Jirani yangu wa kule Goba hakuwa mtu wa kawaida

SteveMollel

JF-Expert Member
Jul 12, 2015
8,449
23,774
Jirani Yangu wa kule Goba Hakuwa Mtu wa Kawaida.

Sasa ni miaka miwili imepita, nimehamia na ninaishi kwengine, lakini yale ya kule Goba nayakumbuka vema kana kwamba yametokea jana yake, na huenda mambo hayo nikayakumbuka hata na milele maana ni moja ya visa ambavyo vilinishangaza sana.

Mwaka 2020 mwanzoni, mimi na familia yangu tuilihamia Goba Kontena, eneo la Mashuka, tukitokea Mbezi Beach, Makonde, kwasababu ya kutafuta eneo kubwa zaidi kukimu ukubwa wa familia. Hapo Goba tukapata mahali pazuri, nyumba kubwa ya wastani ambapo ndani yake tulikuwa tunakaa familia tatu, kila mmoja na mlango wake japo tulikuwa tunaingilia na kutokea mlango mmoja mkubwa uloshika korido, mlango wa grill, kwa nje kulikuwa na wapangaji wengine watatu kwa ujumla ambao walikuwa wanaishi kwenye vyumba vimoja vimoja, kwasababu hiyo basi humu tulimokuwa tunaishi sisi pakawa panajulikana kwa jina la 'nyumba kubwa'.

Nyumba zote hizi zilikuwa ndani ya uzio wenye geti moja dogo na lingine kubwa ambalo kukaa kwangu kote hapo sikuwahi kuliona likifunguliwa lote kwasababu njia ilikuwa imebanwa na ujenzi mwingine, usingeweza kuingiza gari hapo labda pikipiki na baiskeli tena kwa kujibanabana.

Uzuri hakukuwa na mtu mwenye usafiri wa gari, kulikuwa na watu watatu wenye pikipiki tu, mmoja ni bodaboda ambaye alikuwa akirejea usiku mzito nyumbani, mara kadhaa akija asubuhi kabisa pamekucha, saa kumi na mbili au saa moja, wa pili alikuwa ni mfanyabiashara ambaye alikuwa anatumia pikipiki yake kwaajili ya shughuli zake za dukani na wa tatu alikuwa ni mimi mwenyewe, nilikuwa nautumia pikipiki kunipeleka na kunirejesha kazini.

Wote tulikuwa tunapaki katika uwanja mdogo wa nyumba hii, lakini tofauti na wenzangu, pikipiki yangu ilikuwa imeharibika 'lock' kwenye swichi ya funguo hivyo naliweza kuzima tu lakini sikuwa na uwezo wa kuilock pikipiki, swala hilo likawa linanipa mawazo sana juu ya kuibiwa usafiri wangu kwani nilikuwa napaki karibu na geti dogo ninaloingilia na geti hilo halikuwa madhubuti kabisa, limetenguka kwa chini na bati lake la chuma limeshikwa kutu sana, zaidi tulishakuwa na matukio mawili matatu ya wezi kuingia ndani kwasababu ya ufupi wa uzio wetu.

Wanaingia na nyie mpaka mfunguo milango hamuwakuti, wanaruka kama vyura kurukia upande wa pili na kukimbilia korongoni, huko kuna giza totoro hutaweza kuwafuata.

Kwasababu hiyo, mara kadhaa nilikuwa nikichungulia dirishani pale ninapohisi kuna jambo la kutia shaka na hivi mimi nilikuwa mgumu sana wa kupata usingizi nyakati za usiku, jambo hili nililifanya vema. Ningesikia watu wakipita huko njiani, ama wakichota maji nje ama wakienda maliwatoni, japo si kila mtu lakini ilikuwa ni mara kwa mara.

Baada ya mwezi kupita hapo, maisha yakiwa kawaida tu, ndipo tukapata jirani mpya ambaye alihamia kwenye mlango unaofuata baada yangu. Alikuwa ni bwana mmoja mnene mweusi, tulikuja kumfahamu zaidi kwa jina la 'BIGI', alikuwa mtu mwenye maneno machache, sauti yake nyembamba tofauti na mwili wake, na mkewe mfupi mwenye mwili kiasi, rangi yake maji ya kunde, pamoja na mtoto mmoja wa kiume ambaye kwa makadirio alikuwa darasa la nne hivi au la tano.

Nikaendelea kumfahamu zaidi BIG baada ya kukutana naye mara kadhaa barabarani nikiwa narejea nyumbani hivyo nikawa nalazimika kumpatia lifti mpaka home. Katika wiki basi angalau tungekutana mara mbili au tatu, hali hiyo ya kurudi nyumbani pamoja, ikafanya wapangaji wenzangu kudhania mimi na huyu bwana ni marafiki kiasi kwamba mara kadhaa wakawa wananiambia nimfikishie ujumbe kuhusu kulipia zamu za umeme au malipo ya maji, lakini ukweli ni kwamba mimi na wao hatukuwa na tofauti sana, zaidi mimi nilikuwa nakutana naye mara nyingi kuliko wao lakini kukutana naye huko hakukufanya tukawa marafiki wa huyu bwana, angenisalimu na kisha akaketi kwenye pikipiki asiongee neno lingine lolote mpaka tunafika. Ndivyo ilivyokuwa.

"Habari?" Tukionana.

"Asante." Tukiagana.

Nami sikuona taabu wala sikujali, watu hatufanani kama vidole vya mkononi, siku zikaenda mpaka na mwezi hivi, kama sijakosea, tangu wahamie pale.

Nakumbuka baada ya mwezi huo kuisha alikuja mwenye nyumba kusalimu, bila shaka kuna mmoja wa mpangaji alikuwa anadaiwa kodi maana mwenye nyumba alikuwa hapendi kutumiwa pesa kwa njia ya simu, anapendelea cash pekee mkononi, na kwa kawaida yake akifika basi hutaka kusalimu kila mtu, atagonga kila mlango apate kuwajulia hali, mimi binafsi nilikuwa namkwepa maana huwa sipendi maneno yake mengi yasoisha na pia tabia zake za kuanza kukuongelesha mambo ya wapangaji wengine ndo' ilikuwa inan'kera zaidi, lakini siku hiyo sikuwa na namna ya kumkimbia kwani alinikuta nje natazamatazama pikipiki, akanisalimu na kuniuliza habari za hapa na pale kisha akaingia ndani ya nyumba kubwa kwenda kuwagongea wengine.

Mwenye nyumba wetu kwa kabila alikuwa ni Msukuma, alikuwa hawezi kuongea taratibu, akiongea upande wa pili basi hata wewe wa ng'ambo utasikia upende usipende. Hana faragha. Hata kudai kwake kodi ndo' hivyohivyo, hata ukimvutia pembeni ni kujichosha tu.

Alipogonga huko akatoka na kusimama barazani, punde kidogo wakatoka wamama wawili kumsalimu, mama mmoja alikuwa ni mke wa yule jamaa wa dukani na mwingine alikuwa ni yule mke wa BIGI.

Wanawake hawa wote walikuwa wamevalia khanga kifuani na khanga kiunoni kila mmoja, na hapa ndo ikawa mara yangu ya pili kumwona mke wa BIGI tangu amehamia hapa, siku ya kwanza ni ile waloingia na siku ya pili ndo ikawa hiyo, sikuwahi kumwona kamwe hapo katikati, iwe weekend nikiwa nashinda nyumbani au siku ya kazi nikibahatika kurejea na mumewe.

Lakini zaidi, hii ndo' ilikuwa siku yangu pekee niiliyobahatika kumwona mwanamke huyo jua likiwa linawaka kwani siku ile waliyohamia ilikuwa ni majira ya usiku.

Kwa kumtazama harakaharaka nikabaini ana makovu makubwa ya moto mgongoni mwake na kwenye mkono wake wa kuume.

Lakini mbali na hilo, nikiendelea kuwa hapo, nikabaini mwanamke huyo ni bubu, hana uwezo wakuongea. Nilimsikia mwenye nyumba akishangaa kisukuma, "Hiii!" Akamuuliza yule jirani wa muda mrefu, "Huyu hawezi kuongea?"

Yule mama jirani akanyanyua mabega kuashiria hata yeye hajui hayo. Yule mzee akaongeaongea pale haswa na yule jirani mwingine kisha alipomaiza akanifuata na kuniuliza kama nimemeona na yule jirani mpya, yaani BIGI, nikamwambia hapana, mara yangu ya mwisho kumwona ilikuwa ni siku mbili nyuma, akaniambia basi nikimwona nimwambie amtafute mwenye nyumba ampatie mkataba wake wa makazi kwani yeye amejaribu kumtafuta kwa njia ya simu pasipo mafanikio. Ni mwezi sasa umepita anaishi kwa mkataba wa maneno tu.

Na sababu iliyomfanya akanambia mimi ilikuwa ni yule jirani mwingine, alimwambia kuwa mimi ndo' mtu ambaye nipo karibu na BIGI, na japo alimwambia mkewe lakini hakuamini kama atakuwa alimwelewa au lah.

Baada ya hapo akaenda kuwagongea na kuongea na wale wapangaji wanaokaa kwenye vyumba vimojavimoja na kisha akaenda zake. Aliponiaga alinisihi nisisahau jambo lake nami nikamwambia nitajitahidi.

Ikaja kesho na keshokutwa, sijamwona BIGI, ikapita mpaka wiki nzima nisimwone jamaa huyo kitu ambacho hakikuwa kawaida, yani nisimwone hata mara moja? Na sijabadili ratiba wala njia? ... Nikajiaminiisha kuwa huenda bwana huyo atakuwa amesafiri. Nilitamani kumuuliza mkewe lakini ningeanzia wapi?

Lakini .... Em ngoja ... Nikajiuliza.

Kama mwanamke huyo alisikia hodi ya mwenye nyumba akatoka mpaka ndani kuja kuonana naye ila hakuweza tu kuongea, inamaanisha alielewa alichoambiwa, basi nikahitimisha kuwa atamwambia mumewe mambo yao wamalizane wenyewe.

Siku hiyo usiku nikiwa nautafuta usingizi kitandani, muda mfupi tu baada ya kuzima TV, nikasikia kana kwamba kuna mtu nje, majira yalikuwa ni saa tisa hivi ya usiku, nje kumetulia sana na sasa nilikuwa na uwezo wa kusikia karibia kila kitu kwani TV iliyokuwa inatoa sauti nilikwishaizima, nikajongea dirishani kuchungulia, sikutaka kupuuzia hisia zangu.

Uzuri ama sijui ubaya, chumba changu cha kulalia kilikuwa na madirisha mawili, moja lilikuwa linatazama kaskazini kulipo geti dogo na kibaraza cha nyumba kubwa ingali lingine lilikuwa linatazama mashariki lilipo tenki kubwa la maji ambalo halikuwa mbali sana na chemba. Huko mashariki ndiko kulikuwa na taa inayoning'inia kwenye ukuta, kule kibarazani taa yake kubwa ilikuwa hafifu, haikuwa na maisha marefu kuzima, kwahiyo taa ya mashariki ndo' ilikuwa inasaidia kumulika mpaka huku mbele kwenye geti dogo na kibaraza japo kiuhafifu.

Hivyo kwakupitia madirisha haya nilikuwa na uwezo wa kuona 'engo' mbili tofauti, kaskazini na mashariki mwa nyumba.

Nilipotazama katika dirisha hili la kaskazini mwa nyumba nikamwona kijana mmoja mfupi akiwa yu peku, amepachika kandambili zake mikononi, ananyata kuelekea magharibi mwa nyumba.

Huko magharibi kulikuwapo na stoo mbili ambazo kuna wapangaji, hususani wale wa vyumba vimojamoja, wanatumia kuwekea vitu vyao kama vile majiko na vyombo kadha wa kadha kwasababu vyumba vyao havitoshi kuhifadhi vitu vingi. Humo ndani si ajabu ukakuta hata unga, mchele, mkaa, mafuta na kadhalika.

Ukivuka stoo hizo ndipo unaenda kukutana na milango ya wapangaji hao, kila mlango ukiwa na grill yake iliyofungwa haswa kwa nyakati hizi za usiku isipokuwa kile chumba ambacho kinakaliwa na yule bodaboda. Chumba hicho huwa kinabaki na grill wazi maana haijulikani yule jamaa atarejea majira gani. Mkewe alikuwa anafanya hivyo ili kumruhusu mumewe kuingia ndani muda wowote atakaorejea, iwe ni usiku mkubwa au hata asubuhi ya mapema. Yeye akirejea ataufungua mlango kwa funguo yake ya ziada kisha atafunga ule wa grill kwa funguo pekee alonayo.

Nilipoona hivyo, nikaenda sebuleni na kufungua mlango wangu taratibu sana. Nilipotoka nikafuata korido kwa kunyata mpaka kwenye mlango wa kutoka kwenye hii nyumba kubwa, hapo nikafungua mlango mdogo kisha nikaanza kutekenya taratibu mlango wa grill ili nipate kwenda nje.

Mpaka hapo sikuwa namwona tena yule jamaa niliyemshuhudia dirishani, niliamini kabisa atakuwa upande ule wa vyumba ambavyo mimi sikuwa na uwezo wa kuviona kwani dirisha langu na hapa mlangoni palikuwa panaishia kuona kwenye stoo tu, huko kwengine ni kona iliyo mbali na macho yangu.

Na shaka langu likawa kwenye ile nyumba ambayo grill yake iko wazi. Mule ndani kuna mwanamke na mtoto mdogo wa miaka michache.

Nilipomaliza kufungua grill ile, kabla sijaisukuma kwanguvu ili niende nje, nikasikia sauti kali ya kike, "mwiziiiiii!" Kufumba na kufumbua nikamwona mtu akipitia kwa kasi kubwa, alikuwa ni yule bwana niliyemshuhudia dirishani, nikasukuma grill na kutoka ndani kwa kasi lakini kabla sijafanya chochote bwana yule akawa ameshauruka ukuta na kuyoyoma kuelekea kule korongoni.

Sikuelewa aliurukaje ule ukuta kwa kile kimo chake, ni kama vile alikuwa na 'spring' kwenye miguu, nilijaribu kufanya kama yeye lakini niliishia kujiumiza tumbo na kurudi chini nikiwa na michubuko ya kutosha mkononi.

Kazi ikabaki tu kusema, "weweee! Wewee! Utakufa mbwa wewe!" Huku nikiwa sina lingine la kufanya.

Muda kidogo karibia kila mtu akawa ametoka kwenye chumba chake kuja kuuliza nini kimejiri kwasababu sauti ya mwizi mwizi iliwashtua toka usingizini, hivyo hapa kukawa na zogo kiasi, kila mtu akisema maoni yake lakini kubwa ni hali imezidi, inabidi mwenye nyumba aongeze hata mistari miwili ya tofali kwenye uzio ili kuongeza urefu wake na pia achomelee lile geti dogo kwa chini kama sio kuweka jipya kabisa.

Wakati hayo yanaendelea, mimi nikafanya kutazama kule kwenye nyumba kubwa, hamaki, nikaona mtu amesimama koridoni karibu na mlango.

Kwasababu ya uhafifu wa ile taa ya barazani, na mtu yule alikuwa amesimama kwa ndani kidogo, hakuwa anaonekana vema, lakini kwa kile kimo chake nikahisi huenda mtu huyo ni yule mke wa BIGI, kwa kujihakikishia nikasogea karibu ili nipate kumwona mtu huyo lakini ajabu aliponiona najongea akakimbia upesi kama mwizi!

Kha! Nikabaki nimehamaki. Akijikwaa je?

Nikadhani nimeona vya kutosha, lakini kumbe ule ndo' ulikuwa mwanzo kabisa wa mengi yajayo, mwanzo wa kuamini mwanamke yule ama tuseme familia ile haikuwa ya kawaida kabisa.

***
Muendelezo soma Jirani yangu wa Kule Goba hakuwa mtu wa kawaida

====
SEHEMU YA 2
SEHEMU YA 3
SEHEMU YA 4
SEHEMU YA 5
SEHEMU YA 6
SEHEMU YA 7
SEHEMU YA 8
SEHEMU YA 9
SEHEMU YA 10
BONUS-A
BONUS-B
BONUS C
SEHEMU YA 11
SEHEMU YA 12
SEHEMU YA 13
 
Jirani yangu wa kule Goba hakuwa mtu wa kawaida - 02

Siku tatu baada ya tukio lile la mwizi, wakati nikiwa narudi nyumbani tokea kazini majira ya jioni ya saa moja, nikakutana na bwana BIGI akiwa amebebelea begi mgongoni. Bwana huyo alikuwa anashuka na njia ya kuelekea nyumbani, nikamsalimu na kumpakia tupate kumalizia safari yetu.

Kama ilivyo ada, nilimpomshusha akasema "Asante" lakini kabla hajaondoka nikampatia ule ujumbe wa mwenye nyumba kuhusu mkataba, akatikisa kichwa chake na kwenda zake ndani. Hakutia neno.

Siku hiyo katika majira ya saa saba hivi usiku, nikiwa bado nipo sebuleni natazama televisheni kabla sijaenda zangu kulala, nakumbuka nilikuwa nikirudia kutazama moja ya filamu yangu pendwa isiyoisha utamu 'TRIANGLE' maana sikuwa na filamu mpya ya kuitazama, ghafla nikasikia sauti ya kike ikipiga kelele fupi! Nikashtuka na kuanza kuhukumu masikio yangu kama yamesikia kitu sahihi ama ni mang'amng'amu ya filamu.

Nikazima sauti ya televisheni kisha nikatega masikio vema, sikusikia kitu tena, kwa kama dakika tatu hivi kukawa kimya kama ilivyokuwa hapo awali, ila nilipotaka kuendelea na filamu yangu tu mara nikasikia mlango unafunguliwa, si mlango wangu bali wa jirani, alafu kidogo mlango wangu ukagongwa - ngo ngo ngo, nikauliza nani? Sikujibiwa, nikasogea na kuufungua mlango, sikuwa na shaka sana maana niliusikia mlango wa jirani ukifunguliwa hivyo niliamini atakuwa ni jirani tu.

Nilipofungua mlango nikakutana uso kwa uso na BIGI, uso wake unachuruza jasho, amevalia bukta na kaushi tu, akaniomba samahani kunisumbua usiku huo mkubwa kisha akanitaka nimsaidie kumpeleka mkewe hospitali kwani hali yake si nzuri, hapo nikaikumbuka ile sauti niliyoisikia, ina maana ilikuwa ni ya mkewe au? Lakini mwanamke huyo si bubu? Ama ...

Hakukuwa na muda wa kutafakari maana hali yenyewe ni ya dharura, nikarejea ndani kuvaa nguo kamili kisha nikaufungua mlango na kuendea pikipiki nje kuwangoja wahusika, kidogo akatokea BIGI akiwa amembeba mke wake kama mtoto mkononi, nikafungua geti dogo na kutoa pikipiki nje, nao walipotoka nikaurejeshea ule mlango mdogo kisha tukaanza safari ya kwenda hospitali, mgonjwa aliketi katikati yetu, BIGI amekaa mwishoni kabisa kwenye chuma kwasababu ya mwili wake mpana, ukichanganya na uzito wa watu wawili niliowabeba nyuma basi nikawiwa ugumu sana kumudu pikipiki kwenye barabara ile ya vumbi na makorongokorongo, yani mpaka kuifikia barabara ya lami nimetota mgongo mzima kwa jasho, sitamaniki!

Muda wote huo nilikuwa nikimsihi tu BIGI amshikilie mgonjwa vizuri na asiweke miguu yake chini akaharibu balansi ya chombo.

Basi niliposhika lami na kutembea mwendo wa kama dakika hivi, ndo' nikaanza kuhisi vema na mwili wangu, kule korongoni akili haikuwa imetulia kabisaa, mawazo yote yalikuwa ardhini tunapokanyaga, ila hapa lami nikaanza kuhisi baridi fulani hivi, si baridi la upepo, la hasha, bali baridi la mgonjwa!

Mara kadhaa mwanamke yule aliponiegamia nilihisi baridi mgongoni mwangu, nguo niliyokuwa nimevaa ilikuwa ni shati la kawaida tu sema kifuani ndo nilijiziba na kizibao cha ngozi kinachozuia upepo kuniingia ndani, hivyo nilikuwa na uwezo wa kuhisi vizuri tu na mgongo wangu pasi na shida, na mwanamke yule alikuwa ni wa baridi.

Sijawahi kuona mgonjwa anakuwa wa baridi kiasi kile, kwa nijuavyo mimi mgonjwa akiwa anaumwa, tuseme homa, joto la mwili wake hupanda sana, sikuwahi kujua kuna mambo ya joto kushuka kiasi hiki lakini kwasababu sijawahi kuwauguza wagonjwa wote duniani nikaona hilo nalo litakuwa ni jipya kwangu kujifunza.

Baada ya muda wa dakika kumi na tano hivi barabarani, kwa kufuata maelekezo ya BIGI, tukawa tumefika maeneo ya Kawe, Ukwamani. Upande ule wa kulia wa soko, kwa mbele kidogo kuna kibao cha dispensary kinachoonyeshea njia ya vumbi, tukashika njia hiyo mpaka kutokea kwenye zahanati fulani hivi kubwa, hapo BIGI akambeba mgonjwa wake na kunyookea naye mapokezi, mimi nikahangaika kidogo na pa kupakia pikipiki mpaka nilipokuja kusogea mapokezini wao wakawa wameshaenda kuonana na daktari, basi nikaketi kwenye benchi kungoja.

Hapo kwa benchi alikuwepo mama mmoja aliyejitanda kanga, amejiinamia simwoni uso wake, tulikuwa mimi na yeye tu hapo kwa benchi, hakukuwa na mtu mwingine, mazingira ya hapo yalikuwa yametulia mno, ungeweza kusikia kila mbu anayekatiza huku na kule kusaka ridhiki yake, nikamsalimu mama yule, "za saa hizi?" Akanyanyua uso wake kunitazama, alikuwa ni mwanamke mzee, macho yake mekundu kwa kulia. Aliitikia salamu yangu kwa sauti ya chini, "salama" kisha akaunamisha tena uso wake kama nilivyomkuta.

Nikatulia kidogo nikimtazama, bila shaka alikuwa na kubwa linalomsibu, nikashindwa kuvumilia nikamuuliza, "mama kulikoni?" Akiwa amejiinamia vile, akaniambia anajiskia vibaya sana, amekuja hapo kupima na ameambiwa ana maradhi lakini ameshindwa kumudu kununua dawa, mwili wake ni dhaifu na usiku ule alishindwa kabisa kupata hata usingizi wa kuibia mpaka alione jua la asubuhi.

Nikashikwa na imani sana. Mzee kama yule majira yale ya usiku mkubwa yuko kwenye benchi la zahanati tena akiwa hajui hatma yake, kweli dunia haina huruma! Nikajisachi na kutoa noti ya alfu kumi ambayo nilikuwa nimepanga kuiwekea mafuta kwenye pikipiki baadae nikienda kazini, nikampatia mama yule na kumsihi akachukue dawa na kiasi itakayobakia atapata chakula, mama huyo akanishukuru sana sana, kwakweli sikuwahi kuona mtu akishukuru kiasi kile maishani mwangu, laiti ungeliona alivyokuwa ananitazama ungepata picha halisi namaanisha nini hapa, alinyanyuka na kuendea taratibu duka la dawa la hapo zahanati, duka hilo lilikuwa linatazamana na sisi, akachukua dawa na kunirejea tena kuniaga.

Nikamuuliza, "Utaenda na usiku huu?" Akanijibu, "kwangu si mbali, ni hapo tu nyuma." Akaenda zake. Alipiga kama hatua nne hivi za kichovu, akageuka ghafla na kuniuliza, "yule bwana mnene aliyekuwa amebebelea mwanamke, umekuja naye?" Nikamjibu ndio, akaniuliza tena, "ni wateja ama watu unaowafahamu?"

Nikabaini mama huyo atakuwa aliniona nilipoingia eneo hilo na pikipiki hivyo akadhani huenda mimi ni bodaboda, kabla sijamjibu, akaongezea, "kama ni wateja tu wa barabarani, ondoka upesi achana nao."

Sikuelewa anamaanisha nini kwa kuniambia hivyo, nilimwambia wale ni majirani zangu, si wateja, basi akanitazama kwa macho ambayo niliyatafsiri kama mtu anayewazua jambo kichwani lakini hakusema kitu, nikamuuliza, "kwanini umesema hivyo?" Hakunijibu, akageuka na kuendelea na safari yake, nikatamani kumfuata kumuuliza lakini punde bwana BIGI alijiri akinifuata, alikuwa anatokea kule chumba cha daktari, akaniambia mkewe ameshaanza matibabu hivyo ni vema mimi nikarudi nyumbani kwani wao watabaki hapo usiku mzima.

Kwasababu hiyo, nikamuaga na kwenda zangu kuifuata pikipiki nijiondokee, njiani nikatazama huku na kule kama ntamwona mwanamke yule mzee niliyemsadia lakini sikufanikiwa, ni mataa tu na giza za vichochoro, basi nikalazimika kuamini atakuwa ameshafika nyumbani kwake kwani kwa maelezo yake nyumbani ni karibu tu na pale.

Nikawasha pikipiki na kuondoka, njiani nikiwaza mambo haya ambayo yametoka kujiri kuanzia nyumbani mpaka kule zahanati, mawazo hayo yakanifanya nikaona safari imekuwa fupi sana, yani kitambo kidogo tu nikawa tayari nipo mbele ya geti dogo la kuingia nyumbani.

Nikalifungua geti hilo na kuingia ndani, nilipoufunga mlango wa grill wa nyumba kubwa na kushika korido kwenda kwangu nikasikia sauti ya watu wanaongea, nikashtuka, sauti hiyo inatokea wapi? Niliposkiza vizuri nikabaini inatokea kwenye mlango wa chumba anachokaa BIGI, nikasogea karibu hapo mlangoni na kuskiza kwa umakini, nikagundua ni sauti ya televisheni sio watu wa kawaida, bila shaka yule mtoto wao ndo' alikuwa anatazama, nikajiendea zangu ndani kupumzika.

Zilipita kama siku kama nne hivi bila ya kuwa na makutano na familia hiyo, siku ya tano sasa kama sijakosea, katika majira ya usiku wa saa tisa nikiwa chumbani napambana kuupata usingizi, nikasikia kama kuna mtu huko nje, nikajua ni mwizi sasa ametutembelea tena, basi taratibu nikatoka kitandani na kuchungulia dirishani, dirisha la kule magharibi sikuona kitu ila dirisha hili la kaskazini nikamwona mtu ameketi kibarazani, mtu huyo ameketi akitulia tuli kama mbuyu wa nyikani! Nikastaajabu, huyu sio mwizi, lakini ni nani na anafanya nini kibarazani majira yale?

Niliendelea kutazama, taratibu taratibu nikajiridhisha kuwa mtu yule alikuwa ni mke wa BIGI, kumbe alikuwa amesharejea kutoka hospitali, lakini anafanya nini pale usiku mkubwa? Nilijaribu kukumbuka kama nilisikia mtu akiufungua mlango mkubwa kutoka nje lakini sikukumbuka kabisa, kidogo nikasikia mlango unafunguliwa, mlango wa ndani, alafu kidogo mlango wa grill ukachokonolewa na funguo, tulikuwa tunaweka funguo ya grill kwa juu, mlango ukalia kaaakakaaa alafu ukafunguka, huo mlango ndio ulikuwa unalia hivyo ukifunguliwa, akatoka BIGI akiwa anatembea upesi, akamnyakua mwanamke yule kama kipanga na kifaranga cha kuku, wakaingia ndani!

Kama dakika tu, nikamsikia sauti ya mtoto analia...

Muendelezo soma Jirani yangu wa Kule Goba hakuwa mtu wa kawaida
 
Jirani yangu wa kule Goba hakuwa mtu wa kawaida - 03

Haikukaa muda mtoto akanyamaza kisha kukawa kimya sana, kimya cha usiku, nami nikakaa kitandani kubembeleza usingizi ambao baada ya muda ukanichukua.

Usiku huo, sikukumbuka ni nini ila nilikuja kushtuka majira ya saa kumi na moja ya alfajiri nisijue kilichonikurupusha ni kitu gani. Kidogo nikasikia sauti iliyonishtua sana, pengine kwasababu nilikua katika hali ile ya taharuki, ilikuwa ni sauti ya maji yakiichapa ndoo kwa presha kubwa, nilipotazama nikaona moja wa majirani akiwa anachota maji, baada ya hapo sikuupata usingizi tena mpaka majira yangu ya kwenda kazini yalipowadia.

Siku hiyo nilihangaika mno kazini, usingizi ulikuwa unanikaba narembua macho kama mjinga, kila nilipopata nafasi ya kuegemea kitu, hata kama sikudhamiria, nikawa napitiwa na usingizi. Nilikuwa mithili ya teja mwenye arosto.

Nilipochomoka kazini na kufika nyumbani majira ya jioni, sikuchukua muda nikajilaza kwa uchovu. Nililala majira ya saa kumi na mbili, kwasababu hiyo nilijikuta naamka majira ya usiku mnene usingizi umekata, nikatoka kwenda kuoga maana joto nalo lilikuwa jingi na tokea nilivyorudi nyumbani sikupata kuoga, nilijilaza tu kama ng'ombe.

Nje kulikuwa kumetulia sana, kelele zangu za kuchota maji ndo ziliharibu utulivu, bomba lilikuwa na presha kubwa sana kama ugomvi, nilipomaliza nikaingia bafuni lakini nikiwa navua taulo langu mara nikasika kaaa-kaaa-kaaa, sauti ya grill la nyumba kubwa, nikatulia kimya kuskiza, sikusikia kitu, nikahofu anaweza akawa mwizi anaingia ndani hivyo nikachungulia kwa mwanya wa mlango, sikuona kitu, nikafungua mlango ili nione vema, taulo langu kiunoni, nikarusha macho kule kibarazani, sikuona kitu.

Nikatoka bafuni kusogelea nyumba kubwa, hamaki nikasikia kelele za mwizi mwizi, kufumba na kufumbua nikamwona mtu akitoka ndani ya nyumba kubwa kwa kasi kubwa, lengo lake lilikuwa ni kuufuata ukuta akwee lakini aliponiona nipo upande huu wa magharibi ya nyumba akabadili mwelekeo kukimbilia mashariki, kule kwenye geti kubwa, nami nikaongeza mwendo kumkimbiza, mkono wangu wa kuume umeshikilia fundo la taulo iliyomo kiunoni mwangu, kukata kona nikamwona mwizi yule akikwea ukuta, sikumuwahi akawa amesharukia huko nje, na mimi sikujaribu kuhangaika maana niko nusu uchi nisije nikaacha mazaga hadharani, kidogo akatokea jirani mmoja na kisha mwingine akiwa ameongozana na mkewe, mwanamke huyo akasema alimkuta mwizi akiwa anapekua viatu ambavyo vipo mwishoni kabisa wa korido wakati anatoka aende maliwatoni ndipo akapiga kelele za mwizi.

Basi kama ilivyo ada mjadala ukaanza tena wa mambo ya wezi, wakaongezeka na majirani wengine kadhaa haswa wa vile vyumba vya nje, nao wakasimuliwa yaliyotokea na wakatoa maoni yao, tukakubaliana kwa dhati kuwa mwenye nyumba anapaswa kuitwa kikao kuhusu hili maana akipigiwa tu simu na kuelezwa haitatosha, inabidi aje tumsihi atuongezee urefu wa ukuta na pia atuboreshee miundombinu ya usalama mathalani geti, kwani kodi si tunalipa bwana?

Tukiwa tunajadiliana hayo, nilitazama dirisha la chumba anamoishi BIGI maana dirisha hilo limetazama upande huu na halipo mbali sana na geti kubwa, bila shaka hata hapo tulipokuwa tusimama kuongea alikuwa anatusikia vema maana tupo karibu na dirisha hilo. Nilipotazama nikaona dirisha lenye kiza maana ndani hakukuwa kumewashwa taa lakini nilipotia umakini hapo nikabaini pazia la dirisha lilikuwa limefunguliwa kidogo, nikahisi kabisa kuna mtu yumo pale anachungulia nje.

Kitu kilichonifanya nikaamini hivyo ni pale nilipoendelea kulitazama lile dirisha, pazia liliachiwa likafunga, baada ya muda kidogo pazia likafunguliwa tena na nilipotazama nikaona limefungwa upesi. Sikujua ni nani alikuwa dirishani hapo sababu ya giza la chumbani lakini nilipatwa na maswali kama sio kustaajabu na watu wale.

Baada ya muda kidogo, kila mtu alirejea kwenye kiota chake na mimi nikarejea bafuni kuoga. Nilichokifanya sasa niliufunga ule mlango wa grill kwa ufunguo alafu nikaenda nao bafuni kwaajili ya usalama zaidi, lakini kabla sijamaliza kuoga nikasikia mtu akigonga mlango, mlango ule wa grill, hakika nikashtuka, nikasema na nafsi yangu pengine kuna mtu anataka kutoka kwenda maliwato na funguo ninayo mimi, basi nikajifunga taulo upesi pasipo kujikausha mwili ili nipate kutoka haraka, mara nikasikia tena mlango unagongwa, mara hii unagongwa kwanguvu sana bam-bam-bam-bam!

Nikatoka na kuyarusha macho yangu upesi kule kibarazani, nikamwona mtu mkubwa amesimama mlangoni. Mwanga wa kibarazani haukua ang'avu lakini nilimtambua mtu yule alikuwa ni BIGI, mkononi ameshikilia mkoba. Nilimsalimu na kumwambia ufunguo ninao mimi kisha nikamfungulia mlango akaingia ndani, nami nikaingia ndani kumfuatia, mkononi nina ndoo yangu ya kuogea, lakini nilipopiga hatua kadhaa kuufuata mlango wangu nikabaini nimeacha sabuni ya kuogea bafuni kwasababu ya ile haraka yangu, basi sikuwa na budi kurudi nje.

Nilipotoka nikasikia sauti ya pikipiki nje ya uzio, alikuwa ni yule jamaa bodaboda, yale yalikuwa ni moja ya majira yake ya kurejea nyumbani. Alifungua geti dogo akaingia ndani, kabla hajaenda kuegesha chombo chake alinisalimu na kuniuliza kama kuna mtu ameingia hapo nyumbani muda si mrefu, nikamjibu BIGI ndiye ameingia, akaniuliza;

"Yule jamaa mgeni enh?"

Nikamjibu ndio na kumuuliza, "kwani unamjua?" Akaniambia alishawahi mwona siku moja hapo nyumbani, mke wake akamwambia kuwa ni mpangaji mpya na amekuwa akikutana naye mara chache chache huko barabarani usiku mkubwa.

Alisema,

"Basi nilidhani nimemfananisha, nimemwona hapo kilimani akiwa anashuka na mdada fulani hivi, nadhani ni mkewe, nikajaribu kuwashtua ili nije nao lakini sikufanikiwa, nikasema nimeona vibaya nini?"

Pale nyumbani jografia yake ilikuwa hivi, kwa mtu anayetumia usafiri, aidha gari au pikipiki, kuna mahali fulani akifika hatoweza kutumia njia fupi zaidi (shortcut) ya kufika nyumbani kwasababu njia hiyo ni mbovu na nyembamba sana, hivyo atalazimika kuendelea kunyoosha na barabara mpaka mbele kabisa ambapo atakata kona na kuanza kurudi nyuma kwendea nyumbani, kwasababu hiyo ni kawaida kwa mtembea kwa miguu akafika mapema nyumbani kabla ya mwenye usafiri endapo wakiachania hapo.

Tukiachana na hilo, maelezo ya jamaa huyu kwamba alimwona BIGI na mwanamke aliyemdhania kwamba ni mkewe wakiwa wanatembea kuja nyumbani yalinitatiza kiasi kwasababu mimi nilimpokea BIGI akiwa peke yake mlangoni na mkoba wake mkononi, huyo mwanamke sikumwona machoni pangu.

Nikamuuliza kama kweli aliona vema, akasema ana uhakika na alichosema, nami sikutaka kusema zaidi mengine yakabaki ndani yangu, yeye akaenda kupaki chombo chake na kuingia zake ndani, na mimi pia nikaingia ndani na kujilaza kitandani ...

Nikawaza.

Nikajigeuza kitandani nikiwaza.

Hamna nilichoelewa.

Kama BIGI na mkewe hawakuwamo ndani, yule aliyekuwa anachungulia dirishani muda ule ni nani? Ni mtoto wao au? Na huyo mwanamke ambaye alikuwa na BIGI njiani lakini hakufika naye nyumbani, ni mkewe kweli? Kama ndiye mbona sasa ..... Aaagh ... Sikuelewa kitu! Hamna kilichokuwa kinaeleweka, nilikaa hapo mpaka kunakucha maana sikuwa na usingizi kabisa, ajabu wakati jua linawaka ndipo nikaanza kuona macho mazito, nashukuru ilikuwa ni weekend na siku hizo sikuwa naenda kazini basi nikajilalia zangu.

Kesho yake, siku ya jumapili, mwenye nyumba alifika pale nyumbani majira ya mchana kwaajili ya kuitikia wito wetu wa kikao. Kama kawaida yake alipofika alipita kila mlango akigonga na kusalimu na baada ya muda mchache karibia kila mtu akasogea kibarazani kwaajili ya kikao kile cha dharura, watu waliokosekana walikuwa wachache sana; yule jamaa bodaboda pamoja na BIGI ila wengine wote walikuwapo ikiwemo mke wa BIGI pia.

Mwanamke huyo alikuwa ameketi kwenye kona, amejitanda mtandio kichwani, ametulia tuli tofauti kabisa na wenzake, hata kikao kilipoanza karibia kila mtu alisema ya kwake lakini kwake hali ilikuwa tofauti, hakushiriki kwenye chochote, pengine sababu ni bubu hata angesema asingeeleweka, nikajiwazia mwenyewe moyoni, lakini cha ajabu ni kwamba kila niliporusha macho yangu kumtazama, aidha kiwiziwizi ama moja kwa moja, nilikutana na macho yake akinitazama.

Haikujalisha niliupoteza muda kiasi gani baada ya kumtazama ila kila nilipoyarejesha tena macho yangu kwake, nilimkuta mwanamke yule ananitazama. Macho yake hayakuwa ya urafiki.
**

Muendelezo soma Jirani yangu wa Kule Goba hakuwa mtu wa kawaida
 
Jirani yangu wa kule Goba hakuwa mtu wa kawaida - 04

Kikao kilikwisha kwa pande zote mbili kuelewana, mwenye nyumba alisema baada ya siku tatu mafundi watakuja kwaajili ya kuanza ujenzi lakini pia hapohapo kabla kikao hakijaisha akasisitizia kuhusu kodi yake, hili nililijua tu litakuja, alisema na yeye atapata nguvu zaidi ya kuboresha miundombinu endapo sisi tutatoa pesa zake kwa wakati, baada ya kikao kuisha aliaga na kwenda zake na kila mtu akaendelea na shughuli zake, angalau sasa na mimi nikapumzika na macho ya yule shemeji, macho ambayo sikuelewa yanamaanisha nini zaidi ya kunitisha.

Zikapita siku mbili, mafundi hawakuja kama tulivyoambiwa, ikapita siku ya tatu na ya nne, hola, mpaka wiki nzima iliyoyoma si fundi wala mhandisi aliyekuja, mwenye nyumba anatupiga tu kalenda.

Siku moja nikiwa niko nyumbani, sikumbuki haswa zilipita siku ngapi tangu tufanye kile kikao, katika majira ya saa saba usiku nikasikia mtu anafungua mlango wake, sikujua ni nani maana mimi nilikuwa ndani sebuleni lakini ni bayana alikuwa ni jirani mmojawapo katika milango ile miwili, kidogo mlango wa grill ulifunguliwa kakaaa-kakaaaa kisha kukawa kimya, nami nikawa kimya nikiwaza huenda mtu anaenda maliwatoni hivyo nikaendelea na mambo yangu ya kutazama runinga.

Nilikaa kama nusu saa lakini sikusikia mlango ule wa grill ukifungwa, na kwa namna yoyote ile mlango ule usingeweza kufungwa bila kutoa sauti, hapo nikapata shaka. Nilitoka sebuleni nikaenda chumbani ili nipate kuchungulia nje kuna nini kinaendelea, nilipofungua pazia la dirisha kwanza nikatazama pikipiki yangu, nikaona kuna usalama, nikaangaza huku na kule lakini sikumwona mtu, nje kulikuwa kimya sana.

Nilitulia kusikiliza labda kuna mtu bafuni, napo sikusikia kitu, kila pembe ilikuwa kimya sana. Hapo nikapata wasiwasi. Niliufungua mlango nikaenda nje kutazama maana ule mlango wa grill kuwa wazi kwa muda wote huo haikuwa salama kabisa ukizingatia tulinusurika kupigwa tukio mara ya mwisho, huko nje nikatazama upande wa magharibi, hamna mtu, nikatazama upande wa mashariki nao hamna mtu, kabla ya kurudi ndani nikaenda kule bafuni, bafu zote zilikuwa zimezimwa taa hivyo nikahitimisha hamna mtu humo, basi nikarejea mlangoni na kuurejeshea ule mlango wa grill pasipo kuufunga na ufunguo ili kama kuna mtu huko nje basi ataingia na kuufunga mwenyewe, mimi nikareja sebuleni nikaendelea kutazama televisheni.

Nilitazama mpaka nilipohisi naelemewa na usingizi ndipo nikaenda zangu chumbani, huko nikajilaza na kuskilizia lakini muda wote huo sikusikia mlango wa grill ukifunguliwa, kulikuwa ni kimya tu kama hapo awali, nikajiuliza nini kinaendelea au ni mimi ndo' mwenye matatizo? Mpaka napitiwa na usingizi sikupata kusikia kitu, asubuhi palipokucha wakati naenda kuoga niende kazini, pale bombani, nilikutana na jirani yangu wa mlango mwingine ndani ya ile nyumba kubwa, mwanamke huyo alikuwa anafua nguo zake hapo nje, wanawake hawa huwa wana utaratibu wa kuamka mapema kufua kwaajili ya kuwahi kamba, baada ya kunisalimu aliniuliza,

"Shemeji, ni wewe ndo' uliacha mlango wa grill ukiwa wazi jana usiku?"

Nikamweleza namna mambo yalivyotokea kuwa mimi sikuuacha wazi bali niliurejeshea tu baada ya kusikia mtu alitoka, ajabu akaniambia kuwa mumewe asubuhi ya mapema sana alipotoka aliukuta mlango ukiwa wazi kabisa, umeachama kama mdomo! Nikastaajabu kusikia hayo, nilijiuliza ni muda gani mlango ulifunguliwa lakini sikupata majibu, nikaenda zangu kuoga nikilenga kuwa siku n'takayokutana na BIGI nimuulize kuhusu jambo hilo, sikuwa najua ni lini ila nilitumai ndani ya wiki hiyo basi nitambahatisha.

Ikapita siku mbili, sikumwona BIGI wala mkewe, siku ya tatu yake nikiwa sebuleni majira yangu ya usiku mtulivu, siku hiyo sikuwa natazama televisheni bali namalizia kazi fulani kwenye laptop, nikasikia mtu akiufungua mlango na kisha akaufungua mlango wa grill kakakaaa-kaaakaa, nikakaa tenge, mara hiyo sikutaka kupuuzia nilinyanyuka upesi nikaenda chumbani kutazama, ile kufungua tu pazia nikamwona mtu akiishia kwa kulifunga geti dogo, sikumjua mtu huyo ni nani kwani nilichoambulia kukiona ni mkono tu tena kwa muda mchache mno, basi nikabaki hapo nikiendelea kutazama pengine nitaona kitu.

Ngoja lakini wapi! Nilitumia kama nusu saa hapo lakini sikuona kitu nami nilikuwa nina hamu sana ya kumwona mtu huyo kwani niliamini yeye ndiye yule aliyeacha geti wazi siku ile, nilitamani kujua anafanya nini muda huo na kwanini anaacha geti wazi?

Nilikaa hapo dirishani kwa muda mrefu pasipo kuona kitu nikakata shauri kwenda nje, nilipoufungua mlango wangu kudaka korido nilisikia sauti ya watu wakizungumza, nikasita nikiskiliza. Sauti hiyo ilikuwa inatokea kwenye chumba cha BIGI na nilipoisikiliza kwa kitambo kidogo tu nilibaini sauti hiyo haikuwa ngeni masikioni mwangu, nilishawahi kuisikia mahali, ila ni wapi?

Kidogo kuwaza nikaikumbuka, sauti hii ilikuwa ni ileile niliyoisikia siku ile kwenye mlango huuhuu nikajua ni ya televisheni, ina maana imejirudia au ni masikio yangu? Nilistaajabu, lakini kadiri nilivyoisikia sauti hiyo tena na tena, tena kwa umakini, nikaamini kabisa haikuwa sauti ya televisheni, sauti hiyo ilikuwa ya watu wanaozoza na kunong'ona kitu ambacho sikuwasikia vema nikaelewa.

Nikiwa naendelea kuskiza hapo, mara nikasikia kishindo cha hatua za mtu kibarazani alafu mlango wa grill ukafunguliwa kakaaa kaakaaa! Nikashtuka kweli kweli, ni kama vile moyo wangu uliruka pigo moja kwa fujo!

Upesi nilirejea karibu na mlango wangu nikayatupa macho kule langoni, punde nikamshuhudia BIGI akiingia ndani huku amebebelea kiroba kitupu mkononi, huku juu amevalia 'vest' yake ileile aliyokuja nayo wakati mke wake anaumwa, aliponiona alisimama akan'tazama, nahisi na yeye alishtushwa na uwepo wangu pale, alinitazama pasipo kusema kitu chochote ila mimi nikamsalimu, hakujibu, alisimama tu akiendelea kun'tazama, sijui alikuwa anawaza kitu gani, mapigo yangu ya moyo yalikuwa yanapiga kwa kasi sana, niliona ni busara kuingia ndani kwangu upesi nikaufunga mlango kwa funguo kisha nikasimama hapo kusikiliza, kimya, nlidhani nitasikia vishindo vya miguu vikijongea lakini sikusikia chochote zaidi ya sauti ya mlango ukifungwa kisha kukawa kimya tena.

Nilizima kila kitu changu nikaenda chumbani moja kwa moja mpaka dirishani. Nilitazama pale kibarazani nikaona mlango wa grill ukiwa wazi. Nilitamani kwenda kuufunga lakini nikawaza vipi kama bwana yule akawa bado hajamaliza shughuli zake? Nikaona ni stara nikitulia lakini niendelee kungoja kama atatoka tena.

Nilingoja hapo kitandani kwangu mpaka usingizi ukanibeba, sikusikia kitu abadani. Kesho yake niliporejea tu kazini nikaelezwa kulitokea mjadala mkubwa hapo nyumbani juu ya swala la mlango wa grill kuachwa wazi kwa mara nyingine tena usiku ulopita, siku hiyo majira ya saa tatu hivi usiku kama sijakosea, nilikutana na jirani yangu yule wa dukani tukaongea mambo kadhaa kuhusu hapo nyumbani, moja kuhusu swala la ujenzi wa uzio na namna ambavyo mwenye nyumba haeleweki, na pili kuhusu swala la mlango wa grill kuachwa wazi nyakati za usiku. Bwana huyo alikuwa ndo' mtu wa kwanza kutoka asubuhi hivyo yeye ndiye aliyekuwa anaukuta mlango huo ukiwa wazi.

Kwa upande wangu nilimweleza yale niliyoyajua ya kuwa bwana BIGI ndiye anayeacha mlango huo wazi na basi kwa pamoja tukaazimia kumwambia endapo yeyote akipata nafasi hiyo. Siku zikapita, sijui kama yeye alifanikiwa kuonana na jamaa lakini mimi sikufanikiwa na uzuri mlango haukuachwa wazi tena.

Nakumbuka siku ambayo mafundi walikuja kwaajili ya ujenzi ndo siku ambayo nilipata kumwona bwana BIGI. Siku hiyo ilikuwa ni usiku kama wa saa nane hivi kama niko sawa, nilikuwa sebuleni kama kawaida yangu kabla ya kwenda kulala, televisheni inaongea lakini akili yangu yote ipo kwenye simu naperuzi mitandaoni, naingia instagram, whatsapp na JamiiForums.

Nilisikia mlango unafunguliwa na kisha mlango wa grill, nikanyanyuka kwenda kutazama dirishani. Hapo nilimwona BIGI akiwa amebebelea kiroba begani mwake anatoka kwenda geti dogo.

Kwasababu za ujenzi, geti hilo lilikuwa wazi tena limeegeshwa pembeni kabisa hivyo unaweza kuona mpaka nje. Nikamwona mtu huyo akitokomea huko mpaka kiza kikammeza!

Niliendelea kukaa hapo kwa muda kidogo lakini sikumwona akirudi, nikajua ni kama kawaida sitamshuhudia mpaka nitakapolala, lakini siku hiyo hali ilikuwa tofauti, baada ya kurudi kule sebuleni na kukaa kwa dakika kadhaa nilisikia kishindo cha mtu akikatiza koridoni alafu sauti ya mlango ikaita, nikawaza moja kwa moja atakuwa BIGI ndo amerejea lakini kwanini haufungi mlango wa grill? Nikaazimia ningoje kidogo hapo na nikiona kimya basi nitatoka nikaufunge mlango huo mwenyewe.

Kweli nilikaa hapo kwa kama nusu saa hivi, kimya, nilienda chumbani kutazama dirishani, hali ilikuwa shwari, nikauendea mlango wangu kuufungua lakini nilipotekenya tu funguo nikasikia mlango mwingine unafunguliwa, nikatulia kuskiza.

Vishindo vilipita koridoni nikahisi na kuamini kabisa alikuwa ni BIGI, vishindo hivyo vilipofifia nikaufungua mlango na kuchungulia nje, kweli alikuwa BIGI, nilimwona anatoka nje ya uzio akiwa na kiroba chake begani. Sikujua alikuwa anabebelea kitu gani humo lakini kilichonitatiza zaidi ni kwanini alikuwa anafanya zoezi hilo usiku wa manane?

Nilitoka nikatembea kwa upesi lakini pia kwa uangalifu mpaka kwenye geti dogo. Hapo nilirusha macho yangu kule kutazama, kwa mbali kwa msaada wa mataa mengine ya kule nje, nikamwona BIGI akiwa anayoyomea kuelekea kule korongoni, kule ambapo ndiyo wezi wanapokimbilia. Mwendo wake ulikuwa wa haraka sana na kwasababu ya uweusi wake basi kiroba ndo kilikuwa kinaonekana kikikata upepo, kile kinapepea, kilee kinapepea!

Niliijikuta nina hamu ya kwenda zaidi kutazama.
***

Muendelezo soma Jirani yangu wa Kule Goba hakuwa mtu wa kawaida
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom