Chadema na harakati za kudai mabadiliko

Dingswayo

JF-Expert Member
May 26, 2009
4,019
2,923
Kupanda kwa gharama za maisha, ufisadi na mgawo wa umeme ni kero kubwa

Hivi sasa, Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kipo kwenye ziara ndefu inayowakusanya maelfu ya wananchi kwenye kampeni yake ya kupigania rasilimali za taifa.

Kampeni hizi zimeanzia Mwanza, Mara, Shinyanga, Kagera na sasa zinaelekea kuja Dar es Salaam. Kwa mujibu wa ratiba ya kampeni hiyo, baada ya Dar es Salaam itakuwa zamu ya mikoa ya Nyanda za Juu Kusini na kwingineko Tanzania.

Ni mambo mengi ambayo yamekuwa yakielezwa kwenye maandamano hayo ambayo yanawahusisha wabunge wa chama hicho na viongozi wakuu akiwemo Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani bungeni.
Mbowe amekuwa akitoa msimamo mkali kuhusu chama chake akieleza kwamba kimedhamiria kuwakomboa Watanzania kutoka katika hali ngumu ya maisha na mgawo wa umeme, ikiwa serikali haitachukua hatua za dharura kulinusuru taifa.

Agenda kuu ni uzembe wa baadhi ya watendaji serikalini, ufisadi, kupanda kwa gharama za maisha na mgawo wa umeme.
Harakati za Chadema zilianza Februari 24 mwaka huu, kwa kuushtua umma wa Watanzania kutokana na mwamko mkubwa wa wakazi wa jiji la Mwanza waliojitokeza bila ya woga kushiriki katika maandamano ya amani yaliyoandaliwa na chama hicho.
Hawakuhofu kupigwa mabomu ya machozi, kumwagiwa maji ya washawasha wala risasi za polisi kama ilivyokuwa kwa wenzao wa Arusha ambao kila wanapoandamana hukiona cha mtemakuni kutokana na ubabe wa Polisi wanaokataa wasiandamane kudai haki yao.

Mpango huu wa Chadema kufanya maandamano ya amani nchi nzima unatoa mwelekeo wa ajali nyingine ya kisiasa ambayo inaweza kutokea kwa chama kinachoshika hatamu kuanguka kama ilivyokuwa kwa chama cha KANU nchini Kenya.
Hayo yanaweza kutokea kama serikali isipokua makini kutafuta mwarobaini wa matatizo sugu yanayowakabili wananchi kama kukosekana kwa huduma muhimu yakiwemo maji, elimu na zahanati kabla kufikiwa maamuzi magumu na wananchi kwa kupitia kile kinachoitwa ‘Mahakama ya Umma' yaani maandamano ya amani na mikutano ya hadhara.

Yapo mengi ambayo yanaimarisha hoja za Chadema katika mustakabali wa taifa hili, kama mikataba ya kinyonyaji ukiwemo wa Dowans ambayo inatakiwa kulipwa sh 94 bilioni, kupanda kwa bei ya umeme na kutokukubaliana na matokeo ya uchaguzi uliomweka madarakani Meya wa Jiji la Arusha Gaudence Lyimo.

Matatizo mengine mazito yanayolikabili taifa kwa sasa na ambayo hayana dalili za kupata ufumbuzi wa kudumu katika kipindi kifupi kijacho ni pamoja na suala la ajira, kupanda kwa bei ya bidhaa muhimu kama vyakula, kushuka kwa pato la taifa, kuporomoka kwa shilingi na uchumi na mfumuko wa bei.
Sera ya kilimo kwanza nayo bado haijampa mkulima unafuu katika kujikwamua kiuchumi na kukubali kile kinachohubiriwa na serikali ya CCM kwamba kimeongeza tija kwa mkulima.

Wakati suala la kilimo likiwa linaelea, Chadema kimesema kwamba serikali imekuwa ikitenga sh bilioni 400 kwa ajili ya kukodi mitambo ya kuzalisha umeme na kila mwezi sh bilioni 23 zitalipwa.

Ndio maana Chadema kimekimbilia kwenye mahakama ya umma kuishitaki serikali ikiamini kuwa wanaweza kujiimarisha kisiasa kwa kuwaaminisha wananchi kwamba wanao uwezo wa kuyatibu matatizo yaliyoshindikana CCM na serikali yake. Chadema wamefanikiwa kuishitaki serikali ya CCM kwa wananchi kwa kuwaeleza waziwazi namna baadhi ya watendaji wake, makada na viongozi kadhaa wanavyochota bila huruma rasilimali za umma na kujinufaisha binafsi.

Wanayohubiri chama kikuu cha upinzani bungeni (Chadema) huko katika maandamano yao na mikutano yao mikoani kwa sasa, yanagusa moja kwa moja hisia za wananchi jambo ambalo linawafanya waamini ndicho chama pekee kinachoweza kuwakomboa baada ya kuanguka kwa CCM.

Mwitikio wa umma katika maandamano hayo unatokana na serikali kushindwa katika kuchukua hatua dhidi ya matatizo sugu yanayolikabili taifa na badala yake viongozi wa CCM na serikali yao wamesahau kutekeleza na kusimamia sera wanazozihubiri.
Sishangai kuona Chadema wakiishitaki serikali kwa wananchi ikiwa ni miezi michache tu tangu umalizike uchaguzi mkuu uliofanyika mwezi Oktoba mwaka jana.

Naamini kwamba serikali ni serikali, haisukumwi isipokuwa kwa matakwa ya wananchi.
Lakini inaposhindwa kutatua kero za wananchi pamoja na mambo mazito yanayolikabili taifa ni lazima ipate msukosuko wa maandamano ya amani ya umma kama ambavyo Chadema inafanya kwa sasa.
Ninaamini kabisa kwamba Chadema hakijakosea kwa kuwa ni haki yao ya Kikatiba kama wanaona mambo hayaendi sawa. Unafiki wa kisiasa, visasi vinavyotokana na nafasi za madaraka kati ya vyama kwa vyama vinavyoikosoa serikali ni mambo ya kushitaki pia kwa umma.

Hayati, Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema katika kitabu chake cha Tujisahihishe, kwamba umoja wa kundi lolote ni sawa sawa na umoja wa viungo mbalimbali vya mwili au mtambo. Kwa kuwa ni kweli kwamba mara kiungo kimoja kinapokuwa hakina afya safi, huanza kuvunja kanuni za kazi na hatimaye mwili mzima huanza taabu.

Chadema wameanza kutibua nyongo dhidi ya watawala, demokrasi inawapa haki, na ukweli una wapa wajibu wa kuendeleza mawazo yao kadiri wawezavyo.

Hoja za kiufundi zilizoandaliwa na kutolewa na viongozi wa chama cha Chadema kwa ajili ya kuwashitakia watawala kwa wananchi, ndizo zitakazoamsha hasira za umma uliokuwa umejaa tongotongo na kuanza kutoa maamuzi magumu ikiwemo kuiadhibu CCM kwa kutoipigia kura mwaka 2015.

Niliwahi kutoa mfano wa semi moja ya Kiswahili isemayo ‘bora ukungu kuliko mvua ya upepo inayong'oa kasri ya mfalme'.
Ni kama CCM na serikali yake hawajaliona hilo, ila wanatafuta mbinu ya kuidhoofisha Chadema kisiasa, wanasahau kutatua matatizo mazito yanayolikabili taifa badala yake wanaingia katika kumtafuta mchawi katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 aliyesababisha Chadema wawapokonye majimbo makuu ya mijini.

Kama serikali ni sikivu, itakomesha wizi wa rasilimali za taifa, ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka ili kutoshtakiwa kwa umma; lakini kama CCM kitatumia mizengwe kukimaliza Chadema kisiasa, hakika itaibuka chuki kubwa zaidi kwa wananchi na Chadema kitazidi kupata umaarufu na kuimarika.

Julai 23 mwaka 2007, Rais Jakaya Kikwete aliwahi kusema, namnukuu ‘vyama vipo, viko huru. vinaendesha shughuli zao, wanapanda majukwaani, wanafanya maandamano na wanasema, wanachosema.

Mimi sijui mtu anaposema hakuna dhamira ya dhati ya demokrasia, hivi anamaanisha nini; maana unakuwa na chama cha siasa na kipo huru kumwaga sera zake, halafu hakifanyi hivyo unaishia kulaumiwa".

Chadema wameamua kutumia fursa na haki yao kumwaga sera mbadala ambazo wanaamini zinaweza kutibu maradhi yanayolikabili taifa hivi sasa, ni vyema sasa serikali ikatekeleza kwa vitendo madai ya wananchi.

Godfrey Mushi ni Mwandishi wa Gazeti la NIPASHE mkoani Iringa, anapatikana kwa simu namba 0767 535490 au barua pepe, ghandsome79@hotmail.com




CHANZO: NIPASHE
 
Back
Top Bottom