Wimbi la utekaji linawaweka askari hatarini

kapuku94

Member
Nov 7, 2018
66
69
C&p lugman Maloto

TANGU mwanzoni mwa Karne ya 19, mhalifu konkodi, Eugene Francois Vidocq, alipoamua kubadilika na kutumia mbinu zake za ujahili kuisaidia Serikali ya Ufaransa, dunia ilipokea, kuendeleza na kuupanua mfumo wa vyombo vya usalama kuwa na mashushushu ili kurahisisha kunasa wahalifu na mitandao yao.

Mwaka 1811, Vidocq alianzisha mtandao wake wa mashushushu, ukiitwa Surete Nationale, yaani Usalama wa Taifa. Mtandao huo ulifanya kazi za kuzisaidia mamlaka za nchi kuwanasa wahalifu na makundi yao. Surete Nationale kwa sasa ni jeshi rasmi la polisi, likiitwa National Police.

Muongo wa tatu wa Karne ya 19, aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Sir Robert Peel, kipindi akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani, alianzisha mtindo wa kutumia mashushushu kwenye jeshi la polisi la nchi hiyo, The Metropolitan 'The Met', kisha Marekani ilifuata mwanzoni mwa Karne ya 20, polisi New York walipoanzisha idara waliyoiita Kikosi cha Kiitaliano (Italian Squad).

Kila nchi kuna mashushushu, wapo wenye kufanya kazi ndani au nje ya nchi. Wapo mashushushu wa idara za itelijensia, vilevile polisi wanaotumika kwa kazi maalum. Umuhimu wake ni mkubwa katika kulinda na kuzuia uhalifu wa aina mbalimbali kwa nchi na wananchi.

Shushushu wa polisi kwa Kiingereza anaitwa undercover police. Katika Kiswahili tuna msamiati mwingine; askari kanzu, kwa maana ya askari asiyevaa sare rasmi za jeshi lake. Askari kanzu lina upana mkubwa, linamtafsiri kila askari asiyevaa sare. Ndani ya jeshi la polisi, askari wa aina hiyo wanatumika zaidi kitengo cha itelijensia.

Hivi sasa Tanzania imekumbwa na hali ya wasiwasi kuhusu vitendo vya utekaji. Hivi karibuni, mfanyabiashara Mohammed Dewji alitekwa na watu ambao mpaka sasa hawajafahamika na kumshikilia kwa siku nane kabla ya kumwachia. Tukio hilo limewajaza hofu kubwa Watanzania.

Mo alitekwa na watu wenye bunduki ambao walimchukua kwenye Hoteli ya Colosseum, Oysterbay, Dar es Salaam na kumpakia kwenye gari ambalo jeshi la polisi wameshaliweka wazi. Gari hilo pia lilitelekezwa na watekaji, viwanja vya Gymkhana, Dar es Salaam, siku ambayo waliamua kumwachia huru Mo Dewji.

TATIZO NI ENDELEVU

Kati ya Machi na Aprili mwaka jana, mwanamuziki wa Hip Hop nchini, Ibrahim Mshana 'Roma Mkatoliki', akiwa na wenzake watatu, walitekwa na watu wasiojulikana na kuwashikilia kwa takriban siku tatu. Akina Roma walikuwa studio ya muziki ya Tongwe Records, Oysterbay, walipovamiwa na watekaji.

Kwa mujibu wa maelezo ya Roma na wenzake, ni kwamba watekaji walikuwa na bunduki pamoja na pingu. Walivyochukuliwa walidhani ni polisi lakini ikawa kinyume chake. Waliwapiga, kuwavunja meno na kuwaachia majeraha na alama mbalimbali zenye kuonesha kwamba walipewa msoto mkali.

Jinsi mwandishi wa habari wa kujitegemea, aliyekuwa akiripoti gazeti la Mwananchi, Azory Gwanda, alivyopotea, hisia za karibu zaidi ni kwamba alitekwa. Kuna watu waliokuwa wamevalia kiraia walikuwa naye, wakaongozana mpaka kwa mkewe shambani kufuata ufunguo wa nyumba yao, baada ya hapo hakuonekana tena.

Hisia za awali zingeweza kukwambia watu walioongozana na Azory ni polisi waliokuwa katika mavazi ya kawaida. Hata hivyo, baada ya Azory kupotea jumla, jawabu ambalo lina nguvu zaidi ni kuwa wale watu hawakuwa polisi, isipokuwa ni watekaji. Mtanzania aliyefuatilia tukio la Azory anawaza jinsi ya kujilinda dhidi ya watu wenye kuvaa kiraia wenye kujiita polisi.

Ben Saanane, kada wa Chadema aliyekuwa msaidizi binafsi wa Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, alitoweka tangu Novemba 2016. Taarifa za simu yake zinaonesha mara ya mwisho alikuwa Mburahati, Dar es Salaam, kisha alikwenda au alipelekwa Mikocheni ambako simu yake ilizimwa.

Hoja za ndani ya Bunge Aprili mwaka jana, moja ikitoka kwa mbunge wa Nzega Mjini (CCM), Hussein Bashe, aliyedai kutekwa na watu aliowaita maofisa wa Usalama wa Taifa, inaongeza hofu. Bashe alizungumza hayo chini ya mwiko kuwa Idara ya Usalama wa Taifa haitakiwi kujadiliwa bungeni.

Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe, alikwenda mbele zaidi na kuvituhumu bungeni vyombo vya ulinzi na usalama kwa kutofanya kazi sawasawa na kujikuta vikigongana kutoa majibu kuhusu Saanane, namna alivyopotea na watu walio nyuma ya kupotea kwake.

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo, Kigoma, Simon Kanguye, inaelezwa alifuatwa nyumbani kwake. Hisia za mwanzoni kwa wanafamilia au pengine Kanguye mwenyewe, ni kwamba waliomfuata ni maofisa wa polisi ambao hawakuvaa sare au mashushushu wa vyombo vingine vya Serikali.

Baada ya kitambo kirefu kupita na Kanguye kutafutwa vituo vyote vya polisi bila mafanikio, jawabu la karibu ni kuwa wale waliomchukua ni watekaji. Hapohapo ongeza kwamba mitaani kuna watu hujifanya maofisa wa polisi na wengine Usalama wa Taifa. Hujivika wasifu bandia ili kufanya utapeli.

HATARI KWA ASKARI

Kutokana mlolongo wa matukio ya utekaji, tuhuma dhidi ya maofisa wa Idara ya Usalama wa Taifa zilizoelezwa ndani ya Bunge mwaka jana kupitia Zitto na Bashe, vilevile tabia za watu kujivalisha uhusika bandia na kujifanya ni polisi au mashushushu wa usalama, hatari kubwa ipo kwa askari kanzu.

Mwananchi mwenye kufuatilia habari za matukio ya utekaji kwa ukaribu, anayeishi akizongwa na fikra kuhusu watu wasiojulikana. Akifuatwa na askari halali wa jeshi la polisi ambao hawajavaa sare, akikataa kutii amri atakuwa na kosa gani? Ikiwa kuna ambao walitii na kujikuta kwenye mikono ya watekaji?

Kuna askari wasiovaa sare lakini wanatembea na bunduki, kwao mwananchi anaweza kuwatofautisha vipi na watekaji au majambazi? Akipiga mayowe ya wezi na wananchi wakianza kurusha mawe, yule mpiga moyowe kosa lake litakuwa lipi? Ni dhahiri atafanya hivyo kulinda usalama wake kutokana na hali halisi ya utekaji ilivyo.

Wapo askari hutembea na magari ya kiraia, nao huvaa kawaida na bunduki hubeba. Ikitokea wanamfuatilia mtu kwa tuhuma za uhalifu, wanamfikia na kumwamuru asimamishe gari. Akikataa kusimama au kwa hofu kwamba watu hao wanaweza kuwa watekaji, akiamua kuligonga gari lao ili kujinusuru, itakuwaje?

Izingatiwe kuwa mtu huyo ambaye anasimamishwa na polisi wasio na sare, anajua simulizi ya mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, alivyofuatiliwa na gari aina Nissan Patrol nyeupe. Watu wenye bunduki waliokuwemo ndani yake wakamshambulia kwa risasi nyingi. Ni zaidi ya mwaka sasa Lissu hajapona.

Wengine wanamiliki silaha za moto kihalali. Wanajua kuhusu utekaji na visa vyote vya watu wasiojulikana. Je, akisimamishwa na polisi wasio na sare, yeye akilini akawaza ni jamii ya watu wasiojulikana, kisha akatoa silaha yake na kuanza kujihami, italeta sura gani na mazingira ya sasa yanajaza hofu?

Siku moja nilishuhudia gari dogo aina ya salon, likigonga daladala Eicher kwa nyuma eneo Bondeni, Mbezi Beach, Dar es Salaam. Lile gari dogo lilikuwa na kasi sana. Bila shaka lilikuwa linawahi tukio. Ndani yake kulikuwa na watu waliovaa kiraia lakini wana bunduki. Dereva na kondakta walipolifuata lile gari dogo kuomba waelewane kwa sababu wao ndiyo waligonga, waligoma.

Bahati iliyokuwepo ni kwamba gari lile dogo liliharibika sana, kwa hiyo haikuwezekana kuliondoa. Watu kwenye daladala na mashuhuda wengine wakawa wanasema watu hao ni polisi, wengine wakatilia shaka kwamba inawezekana ndiyo hao watu wasiojulikana. Hofu imeshakuwa kubwa.

Hofu hiyo ndiyo ambayo inaleta wasiwasi kuhusu usalama wa askari kanzu. Ni kwa namna gani itakuwa rahisi kueleweka kuwa wao si jamii ya watu wasiojulikana ikiwa wananchi wataanza kuwatuhumu na kuwashambulia? Askari wanahitaji angalizo kubwa la kikazi kipindi hiki.

Ndimi Luqman Maloto

 
Leo nimepita pale jengo la central police DSM nje wamejenga kibanda cha mlinzi naamini ningezidi kuchungulia ndani ningekuta mlinzi wa kampuni ya group 4 security
 
Umenikumbusha mbali mtoa mada, swala LA Polisi kuvaa nguo za kawaida ni tatizo sana hasa katika mazingira yasiyo rasmi mfano barabarani tena usiku, au sokoni, shambani n.k

Mwaka 2010 maeneo kati ya ikwiriri na kilwa( nanjilinji) kama sijakosea majira ya usiku kama SAA 3 kasoro kulitokea ajali mbaya ya gari ya kenta ikiwa imebeba watu na bidhaa za mnadani( ilikuwa iko full yaan) ikagongana na haisi watu wengi walifariki pale pale, sasa ikabidi Polisi wafike eneo LA tukio na gari lao ilikuwa land cruiser mkonge zile, wakapaki pembeni na kuanza kysaidiana na watu kuokoa na kupanga maiti vizuri, majeruhi wengi walipangwa barabarani pembeni kidogo siyo katikati ,
Polisi wengi walikuwa wamevaa kiraia na bunduki zao, basi kuna kuna basi moja ilikuwa inatoka kusini iko speed kidogo basi Polisi akajitokeza njiani kusimamisha, kumbe dereva alijua ni jambazi basi kazidisha speed kufika mbeleee hamadiiiiiiii watu kibao barabarani jamaa aliwakanyagaaa wale majeruhiii na basi ikakosea njia ikaenda kusimama kwenye mtaro...wengi walikufaaa katika wale majeruhii
 
Tatizo ni limatokana na kufanya kazi bila kuzingatia matakwa ya sheria na sheria. Sheria ya TISS inakataza askari wa usalama wa taifa kukamata wahalifu kwa namna yoyote ile wao wanatakiwa kupeleleza na kulitumia jeshi la polisi kama kuna haja ya kukamata siyo wao wenyewe kukamata. Hapo ndiyo hasa chanzo cha tatizo. Endapo kutatolewa maelekezo ya kutenda majukumu yao kwa kufuata sheria huo mkanganyiko hautakuwepo na hakutakuwa na watekaji ambao watajifanya usalama wa taifa na kukamata watu wakati ni watekaji. Endapo hatua ya kutenda kazi kwa kufuata sheria Itazimgatiwa uhalifu wa kuteka watu utapungua sana.
 
Back
Top Bottom