Zitto na Mbowe kinyang'anyiro bungeni

Madikizela

JF-Expert Member
Jul 4, 2009
679
447
TOFAUTI ambazo zimekuwapo kati ya viongozi wawili wa
ngazi za juu wa Chadema, Freeman Mbowe na Naibu Katibu Mkuu wake, Kabwe Zitto, sasa zinahamia bungeni baada ya Zitto kutangaza nia ya kuwania nafasi ya Kiongozi wa Upinzani Bungeni.

Nafasi ya Kiongozi wa Upinzani Bungeni inashikwa na chama chenye wabunge wengi miongoni mwa vyama vya upinzani bungeni, na kwa mujibu wa matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, Chadema ina viti vya majimbo 22 na CUF viti 23.

Hata hivyo, Chadema itaweza kuwa na viti vingi zaidi bungeni kwa sababu ya kura zake nyingi ilizopata katika ushindi huo majimboni kulinganisha na CUF.

Kura za wabunge za majimbo kwa kila chama ni mojawapo ya vigezo vya uteuzi wa kupata idadi ya wabunge wa Viti Maalumu.

Zitto ambaye ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini, ametangaza nia yake ya kuwania nafasi hiyo na anachosubiri ni utaratibu wa chama hicho wa namna ya kumpata kiongozi huyo.

Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu jana, Kabwe alisema ameshatangaza nia yake ya kuwania nafasi hiyo kupitia mtandao wa Facebook na anachosubiri ni utaratibu rasmi wa chama chake.

“Chama hakijaweka utaratibu wa namna kiongozi wa upinzani bungeni anapatikana. Utaratibu ukishawekwa nitatoa taarifa rasmi ila kwa sasa pitia Facebook yangu utaona ujumbe wangu,” alisema.

Katika mtandao huo, Zitto aliandika “nimewajulisha viongozi wangu wa chama Taifa kuwa nina nia ya kugombea nafasi ya Kiongozi wa Upinzani Bungeni.

Mara baada ya taratibu za chama kuhusu nafasi hii kuwa wazi nitawajulisha.” Gazeti hili liliwasiliana na Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Mbowe kuhusu maandalizi ya utaratibu wa kumpata kiongozi huyo wa wapinzani bungeni na kama na yeye, ana nia ya kuwania nafasi hiyo, lakini alijibu kwa kifupi kuwa chama hicho kinaamua mambo yake kupitia vikao na kukata simu.

Ingawa si rasmi na haimo katika kanuni za Bunge, kwa kuwa Mbowe ambaye ni Mbunge Mteule wa Hai atakuwa ndani ya Bunge, kwa wadhifa wake wa uenyekiti wa Taifa wa Chadema, ingetarajiwa ndiye apitishwe kuwa Kiongozi wa Upinzani Bungeni; hali inayoonesha Zitto anaipinga kwa kutangaza nia yake.

Kwa muda sasa, Mbowe amekuwa na tofauti na Zitto katika masuala kadhaa ya uendeshaji wa chama hicho, huku Mbunge huyo kijana akijitokeza hadharani kuweka misimamo yake anapoamini chama kwenda kinyume, na wakati mwingine misimamo hiyo imemletea matatizo na viongozi wengine.

Aliwahi kujitokeza kuwania uenyekiti wa Taifa wa chama hicho mwaka jana, lakini akazuiwa na Baraza la Wazee, kabla ya kujitoa kumkabili Mbowe baada ya wazee kumsihi asifanye hivyo.

Pia alikuwa na msimamo mkali katika uchaguzi wa Baraza la Vijana na Baraza la Wanawake la Chadema baada ya kuhisi mchezo mchafu unataka utendeka, na kuonesha kuwa kulikuwa na rafu, uchaguzi huo ulisimamishwa kiasi cha kuathiri hata uteuzi wa wabunge wa viti maalumu.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, aliyekuwa Kiongozi wa Upinzani katika Bunge lililopita kupitia CUF, Hamad Rashid Mohammed, ambaye alikuwa Mbunge wa Wawi, alisema kwa mujibu wa kanuni za Bunge, chama kinachotoa kiongozi wa upinzani ni chenye
wabunge wengi bungeni.

Alisema katika uchaguzi wa mwaka 2005, CUF ilikuwa na wabunge wengi bungeni ndiyo maana aliwania nafasi hiyo na kushinda ambapo kwa sasa atalazimika kuachia ngazi kwa Chadema.

Katika Bunge lililopita, CUF ilikuwa na wabunge 33 na Chadema 11.

Kutoka Dodoma, Jasmin Shamwepu, anaripoti kwamba viongozi wa Chadema wameandaa mapokezi makubwa ya waliowaita majemadari wa chama hicho walioibuka kidedea katika ubunge.

Akizungumza na HABARILEO jana, Katibu wa Mkoa wa Chama hicho, Stephen Masawe, alisema uongozi umeandaa mapokezi makubwa ya wabunge walioshinda katika majimbo kwa madai kuwa ni wakombozi wa wananchi.
 
Back
Top Bottom