GREGO
JF-Expert Member
- Apr 3, 2014
- 4,279
- 2,921

Ni kichwa cha habari cha kushtusha kidogo ila ukweli ndiyo huo – japo ni jambo ambalo pengine litapingika vikali mitaani kwa kuwa tayari wengi wetu tumekumbatia mitandao hii. Katika miji ya Tanzania ya sasa kila kona unayokwenda utaona simu za mkononi zenye uwezo wa kutumia intaneti alimaarufu kama ‘smartphone’ zimezagaa.
Mtandao wa Reuters ulipata kuandika kwamba watumiaji wa simu za mkononi Tanzania wameongezeka kwa asilimia 16 mwaka 2014 na kufikia watu milioni 31.86. Reuters ilieleza kuwa watumiaji wa intaneti waliongezeka kwa asilimia 22 na kufikia watu milioni 11.35 baadaye mwaka huo huo, hii ikionyesha kwamba sekta ya mawasiliano inaendelea kukua kwa kasi kubwa.
Sasa swali litaibuka: Je, ni kwa namna gani mitandao ya kijamii ni umaskini kwa Tanzania ilihali inachangia katika Pato la Taifa? Hapa ndipo mjadala wangu utaanzia katika makala hii. Nimependa kuandika juu ya mada hii kwa jicho tofauti kidogo na lile la wenzetu wanauchumi ambapo wao huangalia zaidi takwimu za kimahesabu katika kukua kwa uchumi wakisahau sababu za kijamii ambazo husababisha hali fulani kutokea.
Mtandao wa Reuters ulipata kuandika kwamba watumiaji wa simu za mkononi Tanzania wameongezeka kwa asilimia 16 mwaka 2014 na kufikia watu milioni 31.86. Reuters ilieleza kuwa watumiaji wa intaneti waliongezeka kwa asilimia 22 na kufikia watu milioni 11.35 baadaye mwaka huo huo, hii ikionyesha kwamba sekta ya mawasiliano inaendelea kukua kwa kasi kubwa.
Sasa swali litaibuka: Je, ni kwa namna gani mitandao ya kijamii ni umaskini kwa Tanzania ilihali inachangia katika Pato la Taifa? Hapa ndipo mjadala wangu utaanzia katika makala hii. Nimependa kuandika juu ya mada hii kwa jicho tofauti kidogo na lile la wenzetu wanauchumi ambapo wao huangalia zaidi takwimu za kimahesabu katika kukua kwa uchumi wakisahau sababu za kijamii ambazo husababisha hali fulani kutokea.
Nikirejea maneno ya mwanazuoni nguli Dk. Mwami, wakati fulani alishawahi kuniambia ya kuwa ‘one physical phenomenon cannot cause another physical phenomenon’ (tukio moja la kipekee haliwezi kusababisha tukio lingine la kipekee). Ngoja nitoe mfano hapa ili tuweze kuelewa kile ninachotaka kusema.
Mtu akinywa maji inatarajiwa baada ya muda fulani atatoa haja ndogo, lakini je, ni tendo la kunywa maji linaloleta haja ndogo au ni matokeo ya hali zisizoonekana ambazo huendelea katika mwili wa binadamu na mwishowe kuleta haja ndogo hiyo? Hii inaeleza kuwa ujio wa utandawazi nchini kwetu sio jambo jema kama vile ambavyo wengi wetu tumekuwa tukiliona na kulishupalia.
Utandawazi ama kama vile ambavyo wanazuoni wamependa kuuita ‘utanda-wizi’ umechangia kurudisha nyuma maendeleo yetu kwa kiasi kikubwa japokuwa takwimu za wanauchumi zinaonyesha utandawazi umeleta maendeleo kwa kiasi kikubwa.
Makala hii itagusa mahususi kabisa mitandao ya kijamii kama vile Facebook, Twitter, Instagram, WhatsApp, Snapchart, Tango na mingine mingi kwani hii huzuka kila kukicha.
Mitandao hii ya kijamii inaendelea kuwa changamoto kwa rasilimali watu hususan vijana ambao wengi wetu tumeishupalia kwa dhati kabisa na kuifanya kama sehemu muhimu sana ya maisha yetu na kwa wengine hawawezi kuishi bila hiyo mitandao. Kwa uelewa zaidi, hebu turejee historia kidogo ili tukumbuke tulikotoka na tuweze kukihusisha na kile ambacho kinaendelea kwa sasa kwani tusifikiri yale yanayotokea sasa hivi yamekuja tu bila kuwa na chanzo maalumu.
Mwanzoni mwa karne ya 20, bara la Afrika lilitawaliwa na watu kutoka nchi mbalimbali za Ulaya na Uarabuni. Wakati wa ukoloni ili mabwana wakubwa hao waweze kutimiza lengo lao, iliwapasa kwanza kututawala kifikra ili kuonyesha yale tunayoyafanya si ya msingi na kuwa ni mambo yasiyostaarabika na ya kichawi. Ikumbukwe, walivyoanza kuja mabwana wakubwa hawa Afrika walitanguliza wamishenari ili waje kutulegeza kwa jina la kuleta ustaarabu na kutuletea Neno la Mungu kwani waliogopa mkinzano.
Ni muhimu kufahamu kwamba ili uweze kumtawala mtu kiurahisi lazima kwanza uanze kuiteka fikra yake ili uweze kuyaona mambo katika sura moja, ndio maana kuanzia hapa ikawa rahisi kuwatumikisha mababu zetu katika mashamba makubwa kwa kuwaaminisha katika kilimo cha biashara na kuacha kilimo kwa ajili ya chakula.
Ukoloni huu ulizaa utumwa na mateso ya nguvu kwa Waafrika mpaka biashara hiyo ya kikatili ilipokuja kupigwa marufuku.
Ukoloni huu haukuishia hapa, kwani baada ya nchi nyingi za Afrika kupata uhuru wao ndipo ukoloni-mambo-leo ukaanza. Baada ya uhuru nchi nyingi za Afrika zilijua ya kuwa sasa ziko huru kufanya yale ziyatakayo kama nchi kumbe ilikuwa ni muda wa kupitia upande mwingine wa sarafu iitwayo ubepari (Capitalism).
Nchi za magharibi zikiongozwa na Marekani zilifanya juhudi zote kueneza ubepari huu katika nchi zote za Afrika ili kuweza kuzitawala upya bila kuuonyesha uwepo wao moja kwa moja. Ubepari huu ulisambazwa kwa njia ya mashirika ya kimataifa kama vile Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF).
Mashirika haya yalitunga sera mbalimbali ambazo nchi za Afrika zilipaswa kuzifuata kwa kisingizio cha kuzitoa kwenye dimbwi la umaskini. Isitoshe sera hizi kutoka kwa mataifa ya kibepari zilikuwa na masharti endapo zisipofuatwa misaada ya mali na fedha zingesitishwa kuletwa.
Kwa kuwa nchi nyingi za Afrika hususani Tanzania zilikuwa na shida, ikatupasa kuitikia wito wa mabwana wakubwa na kufungulia soko huria kuanzia miaka ya 1980 -tukasahau ujamaa wetu na kuuona hauna maana tena.
Huu ulikuwa muendelezo wa kutawaliwa kifikra ambapo ulitufanya kuona bila kupata misaada kutoka kwa mataifa ya kibepari hatuwezi kuendelea na ndipo hapo utegemezi uliokithiri ulizidi nchini mwetu na kuanza kuagiza kila kitu kutoka nje na kugeuka kuwa soko la malighafi ya kutoka mataifa ya kibeberu.
Kama vile haitoshi, utandawazi ukabisha hodi na Tanzania na nchi nyingine za Afrika tulishazoea kupokea tu kwani tulishaaminishwa katika fikra zetu kila kitu kutoka magharibi ni kizuri tukapokea. Mbaya zaidi, mabepari hao wakasema ni vigumu sana kuishi nje ya utandawazi kwani umefanya nchi zote kuwa karibu kama vile watu waishio kijijini. Inatia simanzi kuona vile ambavyo tulizidi kuaminishwa vitu na tukihoji tunaambiwa misaada itasitishwa.
Mabepari hawa walitaka tuendelee kufuata wasemayo ili waweze kututawala vizuri na ili kufanikisha azma yao hiyo ndio ikaletwa lugha mpya iitwayo Haki za Binadamu (Human Rights) wakisititiza mtu yeyote yuko huru kufanya kile atakacho. Haki hizi za binadamu zilipata tafsiri kutoka nchi za kibepari na zikasambazwa kwa kasi kwa kutumia mashirika ya kimataifa yakisaidiwa kwa karibu na asasi zisizo za kiserikali (NGOs).
Hivi tulishawahi kujiuliza haki za binadamu za Kitanzania ni zipi? Au tafsiri tuliyonayo ni kutoka kwa Umoja wa Mataifa? Tuliache hili tutaliangalia siku za usoni.
Turejee katika mada yetu sasa na tujaribu kuioanisha kwa ukaribu na historia hiyo hapo juu. Tukumbuke hapo juu nilisisitiza ili kuweza kumtawala mtu ni sharti uanze na fikra zake na hivyo ndivyo mabebari hao hufanya mpaka leo kupitia mitandao ya kijamii. Kwanini basi mabepari hao huanzia kwenye fikra zetu?
Jibu ni rahisi: Haki za Binadamu wanataka ukianza kuhoji wakwambie mtu ana uhuru wake wa kuamua afanye nini na aache nini. Na ndio maana hata leo ukijaribu kuwauliza vijana walio wengi mitaani iweje leo mnatumia muda mwingi katika mitandao ya kijamii kuunufaisha umma mambo yako binafsi hata ambayo watu wasingepaswa kujua watakwambia tuna haki kama binadamu kuchagua yale tufanyayo.
Leo hii tunashuhudia watu mbalimbali katika mitandao ya kijamii wakieleza umma kuhusu mahusiano yao na wenza wao, wakionyesha sehemu mbalimbali za miili yao, kueleza matatizo yao binafsi kwa nia ya kutaka ushauri na wengine kudiriki kurusha picha zao za ngono katika mitandao hiyo kwa jina la Haki za Binadamu.
Umaskini kwa Tanzania unaletwaje na mitandao hii ya kijamii? Tukiangalia kwa uwazi kabisa sharti la ubepari ni kuhakikisha kuwa wanapata faida kubwa kwa kupitia wanyonge ambapo wanyonge hao hutumikishwa sana ili kuweza kuleta faida kubwa kwa mabepari hao.
Hebu tuanze na upande wa kwanza wa unyonywaji. Je, tulishawahi kujiuliza gharama ya kutumia simu ya kawaida isiyokuwa na intaneti (maarufu kama simu ya tochi) na ile iliyo kuwa na intaneti (smartphone)? Labda ndio ama hapana, ila ukiwa na simu ya tochi unahitaji vocha kwa ajili ya kutuma ujumbe mfupi wa maneno na kupiga japo gharama yake bado sio ndogo kwani itakupasa kuunga aina fulani ya vifurushi ili kuweza kuwasiliana na mitandao mingine na gharama hii hupanda kila kukicha.
Je, ukiwa na simu iliyounganishwa na intaneti (smartphone) inakuwaje sasa? Hapa kuna tofauti kidogo kwani itakupasa kuwa na fedha kwa ajili ya kupiga, ujumbe mfupi wa kawaida na intaneti. Na ikumbukwe gharama hii ni kubwa kwani wameshakuwekea makundi mbalimbali ambayo unapaswa kuchagua ili kufikia huduma yako.
Na je, usipokuwa na fedha kwenye simu yako hiyo yenye uwezo wa intaneti itakufaa nini? Hapa ndipo utaona watu wakitumia fedha nyingi kuhakikisha wanakuwa na vocha kwenye simu zao kwa ajili ya kuweza kuingia kwenye mitandao hii ya kijamii kila siku ili kuweza kupata au kutoa taarifa.
Cha ajabu zaidi, kuna makundi ya watu ambayo hawafanyi kazi kama watoto na wanafunzi ambao nao wana hizo simu zenye intaneti na huhitaji kuweka vocha kila siku, sijui fedha wanapata wapi au ndio kundi jipya la utegemezi linaanza kuja sasa Tanzania?
Tukiendelea kutafakari zaidi, wanufaikao na mitandao hii ya kijamii, je ni kina nani? Je, ni walaji au wazalishaji? Jibu rahisi hapa ni kampuni za simu za wawekezaji wa kibepari ndio hunufaika zaidi na mitandao hii ya kijamii na kuwaacha walaji kuwa maskini ama kwenda jela, hasa baada ya kutungwa sera mpya ya matumizi ya mitandao mwaka 2015.
Hebu tafakari kidogo sera ya unyonyaji wa kibepari ni kuhakisha unapata faida kutoka kwa wavuja jasho wa hali ya chini mpaka wale wa juu ndio maana leo hii katika kampuni za simu utaona viwango vya kujiunga kifurushi kinaanzia shillingi 250 za Kitanzania wakiamini hata yule mvuja jasho wa hali ya chini kabisa anaweza kumudu. Hebu tujiulize kidogo juu ya unyonyaji huu ambapo wengi wetu yamkini hatuuoni ama tunapuuza. Ni wangapi wetu tunaweza kukaa bila intaneti kwa siku nzima?
Kwa kuwa kampuni hizi za kibepari ziligundua hii ni sehemu ya kumfanya Mtanzania kuwa maskini kwani wengi wetu bado tunavuja jasho kila kukicha ila hatufanikiwi, zimeanzisha huduma za kukopa pesa ili upate intaneti halafu utalipa pindi uwekapo salio. Je, hii siyo namna ya kuongeza umaskini kwa Mtanzania?
Hebu tuangalie aina nyingine ya umaskini uletwao na mitandao ya kijamii. Hivi tulishawahi kujiuliza mitandao hii ya kijamii imeasisiwa na nani na kwa manufaa ya nani? Majibu yanaweza kuwa mengi hapa kutokana na kila mtu afikiriavyo, ila hebu tuangalie ili kuweza kufanya ubepari ushamiri kirahisi ulimwenguni hasa nyakati hizi lazima kuwe na mfumo wa usambazaji ambao utafanya taarifa fulani kufika sehemu nyingi kwa wakati mmoja.
Leo hii tuna aina nyingi sana za mitandao ya kijamii ambayo hutupa taarifa nyingi za kimagharibi ambazo wengi wetu huzifurahia na kuona ndizo zenye tija na kuona zile za kwetu kama zimepitwa na wakati.
Hebu tafakari kidogo, leo hii ukiingia instagram na kuona Kim Kadashian kavaa nywele fulani bandia na kapendeza sana moja kwa moja nasi tunapenda kuwa kama yeye tunaanza kutafuta hizo nywele zenye thamani kubwa sana nasi tuwe kama yeye. Japo nywele hizo ukizivaa hazileti tija yoyote kwa maendeleo zaidi ya kutumia fedha nyingi ambayo ulivuja jasho muda mrefu kuipata.
Je, huku siyo kuendelea kuongeza umaskini kwa Watanzania wanaotaka usasa na kuacha ukale kwani mitandao ya kijamii imeshaonyesha ili uwe wa kisasa lazima uvae nguo za namna fulani, uweke nywele za namna fulani, utumie manukato fulani.
Ambacho wengi wetu tunasahau sasa ni kwamba hizi kampuni za kibepari za nywele bandia, manukato, nguo, pochi, kucha bandia wanatumia watu maarufu kuuza bidhaa zao ili sisi wanyonge tuone ndio mambo ya kisasa na kuanza kupapatika nayo, mwishowe tunazidi kumaskinika ilihali tukizidi kuwanufaisha wao.
Ndugu zangu huu ni ubepari wa hali ya juu, yatupasa kufikiria upya namna ya maisha yetu na kufanya mambo yenye tija ili kuweza kulikomboa taifa letu. Hapa utasikia watu wakisema sasa tufanyaje na ndio hali ya dunia inavyokwenda yatupata kwenda na kasi hiyo.
Wakati nikiwa na mjadala na mke wangu juu ya hili jambo wakati nikiandika makala hii akaniuliza swali: Sasa unawashauri nini Watanzania ili waepukane na unyonyaji huu? Nilimjibu kwamba siyo mimi wakutoa majibu bali inatupasa kama Taifa kuliona hili ili kuweza kulikomboa Taifa kwa kuwa na mijadala kila mahali nchini kwani ukisema tufanye hivi utapata jibu la Haki za Binadamu au uhuru wa binadamu kufanya anachotaka.
Hebu sasa tuangazie upande wa mwisho wa umaskini uletwao na mitandao ya kijamii. Ili kuweza kutengeneza soko zuri kwa mabebari ni sharti kutengeneza taifa tegemezi ambalo litakuwa siyo bunifu na mwishowe kuweza kutoa masoko ya uhakika. Sasa hivi Tanzania kama Taifa lina vita kubwa sana ya kupambana dhidi ya mitandao ya kijamii kwani wengi wetu tumeshaathirika kiasi kwamba ukikaa dakika mbili mbali na simu yako unajihisi mgonjwa.
Kiuhalisia hebu jaribu kukaa na jamaa zako kama wanne mkiwa mahali katika mazungumzo ya jioni halafu angalia vile watu walivyokuwa karibu na simu zao kiasi kwamba meza inakosa mazungumzo kabisa kwani watu wako karibu sana na watu walio mbali na wao kuliko watu walio karibu na wao kiuhalisia.
Ukijaribu kuangalia hili kwa undani utakuta hata familia nyingi watoto wanakosa uangalizi mzuri kwani wazazi wakirudi nyumbani nao wako karibu sana na simu zao kuliko vile walivyo karibu na watoto wao.
Je, hii siyo aina nyingine ya umaskini? Sehemu muhimu ya maendeleo ya binadamu ni kuhakikisha watu wanakutana pamoja kujadili maendeleo ya nchi yao kwa hoja. Leo sote fikra zetu ziko kwenye kuangalia mitandao ya kijamii na kusahau kufanya mijadala yenye tija kwa Taifa letu. Mfano mzuri, leo hii ikitokea ajali kila mtu anataka kuwa mwandishi wa habari wa kwanza kutoa taarifa ya tukio la ajali badala ya kuanza kuwaokoa majeruhi katika ajali hiyo.
Fikra zetu ndio mkombozi wetu kwani zinatuletea ubunifu katika maisha ili kuweza kufanya mambo yenye tija katika taifa ila kwa kuwa tumeukumbaitia ubepari kwa dhati, ubepari huo umeweza kuteka fikra zetu vizuri kiasi kwamba tunasahau kubuni mambo ya msingi ya jamii zetu na kubaki kuwa walaji wa yale yote yanayoletwa na nchi za magharibi tukiona yale wafanyayo kama ni sahihi zaidi.
Mitandao ya kijamii imefanikiwa kuteka fikra zetu na ubunifu wetu na hivi ndivyo Tanzania itaendelea kuwa maskini!
Source: Gazeti la RAIA MWEMA