Kigoma: CCM yatuhumiwa kupora ardhi ya Kanisa Katoliki, yagoma TAKUKURU kuingilia kati

pantheraleo

JF-Expert Member
Jan 5, 2013
691
878
MHESHIMIWA WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI
MJI WA SERIKALI MITUMBA,
S.L.P. 2908, 40477 – DODOMA

Ndugu,
YAH: MGOGORO WA ARDHI KATI YA KANISA KATOLIKI JIMBO LA KIGOMA NA CHAMA CHA MAPINDUZI KATIKA ENEO LA NYAMBUTWE, UVINZA-KIGOMA

Husika na kichwacha habari.

Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi; kwanza tunakushukuru kwani, Wizara unayoongoza imejaribu kuushughulikia mgogoro huu ili kuleta suluhu kwa pande tajwa. Barua yako: Kumb. Na.CBA.166/171/01/57 ya tarehe 22/07/2022 iliweza kutatua tatizo la eneo lile lenye hati miliki; lakini barua yako hii hii imesababisha matatizo makubwa kuhusu eneo lile lisilo na hati kwani badala ya wewe kama MSULUHISHI kutoa maoni na ushauri wako ulitoa MAELEKEZO yaani AMRI kwamba eneo lile la Kanisa lisilo na hati ligawanywe.

Mamlaka ya Wilaya Uvinza wamesema wao wanatekeleza agizo lako la kuigawa ardhi ile isiyo na hati kwamba kwa barua yako ile imeonesha eneo lile LIMETWALIWA na Serikali na sasa ni la serikali na itampatia yeyote kiasi chochote atakachoomba na kwamba hata Kanisa likiyataka MAKABURI walimozikwa WAMISIONARI yaliyo kwenye eneo hili la Kanisa, italazimika tuyaombe kwanza.

Hapa tunaona barua yako badala ya kutatua tatizo imeongeza tatizo. Kwa kuwa jambo hili sasa limeshachukua sura mpya, tunadhani ulitoa maelekezo na maagizo bila kulifahamu vizuri jambo hili. Kwa barua hii na kwa sababu maalumu tunaona tukupe historia ya jambo hili na maoni ya Kanisa Katoliki Jimbo la Kigoma juu ya jambo hili.

Kwa muda mrefu sasa kumekuwepo mazungumzo juu ya ardhi hii baina ya Kanisa Katoliki Jimbo la Kigoma na Chama cha Mapinduzi (CCM). Hapo awali haukuwa mgogoro wa ardhi kwani Kanisa kwa mapenzi mema liliwakubalia CCM kuendesha shule yao ndani ya eneo la Kanisa kwa makubaliano kuwa baadaye watatafuta eneo lao lingine. Mwaka 2017 ndio mgogoro huu ukageuka kuwa wa ardhi baada ya CCM

kugeuka ghafla na kudai kuwa wanalo eneo ndani ya eneo hili la Kanisa.

Mheshimiwa Waziri; mnamo mwaka 1986 wafanyakazi wa mgodi wa chumvi Uvinza walihitaji kujenga shule ya Sekondari kwa ajili ya watoto wao na wanajamii wengine katika eneo la Uvinza. Kwa bahati mbaya wakavamia eneo la Kanisa Katoliki lililopo Nyambutwe-Uvinza lenye ukubwa wa ekari 61 ambalo ndani yake ekari 21.4 zimepimwa na zina hati miliki kwa jina la Kanisa.

Mara tu baada ya kuanza ujenzi huo Kanisa liliwazuia na kisha uongozi wa mgodi ukaja kufanya mazungumzo na Kanisa. Kwa kuwa watu wa mgodi walikuwa wameshatumia raslimali za kutosha kwenye ujenzi huo, uongozi wa mgodi uliliomba Kanisa litumie busara na hekima liwaruhusu watumie eneo hilo kwa muda kuanzishia shule yao na kisha wataihamishia katika eneo lingine.

Kwa hiyo ifahamike kwamba shule hii haikujengwa na CCM bali ilijengwa na mgodi wa Chumvi Uvinza na makubaliano yote ya awali yalikuwa kati ya Kanisa na Mgodi wa Chumvi pamoja na baadhi ya Wanakijiji wa Uvinza. Baadaye shule hii ilipata ugumu katika usajili kwa sababu ilibainika imejengwa kwenye ardhi yenye miliki ya mtu mwingine na ikawalazimu . uongozi wa shule kuja Kanisani na kuomba dhamana kwa Wizara ya Elimu kwa kutumia nyaraka zetu za ardhi ili shule yao ipate usajili. Kanisa kwa upendo mkubwa na kwa kujali umuhimu wa elimu tulifanya hivyo na hadi sasa Wizara ya elimu inafahamu fika shule ya Chumvi ipo ndani ya eneo la Kanisa Katoliki.

Tumekuambatanishia barua ya Wizara ya elimu ambayo Wizara ilimwandikia RAS wa Kigoma kumfahamisha masuala kadhaa ya shule hii. Kwenye aya ya kwanza ya barua hii ya tarehe 30/09/2004 yenye Kumb. Na. ED/USJ/1987/01/40 wizara inatamka ‘Shule ya Sekondari Chumvi – Wazazi iliyopo eneo la Kanisa Katoliki Uvinza Jimbo la Kigoma’. Barua hii haijasema sehemu ya shule imesema shule. Na huu ni uthibitisho kuwa serikali kupitia Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia inajua eneo hili ni la Kanisa. Na bila nyaraka za Kanisa shule hii isingepata usajili.

Mwaka 1991 Kanisa lilibaini mipango ya CCM kulipora eneo letu hilo kwani walikuwa wameshaandaa michoro kwa ajili ya kutaka kumilikishwa eneo hilo, mchoro huu ulichukua eneo lote lenye hati na nusu ya eneo lisilo na hati. Kanisa tulipinga suala hilo na viongozi wa Serikali wa wakati huo wakasitisha mchakato huo wote kwa barua ya tarehe 5/9/1991 yenye Kumb. Na. AR/KGV/40/16. Michoro iliyokuwa imeaandaliwa na CCM kwa ajili ya kupora eneo letu hili tunayo pamoja na nyaraka zingine zote na barua kadhaa za kuhusiana na uporaji huu.

Wakati huo vikao vilifanyika kati ya CCM na Kanisa wakati huo na CCM waliomba radhi na kuahidi kutoendelea na jambo hilo na kwamba watatafuta eneo lao la kuhamishia shule yao pindi Kanisa litakapohitaji eneo lake. Hii inathibitisha kuwa nia ya CCM kutuibia eneo letu lote lile lenye hati na lile lisilo na hati ni ya muda mrefu sana. Ramani hii na baadhi ya barua vyote tuliwapatia kamati yako.

Baadae mwaka 2001 Kanisa lilianza mchakato wa kuwataarifu CCM waondoke kwenye eneo la Kanisa ili walipishe Kanisa lifanye shughuli zake. Uongozi wa shule na CCM wa wakati huo kwa ustaarabu kabisa walianza mchakato wa kupata eneo la kuhamishia shule hiyo na wakafanikiwa kupatiwa na serikali ardhi yenye ukubwa wa EKARI 50 eneo la Kibaoni Uvinza ambapo ni kama kilometa 2 kutoka ilipo shule hii kwa sasa.

Eneo hili lipo hadi leo. Lakini pia mwaka jana (2021) wakati mgogoro huu umekuwa mkubwa na kutishia usalama eneo la Uvinza, Serikali iliwapatia tena CCM eneo la EKARI 10 kwenye kilima ilipo minara ya mawasiliano Uvinza ili wahamishie shule hii na hivyo kuwa na maeneo mawili hadi sasa na hii ilikuwa ni baada ya Kanisa kubaini tena CCM wanataka kupora eneo letu na wameshapeleka wapimaji ndani ya eneo la Kanisa.

Mwaka huo huo wa 2001 viongozi wa CCM na wanajumuiya ya Uvinza walimwandikia Baba Askofu risala ya kukiri kuvamia VIWANJA VYA KANISA (siyo kiwanja) na kumuomba radhi Baba Askofu. Tuliwapatia kamati yako nyaraka hii. Baadaye CCM kwa kuwatumia maafisa ardhi wa ofisi ya Kamishna wa ardhi mkoa walikuja kupima eneo hilo ili kubainisha eneo lenye hati na lile lisilo na hati.

Kwa makusudi maafisa hawa wa ardhi wakaonesha kuwa sehemu kubwa ya madarasa ya shule ya Chumvi ipo nje ya eneo lenye hati jambo ambalo lilikuwa ni upotoshaji mkubwa na Kanisa tulipinga lakini hawa wataalamu wa mkoa walisisitiza kuwa wao wapo sahihi.

Baadaye upimaji huu ulikuja kupingwa na upimaji mpya uliofanywa na maafisa kutoka wizara ya ardhi. Ramani iliyoandaliwa na wataalamu wa kamati ilionesha haya yote na tunajua unayo.

Mazungumzo ya CCM kuhamisha shule hiyo iliyo ndani ya eneo la Kanisa Katoliki lenye ukubwa wa ekari 61 ambalo ekari 21.4 zina hati na ekari zingine kama 39 hazijapimwa japo zina mali kadhaa za Kanisa yakiwemo makaburi ya Wamisionari wetu yaliendelea kwa muda mrefu. Kila wakati CCM walikuwa wakitoa sababu mbalimbali za kuchelewa kuondoa shule yao hii. Kulingana na mahusiano mazuri baina ya Kanisa na CCM tuliendelea kuwaamini wenzetu kuwa wana nia njema. Mwaka 2017 wakati mazungumzo yakiwa yamefikia hatua nzuri tulipokea barua ya mshangao kutoka CCM kwamba na wao wamebaini kuwa ndani ya eneo hilo la Kanisa wana eneo ambalo ni la kwao, hoja hii haikuwahi kutolewa kwenye kikao chochote hapo kabla.

Kwenye barua hiyo ya tarehe 5/09/2017 na Kumb. Na. WAZ/VOL.2/38/172 walieleza kuwa kuna wazee kadhaa wamemwambia katibu wa wazazi mkoa wa Kigoma kuwa wao ndio walioshiriki kuliomba eneo hilo kutoka kwa Kanisa na wana ushahidi wa wao kulifidia Kanisa. Kanisa tuliomba tupatiwe ushahidi huo lakini hadi leo hatujapatiwa, Kanisa tuliiandikia hadi wizara yako iwashauri CCM walete ushahidi huo lakini hatujawahi pata majibu. Mwaka 2021 Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia iliiagiza ofisi ya udhibiti ubora wa elimu Kanda ya Magharibi kuchunguza jambo hili na kuzihoji pande zote na kupokea nyaraka za pande zote ili kufahamu shule hii kama ipo kwenye eneo la nani. Taarifa ya kamati hii hatujaipata.

Tunachojua tu ni kwamba kamati hii itakuwa ilibaini ukweli shule hii ipo kwenye ardhi ya nani maana tuliwapa nyaraka zote muhimu za eneo lenye hati na lile lisilo na hati.

Mgogoro huu uliendelea kuchukua sura mpya kila kukicha hadi ikafikia CCM

wenyewe kwenye kikao tulichokuwa tunajadiliana mambo haya wakaomba kuwa wawaombe Wizara ya Ardhi itusuluhishe sisi Kanisa na CCM. Kanisa tulipinga sana wazo hili la kwenda kusuluhishwa na Wizara; badala yake, Kanisa, tuliomba tusuluhishwe na vyombo vingine kama PCCB na IDARA YA USALAMA WA TAIFA; lakini wenzetu CCM walikataa. Baadaye ghafla mwaka 2021 ilikuja kamati iliyosema imetoka Wizara ya Ardhi kuja kuchunguza mgogoro huo na kuupatia ufumbuzi na kwamba wakikamilisha uchunguzi wao watatoa nakala ya taarifa yao kwa Kanisa, CCM na Wizara.

Tuliwapatia ushirikiano mkubwa na nyaraka zote muhimu za umiliki wa maeneo yote mawili lile lenye hati na lile lisilo na hati yaliyo sehemu moja. Kwa mshangao tumenyimwa nakala ya taarifa ya kamati hiyo kinyume cha makubaliano yaliyofanyika kati ya Kanisa na kamati hiyo.

Kanisa tumeshaandika barua wizarani kwako wa Katibu Mkuu wa wizara ya Ardhi mara mbili kuomba nakala ya taarifa hiyo iliyoandaliwa na wajumbe kutoka wizara ya Ardhi, lakini hadi sasa tumenyimwa taarifa hiyo na hata barua zetu hazijawahi kujibiwa jambo ambalo linatusikitisha sana kuona ofisi ya serikali inagoma kujibu barua za wananchi. Kwa mujibu wa maelezo ya wajumbe wa kamati hiyo walipokuja Kigoma walitueleza ndani ya taarifa hiyo wataandika kila kitu na kila mtu anayedai anamiliki eneo wataomba nyaraka zake na zote wataziweka kwenye taarifa na kila upande sasa utaona nyaraka za mwenzake.

Sasa imekuwa tofauti. Wajumbe walitueleza kuwa taarifa yao itatoa mapendekezo na kama kuna upande hautaridhika na mapendekezo yao basi watashauri mgogoro huo uende kwenye vyombo vya sheria.

Baadaye tuliitwa wizarani kupatiwa majibu ya kamati lakini kwa mshangao kilichotolewa pale kwenye kikao ni maoni ya waziri kuhusu mgogoro huu. Kanisa tulikubali sehemu ya maoni yako na tukapinga sehemu ya maoni yako. Waziri wa ardhi ulitueleza turudi Kigoma kisha ataandika barua ya USHAURI wako kwenye jambo hili. Kwenye kikao hukusema utatoa MAAGIZO bali ulisema utatoa ushauri wako. Maelekezo ya Wizara yapo katika barua; Kumb. Na.CBA.166/171/01/57 ya tarehe 22/07/2022.

Mheshimiwa Waziri; Kanisa linaomba kukupatia taarifa kuwa mgogoro huu kwa sasa una sura ya udini. Watetezi wote wa CCM pale Uvinza na wale wanaoitwa wazee walioiambia CCM kuwa wana ushahidi namna CCM ilivyolipata eneo hilo kutoka kwa Kanisa ni waamini na viongozi wa DINI YA KIISLAMU.

Kwa kuwa Wakatoliki tunafahamu kuwa lile ni eneo letu kwa zaidi ya miaka 100 sasa, na kwa kuwa tunafahamu fika wazee hao kwa makusudi wanaipotosha CCM na kukuza uhasama, sasa Wakatoliki wote pale Uvinza na kwingineko wanaona sasa ni VIONGOZI WA DINI YA KIISLAMU pale Uvinza wameamua kulihujumu Kanisa.

Kwa bahati mbaya sana CCM na viongozi wa serikali ngazi ya Wilaya wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya Ndugu Hanafi H. Msabaha wanashabikia sana mgogoro huu ambao sasa unachukua sura mbaya ya KIDINI. Na huyu mkuu wa wilaya amekuwa akiukuza mgogoro huu kwa kuegemea upande wa CCM. Kwa mfano tarehe 02/12/2022 Mkuu wa Wilaya ya Uvinza aliwakusanya wana CCM wa pale Uvinza ili kuwakabidhi wana CCM eneo la ekari 10 ndani ya eneo hili la Kanisa lisilo na hati na kuwaambia waanze kujenga mara moja, alifika eneo la mgogoro na kuwakabidhi CCM eneo letu hili akiwa ameambatana na wana CCM wengi na vipaza sauti vikiimba nyimbo za CCM. Yaani badala ya Mkuu wa Wilaya kuhamasisha amani anashiriki kikamilifu kuhamasisha vurugu.

Wakati Mkuu wa Mkoa wa Kigoma amekuwa makini sana na anatumia hekima za kutosha katika kulishughulikia jambo hili na alisema kuwa mazungumzo ya pande zote yafanyike kwanza juu ya eneo hili lisilo na hati, huyu DC wa Uvinza yeye amekuwa akitumia ubabe na kejeli kwa Kanisa kulinyanyasa kanisa na kutupora mali zetu.

Mheshimiwa Waziri, kwa miaka yote mgogoro huu ulikuwa baina ya kanisa na CCM, lakini sasa kwa maelekezo ya barua yako yanayotekelezwa kiholela na huyu DC wa Uvinza ni wazi sasa mmeiingiza serikali na kuwa sehemu ya mgogoro huu. Tuliwahi kukuandikia kuwa urekebishe barua yako kuhusu eneo hili lisilo na hati na maelekezo yako yawe ushauri lakini hata majibu hatujajibiwa. Tumeziomba mamlaka za ardhi Kigoma kusitisha kuimilikisha CCM hizo ekari 10 ndani ya eneo la Kanisa kwani kwa kufanya hivyo watatanua mgogoro; lakini wamegoma na wanasema wao wanatekeleza AGIZO lako wewe Waziri; na kwamba kama kuna anayetakiwa kusitisha hilo ni wewe mwenyewe Waziri.

Mheshimiwa Waziri; kwa barua hii tunapinga upimaji na ujenzi huo unaopora eneo letu halali na tunakuomba usitishe hiki kinachoendelezwa katika eneo letu kwa usimamizi wa DC wa Uvinza.

Kwa barua hii tunakufahamisha yafuatayo;

Tayari Jumapili tarehe 4/12/2022 kwenye ibada takatifu iliyohusisha waamini wote wa makanisa ya Uvinza tumewatangazia kuwa Mkuu wa Wialaya ya Uvinza Ndugu. Hanafi H. Msabaha anaonesha wazi chuki kwa KANISA KATOLIKI.

Tutatoa matangazo na nyaraka zote zinazohusu jambo hili kwenye vyombo vya habari ili jamii ya waTanzania ifahamu ukweli.

Kanisa sasa tunaandaa waraka maalumu utakaosomwa hadharani kwenye makanisa yote Mkoa mzima wa Kigoma kuwafahamisha Wakatoliki wote wa Mkoa mzima wa Kigoma kuwa CCM imetumia nguvu ya Serikali kupora mali za kanisa Katoliki.

Kanisa tumeunda kamati maalumu itakayotembea mkoa mzima wa Kigoma kufafanua juu ya dhuluma hii tuliyofanyiwa na CCM.

Kanisa tumemwandikia Mwenyekiti wa mahusiano mema ya Dini mbalimbali Mkoa wa Kigoma ambaye ni Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Kigoma kumjulisha jambo hili na kumtaka aoneshe mshikamano.

Kanisa tunakusudia hapo baadaye kulipeleka jambo hili mahakamani na kuitaka Mahakama itengue na kubatilisha agizo BATILI na lililo kinyume cha sheria

Tumefikia hatua hii kwa kuwa tumevumilia na kufuatilia jambo hili kwa karibu miaka 20 sasa lakini tumeona wenzetu wana nia mbaya dhidi ya Kanisa. Inatuuma sana kuona wema ambao tumeitendea CCM kuwaruhusu waendeshe shule yao ndani ya eneo la Kanisa kwa miaka zaidi ya 30 bila kutulipa chochote huku sisi tukiendelea kulipia kodi ya ardhi ya kila mwaka, ardhi ambayo inatumiwa na CCM.

Pia inatushangaza na kutuumiza kuona kuwa badala ya CCM kutuandikia hata barua ya asante na kisha kwenda kwenye maeneo yao yasiyo na mgogoro badala yake shukrani yao imekuwa kushirikiana na DC wa Uvinza kujimegea EKARI 10 kutoka ndani ya eneo letu.

Asante kwa kutuelewa. Asante kwa ushirikiano katika mengi. Asante kwa utayari wa kushughulikia jambo hili katika ukweli na haki kama ambavyo mmekuwa mkifanya katika mambo mengi. Tunakutakia Baraka za Mungu katika shughuli zako za kumtumikia Mungu na Taifa katika kutoa huduma kwa watanzania na wale wanaoishi Tanzania.

Pamoja katika huduma kwa jamii na katika utumishi.

Nakala:
Katibu Mkuu wa CCM Taifa
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma
RSO – Kigoma
RPC – Kigoma
Mkuu wa Wilaya ya Uvinza
Kamishna Msaidizi wa Ardhi-Kigoma
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kigoma
Katibu wa CCM Mkoa wa Kigoma.
 
Tumsifu Yesu Kristu.

Ebr 13:14​

Maana hapa hatuna mji udumuo, bali twautafuta ule ujao.

CCM ifike mahali ilipe kanisa stahiki yake.

Kwanini kuwasumbua waliowekwa kuponya Roho za watu washinde mahakamani?
Wanaponya roho za watu au wanakula sadaka tu!!?..wao wananona waamini tunafubaa kila uchao
 
Mkuu wa Wilaya unachokitafuta kwa Wakristo utakipata.Nasisitiza Wakristo,siyo wakatoliki pekee,maana hapa ni mgogoro wa Dini,ambao Waanglican Walutheran pia madhehebu mengine ya Wakristo hawatakaa kimya kuona Wakristo wenzao wananyanyaswa kwa kudhulumiwa.Mkuu wa Wilaya tambua Kanisa catholic halijawahi shindwa kwenye mapambano yoyote.Na nikuhakikishie,Mkeka ujao haumo kwenye madaraka
 
Kila siku tunasema na kuandika kuwa CCM ni genge la wazulumaji,waongo,mafisadi,washirikina,wazinzi,waasherati.

Huu uporaji wa CCM upo maeneo mengi hapa nchini, ni kwa vile tu wao ni "genge dola" ndio maana wananchi na taasisi zinaogopa kuyaweka hadharani maovu yao.

Hapa kwa RC, naamini hili genge limeingia "cha kike".
 
Mkuu wa Wilaya unachokitafuta kwa Wakristo utakipata.Nasisitiza Wakristo,siyo wakatoliki pekee,maana hapa ni mgogoro wa Dini,ambao Waanglican Walutheran pia madhehebu mengine ya Wakristo hawatakaa kimya kuona Wakristo wenzao wananyanyaswa kwa kudhulumiwa.Mkuu wa Wilaya tambua Kanisa catholic halijawahi shindwa kwenye mapambano yoyote.Na nikuhakikishie,Mkeka ujao haumo kwenye madaraka
Serikali baada ya kujaa waislamu tupu wameanza kuchokoza wakristo
 
Wiki chache zilizopita si nilisikia kwamba shule inabolowa ili kurudisha ardhi kwa wenyewe (wakatoliki) au nilielewa vibaya?
Anayefahamu anifafanulie hapa
 
Back
Top Bottom