgolole, Mufindi karibu na Makambako kijengwe huko badala ya kusafirisha magogo kwa TAZARA kuja kutengeneza karatasi Dar es Salaam. Gharama nyingi ziliepukika na pia ajira ilipatikana sehemu hilo badala ya watu wa huko kulazimika kuja Dar kupata ajira.
Tungetazamia wabunge wangeanzisha mjadala wa jambo hili kuishinikiza serikali kusitisha mpango huu kwani hoja ya kuwauzia mitungi ya gas wananchi wa Mtwara si ufumbuzi wa ajira na mendeleo, bali ujenzi wa viwanda vitakavyoendeshwa au kuzalisha gas na pia ujenzi wa vinu vya kufua umeme huko kutawanufaisha zaidi wananchi, taifa, na pia kuondolea taifa msongo wa ukuaji jiji la Dar es Salaam.