ACT-Wazalendo yaridhia kushiriki kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar na Vyombo vya Uwakilishi

Mwl.RCT

JF-Expert Member
Jul 23, 2013
13,592
18,639
ADO SHAIBU: Kamati kuu ilikutana jana jijini Dar es Saalam Tarehe 5 Disemba katika hoteli ya Onomo ambayo iko Posta kwa ajili ya kutafakari hali ya kisiasa inayoendelewa nchini kwetu.

Tumetoka katika uchaguzi uliofanyika tarehe 28 ya mwezi Oktoba, uchaguzi ambao ulitawaliwa na uchafuzi mkubwa sana, uchaguzi ambao umepoteza sifa zote za kuitwa uchaguzi huru, wa haki na wa kuaminika kwa maana ya free, fair and credible election. Ni uchaguzi ambao laiti kama ungekuwa huru na haki, chama chetu cha ACT-Wazalendo kingepata matokeo makubwa sana.

Ni uchaguzi ambao kwa yeyote yule mwenye jicho la kisiasa ni wazi kabisa ACT-Wazalendo ingeshinda Zanzibar, ingepata wabunge wengi sana, ingepata wawakilishi wengi sana vivyohivyo kwa madiwani kwa sababu chama hiki kilijiandaa kushika dola.

Kamati kuu ilitafakari hali yote hii na kutafakari hatua za kuchukua na hapa nitawasomea azimio lenyewe kwa ajili ya unyeti wake nitalisoma kama lilivyoandaliwa.

Katika mjadala wa kina uliojikita katika maoni yaliyotolewa na wanachama, kamati kuu imezingatia kwamba

Mosi, historia ya kisiasa ya Zanzibar kila uchaguzi tangu uhuru na hata baada ya kurejeshwa mfumo wa vyama vingi, imekuwa ikigubikwa na hali iliyojaa majeraha, uhasama mkubwa wa kisiasa, watu kuuawa na wengine wengi kujeruhiwa, kudhalilishwa kijinsia na mali kuharibiwa. Hali hii imejirudia tena katika uchaguzi wa mwaka 2020 ambapo watu 17 wamefariki kutokana na matukio mbalimbali ya kwenye uchaguzi ikiwemo watu kupigwa risasi, vipigo na mashambulizi ya kimwili na watu 302 kujeruhiwa na wengine kudhalilishwa kijinsia na mali zao zikiharibiwa na kuibiwa.

*****************

Ado Shaibu: Kamati kuu ya chama chetu imeazimia kwamba, wawakilishi wachache kwa maana ya madiwani, wajumbe wa baraza la wawakilishi na wabunge ambao wametangazwa kushinda waruhusiwe kushiriki kwenye vyombo vyao vya uwakilishi ili waendeleze mapambano kwenye vyombo hivyo.

Ni muhimu ieleweke kwamba, kamati kuu imefikia uamuzi huu sio kwamba tunaufurahia, kamati kuu ilikuwa kwenye njia panda ya kuchagua njia moja kati ya njia mbili. Ilikuwa ni kuchagua ama uamuzi mbaya, ama uamuzi mbaya zaidi.

Haikuwa chagua baina ya uamuzi mzuri sana na uamuzi mbaya, hilo ni muhimu sana lieleweke. Kwa hiyo tumechagua njia mbayo tumeona ina nafuu.

Pili, kamati kuu ya chama chetu kwa kuzingatia ibara ya 9(3) ya katiba ya Zanzibar imeridhia chama kushiriki kwenye serikali ya umoja wa kitaifa Zanzibar na imeielekeza kamati ya uongozi ya chama chetu kupendekeza jina la mwanachama ataekuwa makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar na muhimu ieleweke katika kuhitimisha, kamati kuu ya chama chetu imefikia maamuzi haya baada ya kufanya tafakuri ya kina.


==========
MASWALI 10 NA MAJIBU JUU YA UAMUZI WA ACT KUJIUNGA SERIKALI YA UMOJA WA KITAIFA ZANZIBAR (SUK)

1. Kujiunga SUK ni kuhalalisha Uchaguzi haramu?

Hapana. ACT Wazalendo kimechukua na kinaendelea kuchukua hatua mbalimbali za ndani na nje ya nchi kuupinga uchaguzi huu na matokeo yake. Chama kitaendelea kufanya hivyo, ikiwemo kupigania Katiba Mpya na Tume Huru ya Uchaguzi ili kuhakikisha uchaguzi nchini unakuwa huru na wa haki.

2. SUK ni hisani ya CCM?
Hapana. SUK ipo kikatiba. Hatupewi na CCM. Tumepewa na Katiba ya Zanzibar. Majimbo tuliyotangazwa kushinda (Pemba) tulishinda kweli. Hata hivyo, Kuporwa kingi hakuhalalishi kususia kidogo kilichopatikana. Ni muhimu ikumbukwe pia kuwa SUK ni zao letu. Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Ndugu Maalim Seif Sharif kwa kushirikiana na Rais Mstaafu wa Zanzibar Ndugu Amani Abeid Karume ndio waliokuwa waasisi wa SUK kwa ajili ya kuleta muafaka na maelewano miongoni mwa Wazanzibari.

3. Kujiunga SUK ni kuwasaliti wenzetu waliokamatwa, kuteswa, kuachwa vilema na kuumizwa na wale waliouawa kutokana na uchaguzi?
Hapana. Vitendo vilivyofanywa na Vikosi vya Zanzibar, Vikosi vya JMT (Polisi, Jeshi, Usalama wa Taifa) vya kuuwa, kutesa na kujeruhi watu tena baadhi yao wakiwa mikononi mwa vyombo husika ni vitendo vya kijinai. Jinai haifi. Tutaendelea kutetea haki yao ndani na nje ya nchi hadi haki ipatikane na waliotenda unyama wawajibishwe.

4. Kujiunga SUK kutafifisha kesi yetu ICC?
Hapana. Chama hakitaachana na kesi yake ICC. Kesi itaendelea hadi waliofanya unyama kwenye Uchaguzi Mkuu wawajibishwe.

5. Kujiunga SUK kutafifisha madai yetu kimataifa (Jumuiya ya Madola, AU, Jumuiya ya Ulaya n.k) kuhusu uchaguzi kuhujumiwa?
Hapana. Chama hakitaondoa malalamiko yake kwenye vyombo vya kimataifa kuhusu hujuma kwenye Uchaguzi Mkuu. Tutaendelea kupaza sauti ndani na nje ya nchi kupigania Tume Huru ya Uchaguzi na Katiba Mpya ili Uchaguzi uwe huru, haki na wa kuaminika.

6. Viti vilivyotangazwa ni vichache, hakuna mabadiliko yoyote tutakayoleta SUK?
Ni kweli tumedhulumiwa sana. Uchaguzi ungekuwa huru na wa haki, tungepata wawakilishi wengi zaidi. Lakini hilo halitunyimi kuwaruhusu wachache waliotangazwa kwenda kwenye vyombo vya Uwakilishi. Wakati mwingine, wingi si hoja. Kwenye Bunge lililopita tulikuwa na Mbunge mmoja tu, Zitto Kabwe. Lakini, alikuwa na mchango wa kipekee Bungeni. Chama kitahakikisha kuwa kinawasimamia Wawakilishi wake kwenye vyombo vyote wasimame kidete kutetea maslahi ya umma.

7. Kujiunga SUK ni kukosa msimamo kama wa wenzetu CHADEMA?
Hapana. Kila Chama kinapaswa kufanya maamuzi yake kwa kuzingatia maslahi ya Chama na maslahi ya Taifa. Maamuzi haya yamefanywa na vikao halali vya Chama kwa kuzingatia maslahi ya ACT Wazalendo na Taifa kwa ujumla.

8. Kujiunga SUK ni kuwasaliti Wazanzibar?
Hapana. Chama chetu kimezungumza na wanachama na viongozi wetu kwenye Mikoa yote ya Zanzibar. Wengi wanaunga mkono Chama kujiunga SUK.

9. Kujiunga SUK ni kujali maslahi binafsi (Ruzuku, vyeo n.k?)
Hapana. Chama hiki kimesheheni viongozi wengi ambao wana rekodi zisizoyumba za kutanguliza maslahi ya Taifa badala ya maslahi yao binafsi. Hata uamuzi wa sasa wa kujiunga SUK unazingatia maslahi ya Chama badala ya maslahi binafsi ya mtu.

10. Kujiunga SUK ni kurejesha nyuma madai ya Msingi ya harakati ya mageuzi?
Hapana. Mapambano ya kupigania mageuzi nchini hayatakoma hadi mabadiliko ya msingi yanayopiganiwa kwenye nyanja za kiuchumi, kisiasa na kijamii yapatikane.

====

MAAZIMIO YA KIKAO CHA KAMATI KUU YA CHAMA CHA ACT WAZALENDO KILICHOKUTANA TAREHE 05 DISEMBA 2020: ONOMO HOTEL DAR ES SALAAM

Jana tarehe 05 Disemba, 2020 Kamati Kuu ya Chama cha ACT Wazalendo ilikutana katika kikao chake maalum, ikiwa na lengo la kujadili na kufikia maamuzi juu ya masuala kadhaa yanayohusu mustakabali wa Taifa na Chama chetu.

Katika kikao hicho pamoja na mambo mengine, Kamati Kuu ilipokea taarifa ya maoni ya wanachama juu ya hali ya siasa nchini hususani Uchaguzi Mkuu uliofanyika mwezi Oktoba, 2020 Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

Katika mjadala wa kina, uliojikita katika maoni yaliyotolewa na wanachama, Kamati Kuu imezingatia kwamba;-

• Historia ya kisiasa ya Zanzibar kwa kila uchaguzi tangu uhuru na hata baada ya kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi imekuwa ikigubikwa na hali iliyojaa majeraha, uhasama mkubwa wa kisiasa, watu kuuawa na wengine wengi kujeruhiwa, kudhalilishwa kijinsia na mali za watu kuharibiwa. Hali hii imejirudia tena katika uchaguzi wa mwaka 2020, ambapo watu 17 wamefariki kutokana na madhila ya uchaguzi huu ikiwemo kupigwa risasi, vipigo na mashambulizi ya kimwili, na 302 wamejeruhiwa na wengine kudhalilishwa kijinsia na mali zao zikiharibiwa na kuibiwa.

• Wakati pekee ambao Zanzibar imefanya uchaguzi wa kistarabu na wananchi kusalimika na maafa pamoja na madhila yanayotokana na uchaguzi katika historia ya chaguzi Zanzibar ni kwenye uchaguzi wa mwaka 2010 ambapo Zanzibar ilikuwa imeingia katika Maridhiano ya Novemba 5, 2009 kabla ya uchaguzi huo. Pia katika Uchaguzi wa mwaka 2015 ambao ulikuwa ni uchaguzi bora kuliko chaguzi zote kabla ya kufutwa kwake. Uchaguzi huu nao ulifanyika wakati ambapo Zanzibar ilikuwa ipo chini ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa ambayo ni zao la Maridhiano.

• Kamati Kuu imejiridhisha kuwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa iliyoundwa kwa moyo Safi itakuwa ni kwa maslahi ya Zanzibar, Wazanzibari na Taifa kwa ujumla katika kuhakikisha kuwa vitendo vya uvunjifu wa haki za binaadamu na uvurugaji wa Uchaguzi vinadhibitiwa kama ilivyokuwa wakati wa Uchaguzi wa mwaka 2010. Dhima ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar kwa maslahi ya Wananchi inapaswa pamoja na mambo mengine kuhakikisha kuwa;

i. Uchunguzi wa matukio yote yaliyotokea kabla, wakati na baada ya Uchaguzi ya uvunjaji wa haki za binaadamu, unafanyika na kuwafariji waathirika wote pamoja na kuwachukulia hatua za kisheria waliohusika kupanga na kutekeleza matukio hayo.
ii. Kunafanyika Mabadiliko ya mfumo wa Uchaguzi Zanzibar ili kurejesha imani ya wananchi juu ya uwepo wa uchaguzi huru na wa haki.
iii. Kunafanyika Marekebisho ya uendeshaji wa vyombo vya Idara Maalum za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ili vifanye kazi kwa Weledi (professionalism) na bila ubaguzi wa kisiasa.

• Kamati Kuu imezingatia hali ilivyo Zanzibar hivi sasa ambapo siasa za chuki na uhasama zimerudi upya kutokana na makovu yanayotokana na uchaguzi wa Mwaka 2020. Kwamba Zanzibar inahitaji busara kubwa katika kuponya majeraha yaliyotokana na uchaguzi huo. Pia, Zanzibar inahitaji hekima na busara katika kuhakikisha kuwa matukio ya namna hii hayajirudii tena na kwamba lazima kuwe na utaratibu wa kuhakikisha kuwa chaguzi zijazo zinakuwa huru, za haki, zinazokubalika na zenye hali ya utulivu.

Hivyo basi, Kamati Kuu kwa kauli moja imefikia maazimio yafuatayo:-

1. Kamati Kuu IMEAZIMIA Chama kiwaruhusu Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, Wabunge, na Madiwani waliochaguliwa kwenda kukiwakilisha Chama na Wananchi waliowachagua.

2. Kwa kuzingatia Ibara ya 9(3) ya Katiba ya Zanzibar, Kamati Kuu imeridhia Chama kushiriki kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar na imeielekeza Kamati ya Uongozi kupendekeza jina la mwanachama atakayekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.

Kamati Kuu imefikia maamuzi haya kwa kuzingatia maoni ya wanachama na viongozi wa Chama chetu, tathmini ya historia ya mapambano ya demokrasia Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

Ado Shaibu,
Katibu Mkuu,
ACT Wazalendo,
06 Disemba, 2020.
 
Matangazo ya moja kwa moja

Tunawapongeza kwa kufanya Uamuzi wa hekima

Sote ni Ndugu na tunajenga nyumba moja

Sasa ni Wakati wa kuchapa Kazi kwa Wazanzibar na Watanzania wote


FB_IMG_16072429023876542.jpg
 
Naona wametengeneza maswali yao na majibu yao, that's interesting!. Hilo jibu la swali la ruzuku ni jepesi sana, naamini ruzuku ndio iliyowapeleka kwenye hiyo serikali, sababu nyingine zote kelele tu.

Zitto anaendelea na tabia zake za opportunist, chance yoyote itakayotokea mbele yake anaitumia tu.

Alijaribu karata ya Membe ikagoma, sasa kaona aje na hii mpya, sidhani kama hii ni njia nzuri ya kukijenga chama chake.

Vyema sasa azunguke huko mikoani kukitangaza chama chake, hii tabia ya kusubiri matukio yakitangaze chama itamchelewesha kama sio kumpoteza kabisa.
 
Zitto anaendelea na tabia zake za opportunist, chance yoyote itayotokea mbele yake anaitumia tu.

Alijaribu karata ya Membe ikagoma, sasa kaona aje na hii mpya, sidhani kama hii ni njia nzuri ya kukijenga chama chake.

Vyema sasa azunguke huko mikoani kukitangaza chama chake, hii tabia ya kusubiri matukio yakitangaze chama itamchelewesha kama sio kumpoteza kabisa.
Vijana wa Mbowe mnaopoteza muda
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom