CHADEMA yasitisha maandamano Moro

nngu007

JF-Expert Member
Aug 2, 2010
15,862
5,797


Baraza la Vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo ,CHADEMA, (BAVICHA) mkoa wa Morogoro limesitisha maandamano ya amani yaliyoandaliwa na Baraza hilo.


Maandamano hayo yalipangwa kufanyika tarehe 5/3/2012 katika mkoa wa Morogoro.

Madhumuni ya maandamano hayo yalikuwa kupinga vitendo vya unyanyasaji vinavyofanywa na Jeshi la Polisi dhidi ya wananchi wasio na hatia na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Maandamano hayo yalikuwa yafanyike katika wilaya zote za mkoa wa Morogoro na kushirikisha wafuasi wa CHADEMA, wanaharakati, wasomi pamoja na wananchi wanaoguswa na vitendo vya unyanyasaji vya jeshi la Polisi.

Lengo kuu lilikuwa kufikisha ujumbe kwa Serikali na Jeshi la Polisi kiujumla juu ya vitendo hivyo vya unyanyasaji ambavyo vimekuwa chanzo
cha mauaji ya wananchi wasio na hatia na hivyo kuhatarisha amani ya nchi.

Hata hivyo, BAVICHA Mkoa wa Morogoro imeamua kusitisha maandamano hayo kufuatia kikao cha pamoja kilichofanyika tarehe 2/3/2012 kati ya mkuu wa mkoa wa Morogoro, Mh. Joel Bendera na viongozi wa BAVICHA mkoa na wilaya ya Morogoro.

Katika kikao hicho kilichofanyika katika ofisi za mkuu wa mkoa, CHADEMA iliwakilishwa na mwenyekiti wa BAVICHA Mkoa, Mh. Boniface Ngonyani na mwenyekiti wa BAVICHA wilaya, Mh. Innocent Zawadi.

Kikao hicho kilifuatia wito wa mkuu wa mkoa wa Morogoro, Joel Bendera kukutana na viongozi hao kwa lengo la kujadiliana juu ya mambo mbalimbali kabla ya maandamano hayo kufanyika.

Hata hivyo, katika kikao hicho, imekubaliwa kuwa uongozi wa BAVICHA mkoa wa Morogoro uwasilishe kwanza kwa mkuu wa mkoa kero mbalimbali kwa lengo la kufanyiwa kazi na Serikali ya mkoa.

Mkuu wa mkoa alieleza kuwa serikali (kwa ujumla) haijashindwa kutatua kero zinazolalamikiwa na BAVICHA hivyo ni busara zikawasilishwa kwake kwanza ili ziweze kufanyiwa kazi.

Hivyo, imekubaliwa kuwa viongozi wa BAVICHA mkoa wa Morogoro watakutana tena na mkuu huyo wa mkoa tarehe 8/3/2012, saa 4.00 Asubuhi katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya mkuu wa mkoa wa Morogoro kwa lengo la kuwasilisha kero hizo.

TAHADHARI:

BAVICHA mkoa wa Morogoro
imekubaliana na maombi ya mkuu wa mkoa ya kutaka kusitishwa kwa maandamano hayo
na kuwasilishiwa kero mbalimbali kwa njia aliyoona inafaa na hivyo kutangaza
rasmi kusitisha maandamano ya tarehe 5/3/2012.

Hata hivyo,
BAVICHA inapenda kutoa tahadhari kwa mkuu wa mkoa wa Morogoro (Serikali ya
mkoa) kushughulikia ipasavyo kero mbalimbali za kijamii zitakazowakilishwa
kwake.

Iwapo itashindikana, BAVICHA
itafufua upya mpango wake wa kuandaa maandamano makubwa na ya amani mkoani
Morogoro hadi pale kero hizo zitakapopatiwa ufumbuzi.

Aidha, BAVICHA inatoa wito
kwa wafuasi wa CHADEMA mkoa wa Morogoro kuwa watulivu baada ya kusitishwa kwa
maandamano hayo na kwamba kila hatua ya mazungumzo kati ya mkuu wa mkoa na
viongozi wao watajulishwa.




MWENYEKITI BAVICHA MKOA MOROGORO
BONIFACE NGONYANI

 
Back
Top Bottom