Kama taifa tuna uhakika kile klilichomo kwenye mitaala yetu kuanzia shule za msingi hadi vyuoni vinakidhi matarajio ya taifa?

Quartz360

Senior Member
Mar 27, 2023
124
302
Kuna muda nakaa najiuliza ni nani alaumiwe katika hili?

Toka ukoloni mpaka sasa mfumo wa elimu kwa nchi za kiafrika umeweza kupitia vipindi mbalimbali vyenye milima na mabonde, ambapo kwa kiasi kikubwa mfumo wa ufundishaji na ujifunzaji hauna utofauti sana na mfumo uliotumiwa na wakoloni enzi hizo.

Kwa maana lengo la serikali ya kikoloni ilikuwa ni kupata waafrika wachache tu watakaowasaidia kufanya shughuli mbalimbali katika ngazi za chini.

Japo mabadiliko kadhaa ya mitaala yamefanyika, lakini bado ubora wa elimu yetu haukidhi mahitaji ya dunia ya sasa.

Nachelewa kuamini kama nchi za ulaya zinasoma historia ya Afrika kama sisi tunavyosoma historia yao, lakini ni Afrika tunapofundishwa mambo ya Dictatorship in Germany, Socialism in Russia, Pipeline transport in Norway na Rubber production in Sri Lanka. Sijajua kama huyu kijana anayeishi Namtumbo,Kakonko,Ngara, Ushirombo, Nyang’hwale, Nanjilinji, Nachingwea, Bariadi ama Urambo atafaidika na hivyo vitu pindi atakapomaliza masomo yake.

Siamini pia ya kwamba tangu tuanze kuzalisha mainjinia katika nchi yetu bado wataalamu hao wazawa hawana uwezo wa kuendesha miradi mikubwa katika taifa letu, Napata mashaka juu ya kile walichojifunza chuoni.

Siamini kama ni kweli kozi zetu zinazofundisha masuala ya teknolojia zimeshindwa kuzalisha wataalamu walio bobea katika masuala ya teknolojia wenye uzalendo na ari ya kuchochea ukuaji wa teknolojia katika taifa letu.

Siamini pia kama elimu yetu ya chuo kikuu imeshindwa kuleta mtazamo chanya kwa vijana kuweza kuwa na fikra tunduizi zenye mawanda thabiti ya kuleta mabadiliko katika taifa letu.

Leo ni kawaida kuona mhitimu aliyesomea masuala ya biashara analia kuhusu mtaji, ni kawaida kukuta mtu aliyesomea IT anafanya biashara ya duka, Ni kawaida kumkuta mtu aliyesomea masuala ya uhasibu anaendesha bodaboda, ni kawaida kumkuta pia mtu aliyesomea masuala ya kilimo amefungua kibanda cha kuchoma chipsi.

Si kwamba kazi wanazofanya hazifai, la hasha bali nawaza miaka 3/4/5 waliyotumia chuoni kujifunza taaluma hizo ilikuwa na lengo gani?

Nawaza kama ni kweli hawa vijana walienda kusomea kozi wanazozipenda, ama tangu utoto wao walitamani kusomea kozi hizo, nashindwa kuamini kama vitu vyote walivyojifunza vimeshindwa kuwapa fikra chanya za kuweza kufanya mabadiliko makubwa katika taifa lao.

Nadhani matokeo ya mitaala yetu tunaweza kuyaona bayana kwa kile kinachoendelea kwa vijana wetu kwa sasa punde tu baada ya kuhitimu masomo yao, sidhani kama taifa huwa tunafanya uchambuzi wa mitaala yetu mara kwa mara.

Kila mwaka tunapokea makontena mapya ya wahitimu kutoka vyuoni lakini hatuoni matokeo ya hao wahitimu kama taifa.

GPA za maana zimepatikana huko vyuoni lakini matokeo yake mtaani yanakuwa ni hafifu kiasi cha kutoamini katika usomi wao.

Vijana wengi siku hizi umahiri umekuwa ni kikwazo kwao, ubunifu umekuwa ni changamoto na uwezo wa kujitegemea wao wenyewe umekuwa ni mdogo, na je? pale IAA, MIPANGO, UDOM, MZUMBE, SUA, UDSM, SAUT, IFM, CBE, MAKUMIRA, TIA, TEOFIRO, JORDAN, MUM, SAINT JOHN, ARDHI, KIUT n.k walienda kufanya nini?.

JE, Shida ni wazazi,serikali ama wahitimu wenyewe? Kila mtu ana mtupia jiwe mwenzake.

Serikali inasema vijana waache uvivu wajiajili, Wahitimu wanaungana na wazazi kuilaumu serikali ya kwamba haitoi ajira, hakuna mazingira wezeshi ya wao kuweza kujiajili na wakati mwingine pia wazazi huwalaumu watoto wao pindi hali ya utegemezi inapokuwa ni kubwa.

Kama taifa tuna uhakika kile klilichomo kwenye mitaala yetu kuanzia shule za msingi hadi vyuoni vinakidhi matarajio ya taifa katika siku za usoni kuwa na wasomi wenye uelewa mpana,ubunifu na fikra chanya za kuweza kulifikisha taifa katika nchi ya ahadi?

Kama taifa tulitafakari hili.

#MyCountryPeople.
 
Back
Top Bottom