Halisi
JF-Expert Member
- Jan 16, 2007
- 2,802
- 613
Jenerali Ulimwengu
TUMEONA katika makala ya wiki jana jinsi kitoto kilichozaliwa katika familia ya mafisadi kinavyolelewa kifisadi, kinavyosomeshwa kifisadi, kinavyofanywa 'kifaulu' kifisadi, kinavyoajiriwa kifisadi, kinavyoozeshwa kifisadi na kinavyokuwa kitu kingine cha ufisadi katika mwendelezo wa utamaduni wa ufisadi kilimozaliwa.
Sidhani kwamba tunaweza kuwa na matumaini ya kupata lo lote la maana kutoka kitoto hicho kwa maana ya kuiendeleza nchi na kuwaendeleza watu wake. Watu wa aina ya kitoto hicho hawawezi kuijenga wala kuiongoza nchi, kwa sababu wao hawajajengwa wala kuongozwa katika misingi ya kujenga lo lote la maana isipokuwa kuendeleza utamaduni uliowazaa na kuwalea.
Kwa bahati mbaya, katika mazingira yetu, na katika mazingira ya nchi nyingi za Kiafrika, hawa ndio watu wanaoelekea kuchukua mikoba ya utawala kutoka kwa wazazi wao, katika mazingira ambamo mifumo ya utawala haiwaachii wananchi nafasi ya kuchagua viongozi wao.
Haya ni mazingira ambamo, kama nilivyoeleza katika makala zangu za nyuma, watawala wanaendesha nchi bila itikadi ya kimsingi inayowaelekeza na wanachofanya ni kila siku kuzuka na jipya lisilokuwa sehemu ya mwendelezo wa jambo jingine lo lote walilosimamia huko nyuma wala wanalotaraji kulisimamia siku za usoni.
Unakuwa ni uongozi wa kubabaisha, wa kila siku kuokoteza 'sound bite' za kauli-mbiu zisizodumu hata mwaka mmoja. Baada ya muda ukiwaangalia wanaonekana kama vile wamekwisha kusahau kauli-mbiu ya mwaka jana na sasa wanazindua nyingine.
Ni hali hii ndiyo inayojenga utegemezi wa kila aliye ndani ya utawala kwa 'busara' za Bwana Mkubwa, kwa maana ya kiongozi wa juu kabisa wa wakati huo, ambaye atakuwa na 'busara' kubwa sana ambazo hakuwahi kuwa nazo kabla hajaingia madarakani, na ambazo akiondoka madarakani anaziacha ofisini; anarudia kuwa mtu wa kawaida, wa akili kama zako na zangu.
Bila shaka hapa kuna tatizo: Waliomzunguka Bwana Mkubwa, kwa kukosa itikadi au mfumo wa fikra unaowaunganisha, na kwa kuhofia kupoteza 'kibarua' chao, wanajenga ukimya mkubwa na hatimaye hata uwezo wa kufikiri na kutamka kile wanachoamini unavia. Baada ya miongo michache katika hali hiyo hata yule aliyewahi kuwa mwalimu mzuri wa shule ya msingi hawezi tena kazi hiyo kwa kuwa kapoteza mazoea ya kufikiri, hata kwa kiwango hicho.
Papo hapo tunajua kwamba 'busara' za Bwana Mkubwa nazo hazina uhalisi wo wote kwa sababu zimetokana na sifa anazomwagiwa na waajiriwa wake na wapambe wengime. Sasa tukiunganisha 'busara' hizi feki na mazoea hafifu ya kutumia akili ya wasaidizi na wapambe wake, kinachozalishwa ni ombwe (vacuum) katika uongozi hata kama utawala unaweza kuwa na ufanisi wa kufanya menejimenti ya kilipo bila maendeleo.
Kwa kuwa maumbile hayapendi ombwe, Bwana Mkubwa na wapambe wake watajikuta wanafunikwa na itikadi kutoka kwingineko, kutoka nchi na asasi ambazo maslahi yake siyo lazima yasadifu na maslahi ya watu wetu. Mara nyingi haya maslahi ya pande mbili yanakuwa yanakinzana moja kwa moja, na vikali.
Yote hii ni kusema kwamba mazingira ambamo watawala wanaendesha utawala wao bila mfumo wa fikra, bila mtazamo wa kimkakati kuhusu mustakabali wa nchi yao na watu wao, katika mazingira hayo kitakachowaunganisha watawala hao ni ufisadi.. ufisadi wa ndani ya nchi ukisaidiana na kuelekezwa na ufisadi wa nje ya nchi.
Lile ombwe nililolitaja hapo juu linadhihirika hadi nje ya nchi, na wenye maslahi yao hawashindwi kulitambua hilo na kulifanyia kazi. Wanachofanya ni kuwapata mawakala wao katika nchi zetu watakaowatumikia. Malipo yao ni madaraka ya kisiasa, ambayo watawasaidia kuyapata katika gulio la kura pamoja na mapesa ya kuwapa ukwasi wa kuazima.
Hali ikiisha kuwa hivyo, hakuna linaloweza kufanyika kubadilisha fikra za watawala wa aina hii, kwa sababu ufinyu wao wa kufikiri na maslahi ya mabwana zao kutoka nje vinakuwa vimejenga ubia imara usiomsikia mtu wala jini. Mambo yao 'yanajipa' katika utaratibu tuliokuwa tukiujua kama Ubeberu lakini hivi sasa unatambulishwa kwa jina laini la Utandawazi.
Hii siyo hali ya kuruhusu, achilia mbali kuchochea, maendeleo. Maendeleo hayapatikani kutokana na mchakato unaoendeshwa na mawakala wa ndani wanaofanya kazi kwa kusimamiwa na kuelekezwa na maslahi ya kiuchumi ya Ubeberu. Hii ni hali ya kudumisha na kuimarisha uduni, udhaifu na umasikini wetu ndani ya kila aina ya neema tuliyopewa na maumbile na Mwenyezi Mungu.
Msomaji atakuwa amenielewa ni nini nataka kusema: kila kiongozi mwenye nia njema na watu wake na aliyedhamiria kuwaongoza ili waweze kujiletea (siyo kuwaletea) maendeleo ya kweli, hana budi kuwa na ubia katika uongozi wake. Kwanza atakuwa ameingia ubia na wananchi anaowaongoza; pili ataingia ubia na asasi anazozitumia katika malengo yake (tuseme chama, kwa mfano); tatu ndani ya asasi hizo ataunga ubia, atakula yamini, na viongozi wenzake wenye malengo kama yake.
Asipofanya hivyo, na akizidi kung'ang'ania kwamba uongozi wake hauna ubia, mtawala huyo anajidanganya, na wanaomwangalia na kumsikiliza watagundua baada ya muda si mrefu kwamba anao wabia ambao inamuwia vigumu kuwatangaza.
Hii si hali ya kuridhisha hata kidogo, na ni hali hiyo inayoifanya Afrika iendelee kumenyeka na umasikini wakati inao kila aina ya utajiri. Mojawapo ya mambo yanayoweza kuchochea maendeleo ni utawala bora, na utawala bora lazima uwe ni utawala wa pamoja, angalau kwa watu waliokula yamini ya pamoja ya kufanya mambo fulani ili kufanikisha malengo maalumu.
Kinyume cha hilo ni nini? Iko mifano lukuki, lakini mmoja ni wa hivi karibuni na unahusu maneno yaliyojaa masikioni hata wakati nikiandika makala hii. Imezinduliwa kampeni kubwa, na yenye kelele nyingi, inayoitwa 'Kilimo Kwanza.' Lengo lake la jumla ni kutoa kipaumbele kwa kilimo, ambalo ni jambo jema na sahihi.
Hata hivyo, wakuu wa Serikali wanajua kwamba ilikuwapo sera iliyoitwa 'Siasa ni Kilimo' iliyotangazwa mwaka 1972 kisha ikawekwa kabatini. Alipoondoka Mwalimu madarakani na sera hiyo ikaondoka, kwa sababu, kama ninavyosema, alijizungushia ukuta wa matarishi badala ya kujijengea wigo wa viongozi wenzake.
Baadaye sana, mmoja wa warithi wake, ambaye kwa hakika zamani alikuwa ni mmoja wa hao matarishi wake, aliulizwa ni jambo gani alidhani alikuwa amesahau kulishughulikia katika utawala wake wa miaka kumi. Jibu lake? Kilimo .
Tunashangaa nini? Katika 'uongozi' usiokuwa na ubia, ni nani katika watu waliokuwa wamemzunguka angethubutu kumwambia, Mzee, samahani sana kwa usumbufu wangu, lakini naona kama vile tumesahau kilimo? Tena, hata kwa kusema "tumesahau" ili aonekane naye anahusika katika uzembe huo.
Tunajua tayari kwamba watawala wa Kiafrika hawana washauri. Ofisi za 'washauri' ni vituo vya kuwazawadia wapambe waliotoa huduma kwa Bwana Mkubwa (aghalabu huduma chafu) wakati akisaka madaraka. Hakuna ushauri wo wote wanaotoa mbali na kumshangilia Bwana Mkubwa na kumwambia, Mzee ile hotuba yako ya leo, haijapata kutokea! na upuuzi mwingine kama huo. Hakuna washauri bali wamejaa wapiga debe, mashabiki, wapambe na washikaji, wote wakigharimu fedha nyingi mno za walipa kodi.
Sasa mawaziri ndio hao, na washauri ndio hao. Ni kwa nini hasa tunataraji kupata maendeleo? Nakumbushia tena: Kufanya jambo lile lile kila siku kwa njia ile ile, na kutaraji kupata matokeo tofauti, ni ishara mojawapo ya taahira ya akili.
Itaendelea
Source: http://www.raiamwema.co.tz/news.php?d=1596
Nashauri isomwe pamoja na hii:
https://www.jamiiforums.com/jukwaa-la-siasa/35474-ikulu-watakubali-kunipa-kibarua-nilichoomba.html
Nashauri pia baadaye hii yangu Mods waiunganishe kule kwa MM