Bodi ya mikopo kutinga kortini kwa kutowadai wakopaji

HISIA KALI

JF-Expert Member
Oct 26, 2010
694
108
Bodi ya mikopo kutinga kortini kwa kutowadai wakopaji


Mtanzania Sunday, 06 February 2011 21:54

Daniel Mjema,Moshi
WAKILI mashuhuri wa kujitegemea nchini, Albert Msando amesema anakamilisha taratibu za kisheria kwa ajili ya kuishitaki Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Vyuo vya Elimu ya Juu (HESLB) kwa madai ya kushindwa kukusanya mikopo kutoka kwa wakopaji.

Akizungumza na Mwananchi jana, Wakili huyo alisema HESLB imeshindwa kukusanya madeni hayo ya mikopo kutokana na utaratibu mbovu wa kuwafikia wadaiwa ambao baadhi yao sasa ni watu wenye uwezo wa kifedha.

“kisingizio kinachotumika kuhalalisha kutokusanywa kwa madeni hayo ni ukosefu wa ajira, lakini baadhi yetu tuliosomeshwa na HESLB tunamiliki mali za mamilioni na tunajenga majumba ya kifahari”alilalamika Msando.

Wakili huyo alisema HESLB ilianzishwa kwa sheria namba 9 ya mwaka 2004 iliyoanza kutumika mwaka 2005 na kwamba malengo ni kwamba fedha hizo ziwe zinazunguka (revolving) ili Watanzania wengi zaidi wanufaike.

“Tunaambiwa hadi sasa HESLB haijakusanya Sh 53 bilioni na si kweli kwamba hawa ambao wanatakiwa warudishe mikopo hiyo hawana ajira au uwezo wa kifedha, ni uzembe na utaratibu mbovu wa HESLB”alidai.

Msando aliliambia Mwananchi kuwa kesho anatarajia kuipa Bodi hiyo muda wa siku saba kutaja hadharani majina ya waliopaswa kurejesha mikopo hiyo na kiasi wanachodaiwa ili umma wa Watanzania uwafahamu.

Kwa mujibu wa Msando,wengi wanaorejesha mikopo hiyo ni watumishi wa vyeo vya chini na kati serikalini wanaokatwa mishahara yao, lakini wafanyabiashara,wanasiasa na wenye uwezo hawajaanza kurejesha mikopo.

Wakili huyo alisema waliokopeshwa fedha hizo waliweka saini mikataba kati yao na HESLB ambayo inaainisha hatua za kisheria kwa watakaoshindwa kurejesha mikopo hiyo na kuhoji ni wangapi wamekwishashitakiwa hadi sasa.

“Kama HESLB ingekuwa inasimamia sheria na kanuni zake, fedha hizi za umma zingekuwa zimerejeshwa na kukopeshwa watu wengine na hata hii migomo ya wanafunzi wa vyuo vikuu isingekuwepo”alisisitiza Wakili Msando.

Wakili Msando alisema anaamini HESLB inashikwa na kigugumizi cha kuwachukulia hatua wakopaji kwa kuwa baadhi ya waliokopeshwa sasa wana nyadhifa za juu za kisiasa na kiserikali vikiwamo vyombo vya maamuzi.

Aliwataka viongozi wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) waliojitokeza hadharani wakitaka HESLB ivunjwe nao wajitazame na kujipima nafsi zao kama nao si sehemu ya watu waliochangia kudhoofisha uwezo wa Bodi kukopesha.

“Nayasema haya leo kwa moyo safi kabisa kwamba tusiwe wa kwanza kuinyooshea kidole HESLB wakati sisi ni miongoni ambao hatujarudisha mikopo yetu, wanafunzi watakopeshwa kwa fedha zipi?”alihoji Wakili Msando.

Miongoni mwa viongozi wa UVCCM taifa walioishambulia Bodi hiyo ya mikopo ni pamoja na Kaimu Mwenyekiti Taifa, Benno Malisa na Katibu Mkuu wake, Martin Shegella ambao walitaka Bodi hiyo ya mikopo ivunjwe na kuundwa upya.

Wananchi mbalimbali jana walituma pia maoni yao kwenye mtandao wa Jamii Forums wakidai walikwenda waliandikiwa barua wakalipe mikopo yao HESLB, lakini walipofika wakaambiwa kumbukumbu zao hazionekani.

Wakili Msando pia alitumia mtandao huo kutoa orodha ya vigogo mbalimbali serikalini wakiwamo Mawaziri na Wabunge ambao hawajarejesha mikopo yao na kumtaka Rais Jakaya Kiwete kuchukua hatua haraka.

Katika siku za hivi karibuni, vyuo vikuu vimetaliwa na migomo nchi nzima kutokana na wanafunzi kulalamikia kutopewa mikopo na HESLB, lakini juzi Waziri Mkuu, Mizengo Pinda aliwataka Wanafunzi kuwa watulivu wakati madai yao yakifanyiwa kazi.
 
Back
Top Bottom