Kauli ya Mbowe ya kutoshirikiana na vyama vingine yaibua mazito

benzemah

JF-Expert Member
Nov 19, 2014
1,504
3,034
Kauli ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kuhusu nia ya chama hicho kutoshirikiana na vyama vingine imezua mjadala kwa baadhi ya vyama vya siasa huku baadhi vikidai inatokana na ushirika wa chama hicho na CCM katika maridhiano na vingine vikiiunga mkono.

Mjadala huo umetokana na kauli aliyoitoa Mbowe juzi wakati akihutubia hafla ya kuwapokea wanachama karibu 400 kutoka CUF, kuwa “ingawa Chadema awali iliamini katika kuunganisha vyama, kwa sasa haitafanya hivyo badala yake itatekeleza wajibu wake kwa kuunganisha wanachama na wananchi wenyewe.”

Hoja yake hiyo inatokana na alichokifafanua kuwa, safari ya ushirikiano na vyama vingine, imekuwa ikiingia misukosuko kwa kuwa baadhi ya vyama baadaye vilikengeuka.

Kauli za vyama
Akizungumza na Mwananchi jana kuhusu kauli hiyo ya Mbowe, Makamu Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, Joseph Selasini alisema kwa uzoefu wa madhila yaliyoipata NCCR Mageuzi wakati wa ushirikiano wa Ukawa, chama hicho hakitarudia makosa hayo.

Hata hivyo, alisema “hakuna chama kilichosajiliwa kubebwa na kingine, kila kimoja kinapaswa kusimama chenyewe.”

Kwa mujibu wa Selasini, uzoefu unaonyesha muungano wa vyama nchini haulengi kuiondoa CCM madarakani, bali kuviangamiza vingine akirejea mwaka 2015 wakati wa Ukawa.

“Muungano ule ulilenga kiviua vyama vingine na Chadema ndiyo ilikuwa namba moja kuvimaliza vyama vingine, NCCR Mageuzi haitarudia makosa yake,” alisema Selasini ambaye mwaka 2015 aligombea na kushinda ubunge wa Rombo kupitia Chadema.

Hata hivyo, alisema kuungana si turufu ya ushindi wa upinzani nchini bali kinachohitajika ni sera nzuri na wananchi ndiyo watakaoamua.

“Mnaweza mkaungana hata vyama vingapi mkikosa hoja CCM itawashinda, mnaweza mkafanya lolote msiposhawishi wananchi CCM itaendelea kusalia madarakani,” alisema Selasini.

Hata hivyo, Selasini alisema Chadema imesema hivyo kwa sababu tayari “inaye mshirika wake mwenye dola”.
“Hawataki kushirikiana na vyama vingine vya upinzani kwa sababu wanaye mshirika wao maalumu ambaye ndiye mwenye dola,” alisema Serikali.

Naye Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe alisema shabaha ya chama chake ni kujenga Taifa na masilahi ya wote na si kuwaza majimbo.
“Sisi tunawaza nchi nzima. Tunawaza kubadili siasa zetu ili ziwe za kiukombozi na si za kugawana vipande vya nchi,” alisema.

“Kama mnataka kuleta mageuzi nchini, ina maana ni lazima mkiondoe chama kilichopo madarakani na hakiwezi kuondoka kwa tambo za operesheni bali kwa mawazo yanayokonga nyoyo za watu,” alisema.
Alisema “tunawapa changamoto wenzetu waeleze wanaleta nini sokoni tushindane kwa mawazo ya kuunganisha nchi si mawazo ya kugawana au kutogawana majimbo,” alisema.

Mwanasiasa mwingine aliyezungumzia suala hilo ni Tozy Matwanga, Katibu mkuu wa NLD aliyesema chama hicho hakina hamu tena ya kushirikiana na Chadema kwa kuwa kiliathirika na muungano uliotokea mwaka 2015. Alisema kwa kilichotokea katika muungano huo ni vigumu kwa upinzani kurudia kushirikiana.

Ni muhimu kuungana
Mbali na maoni ya wanasiasa hao wa vyama tofauti, mwanasheria na mchambuzi wa masuala ya siasa, Dk Onesmo Kyauke alisema kwa siasa za Afrika na Katiba, hasa ya Tanzania, hapana budi kwa upinzani kushirikiana ili kushika dola.

“Kama upinzani unataka kushika dola kwanza inabidi ukubali kumaliza tofauti zao ndogo ndogo kisha waunganishe nguvu kushindana na CCM,” alisema.

Dk Kyauke alisema hakuna tija ya kuwa na utitiri wa vyama vinavyoishia kugawana kura hivyo ni vema viungane kuzikusanya pamoja.

Alirejea uchaguzi wa mwaka 2015 ambao upinzani ulifanya vizuri kuliko wakati mwingine wowote, akisema hayo ni matunda ya kuungana.

“Hakuna namna ya kuiondoa CCM kama hawataungana, bahati nzuri sasa hivi kuna mabadiliko ya sheria yanaruhusu kuwepo mkataba, mnaungana kwa mkataba unaoeleza nani atapeleka wapi mgombea na mtagawanaje ruzuku, hili litapunguza dhuluma,” alisema.

Alichosema Mbowe
Katika hotuba yake Mbowe alifafanua kile anachomaanisha akisema “Huko nyuma tuliamini sana kwenye kuunganisha vyama na Chadema hata kwenye Katiba yetu ya chama kuna kipengele kinazungumza kwamba Chadema ni chama kitakachojitahidi kuunganisha vyama.

“Lakini azma yetu hii mara nyingi imekutana na misukosuko kwa sababu wenzetu mbele ya safari hukengeuka, kwa hiyo hatimaye Chadema tumesema wajibu wetu tutaufanya si kwa kuunganisha vyama, tutafanya wajibu huu kwa kuunganisha wanachama wenyewe na wananchi wenyewe,” alisema.

Kwa mujibu wa Mbowe, badala ya kupoteza muda wa kupatana na vyama visivyo na dhamira moja, Chadema itazunguka kila kijiji, mtaa, kitongoji na kata kuliandaa Taifa na siku zijazo kwa kuwa wananchi wanahitaji chama mbadala na umoja.

Kauli hiyo ya Mbowe na hizo za wapinzani wa vyama vingine zinakuja wakati uzoefu katika baadhi ya mataifa ya Afrika unaonyesha mafanikio ya upinzani kuving’oa vyama tawala madarakani hutokana ama na muungano au ushirikiano na vyama vingine.

Kenya ni moja ya nchi ambayo muungano wa vyama uliupa upinzani nguvu ya kushika dola kwa mara ya kwanza mwaka 2002 baada ya chama tawala cha Kanu kuongoza kwa miaka 40. Hata hivyo, muungano wa vyama katika chaguzi za Kenya unapata baraka za Katiba inayoruhusu ushirikiano huo.

Vilevile, muungano wa vyama vya upinzani ndio uliomwezesha Rais Felix Tsishekedi wa Jamhuri ya Demokrasi ya Congo kuingia madarakani mwaka 2018.

Kwa hapa nchini, nguvu ya muungano wa upinzani, inathibitika katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 nchini, ambao pamoja na CCM kuendelea kusalia madarakani, vyama vya upinzani vilipata ushindi katika majimbo mengi.

Katika uchaguzi huo, Chadema ilipata wabunge 34 ambao ni wengi zaidi ya miaka yote, huku CUF kikipata wabunge 32, CCM wabunge 188 na ACT Wazalendo mbunge mmoja. Anguko lilikuwa kwa NCCR Mageuzi pekee iliyopata mbunge mmoja, ilhali awali ilikuwa na wanne iliowapata katika uchaguzi wa mwaka 2010.

Katika uchaguzi wa mwaka 2015, kulikuwa na makubaliano ya baadhi ya vyama kwamba kile chenye mgombea mwenye nguvu eneo fulani ndicho kitakachomsimamisha mgombea wake kwenye jimbo husika.

Baadaye mambo yalikwenda tofauti baada ya vyama hivyo, kujikuta kila kimoja kikisimamisha mgombea katika majimbo husika, mfano Segerea, Kigamboni, Mbarali, Geita Vijijini, Gairo, Mtwara, Mpwapwa, Geita Mjini, Mwanga na Serengeti.

Chanzo: MWANANCHI
 
Sioni umuhimu wa vyama kuungana kuelekea kupiga kura.

Ni muhimy vikaungana endapo matokeo ya kura yanahitaji jambo hilo.
 
Back
Top Bottom