Duru za Siasa: Awamu ya 5 - Uongozi na Yanayojiri

KWANINI WATANZANIA HAWATAKI NA NI WAVIVU WA KUHOJI!
KWANINI KUHOJI IONEKANE NI KOSA AU UTOVU WA NIDHAMU?


ELIMU BURE

Wakati wa kampeni hapa duru tulihoji, kwanini Watanzania hawadai maelezo ya kina (details) kuhusu sera za vyama?

Tukasema mbele ya safari tusijeshangaa tukiuziwa mbuzi ktk gunia

Wapinzani wa UKAWA walikuwa na sera ya elimu bure. Wengi wakahoji kwa ukubwa wa wizara husika na udogo wa bajeti hilo linawezekanaje?

Tuliambiwa ni kupitia makusanyo ya kodi na ongezeko la wigo wa kodi ambayo hayakidhi viwango kwa sasa. At least walisema

CCM wakaiuchukua hoja ya wapinzani, tukasikia mgombea wao ambaye sasa ni Rais akiseama elimu itatolewa bure katika kiwango cha sekondari.

Wengine tukahoji kilishindikana nini miaka zaidi ya 20 na kipi kitafanyika tofauti sasa hivi? Tukaambiwa litawezekana chini ya falsafa ya Hapakazi

Awamu ya 5 ikaingia na kutoa uamuzi wa elimu bure, mabilioni yakipelekwa mikoani
Tunachoshuhudia ni wanafunzi kukalia mawe, wakisoma chini ya miti km chache kutoka Dar zilipo ofisi za serikali

Pesa zinazopelekwa hazikidhi mahitaji ya shule na changamoto zake

Tunaambiwa, tatizo linaonekana kusababishwa na wanafunzi waliokuwa hawendi shule.
Kwamba kuna ongezeko la wanafunzi baada ya elimu kutolewa bure

Kwa lugha zile zile za kawaida, tunaambiwa hiyo ni changamoto serikali inakabiliana nayo

Haya yanatokana na wananchi si serikali. Yaliposemwa majukwaani hakuna aliyehoji. Tulipohoji jamvini tulionekana 'wendawazimu' msimu wa vichwa kupata moto ulifika.

Tunachotakiwa leo si kuhoji tena matatizo ya elimu kama tunavyoambiwa
Tunatakiwa tuwaulize wahusika, hivi walitumia vigezo gani kusema elimu itatolewa bure?

Hoja ya ongezeko la wanafunzi waliokuwa hawaendi shule haina mashiko.
Nchi inajua idadi ya watoto na wananchi kwa ujumla.

Ilikuwaje tukaambiwa elimu itatolewa bure huku wahusika wakiwa hawana takwimu?

Je, walifanyi a kazi takwimu (homework) kabla ya kujiridhisha na kauli za elimu bure ?

Pili, kuna tofauti gani na mabilioni 21 yalitolewa kiholela bila kuhojia na hili la elimu bure?

Bilioni 21 zilitolewa bila mchanganuo wa kitaalamu, faida za muda mfupi na muda mrefu.

Hatukuhoji, kama ambavyo hatukuhoji elimu bure kwa uwezo gani?

Ndio maana tunasema, hii dhana ya kuimba tu kila kinachosemwa haitatusaidia.

Utamaduni wa kudhani kuhoji ni uhalifu, kupinga au utovu inatudumaza kifikra.

Tubadilike na kuhoji tukitaka majibu na si kumeza kila kitu bila kutafuna

Hizi mila za kuimba tu kila kitu bila kuhoji zinatuumiza kama taifa.
Hatuhoji, hivi tatizo letu ni lipi kati ya haya mawili, elimu bure au elimu bora

Lini tutasimama kwa muskatabali wa Taifa letu?

Tupo bize na name calling, hatuhoji tunasubiri ahadi nyingine tamu tamu tuimbe

Tusemezane
 
VYOMBO VYA HABARI

SASA WAKIRI NI MUHIMU KATIKA MAPAMBANO DHIDI YA MAOVU

WATAMBUA HAKUNA MAFANIKIO KWA KUSIFIWA NA VYOMBO VYA UMMA

Nape: Maslahi tasnia ya habari kulindwa

Katika mabandiko 90-94 tumezungumzia umuhimu wa vyombo vya habari na jinsi awamu ya 5 inavyojitenga navyo

Mgogoro mkubwa ni ule wa kuondoa matangazo ya TBC kwa kisingizo cha gharama.
Ukweli unaonekana, lengo ni kuficha maouvu na kuinusuru serikali. yalisemwa bunge lililopita, CCM na nyanatekelezwa

TBC kinachoendeshwa kwa kodi. Ukimsikiliza waziri , madeni ya TBC na TSN yanalipwa wananchi.
Hivyo, kuitumia TBC kama cha propaganda cha CCM na serikali ni ukikujaji wa maadili ya kiroho( immoral)

Wananchi hawakuhitaji udanganyifu wa gharama. Tunajua kwa maneno ya waziri vyombo hivyo vinadaiwa.
Hili ni jambo la kushangaza na kusikitisha na haionekani kama waziri ameliona tatizo halisi

TBC na TSN vinapata ruzuku na kuendesha biashara. Kama haviwezi kulipa bili zake pamoja na advantage zote hizo kuna tatizo kubwa. Vile vya binafsi vinawezaje? Na hapa tusema vya umma haviaminiki au haviendeshwi kitaalam n.k.

Tulisema katika mabandiko kuwa vyombo vya umma haviaminiwi wala havina mvuto kutokana na hulka ya kuchuja habari na kuwalisha wananchi habari za propaganda za CCM na serikali. Nyakati hizi za ushindani nani atasikiliza au kusoma ?

Waziri anarudi kujibu hoja zetu. Tuliuliza, awamu ya 5 inapIgana na maouvu itafanikiwa vipi ikivitenga vyombo binafsi?
Na kwanini inaficha habari au kutaka kudibiti habari za maouvu? Maouvu gani wanayopigana nayo na yapi bora yafichwe?

Waziri anarudi 'kuviangukia' vyombo binafsi.Siku 100 serikali imeona, shangwe za vyombo vya umma haisaidii na kuungwa mkono kutoweka kasi. Wananchi wanatafuta habari zao na si kusbiri zilizochujwa! wananona ukweli wanabaini ufichaji

Na endapo ubabe wa kutunga sheria uitaendelea, serikali itafeli kwasababu haitakuwa na msaada mwingine kutoka nje.

Waziri Nape anataka vyombo viaminiwe. Hilo si suala la kauli ni suala la utendaji.

Tido Mhando alirudisha heshima ya TBC, ni hawa hawa CCM waliokaa na kuunda majungu ya kumuondoa.
Leo CCM hao hao wanarudi kutueleza wanataka TBC na TSN viaminiwe!!! Huyu si tembo mweupe, na nani anadanganywa

Ukweli kwa waziri,vyombo ni spika za propaganda za CCM haviwezi kutumikia mabwana wawili, Umma na kisha CCM

Katika zama hizi za teknolojia, waziri aviimarishe tu kwa masilahi, si kuaminika na asitegemee kuaminika! myth

Tujiulize zaidi, hivi Rais anapoteua mwenyekiti wa bodi na waziri wajumbe, chombo hicho kina uhuru?

Bodi itasikiliza maelekezo ya Rais na waziri, halafu tunategemea iaminike!

Tume ya Warioba ilieleza vema namna ya kupata watu watakaolitumikia taifa, sasa hivi ni uamuzi wa mtu au watu

Tusemezane
 
Tukiangalia sasa hivi, viongozi wetu hawana maono. Hili la Zanzibar linaeleza kwa undani zaidi.

Hebu tulijadili bandiko linalofuata kabla ya kujadili 'mission'

La ZNZ na maono ya siku za baadaye

Itaendelea
I am so concerned ya wapi hasa Zanzibar inaelekea hivi sasa. Shaka yangu inazidi pale inapoonekana wazi kwamba agenda ya Zanzibar yenye mamlaka kamili is no longer CUF agenda as it used to be lakini hivi sasa hata wafuasi kindakindaki na wenye ushawishi ndani ya CCM nao wanaunga mkono hoja hii na ndio maana haikushangaza defeat ya CCM kwenye uchaguzi uliopita huko visiwani.
 
I am so concerned ya wapi hasa Zanzibar inaelekea hivi sasa. Shaka yangu inazidi pale inapoonekana wazi kwamba agenda ya Zanzibar yenye mamlaka kamili is no longer CUF agenda as it used to be lakini hivi sasa hata wafuasi kindakindaki na wenye ushawishi ndani ya CCM nao wanaunga mkono hoja hii na ndio maana haikushangaza defeat ya CCM kwenye uchaguzi uliopita huko visiwani.
Watu wenye mapenzi na taifa wapo concern kama wewe kwa sababu mbali mbali

Kwanza, tatizo la ZNZ kama unavyosema mwisho wake hautakuwa ZNZ tu, litatengeneza mazingira mazuri ya matatizo zaidi.

Tunasema hivyo kwasababu kama Rais wa JMT amejiwekea mzingo wa madaraka, mbele ya safari atasema nini?

Kama umesoma mabandiko tumeeleza agenda ya muungano wa mkataba inapata nguvu, agenda ya S3 haipingiki na agenda ya S2 imekwisha

Agenda ya mkataba na S3 ndizo option CCM inayotaka S2 imeonyesha hilo

Kama mkataba na S3 haziwezekani, option itakayokuja ni kupasua jahazi tugawane mbao

Ndani ya CCM znz wapo kama ulivyosema.
Hakuna mgombea CCM aliyelalamika, mawakala walikubali na kusaini fomu.

Kilichobaki ni kikundi cha watu wachache chenye nguvu sana ndani ya CCM

Nguvu yao ni kutishia kuirudisha ASP kama balozi alivyosema.

CCM wanakiogopa kikundi hiki bila kujua wanawaunganisha wnz na siku joto likipotea litahamia katika muungano.

Hawa viongozi wanaokwepa hawatakuwa na jinsi
Dhana ya muungano kulindwa kwa silaha ni mfu na hatujui kwanini hawajui

Mbaya Zaidi kwa Taifa la Tanzania ni haya

1. Tumeshaanza utamaduni wa kutoheshimu sharia na taratibu.
Kwamba, kutunga sababu na kuwadanganya wananchi na wanajua wanadanganywa. Uchaguzi wa ZNZ hauna utetezi wa aina yoyote

2. Tunajenga utamaduni wa mbegu mbaya. Kwamba, ili watu washinde lazima wachomeke mbegu za uovu bila kujali madhara yake.

Ubaguzi unaoonekana ZNZ kutendwa na CCM dhidi ya Raia ni hatari

Ipo siku watakosa hoja ya ubaguzi, watachomeka nyingine isiyofikirika. Tutajikuta katika matatizo makubwa

3. Imeanza kulea viongozi katiba tabia mbaya.
Hivi vijana wa UVCCM au UVCUF wanajifunza nini kutokana na haya yanayoendelea ZNZ? Nania takayeonea haya sharia za nchi tena

4. Imetuonyesha udhaifu katika uongozi.
Kwamba, hatuna viongozi wanaosimama na kusema hili sawa hili hapana. Tuna ombwe la wazee wanaoweza kusema hili ndiyo hili hapana.

5. Limetuvunjia heshima katika uso wa dunia.
Ile moral yetu imekuwa eroded na hatuna uwezo wa kusimama na kukeme immoral tena. Tunakwenda kukemea wapi na kwasababu zipi?

Kwa uchache hili limetubomoa kama Taifa kutoka kila kona.

Wanakimbia majukumu wakidhani majibu yatapatikana yenyewe.
 
Nguruvi3,

Moja ya mambo ambayo umeyaeleza hapo juu kuna hili: "Kama mkataba na S3 haziwezekani, option itakayokuja ni kupasua jahazi tugawane mbao...!" Kuna jambo nimekuwa nikihoji mara kwa mara hapa lakini sijapata jibu la kuridhisha... na hilo ndo hasa ambalo lilinifanya nipendekeze serikali tatu badala ya mbili za sasa! Ni kwanini CCM hawaoni kwamba hawana guarantee ya kuufanya muungano huu kwamba utakuwa ni wa milele daima? Ikiwa dola kubwa kama USSR lilisambaratika nini kitashindikana kwa kidola kidogo kama Tanzania? Ikiwa Yugoslavia ilisambaratika what's so special kwa Tanzania? The question is; hivi ikitokea muungano umevunjika automatically Rais wa Muungano anakuwa ameshapoteza sifa za kuongoza kwa kuwa alichaguliwa na pande mbili za muungano?! JPM atakuwa tayari kumpisha Kassim Majaliwa, au spika wa bunge au Jaji Mkuu? Hata huyo Spika wa Bunge au PM nao si walipigiwa kura na Wazanzibar? Hao nao si watapoteza uhalali? What if kama Jaji mwenyewe ndo kama huyu tuliyenaye sasa ambae ni Mzanzibar? Ninachojaribu kuangalia ni pale panapotokea ombwe la nani hasa anastahili kuongoza... hoja mbalimbali za kikatiba zitatolewa kuhusu ni nani hasa anastahili kuendelea kuongoza katika kipindi cha mpito. Katiba yetu inasema nini katika hili... au ndo tunaona muungano huu hauwezi kuvunjika ima fahima?! Lakini mgogo huu unaweza kukukosa nguvu endapo panakuwa na serikali 3.
 
Nguruvi3,

Moja ya mambo ambayo umeyaeleza hapo juu kuna hili: "Kama mkataba na S3 haziwezekani, option itakayokuja ni kupasua jahazi tugawane mbao...!

" Kuna jambo nimekuwa nikihoji mara kwa mara hapa lakini sijapata jibu la kuridhisha... na hilo ndo hasa ambalo lilinifanya nipendekeze serikali tatu badala ya mbili za sasa! Ni kwanini CCM hawaoni kwamba hawana guarantee ya kuufanya muungano huu kwamba utakuwa ni wa milele daima? Ikiwa dola kubwa kama USSR lilisambaratika nini kitashindikana kwa kidola kidogo kama Tanzania? Ikiwa Yugoslavia ilisambaratika what's so special kwa Tanzania? The question is; hivi ikitokea muungano umevunjika automatically Rais wa Muungano anakuwa ameshapoteza sifa za kuongoza kwa kuwa alichaguliwa na pande mbili za muungano?! JPM atakuwa tayari kumpisha Kassim Majaliwa, au spika wa bunge au Jaji Mkuu? Hata huyo Spika wa Bunge au PM nao si walipigiwa kura na Wazanzibar? Hao nao si watapoteza uhalali? What if kama Jaji mwenyewe ndo kama huyu tuliyenaye sasa ambae ni Mzanzibar? Ninachojaribu kuangalia ni pale panapotokea ombwe la nani hasa anastahili kuongoza... hoja mbalimbali za kikatiba zitatolewa kuhusu ni nani hasa anastahili kuendelea kuongoza katika kipindi cha mpito. Katiba yetu inasema nini katika hili... au ndo tunaona muungano huu hauwezi kuvunjika ima fahima?! Lakini mgogo huu unaweza kukukosa nguvu endapo panakuwa na serikali 3.
Haya maswali CCM hawataki kuyasikia, watasema ni uchuro kama si uchochezi. Kwao facts ni uchochezi

Kwanini CCM hawaoni kama hawana gurantee? Wapo kwa ajili ya leo si kesho
Kwao, madaraka ni sehemu ya kuweka 'mambo' sawa
Mfano, JK hakupaswa kukabidhi madaraka kati kati ya mgogoro mkubwa kama tulio nao

Mgogoro si ZNZ tu, kuna hoja ya uhalali wa Rais wa JMT kutokana na sababu zilizotolewa za kuvurugika kwa uchaguzi wa ZNZ. ''Akakimbia'' kwasababu amemaliza miaka 10

CCM wanaamini matumizi ya udanganyifu na vyombo vya dola yatadumu milele
Hawafikirii trend ya kinachotokea. Nani alidhani Dar itaanguka kwa wapinzani.

Si bahati mbaya umma unazungumza na ipo siku utapaza sauti

Rais anasema hana mamlaka na ZNZ kazi ni ulinzi kwa wafanyao fyoko. Can you imagine!
Kwamba, nchi imaemdeshwa kwa mabavu ya dola, si maridhiano ya wananchi

Katika uzi wa Tathmini ya uchaguzi hapa hapa, nimeeleza kwanini Hoja ya mkataba na S3 zitarudi kwa nguvu na kwanini S2 haitakuwa agenda tena,imefutika kabisa

Kuhusu viongozi hadi sasa Magufuli ni Rais wa ''upande mmoja''.

Hakuna kiungo cha SMZ na JMT . Na Rais kasema hana mamlaka ZNZ isipokuwa ulinzi.
Anachosema amani ikiwepo ZNZ, yeye hana lolote kule, ni Rais wa ''Tanganyika''

Kuhusu waziri mkuu, kuna vituko. Anaidhinishwa na bunge, hana mamlaka na Zanzibar.

CCM hawaoni ni jadi , na kwamba posho, vyeo n.k. ni muhimu kuliko mustakabali wa Taifa

Spika anachaguliwa na wote lakini mambo mengi anayosimamia ni ya Tanganyika.

Ndivyo ilivyo kwa kamati za bunge wazanzibar wanasimamia mambo yasiyowahusu

Kuhusu Majaji, nako ni vioja, yupo wa JMT na yupo wa ZNZ.

Nimekupa mifano hiyo kuonyesha maswali yako ni mazito CCM wasingependa kuyasikia

Kwao, siku inaingia inatoka. Matatizo yote CCM wanahusika. Hakuna aliyewahi kutawala
Haionekani wanajifunza kutoka dunia nyingine.

Viongozi wenye vision kama Nyerere walikubali mfumo wa vyama vingi wakijifunza kutoka kwingine. Hawa wa sasa ni kumaliza muda na kusubiri mafao na raha baada ya kuongoza

Kwa ya ZNZ, naweka kumbukumbu, yatakuwa na matokeo magumu sana mbele ya safari.

Yatarudi yakiuma 'sting back' vibaya sana.

Moja ya mambo yatakayobadilika ni muundo wa serikali. S1 au S2 ni off the table

Waliosimamia S2 wanajiona ni wapuuzi,walichoambiwa ni uongo maana ukweli unasemwa na wenye, hawana mamlaka ZNZ. Kama hawana, ni muundo gani uliopo sasa?

Rais atawaambia nini wananchi kuhusu ZNZ ikiwa amesema ZNZ ina mambo yao ''akiunga ''mkono hoja ya mkataba (ulinzi na usalama). hataweza kuipinga hoja ikurudi

S3 ndiyo option iliyobaki mezani

Nyingine ni kusoma vitabu vya Jose Bros Tito wa Yugoslavia, na Brezhenev wa USSR
kuhusu sambaratiko na sisi kama kadola itakuwa tatizo kweli.

Eritrea, Timor, Senegambia , Egypt/Syria walikuwa kama sisi, lakini CCM inaona sisi ni mabingwa haioni inavyopoteza ubingwa , haijifunzi inavyochukiwa na wananchi.

Haitazami ukweli kuhusu taswira yao ! Hawana kioo wana dola!
 
UINGEREZA NA UONGOZI
Uongozi si lazima uwe mafanikio.Yapo mafanikio, haba au kutokuwepo kabisa
Muhimu ni kutangulia na kukabiliana na changamoto,kuongoza umma

Kukimbia, kujificha au kukaa kimya si sifa(charater) za uongozi

Wakati wa machafuko ya 'hewa'ZNZ nyerere alisimama kukabiliana nayo
Hakutoa kisingizio, alitoa msimamo unaoweza kuwa sahihi au la

Mwalimu alijua, kukimbia tatizo , kujificha au kukaa kimya si suluhu
Akapoteza umaarufu visiwani ,hakujali alifanya kilicho sahihi, huo ni uongozi

1978 Rais Carter aliamuru kuokoa mateka wa Marekani nchini Iran.
Zoezi lilishindwa na kupoteza maisha zaidi. Uchaguzi uliofuata akapoteza.

Carter aliamini ni bora kuchukua hatua kuliko kukaa kimya, huo ni uongozi

Rais Obama akachukua hatua za kuvamia makazi ya Osama Pakistani
Alijua yaliyomtokea Carter yanaweza kujirudia

Aliamini kutenda ni muhimu kuliko kukaa kimya,huo ni uongozi

NasDaz Scotland. Cameron aliwaahidi waingereza mambo matatu. Kwanza, kura ya maoni ya Scotland

Pili, kutoa madaraka kwa washirika wengine kama ilivyo Scotland

Na tatu, kura ya maoni ya UK kubaki au kuondoka EU

Kura ya Scotland ilimazilika Cameron alisimama na serikali kuwataka Wascotch wasiondoke. Alitetea kwa hoja akiahidi kuangalia washirika wote

Juzi, amekwenda Brussles ambako EU ilikuwa na mashauri na UK kuhusu kubakia EU. Mashauri yalijadiliwa na EU kuipa '' upendeleo maalumu''

Cameron amerejea uingereza na kura ya maoni itafanyika June 23 2016

Msimamo wake ni kuwashawishi wananchi wa UK wabaki ndani ya EU

Wahafidhina wa serikali conservative wametangaza kutounga mkono EU

Cameron anajua uamuzi anaouchukua unaweza kumgharimu kisiasa.

Anafanya kwasababu ni wajibu wake kwa Taifa hadi wananchi atakavyoamua vinginevyo. Anawaongoza wafikie hitimisho. Huo ni uongozi

Suala la ZNZ linajirudia rudia. Muhimu ni kuelewa lipo na linarudi kila mara

Rais Kikwete alikaa kimya na kulikimbilia. Limerudi tena

Inaendelea
 
RAIS JK

Mwaka 2010 alikataa kuwaambia wazanzibar hatua za kurekebisha katiba yao, kuondoa na kuongeza mambo nje ya utaratibu ni kudhofisha muungano

''Alikaa kimya'' wznz wakitenda yao. 2016 katiba ya JMT imepoteza nguvu ndani ya Zanzibar. Bado tunaamini muungano una nguvu.

Kama kawaida, kila Rais huapa kuulinda muungano kwa nguvu zake zote

Pengine maana ya kuulinda haieleweki, lakini viongozi wa Uingereza wanatuonyesha

Muungano haulindwi na maderaya/mitutu, unalindwa kwa maridhiano na hoja

Rais wa awamu ya 5 amesema, atakaa kimya na hataingilia suala la ZNZ
Naye kama mtangulizi wake pengine haoni udhafu anaoujenga

wznz watakapomaliza matatizo yao, wataungana kutenda ya 2010

Wataunganishwa na kauli ''hana mamlaka znz'' na pengine ulinzi hautahitajia

Muungano utaodhoofika na pengine kufikia kikomo

Hatuwezi kukimbia, kujificha au kusingizia mambo, huo si uongozi ni udhaifu

Tusemezane

Humphrey Polepole
 
WANAOSEMA 'KUKURUPUKA' WANAKOSEA WAPI?

WAZIRI WA ARDHI 'AKWEPA' MZIGO WA BOMOA BOMOA

SERIKALI YA MITAA NA SERIKALI KUU ZAKAA 'KIMYA' UMEYA

Mabandiko ya awali tumeeleza kwa uchache maana ya uongozi.
Hoja ni kwamba, uongozi ni kuunganisha,kuonyesha na kukabiliana na changamoto

Tumetoa mifano kichache ya viongozi wa dunia na turudie michache tena

Mandela alipoachiliwa 'Umkhonto' walimuomba mikuki na mapanga walipe kisasi.
Mandela aliwajibu, kama ndivyo wanavyotaka yupo tayari asiwe kiongozi wao

Hakujali vijana wale walipigana na kumtetea kwa namna gani akiwa gerezani
Mandela alijali kilicho muhimu kwa Taifa.

Aliunda Tume ya maridhiano hata pale waliodhulumiwa hawakukubaliana naye.

Madiba alikabiliana na mzozo wa Inkhanta si kwa kukimbia au kukaa kimya

Kwa haya yanayoendelea nchini, zile thamani za uongozi zinatia shaka

Tumeona ya Zanzibar na jinsi yatakavyosumbua siku za mbeleni

Wapo waliohoji, hatua za serikali ni za kudumu, zimefanyia uchambuzi na zinajibu matatizo au ni hatua za kukurupuka. Taratibu tunaanza kupata picha

Hatua zilianaza kwa kuvunja nyumba za mabondeni.

Hakika kupanga miji na kukokoa maisha hilo ni muhimu.

Wengine tulihoji, kulikuwa na tafakuri au ilikuwa alimselema alija ili kupata sifa? Tukahoji sana, tatizo si ujenzi tu bali mfumo mbovu ulliosababisha hayo kutokea

Waziri wa ardhi ameelekeza ramani za maeneo zitakabidhiwa kwa wenyeviti wa vitongoji. Hao ndio watashirikiana na serikali kubaini maeneo yasisyostahili makazi

Hili ni baada ya kiongozi mmoja wa CCM aliyeshiriki kampeni kugusia 'kero'
Serikali ikasitisha zoezi na sasa inalirudisha kwa njia nyingine ikikwepa wajibu wake

Kwanini serikali ilianza bomoa bomoa na kwanini sasa inarudi kwa njia nyingine?

Majibu ya maswali hayo yanapatikana katika sehemu mbili
1. Kwamba zoezi halikuwa limeratibiwa, bali ilikuwa kukurupuka
2. Mfumo haukuwepo na sasa ndipo wanaona tatizo

Kukwepa lawama za CCM/serikali kuvunja,wanapeleka zigo kwa wenyeviti vitongoji

Zoezi lilikuwa zuri tu na linaungwa mkono, kasoro ni upangaji na utekelezaji

Katika uongozi hilo ni udhaifu. Viongozi wangeangalia tatizo kwa upana wasingefika hapo na zoezi la kuhamisha watu wa mabondeni lingebaki na maana yake nzuri

Itaendelea
 
YA WAZIRI WA ARDHI

Kurudisha zoezi la uvunjaji kwa wenyeviti ni kurudi katika mfumo

Zoezi la mkazi lilitakiwa liratibiwe na serikali za mitaa kama wajibu wao
Katika mfumo mbovu, ipo wizara ya ardhi na TAMISEMI.

Majukumu yake hayakuwa wazi, ndicho chanzo cha matatizo

Maafisa ardhi waliotoa vibali kwa baadhi wa wajenzi ni waajiriwa wa serikali kuu

Vipi serikali leo ione umuhimu wa kushirikisha serikali za mitaa?
Jibu ni kuwa mfumo wetu mbovu ndio uliozaa tatizo la ujenzi holela

Katika kurekebisha hilo, makosa yanaendelea kufanywa

Waziri wa ardhi anapowasiliana na viongozi wa serikali za mitaa, waziri wa TAMISEMI yupo wapi katika kuratibu shughuli zinazohusu eneo lake?

TAMISEMI ipo ofisi ya Rais, waziri wa ardhi anafanya kazi bila Tamisemi

Rais ni kiongozi wa serikali kuu, sasa anaongoza serikali za mitaa(TAMISEMI)

Wapi ilipo maana ya serikali kuu na serikali za mitaa?

Ndiyo sababu waziri wa ardhi anachukua majukumu ya waziri wa Tamisemi.
Kuongea na viongozi wa serikali za mitaa ni kuchukua jukumu lisilolake

Hapa ndipo mfumo mbaya ulipo na ndipo wengi wasipoelewa
Mfumo mbaya unaopigiwa upatu wa shamra shamra unajitokeza eneo la Umeya

Umeya! Inaendelea
 
UMEYA
Majiji mawili ya Tanga na Dar hayajakamilisha uchaguzi.

Hakuna sababu za maana ikiwa inajulikana wengi wanapewa.
Wapinzani wanaviti vingi kwa mfano Dar. CCM inakataa na serikali imekaa kimya

Hii ni kazi ya wizara ya Tamisemi inayomgusa Rais moja kwa moja
Hivi kweli hatuwezi kufanya uchaguzi wa Mameya ikiwa tulifanya uchaguzi mkuu!!

Serikali kuu na serikali za mitaa wanaogopa kukabiliana na ukweli kuwa CCM imepoteza chaguzi za majiji na zimekaa kimya kama ilivyo kimya suala la Zanzibar

Katika uongozi hilo ni kushindwa kwa kiwango cha juu.

Nchi hii ni yetu sote kuna tatizo gani demokrasia ikipewa nafasi yake?
Nani asiyejua wenye madiwani wengi ndio wenye meya?

Nani asiyejua wenye wabunge wengi ndio wenye Spika? Mbona halikuwa tatizo?

Tunachokiona ni matumizi ya vyombo vya dola.
Bila kutafuta ukweli kwanini uchaguzi unaahirishwa , vyombo vinakamata baadhi ya watu

Ile amri ya mahakama iliyosemwa ipo? Je, hilo vyombo vyetu vinalijua?

Hivi uchaguzi wa Meya ukifanyika baadhi wajumbe wakiwa hawapo kutokana na kamata kamata au kesi, kutakuwa na tofauti gani na uchaguzi wa marudio?

Kuna nini kinachotaka kufichwa katika majiji husika?

Kukaa kimya kwa serikali kunatoa picha mbaya. Kwamba, lipo jambo linalofichwa ambalo CCM na serikali yake wasingependa lionekane kwa kupoteza madaraka

Kukaa kimya na matumizi ya dola ni dalili za kushindwa maridhiano na uongozi

Kibaya, mfumo mzima umamhusisha Rais kupitia serikali kuu kama kiongozi na kupitia Tamisemi iliyo chini ya ofisi yake

1. Kushindwa kwa zoezi la vunja mabondeni ni dalili za awali za kukwama
2. Kushindwa kwa uchaguzi wa mameya ni kushindwa kwa demokrasia/ kujitawala

Bila kuwa na mfumo makini, tutaimba nyimbo zote, mwisho watatuambia hawajui kwanini sisi ni masikini. Wanaenda kula pensheni na marupu rupu na wajuu zao

Tutakuwa Taifa la kutumbua majipu na si kuongoza watu.

Hatuwezi kuongozwa ikiwa kuna nia ya mbaya nyuma yake.

Tutacheza mduara, na dalili zinaonekana kwa wenye macho! Tutafeli

Tusemezane
 
HILI LA 'UMEYA' NI AIBU YA TAIFA

HIVI KWELI TUMEFIKIA HAPA KAMA TAIFA?

Katika uzi huu Mitazamo na tathmini ya Uchaguzi 2015 tulieleza changamoto zinazomkabili Rais Magufuli.

Tulisema baada ya uchaguzi kazi kubwa ni kuwaunganisha wananchi kujenga nchi

Waziri mkuu alipokuwa jimboni kwake alitoa kauli ya 'uchaguzi umeisha...' sasa ni wakati wa kufanya kazi za maendeleo

Uchaguzi wa Meya unagubikwa na sintofahamu zinazotia aibu Taifa. Miaka 50 ya uhuru tumeshindwa kuheshimiana na kupanga namna ya kujitawala, bado tuna ndoto za Tanzania mpya inayonadiwa kwa nderemo na vifijo

Sheria za uchaguzi wa Mameya zipo wazi. Tulisikia wajumbe wakilalamika idadi inayorusiwa
Tukasikia hata fomu zao za wapi wanaishi zinapatikana tume ya uchaguzi (NEC)

Uchaguzi wa serikali za mitaa hauhusishi NEC, ilishangaza uwepo wa mahusiano yasiyoelezeka! mfumo wetu mbovu

Uchaguzi umeahirishwa mara kadhaa , kisa ni CCM kugomea na kutaka kutoa Meya.

Idadi ya madiwani inajulikana kama ile ya wabunge. Iweje basi wabunge wapate Spika na iwe nongwa kwa madiwani?

Wizara husika zipo zimekaa kimya. Wahusika wapo hawachukui hatua. Sheria zipo hazifuatwi

Tunaishi kama shamba la wanyama pori, kwamba mwenye nguvu ndiye atakayeishi siku hiyo na inayofuata

Imefikia mahali watu wanaongopa uwepo wa zuio la mahakama.

Mahakama imekanusha uwepo wa zuio hilo. Upo udanganyifu kwa kutumia chombo cha sheria, udanganyifu unao onyesha CCM hawana sababu za msingi za kuzua tafrani hii yenye aibu

Vurugu zimetokea , mbunge akawekwa rumande.
Mbunge ni public figure, yapo makosa yasiyohitaji hata kumweka rumande

Kilichofanyika ni kutaka tu kutoa ''adhabu'' hata kabla ya sheria kuchukua mkondo wake

Katika timbwili za namna hii inayopoteza si mameya wala madiwani, ni serikali.

Kwa muda wa siku kadhaa attention ya watu imehamia katika mgogoro huu usio na ulazima wa aina yoyote

Ufa na makovu ya uchaguzi yanaibuka upya. Katika Taifa lililogawanyika hali hiyo haisaidii serikali husika

Leo watu hawaongelei mambo muhimu ya Taifa wanaongelea uchaguzi wenye matatizo ya kutengenezwa

Yote yanaeleza jambo moja, kwamba, tumeshindwa kujitawala. Tumeshindwa!

Uchaguzi wa meya unaondoa focus ya mambo muhimu na kujenga chuki zisizo na maana hata kwa watoto wadogo

Hii ni aibu ya Taifa, tujiulize serikali hii itaongoza kwa maguvu hadi lini?
Nani aliwahi kusema gundi ya Taifa ni kutumia maguvu ?

Kwa haya ya mameya, yale matumaini ya wananchi kuhusu serikali iliyopo yanaondoka

Taratibu wanabaini hakuna kilichobadilika isipokuwa watu tu kubailishana viti

Tunafeli kama Taifa kwa mambo yasiyo na maana. Tuna viongozi na wamesimama wakiangali tuna feli

Kushindwa tu kupanga taratibu zetu na kuzisimamia kwa haki kama zilizvyo ni kufeli

Tutaendelea kufeli kama taifa hadi lini? Tutachekwa hadi lini? Na hili la mameya tunahitaji waangalizi wa kimataifa?

Hii aibu ifike mwisho, ni dhalili kwa Taifa ni fedheha kwa uongozi na kwetu sote. Haki itolewe tulijenge Taifa

Inasikitisha sana miaka 50 viongozi wanaendekeza haya bila aibu wakitueleza sasa ni mwendo mpya! Upi huu tunaoona?

Tusemezane
 
UMEYA: SERIKALI 'INAJICHAFUA'

TUNAFELI: TUNATUMBUA MAJIPU, TUNALINDA MAJIPU KWA ULAGHAI


Zipo sheria za kuwabana watoa matamshi ya kuvuruga amani katika jamii.
Zimetumika si mara moja au mbili, marehemu Mtikila akiwa muathirika

Uchaguzi wa Meya wa Dar uliahirishwa kwa 'uwepo wa zuio la mahakama'
Mahakama imekana uwepo zuio. Hakuna shaka na kauli ya chombo cha sharia

Vurugu zimetokea na kuweka amani katika majaribu. Aliyetoa kauli anajulikana.
Si mtu au mjumbe bali kiongozi wa serikali yupo huru licha ya kuvuruga amani

Waliokamatwa pengine walitenda kwa kuchagizwa(provocation)

Vyombo vya dola vimewakamata na si aliyeleta tatizo. Sheria ipo wapi kwa hili?

Kulikuwa na mgawanyiko baada ya uchaguzi mkuu.
Wananchi 'wakasahau'wakitumaini kuona nchi inasonga mbele na si kuingia matatizoni

Duru tulisema viongozi ni wale waliokuwa kimya Taifa likigeuzwa mali ya watu, kuporwa n.K.. Haiwezekani waliosoma vitabu vya zamani wakaja na mbinu mpya!

Majipu yakatumbuliwa. Zikawepo hisia watu wakihusisha utumbuaji na mirengo ya kisiasa. Kwamba, waliokataa 'kushirikiana' na wenzao walipewa 'kibano'

Wananchi walipuuza hisia na tetesi wakaelekeza macho yao kwa utendaji wa serikali

Haya ya Umeya yanarudisha hisia na chuki za uchaguzi zilizokuwa zimekwisha.

Wapo wanaojiuliza, ikiwa umeya unafanyiwa hila, nini kilitokea uchaguzi mkuu ?

Ikiwa vyombo vya dola vinachukua hatu tulizosema hapo juu, nani alisimamia haki za upande mwingine wa uchaguzi?

Mjumbe anakamatwa, aliyesababisha yu huru,nini kilishindikana uchaguzi mkuu?

Hoja nyingine inayozunguka midomoni ni ukweli ulio wazi.
Mbona wabunge wa upinzani na wa chama tawala mkoa mmoja na hakuna tatizo?

Nini kinatokea katika umeya? Ni kipi kinapiganiwa au kinachofichwa kisijulikane?

Zipo hisia bila ushahidi kinachotakiwa kulindwa ni utawala wa miji na majiji yaliyotumika katika maovu, zinasemwa, kwa mazingira zinapata miguu bila sababu

Ukitazama mchangyiko wa hisia na matukio si wote wanaweza kuamini
Wapo watakaochukulia hisia ,tetesi na kupata maana ya kufikirika

Ukizingatia kuwa Tamisemi ipo chini ya ofisi ya Rais ambayo imekaa kimya yapo yanayojitokeza. Kwanza, ni kipi kinacholindwa na serikali na kwasababu gani

Pili, serikali inayotumbua majipu inatenda inachosema?(walk the talk)

Tatu, serikali hii itatumbuaje majipu ikiwa uadilifu unajengewa mashaka?

Katika hili serikali ndiyo inayopoteza sana. Focus imeondoka, wananchi hawajali kinachozungumzwa bali kuzungumzia kukamatwa wabunge.

Imani inaondoka kwa serikali ,watu wakiuliza ndiyo mabadiliko waliyotaka?

Bila haki kutendeka, kila kitakachofanywa na serikali kitaonekana mbele ya watu kama uonevu tu, mazoea yale yale, ni wale wale, hawana jipya n.k.

Hata zikitumika mbinu kulinda kinacholindwa, serikali inapoteza kila dakika timbwili hili likiendelea. Usikivu wa wananchi unapotea, umoja wa Taifa unaingia doa.

Wananchi watakata tamaa wakisema CCM na serikali yake ni ile ileee waliyoichukia!

Ndio mwanzo wa kufeli kwa nchi. Tutafeli kama Taifa kwasababu uongozi utatufelisha kama siku za nyuma ilivyotokea. Wananchi watahisi kudharauliwa.

Hawataiangalia serikali kama ya kidemokrasia bali ya maguv na ubabe.
Haya ndiyo yaliyoijengea sana chuki CCM wakati wa uchaguzi hadi kukana jina lao

Hili la umeya tunarudia , linaichafua serikali, linawagawa wananchi, linajenga chuki

Hivi umeya umekuwa tatizo linalohitaji fedha za kigeni au wasimamizi wa mataifa!!!

Hii kama si kufeli na aibu ni kitu gani?

Tusemezane
 
WAZIRI TAMISEMI AJIUZULU

NI KUINUSURU SERIKALI NA KADHIA/ AIBU ZINAZOENDELEA

TAMISEMI IPO CHINI YA OFISI YA RAIS

Ni takribani mieizi mitatu kumalizika uchahuzi mkuu ukiwemo wa madiwani
Baadhi ya majiji yamekumbukwa na tatizo la kupata viongozi kwasababu zisizojulikana

Hata hivyo ni haki kusema, pale CCM waliposhinda hakna tatizo. Tatizo lipo eneo waliloshinda wapinzani. Kwamba, CCM hawataki wapinzani washike madaraka

Mfano ni Jiji la Dar es salaam ambalo Rais anaishi hatua chache kutoka jengo la Karimjee. Wizara ya Tamisemi ipo katika Ofisi ya Rais ikisimamia shughuli za serikali za mitaa

Mvurugano unaoendelea unaashiria CCM kutokubali kukabidhi Jiji kwa wapinzani.

Wananchi walipoamua kwa njia ya kura,CCM kwa kiburi nakutumia serikali wanakataa

Ipo ''hoja''miradi na ufisadi mwingi unaohusisha watu wazito imefanyika kupitia Jiji.

Zipo ''.hoja'' kuwa uuzwaji wa mashirika kama UDA ulifanyika kunufaisha familia.
Na zipo hisia pesa nyingi zilipitia Jiji kwa kutafunwa

Uchaguzi wa wiki iliyopita umeahirishwa kipuuzi na kitoto na kijinga sana

Mahakama imekataa kuwepo kwa zuio. Kinachoshangaza, mwanasheria wa jiji na afisa tawala inasemekana walisoma taarifa waliyopewa.

Waziri husika anataka uchunguzi kwa jambo lililo wazi! kwamba hajui kinachoendelea!!

Kitendo cha uzembe katika uchaguzi ni ishara waziri husika ima hafai, ameshindwa kazi. Kama anafaa basi ni kwa maelezo ya juu na hapo tutahoji maadilli

Kitendo cha waziri kushindwa kupata taarifa za zuio mapema pengine kuliko mtu mwingine, kina maana moja, Hafai na ameshindwa kazi.

Kama si yeye ofisi ya Rais inajua nini kinaendelea katika aibu hii kubwa?

Inaendelea
 
Rais amenukuliwa mara nyingi na juzi akiwa Arusha alisema ni Rais wa wote
Hatawabagua kiitikadi za siasa kikabila kidini au kwa namna yoyote

Rais 'amezungumzwa' kama mtu mwenye imani kwa maana anamuogopa mungu

Yote mawili yana maana kubwa katika uongozi wa nchi. Kwamba, atasimamia haki

Haki ni ya wapinzani kuongoza Jiji, si kwasababu ya huruma ni kupitia sanduku la kura

Inapotokea haki ikaminywa kwa hila, tujiulize, wote wanatendewa bila kuwagua?

Kwamba,mungu anayeogopwa ni kweli anaogopwa au ni kauli tu za midomoni 'lip service'

Katika mazingira ya kawaida waziri Tamiseni anayemsaidia Rais ameshindwa kazi.

Mbona hatumbuliwi kama majipu mengine? Migogoro ni ishara Tamisemi imeshindwa

Mbinu za kukamata wapinzani hazisaidii na zinajenga hisia za uonevu! Mungu anaogopwa?

Waliosababisha matatizo wanajulikana, hawachukuliwi hatua kwasababu ni 'mpango' kutoka wasikojua hata wao.

Wanapewa karatasi na kuzisoma bila kujua nini kifanyike. Kuna haki? Mungu yupi anayegopwa? Kuna maadili hapo na ubaguzi je!

Kwanini wasifukuzwe kazi kwa kusababisha uvunjifu wa amani?

Ule ucha mungu unaongoza kutobagua upo wapi?

Ile fagia fagia inayokumba wengi mbona inaacha baadhi? Hali ipo wapi? haki ipo wapi?
Wanaosimaia haki wanatenda haki? Wanamuogopa mungu?

Kwa hili la uchaguzi, Waziri ajiuzulu kwa uzembe kuikoa ofisi ya Rais inayohusika

Endapo hatajiuzulu, ofisi ya Tamisemi chini ya ofisi ya Rais itabeba mzigo mzima

Wapo watakahoji, ile kauli ya kuhudumia bila ubaguzi ina maana tena ?

Wapo watakahoji uadilifu, na kama fomu za maadili zina maana yoyote

Hakuna namna itakayoweza kuikoa ofisi ya Rais kutokana na hili isipokuwa kwa njia mbili

1. Waziri ajiuzulu ili kuinusuru serikali
2. Rais amwajibishe waziri kama sehemu ya majipu

Hayo yasipotokea wananchi wanaweza kuhoji mambo kadhaa
1. Kuna uadilifu katika kutenda bila kuonea au kubagua?
2. Ile kauli ya kumuogopa mungu na kwamba viongozi waombewe ina maana tena?
3. Kuna sababu ya kutumbua majipu na nini lengo la kutumbua ikiwa wengine wanalindwa?
4. Watakaoamini kumelenga baadhi ya ''watu, makundi'' watakuwa wamekosea nini?

Mbele ya safari hili suala litaisumbua sana serikali. Kuna maswali yatakayojiokeza kila siku

Kuepuka hilo, hatua za kuinusuru serikali na kadhia hii zichukuliwe mapema, waziri wawajibike au awajaibishwe.

Bila hivyo Rais atakwazika, uadilifu utahojiwa, ucha mungu utatiliwa mashaka, na kutenda bila kubagua itakuwa kinyume chake

Tumefeli kwasababu hizi za kulindana na haineokani kama utamaduni umeachwa

Tutafeli tena kwasababu wanalindana, wakitumbua majipu ya wasioweza kulindwa!

Tunafeli na tunacheza mduara!

Tusemezane
 
UADILIFU NA KUKURUPUKA

WANANCHI WANAPOSHINDWA KUHOJI

Turejee mabandiko yafutayo #73 na 74 tulieleza kuhusu 'nia' na dhamira.
Tukasema nia inaweza kuwepo lakini dhamira ni 'courage' ya kutimiza nia.

Bandiko #83 tukasema hata kama Rais ana nia, dhamira imezingirwa na CCM
Tukaonyesha wanavyojipanga bungeni hadi katika chama 'kumzingira' katika kutimiza nia

Hili sakata la uchaguzi wa mameya linaeleza tuliyosema. hatuamini kama uchaguzi mdogo sana unazungushwa miezi 3.

Kinachoonekana CCM inapanga mbinu kubaki-uongozi wa Jiji.

Demokrasia imeshasema, haya yanatokeaje? Hapa ndipo dhamira inapokuja.

Pamoja na nia ya kukabiliana na maovu, dhamira ya kufanya hivyo haipo.

Na kwamba, tayari CCM wameshazingira nia na dhamira, kinachoonekana ni kushindwa kwa Tamisemi na Taifa kwa ujumla

Endapo nia ni kupambana na maovu, nini kinasumbua CCM kiasi hiki? Hofu ya nini?

Kinachotakiwa kufichwa na CCM ni kung'ang'ania uongozi na kua ''nia na dhamira''

Tunasisitiza, hii ni aibu ya Taifa, inayondoa sehemu kubwa sana ya '' nia na dhamira'' ya kupambana na uovu. Mapambano ya uovu hayachagui, iweje yanachaguliwa baadhi?

Katika bandiko [HASHTAG]#106[/HASHTAG] tumeuliza, hivi ni kwanini Watanzania hatuna utamaduni wa kuhoji?

Tumezungumzia sana suala hili. Yanayoendelea yanazidi kutukumbusha tatizo la kutohoji

1. Hatuhoji nini kinafichwa kwa CCM kung'ang'ania ongozi wa majiji na halmashauri
2. Hatuhoji fomu za maadili ya viongozi na tume ya maadili ina maana gani kwetu
3. Hatuhoji haya mauza uza ya NSSF yanatokeaje na kwanini yaotoke

Tumejikita katika kudakia hoja bila kwenda kwenye mzizi wa chanzo.
Wengi wanamlaumu waziri kwa sakata la NSSF, hawajiulizi limeanzaje na kingezuiwaje

TUANZE NA FOMU ZA MAADILI
Kauli ya mawaziri kutakiwa kurudisha fomu katika masaa machache ama sivyo watajifukizisha kazi ilitawala anga za habari kama tukio kubwa.

Kwamba, mawaziri wanapewa deadline ikionyesha seriousness katika kazi i.e hapakazi

Hakuna anayejiuliza fomu hizo kwanini haziwekwi hadharani tukajua kilichomo.

Inasemwa anayetaka anaweza kwenda kuziona, lakini ni mlolongo mrefu wenye urasimu usiotoa fursa kirahisi. Suala si kwanini mawaziri hawakujaza, suala ni nini walichojaza !

Tukavutwa na masaa yalitolewa bila kuhoji kurudishwa kwa fomu kuna athari gani kwetu
Kwanini wasiongee huko wenyewe kwa wenyewe kwavile sisi hatujui wala kuona walichoandika. Hapa ndipo tatizo letu lilipo, tunashabikia hatuhoji

Zipo hoja tatu kuhusu suala la fomu za maadili linalojadiliwa katika mitandao, JF ikiwemo
1. muda waliopewa mawaziri kurudisha fomu
2. Umuhimu wa Tangazo kwa umma
3. Hakukuwa naumuhimu wa kutaarifu umma

Tutafafanua......
 
FOMU ZA MAADILI

Inaendelea...

1. Muda waliopewa mawaziri kurudisha Fomu

Tangazo lililenga kutoa ujumbe kuwa katika suala la maadili hakuna atakayesalimika.

Na kwamba atakayeshindwa aone mfano wa mawaziri, na kwamba hapa ni kazi

Tuliambiwa baraza limeundwa kwa muda mrefu ili kupitia majina na kupata watu safi.

Kwanini watu hao safi wasite kurudisha fomu zao? Nini kiliwakwaza?

Tangazo ni jema, yanayotokana na tangazo yanatia shaka Zaidi

2. Umuhimu wa tangazo kwa umma

Wenye hoja hii wanasema ni muhimu umma ukaona serikali ikisimamia maadili ya viongozi.

Kwamba, walipochaguliwa tulitaarifiwa,vipi wanapochelewa kurudisha fomu tusiambiwe?

Hoja hii ina swali moja, kutangazia umma kama ni muhimu mbona hatuambiwi fomu zina kitu gani na kwanini kuna urasimu kuzifikia?

3. Wapo wanaosema hakukuwa na umuhimu wa Tangazo

Kwamba, waziri mkuu na mawaziri wangewasiliana tu. Hoja hii inajengwa na hoja kuwa kutangaziwa na muda wa kurudisha hakubadili lolote ikiwa hatuambiwi fomu zina nini na kwanini kuna urasimu wa kupata habari zake

Msingi wa hoja ni kuwa kama tume ya maadili ingalikuwa na meno ya kutosha hilo halikuwa suala la waziri mkuu au ofisi ya Rais.

Tunarudi kule kule kuwa mfumo wetu una unga unga haupo kamili na unahitaji kufumuliwa

Tusichukue hoja nzito na kuzifanyia tathmini nyepesi , tutapotea. Ni muhimu kushughulisha akili zetu ili tusije kuwa waathirika wa mbwemmbwe za kisiasa 'political stunt'

NSSF kimetokea nini? Inaendelea....
 
MKANGANYIKO NSSF
HAUKUTOKEA KWA BAHATI MBAYA, MFUMO NDIVYO ULIVYO

Mjadala unaendelea baada ya waziri kumchagua mrithi wa mkurugenzi mkuu wa NSSF

Kizungumkuti ni pale uteuzi ulipotenguliwa siku hiyo hiyo

Sababu ni kutokamilika kwa baadhi ya taratibu, kauli za kawaida kuficha ubovu

Mjadala wa uraia wa mteule haupo baada ya mamlaka husika kutoa ushahidi wa uraia

Kama tulivyosema bandiko 106, Watanzani ni watu wa matukio na wasiopenda kuhoji

Tatizo si waziri , yeye ni 'muathirika' wa hatua zilizochukuliwa pengine bila kushirikishwa

Rais wa JMT alitoa taarifa ya kuteua mabalozi akiwemo mkurugenzi wa NSSF

Kwa maujibu wa tangazo, mabalozi wateule walisubiri kupangiwa vituo.

Kwa maana nyingine waliteuliwa kwanza kabla ya kujua watatumikia Taifa eneo gani

Yapo mashaka, kulikuwa na ulazima gani wa kuwaweka viporo nje ya nafasi walizotumikia?

Nini kingeharibika iwapo wangeendelea na kazi hadi siku watapoteuliwa na vituo vyao?

Kuwaondoa katika nafasi bila kujaza inaleta maswali sana.

Kulikuwa na dharura yoyote ya kuteua mabalozi wasio na vituo hadi wakati huo?

Na tujiulize, hivi mabalozi wanateuliwa bila kuzingatia sifa zao na eneo waendako?

Hali hiyo ikazaa ombwe (vacuum). Wasomi wa physics watatusaidia kueleza, kwamba kunapokuwa na pressure na kukatokea ombwe, pressure hujielekeza kuziba ombwe

Ndicho kilimkuta waziri husika. Kwamba, alitakiwa ajaze nafasi iliyoachwa(vacuum) katika pressure kubwa kutokana na uzito na umuhimu wa taasisi husika

Kilichofuata ni kutofuata 'taratibu' na kutengua uteuzi siku ulipotangazwa

Waziri hapaswi kulaumiwa, tatizo halikuanzia kwake.

Tutakapoongelea kuteua 'raia' wa nje, ingalitokea kuwa ni kweli bado asingelaumiwa.

Rasimu ya Warioba ilipendekezwa tume ya utumishi ili kuchunguza wahusika kwa sifa

Hili lililenga kumuondolea Rais pressure inayotokana na teuzi kama hizi.

CCM na Serikali yake wakakataa rasimu husika, madhara yanaonekana sasa

Hili linakuja katika suala lile lile mfumo wetu ni mbovu na huu ni mfano mzuri

Kumtwisha waziri lawama kwa mfumo mbovu, kwa hatua zilizochukuliwa bila kuzingatia matatizo yanayoweza kujitokeza, kwa hatua za haraka zisizo na sababu ni kumuonea

Tusemezane
 
KULIKONI NA HAYA YANAYOTOKEA?
ILIKUWA HAZINA, IKAWA NSSF NA SASA IKULU


Habari iliyobeba uzito wikiendi ni kuondolewa kwa katibu mkuu kiongozi Ikulu(CS)
Katibu mkuu kiongozi ndiye msimamizi wa utumishi serikali

Majukumu yake si ya Ikulu, yupo katibu mkuu wa Ikulu katika majukumu hayo

Katibu mkuu kiongozi(CS) aliteuliwa awamu ya nne na kuteuliwa tena na Rais tena

Ieleweke vema, kulikuwa na uteuzi rasmi wa nafasi hiyo, na hakuwa anaendelea tu!!

Nafasi ya CS ni ya uteuzi wa Rais kupata mtu wa kufanya nae kazi kwa ukaribu

Kinacholeta maswali ni ile hali ya uteuzi na utenguzi katika muda mfupi.
Aidha, hakuna historia ya watangulizi wa nafasi hizo kupangiwa kazi nyingine

Siku za nyuma Rais alimteua bwana Maswi katika nafasi ya unaibu Hazina.

Zikawepo tetesi tetesi sakata la Escrow linaweza kurudi bungeni.

Uteuzi ukatenguliwa na mhusika kupangiwa ukatibu tawala baada ya 'kazi maalumu'

Wiki chache zilizopita kulifanyika uteuzi wa mabalozi wakisubiri kupangiwa vituo!!
Uteuzi ulimkumba mkurugenzi mkuu wa NSSF.

Kuondolewa mkurugenzi wa shirika la umma na kupewa ubalozi, imezua maswali mengi

Wiki iliyopita gazeti moja liliandika tuhuma dhidi ya katibu mkuu kiongozi(CS) kushirikia kwa kile kilichoonekana mambo kinyume na taratibu au miiko au maadili

Ikulu ili onya gazeti kukanusha habari kinyume chake sheria zitachukua mkondo wake

Pia wiki hii, kumefanyika uteuzi wa mkurugenzi wa NSSF na kutenguliwa siku iliyofuata

Historia inaonyesha nafasi ya CS hushikiliwa kwa muda mrefu.

Inapotokea uteuzi wa miezi michache kutenguliwa inazua maswali.
Tunasema hayo kwasababu kulikuwa na barua rasmi ya uteuzi wa CS

Maswali ya kujiuliza
Je, utenguzi huu una sababu nyingine inayohusiana na tuhumu zilizotolewa?
Je, ni hatua za kupata watendaji anaowaamini,kwanini hakufanya hivyo alipoingia ofisini?
Je, ni kushindwa kasi na kutokea madudu kama ya NSSF ambayo CS ana sehemu yake?
Ni wakati gani katika historia ya nchi yetu CS aliwahi kupangiwa kazi 'nyingine"

Kwavile utamaduni wa kutumbua majipu umekuwa wa uwazi, umefanyika hadharani, wananchi wangependa kusikia kuliko kwa hili la katibu mkuu?

Ni fair kusema hivyo kwasababu tumeweka viwango(std), kutumbua na kueleza kwanini

Tusemezane
 
WALK THE TALK (KUISHI KWA KAULI)

HAKI ZA RAIA ZILINDWE, UONEVU NI KINYUME CHA KATIBA

LINI TUTAJIFUNZA KUHESHIMU TARATIBU ZETU WENYEWE?


Sehemu ya I katika III

Matukio kadhaa yanayoendelea kuchukua kasi yakihusisha ukiukwaji wa haki za Raia
Haki za Raia zimeanishwa bayana katika katiba yetu(mwaka 1977)

Viongozi wanapopatikana, kiapo chao kikubwa ni kulinda na kuwatumikia Raia kwa haki
Rais amelisema mara nyingi, na juzi akiwa Arusha amerudia kulisema.

Kwamba ni Rais wa wote bila kubagua itikadi za kisiasa, dini ukabila au ukanda
Kauli hiyo si ya hisani ni wajibu kwa mujibu wa kiapo chake.

Swali tunalotakiwa kujiuliza, je viongozi wetu 'wanaishi kwa kauli zao''?(walk the talk)

Tunauliza swali hili kwa kutazama vitendo vinavyoendelea ukilinganisha na kauli ya Rais

Yapo matukio ya 'kuminya au kunyang'anya' uhuru wa wananchi kwasababu zisizo za kikatiba/kisheria zeye chembe za uonevu kwa matumizi yasiyo mazuri ya vyombo dola

Raia wa nchi ni huru kwa mujibu wa katiba hadi katiba na sheria zitakapoeleza vinginevyo.

Kumuondolea uhuru kwa dakika, ni kukiuka haki za binadamu, katiba na utawala bora

Sheria zinaeleza taratibu za kuondoa au kunyang'anya uhuru wa mhusika inapobidi.
Zimetoa haki kwa mtuhumu/mtuhumiwa kuhakikisha taratibu(procedure)zinalindwa

Na mhusika anabaki kuwa hana hatia hadi sheria itakapoeleza vinginevyo kwa mujibu wa katiba.
Na kwamba, raia wote wana haki sawa mbele ya sheria na kupata sheria ni haki

Hata anapokuwa na tuhuma, au hatia zipo haki zisizotakiwa kukiukwa kwa utashi wa watu wenye dhamana ya kulinda sharia, kusimamia au madaraka ya kisiasa au kiutawala

Kukamatwa/kukamata/ kushtakiwa/ kushtaki/ kusomewa mashtaka/dhamana ni haki za kawaida kabisa zinazoongozwa na sheria na si utashi wa mtu, watu au kundi la watu

Kwanini basi haya hayatendeki tunashuhudia sheria za kufikirika na kukomoana?

Kwanini vyombo husika vinachukua hatua kwa matakwa na utashi na si taratibu au sharia?

Inaendelea....
 
Back
Top Bottom