Kesi ya Mirathi ya Dkt. Likwelile: Vicky Kamata ashindwa, mahakama yasema ndoa yao haikuwa halali

Nobunaga

JF-Expert Member
Mar 22, 2019
1,169
4,985
Vicky Kamata ameungukia pua kwenye kesi ya mirathi ya aliyekuwa mume(danga) wake Dr. Servacius Beda Likwelile. Mahakama imesema ndoa hiyo haikuwa halali kwa sababu Dr. Likwelile alikuwa ameoa hapo mwanzo na hajawahi kutalikiana na mke wake.

Hivyo ndoa ya Vicky Kamata haikuwa halali na hivyo hahusiki kwenye mgao wa mali za marehemu, warithi halali ni watoto wake na wengine waliomo kihalali.

======

"The late Dr. Servacius Beda Likwelile died intestate on 19th February 2021. Since his demise, his estate, however, has never been peaceful. Before this court was a legal battle between his children and Vicky Paschal Kamata styled as his legal wife"

IT IS HEREBY ORDERED THAT:

i. The caveat is fails.

ii. That the caveator Vicky Paschal Kamata was not the legally married to the deceased.

iii. That the properties listed in the petition should not be excluded from the estate of the deceased.

iv. That the petitioner Raymond Babu Likwelile is appointed to administer the estate of the deceased.

v. That, before letters are issued to him, he should comply with rule 66 of the Probate and Administration Rules, by providing the administration bond to be twice the gross value of the estate, which has been estimated at 4 billion. This is to be done in 14 days from the day of this judgement.

vi. No order as to costs.

1.jpg
2.jpg
3.jpg



HABARI ZAIDI..

FB_IMG_1695209906681.jpg

Mahakama yakataa Vick Kamata ‘kumiliki’ mali za Sh4 bilioni, yasema hakuwa mke halali wa Likwelile

Na Daniel Mjema


Jumatano, Septemba 20, 2023


Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imelikataa pingamizi la mbunge wa zamani wa viti maalum (CCM), Vicky Kamata la kupinga mtoto wa ‘mumewe’, asiteuliwe kuwa msimamizi mirathi na mali za marehemu zenye thamani ya zaidi ya Sh4 bilioni.

Dar es Salaam. Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imelikataa pingamizi la mbunge wa zamani wa viti maalum (CCM), Vicky Kamata la kupinga mtoto wa ‘mumewe’, asiteuliwe kuwa msimamizi mirathi na mali za marehemu, Dk Servacius Likwelile zenye thamani ya zaidi ya Sh4 bilioni.

Machi 19, 2016, Vicky Kamata aliyekuwa mbunge kwa vipindi viwili vya Bunge la 9 na Bunge la 10, alifunga ndoa na aliyekuwa katibu mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dk Servacius Likwelile ambaye, alifariki dunia Februari 19, 2021.

Katika hukumu ya shauri la kuomba kuwa msimamizi wa mirathi ya Dk Likwelile iliyofunguliwa na mwanae, Raymond, iliyotolewa Septemba 15, 2023, na Jaji Augustine Rwizile, amesema Vicky hakuwa mke aliyeolewa kihalali na marehemu.

[https://www]

Kwa hiyo Mahakama imeamuru mali ambazo Vicky alikuwa akipinga kuingizwa katika orodha ya mali za marehemu akidai ziliingizwa kimakosa, zijumuishwe katika orodha ya mali za marehemu.

Mali hizo ni nyumba iliyopo kiwanja namba 116 iliyopo Mbweni, Kinondoni jijini Dar es Salaam ambayo alisema walichuma pamoja na nyumba mbili zilizopo huko Mpiji Magoe jijini humo kwenye eneo lenye ukubwa wa hekari 9.5 ambayo alidai ana hisa asilimia 50.

Mbali na hizo, ipo nyumba viwanja namba 387 na 389 iliyopo kitalu D Sinza iliyopo kwa jina lake, nyumba iliyopo Kibamba kwa jina la mtoto wake Gloria Likwelile na viwanja namba 318,319,320 na 321 vilivyopo Mpigi Magoe Ubungo.

Viwanja hivyo vinamilikiwa na kampuni ya Beda Group Limited na Beda Farms Limited ambavyo Vicky alidai kuwa na asilimia 50 ya hisa na pia alipinga gari aina ya Toyota Prado namba T731 CQR na pikipiki Toyota namba MC 588 AHT.

Katika hukumu hiyo iliyopatikana katika mtandao wa mahakama jana Jumanne, September 19, 2023, mtoto wa marehemu aitwaye Raymond Likwilile ameteuliwa kuwa msimamizi wa mirathi na atatakiwa kabla ya kupewa barua, atimize takwa la kanuni namba 66 la mirathi.

Jaji Rwizile alisema tangu kufariki kwa Dk Likwelile familia yake haijawahi kuwa na utulivu ambapo kuliibuka vita ya kisheria kati ya watoto wa marehemu na Vicky aliyekuwa akionekana mke halali wa ndoa wa marehemu.

Hata hivyo, Jaji alisema kwa upande wa pili, familia ya marehemu walikuwa wakimtuhumu mbunge huyo wa zamani kama mtu aliyejiingiza katika maisha ya baba yao kwa malengo binafsi na alikuwa hawara na hakuwa mke halali.

Pingamizi la Vicky lilikuwaje

Katika pingamizi la mbunge huyo wa zamani alikuwa amemtuhumu Raymond kugushi nyaraka.

Vicky alidai mtoto huyo wa marehemu aliidanganya Mahakama kwa kuwasilisha muhtasari uliogushiwa wa kikao cha familia na kujiwakilisha mwenyewe kuwa ndiye aliyeteuliwa msimamizi wa mirathi bila kubainisha aliteuliwa pamoja naye.

Kwamba muombaji huyo alisambaza katika mitandao ya kijamii maandiko ya kashfa dhidi yake, jambo ambalo lilisababisha wawe katika mahusiano mabaya na kushindwa kubadilishana taarifa zozote na pia hastahili kuwa msimamizi.

Pia, alidai muombaji huyo kwa makusudi na akiwa na nia mbaya aliondoa jina lake (la Vicky) katika orodha ya wanufaika wa mali za marehemu na kwamba pingamizi lake lina taarifa zinazothibitisha atambagua kama atateuliwa.

Akaongeza kudai muombaji huyo sio mtu mwaminifu ambaye atakusanya na kugawa mali za marehemu bila upendeleo na atahodhi mali hizo kwa kisingizio kuwa marehemu ni baba yake hivyo akaomba yeye ndio ateuliwe msimamizi.

Mabishano ya ndoa, mali

Wakili Nkalani aliyekuwa akimwakilisha mtoto wa marehemu, alisema isingewezekana kuwepo kwa ndoa halali kati ya Vicky na marehemu kwa kuwa marehemu alikuwa na ndoa ya kikristo na Mary Ibrahim tangu mwaka 1986.

Ndoa hiyo ilidumu hadi Aprili 26, 2020 ambapo Mary alipofariki dunia na kwa kuwa ndoa ya wawili hao haikuwahi kuvunjwa na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita) wamethibitisha hapajawahi kuwepo ndoa baina ya Vicky na marehemu, cheti cha ndoa alichotoa Vicky kimeghushiwa.

“Hii ndio sababu, katika uchunguzi wa Rita, ilitolewa hoja kuwa mpingaji (Vicky) alitakiwa kurejesha cheti cha kifo (cha Likwelile) alichokipata isivyo halali kwa kujifanya ni mke halali wa marehemu,” alieleza wakili huyo kwenye hoja zake.

Wakili huyo alieleza muombaji (Raymond) ndio aliyeteuliwa kusimamia mirathi na kwamba katika kikao cha familia, Raymond na Vicky waliteuliwa kuwa wasimamizi lakini baadae walibaini kuwa Vicky hakuwa mke halali wa ndoa.

Kuhusu hoja ya kugushiwa kwa mihtasari, wakili huyo alisema ni kweli kikao cha familia kiliketi Aprili 14, 2021 na kuwateua Raymond na Vicky kuwa wasimamizi lakini hiyo ilitokana na Vicky kufanya udanganyifu uliowafanya waamini ni mke.

“Kikao kilikuwa halali na ‘minutes’ ziliandikwa na kusainiwa na wanufaika wote wa mali za marehemu waliohudhuria. Muhtasari ulipatikana kihalali kwa kuwa ulikubaliwa na wanufaika wote isipokuwa Vicky ambaye si mke halali,” alisema.

Kuhusu mali alizoziorodhesha, wakili huyo alisema Vicky hakuwasilisha kielelezo chochote mahakamani kuthibitisha ama ni mali ya wanandoa ama ana maslahi nazo hivyo Mahakama ilitupe pingamizi hilo.

Akijibu hoja hizo, wakili Alex Balomi aliyekuwa akimtetea Vicky alisema Aprili 11, 2021, kikao cha familia kiliketi ambapo Raymond na mteja wake walitakiwa kuomba mahakamani kwa pamoja, barua ya kuteuliwa kuwa wasimamizi.

“Lakini kwa mshangao wa anayepinga (Vicky) alishangaa muombaji (Raymond) kwa siri aliwasilisha maombi ya kupatiwa barua ya kuteuliwa kuwa msimamizi wa mirathi ya marehemu bila mpingaji yaani Vicky,”alisema wakili huyo.

Kulingana na maelezo ya mbunge yaliyowasilishwa kortini na wakili wake ni kwamba marehemu ameacha mjane ambaye ni yeye Vicky Kamata, Masuria (concubines) 7 na watoto 7 na ilisisitizwa kuwa wengine walizaliwa nje ya ndoa.

Kuthibitisha yeye ni mke halali wa ndoa, Vicky aliwasilisha cheti cha ndoa kilichotolewa na Rita Januari 30, 2016 chenye namba 0580353 na kwamba hata Ofisa wa Rita hakuthibitisha kama ndoa hiyo haikuwepo kwenye vitabu vyao.

“Vicky habishi kwamba marehemu na Mary walifunga ndoa Desemba 5, 1986 kama ushahidi ulivyotolewa na kwamba alifariki Aprili 26, 2020. Kitu (Vicky) anachokanusha ni kuwa na ufahamu wa uwepo wa ndoa au talaka,”alisema.

“Yeye amekuja kukionea cheti cha ndoa baina ya Mary na marehemu hapa mahakamani,” alisema na kuongeza amekuwa katika ndoa ya mke mmoja na hakuwahi kufahamu kama alikuwa na ndoa nyingine.

Alieleza kabla ya ndoa, taratibu zote za kimila zilifanyika na wawili hao waliishi katika paa moja kwa miaka saba, kwa maana miaka miwili kabla na miaka mitano baada ya kufunga ndoa katika kanisa la Deliverance and Restoration, Arusha.

Aliendelea kutoa hoja kuwa mahari ililipiwa kwa Sh1.6 milioni na ndoa ilisherehekewa huko Tuliani mbele ya ndugu, familia na marehemu mwenyewe na wakaiomba Mahakama itamke kuwa ndoa baina ya wawili hao iliku halali.

Uamuzi wa Mahakama

Akichambua hoja iwapo Vicky alikuwa na ndoa halali na Dk Likwelile, Jaji Rwizile alisema ushahidi unaonyesha marehemu alifunga ndoa ya kikristo na Mary mwaka 1994 katika Kanisa Katoliki la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Upo ushahidi wa cheti cha ndoa chenye namba 00966259, lakini kwa upande mwingine, Vicky Kamata alisema aliolewa na Dk Likwilile ndoa ya kikristo Januari 30, 2016 Jijini Arusha na kuwasilisha cheti cha ndoa namba 0580353.

Jaji alisema kwa mujibu wa vifungu 10(a) na (b) cha Sheria ya Ndoa ya Tanzania (LMA) sura ya 29 kama ilivyofanyiwa marejeo na Bunge mwaka 2019, zipo ndoa za aina mbili tu Tanzania ambazo ni ndoa ya wake wengi na ndoa ya mke mmoja.

“Kwa hiyo tunaweza kusema kwa dhati kwamba ndoa ya kikristo ni ya mke mmoja kwa hiyo ni kati ya mwanamme na mwanamke. Kwa hiyo ni kosa kwa mwanaume au mwanamke aliyeko kwenye ndoa kuoa wakati ndoa nyingine iko hai,” alisema.

“Kwa maoni yangu hakuna ushahidi (Vicky) aliolewa na mwanamme mwingine baada ya kuoana na marehemu. Lakini hakuna ushahidi Vicky na marehemu walipoona 2016, ndoa kati ya marehemu na Mary ilikuwa imevunjwa kwa talaka au kifo,” alieleza Jaji.

“Kwa hiyo ni jambo lililo wazi kwangu, kwamba kukosekana kwa ushahidi wa talaka kati ya Mary Ibrahim na Servacius kipindi Vicky Kamata anaolewa, marehemu hakuwa na mamlaka ya kisheria kuoa,”alieleza Jaji na kuongeza kusema kuwa;-

“Inatosha kusema kuwa kama wawili hawana mamlaka ya kuoana, inafikiriwa hakuwezi kuwa na upendeleo dhidi yao. Haijalishi wameishi miaka mingapi. Ukweli kuwa waliishi kwa miaka saba na kufahamika kwa umma haiwezi kuokoa jahazi,”

“Imeelezwa kuwa kulikuwa na ndoa (baina ya Vicky na Servacius) lakini imekanushwa na imeelezwa cheti cha ndoa hicho hakipo na mchungaji (minister) aliyedaiwa kufungisha hiyo ndoa amekanusha kufungisha ndoa hiyo,” alieleza Jaji Rwizile.

“Yote kwa yote, iwe aliolewa au hakuolewa 2016, kwa kuwa imeshaelezwa, ndoa hiyo ilifungwa na pande mbili ambazo hazikuwa na mamlaka ya kisheria kuoana basi inahesabika ndoa hiyo ni batili kisheria,” alisema.

“Kwa hiyo nasema hakukuwa na ndoa kati ya marehemu Dk Servacius na Vicky Kamata. Walichofikiri kuwa ilikuwa ni ndoa halali baina yao ilikuwa ndoa ya uongo hivyo ni batili. Kwa hiyo Vicky Kamata hakuwa mke bali Masuria kama wale saba,” alisema

Kwa mujibu wa Kamusi ya Kiswahili ya Baraza la Kiswahili la Taifa, toleo la 2, maana ya neon suria ni mjakazi ambaye wazazi wake humfanya kuwa mke bila kufuata taratibu za sheria za ndao.

Katika uamuzi wake, Jaji alisema hoja ya pili kwa mujibu ilikuwa ni kumteua msimamizi wa mirathi ambayo hiyo ni mamlaka ya mahakama hivyo muombaji ni mtoto wa damu wa marehemu kulinganisha na anayepinga ambaye aliishi tu kama hawara au mtegemezi.

“Inatosha kusema maslahi yake (Vicky) kwenye mali ni ya mbali sana. Bila kupoteza muda na bila kumung’unya maneno, muombaji (mtoto wa marehemu) ndio bora na ndiye anastahili kuteuliwa kama msimamizi wa mirathi,”alisema Jaji.

Kuhusu madai ya muhtasari, Jaji alisema amepitia ushahidi wa pande zote mbili na hakuna mahali panapoonyesha mihtasari hiyo ya kikao cha familia iligushiwa na haoni ushahidi wowote kuwa muhtasari huo haukupatikana kihalali.

Jaji alisema Vicky Kamata alikuwa na wajibu wa kuthibitisha kuwa mali zilizoorodheshwa na muombaji ni za kwake na si za mtu mwingine ili sasa zisijumuishwe kwenye mali za marehemu na bila hilo haiwezi kuhisia tu kuwa sio za marehemu.

“Ukweli katika kesi hii ni kwamba ili kuthibitisha kuwa mali hizo walichuma pamoja hiyo ingefanyika katika masuala ya wanandoa ambapo wanandoa wana nafasi ya kuthibitisha namna zilivyopatikana. Mahakama hii sio wajibu wake,”alisema Jaji.

Jaji alisema kiufupi, haijaweza kuthibitishwa mahakamani hapo kwamba mali hizo zilizoorodheshwa na Vicky Kamata katika pingamizi hilo kuwa sio sehemu ya mali za marehemu bali ni mali ambazo ana maslahi nazo au walichuma pamoja.
 

Attachments

  • Likwelile_Vicky Kamata Judgment and Decree.pdf
    37 MB · Views: 5
Back
Top Bottom