Historia ya Muziki wa Rumba nchini Kongo (Rumba Congolais)

Wildlifer

JF-Expert Member
May 12, 2021
1,883
5,190
Salam wanaJF.

Katika uzi huu nitaelezea Historia ya Muziki wa Rumba la Kikongo. Hii itagusa Congo zote mbili yaani Kongo Brazzaville na Kongo Kinshasa. Huu ni mkusanyiko kutoka vyanza mbalimbali, na hasa imehamasishwa na Mtafiti wa Chimbuko na asili ya Muziki (Ethnomusicologists), Masoud Masoud wa TBC kupitia kipindi chake cha zilipendwa. Lakini pia taarifa zingine zimetoka kwenye kitabu cha Rumba on the River chake Gary Stewart, lakini pia tafiti za Professor Kazadi wa Mukuna.

SEHEMU YA I: HISYORIA HADI KUFIKIA MWAKA 1940

Mto Kongo unatenganisha miji miwili. Miji hii ni kama almasi iliyosafishwa kwenye mto huo, moja ikiwa safi na angavu na ya pili ikiwa iko chafu bado. Lakini kama ilivyo tabasamu la mtu mwenye kujiamini, almasi hizi zinahadaa. Almasi hizi mbili ni matokeo ya nguvu ya waafrika na mkono wa chuma wa wazungu. Katika miji hii miwili iliyotengenezwa na ubunifu wa wanadamu, waafrika walikutana na ukristo wa wazungu pamoja na biashara na matokeo yake ukazaliwa muziki wenye ubunifu wa hali ya juu na kuwa mshindani wa ule wa New Orleans. Kwenye mto huo eneo kubwa liloitwa Stanley pool, wabelgiji na wafaransa waliamua kutengeneza makoloni yao. Upande wa kusini mashariki mwa ukingo huo, walikaa wabelgiji, mjio huo ulikuwa ndio almasi safi na kuakisi hulka za wabelgiji za ufanyaji kazi na mafanikio na wasiokuwa na masihala kwenye mambo yao- Leopoldville (Belgian Congo). Kaskazini magharibi mwa mto kongo ilikuwa ni sawa na almasi isiyokatwa huku ikiwa na uchafu wake bado kuakisi mji ambao hakuwa umeendelezwa sana, na ikiwa chini ya wafaransa- Brazzaville (French Congo).

Waafrika kwa utashi au lazima, walitoka vijijini na kwenda kwenye majiji ili kutafuta maisha bora. Kama ilivyokuwa kwa watumwa walioenda America, ndivyo kwa waafrika waliokuwa ndani ya Kongo walisafiri na muziki wao. Waliazima vitu vilivyowapendeza kutoka kwa Wazungu na kuunganisha kwenye mila na historia yao na kuupa usasa muziki wao.

Wageni waliongia kwenye majiji hayo mawili, waliingia na lugha na mila zao Sambamba na muziki ulioakisi shughuli zao za kila siku. Magitaa yaliyokuwa yakiingia afrika kutoka ughaibuni, licha ya kuwa na bei rahisi, lakini yalibadili muziki kutoka wa asili na kuwa wakisasa. Muunganiko huu ulizalisha aina mpya ya muziki iliyoleta mapinduzi barani afrika kama jinsi Jazz ilivyoleta mapinduzi nchini Marekani. Waafrika wengi waliuita muziki huu 'Congo Music' na wazungu kwa wingi muziki huu huuita Soukous.

Mwaka 1946, Henri Bowane alifunga safari na kuelekea mji wa Lipopo huko Leopoldville. Njiani alisikia habari nyingi kuhusu uzuri wa maisha mjini na pia kuhusu muziki. Wanamuziki wanaotokea Lipopo hawakuwa wageni kwake sababu alishawashudia mara kadhaa wakija kwa ajili ya kutumbuiza.

Bowane aliukuta mji wa kongo ukiwa umegawanyika kutokana na asili. Sehemu ya kaskazini mwa mto kongo, wenyeji waliita Ville na lilikuwa kando ya mto, waliishi wazungu. Katika eneo hili upande wa mashariki ilikuwa ni eneo la biashara, magharibi ni makazi na katikati ilikuwa ndipo serikali ilipo. Kuelekea upande wa kusini kulikuwa na Nyumba ya maonyesho ya wanyama na wafanyakazi wa kiafrika wengi walikuwa eneo hili na lilijulikana kama cite indigine. Eneo hili lilokuwa na waafrika wengi lilikuwa na wilaya mbili zilizokuwa zikikua kwa kasi, Kinshasa upande wa mashariki na kintambo upande wa magharibi huku ikiwa imetenganishwa na kambi ya jeshi na kiwanda. Wabelgiji walihofia kuongezeka kwa wakazi waafrika wa eneo hili, hivyo waliweka sheria ya kudhibiti 'wahamiaji haramu'😤 na iliwalazimu waafrika kuwa na passport ili kuingia mji hiyo lakini wengi walitumia mbinu za ujanja kuingia na kuishi. Wakati wa mchana maisha yalikuwa na changanyike ya waafrika na wazungu waliofanya biashara maeneo ya wazungu, ila ilipofika saa 3 usiku hadi saa alfajiri ni wafanyakazi halali tu wa kiafrika ndio walioruhusiwa kuonekana maeneo hayo ya wazungu na sharti ilikuwa ni lazima wawe wanaishi kwenye nyumba za wazungu. Hata maeneo waliyokuwa wakiishi waafrika-cite-waafrika hawakutakiwa kutembea nje kuanzia saa 4 usiku hadi saa 10 alfajiri (curfew). ☹️Mtu anakukuta kwenye nchi yako lakini anakupangia na masharti yake ya Kuishi.

Mahusiano ya wazungu na waafrika ya kati yalianza mwaka 1483, wakati mpelelezi wa kireni Diego Cao alipofika kwenye mto Nzadi, ambao wareno kimakosa walikuwa wakitamba Zaire, leo hii inajulikana kama Kongo. Mto huu ulipita kwenye falme ilikuwa ikiongozwa na mani(mfalme) wenye makao yake makuu mbaza eneo la kaskazini mwa Angola. Mahusiano haya yaliyoanza kama ya 'usawa wenye utofauti' yaliishia kuwa ni operation ya wazungu kuijineemesha kwa ghalama za waafrika. Hatimaye kwa kigezo kuwa waafrika walikuwa ni watu pungufu, washenzi na wasiostaarabika, walichukuliwa utumwani kwenye mashamba na migodi huko Amerika.

Kwa takribani miaka 400,1450 hadi 1880, Watu takribani Milioni 20, mil 5 kutoka Kongo pekee walitwaliwa au kuuliwa katika biashara iliyoharibu mifumo na taasisi za kiafrika na iliyoshusha utu wa watu wote wazungu na waafrika. Eneo la afrika mashariki waarabu kutoka sudan, misri na Ghuba ya uarabuni kama iran, saudi walichukua watumwa weusi takribani watu 10,000 kutoka pwani ya afrika mashariki na 12,000 kutoka pwani ya bahari ya sham. Kufikia karne ya 19, vuguvugu la kupuga vita utumwa, lilipelekea Kuibuka kwa mambo matatu, Ukristo, Biashara na 'kustaarabisha' waafrika kama tiba ya utumwa. Hivyo wakombozi wa afrika ndio walitegemewa kuwa suluhu ya utumwa.

Katika Maendeleo ya muziki, wakombozi wa muhimu ni Mmarekani mwenye asili ya Wales Morton Stanley na Muitaliano aliyechukua uraia wa Ufaransa Savorgnan De Brazza kila mmoja akifanya kazi pekee yake ila kwa ushindani. Stanley alianza safari yake Nov 1843 na kufika Zanzibar kisha kuelekea na kufika mto Kongo. Kwenye safari yake hii alikuwa na Wazungu wasaidizi wake watatu na waafrika takribani 350 wakiwa ni wabeba mizigo, watumishi na askari pia. Safari yake hii ya 'uvumbuzi' ilisababisha mauji ya mamaia ya waafrika waliopingana na uvamizi wake. Mwaka 1875, Brazza alianza safari iliyompeleka hadi Gabon, akiwa na usaidizi wa wazungu watatu na mabaharia wa kisenegali. Brazza hakuwa na msafara mkubwa na hakusababisha madhila mengi kama stanley. Mwaka 1877, wakati Stanley akiwa Boma, karibu na bahari ya Atlantic, Brazza alikuwa kilometers kadhaa kutokea mto Kongo, ambapo wenyeji walisimama imara na kumfurusha.

w.jpg


stanley-hub_2784602a.jpg

Safari za kipelelezi wa kina Brazza na wenzake ndizo zilizowapa ufahamu wazungu juu ya Afrika. Mfano, Stanley aliwaambia waingereza kuwa kuna takribani waafrika Mil 40 wanaotembea uchi hivyo hii ikawa ni hamasa kwa viwanda vya nguo vya Manchester. Pia waafrika walikuwa ni wapagani hivyo wahubiri waje wawape ubatizo. Lakini wakati huu waingereza walikuwa na hali ngumu kiuchumi na walikuwa wakipambana dhidi ya wafaransa kuikamata Misri (suez canal). Jibu pekee kwao likawa ni Mfalme Leopold wa Pili wa ubelgiji ambaye walikuwa na mawazo ya kufanana.

Mfalme Leopold II alikuwa ni mwenye asili ya ujerumani na Binamu wa Queen Victoria wa Uingereza. Alikuwa mfalme wa nchi ndogo iliyotoka kupata uhuru kutoka kwa Denmark mwaka 1825. Yeye alipata ufalme mwaka 1865. Ubelgiji ilikuwa nchi yenye mivutano ya watu wa Flemming na walloon. Kikatiba mfalme hakuwa na mamlaka yeyote kiutawala, lakini alitamani kuwa na koloni kwa faida ya nchi yake na yake binafsi, na afrika ya kati ndiyo iliyokuwa ikimvutia.

Leopold_ii_garter_knight.jpg


Mfalme Leopold II alikuwa akifuatilia kwa kina yanayoendelea juu ya upelelezi wa bara la Afrika, hivyo mwaka 1876 alianzisha taasisi iliyoitwa International Africa Association ikiwa na kusanyiko la wafanyabiashara, wanasayansi na wapelelezi juu ya kulifungua bara la afrika kwa utafiti zaidi. Aliwaita Brazza na Stanley. Brazza alimkatilia ombi lake sababu muda huo alikuwa amechukua uraia wa Ufaransa na alitaka kuifaidisha taifa lake jipya hilo. Stanley ambaye hakua na chaguzi, ilibidi amkubalie na kurudi tena afrika, safari hii kwa ufadhili na kazi y Mfalme Leopold II wa Ubelgiji. Wakati harakati zao zikiendelea, Brazza Aliteremka na mto Orwege kwenye pwani ya Gabon na hatimaye kufika Mwaka 1880 alitokea mto mkongo na kukutana na mfalme(makoko) wa eneo la Teke kaskazini mwa Stanley Pool. Baada ya mwezi wa Majadiriano, makoko alitiliana saini na Brazza na kuiweka eneo lake chini ya Ulinzi wa Ufaransa. Huko Ubelgiji, International Africa Association ilibadilika na kuwa Committee for the Study of Upper Congo iliyokuwa na uungwaji mkono na wafanyabiashara wa kibelgiji. Mwaka 1881 wakati Stanley anafika tena Kongo, anakuta Bendera ya ufaransa ikipepea kwenye kijiji kiitwacho Ntamo, na punde kuitwa Brazzaville. Stanley alijua amepoteza eneo hilo sasa alihitaji kuharakisha kuchukua eneo kwa ajili ya Mfalme Leopold II. Hivyo aliingia makubaliano na Mfalme mwingine wa Teke aliyeitwa Ngaliema, na kukubaliana eneo la kusini liwe chini ya ubelgiji na kujenga kituo kilichoitwa Leopoldville kilichokuwepo karibu na kijiji kilichoitwa Nshasa, kabla ya wazungu kuiita kinshasa hapo baadae. (Baadae Stanley aligundua kuwa ametapeliwa na Ngaliema hivyo kulazimika kufanya makubaliano upya na mfalme halisi wa Nshasa).

Baadae makubaliano haya yalifikishwa kwenye mataifa yao na kuidhinishwa. Leopold II kwa ushawishi na ulaghai mkubwa alifanikiwa kupitia mkutano wa Berlin wa 1884 hadi 1885 kuifanya Congo yake kuwa huru- Congo Free State kwa maana ya Free from Taxes. Kufutia uhitaji mkubwa wa Mpira na pembe za ndovu, ujangili mkubwa ulifanywa nchini Kongo. Huku akiihadaa dunia kuwa taasisi yake ya International Africa Association ina kazi ya kiutu ya kukomesha utumwa, alifanya kazi kubwa ya kujinufaisha kwa kuua Takribani milioni wa tembo, alichukua mamia ya wakongo kama watumwa, aliua mamia ya wakongo. Madhila yalizidi na kelele za jumuiya ya kimataifa kuwa kubwa hasa kutoka Marekani, hatimaye serikali ya Ubelgiji mwaka 1908 iliichukua Kongo kutoka kwa mfalme Leopold II ambaye alifariki mwaka 1909 lakini akiwa hajawahi tia mguu wake nchini Kongo hata mara moja. Hadi kufikia mwaka 1910, dola kubwa ya Kongo ilikuwa ikitawaliwa na mataifa ya Ufaransa, ubelgiji na wareno. Ufaransa aliichukua Brazzaville, aliunganisha na Gabon, Oubangui Chari (Jamhuri ya Afrika ya Kati) na Chad na kuunda Federation of French Equatorial Africa. Koloni hilo la Ufaransa lilikuwa na eneo karibu sawa na Kongo ya Ubelgiji, lakini watu wachache zaidi huku miji ya Brazzaville na Leopoldville ikikua na kuwa ya kisasa.

******************
Alipofika Leopoldville, Bowane alikuta maeneo ya weusi zuio la kutotoka usiku kwa waafrika halikuwa kali maeneo ya waafrika kama ilivyokuwa kwa wazungu hivyo, maisha ya usiku yaliendelea. Baa zilianza kuchipuka huku bia zikiuzwa na live band zikipigwa au wakati mwingine muziki kutoka nje ulichezwa. Silivangi, Quist, Kongo, Congo-Moderne na Macaulay zilikuwa baa kubwa zilizokuwa eneo moja.
tumblr_ltbchycq9i1qgwmzso1_500.jpg


Mwaka 1904 ndipo Phonograph za kwanza kabisa kuingia Kongo ya Ubelgiji. Kufikia mwaka 1930 muziki wa ulaya kama classical music na dini zilikuwa zimeshamiri Kongo ya Ubelgiji. Wanamuziki kama King Oliver, Louis Armstrong, Tino Rossi pia muziki kutoka maeneo mbalimbali ya afrika na latin Amerika ulikuwa umeingia nchini humo. Wakongo wengi waliupenda muziki kutoka amerika kusini sababu muziki ule ulikuwa na vionjo vingi ambavyo wao wakongo walikuwa wakiviona kama vya kwao. Muziki huo uliongia nchini humo ulikuwa ni mradi wa label ya Kiingereza ya His Master's Voice ambao ulianzishwa mwaka 1933 ili kusambaza kazi ya Kampuni ya Kimarekani iliyoitwa Victor na Kiingereza iliyoitwa Gramophone na kufupishwa GV. Wakongo waliita Grande Vocaliste. Muziki wa walatini kama Havana Casino Ochestre na Sexteto Habanero kwa wakongo ilikuwa ni kurudi nyumbani kwa muziki wao, kwani muziki wa kilatino ulitokana kwa asilimia kubwa na watumwa wa kikongo. Pia mfumo wa uimbaji wa muziki huo ulishabihiana sana na wakongo hasa utamshi wa maneno ya kihispania ambao kwa wakongo walihisi ni lugha yao hasa lugha iliyokuwa ikiibukia wakati huo ya lingala.

Screenshot_20210710-121411.png

412DWHCXW0L._AC_.jpg

Mbali GV hizo, vyombo mbalimbali vya Muziki vilikuwa vimeingia afrika ya kati kabla ya GV, kutoka kwa wamisionary, wapelelezi na Wafanyabiashara. Mfano, Magita, banjo, pembe za kupuliza. Katika timu ya Stanley, lutenanti wake alikuwa na bugle. Stanley mwenyewe aliwaburudisha mara kwa mara timu yake kwa Kutumia kifaa cha accordion. Moja ya kifaa cha muhimu sana kwenye muziki wa Kongo, na pengine afrika nzima ni kiitwacho, kwa kongo, likembe. A thumb piano.

Likembe-lamellaphone-RDC-before-1877-Gift-A-Vivier-C-MIM-inv-108-Photo-Simon.png

Sambamba na hilo, kwaya za wamisionary walizofunzwa waafrika kwa kutumia vyombo vya kizungu vilichangia pia kuboresha muziki wa kikongo. Wamisionary walipiga marufuku vyombo vya kikongo kwa hoja kuwa zinafungamana na ushirikina. Lakini kuendana na jamii, ililazimu wakati mwingine kufuata tamaduni za wakongo. Mfano, nyimbo zilipigwa kwa kufuata mirindimo ya kikongo. Pia wakati mwingine walitunga kwanza katika lugha ya kikongo, kisha kuzihamishia katika utashi wa Kanisa.

Kufuatia makampuni ya kikoloni yalikuwepo Africa magharibi i.e Dahomey (benin) kutoka miji miwili ya Grande Popo na Petit Popo, Ghana, Sierra Leone kufungua matawi kongo kama Ollivant na Lever, wafanyakazi waliotoka nchi hizo za afrika magharibi kama waalimu na watu wa bandari, walikuja na vifaa vya muziki kama magitaa kutoka ulaya. Kwa kuwa walitokea miji hiyo iitwayo popo, wakongo waliwaita Popo. Ikimaanisha watu wa Pwani. Wakiwa nchini Kongo, walikuwa na makazi yao sehemu ya pamoja mjini yakiitwa Citas, mashariki mwa Leopoldville. Mida ya jioni watu hawa walikuwa wakijiburudisha kwa muziki. Hili liliwavutia wakongo kutoka sehemu zote mbili za mto Kongo ie Brazzaville na Leopoldville. Wakongo walikuwa wakiiga nyimbo za kigeni wakati mwingine wakifundishwa na Popo kupiga vyombo vyao. Mfano, wimbo maarufu sana wa El Manicero (Muuza Karanga) ulibadilishwa maneno na kuwa Eh Marie [mfumo huu hata kwenye Bongoflava wakati inaanza ulitumika sana].

s-l300.jpg

R-5407410-1392587253-9307.jpeg.jpg

Wakati wakijaribu vyombo hivi vya kigeni, waliendeleza sambamba na matumizi ya likembe. Mfano mtindo wa uchezaji wa agbaya ambao ulitumiwa na wakongo wengi waliokuwa Leopoldville ulichezwa kwa kuwa na vyombo kama Likembe na ngoma. Mtindo mwingine wa uchezaji maarufu ulikuwa ni Kebo, ambao ulikuwa maarufu sana miongono mwa wanawake. Mwaka 1929, mtindo mwingine wa muziki uliibuka, ukiitwa Maringa [ukitokana na Malinga uliokuwepo kwa muda mrefu ukitokana na jina la ngoma iitwayo Malinga]. Mtindo huu ulishamiri kiasi pande zote mbali za mto kongo kwa mpakani. Maringa ilihusisha likembe, chupa, Accordion, ngoma ya pembe nne iitwayo patenge. Mtindo huu ulijumuisha vionjo kutoka maeneo tofauti mfano kwaya za kiprotestant, midundo ya jeshi, na ulikuwa umeathiriwa na uzungu zaidi huku ukikosa muunganiko na kabila lolote la kikongo hivyo haukukua sana. Mchanganyiko wa wenyeji, muziki ulioletwa kutoka kwenye makoloni ya ufaransa, muziki ulioletwa katika GVs kutoka Latin America ulishahabiana sana na muziki wa jazz ulivyozaliwa Marekani kutokana na mchanganyiko wa waafrika, wahispania wenye asili ya afrika na muziki kutoka Ufaransa. Ufanano mkubwa wa Jazz na muziki wa kongo ulikuwa kutokana na Wote kuathiriwa na matumizi ya vyombo vya kizungu. Lakini tofauti ni moja, Muziki wa jazz Ulishikiria hasa matumizi ya Piano, brass na woodwinds zilizokuwa na asili ya ulaya. Muziki wa kongo wa kisasa, wenyewe ulishikiria hasa matumizi ya Gitaa ambalo sauti yake iliendana kabisa na ala yao ya asili ya likembe. Brass bands na piano hazikushamiri lakini Gitaa lilivuka pande zote mbili za mto Kongo.
***********
Kama ambavyo muziki, dini na mitindo ya kucheza kutoka ulaya ilivyoigwa na waafrika, ndivyo siasa za ulaya nazo zilivyowaathiri waafrika. Vita ya kwanza na ya pili ilihusisha mambo mawili, moja uzalishaji ulipaswa kuongezeaka zaidi kwenye migodi na viwanda ili kuhudumia vita na pili wakongo wengi walichukuliwa kwenda kupigana kwa upande wa Allies Powers. Mfano kampuni ya kibelgiji iliyokuwa ikichimba madini jimbonu katanga, Union Company Miniere de Haule Katanga, iliongoza zaidi uzalishaji wa madini kama ya Tin na Copper. Migodi iliyokuwepo kaskazini ya Kivu iliongeza uzalishaji dhahabu ili kuhudumia vita. Pia uzalishaji wa nguo na sukari uliongezwa zaidi. Hii yote ilimaanisha kuwa watu walitolewa zaidi vijijini na kupelekwa nje ya nchi kwenye vita na pia miji ya uzalishaji na majiji Ya kinshasa kwa Leopoldville na Ntiamo huko Brazzaville watu waliongezeka mara nne zaidi. Hii ilivuruga tamaduni za kikongo kwa kiasi kikubwa.

Kuongezeka kwa watu katika majiji hayo, kulienda sambamba na kukua kwa vipato vyao, hii ilimaanisha kuongezeka zaidi kwa mahitaji ya bidhaa kutoka ulaya, ikiwemo vifaa na bidhaa za muziki mfano magitaa, horns na Gramophone.

Mwaka 1935, radio ya kwanza ilifunguliwa na wazungu nchini Brazzaville, lakini ikiwa na eneo dogo la kushika. Serikali ilitia mkono wake, na mwaka 1940 iliiboresha kwa kufunga transmitter ya 50 kilowatts na hivyo kuwezesha Radio Brazzaville kushika kwenye makoloni yote ya ufaransa na maeneo mengi duniani. Leopoldville ilifunguliwa Radio ya kwanza, Radio leo mwaka 1937.

Radio-Brazza-1.jpg


artworks-reTMMafQMuB5Qis3-BinDxQ-t500x500.jpg

Na mwaka 1939 ilifunguliwa Radio nyingine iliyoitwa Radio Congolia chini ya umiliki wa Jean Hourdebise. Congolia ilitangaza kwa lugha ya kifaransa pamoja na za asili nne; kiswahili, lingala, tshiluba na kikongo. Sababu miji ya waafrika bado wengi hawakuwa na uwezo wa kununua radio, zilifungwa spika kubwa kwa ajili ya kusikiliza Radio Congolia ikiwemo muziki wa kutoka nje, Jazz na Pop hasa kutoka Latin America. Na siku ya jumapili iliwekwa kwa ajili ya kurekodi kwa wanamuziki kwa ajili ya kuchezwa baadae.

15740955_10211801470333202_2559952667826206696_n.jpg


image-54.jpg

Wakati wa vita vya pili vya dunia, serikali ya Ubelgiji ilifungua radio Congo Belge kwa lengo la kuhabarisha yanayojili juu ya vita kutokea BBC.

00000er15.jpg


jesse_01_kl.jpg


Kabla ya miaka ya 1930, wanamuziki wengi wa kikongo wasioimba nyimbo za kitamaduni, walikuwa wakiimba mmoja mmoja katika mabaa au sherehe kwa kupewa vinywaji bure au pesa kidogo. Miaka ya 1930 mwishoni, vikundi vya muziki kwa neno la kifaransa Ochestre(band) vilianza jitokeza. Kwa Leopoldville, Popo waliunda band yao iliyoitwa Ochestre Excelsior, iliyotokana na jina la band iliyokuwepo huko kwao Ghana iliyokuwepo miaka ya 1900. Askari jeshi wa kifaransa, Jean Rèal alikusanya na vijana wakikongo huko Brazzaville na kuunda band iliyoungwa Congo Rumba. Mwaka 1939, Albert Loboko wa Brazzaville aliyekuwa na uwezo wa kucheza Gita, Piano, mandolin, banjo na saxaphone Aliunda band aliyoiita Bone Esperance (Tumaini Jema) na kumchukua Paul Kamba aliyekuwa karani katika Kampuni ya madini huko kongo ya mashariki na kuwa manager wao. Paul Kamba alikaa miaka miwili, tu na mwaka 1942 alianzisha band yake iliyoitwa Victor Brazza.

Screenshot_20210710-125229.png
Band hii ilivutia sana mashabiki, na walisema wakongo kuwa kabla ya kuandisha mashairi yake, alikuwa akifanya mkataba na shetani. Brazzaville ilikuwa imetawaliwa na utabaka. Makazi yalikuwa kati ya wazungu na weusi. Lakini mji ya weusi ilikuwa ikukuwa kwa kasi na mkubwa ilikuwa ni Poto Poto na Bacongo. Lakini ubaguzi haukuwa mkubwa na masharti ya kufungiwa ndani usiku hayakuwa makubwa kama ilivyokuwa Leopoldville. Paul Kamba alikuwa eneo la Poto Poto. Upande wa Bacongo alikuwepo mkali wa eneo hilo, iliyeitwa Bernard Massamba maarufu Bernard Lebel. Aliungana na rafiki yake François banamabie na kuunda kundi lililoitwa Jazz Boheme. Hadi kufikia miaka ya 1940 katikati, Brazzaville tayari ilikuwa na Live music performances wakitumia hasa Ngoma, vyupa na scrappers. Walitumbuiza hasa kwenye shughuli za kijamii kama misiba, harusi n.k huku wakipata malipo kadri walivyokubaliana na matabi (kutuzwa)-msingi wa 'mapedegjee' kwenye muziki huu.
 
Dooh Shukrani sana mkuu..Nimeisoma yote japo ni ndefu nimejifunza vingi sana..Ngoja ni'play Rhumba moja la Anelka, El Mara."Fally Ipupa"APA linaitwa Mariana
 
Mimi sijawahi kuona mtangazaji kama Massoud Massoud. Jamaa ni mwamba HASWA.
AMESOMA MZIKI NA ANAJUA MUZIKI WA KILA AINA.

Binafsi Huwa naamka saa nane, saa Tisa saa saba na saa kumi na moja kumsikiliza masoud.

Mwenye Mawasiliano yake anisaidie wakuu.
 
Mimi sijawahi kuona mtangazaji kama Massoud Massoud. Jamaa ni mwamba HASWA.
AMESOMA MZIKI NA ANAJUA MUZIKI WA KILA AINA.

Binafsi Huwa naamka saa nane, saa Tisa saa saba na saa kumi na moja kumsikiliza masoud.

Mwenye Mawasiliano yake anisaidie wakuu.
Huyu mzee fundi sana. Nilitamani sana vipindi vyake viwe kwenye podcast. Nilikuwa namuambia jamaa mmoja yuko hapo hapo TBC juu ya wazo hilo, akaniambia, Mzee ni conservative sana kwenye modern tech hataki mambo hayo.
 
Mimi sijawahi kuona mtangazaji kama Massoud Massoud. Jamaa ni mwamba HASWA.
AMESOMA MZIKI NA ANAJUA MUZIKI WA KILA AINA.

Binafsi Huwa naamka saa nane, saa Tisa saa saba na saa kumi na moja kumsikiliza masoud.

Mwenye Mawasiliano yake anisaidie wakuu.
Ehhh Mkuu kumbe tuko wengi aisee cheers
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom